-
Kwa Nini Maadili Yanabadilika?Amkeni!—2003 | Juni 8
-
-
Kwa Nini Maadili Yanabadilika?
“Ni jambo gani lililo muhimu zaidi maishani?”
Watu 50,000 katika nchi 60 waliulizwa swali hilo. Matokeo ya kura ya maoni ya Gallup yalionyesha kwamba jibu lililotolewa na watu wengi zaidi kutoka kila sehemu ya ulimwengu lilikuwa “kuwa na maisha ya familia yenye furaha” na “kuwa na afya bora.”
UKIANGALIA kijuu-juu tu, utadhani kwamba watu ulimwenguni pote wana maadili mema. Hata hivyo, mambo ni tofauti kabisa. Zamani watu walikuwa na maadili yaliyotegemea kanuni za dini na adabu za kale. Lakini hali inabadilika haraka sana. Mtafiti Marisa Ferrari Occhionero anasema hivi kuhusu nchi ya Italia: “Vijana wana tabia ambazo zinaonyesha kwamba wamesahau maadili ya kale ya wazazi wao, ya kidini na kitamaduni.” Hali iko hivyo pia kwa watu ulimwenguni pote, vijana kwa wazee.
Profesa Ronald Inglehart, msimamizi wa utafiti unaoitwa Uchunguzi wa Maadili Ulimwenguni anasema hivi: “Kuna uthibitisho mkubwa kwamba maoni ya watu yamebadilika sana.” Ni nini kinacholeta mabadiliko hayo? Inglehart asema: “Mabadiliko hayo yanaletwa na maendeleo ya kiuchumi na kitekinolojia.”
Kwa mfano, kura ya maoni ya Gallup, ilifichua kwamba katika nchi tajiri kuajiriwa kazi kulichukua “nafasi ya chini sana” katika mambo yanayoonwa kuwa muhimu maishani. Lakini kupata kazi kulionwa kuwa jambo muhimu zaidi katika nchi zinazoendelea. Hii yaonyesha kwamba watu maskini wanaona kupata mahitaji ya kila siku kuwa jambo muhimu zaidi. Nchi zinapoendelea kiuchumi, watu huanza kutilia maanani mambo kama vile afya, furaha ya familia, na uhuru wa kusema.
Kwa sababu ya maendeleo ya kitekinolojia, watu katika nchi zinazoendelea wataathiriwa na maadili mapya. Gazeti The Futurist linasema hivi: “Imani na maadili yetu huathiriwa na yale tunayoona na kusikia.” Hivyo, vyombo vya habari vinaathiri sana maadili ya nchi za Magharibi. Gazeti The Futurist linasema: “Vyombo vya habari vinaathiri watu ulimwenguni pote.”
Ni mabadiliko gani ambayo yametokea katika mitazamo na tabia za watu? Mabadiliko hayo yamekuwa na athari gani kwako na kwa familia yako?
-
-
Je, Maadili Yanazorota?Amkeni!—2003 | Juni 8
-
-
Je, Maadili Yanazorota?
ZAWADI kubwa sana ambayo wazazi wanaweza kuwapatia watoto wao ni upendo wa kweli na maadili ambayo wanayafuata wala si kuyafundisha tu.
Bila maadili, maisha hayana maana. Maadili hufanya maisha yaridhishe. Yanafanya mtu ajue mambo yanayopasa kutangulizwa, yale anayopaswa kufanya na yale asiyopaswa kufanya.
Hata hivyo, maadili mengi ya kale yanabadilika haraka sana. Kwa mfano, Profesa Ronald Inglehart anasema kwamba “siku hizi jamii inaendelea kuwaruhusu watu watosheleze tamaa yao ya ngono jinsi wapendavyo na kuwapa uhuru wa kusema.” Katika mwaka wa 1997, kura ya maoni ya Gallup iliyohusisha nchi 16, iliwahoji watu kuhusu wanawake wanaopata watoto nje ya ndoa. Ripoti ya Gallup inasema: “Tabia hiyo inakubalika kwa kiwango cha kuanzia asilimia 90 au zaidi huko Ulaya Magharibi hadi chini ya asilimia 15 nchini Singapore na India.”
Watu wengine wameisifu tabia hiyo iliyopotoka. Hata hivyo, kitabu The Rise of Government and the Decline of Morality, cha James A. Dorn kinasema kwamba “ongezeko la watoto wanaozaliwa nje ya ndoa” na “kuvunjika kwa familia,” ni “mambo yanayoonyesha wazi kwamba maadili yamepotoka.”
Maadili Mengine Yanayozorota
Maadili mengine ambayo yamekuwapo kwa miaka mingi yanazorota pia. Uchunguzi wa Maadili Ulimwenguni, ulioongozwa na Profesa Inglehart, unaonyesha kwamba katika nchi zilizoendelea watu “wanazidi kudharau mamlaka.”
Tangu jadi watu wamekuwa na maadili ya kuwajibika kazini. Lakini kuna uthibitisho kwamba maadili hayo pia yanazorota. Huko Marekani, Shirika la Kitaifa la Wafanyabiashara wa Kujitegemea liliwachunguza waajiri zaidi ya nusu milioni. “Asilimia 31 walisema kwamba ni vigumu kujaza nafasi za kazi zilizo wazi, na asilimia 21 walisema kwamba kwa ujumla, kazi haifanywi vizuri.” Mwajiri mmoja alisema hivi: “Inaendelea kuwa vigumu kupata wafanyakazi ambao wanataka kufanya kazi kwa zaidi ya siku moja, wanaofika kazini bila kuchelewa, na ambao hawajalewa.”
Huenda hali hiyo inaletwa na sababu za kiuchumi. Faida ya biashara inapopungua, wafanyakazi wanafutwa au wanapunguziwa marupurupu fulani. Gazeti Ethics & Behavior linasema hivi: “Wafanyakazi wenye waajiri kama hao wasio waaminifu na wasiowajibika, huanza kuwa na maoni yasiyofaa kuwaelekea. Hawawezi kufanya kazi kwa bidii kwa sababu huenda kesho wakafutwa.”
Nidhamu na adabu ni mambo mengine ambayo yamezorota sana. Uchunguzi uliofanywa nchini Australia ulifikia mkataa huu: “Zaidi ya asilimia 87.7 ya wafanyakazi walisema [kwamba] utovu wa nidhamu unapunguza bidii kazini.” Wafanyabiashara mashuhuri nchini Marekani walipohojiwa, “asilimia themanini kati yao walisema kuna ongezeko la matusi katika biashara.” Kulingana na shirika la habari la CNN, “wateja wengi hawahudumiwi vizuri na karibu nusu ya wale waliohojiwa walisema kwamba iliwabidi waondoke dukani bila kununua chochote mwaka uliopita. Nusu yao walisema kwamba wao huwaona watu wakizungumza kwa simu ya mkononi kwa sauti kubwa au kwa njia yenye kuudhi. Pia madereva sita kati ya 10 walisema kwamba wao huwaona wengine wakiendesha gari bila kujali.”
Je, Uhai wa Mwanadamu Una Thamani?
Wakati mwingine, watu husema kwamba wanafuata “maadili” fulani, lakini hawatendi kulingana na maneno yao. Kwa mfano, Taasisi ya Maadili Duniani ilifanya kura ya maoni katika nchi 40. Asilimia 40 walisema “kuheshimu uhai” ni mojawapo ya maadili matano “yaliyo muhimu zaidi.”a
Lakini mambo yakoje kihalisi? Bila shaka mataifa yaliyoendelea yana uwezo wa kukomesha mateso mengi kati ya yale yanayowapata wanadamu. Lakini katika mwaka wa 1998, kitabu kilichoandikwa na Carol Bellamy, mkurugenzi mkuu wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, kilisema kwamba utapiamlo “huchangia zaidi ya nusu ya vifo vya watoto wapatao milioni 12 wenye umri wa chini ya miaka mitano kila mwaka katika nchi zinazoendelea. Idadi hiyo ya vifo ni ya juu zaidi tangu tauni ilipotokea huko Ulaya katika karne ya 14.” Taarifa kama hizo humsikitisha mtu yeyote anayethamini uhai. “Lakini,” asema Bellamy, “janga la ulimwenguni pote la utapiamlo limewagutusha watu wachache sana, licha ya kuwa sayansi imepiga hatua kubwa kuonyesha kwamba ugonjwa huo ni hatari. Watu hukazia zaidi habari za kupanda na kushuka kwa bei katika soko la hisa ulimwenguni kuliko hatari kubwa ya utapiamlo, au kuliko umuhimu wa kuwapatia watu lishe bora.”
Vilevile inaonekana wazi kuwa wataalamu wa tiba wana maoni yasiyofaa kuhusu uhai. Katika mwaka wa 1970, watoto waliozaliwa baada ya kukaa tumboni mwa mama kwa majuma 23, hawakuwa na tumaini lolote la kupona. Leo, asilimia 40 ya watoto hao wanaweza kuokoka. Kwa hiyo, ni jambo la kusikitisha sana kwamba ulimwenguni pote vijusi milioni 40 hadi 60 hufa kutokana na utoaji wa mimba kila mwaka! Vijusi vingi hutolewa majuma machache tu kabla ya kufikia umri wa watoto wale ambao madaktari hujitahidi kuokoa! Je, jambo hilo halionyeshi kwamba maadili yamezorota sana?
Mwongozo wa Maadili Unahitajika
Watu walipoulizwa, “Ni kitu gani chenye umuhimu mdogo zaidi maishani?” katika kura ya maoni ya Gallup, wengi walisema moja kati ya mambo mawili yenye umuhimu mdogo sana ni ‘kuwa mwaminifu kwa dini yao.’ Basi si ajabu kwamba watu wanaoenda kanisani wanazidi kupungua. Profesa Inglehart anasema kwamba nchi za Magharibi “zinawafanya watu wahisi wakiwa salama sana” na kwamba jambo hilo “limepunguza uhitaji wa usalama waliopata katika dini zamani.”
Kadiri watu wanavyoacha dini, ndivyo wanavyoendelea kukosa imani katika Biblia. Katika uchunguzi mmoja wa kimataifa, watu waliulizwa walipata mwongozo kutoka kwa nani au kutoka wapi walipotaka kujua mambo yanayofaa au yasiyofaa. Wengi sana walisema walitegemea ujuzi wao maishani. “Ni wachache sana waliosema kwamba walitegemea neno la Mungu,” yasema ripoti ya uchunguzi huo.
Si ajabu basi kwamba maadili yanazidi kuzorota! Kukosa mwongozo wa maadili, kukazia utafutaji wa mali, na ubinafsi umeleta pupa na kutojali hisia za wengine. Matokeo yamekuwa nini?
[Maelezo ya Chini]
a Zaidi ya miaka 50 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitangaza Azimio la Haki za Binadamu. Kifungu cha 1 cha Azimio hilo kinasema hivi: “Wanadamu wote huzaliwa wakiwa huru na wakiwa na cheo na haki sawa.”
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Kuvunjika kwa familia, kutowajibika kazini, na utovu wa nidhamu ni mambo yanayoletwa na kuzorota kwa maadili
[Picha katika ukurasa wa 6]
Mamilioni ya vijusi vichanga kuliko kitoto hiki hutolewa kila mwaka
-
-
Je, Unahisi Maadili Yamezorota?Amkeni!—2003 | Juni 8
-
-
Je, Unahisi Maadili Yamezorota?
“NI TATIZO gani linalowaathiri watu wengi zaidi katika nchi hii?” Watu wengi walipoulizwa swali hilo huko Marekani, walisema kwamba kuzorota kwa maadili na kuvunjika kwa familia ndiyo matatizo makubwa yanayowahangaisha. Watu wengine pia wana maoni kama hayo.
Kwa mfano, gazeti la Paris International Herald Tribune lilisema hivi: “Inaonekana vijana wanatafuta jambo la kuwaunganisha, yaani, wanatafuta maadili yanayoweza kutumiwa kukomesha matatizo ambayo yanaenea ulimwenguni kama vile pupa, ubinafsi, na ukosefu wa ushirikiano katika jamii. . . . Jitihada hizo za kutafuta maadili ya kuongoza ulimwengu wote zinaonyesha kwamba hakuna maadili.”
Je, unafikiri kwamba serikali, viongozi wa ulimwengu, na wafanyabiashara mashuhuri wana maadili yanayoweza kutuletea wakati ujao wenye furaha na ulio salama zaidi? Je, unahisi pengo fulani unapoona matokeo ya kuzorota kwa maadili?
Huenda jambo moja linalokuhangaisha sana ni usalama wako. Je, unaishi mahali ambapo unaweza kuacha mlango wako ukiwa wazi na usiibiwe vitu? Je, wewe huhisi ukiwa salama unapotembea barabarani usiku? Hata ikiwa unaishi katika eneo ambalo halina vita, fujo za kikabila, au mapigano kati ya magenge, huenda bado unaogopa kushambuliwa, kunyang’anywa vitu kwa nguvu, kuvamiwa na wakora nyumbani, au kuibiwa vitu. Mambo hayo yanaweza kukufadhaisha na kusababisha pengo maishani mwako.
Huenda pia umeacha kuwatumaini watu kwa kadiri fulani. Labda katika maisha yako na kazini umekutana na watu wanaotaka kukuumiza ili wajifaidi, hata ikiwa watafaidika kidogo tu.
Serikali Zinapaswa Kuweka Mfano Mzuri
Katika historia yote, maadili ya watu yameathiriwa sana na maadili ya viongozi wanaowatawala. Calvin Coolidge alisema hivi kabla hajawa rais wa Marekani: “Watu husema kwamba kuna haki za kiasili, lakini ningependa mtu ajitokeze na aniambie wakati hususa ambapo haki zozote zimekuwapo au zimetambuliwa, isipokuwa tu iwe ni baada ya sheria kutungwa ili kuzitambulisha waziwazi na kuzilinda.”
Kwa hakika, serikali inayotawala—hata iwe ilitumia njia gani kuingia mamlakani—ndiyo inayoweza kuruhusu au kuzuia haki za wanadamu kama vile uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kidini, uhuru wa kusema hadharani, haki ya kutokamatwa au kusumbuliwa bila idhini, na kupata hukumu ya haki.
Abraham Lincoln alisema hivi kabla hajawa rais wa Marekani: “Kusudi kuu la serikali ni kuwafanyia watu mambo wanayotaka kufanya, lakini ambayo hawawezi kujifanyia, au ambayo hawawezi kuyafanya vizuri kwa uwezo wao wenyewe wakiwa mmoja-mmoja.” Serikali zinapojitahidi kutimiza makusudi hayo mazuri, watu huwatumaini viongozi.
Hata hivyo, watu leo hawawatumaini viongozi na badala yake wana shaka na wasiwasi kuwahusu. Uchunguzi mmoja uliofanywa huko Marekani uliripoti kwamba asilimia 68 ya wale waliohojiwa walisema kuwa matendo ya maafisa wa serikali yanaridhisha kwa kadiri au hayaridhishi kabisa. Katika nchi nyingi watu wameacha kuwaamini maafisa wa serikali kwa sababu ya kashfa nyingi za hongo na ufisadi. Hiyo ndiyo sababu watu wengi leo wanahisi kuna pengo fulani maishani mwao.
Mfano Mzuri wa Mfalme Solomoni
Mfano mmoja wa kale unaonyesha jinsi maadili ya watawala yanavyoweza kuwa na athari kubwa sana. Mfalme Solomoni alitawala yale makabila 12 ya Israeli kuanzia mwaka wa 1037 hadi 998 K.W.K. Mfalme Daudi, baba yake, alikuwa mmoja wa wafalme wazuri wa Israeli. Biblia inasema kwamba Daudi alipenda kweli na uadilifu na, zaidi ya yote, alikuwa na imani na usadikisho thabiti katika Mungu wake, Yehova. Daudi alimfunza Solomoni maadili hayohayo.
Mungu Mweza-Yote alimtokea Solomoni katika ndoto na kumwambia: “Omba utakalo nikupe.” (2 Mambo ya Nyakati 1:7) Badala ya kuomba mali nyingi, utukufu, na ushindi wa kivita, Solomoni alionyesha maadili yake mema kwa kuomba moyo wa hekima, wa uelewevu, na mtiifu ili aweze kutawala taifa la Israeli vizuri.
Utawala wa Solomoni uliwaletea raia zake matokeo gani? Mungu alimbariki kwa kumpa hekima, utukufu, na utajiri maadamu aliendelea kufuata maadili ya kiroho ya taifa hilo. Vitu vilivyochimbuliwa vinathibitisha kwamba kulikuwa na ufanisi mwingi wakati wa utawala wa Solomoni. Kitabu The Archaeology of the Land of Israel kinasema: “Utajiri uliotoka pande zote na kuingia katika makao ya kifalme, na biashara iliyotia fora . . . zilileta maendeleo ya haraka ya kila aina.”
Naam, utawala mzuri wa Solomoni uliwaletea raia zake amani, usalama, na furaha. “Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani.”—1 Wafalme 4:20, 25.
Mfano Mbaya wa Mfalme Solomoni
Hata hivyo, inasikitisha kwamba maadili ya Solomoni yalizorota kama vile maadili ya viongozi wengi wa leo. Biblia inasema hivi: “Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”—1 Wafalme 11:3, 4.
Maadili ya Mfalme Solomoni yalipozorota, raia zake waliathiriwaje? Ijapokuwa alikuwa na uwezo mkubwa na hekima nyingi, Solomoni akawa mtawala mwonevu mwishoni-mwishoni mwa utawala wake. Uchumi wa taifa ulizorota sana kwa sababu ya matumizi mengi ya serikali yake. Wafanyakazi wake hawakuridhika. Wapinzani wa kisiasa wakampinga mfalme na wakapanga njama za kumpindua. Taifa likapoteza umoja. Inashangaza kwamba Solomoni mwenyewe ndiye aliyeandika hivi: “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; bali mwovu atawalapo, watu huugua.”—Mithali 29:2.
Muda mfupi baada ya kifo cha Solomoni, msukosuko wa kisiasa na wasiwasi ulifanya taifa hilo ligawanyike na baadaye kukawa na magumu, mtengano, na hali zikazorota. Waisraeli walihisi pengo kubwa maishani mwao. Maadili ya serikali yao yalikuwa yamezorota, na ikaacha kuwajali. Tatizo kuu lilikuwa kwamba viongozi wao walimpuuza Yehova na sheria zake. Basi, taifa lote likaumia.
Watu Wengi Hawatumainiani Leo
Wakuu wengi katika serikali, biashara, na dini hawajali maadili yao. Hilo limewafanya watu wengi wahisi kuna pengo maishani mwao. Serikali na viongozi wanaendelea kushindwa kutatua matatizo ya msingi ya nchi zao.
Kwa mfano, wameshindwa kukomesha vita, kupunguza gharama zinazozidi kupanda za matibabu, au matokeo mabaya ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Pia, elimu imeathiriwa. Serikali fulani-fulani hata huanzisha vituo vya kuchezea kamari. Vilevile, wafanyabiashara mashuhuri na viongozi wa dini wamehusika katika matendo ya kusikitisha ya ufisadi na upotovu wa maadili. Basi haishangazi kwamba watu wengi leo hawawatumaini viongozi.
Je, kweli inawezekana kwa serikali yoyote ile kulinda na kutegemeza haki na maadili ya wanadamu? Ndiyo, inawezekana. Makala ya mwisho itaeleza jinsi inavyowezekana.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
‘Pupa, ubinafsi, na ukosefu wa ushirikiano katika jamii ni mambo yanayoenea ulimwenguni.’ —International Herald Tribune
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mfalme Solomoni alipotii sheria za Mungu, aliwasaidia raia zake wawe na maadili mema
-