Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maadili Yakoje Leo?
    Amkeni!—2000 | Aprili 8
    • Maadili Yakoje Leo?

      Asubuhi moja katika Aprili 1999, hali ya utulivu ilivurugwa katika mji wa Littleton, karibu na Denver, Colorado, Marekani. Vijana wawili waliokuwa wamevalia makoti meusi ya mvua waliingia katika shule moja ya sekondari na kuanza kuwafyatulia risasi wanafunzi na walimu. Pia walilipua mabomu. Wanafunzi 12 na mwalimu mmoja waliuawa, na zaidi ya 20 wakajeruhiwa. Wavamizi hao walijiua hatimaye. Walikuwa na umri wa miaka 17 na 18 peke yake nao walichukia sana vikundi fulani.

      KWA kusikitisha, mfano uliotajwa juu ni kisa cha kawaida. Magazeti, redio, na televisheni huripoti matukio kama hayo ulimwenguni pote. Kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Takwimu za Elimu, mnamo mwaka wa 1997 kulikuwa na visa vya kijeuri takriban 11,000 vinavyohusisha silaha katika shule za Marekani. Katika Hamburg, Ujerumani, ripoti za vitendo vya kijeuri ziliongezeka kwa asilimia 10 mnamo 1997, na asilimia 44 ya washukiwa walikuwa ni vijana walio na umri unaopungua miaka 21.

      Ufisadi miongoni mwa wanasiasa na maofisa wa serikali ni jambo la kawaida. Ripoti moja ya mjumbe wa Muungano wa Ulaya (EU) Anita Gradin katika mwaka wa 1998 ilifunua kwamba gharama ya ufisadi miongoni mwa Muungano wa Ulaya mnamo mwaka wa 1997 ilikadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 1.4. Ulihusisha kila kitu kuanzia kupuuzwa kwa maonyo ya kuegesha hadi kupokea mikopo ya kilimo au pesa nyinginezo za Muungano wa Ulaya kwa njia ya udanganyifu. Kubadili kiasi kikubwa cha fedha haramu na magendo ya silaha na mihadarati kuliruhusiwa, na wafanyakazi wa Muungano wa Ulaya walikuwa wamehongwa na mashirika ya wahalifu ili wanyamaze. Tume nzima ya Muungano wa Ulaya ilijiuzulu mnamo mwaka wa 1999.

      Hata hivyo, udanganyifu hauhusishi tu wale wenye cheo cha juu katika jamii. Ripoti moja kutoka Tume ya Muungano wa Ulaya inayohusu wafanyakazi haramu ilifunua kwamba asilimia 16 ya pato kuu la kitaifa la Muungano wa Ulaya hutia ndani mapato yanayotoka kwa biashara ambazo hazijasajiliwa wala kulipiwa kodi. Katika Urusi mapato haramu yanaripotiwa kuwa asilimia 50 ya mapato yote kwa ujumla. Isitoshe, katika Marekani, Shirika Lenye Kibali cha Kuchunguza Upunjaji lilisema kwamba makampuni mengi ya Amerika hupoteza zaidi ya dola bilioni 400 kila mwaka kwa sababu ya wafanyakazi kuyaibia fedha au mali.

      Watu wengi wanaovutiwa kingono na watoto wametumia Internet ili kushawishi watoto wajihusishe na vitendo vya ngono haramu. Msemaji wa shirika la Save the Children huko Sweden alisema kwamba kuna hangaiko kubwa kuhusu ponografia ya watoto kwenye Internet. Katika Norway mnamo mwaka wa 1997, shirika hilo lilipokea vidokezi 1,883 kuhusu Website katika Internet zenye ponografia ya watoto. Mwaka uliofuata idadi ya vidokezi hivyo iliongezeka sana kufikia 5,000 hivi. Nyingi ya habari hii hutokezwa katika nchi ambazo serikali au serikali za mitaa haziwezi kudhibiti utendaji huu wenye kudharaulika.

      Je, Ilikuwa Afadhali Zamani?

      Watu wengi wanaotishwa na hali mbaya ya maadili katika ulimwengu leo, huenda wakakumbuka siku za wazazi au za babu na nyanya zao ambapo kulikuwa na ushirikiano wa jamii. Labda walikuwa wamesikia kwamba watu waliishi maisha ya utulivu wakati huo na kwamba ufuatiaji wa haki na sifa nyingine za kiadili zilithaminiwa na watu wote katika jamii. Watu wenye umri mkubwa zaidi huenda walizungumza kuhusu wakati ambapo watu wenye kufanya kazi kwa bidii walivyosaidiana, vifungo vya familia vilikuwa imara, na vijana walikuwa salama na kusaidia kwenye mashamba na karakana za wazazi wao.

      Hilo laongoza kwenye maswali haya: Je, kwa kweli maadili ya watu yalikuwa bora hapo zamani? Au je, kuna hisia tu ya mambo yaliyozoewa ambayo huvuruga kumbukumbu letu la wakati uliopita? Acheni tuone jinsi wanahistoria na wachanganuzi wengine wa kijamii wanavyotoa jibu.

  • Je, Maadili Ni Mabaya Zaidi Kuliko Awali?
    Amkeni!—2000 | Aprili 8
    • Je, Maadili Ni Mabaya Zaidi Kuliko Awali?

      IKIWA ungewauliza wanahistoria, “Je, maadili ya watu leo ni bora au ni mabaya zaidi kuliko awali?” huenda wengine wakajibu kwamba ni vigumu kulinganisha maadili ya vipindi tofauti-tofauti. Huenda wakawa na maoni kwamba kila kizazi chapasa kuonwa kulingana na jinsi kilivyo.

      Kwa mfano, fikiria kutokea kwa uhalifu wenye jeuri katika Ulaya tangu karne ya 16. Miaka 400 iliyopita visa vya uuaji-kimakusudi vilikuwa jambo la kawaida. Mara nyingi watu walichukua sheria mikononi, na uhasama kati ya watu wa ukoo ulikuwa jambo la kawaida.

      Hata hivyo, wanahistoria Arne Jarrick na Johan Söderberg waandika katika kitabu Människovärdet och makten (Adhama na Uwezo wa Binadamu) kwamba kipindi cha kati ya mwaka wa 1600 na wa 1850 “kilitofautishwa kwa ustaarabu wa kweli katika maisha ya jamii” katika sehemu fulani. Watu walikuwa bora kwa kuzingatia mahitaji ya wengine—walikuwa wenye hisia-mwenzi zaidi. Kwa mfano, wanahistoria wengine wanasema kwamba wivi na uhalifu dhidi ya mali haukuwa wa kawaida sana katika karne ya 16 kama leo. Magenge ya wezi yaliyopangwa yalikuwa nadra, hasa miongoni mwa watu wa mashambani.

      Bila shaka, utumwa ulikuwa umeanzishwa na ulitokeza uhalifu mbaya zaidi katika historia—kutekwa nyara kwa Waafrika na wafanya-biashara wa Ulaya na kutendwa kinyama kwa mamilioni ya watumwa hao wakiwa katika nchi walizopelekwa.

      Hivyo, tukumbukapo karne zilizopita, kwa kuchunguza historia, huenda tukaona kwamba hali nyingine zilikuwa bora, ilhali nyingine zilikuwa mbaya zaidi. Hata hivyo, jambo fulani tofauti kabisa na baya sana—kwa kweli lisilo na kifani—lilitukia katika karne ya 20 na lingali linatukia.

      Karne ya 20—Wakati wa Badiliko

      Wanahistoria Jarrick na Söderberg wasema: “Katika miaka ya 1930 visa vya uuaji-kimakusudi na uuaji wa binadamu viliongezeka tena, na, kwa kusikitisha, tangu wakati huo mwelekeo huu umeendelea kwa zaidi ya nusu karne.”

      Kulingana na watoaji-maoni wengi, maadili yalizorota sana katika karne ya 20. Insha moja inayohusu falsafa za maadili yasema hivi: “Mtu aweza kuona waziwazi kwamba maoni ya jamii kuhusu ngono na mambo yanayokubalika kiadili yamebadilika sana katika miaka 30 hadi 40 iliyopita—zamani jamii ilionyesha waziwazi mambo yanayofaa kiadili, kupitia sheria kali, siku hizi kuna maoni ya kibinafsi na ya uhuru.”

      Hii yamaanisha kwamba mwenendo wa kingono na mambo mengine yahusuyo maadili ni mambo ambayo watu wengi sasa huhisi kwamba wanaweza kujiamulia. Kwa kielelezo, insha hiyo yataja takwimu zinazoonyesha kwamba katika mwaka wa 1960 ni asilimia 5.3 tu ya watoto wote Marekani waliozaliwa nje ya ndoa. Katika mwaka wa 1990 tarakimu hiyo ilikuwa asilimia 28.

      Katika mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Notre Dame, Seneta wa Marekani Joe Lieberman alifafanua maadili ya wakati wetu kuwa “kipindi kisicho na kanuni zozote, . . . ambapo mawazo ya kidesturi ya linalofaa na lisilofaa yamepuuzwa hatua kwa hatua.” Kulingana na Lieberman, “hali hiyo imekuwako kwa vizazi viwili.”

      Kupuuza Dini

      Wanahistoria na wachanganuzi wengine hutoa sababu gani kwa tukio hili kubwa sana katika karne ya 20? “Mojawapo ya mabadiliko ya maana zaidi katika jamii katika karne mbili zilizopita ni kupuuza dini,” chasema kitabu Människovärdet och makten. Kupuuza dini kulimaanisha kwamba “watu wangepewa fursa ya kuchukua msimamo wa maoni tofauti-tofauti kwa kujitegemea. Wazo hilo . . . lilitokana na wanafalsafa wa karne ya 18 wa chama cha Enlightenment, waliokuwa wa kwanza . . . kukataa Biblia kuwa chanzo pekee cha kweli.” Hivyo, dini, hasa zile za Jumuiya ya Wakristo, hazitegemewi kuandaa mwongozo wa kiadili kama zilivyotegemewa sana zamani.

      Lakini ni kwa nini falsafa iliyoanzishwa karne ya 18 ilichukua zaidi ya miaka 200 ili kupendwa? “Mawazo hayo hayakuenezwa kwa urahisi kwa umma,” chasema kitabu kilichotajwa juu. “Harakati ya kupuuza dini ilikuwa ya polepole.”

      Hata ikiwa mwelekeo wa kuacha viwango vya kiadili vya zamani na kanuni za Kikristo ulichukua muda katika kipindi kirefu cha miaka 200 iliyopita, uliongezeka sana katika karne ya 20. Imekuwa hivyo hasa katika miongo michache iliyopita. Kwa nini iwe hivyo?

      Ubinafsi na Pupa

      Jambo kuu linalochangia ni maendeleo ya haraka ya kitekinolojia na kiuchumi katika jamii mnamo karne ya 20. Makala moja katika gazeti la Kijerumani Die Zeit yalisema kwamba tunaishi katika “kipindi maalumu cha mabadiliko na si kama ilivyokuwa katika karne zilizopita, katika ulimwengu uliokuwa tuli.” Makala hayo yalieleza kwamba hiyo imeongoza kwenye mfumo wa soko huru, unaotegemea mashindano na kuchochewa na ubinafsi.

      Makala hiyo iliendelea kusema “ubinafsi huu, hauwezi kukomeshwa na chochote. Tokeo limekuwa kuongezeka kwa unyama unaotendeka kila siku, na vilevile ufisadi, ambao katika nchi nyingi umehusisha hata serikali. Watu hujifikiria wenyewe na kutosheleza tamaa zao kwa kiwango kikubwa zaidi.”

      Mwanasosholojia Robert Wuthnow, wa Chuo Kikuu cha Princeton, kupitia kura ya maoni aliyofanya kikamili alipata kwamba leo Wamarekani huhangaikia pesa zaidi kuliko walivyofanya kizazi kimoja kilichopita. Kulingana na uchunguzi huo “Wamarekani wengi huhofu kwamba tamaa ya pesa imetangulizwa kuliko maadili mengine kama vile watu kustahiana, ufuatiaji wa haki kazini na kushiriki katika jumuiya zao.”

      Pupa katika jamii imeongezeka zaidi kwa sababu wasimamizi wengi wa biashara wamejiongezea mishahara mikubwa na marupurupu mengi ya kustaafu huku wakiwahimiza wafanyakazi wao wadai mishahara ya kiasi. “Tatizo linalohusu ufuatiaji wa faida miongoni mwa wasimamizi wa biashara ni kwamba mtazamo wao huathiri wengine na kupunguza kiwango cha maadili miongoni mwa watu kwa ujumla,” asema Kjell Ove Nilsson, profesa mwandamizi wa maadili na mkurugenzi wa theolojia kwenye Baraza la Kikristo la Sweden. “Bila shaka, jambo hili huathiri sana maadili—katika jamii na vilevile ya mtu mmoja-mmoja.”

      Utamaduni wa Vyombo vya Habari

      Jambo jingine kuu linalochangia kuzorota haraka kwa maadili mwishoni mwa karne ya 20 ni utamaduni wa vyombo vya habari. “Vyombo vipya vya kusambaza maadili ni watayarishaji wa vipindi vya televisheni, watu mashuhuri katika sinema, watangazaji-mitindo, waimbaji wa rapu ya magenge ya mitaani, na wengine wengi katika utamaduni tata wa vyombo vya habari vya elektroni,” asema Seneta Lieberman. “Watu hao wanaoanzisha mitindo huathiri sana utamaduni wetu na watoto wetu hasa, na mara nyingi hawakubali kulaumiwa kwa kueneza maadili yenye kudhuru.”

      Kwa mfano, Lieberman ataja wimbo uliotungwa na bendi ya muziki wenye mdundo mzito iliyoitwa Cannibal Corpse. Waimbaji wafafanua kwa undani kubakwa kwa mwanamke mmoja huku akiwa ameelekezewa kisu. Yeye pamoja na mfanyakazi mwenzi waliomba kampuni ya kurekodi iondoe rekodi hiyo. Lakini kama asimuliavyo Lieberman, hawakufanikiwa.

      Kwa hiyo, leo wazazi wanaochukua madaraka kwa uzito wanapambana vikali na utamaduni wa vyombo vya habari ili kubainisha ni nani atakayelea watoto wao na kuwa na uvutano juu yao. Lakini vipi juu ya familia ambazo wazazi si waangalifu? “Katika visa hivyo,” asema Lieberman, “utamaduni huo haupingwi bali huonwa kuwa kiwango, na uwezo wa mtoto wa kutofautisha mema na mabaya na mambo anayotanguliza maishani huathiriwa hasa na kile anachojifunza kwenye televisheni, sinema, na redio yenye CD.” Na hivi karibuni zaidi, twaweza kuongezea Internet kwenye orodha hiyo.

      Kurudia “Maadili ya Enzi ya Vyombo vya Mawe”

      Athari za mavutano hayo yasiyofaa zinaonekanaje miongoni mwa vijana? Kwanza, katika miaka ya karibuni watoto na matineja wengi zaidi wamefanya vitendo vikatili vya jeuri dhidi ya watoto wengine na vilevile dhidi ya watu wazima.

      Kisa chenye kushtua kilitukia huko Sweden mwaka wa 1998. Wavulana wawili, wenye umri wa miaka mitano na saba, walimkaba koo mwenzao mwenye umri wa miaka minne waliyekuwa wakicheza naye hadi akafa! Wengi walijiuliza swali hili: Je, watoto hawana uwezo wa kujizuia kabla ya kufanya jambo linalopita kiasi? Daktari wa magonjwa ya akili ya watoto alitoa maelezo haya yenye uzito: “Kujizuia kufanya jambo linalopita kiasi, ni jambo ambalo lazima watu wajifunze,” alisema. “Kungehusu . . . vielelezo ambavyo watoto huona na kile wanachojifunza kutoka kwa watu wazima walio karibu nao.”

      Tukio linalofanana na hilo laweza kuonwa miongoni mwa wahalifu wenye jeuri. Kulingana na Sten Levander, profesa wa magonjwa ya akili katika Sweden, kati ya asilimia 15 hadi 20 ya wafungwa wote leo ni wagonjwa wa akili—watu ambao wanajifikiria sana, wasio na hisia-mwenzi, na wasioweza au wasiotaka kuelewa dhana ya jema na baya. Hata miongoni mwa watoto na vijana wanaoonekana kuwa wa kawaida, watazamaji wameona maadili yakipuuzwa. “Tumerudia maadili ya Enzi ya Vyombo vya Mawe,” adai Christina Hoff Sommers, profesa wa falsafa. Alisema kwamba wanafunzi wake wachanga wanapokabili suala lihusulo jambo linalofaa na lisilofaa, wengi wao hawajihisi salama kabisa. Kisha hujibu kwamba hakuna kitu kama jambo linalofaa au lisilofaa. Wanaamini kwamba kila mtu apaswa kufikiria kile kinachomfaa.

      Katika nyakati za karibuni, wengi wa wanafunzi wake wamepinga kanuni ya adhama ya pekee na thamani ya uhai wa kibinadamu. Kwa mfano, walipoulizwa wangefanya nini ikiwa wangekabili uamuzi kati ya kuokoa uhai wa mnyama kipenzi wao au uhai wa mwanadamu mwenzao wasiyemjua, wengi walisema wangechagua mnyama huyo.

      “Tatizo si kwamba vijana hawana ujuzi, hawaaminiki, ni wakatili, au ni wahaini,” asema Profesa Sommers. “Kusema waziwazi, hawajui jema na baya.” Adai kwamba vijana wengi leo kwa kweli hutilia shaka kama kuna jema au baya, anaona kwamba mtazamo huo hutokeza mojawapo ya tisho kubwa zaidi kwa jamii.

      Kwa hiyo, kupuuza maadili katika nyakati zetu ni jambo halisi. Wengi huhofu kwamba kungeweza kuwa na matokeo hatari. Makala katika gazeti la Die Zeit lililorejezewa mapema yasema kwamba uchumi wa soko huru la leo ungeweza ‘kudhoofika hatua kwa hatua na labda siku fulani kuporomoka kama ilivyotukia kwa mfumo wa kisoshalisti hivi karibuni.’

      Kwa kweli haya yote yanamaanisha nini? Na twapaswa kutazamia wakati ujao wa namna gani?

      [Picha katika ukurasa wa 6, 7]

      “Vyombo vipya vya kusambaza maadili ni watayarishaji wa vipindi vya televisheni, watu mashuhuri katika sinema, watangazaji-mitindo, waimbaji wa rapu ya magenge ya mitaani . . .”

  • Yote Hayo Yamaanisha Nini?
    Amkeni!—2000 | Aprili 8
    • Yote Hayo Yamaanisha Nini?

      IKIWA ungechanganua viwango vya maadili katika miaka ya karibuni, ungeona mwelekeo dhahiri. Bila shaka, viwango vya kiadili vinazidi kuzorota miongoni mwa idadi inayoongezeka ya watu. Maana halisi ya hilo ni nini?

      Je, yamaanisha, kama wengine wadaivyo kwamba ustaarabu wetu wote na wanadamu wote wamehukumiwa maangamizi au wanakaribia kuangamizwa? Au je, mabadiliko hayo ni sehemu tu ya kuzorota na kuboreka kwa hali ambako ni kwa kawaida katika historia?

      Watu wengi hufikiri hivyo. Wanaona kuvunjika kwa maadili katika siku zetu kuwa mojawapo tu kati ya mielekeo mingi, ambayo imekuwapo katika historia yote. Wanatarajia kabisa kwamba hatimaye mwelekeo wa kawaida utarudi na kwamba viwango vya juu vya maadili vitarejea. Je, wako sahihi?

      “Siku za Mwisho”

      Acheni tuzingatie mambo hakika kwa kufikiria kitabu ambacho kwa karne nyingi kilikuwa na mamlaka inayokubaliwa na wengi kuhusu masuala ya kiadili—Neno la Mungu, Biblia. Inaelimisha sana kulinganisha ulimwengu wa leo na ufafanuzi wa unabii unaotolewa katika Biblia kuhusu muhula wa kukata maneno katika historia ya kibinadamu. Hiki ndicho kipindi inachokiita “siku za mwisho” au “umalizio wa mfumo wa mambo.” (2 Timotheo 3:1; Mathayo 24:3) Kama idokezwavyo na semi hizo, kipindi hiki kitaashiria mwisho hususa wa kipindi maalumu na mwanzo wa kipindi kingine kipya.

      Neno la Mungu lilitabiri kwamba siku za mwisho zingeashiriwa na “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” Ili kusaidia watazamaji walio makini watambue siku za mwisho, Biblia hutoa habari kadhaa ambazo kwa pamoja hufanyiza ufafanuzi dhahiri, au ishara yenye mambo mengi, ya kipindi hiki cha pekee.

      Tabia Mbaya za Watu

      Ona mojawapo ya ishara hizo ambayo ni yenye kutokeza zaidi leo: “Watu watakuwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakithibitika kuwa si kweli kwa nguvu ya hiyo.” (2 Timotheo 3:2, 5) Hakujawa na kipindi kingine katika historia kilichotiwa alama na kupuuzwa kabisa kwa dini kwa njia ya kupindukia. Mungu amepuuzwa kila mahali kuwa mamlaka pekee, na watu wengi hawaikubali Biblia kuwa chanzo pekee cha kweli. Bila shaka, kungali kuna dini, lakini nyingi zina uvutano mdogo. Zimekuwa wonyesho tu.

      Biblia hutaja sehemu nyingine ya ishara hiyo: “Watu watakuwa . . . wasio na hali ya kujidhibiti, wakali,” na “kwa sababu ya kuongezeka kwa uasi-sheria upendo wa idadi iliyo kubwa zaidi utapoa.” (2 Timotheo 3:2, 3; Mathayo 24:12) Neno la Kigiriki lililotafsiriwa “kali” lamaanisha, miongoni mwa mambo mengine, “kukosa hisia-mwenzi za kibinadamu.” Leo watoto wachanga zaidi wanadhihirika kuwa “wakali” na wanafanya uhalifu unaozidi kuwa wenye jeuri.

      Zaidi ya hilo, maendeleo ya haraka ya tekinolojia na ya kiuchumi na pupa ambayo imesababishwa nayo yamefanya watu wengi zaidi wapuuze maadili ya zamani. Bila kuwajali wengine, wanatumia njia yoyote ile, pamoja na njia zisizo za haki, kunyakua vitu vingi kadiri wawezavyo ili kutosheleza tamaa yao ya kichoyo. Ongezeko kubwa la kucheza kamari ni uthibitisho mwingine wa uchoyo, na takwimu za uhalifu uliofanywa miongo michache iliyopita zadhihirisha kabisa jambo hilo.

      Jambo ambalo limeenea hasa katika kipindi chetu ni hili: “Watu watakuwa . . . wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu.” (2 Timotheo 3:2, 4) Mfano mmoja wa hilo ni kwamba watu wanataka raha za kimwili, lakini hawataki daraka la kuishi na mwenzi mmoja wa ndoa maishani. Tokeo limekuwa visa vingi vya familia zilizovunjika, watoto wasio na furaha na ufungamano wa familia, wazazi wasio na wenzi, na maradhi ya kuambukizwa kingono.

      Jambo jingine kuhusu ishara hiyo ni kwamba “watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha.” (2 Timotheo 3:2) Kulingana na gazeti la Kijerumani Die Zeit, “ubinafsi ndio huchochea mfumo wa [kiuchumi wa leo].” Ufuatiaji wa pesa ndio jambo la maana zaidi maishani mwa wengi kuliko wakati mwingine wowote. Maadili mengine hupuuzwa katika ufuatiaji huu wa kibinafsi.

      Matukio ya Ulimwengu

      Mbali na kufafanua kuporomoka kwa maadili ya kibinadamu, Biblia pia ilitabiri kwamba siku za mwisho zingetiwa alama na mabadiliko makubwa yasiyo ya kawaida ambayo yangeathiri familia ya kibinadamu. Kwa mfano, inasema kwamba “taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme; na kutakuwa na matetemeko makubwa ya dunia, na katika mahali pamoja baada ya pengine magonjwa ya kuambukiza na upungufu wa chakula.”—Luka 21:10, 11.

      Mbali na karne ya 20, hakujawa na kipindi kingine katika historia ambapo watu wengi sana wamehusika na misiba mikuu katika kipindi kifupi kama hicho. Mathalani, zaidi ya watu milioni 100 walikufa katika vita wakati huo, idadi iliyo kubwa zaidi kuliko idadi ya makafara wa vita katika karne kadhaa zilizopita wanapojumlishwa pamoja. Karne ya 20 ilitokeza vita viwili vilivyokuwa tofauti kabisa na vingine hivi kwamba vikaitwa vita vya ulimwengu. Mapambano ya ulimwenguni pote kama hayo hayakuwa yamepata kutokea.

      Kichocheo Kutoka kwa Kani Mbovu

      Biblia hufunua pia kuwepo kwa kiumbe mwovu wa roho mwenye nguvu, “aitwaye Ibilisi na Shetani,” ambaye kusudi lake ni kushawishi watu waache maadili ya kweli na kuwatumbukiza kwenye ufisadi wa kiadili. Inasema kwamba katika siku za mwisho, ameteremka kwenye dunia, “akiwa na hasira kubwa, akijua ana kipindi kifupi cha wakati.”—Ufunuo 12:9, 12.

      Katika Biblia Ibilisi hufafanuliwa kuwa “mtawala wa mamlaka ya hewa, roho ambayo sasa hutenda katika wana wa kutotii.” (Waefeso 2:2) Hilo ladokeza kwamba Ibilisi hudhihirisha uvutano wenye nguvu juu ya wanadamu wengi, kwa kawaida bila wao kutambua, kama vile huenda nyakati nyingine tukakosa kuona kichafuzi katika hewa.

      Kwa mfano, uvutano wa Shetani huonekana katika njia nyingi za mawasiliano ya kisasa: vidio, sinema, televisheni, Internet, matangazo ya biashara, vitabu, na magazeti. Habari nyingi, hasa ile inayoelekezwa kwa vijana wasio na ujuzi, imejaa mielekeo yenye kuchukiza, kama vile ubaguzi wa rangi, uchawi, ukosefu wa adili, na jeuri ya kikatili.

      Watu wengi wenye moyo mweupe wamevutiwa na ufanano kati ya ufafanuzi wa Biblia kuhusu siku za mwisho na hali halisi katika ulimwengu wa leo. Ni kweli kwamba kumekuwa na matukio fulani katika historia kabla ya karne ya 20 ambayo kwa kadiri ndogo yalilingana na ufafanuzi wa Biblia. Lakini mambo yote yahusuyo ile ishara yameonekana tu katika karne ya 20, na sasa katika karne ya 21.

      Kipindi Kipya Maalumu Kinachokuja

      Wale wanaoamini kwamba wanadamu wataangamizwa, na wale wanaodai kwamba mambo yataendelea kama kawaida wamekosea. Badala yake, Biblia huonyesha waziwazi kwamba mahali pa jamii ya ulimwengu ya sasa inayotawala dunia patachukuliwa na kitu fulani kipya kabisa.

      Baada ya Yesu kuorodhesha idadi kadhaa ya matukio ya ishara ya siku za mwisho, alisema: “Katika njia hii nyinyi pia, wakati mwonapo mambo hayo yakitukia, jueni kwamba ufalme wa Mungu uko karibu.” (Luka 21:31) Ufalme wa Mungu wa kimbingu ndio uliokuwa kichwa kikuu cha mahubiri ya Yesu. (Mathayo 6:9, 10) Naye Mungu alimteua awe Mfalme wa Ufalme huo, ambao ni serikali itakayotawala dunia yote hivi karibuni.—Luka 8:1; Ufunuo 11:15; 20:1-6.

      Mwishoni mwa siku za mwisho, Ufalme wa Mungu wa kimbingu mikononi mwa Kristo utaondoa wote ambao ni maadui wake—Ibilisi na wale wanaomuunga mkono—na kuleta ulimwengu mpya wa uadilifu badala ya jamii ya sasa iliyozorota kiadili. (Danieli 2: 44) Katika ulimwengu huo mpya, watu wenye moyo mzuri watafurahia uhai udumuo milele katika dunia iliyogeuzwa kuwa paradiso.—Luka 23:43; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:3, 4.

      Wale ambao wanachukia sana kupotoka kwa sasa kwa maadili na kutambua kwamba ishara yenye mambo mengi ya siku hizi za mwisho inatimizwa kwa matukio ya kisasa wanaweza kutazamia wakati ujao mtukufu. Kwa sababu hiyo tunamshukuru Mungu Mweza Yote, anayetujali sisi wanadamu na ambaye ana kusudi tukufu kwa uumbaji wake, dunia.—Zaburi 37:10, 11, 29; 1 Petro 5:6, 7.

      Mashahidi wa Yehova wanakualika ujifunze mengi kuhusu Muumba wetu mwenye upendo na tazamio la uhai katika ulimwengu safi kiadili, aliotayarishia wote wanaomtafuta. Kama isemavyo Biblia, ‘hii yamaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.’—Yohana 17:3.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki