-
Moldova2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
Msukosuko wa Siku za Kale Nchini Moldova
Zamani, njia kuu ya kuelekea Ulaya ilipitia nchi hiyo iliyo kati ya Mto Dniester na Prut, ambayo kwa mamia ya miaka iliitwa Bessarabia na Moldavia. Kutoka mwaka wa 1000 K.W.K. hadi mwaka wa kwanza K.W.K., eneo hilo lilikuwa sehemu ya Skithia. Baadaye, Milki ya Roma ilitawala nchi hiyo kwa kiasi fulani. Ilivamiwa pia na watu kama vile Wagothi, Wahuni, na Waavari. Katika karne ya 13 na 14, Moldavia ilitawaliwa na Waturuki, na katika karne ya 16 ikawa sehemu ya Milki ya Uturuki. Katika Mkataba wa Bucharest wa mwaka wa 1812, Waturuki walisalimisha Bessarabia na nusu ya Moldavia kwa Warusi, na eneo hilo lote likaitwa Bessarabia.
Bessarabia ikawa sehemu ya Rumania mwaka wa 1918. Hata hivyo, ilikuwa sehemu ya miliki ya Urusi kwa muda mfupi katika mwaka wa 1940, na tena katika mwaka wa 1944. Chini ya utawala wa Muungano wa Sovieti, eneo hilo liliitwa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Sovieti ya Moldavia (SSR). Utawala wa Kikomunisti wa Sovieti ulipoanguka hatimaye, SSR ya Moldavia ilikataa utawala wa Sovieti na kuwa nchi huru ya Jamhuri ya Moldova, Agosti 27, 1991.a Jiji la Chisinau, lililokuwa Kishinev, ndilo jiji kuu la Moldova.
Idadi ya watu iliongezeka sana nchini Moldova katika miaka ya 1960, lakini tangu miaka ya 1970 ongezeko hilo limepungua. Kwa sasa kuna watu milioni 4.3 hivi nchini humo. Wakazi wengi wa Moldova hufanya kazi katika mashamba ya mizabibu na viwanda vya divai, na asilimia 3 ya divai yote ulimwenguni inatengenezwa Moldova. Divai kutoka Moldova inapendwa sana Urusi na Ulaya Mashariki. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 71.) Lakini nchini Moldova, kuna shamba lingine kubwa sana la mizabibu ambalo hutoa mazao bora, yaani, sifa kwa Yehova.
-
-
Moldova2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
a Jina Moldova litatumiwa katika masimulizi haya badala ya jina Bessarabia na Moldavia, ila tunapozungumzia kipindi ambapo jina lingine lilitumiwa. Ni vizuri kukumbuka kwamba mipaka ya Moldova ya kisasa si sawa na mipaka ya nchi ya kale ya Bessarabia na Moldavia. Kwa mfano, eneo fulani la Bessarabia liko Ukrainia, na sehemu ya Moldavia iko Rumania.
-