-
Moldova2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
Mbinu ya Wasovieti ya Kuwahamisha Watu
Ujerumani ilipoelekea kushindwa vitani, baadhi ya maafisa wa serikali ya Rumania iliyoongozwa na Mfalme Michael, walipindua serikali ya Antonescu mwaka wa 1944. Kisha Rumania ilivunja uhusiano wake na muungano wa Ujerumani, Italia, na Japani na ikajiunga na Urusi. Mwaka uo huo, jeshi la Sovieti lilitwaa tena eneo hilo, kwa hiyo, Moldova ikawa tena sehemu ya Muungano wa Sovieti, na kuitwa SSR ya Moldavia.
Mwanzoni, watawala Wakomunisti wa Moldova hawakuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova. Lakini amani hiyo haikudumu kwa muda mrefu. Punde msimamo wa Kikristo wa kutounga mkono mambo ya siasa ulipingwa vikali tena, kutia ndani msimamo wa Mashahidi wa kukataa kupiga kura katika uchaguzi wa chama. Chini ya utawala wa Sovieti, kutounga mkono siasa hakukubaliwa hata kidogo. Kwa hiyo, serikali ilinuia kutatua tatizo hilo kwa kuwahamisha Mashahidi wa Yehova na watu wengine “wasiotakiwa” kuanzia mwaka wa 1949.
“Uamuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Chama cha Wakomunisti” kuwahusu watu kutoka SSR ya Moldavia ambao wangehamishwa ulionyeshwa katika hati fulani rasmi. Baadhi ya watu hao walikuwa “wamiliki wa mashamba, wenye biashara kubwa, watu walioshirikiana na wavamizi Wajerumani, wale waliowasaidia polisi wa Ujerumani na Rumania, wanachama wa vyama na mashirika ya Wafashisti, shirika fulani la Wafinland lisilokuwa la Kisoshalisti, waumini wa madhehebu yasiyo halali, na pia familia za watu hao wote.” Wote hao walipaswa kupelekwa magharibi mwa Siberia hadi “wakati usiojulikana.”
Uhamisho mwingine ulianza mwaka wa 1951, lakini wakati huo ni Mashahidi wa Yehova pekee waliohamishwa. Stalin mwenyewe aliagiza uhamisho huo ulioitwa Operation North. Zaidi ya familia 720 za Mashahidi, yaani, watu 2,600 hivi, walihamishwa kutoka Moldova hadi Tomsk, magharibi mwa Siberia, umbali wa kilometa 4,500 kutoka Moldova.
Maagizo ya serikali yalisema kwamba watu walipaswa kupewa nafasi ya kutosha kufunga virago vyao kabla ya kupelekwa kwenye magari-moshi. Na zaidi ya hayo, mabehewa yalikuwa “yatengenezwe vizuri ili yafae kuwasafirisha wanadamu.” Lakini maagizo hayo hayakutiwa maanani.
Kwa kawaida, wanajeshi na maafisa wanane hivi walifika nyumbani kwa Mashahidi usiku wa manane. Waliwaamsha na kuwaonyesha barua ya uhamisho. Waliwapa saa chache tu kufunga virago vyao kabla ya kuwapeleka kwenye magari-moshi.
Walisafirishwa kwa mabehewa ya mizigo. Watu 40 hivi walisongamana katika kila behewa kwa majuma mawili ya safari. Hakukuwa na viti na baridi iliingia kwenye mabehewa. Katika pembe moja ya behewa kulikuwa na shimo sakafuni ambalo lilitumiwa kama choo. Kabla ya kuwahamisha ndugu, maafisa walipaswa kuandika orodha ya mali za kila mtu. Hata hivyo, mara nyingi waliorodhesha tu vitu duni; vitu vyenye thamani “vilipotea” tu.
Hata hivyo, licha ya magumu yaliyowapata, ndugu hawakupoteza furaha yao ya Kikristo. Magari-moshi yaliyowasafirisha Mashahidi yalipofika kwenye vituo vya gari-moshi, sauti za nyimbo za Ufalme zilisikika kutoka ndani ya mabehewa. Hivyo, ndugu katika kila gari-moshi walijua kwamba hawakuwa peke yao, bali walikuwa wakihamishwa pamoja na mamia ya Mashahidi wenzao. Kuwaona wengine wakidumisha furaha katika hali hizo ngumu kuliwatia moyo na kuwaimarisha wote wadumishe uaminifu wao kwa Yehova katika hali yoyote ile.—Yak. 1:2.
Imani Inayostahili Kuigwa
Ivan Mikitkov ni mmojawapo wa watu wa Moldova waliopelekwa uhamishoni Siberia. Ivan alikamatwa kwa mara ya kwanza huko Moldova pamoja na Mashahidi wengine mwaka wa 1951, na kupelekwa uhamishoni Tomsk. Alipewa kazi ya kukata miti katika msitu mkubwa wa Siberia unaoitwa taiga. Ingawa hakuishi katika kambi ya kazi ngumu, bado alikuwa chini ya vizuizi, na polisi wa siri walipeleleza utendaji wake wote. Hata hivyo, yeye na ndugu zake wa kiroho waliwahubiria wengine kila walipopata nafasi.
Ivan anasema hivi: “Tulipanga kuwe na makutaniko katika mazingira hayo magumu. Hata tulianza kunakili vitabu. Muda si muda, watu kadhaa ambao tuliwahubiria walikubali kweli na kubatizwa. Lakini, hatimaye wenye mamlaka walitambua utendaji wetu na wakapeleka baadhi yetu kwenye kambi za kazi ngumu.
“Mimi na Mashahidi wenzangu Pavel Dandara, Mina Goraş, na Vasile Şarban, tulihukumiwa kifungo cha miaka 12 katika kambi ya kazi ngumu chini ya usimamizi mkali. Wenye mamlaka walifikiri kwamba vifungo hivyo vikali vingewatisha wengine wasihubiri, lakini mbinu hiyo haikufua dafu. Ndugu zetu waliendelea kuhubiri kotekote walikopelekwa. Niliachiliwa mwaka wa 1966, baada ya kukamilisha kifungo changu. Nilirudi Tomsk na kukaa huko kwa miaka mitatu.
“Mwaka wa 1969, nilihamia Bonde la Donets ambako nilikutana na Maria, dada mwaminifu na mwenye bidii ambaye nilimwoa. Nilikamatwa tena mwaka wa 1983. Wakati huo nilihukumiwa adhabu maradufu, kifungo cha gereza cha miaka mitano, na uhamisho wa miaka mitano. Bila shaka nilihisi kwamba hukumu hiyo ilikuwa ngumu zaidi kuliko ile ya kwanza kwa sababu wakati huu ningetengana na mke na mtoto wangu ambao pia wangepatwa na magumu. Ninashukuru kwamba niliachiliwa mwaka wa 1987, baada ya Mikhail Gorbachev kuwekwa kuwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Sovieti. Niliruhusiwa kurudi Ukrainia na hatimaye Moldova.
“Niliporudi Bălţi, jiji la pili kwa ukubwa nchini Moldova, jiji hilo lilikuwa na wahubiri 370 na makutaniko matatu. Leo jiji hilo lina zaidi ya wahubiri 1,700 na makutaniko 16!”
“Je, Unataka Kufa Kama Vasile?”
Wasimamizi wa kambi na wapelelezi wa KGB (Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti) walitunga mbinu za kinyama ili kuvunja uaminifu wa ndugu. Constantin Ivanovici Şobe anasimulia kile kilichompata babu yake Constantin Şobe: “Mwaka wa 1952, Babu alikuwa amefungwa katika kambi moja ya kazi ngumu katika wilaya ya Chita, mashariki ya Ziwa Baikal huko Siberia. Maafisa wa kambi walitisha kumpiga risasi yeye na Mashahidi wengine wasipokana imani yao.
“Kwa sababu ndugu hao walikataa kukana imani yao, maafisa waliwakusanya nje ya kambi karibu na msitu. Giza lilikuwa likiingia walipompeleka Vasile, rafiki wa karibu zaidi wa Babu, msituni na kutangaza kwamba watampiga risasi. Ndugu walingoja wakiwa na wasiwasi. Punde walisikia bunduki zikifyatuliwa.
“Askari walirudi na kumpeleka Shahidi wa pili, babu yangu, msituni. Baada tu ya kuingia msituni, walifika kwenye uwanja fulani wenye makaburi kadhaa yaliyokuwa yamechimbwa, na moja lilikuwa limefukiwa. Afisa mkuu alisema hivi akimwangalia Babu na kuelekeza kidole kwenye kaburi lililofukiwa: ‘Je, unataka kufa kama Vasile, au unataka kurudi nyumbani kwa familia yako ukiwa mtu huru? Una dakika mbili kufanya uamuzi.’ Babu hakuhitaji dakika mbili. Mara moja alijibu: ‘Vasile, mliyempiga risasi, alikuwa rafiki yangu kwa miaka mingi. Sasa ninatarajia kumwona tena atakapofufuliwa katika ulimwengu mpya. Nina hakika kwamba nitakuwa katika ulimwengu mpya pamoja na Vasile. Lakini, vipi wewe?’
“Afisa huyo hakutarajia jibu hilo. Alimrudisha babu na wale wengine kambini. Hata hivyo, babu hakuhitaji kungoja hadi ufufuo ili kumwona Vasile tena. Hiyo ilikuwa mbinu mbovu iliyokusudiwa kuvunja uaminifu wa ndugu.”
Mbinu ya Wakomunisti ya Kueneza Uwongo Haikufaulu
Wakomunisti walichapisha vitabu na vijitabu, na kutengeneza sinema zilizoeneza uwongo juu ya watu wa Mungu ili kuwachochea watu wawachukie na kuwashuku Mashahidi wa Yehova. Kijitabu kimoja kilikuwa na kichwa Double Bottom. Kijitabu hicho kilipewa jina hilo kwa sababu ndugu walikuwa wakitengeneza sehemu ya siri ya kufichia vitabu katika masanduku ya nguo na mikoba yao. Nicolai Voloşanovschi anakumbuka jinsi kamanda wa kambi alivyojaribu kutumia kijitabu hicho kumfedhehesha mbele ya wafungwa wengine.
Nicolai anasema hivi: “Kamanda huyo alikusanya wafungwa wote katika jengo moja kambini. Kisha akasoma sehemu mbalimbali katika kijitabu hicho, kutia ndani sehemu zilizokuwa na maelezo ya uwongo kunihusu. Alipomaliza, nilimwomba ruhusa kuuliza maswali machache. Bila shaka kamanda huyo alikubali ombi langu akidhani kwamba angepata nafasi ya kunifanyia mzaha.
“Nilimwuliza kamanda huyo ikiwa anakumbuka aliponihoji mara ya kwanza nilipokuja kambini. Alisema anakumbuka mahojiano hayo. Kisha nikamwuliza kama anakumbuka maswali ambayo aliniuliza kuhusu nchi niliyozaliwa, uraia wangu, na kadhalika alipokuwa akijaza fomu za kuniandikisha kambini. Tena alijibu ndiyo. Hata aliwaambia wale waliokuwa wakisikiliza majibu niliyotoa wakati huo. Kisha nikamwomba aeleze yale aliyoandika katika fomu hizo. Alikiri kwamba yale aliyoandika hayakupatana na majibu yangu. Niliwatazama wasikilizaji na kusema: ‘Mwaona, kijitabu hiki kiliandikwa kwa njia iyo hiyo.’ Wafungwa walipiga makofi, na kamanda akatoka kwa hasira.”
-
-
Moldova2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
[Picha katika ukurasa wa 96]
Mabehewa ya mizigo yaliyotumiwa kuwahamisha Mashahidi hadi Siberia
-