Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kutumia Dawa Vibaya
    Amkeni!—2009 | Mei
    • Kutumia Dawa Vibaya

      “NILIANZA kutumia dawa kwa ajili ya matibabu nilipokuwa na umri wa miaka 14,” akasema mwanamke anayeitwa Lena.a “Nilitamani kuwa na mwili mwembamba unaovutia, kwa hiyo daktari wa familia akanipa dawa za kupunguza uzito. Nilijihisi vizuri wakati tu nilipowavutia vijana. Mwishowe nikaanza kutumia dawa za kulevya na kuishi maisha mapotovu. Kila wakati nilikuwa nikijitahidi kulewa kabisa.”

      Mwanamke anayeitwa Myra alikuwa na ugonjwa wa kipanda-uso, kwa hiyo daktari wake akampa dawa za kutuliza maumivu. Baada ya muda, akaanza kumeza dawa nyingi zaidi, si kwa ajili ya kutuliza maumivu tu bali pia ili kutosheleza uraibu wake. Isitoshe, alianza kumeza dawa za washiriki wengine wa familia yake.

      Ripoti zinaonyesha kwamba idadi inayoongezeka ya vijana na watu wazima wanatumia vibaya dawa zinazopendekezwa na daktari. Wanazitumia ili kujituliza, kukabiliana na mahangaiko, kuwa macho, kupunguza uzito, au kulewa. Dawa zinazotumiwa vibaya mara nyingi ni zile zinazopatikana nyumbani: dawa za kutuliza maumivu, za kutuliza akili, za kuchochea utendaji wa mwili, na za kumsaidia mtu alale.b Pia, watu hutumia vibaya dawa zinazouzwa bila maagizo ya daktari kama zile za kumsaidia mtu alale, za kuzibua pua, na za mizio.

      Tatizo hilo limeenea sana na linazidi kuongezeka. Kwa mfano, katika sehemu fulani za Afrika, Ulaya, na Asia Kusini, watu wanatumia vibaya dawa za kitiba kuliko vile wanavyotumia dawa za kulevya. Nchini Marekani, matumizi mabaya ya dawa za kitiba yanazidi matumizi ya dawa zote za kulevya isipokuwa dawa mbalimbali zinazotokana na bangi. Kulingana na ripoti ya gazeti la hivi karibuni, idadi inayoongezeka ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 17 “wanatumia vibaya dawa zinazopendekezwa na daktari kuliko wanavyotumia kokeini, heroini, na metamfetamini zikiwa pamoja.” Kwa kweli, watu wanatumia sana dawa hizo hivi kwamba wamefanya kuwe na biashara ya dawa bandia za kitiba.

      Wewe na watoto wako mnaweza kujilinda jinsi gani msitumie dawa vibaya, iwe ni zile zinazopendekezwa na daktari au za kulevya? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Majina katika makala hizi yamebadilishwa.

      b Mambo yanayozungumziwa katika makala hizi yanaweza kutumika pia kuhusu dawa za kulevya na kutumia kileo vibaya.

      [Sanduku katika ukurasa wa 3]

      “Uraibu wa dawa huonekana mtu anaposhindwa kujizuia kuzitumia, anapozitumia kwa sababu zisizo za kitiba, na anapoendelea kuzitumia licha ya kupata madhara au kujua hatari ya kuzitumia,” linasema jarida Physicians’ Desk Reference. Uraibu huonekana mtu anapokosa kujidhibiti na anapopendezwa kupita kiasi na dawa hizo.

      Utegemezi wa kimwili huonekana mtu anapoathirika kwa sababu ya kuacha kutumia dawa fulani aliyopendekezewa na daktari. Hilo ni jambo la kawaida na halionyeshi kwamba mtu ni mraibu.

      Stahamala ni neno linalotumiwa kuonyesha hali ambayo hutokea mwili unapozoea dawa kabisa hivi kwamba mtu anahitaji kuongezewa kiwango anachotumia ili apunguze maumivu.

  • Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba
    Amkeni!—2009 | Mei
    • Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba

      MSICHANA anayeitwa Angie aliwasikia wazazi wake wakisema kwamba dawa za ndugu yake zilisaidia kupunguza hamu yake ya kula. Kwa sababu Angie alihangaika sana kuhusu uzito wake, alianza kutumia dawa za ndugu yake, akimeza tembe moja baada ya siku chache. Ili wazazi wake wasigundue, alimwomba rafiki yake aliyekuwa akitumia dawa hizohizo ampe tembe kadhaa.a

      Kwa nini watu wengi hutumia dawa vibaya? Sababu moja ni kwamba zinapatikana kwa urahisi nyumbani. Pili, vijana wengi hujidanganya kwamba hawavunji sheria yoyote kwa kutumia dawa bila maagizo ya daktari. Na tatu, inaonekana kwamba dawa zinazopendekezwa na daktari hazina madhara sana kama dawa za kulevya. Vijana fulani hujiambia, ‘Ikiwa mtoto anaweza kunywa dawa fulani, basi bila shaka ni salama kuitumia.’

      Ni kweli kwamba zinapotumiwa vizuri, dawa zinazopendekezwa na daktari zinaweza kuboresha afya na hata kuokoa uhai. Lakini zinapotumiwa vibaya zinaweza kuwa hatari kama dawa za kulevya. Kwa mfano, mtu anapotumia vibaya dawa fulani za kuchochea utendaji wa mwili, anaweza kufanya moyo uache kupiga au kupatwa na kifafa. Dawa nyingine zinaweza kupunguza mwendo wa kupumua na mwishowe kusababisha kifo. Pia dawa inaweza kuwa na madhara ikitumiwa na dawa nyingine au kileo. Mapema mnamo 2008, mwigizaji mmoja maarufu alikufa “kwa sababu ya kuchanganya dawa sita za kumtuliza mtu akili, za kulala, na za kutuliza maumivu,” lilisema gazeti Arizona Republic.

      Hatari nyingine ni kwamba mtu anaweza kuwa mraibu. Dawa nyingine huwa kama dawa za kulevya kwani zinapotumiwa kupita kiasi au kwa sababu isiyofaa, zinachochea sehemu za ubongo zinazoufanya mwili usisimke na hivyo kufanya mtu awe na hamu yenye kuendelea ya dawa hizo. Lakini badala ya kutokeza msisimko unaoendelea au kuwasaidia watu wakabiliane na matatizo maishani, kutumia dawa vibaya hutokeza matatizo zaidi. Dawa hizo zinaweza kuongeza mfadhaiko na kushuka moyo, kuharibu afya na uwezo wa mwili wa kufanya kazi kwa njia ya kawaida, zinaweza kumfanya mtu awe mraibu, au kusababisha mambo haya yote. Mambo hayo humfanya mtu awe na matatizo nyumbani, shuleni, au kazini. Kwa hiyo, tutatofautisha jinsi gani ikiwa dawa zilizopendekezwa na daktari zinatumiwa vizuri au vibaya?

      Matumizi Mazuri na Mabaya

      Unatumia dawa vizuri ikiwa unazimeza kulingana na maagizo ya daktari ambaye anajua ugonjwa wako. Hilo linatia ndani kumeza kiasi cha dawa ulichoambiwa, wakati unaofaa, kwa njia inayofaa, na kwa sababu zinazofaa za kitiba. Hata hivyo, unaweza kupatwa na matatizo mengine yasiyofaa au yaisiyotazamiwa. Hilo likitukia, mwone daktari mara moja. Anaweza kukubadilishia dawa au kukuambia uache kutumia dawa hiyo. Unaweza kufuata mwongozo huo unapotumia dawa unazoweza kununua bila maagizo ya daktari: Zitumie tu ikiwa una sababu nzuri ya kufanya hivyo na ufuate kwa uangalifu maagizo yaliyo kwenye kibandiko.

      Watu hujihatarisha wanapotumia dawa kwa sababu zisizofaa, wasipomeza kiwango walichopendekezewa na daktari, wanapotumia dawa za mtu mwingine, au kutumia dawa kwa njia isiyofaa. Kwa mfano, tembe fulani zinapaswa kumezwa zikiwa nzima ili ziweze kufanya kazi polepole mwilini. Mara nyingi watu hutumia dawa hizo vibaya kwa kuzipondaponda au kuzitafuna, kuzisaga na kuzinusa, au kuziyeyusha ndani ya maji na kujidunga mwilini kwa kutumia sindano. Kufanya hivyo kunaweza kumlewesha mtu, lakini hiyo inaweza kuwa hatua ya kwanza ya kumfanya mtu awe mraibu. Isitoshe, kufanya hivyo kunaweza kusababisha kifo.

      Kwa upande mwingine, ikiwa mtu anatumia dawa kwa njia inayofaa lakini anashuku kwamba huenda inamfanya awe mraibu, anapaswa kumjulisha daktari bila kukawia. Daktari atajua jinsi ya kurekebisha hali hiyo bila kupuuza ugonjwa wa mtu huyo.

      Kuenea sana kwa matumizi mabaya ya dawa, kunaonyesha jinsi hali ilivyo katika nyakati zetu. Mpango wa familia, mahali ambapo mtu angetazamia kupata upendo na kimbilio kutokana na matatizo ya kila siku, unakumbwa na hali ngumu. Viwango vya maadili na vya kiroho vinapotea, na watu pia hawaheshimu uhai. (2 Timotheo 3:1-5) Sababu nyingine ni kwamba watu hawana tumaini la kuwa na wakati ujao mzuri. Watu wengi wanatazamia tu mabaya. Hivyo, wanafanya mambo bila kufikiria madhara na wanafuatilia anasa bila kujali. Biblia inasema: “Mahali pasipo na maono watu hujiachilia.”—Methali 29:18.

      Ikiwa wewe ni mzazi, bila shaka unataka kuilinda familia yako kutokana na upotovu wa maadili wa ulimwengu na ufuatiliaji wa mambo yasiyo muhimu. Lakini unaweza kufanya hivyo jinsi gani? Na unaweza kupata wapi mwongozo unaofaa na tumaini linalotegemeka la wakati ujao mzuri? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Imetolewa katika Tovuti ya TeensHealth.

      [Sanduku katika ukurasa wa 4]

      WATAFANYA LOLOTE ILI WALEWE

      Watu fulani watajaribu kufanya jambo lolote lile ili tu walewe. Mazoea yenye kudhuru sana yanatia ndani kuvuta kemikali za kusafisha, rangi za kupaka kucha, kemikali za kung’arisha fanicha, petroli, gundi, rangi, na kemikali nyingine zinazoweza kugeuka kuwa mvuke. Mtu anapovuta harufu ya kemikali, harufu hiyo huingia moja kwa moja kwenye mfumo wa damu na hivyo kumfanya mtu alewe mara moja.

      Zoea lingine lenye kudhuru ni matumizi mabaya ya dawa zinazonunuliwa bila maagizo ya daktari ambazo zina alkoholi au zinazomfanya mtu ahisi kulala. Zinapotumiwa kwa kiasi kikubwa, zinaathiri hisi za mtu, hasa hisi ya kusikia na kuona, na zinaweza kumfanya mtu achanganyikiwe, aone njozi, afe ganzi, na aumwe na tumbo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      “MBINU ZA KUPATA DAWA”

      “Waraibu na watu wanaotumia dawa vibaya wana ‘mbinu za kupata dawa,’” linasema jarida Physicians’ Desk Reference. “Mbinu za kupata dawa hutia ndani kupiga simu za dharura au kwenda kwenye vyumba vya matibabu ya dharura saa za kazi zinapokaribia kwisha, kukataa kufanyiwa uchunguzi unaofaa wa kitiba au kutumwa kwa daktari mwingine, kudai mara nyingi kwamba wamepoteza karatasi ya dawa, kubadili maandishi ya dawa, na kukataa kutoa habari za matibabu ya awali au majina ya madaktari wengine ambao wamewahi kumtibu. Ni jambo la kawaida kwa watu wanaotumia dawa vibaya na kwa waraibu kubadilisha-badilisha madaktari ili kuandikiwa dawa zaidi.”

      Aina tatu zifuatazo za dawa hutumiwa vibaya mara nyingi:

      ◼ Dawa zenye kasumba (Opioids)—dawa za kutuliza maumivu

      ◼ Dawa za kupunguza wasiwasi—barbiturate na benzodiazepine zinazotumiwa kupunguza wasiwasi au kumfanya mtu apate usingizi

      ◼ Dawa za kuchochea utendaji wa mwili—zinatumiwa kutibu tatizo la upungufu wa makini kutokana na utendaji wa kupita kiasi, kusinzia mchana, au kunenepa kupita kiasi.b

      [Maelezo ya Chini]

      b Habari hii imetolewa na Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      MIONGOZO YA KUTUMIA DAWA VIZURI

      1. Fuata maagizo kwa uangalifu.

      2. Usibadili kiasi cha dawa bila kumuuliza daktari.

      3. Usiache kutumia dawa ulizoandikiwa bila kuagizwa na daktari.

      4. Usipondeponde au kuvunja tembe ikiwa hujaagizwa kufanya hivyo.

      5. Tambua madhara ambayo dawa hizo zinaweza kukusababishia unapoendesha gari au unapofanya utendaji mwingine.

      6. Chunguza madhara ya kuchanganya dawa hiyo na alkoholi au dawa nyingine, iwe umeandikiwa na daktari au umeinunua bila maagizo ya daktari.

      7. Ikiwa umewahi kutumia dawa vibaya au vitu vingine vinavyolewesha, mwambie daktari.

      8. Usitumie dawa alizoandikiwa mtu mwingine, na usiwape watu wengine dawa ulizoandikiwa.c

      [Maelezo ya Chini]

      c Habari hii inategemea madokezo yaliyotolewa na Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani.

  • Wazazi—Walindeni Watoto Wenu!
    Amkeni!—2009 | Mei
    • Wazazi—Walindeni Watoto Wenu!

      WAZAZI wanaojali huuliza hivi, “Kwa nini vijana wengi wanatumia dawa za kitiba vibaya?” Sababu za wao kufanya hivyo zinatofautiana. Vijana fulani huzitumia kwa ajili ya msisimuko. Wengine wanataka kujifunza vizuri zaidi au kupunguza wasiwasi. Huenda wengine wakawa wanaugua kimwili au kihisia na wanataka tu kupata nafuu. Kwa kweli, hata watoto wenye umri wa miaka 12 wamekuwa wakitumia dawa vibaya, na huenda wamekuwa wakizipata kupitia mamia ya maelfu ya Tovuti zinazouza dawa hizo, bila kujali ni nani anayezinunua. Wengine wamenunua tembe kutoka kwa watu wanaodai kuwa marafiki. Ikiwa wewe ni mzazi, unaweza kufanya nini ili uwalinde watoto wako?

      Hatua moja ni kuzungumza nao waziwazi kuhusu hatari za kutumia dawa iwe zimeagizwa na daktari au zile za kulevya. Hatua nyingine ni kuweka dawa mahali salama, labda hata kuzifungia katika kabati. Fahamu ni dawa gani zilizo nyumbani na uchunguze ni kiasi gani kinachotumiwa. Ikiwa dawa haitumiwi tena, itupe. Ikiwa kijana wako ameacha kukohoa lakini bado anatumia dawa, mwulize kwa nini anafanya hivyo. Mwishowe, uwe macho ili utambue anapobadili marafiki, sura, au tabia yake au maksi zake zinaposhuka kwa ghafula shuleni.

      Ikiwa Mtoto Anatumia Dawa Vibaya

      Ikiwa mtoto wako anatumia dawa vibaya au unashuku kwamba ana tatizo hilo, unaweza kufanya nini? Unahitaji kuzungumza kwa upendo na fadhili na mtoto wako kuhusu wasiwasi wako. “Fikra za mtu zimefichika kama kilindi cha maji,” inasema Biblia, “lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo.” (Methali 20:5, Biblia Habari Njema) Kupata ukweli kutoka kwa mtoto anayedhaniwa kuwa anatumia dawa vibaya ni kama kuteka maji kwa kutumia kamba inayoweza kukatika kwa urahisi. Ukivuta kamba hiyo kwa nguvu sana kwa kumshutumu au kumkasirikia kwa uchungu, unaweza kukata kamba ya mawasiliano. Kumbuka kwamba unataka kutimiza mambo mawili. Kwanza, unataka kujua ikiwa kuna tatizo. Na pili, ikiwa kuna tatizo, ni nini kinacholisababisha. Mara nyingi, tatizo linaweza kusababishwa na moja kati ya mambo haya.

      ◼ Marafiki wasiofaa na kushinikizwa nao. “Msidanganyike,” inasema 1 Wakorintho 15:33, “urafiki mbaya huharibu tabia njema.” (BHN) Kwa hiyo, wazazi wenye hekima watawasaidia watoto wao waone hatari ya kuwa na marafiki wasiofaa ambao wanaweza kuwa na uvutano mkubwa kwao. Kwa upande mwingine, wazazi kama hao watawasaidia watoto wao wachague marafiki wazuri. (Methali 13:20) Huenda Baba na Mama wakawaalika marafiki kama hao nyumbani au kwenye tafrija ya familia.

      ◼ Mfadhaiko. Katika ulimwengu wa leo, watoto wanashinikizwa sana wafanikiwe, na wazazi wanafanya mambo yawe mabaya hata zaidi kwa kuwashinikiza zaidi.a Je, unajua uwezo na udhaifu wa watoto wako? Je, unawawekea miradi yenye kiasi na kuwasaidia kuifikia? Je, sikuzote unaepuka kumlinganisha mtoto wako na wengine ili asishuke moyo? Kwa kweli, ikiwa watoto hawatimiziwi mahitaji yao ya kihisia nyumbani, wataenda kutafuta upendo na urafiki wanaotaka kwingineko. Pia wazazi wenye hekima hujaribu kusitawisha mazoea mazuri ya ibada nyumbani, labda kwa kusoma Biblia pamoja na watoto wao. Yesu Kristo alisema: “Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho.”—Mathayo 5:3.

      ◼ Kukosa kuwekewa mipaka. Vijana fulani hutumia dawa vibaya kwa sababu wazazi wao huwaendekeza. “Mvulana [au msichana] aliyeachiliwa atamletea mama yake aibu,” inasema Methali 29:15. Ukweli ni kwamba watoto huthamini sheria zilizo wazi zinazowafanya wahisi wakiwa salama na wanapendwa, licha ya kwamba wao hulalamika kuzihusu. Hivyo, Biblia inawatia moyo wazazi wawawekee watoto wao miongozo inayofaa na vilevile wawawekee mfano mzuri. (Waefeso 6:4) Pia Biblia inasema wanapaswa kuhakikisha kwamba sheria hizo zinafuatwa na wawe thabiti. “Acheni Ndiyo yenu imaanishe Ndiyo, na Siyo yenu, Siyo.”—Yakobo 5:12.

      Bila shaka, ukijua kwamba mtoto wako anatumia dawa vibaya, itafaa uzungumze na daktari kuhusu jambo hilo. Inaweza kuwa vigumu kuacha uraibu na huenda mtu akahitaji usaidizi kutoka kwa wataalamu. Pia, ikiwa familia yako ni sehemu ya kutaniko la Kikristo la Mashahidi wa Yehova, unapaswa kuomba msaada wa wazee. (Yakobo 5:13-16) Wanaume hao wenye sifa za kustahili kiroho wanaweza kukusaidia kutumia kanuni za Biblia ambazo zitasaidia kuacha zoea hilo.

      Makala inayofuata itazungumzia kanuni nyingine na pia tumaini zuri la wakati ujao tunaloweza kuwa nalo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona makala “Watoto Waliofadhaika,” kwenye ukurasa wa 14.

      [Blabu katika ukurasa wa 7]

      “Fikra za mtu zimefichika kama kilindi cha maji; lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo.”—Methali 20:5, Biblia Habari Njema

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      DALILI ZA VIJANA WALIO HATARINI

      ◼ Kuna mtu fulani katika familia ambaye amewahi kutumia vibaya dawa au kileo

      ◼ Kushuka moyo au kujiona hawafai

      ◼ Kuhisi kwamba hawawezi kuchangamana na wengine; kujiona wao si maarufu

      ◼ Kujihisi walegevu mara kwa mara; kukosa usingizi

      ◼ Wajeuri, wenye mtazamo wa kuasi mamlakab

      [Maelezo ya Chini]

      b Inategemea habari zilizochapishwa na Teen Help.

  • Suluhisho Bora Kuliko Dawa
    Amkeni!—2009 | Mei
    • Suluhisho Bora Kuliko Dawa

      LENA, aliyetajwa katika makala ya kwanza, alipokuwa na umri wa miaka 32, “alimezwa na hisia za hatia, kutokuwa na tumaini, na hofu ya kufa,” hasa kwa sababu ya tatizo lake la kutumia dawa vibaya. “Nilitaka kuwa mke na mama mzuri,” akaandika, “lakini kila kitu maishani mwangu na ulimwenguni kilinihuzunisha sana na kunitamausha na sikuwa na sababu ya kuwa mzuri. Na mara chache nilipojaribu, sikufanikiwa.”

      Kisha Lena akaanza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Muda si muda, kweli ya Biblia ikamfanya awe na amani ya akili na kitulizo, ambacho alieleza kuwa “hisia bora zaidi ambayo nimewahi kuwa nayo.” Kuelewa kanuni za Biblia na tumaini zuri la wakati ujao kulimchochea kubadili maisha yake na kuacha uraibu wake.

      Kanuni za Maisha

      Sheria na kanuni zinazopatikana katika Biblia ziliwekwa hasa kwa ajili yetu na Muumba wetu, Yehova Mungu. Zaburi 19:7, 8 inasema hivi: “Sheria ya Yehova ni kamilifu, huirudisha nafsi. . . . Maagizo kutoka kwa Yehova ni manyoofu, huufanya moyo ushangilie; amri ya Yehova ni safi, huyafanya macho yang’ae.”

      Kwa mfano, 2 Wakorintho 7:1 linatuhimiza “tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili na roho.” Lena alichukua maneno hayo kwa uzito na hilo lilimsaidia kuacha zoea hilo baya. Ilikuwa vivyo hivyo kwa Myra, ambaye pia alitajwa katika makala ya kwanza ya gazeti hili. Huenda unakumbuka kwamba alikuwa mraibu wa madawa aliyoandikiwa na daktari kwa ajili ya maumivu ya kichwa. Myra alikabiliana jinsi gani na tatizo lake? Alizungumzia jambo hilo waziwazi na daktari ambaye alimsaidia kupata matibabu mengine.a Zaidi ya hilo, alitafuta msaada katika kutaniko la Kikristo na akatiwa moyo.

      Pia Lena na Myra walitafuta msaada kupitia sala. Andiko la Wafilipi 4:6, 7 linasema: “Msihangaike juu ya kitu chochote, bali katika kila jambo kwa sala na dua pamoja na kutoa shukrani maombi yenu na yajulishwe Mungu; na amani ya Mungu yenye ubora unaozidi fikira zote itailinda mioyo yenu na nguvu zenu za akili.” Mtumishi wa Mungu wa nyakati za kale aliyepata amani hiyo ya akili aliandika kwamba ‘fikira zake zinazofadhaisha zilipokuwa nyingi,’ maneno ya Mungu yenye kutia moyo yalimpa kitulizo, yalimfariji, na kumpa shangwe ya moyoni. (Zaburi 94:19) Maneno kama hayo yenye kufariji yanaweza kupatikana katika Biblia na kutoka kwa washiriki Wakristo, kutia ndani wazee Wakristo wanapotutia moyo na kututegemeza.

      Hata hivyo, nyakati nyingine, kwa sababu ya zoea la kutumia dawa vibaya, mtu anaweza kujihisi hafai kabisa. Janice, Mkristo ambaye kwa miaka mingi alikuwa mraibu wa dawa za kitiba aliandika hivi: “Waraibu wanaweza kuliona kuwa jambo gumu kumwomba Yehova msaada kwa sababu ya hali yao mbaya ya kiroho na kwa sababu wanajichukia.” Chini ya hali hizo, ni muhimu sana kutafuta msaada wa Wakristo wakomavu. Upendo na subira wanayoonyesha wanapokutia moyo na sala yao ya imani inaweza ‘kumponya mtu asiyejisikia vizuri.’ (Yakobo 5:15) Bila shaka, ikiwa mraibu ni mtoto, wazazi wanapaswa kumsaidia aache uraibu huo na kuwa na uhusiano mzuri na Yehova ili asirudie tena zoea hilo.

      Janice alienda kwenye kituo cha matibabu, akashinda zoea lake, na tangu wakati huo hajatumia tena dawa vibaya. Aliandika hivi: “Mimi humtegemea Yehova anisaidie ninapopata hamu ya kutumia dawa. Sasa nina utulivu na utu wenye kupendeza niliokuwa nao zamani.”

      Matatizo Yetu Yote Yatakapokwisha

      Hivi karibuni, hakutakuwa na dawa zozote. Hilo litawezekanaje? Ufunuo 21:3, 4 inajibu hivi: “Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu . . . Naye atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena. Mambo ya zamani [kutia ndani matatizo tuliyo nayo sasa] yamepitilia mbali.”

      Biblia inalinganisha tumaini la Kikristo na “nanga ya nafsi, likiwa hakika na imara.” (Waebrania 6:18, 19) Mabaharia wa nyakati za kale walipokumbwa na dhoruba, waliangusha nanga ya meli kwenye bahari. Ikiwa nanga ingeshika sakafu ya bahari, ingeizuia meli hiyo isipeperushwe na dhoruba na kugonga matumbawe hatari au fuo za bahari. Vivyo hivyo, tumaini “hakika na imara” linalopatikana katika Biblia linaweza kutufanya tuwe imara kihisia, kiakili na kiroho wakati majaribu yaliyo kama dhoruba yanapotokea, na bila shaka majaribu kama hayo yatatokea.

      Tunakualika uchunguze Biblia na uone jinsi ambavyo mashauri na mafundisho yake yanafaa na ni yenye kutia moyo. Mashahidi wa Yehova watafurahi kukusaidia, nawe hutakatishwa tamaa.

      [Maelezo ya Chini]

      a Hali zote hazifanani na za Myra. Kwa mfano, huenda watu fulani wakawa wanaugua ugonjwa wenye maumivu mengi na wakapendekezewa na daktari dawa kali za kutuliza maumivu ambazo zinaweza kuwafanya wawe waraibu. Mgonjwa kama huyo hatumii dawa hizo ili alewe wala si mraibu.—Ona Methali 31:6.

      [Blabu katika ukurasa wa 9]

      “Msihangaike juu ya kitu chochote, bali katika kila jambo kwa sala na dua . . . , maombi yenu na yajulishwe Mungu; na amani ya Mungu . . . itailinda mioyo yenu na nguvu zenu za akili.”—Wafilipi 4:6, 7

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      NJIA ZA KUBORESHA AFYA YAKO

      Mazoezi yanaweza “kuboresha hisia zako kwa muda na kukusaidia kutuliza mshuko wa moyo,” kinasema kitabu Managing Your Mind—The Mental Fitness Guide. Pia kubadili jinsi unavyokula na mazoea yako, ya kimwili na ya kiakili, kunaweza pia kukusaidia. Fikiria mfano wa Valerie, ambaye alitendewa vibaya alipokuwa mtoto. Alikuwa mraibu wa dawa 12 hivi za kitiba. Hata hivyo, alifaulu kuacha zoea hilo na kuishi maisha ya kawaida. Siri ilikuwa nini?

      Badala ya kutazama televisheni na kusoma vitabu vya hadithi vyenye kutiliwa shaka, Valerie alisitawisha ratiba nzuri ya kujifunza Biblia na akatenga wakati wa kusoma vichapo vinavyotegemea Biblia vinavyochapishwa na Mashahidi wa Yehova, kutia ndani gazeti hili. Pia alisali bila kukoma ili apate nguvu kutoka kwa Mungu, akaomba msaada kutoka kwa kutaniko la Kikristo, na akatumia wakati wake mwingi akifanya mambo yanayofaa kama vile kuwaambia wengine kuhusu ujumbe wa Biblia wenye kufariji. Zaidi ya hayo, alibadili sana chakula alichokuwa akila ambacho kilitia ndani vyakula visivyo na lishe. Matokeo yalikuwa kwamba alipona haraka hivi kwamba hata madaktari walishangaa. Hajatumia dawa vibaya kwa miaka mingi sasa.b

      [Maelezo ya Chini]

      b Ikiwa unatumia dawa kwa ajili ya ugonjwa wa kushuka moyo, wa kubadilika-badilika kwa hisia, au ugonjwa mwingine wa akili, hali yako si sawa na ya Valerie. Kwa hiyo, usifanye mabadiliko yoyote bila kuwasiliana na daktari.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki