Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Moldova
    2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
    • Maafisa Watenda Kinyama

      Mambo yaliyowapata Dumitru Gorobeţ na Cazimir Cislinschii yanaonyesha kwamba mara nyingi upinzani dhidi ya kazi ya kuhubiri ulichochewa na maafisa waliowachukia Mashahidi na waliokuwa waumini washupavu wa Kanisa la Othodoksi. Dumitru na Cazimir walijifunza kweli ya Biblia katika kijiji cha Tabani. Muda si muda, walijulikana sana na kupendwa na ndugu kwa sababu ya sifa zao nzuri na bidii yao katika utumishi. Mwaka wa 1936, walikamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi katika mji wa Khotin (sasa mji huo uko Ukrainia).

      Kwanza, polisi waliwapiga Dumitru na Cazimir kikatili. Kisha wakajaribu kuwalazimisha wafanye ishara ya msalaba. Lakini walisimama imara licha ya kupigwa tena na tena. Hatimaye, polisi walisalimu amri. Hata waliwaruhusu Dumitru na Cazimir kurudi nyumbani. Lakini ndugu hao waaminifu walivumilia magumu mengi zaidi chini ya utawala wa Wafashisti na Wakomunisti kwa ajili ya habari njema. Dumitru alikufa mapema mwaka wa 1976 huko Tomsk, Urusi, na Cazimir alikufa Novemba 1990 huko Moldova.

  • Moldova
    2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
    • Majaribu Makali Chini ya Utawala wa Wafashisti

      Punde si punde, serikali ya Kifashisti ya Antonescu, iliyoshirikiana na Hitler na muungano wa Ujerumani, Italia, na Japani, ilijaribu kuvunja uaminifu wa Mashahidi wa Yehova kwa kutumia nguvu. Fikiria kisa cha Anton Pântea aliyezaliwa mwaka wa 1919. Anton alijifunza kweli alipokuwa kijana na alikuwa na bidii katika kazi ya kuhubiri nyumba kwa nyumba. Alikuwa karibu kupigwa mara kadhaa, lakini aliepuka jambo hilo kwa muda kwa kutetea kijasiri haki ya kusema juu ya imani yake akiwa raia wa Rumania. Hata hivyo, hatimaye polisi walimkamata. Maafisa Wafashisti walimburuta hadi kwenye kituo cha polisi, wakampiga usiku kucha, kisha, wakamwachilia. Ndugu Pântea ana umri wa miaka 84 sasa na bado ameazimia kumtumikia Yehova kwa uaminifu.

      Mtu mwingine mwaminifu ni Parfin Palamarciuc aliyejifunza kweli ya Biblia huko Moldova katika miaka ya 1920. Yeye pia alikuwa mtangazaji mwenye bidii wa habari njema. Mara nyingi, alihubiri katika miji na vijiji kuanzia Chernovtsy hadi Lvov huko Ukrainia bila kurudi nyumbani kwa majuma kadhaa. Kwa sababu Parfin alikataa kujiunga na jeshi, Wafashisti walimkamata mwaka wa 1942 na kumfikisha mbele ya mahakama ya jeshi huko Chernovtsy.

      Nicolae, mwana wa Parfin, alisema hivi juu ya matukio hayo: “Ndugu 100 walihukumiwa kifo katika mahakama hiyo. Walikuwa wauawe mara moja baada ya kuhukumiwa. Maafisa waliwakusanya ndugu hao na kuwachagua ndugu kumi ambao wangepigwa risasi kwanza. Lakini hao kumi walilazimishwa kuchimba kwanza makaburi yao, huku wale wengine 90 wakitazama. Lakini kabla ya kuwapiga risasi, maafisa waliwapa nafasi nyingine kukana imani yao na kujiunga na jeshi. Wawili walikana imani; wanane wakapigwa risasi. Kisha wengine kumi wakapangwa katika mstari. Lakini kabla ya kupigwa risasi walilazimishwa kuwazika waliouawa.

      “Ndugu walipokuwa wakifukia makaburi, afisa mmoja wa cheo cha juu aliwasili. Aliuliza ni Mashahidi wangapi waliokana imani. Alipoambiwa ni wawili tu, alisema kwamba kama watu 80 wangehitaji kufa ili 20 wajiunge na jeshi, basi ni afadhali wale 92 waliobaki wapelekwe kufanya kazi katika kambi. Kwa hiyo, hukumu ya kifo ilibadilishwa kuwa kifungo cha miaka 25 katika kambi ya kazi ngumu. Hata hivyo, yapata miaka mitatu baadaye, jeshi la Sovieti liliwaweka Mashahidi huru kutoka katika kambi za Rumania. Baba yangu aliokoka magumu hayo na mengine mengi. Alikuwa mwaminifu kwa Yehova hadi kifo chake mwaka wa 1984.”

      Je, Ni Kosa Kukataa Desturi za Kanisa la Othodoksi?

      Vasile Gherman alikuwa kijana, na mke wake alikuwa amejifungua mtoto wa kike wakati Wafashisti walipomkamata Vasile mnamo Desemba 1942. Vasile alishtakiwa kwa “makosa” mawili, kukataa kujiunga na jeshi na pia kukataa binti yake abatizwe katika Kanisa la Othodoksi. Anasema hivi kuhusu kesi hiyo: “Kesi yangu na kesi za ndugu wengine waaminifu 69 zilisikilizwa katika mahakama ya jeshi huko Chernovtsy Februari 1943. Kabla ya kuhukumiwa, wenye mamlaka walitulazimisha kutazama wahalifu sita wakiuawa. Kwa hiyo, tulikuwa na hakika kwamba tungehukumiwa kifo.

      “Tulizungumzia jambo hilo na kuazimia kusimama imara katika imani na kujitahidi sana kudumisha shangwe hadi kesi imalizike. Kwa msaada wa Yehova tulifaulu. Kama tulivyotarajia, sisi sote 70 tulihukumiwa kifo, tulihisi kwamba tulikuwa tukiteswa kwa ajili ya uadilifu. Hakuna hata mmoja kati yetu aliyevunjika moyo, na jambo hilo liliwaudhi sana adui zetu. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba badala ya kutupiga risasi, wenye mamlaka walibadili hukumu yetu kuwa kifungo cha miaka 25 katika kambi ya kazi ngumu huko Aiud, Rumania. Lakini baada ya miezi 18 tu, mnamo Agosti 1944, jeshi la Wasovieti liliwaweka huru wafungwa waliokuwa katika kambi hiyo.”

      Mwaka wa 1942, Wafashisti waliwaandikisha watu 800 hivi kutoka kijiji cha Şirăuţi, Moldova, katika jeshi la Jenerali Antonescu. Kati yao kulikuwa na Mashahidi kadhaa kutia ndani Nicolae Anischevici. Nicolae anasema hivi: “Walipokuwa wakituandikisha, polisi walituamuru tushiriki katika sherehe fulani ya kidini. Sisi Mashahidi tulikataa. Tulikataa pia kubeba silaha. Kwa hiyo, polisi walitushutumu kuwa Wakomunisti na wakatukamata. Hata hivyo kabla ya kutufunga, walituruhusu kueleza sababu ya kutojiunga na jeshi.

      “Kesho yake tulihamishwa hadi Briceni, kitovu cha mahakama ya wilaya hiyo. Tulivuliwa mavazi yote na miili yetu ikachunguzwa kabisa. Kisha kasisi mwenye cheo cha juu jeshini akatuhoji. Alikuwa mwenye fadhili, alielewa kwamba uamuzi wetu ulitegemea dhamiri, na alipanga tupewe chakula. Na zaidi ya hayo, aliandika kwamba tulikataa kujiunga na jeshi kwa sababu tunamwamini Yesu.

      “Kutoka Briceni tulipelekwa hadi kwenye kituo cha polisi huko Lipcani. Huko, polisi walitupiga kikatili hadi usiku. Kisha wakatufunga katika chumba fulani pamoja na ndugu wengine wawili na mwanamke mmoja. Baadaye tuligundua kwamba mwanamke huyo alikuwa mpelelezi. Tulipigwa kila siku, kwa siku kadhaa. Hatimaye, mimi nilipelekwa Chernovtsy ili nihukumiwe katika mahakama ya jeshi. Nilipewa wakili ambaye alinisaidia sana nikiwa huko. Hata hivyo, afya yangu ilikuwa imezorota sana kwa sababu ya mateso hivi kwamba wakuu wa jeshi walifikiri ningekufa. Mwishowe waliamua kunipeleka nyumbani bila kunihukumu.”

      Dada Jasiri Wadumisha Uaminifu

      Dada pia walikabili mateso kwa sababu ya hasira ya Wafashisti. Mmojawapo ni Maria Gherman (yeye si mtu wa ukoo wa Vasile Gherman lakini walikuwa katika kutaniko moja). Maria alipokamatwa mwaka wa 1943, alipelekwa kwenye kituo cha polisi huko Balasineşti. Anasema hivi: “Polisi walinikamata kwa sababu nilikataa kwenda katika kanisa la Othodoksi. Kwanza walinihamisha hadi Lipcani, Moldova, kisha nikapelekwa Chernovtsy, Ukrainia, ambako nilihukumiwa.

      “Hakimu aliniuliza kwa nini nilikataa kwenda kanisani. Nilimwambia kwamba ninamwabudu Yehova tu. Mimi na dada wengine 20 tulihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa sababu ya ‘kosa’ hilo. Baadhi yetu tuliingizwa kwenye chumba kidogo sana pamoja na wafungwa wengine 30. Hata hivyo, mchana nilifanya kazi katika nyumba za matajiri. Watu hao walinitendea vizuri kuliko maafisa wa gereza, angalau walinipa chakula cha kutosha!

      “Baada ya muda, tulifaulu kuwasiliana na ndugu waliokuwa katika sehemu nyingine ya gereza. Jambo hilo lilileta faida nyingi kwa kuwa tuliweza kuwasaidia ndugu kupata chakula cha kiroho na cha kimwili pia.”

      Mara tu baada ya mateso ya Wafashisti kukoma, ndugu hao waaminifu pamoja na Mashahidi wengine wengi huko Moldova, walikabili shambulizi lingine la imani yao chini ya serikali ya Kikomunisti ya Urusi iliyotawala eneo hilo baada ya Wafashisti.

      Mbinu ya Wasovieti ya Kuwahamisha Watu

      Ujerumani ilipoelekea kushindwa vitani, baadhi ya maafisa wa serikali ya Rumania iliyoongozwa na Mfalme Michael, walipindua serikali ya Antonescu mwaka wa 1944. Kisha Rumania ilivunja uhusiano wake na muungano wa Ujerumani, Italia, na Japani na ikajiunga na Urusi. Mwaka uo huo, jeshi la Sovieti lilitwaa tena eneo hilo, kwa hiyo, Moldova ikawa tena sehemu ya Muungano wa Sovieti, na kuitwa SSR ya Moldavia.

      Mwanzoni, watawala Wakomunisti wa Moldova hawakuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova. Lakini amani hiyo haikudumu kwa muda mrefu. Punde msimamo wa Kikristo wa kutounga mkono mambo ya siasa ulipingwa vikali tena, kutia ndani msimamo wa Mashahidi wa kukataa kupiga kura katika uchaguzi wa chama. Chini ya utawala wa Sovieti, kutounga mkono siasa hakukubaliwa hata kidogo. Kwa hiyo, serikali ilinuia kutatua tatizo hilo kwa kuwahamisha Mashahidi wa Yehova na watu wengine “wasiotakiwa” kuanzia mwaka wa 1949.

      “Uamuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Chama cha Wakomunisti” kuwahusu watu kutoka SSR ya Moldavia ambao wangehamishwa ulionyeshwa katika hati fulani rasmi. Baadhi ya watu hao walikuwa “wamiliki wa mashamba, wenye biashara kubwa, watu walioshirikiana na wavamizi Wajerumani, wale waliowasaidia polisi wa Ujerumani na Rumania, wanachama wa vyama na mashirika ya Wafashisti, shirika fulani la Wafinland lisilokuwa la Kisoshalisti, waumini wa madhehebu yasiyo halali, na pia familia za watu hao wote.” Wote hao walipaswa kupelekwa magharibi mwa Siberia hadi “wakati usiojulikana.”

      Uhamisho mwingine ulianza mwaka wa 1951, lakini wakati huo ni Mashahidi wa Yehova pekee waliohamishwa. Stalin mwenyewe aliagiza uhamisho huo ulioitwa Operation North. Zaidi ya familia 720 za Mashahidi, yaani, watu 2,600 hivi, walihamishwa kutoka Moldova hadi Tomsk, magharibi mwa Siberia, umbali wa kilometa 4,500 kutoka Moldova.

      Maagizo ya serikali yalisema kwamba watu walipaswa kupewa nafasi ya kutosha kufunga virago vyao kabla ya kupelekwa kwenye magari-moshi. Na zaidi ya hayo, mabehewa yalikuwa “yatengenezwe vizuri ili yafae kuwasafirisha wanadamu.” Lakini maagizo hayo hayakutiwa maanani.

      Kwa kawaida, wanajeshi na maafisa wanane hivi walifika nyumbani kwa Mashahidi usiku wa manane. Waliwaamsha na kuwaonyesha barua ya uhamisho. Waliwapa saa chache tu kufunga virago vyao kabla ya kuwapeleka kwenye magari-moshi.

      Walisafirishwa kwa mabehewa ya mizigo. Watu 40 hivi walisongamana katika kila behewa kwa majuma mawili ya safari. Hakukuwa na viti na baridi iliingia kwenye mabehewa. Katika pembe moja ya behewa kulikuwa na shimo sakafuni ambalo lilitumiwa kama choo. Kabla ya kuwahamisha ndugu, maafisa walipaswa kuandika orodha ya mali za kila mtu. Hata hivyo, mara nyingi waliorodhesha tu vitu duni; vitu vyenye thamani “vilipotea” tu.

      Hata hivyo, licha ya magumu yaliyowapata, ndugu hawakupoteza furaha yao ya Kikristo. Magari-moshi yaliyowasafirisha Mashahidi yalipofika kwenye vituo vya gari-moshi, sauti za nyimbo za Ufalme zilisikika kutoka ndani ya mabehewa. Hivyo, ndugu katika kila gari-moshi walijua kwamba hawakuwa peke yao, bali walikuwa wakihamishwa pamoja na mamia ya Mashahidi wenzao. Kuwaona wengine wakidumisha furaha katika hali hizo ngumu kuliwatia moyo na kuwaimarisha wote wadumishe uaminifu wao kwa Yehova katika hali yoyote ile.—Yak. 1:2.

      Imani Inayostahili Kuigwa

      Ivan Mikitkov ni mmojawapo wa watu wa Moldova waliopelekwa uhamishoni Siberia. Ivan alikamatwa kwa mara ya kwanza huko Moldova pamoja na Mashahidi wengine mwaka wa 1951, na kupelekwa uhamishoni Tomsk. Alipewa kazi ya kukata miti katika msitu mkubwa wa Siberia unaoitwa taiga. Ingawa hakuishi katika kambi ya kazi ngumu, bado alikuwa chini ya vizuizi, na polisi wa siri walipeleleza utendaji wake wote. Hata hivyo, yeye na ndugu zake wa kiroho waliwahubiria wengine kila walipopata nafasi.

      Ivan anasema hivi: “Tulipanga kuwe na makutaniko katika mazingira hayo magumu. Hata tulianza kunakili vitabu. Muda si muda, watu kadhaa ambao tuliwahubiria walikubali kweli na kubatizwa. Lakini, hatimaye wenye mamlaka walitambua utendaji wetu na wakapeleka baadhi yetu kwenye kambi za kazi ngumu.

      “Mimi na Mashahidi wenzangu Pavel Dandara, Mina Goraş, na Vasile Şarban, tulihukumiwa kifungo cha miaka 12 katika kambi ya kazi ngumu chini ya usimamizi mkali. Wenye mamlaka walifikiri kwamba vifungo hivyo vikali vingewatisha wengine wasihubiri, lakini mbinu hiyo haikufua dafu. Ndugu zetu waliendelea kuhubiri kotekote walikopelekwa. Niliachiliwa mwaka wa 1966, baada ya kukamilisha kifungo changu. Nilirudi Tomsk na kukaa huko kwa miaka mitatu.

      “Mwaka wa 1969, nilihamia Bonde la Donets ambako nilikutana na Maria, dada mwaminifu na mwenye bidii ambaye nilimwoa. Nilikamatwa tena mwaka wa 1983. Wakati huo nilihukumiwa adhabu maradufu, kifungo cha gereza cha miaka mitano, na uhamisho wa miaka mitano. Bila shaka nilihisi kwamba hukumu hiyo ilikuwa ngumu zaidi kuliko ile ya kwanza kwa sababu wakati huu ningetengana na mke na mtoto wangu ambao pia wangepatwa na magumu. Ninashukuru kwamba niliachiliwa mwaka wa 1987, baada ya Mikhail Gorbachev kuwekwa kuwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Sovieti. Niliruhusiwa kurudi Ukrainia na hatimaye Moldova.

      “Niliporudi Bălţi, jiji la pili kwa ukubwa nchini Moldova, jiji hilo lilikuwa na wahubiri 370 na makutaniko matatu. Leo jiji hilo lina zaidi ya wahubiri 1,700 na makutaniko 16!”

      “Je, Unataka Kufa Kama Vasile?”

      Wasimamizi wa kambi na wapelelezi wa KGB (Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti) walitunga mbinu za kinyama ili kuvunja uaminifu wa ndugu. Constantin Ivanovici Şobe anasimulia kile kilichompata babu yake Constantin Şobe: “Mwaka wa 1952, Babu alikuwa amefungwa katika kambi moja ya kazi ngumu katika wilaya ya Chita, mashariki ya Ziwa Baikal huko Siberia. Maafisa wa kambi walitisha kumpiga risasi yeye na Mashahidi wengine wasipokana imani yao.

      “Kwa sababu ndugu hao walikataa kukana imani yao, maafisa waliwakusanya nje ya kambi karibu na msitu. Giza lilikuwa likiingia walipompeleka Vasile, rafiki wa karibu zaidi wa Babu, msituni na kutangaza kwamba watampiga risasi. Ndugu walingoja wakiwa na wasiwasi. Punde walisikia bunduki zikifyatuliwa.

      “Askari walirudi na kumpeleka Shahidi wa pili, babu yangu, msituni. Baada tu ya kuingia msituni, walifika kwenye uwanja fulani wenye makaburi kadhaa yaliyokuwa yamechimbwa, na moja lilikuwa limefukiwa. Afisa mkuu alisema hivi akimwangalia Babu na kuelekeza kidole kwenye kaburi lililofukiwa: ‘Je, unataka kufa kama Vasile, au unataka kurudi nyumbani kwa familia yako ukiwa mtu huru? Una dakika mbili kufanya uamuzi.’ Babu hakuhitaji dakika mbili. Mara moja alijibu: ‘Vasile, mliyempiga risasi, alikuwa rafiki yangu kwa miaka mingi. Sasa ninatarajia kumwona tena atakapofufuliwa katika ulimwengu mpya. Nina hakika kwamba nitakuwa katika ulimwengu mpya pamoja na Vasile. Lakini, vipi wewe?’

      “Afisa huyo hakutarajia jibu hilo. Alimrudisha babu na wale wengine kambini. Hata hivyo, babu hakuhitaji kungoja hadi ufufuo ili kumwona Vasile tena. Hiyo ilikuwa mbinu mbovu iliyokusudiwa kuvunja uaminifu wa ndugu.”

      Mbinu ya Wakomunisti ya Kueneza Uwongo Haikufaulu

      Wakomunisti walichapisha vitabu na vijitabu, na kutengeneza sinema zilizoeneza uwongo juu ya watu wa Mungu ili kuwachochea watu wawachukie na kuwashuku Mashahidi wa Yehova. Kijitabu kimoja kilikuwa na kichwa Double Bottom. Kijitabu hicho kilipewa jina hilo kwa sababu ndugu walikuwa wakitengeneza sehemu ya siri ya kufichia vitabu katika masanduku ya nguo na mikoba yao. Nicolai Voloşanovschi anakumbuka jinsi kamanda wa kambi alivyojaribu kutumia kijitabu hicho kumfedhehesha mbele ya wafungwa wengine.

      Nicolai anasema hivi: “Kamanda huyo alikusanya wafungwa wote katika jengo moja kambini. Kisha akasoma sehemu mbalimbali katika kijitabu hicho, kutia ndani sehemu zilizokuwa na maelezo ya uwongo kunihusu. Alipomaliza, nilimwomba ruhusa kuuliza maswali machache. Bila shaka kamanda huyo alikubali ombi langu akidhani kwamba angepata nafasi ya kunifanyia mzaha.

      “Nilimwuliza kamanda huyo ikiwa anakumbuka aliponihoji mara ya kwanza nilipokuja kambini. Alisema anakumbuka mahojiano hayo. Kisha nikamwuliza kama anakumbuka maswali ambayo aliniuliza kuhusu nchi niliyozaliwa, uraia wangu, na kadhalika alipokuwa akijaza fomu za kuniandikisha kambini. Tena alijibu ndiyo. Hata aliwaambia wale waliokuwa wakisikiliza majibu niliyotoa wakati huo. Kisha nikamwomba aeleze yale aliyoandika katika fomu hizo. Alikiri kwamba yale aliyoandika hayakupatana na majibu yangu. Niliwatazama wasikilizaji na kusema: ‘Mwaona, kijitabu hiki kiliandikwa kwa njia iyo hiyo.’ Wafungwa walipiga makofi, na kamanda akatoka kwa hasira.”

      Njama ya Kusababisha Migawanyiko ili Kushinda

      Katika miaka ya 1960, viongozi wa Sovieti walioudhika walitunga mbinu mpya za kuharibu umoja wa Mashahidi wa Yehova. Kitabu Upanga na Ngao (The Sword and the Shield), kilichochapishwa mwaka wa 1999, kinazungumzia baadhi ya ripoti za KGB, ambazo zilikuwa za siri wakati huo, zilizopatikana katika hifadhi za nyaraka za serikali. Ripoti hiyo inasema: “Maafisa wakuu wa KGB ambao waliongoza ‘pambano dhidi ya Mashahidi wa Yehova’ walifanya mkutano mnamo Machi 1959, na kuamua kwamba mbinu bora ingekuwa ‘kuendelea kuwakandamiza [Mashahidi wa Yehova] kwa kusababisha migawanyiko.’ Maafisa wa KGB waliazimia kusababisha migawanyiko miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, kuwavunja moyo, kuwavunjia heshima, na vilevile kuwafunga viongozi wao wakuu kwa mashtaka ya uwongo.”

      Mbinu za “kusababisha migawanyiko” zilihusisha jitihada za pamoja za kuwafanya ndugu wawashuku ndugu wenzao kotekote katika Muungano wa Sovieti. Ili kutimiza lengo hilo, KGB ilieneza uvumi kwamba ndugu kadhaa walioongoza walikuwa wameanza kushirikiana na KGB. Wapelelezi wa KGB walieneza uvumi huo kwa ujanja sana hivi kwamba Mashahidi wengi walianza kuwashuku ndugu wenzao.

      Mbinu nyingine ya KGB ilikuwa kuwazoeza wapelelezi kujifanya kuwa Mashahidi wa Yehova “wanaohubiri kwa ukawaida,” kisha wangejaribu kustahili kupata madaraka katika tengenezo. Bila shaka, wapelelezi hao walikuwa wakiwasiliana na KGB. Wapelelezi wa KGB pia waliwaendea kisiri Mashahidi wa kweli na kujaribu kuwahonga kwa kiasi kikubwa cha pesa ili waunge KGB mkono.

      Jambo la kusikitisha ni kwamba mbinu hizo zilifaulu kwa kadiri fulani kuharibu umoja wa ndugu, kutia ndani ndugu wa Moldova. Hivyo, polepole ndugu walianza kuwashuku ndugu wenzao. Baadhi ya ndugu walijitenga na tengenezo na kuanzisha kikundi ambacho kilijulikana kama upinzani.

      Kabla ya matukio hayo, ndugu katika Muungano wa Sovieti walitumia neno “njia,” walipokuwa wakirejezea tengenezo la Yehova, chakula cha kiroho, na ndugu walioongoza. Sasa ndugu walichanganyikiwa na kutilia shaka njia hiyo. Walitatuaje vurugu hiyo? Kwa kushangaza, Serikali ya Sovieti iliwasaidia. Ndiyo, wale waliotunga njama hiyo walisaidia kutatua matatizo waliyosababisha. Vipi?

      Walipuuza Roho ya Mungu

      Mapema katika miaka ya 1960, wenye mamlaka wa Sovieti waliwafunga “viongozi” wengi wa Mashahidi kutoka sehemu zote za Muungano wa Sovieti katika kambi moja iliyokuwa umbali wa kilometa 150 kutoka jiji la Saransk katika jamhuri ya Mordvinia, magharibi mwa Urusi. Kabla ya hapo, ndugu hawakuweza kuwasiliana vizuri kwa sababu walikaa mbali sana na wenzao, hivyo kutoelewana kulitokea kwa urahisi. Lakini sasa wale wafuasi wa kikundi cha upinzani, na wale wasiojiunga na kikundi hicho, walikuwa pamoja. Kwa hiyo, waliweza kuongea ana kwa ana na kutofautisha kweli na uwongo. Kwa nini wenye mamlaka waliwaweka ndugu hao wote pamoja? Inaonekana walifikiri kwamba ndugu wangezozana, na hivyo kuzidisha migawanyiko iliyokuwapo. Hata hivyo, mbinu hiyo iliyopangwa kwa werevu, haikufua dafu kwa sababu walioitunga walipuuza roho ya Yehova inayoleta umoja.—1 Kor. 14:33.

      Ndugu mmoja aliyepelekwa Mordvinia ni Gheorghe Gorobeţ. Anasema hivi: “Muda mfupi baada ya kukamatwa na kupelekwa gerezani, ndugu mmoja aliyekuwa mfuasi wa kikundi cha upinzani alifungwa pamoja nami. Alipoona kwamba ndugu walioongoza bado walikuwa wamefungwa, alishangaa, kwa kuwa alikuwa ameambiwa kwamba sisi sote tuliachiliwa huru na tulikuwa tukiishi raha mustarehe na kupewa pesa na KGB!”

      Ndugu Gorobeţ anaongeza hivi: “Katika mwaka wangu wa kwanza gerezani, zaidi ya watu 700 walifungwa kwa sababu za kidini. Wengi wao walikuwa Mashahidi wa Yehova. Sote tulifanya kazi katika kiwanda kimoja na tulikuwa na nafasi ya kuongea na wale waliokuwa wamejiunga na kikundi cha upinzani. Hivyo, mambo mengi yaliyosababisha migawanyiko yalitambuliwa katika mwaka wa 1960 na 1961. Hatimaye, mwaka wa 1962, ndugu wa halmashauri ya nchi waliosimamia kazi katika Muungano wa Sovieti waliandika barua wakiwa katika kambi ya kazi ngumu. Barua hiyo ilitumiwa makutaniko yote katika Muungano wa Sovieti na matatizo mengi yaliyosababishwa na mbinu za KGB yalitatuliwa.”

      Kutambua Njia ya Kweli

      Ndugu Gorobeţ alirudi Moldova mara alipoachiliwa kutoka katika kambi ya kazi ngumu mnamo Juni 1964. Alipowasili Tabani, aligundua kwamba Mashahidi wengi huko bado walikuwa wamechanganyikiwa kuhusu njia ambayo Yehova anatumia kuwalisha na kuwaongoza watu Wake. Ndugu kadhaa walisoma Biblia peke yake.

      Halmashauri ya ndugu watatu waliokomaa kiroho iliwekwa ili kurekebisha hali hiyo. Kwanza walitembelea makutaniko yaliyokuwa kaskazini mwa Moldova, ambako Mashahidi wengi waliishi. Ndugu walipoona kwamba ndugu hao na waangalizi wengine Wakristo bado walikuwa waaminifu licha ya kuteswa sana, walisadikishwa kwamba bado Yehova anatumia tengenezo lilelile lililowafundisha kweli.

      Mwishoni mwa miaka ya 1960, KGB ilitambua kwamba kazi ya kuhubiri ilikuwa ikiendelea licha ya mateso na mbinu nyingine. Kitabu Upanga na Ngao kinaeleza hatua ambayo KGB ilichukua: “Maafisa wa [KGB] walishikwa na wasiwasi waliposikia kwamba hata ndani ya kambi za kazi ngumu, ‘viongozi wa Mashahidi wa Yehova walidumisha imani yao inayopinga Ukomunisti na waliendelea kufanya kazi ya Yehova.’ Maafisa wa KGB ambao walikuwa wakitunga njama dhidi ya Mashahidi wa Yehova walifanya mkutano [huko Chisinau] mnamo Novemba 1967 ili kuzungumzia mbinu mpya za ‘kuzuia kazi ya Mashahidi’ na ‘mafundisho yao yanayopinga Ukomunisti.’”

      Kunyanyaswa na Ndugu Waasi

      Ni jambo la kuhuzunisha kwamba baadhi ya Mashahidi walidanganywa na “mbinu [hizo] mpya” na hivyo kutimiza kabisa lengo la KGB. Baadhi yao walivunja uaminifu wao kwa sababu ya pupa au woga; wengine walikuwa ndugu waliotengwa ambao waliwachukia Mashahidi. Wenye mamlaka walianza kuwatumia ili kuvunja uaminifu wa Mashahidi waaminifu. Mashahidi waliokuwa wamevumilia vifungo vya gereza na kazi ngumu katika kambi walisema kwamba kunyanyaswa na ndugu waliotengwa, ambao baadhi yao walikuwa waasi-imani, lilikuwa jaribu gumu kuliko majaribu mengine yoyote ambayo walipata.

      Waasi-imani wengi walikuwa wafuasi wa kikundi cha upinzani. Mwanzoni, kikundi hicho kilikuwa na Mashahidi kadhaa waliokuwa wamechanganyikiwa kwa sababu ya uwongo ulioenezwa na KGB. Lakini baadhi ya wale ambao bado walishirikiana na kikundi hicho mwishoni mwa miaka 1960 walionyesha roho ya jamii ya mtumwa mwovu. Kwa sababu walipuuza onyo la Yesu, walianza “kuwapiga watumwa [wenzao].”—Mt. 24:48, 49.

      Hata hivyo, ijapokuwa maafisa wa KGB na wafuasi wao walijitahidi kwa muda mrefu kusababisha migawanyiko ili kuwashinda watu wa Mungu, mbinu yao haikufua dafu. Mapema katika miaka ya 1960, ndugu waaminifu walipoanza kurudisha umoja katika tengenezo nchini Moldova, ndugu wengi nchini humo walikuwa wamejiunga na kikundi cha upinzani. Lakini kufikia mwaka wa 1972, karibu wote walikuwa wakifanya kazi kwa uaminifu pamoja na tengenezo la Yehova.

      Mtesaji Aliyefurahia Kusoma Gazeti Letu

      Ndugu waaminifu waliobaki Moldova wakati wa utawala wa Kikomunisti waliendelea kufanya kazi ya kuhubiri kwa kadiri walivyoweza. Waliwahubiria watu wa familia zao, marafiki, wanashule na wafanyakazi wenzao. Lakini walihubiri kwa tahadhari sana kwa sababu maafisa wengi wa chama nchini Moldova walikuwa Wakomunisti washupavu. Hata hivyo, si Wakomunisti wote waliowadharau Mashahidi wa Yehova.

      Simeon Voloşanovschi anasema hivi: “Polisi walipekua nyumba yetu na kutunyang’anya magazeti na vitabu vingi, ambavyo afisa mkuu aliorodhesha. Baadaye afisa huyo alirudi na orodha hiyo na kuniomba nihakikishe kwamba magazeti na vitabu vyote viliorodheshwa kwa usahihi. Nilipochunguza orodha hiyo, niliona kwamba gazeti moja la Mnara wa Mlinzi, ambalo linazungumzia jinsi ya kufanya maisha ya familia yawe yenye furaha zaidi, halikuwa limeorodheshwa. Nilimwuliza afisa huyo juu ya gazeti hilo. Alijibu hivi kwa aibu: ‘Nililipeleka nyumbani, na tulilisoma pamoja na familia yangu.’ Kisha nikamwuliza, ‘Lakini mlilipenda?’ ‘Bila shaka, tulilipenda sana!’ akajibu.”

      Upinzani Wapungua, Ongezeko Laendelea

      Wakomunisti waliacha kuwakamata na kuwahamisha watu wa Yehova katika miaka ya 1970. Hata hivyo, mara kwa mara ndugu walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa sababu ya kuhubiri au kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Lakini hawakuhukumiwa vifungo vikali sana.

  • Moldova
    2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
    • [Sanduku katika ukurasa wa 83-85]

      Wakristo Waliodumisha Msimamo wa Kutokuwamo

      George Vacarciuc: Ndugu Vacarciuc alilelewa na wazazi waliokuwa Mashahidi wa Yehova. Mnamo Desemba 1942 aliitwa na Wafashisti ajiandikishe katika jeshi. Kwa sababu alikataa kujiunga na jeshi, alifungwa katika chumba chenye giza tititi kwa siku 16 na kupewa chakula kidogo sana. Wenye mamlaka walimwita tena, na bila kumwambia hukumu yake, walimwahidi kwamba hukumu hiyo ingefutwa kama angejiunga na jeshi. Alikataa tena.

      George alihukumiwa kifungo cha miaka 25. Lakini aliachiliwa na jeshi la Sovieti Septemba 25, 1944. Hata hivyo, miezi miwili haikupita na Wasovieti wakajaribu tena kumwandikisha jeshini. Kwa sababu hakukubali kutenda kinyume cha dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia, alihukumiwa kifungo cha miaka kumi katika kambi mbalimbali za kazi ngumu. Kwa muda wa mwaka mmoja, familia yake haikujua mahali alipokuwa. Baada ya miaka mitano, Ndugu Vacarciuc aliachiliwa Desemba 5, 1949. Alirudi nyumbani huko Corjeuţi na aliendelea kuwa mwaminifu hadi kifo chake Machi 12, 1980.

      Parfin Goreacioc: Ndugu Goreacioc alizaliwa mwaka wa 1900, na alijifunza kweli ya Biblia katika kijiji cha Hlina kati ya mwaka wa 1925 na 1927. Yeye na ndugu zake, Nicolae na Ion, walifundishwa kweli na Damian na Alexandru Roşu, Wanafunzi wa Biblia wa kwanza katika kijiji hicho.

      Parfin na Mashahidi wengine walikamatwa mwaka wa 1933 na kupelekwa hadi mji wa Khotin, ambako walihojiwa na kutozwa faini kwa sababu ya kuhubiri. Katika mwaka wa 1939, kwa sababu ya uchochezi wa kasisi wa kijiji, Parfin alipelekwa kwenye kituo cha polisi katika kijiji jirani cha Ghilavăţ. Polisi walimlaza kifudifudi kwenye kitanda cha mbao, wakamfunga, na kumpiga tena na tena kwenye nyayo.

      Wafashisti walipotwaa mamlaka, Parfin alikamatwa tena na kupelekwa gerezani. Hata hivyo, mwaka uo huo, Wasovieti walimweka huru, lakini muda mfupi baadaye walimkamata tena kwa sababu alikataa kujiunga na jeshi. Alifungwa Chisinau kwa miezi kadhaa kisha akaachiliwa.

      Wasovieti walimkamata Parfin tena mwaka wa 1947, na kumhukumia adhabu ya uhamisho wa miaka minane kwa sababu ya kuhubiri juu ya Ufalme wa Mungu. Watoto wake walihamishwa hadi Siberia mwaka wa 1951. Lakini hawakujiunga na baba yao wala hawakumwona tena kamwe. Parfin akawa mgonjwa sana alipokuwa uhamishoni na alidumisha uaminifu wake hadi kifo chake mwaka wa 1953.

      Vasile Pădureţ: Ndugu Pădureţ alizaliwa mwaka wa 1920 katika kijiji cha Corjeuţi, na alijifunza kweli mwaka wa 1941 chini ya utawala wa Wafashisti. Kwa hiyo, yeye pia aliteswa na Wafashisti na Wasovieti. Aliwaambia Wasovieti hivi kwa ujasiri: “Sikuwapiga risasi Wakomunisti wala sitawaua Wafashisti.”

      Vasile alihukumiwa kifungo cha miaka kumi katika kambi ya kazi ngumu huko Urusi kwa sababu aliongozwa na dhamiri yake kuchukua msimamo huo unaopatana na Biblia. Hata hivyo, kifungo hicho kilipunguzwa na baada ya miaka mitano, Agosti 5, 1949, alirudi nyumbani. Alipokamatwa kwa mara ya tatu mpango wa kuwahamisha Mashahidi hadi Siberia ulikuwa umeanzishwa. Kwa hiyo, Aprili 1, 1951, Vasile na familia yake walipanda gari-moshi kwenda Siberia. Baada ya kukaa huko kwa miaka mitano, waliruhusiwa kurudi Corjeuţi, Moldova. Vasile alikuwa mwaminifu hadi kifo chake, Julai 6, 2002, wakati masimulizi haya yalipokuwa yakiandikwa.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 89, 90]

      ‘Singebadilisha Utumishi Wangu kwa Chochote Kile’

      Ion Sava Ursoi

      Alizaliwa: 1920

      Alibatizwa: 1943

      Maisha yake: Alitumikia kama mwangalizi wa mzunguko wakati wa utawala wa Wakomunisti.

      Nilizaliwa Caracuşeni, Moldova, na nilijifunza kweli kabla ya Vita vya Pili vya Ulimwengu. Mke wangu alikufa mwaka wa 1942. Wakati wa mazishi yake watu wenye ghasia walinifukuza kutoka makaburini. Kwa nini? Kwa sababu nilikuwa nimeacha dini yangu. Baadaye katika mwaka huo, serikali ya Kifashisti ilijaribu kuniandikisha jeshini. Lakini kwa sababu sikutaka kuunga mkono siasa, nilikataa. Nilihukumiwa kifo, lakini hukumu hiyo ilibadilishwa kuwa kifungo cha miaka 25. Nilihamishwa kutoka kambi moja hadi nyingine. Jeshi la Sovieti lilituweka huru nilipokuwa gerezani huko Craiova, Rumania.

      Lakini mara tu baada ya kuachiliwa, Wakomunisti walinifunga gerezani tena. Walinipeleka Kalinin, Urusi. Miaka miwili baadaye, katika mwaka wa 1946, waliniruhusu kurudi nyumbani, ambako nilisaidia kupanga upya kazi ya kuhubiri. Kisha Wasovieti walinikamata tena mwaka wa 1951. Wakati huu walinihamisha hadi Siberia pamoja na Mashahidi wengine wengi. Sikurudi nyumbani hadi mwaka wa 1969.

      Ninapofikiria maisha yangu, ninakumbuka pindi nyingi ambapo Yehova alinipa nguvu ya kudumisha uaminifu wangu. Singebadilisha utumishi wangu kwa Muumba kwa chochote kile ulimwenguni. Sasa ninapambana na matatizo ya afya na uzee. Lakini tumaini langu thabiti la kuishi katika ulimwengu mpya, wakati mwili wangu utakapokuwa na nguvu za ujana tena, huimarisha azimio langu la kuendelea “kufanya yaliyo mema.”—Gal. 6:9.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 100-102]

      Nina Sababu Nyingi za Kuimba

      Alexandra Cordon

      Alizaliwa: 1929

      Alibatizwa: 1957

      Maisha yake: Alikabili magumu chini ya utawala wa Sovieti na kwa sasa yeye ni mhubiri wa habari njema.

      Ninapenda sana kuimba na jambo hilo lilinisaidia kupata kweli, na baadaye, liliniimarisha kiroho imani yangu ilipojaribiwa. Nilipokuwa kijana katika miaka ya 1940, nilipata kuwajua vijana fulani huko Corjeuţi waliofurahia kuimba nyimbo za Ufalme na kuzungumzia Biblia walipokuwa na nafasi. Kweli za kiroho nilizojifunza katika mazungumzo hayo na katika nyimbo tulizoimba zilinivutia sana.

      Muda si muda, nikawa mhubiri wa habari njema. Mwaka wa 1953, mimi na Mashahidi wengine kumi tulikamatwa kwa sababu ya kuhubiri habari njema. Nilifungwa katika gereza moja huko Chisinau nikingoja kufikishwa mahakamani. Nilidumisha nguvu yangu ya kiroho kwa kuimba nyimbo za Ufalme, jambo ambalo lilimkasirisha askari mmoja. Alisema hivi: “Uko gerezani. Haifai kuimba hapa!”

      Nilimjibu hivi: “Nimeimba maisha yangu yote. Kwa nini niache sasa? Unaweza kunifunga gerezani, lakini huwezi kuifunga midomo yangu kwa kufuli. Moyo wangu u huru, nami nampenda Yehova. Kwa hiyo nina sababu nyingi za kuimba.”

      Nilihukumiwa kifungo cha miaka 25 katika kambi ya kazi ngumu huko Inta karibu na Mzingo wa Aktiki. Katika miezi michache ya kiangazi, mimi na Mashahidi wengine tulifanya kazi msituni. Wakati huo pia, nyimbo za Ufalme ambazo tulijua, zilitusaidia kuwa wenye nguvu kiroho na kuhisi moyoni kwamba tulikuwa huru. Zaidi ya hayo, tofauti na yule askari huko Chisinau, askari huko Inta walitutia moyo tuimbe.

      Nilikaa katika kambi ya Inta kwa miaka mitatu, miezi mitatu, na siku tatu. Kisha, msamaha ulitolewa na nikaachiliwa. Nilienda Tomsk, Urusi, kwa sababu sikuruhusiwa kurudi Moldova. Huko niliungana tena na mume wangu ambaye pia alikuwa amefungwa kwa kipindi fulani. Tulikuwa tumetengana kwa miaka minne.

      Kwa sababu ya kukamatwa, sikuweza kubatizwa ili kuonyesha kwamba nimejiweka wakfu kwa Yehova. Hivyo, niliwauliza ndugu huko Tomsk kuhusu jambo hilo. Kwa kuwa wengine pia walitaka kubatizwa, mara moja ndugu walipanga kuwe na ubatizo. Hata hivyo, kwa sababu ya marufuku, waliamua kufanya ubatizo huo usiku katika ziwa lililokuwa katika msitu wa karibu.

      Wakati uliopangwa ulipowadia, tuliondoka katika viunga vya Tomsk na kuingia msituni tukiwa wawili-wawili ili mpango wetu usigunduliwe. Watu walipaswa kufuatana wawili-wawili hadi wafike salama kwenye ziwa. Hivyo ndivyo ilivyopangwa. Lakini, dada wawili wazee waliotutangulia mimi na mwenzangu walipotea njia. Sisi tuliwafuata, na kama ilivyopangwa wale waliokuwa nyuma yetu wakatufuata. Punde, mimi, mwenzangu, na watu wengine wanane hivi tulipotea msituni. Tulilowa kabisa kwa sababu ya unyevu vichakani na tulitetemeka kwa baridi. Tulihofia kwamba tungekutana na dubu au mbwa-mwitu ambao wanapatikana katika eneo hilo. Tulikuwa na wasiwasi sana hivi kwamba tulishtuka kila tuliposikia sauti fulani.

      Nilitambua kwamba ingekuwa hatari kushikwa na hofu au kukata tamaa, kwa hiyo, nilipendekeza tusimame tuli na kupiga mbinja ya wimbo wa Ufalme, huenda wale wengine wangetusikia. Tulisali pia kwa moyo wote. Wazia furaha yetu tuliposikia sauti ya wimbo uleule ikitufikia polepole katika msitu huo wenye giza! Naam, ndugu zetu walikuwa wamesikia wimbo wetu! Mara moja waliwasha tochi ili tujue mahali walipokuwa. Baada ya muda mfupi, tulizamishwa katika maji baridi sana ziwani, lakini tulifurahi sana hivi kwamba hata hatukusikia baridi.

      Sasa nina umri wa miaka 74 na nimerudi Corjeuţi, ambako nilikuwa nimejifunza kweli. Licha ya uzee, bado ninaimba mara nyingi, hasa ili kumsifu Baba yetu wa mbinguni.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 104-106]

      Nilijitahidi Kuwaiga Wazazi Wangu

      Vasile Ursu

      Alizaliwa: 1927

      Alibatizwa: 1941

      Maisha yake: Alikuwa msimamizi wa kutaniko na alifanya kazi ya kuchapa vitabu kisiri.

      Wazazi wangu, Simeon na Maria Ursu, walibatizwa mwaka wa 1929. Kati ya watoto wao watano, mimi ndiye mkubwa. Wakati wa utawala wa Wafashisti, Baba na Mama walikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 katika kambi ya kazi ngumu kwa sababu hawakuunga mkono siasa. Ndugu na dada wa kiroho wa kutaniko la Corjeuţi walitutunza sisi watoto na walilima shamba la familia yetu. Kwa hiyo hatukukosa chakula kamwe. Nyanya yetu mzee, ambaye hakuwa Shahidi, alisaidia pia kututunza. Nilikuwa na umri wa miaka 14 wakati huo.

      Kwa sababu ya mfano mzuri wa wazazi wangu, nilijitahidi sana kuwasaidia ndugu na dada zangu kiroho. Hivyo, niliwaamsha mapema kila asubuhi ili tujifunze sehemu fulani katika kitabu kinachozungumzia Biblia. Hawakufurahi nilipowaamsha, lakini sikuwaruhusu kuendelea kulala. Nilitambua umuhimu wa kujifunza kwa ukawaida. Kwa hiyo, wazazi wetu walipoachiliwa na kurudi nyumbani mwaka wa 1944, walifurahi kuona kwamba hali yetu ya kiroho ilikuwa nzuri. Tulifurahi sana wazazi wetu waliporudi! Lakini furaha yetu haikudumu.

      Mwaka uliofuata, Wasovieti walimkamata Baba na kumfunga huko Norilsk, Siberia, kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki. Miaka mitatu baadaye, nilimwoa Emilia, dada mchangamfu aliyependa mambo ya kiroho. Nilimjua Emilia vizuri sana tangu utotoni. Mwaka mmoja tu baada ya arusi yetu, mimi na mama yangu tulikamatwa. Tulipelekwa Chisinau, ambako tulihukumiwa kifungo cha miaka 25 katika kambi ya kazi ngumu. Emilia aliwatunza kwa upendo ndugu na dada zangu ambao sasa walikuwa wamenyang’anywa wazazi wao na kaka yao.

      Hatimaye nikapelekwa Vorkuta ili kufanya kazi katika migodi ya makaa. Kambi hiyo ya kazi ngumu iliyokuwa kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki ilijulikana kuwa mbaya sana. Miaka miwili baadaye, mwaka wa 1951, Emilia, ndugu zangu watatu, na dada yangu mmoja walihamishwa hadi Tomsk, magharibi mwa Siberia. Mwaka wa 1955, Emilia aliomba ahamishwe hadi Vorkuta ili aungane nami. Alipokuwa huko alijifungua mtoto wa kike ambaye tulimwita Tamara. Baadaye tulipata watoto wengine wawili.

      Msamaha ulitangazwa mnamo Septemba 1957, na tukaachiliwa. Lakini mwezi mmoja baadaye nilikamatwa tena. Nilihukumiwa kifungo cha miaka saba katika kambi ya kazi ngumu huko Mordvinia, karibu na Saransk, Urusi. Ndugu wengine wengi walifungwa huko pia, na wengine walikuja baadaye. Wake wetu walipokuja kututembelea, walituletea kisiri magazeti na vitabu kwa ukawaida. Tulithamini sana jambo hilo. Mnamo Desemba 1957, Emilia alihamia Kurgan, magharibi mwa Siberia, ili amtunze binti yetu, Tamara, aliyekuwa anakaa na wazazi wa Emilia. Kwa sababu hiyo, mimi na Emilia tulitengana kwa miaka saba. Hatukuwa na njia nyingine ya kuzuia Tamara asipelekwe kwenye shule ya serikali.

      Niliachiliwa mwaka wa 1964, lakini sikuruhusiwa kurudi nyumbani Moldova. Ijapokuwa sikuweza kusafiri kwa uhuru, niliweza kujiunga na mke wangu na binti yangu huko Kurgan, ambako nilitumikia kama kiongozi wa funzo la kitabu kutanikoni. Mwaka wa 1969, tulihamia Krasnodar katika Milima ya Kaukasus. Baada ya kutumikia huko kwa miaka minane, tukahamia Chirchik, Uzbekistan. Huko nilifanya kazi ya kuchapa vitabu kisiri. Hatimaye, tuliruhusiwa kurudi Moldova mwaka wa 1984. Tulihamia jiji la Tighina lenye wakazi 160,000 na wahubiri 18 tu. Tangu wakati huo idadi hiyo imeongezeka na sasa kuna makutaniko tisa na karibu wahubiri na mapainia 1,000 katika mji huo.

      Je, ninajuta kwamba nilikaa miaka mingi katika kambi za kazi ngumu na magereza kwa ajili ya Bwana? Hata kidogo! Nilipobatizwa nikiwa kijana mwenye umri wa miaka 14, tayari nilielewa waziwazi masuala yaliyohusika: ama unampenda Mungu ama unaupenda ulimwengu! Kwa sababu nilikuwa nimeamua kumtumikia Yehova, sikufikiria kamwe kuvunja uaminifu wangu.—Yak. 4:4.

      [Picha]

      Kushoto: Vasile Ursu

      Kushoto kabisa: Vasile na mke wake Emilia, na binti yake, Tamara

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki