Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuenea kwa Chuki
    Mnara wa Mlinzi—2000 | Agosti 15
    • Kuenea kwa Chuki

      “Watu hawafahamu kamwe wale wanaochukia.”—JAMES RUSSELL LOWELL, MWANDISHI WA INSHA NA BALOZI.

      INAONEKANA kama chuki imetuzunguka pande zote. Majina kama Timor Mashariki, Kosovo, Liberia, Littleton, na Sarajevo—vilevile makundi yenye kufuata sera za Nazi, magenge yenye kunyoa upara, na makundi ya wazungu wenye ubaguzi wa rangi—Maiti pamoja na picha za majengo yaliyoteketezwa, makaburi walimozikiwa watu wengi ambayo yamechimbuliwa karibuni, yamedumu akilini mwetu.

      Matazamio ya wakati ujao usio na chuki, mapambano, na jeuri yamevunjika. Danielle Mitterand, mke wa aliyekuwa rais wa Ufaransa aliyekufa, akumbuka hivi kuhusu wakati alipokuwa kijana: “Watu walikuwa na tazamio la kuishi katika jamii huru yenye kutumainika; wakiwa wenye amani ya akili wakiwa miongoni mwa wengine; walitazamia maisha yenye afya, amani na adhama wakilindwa na ulimwengu mkarimu na thabiti.” Mawazo hayo yalipatwa na nini? Aliomboleza hivi: “Miaka hamsini baadaye, kwa wazi tazamio letu limepatwa na pigo.”

      Kuibuka tena kwa chuki hakuwezi kamwe kupuuzwa. Imeenea kote na inazidi kuonekana katika njia mbaya zaidi. Usalama wa kibinafsi ambao mamilioni ya watu huchukua kuwa jambo la kawaida umedhoofishwa na wimbi la vitendo vibaya vya chuki, yaonekana kila kitendo kinachofuata ni chenye kuhofisha kuliko kilichotangulia. Hata ikiwa hamna chuki nyumbani kwetu au nchi tunamoishi, kuna chuki kwingineko. Huenda tunaona uthibitisho wa hilo kila siku kwenye televisheni katika habari na programu za matukio. Hata chuki imeenea katika Internet. Fikiria mifano michache.

      Mwongo uliopita umekuwa na ongezeko lisilo na kifani la utukuzo wa taifa. “Utukuzo wa taifa,” asema Joseph S. Nye, Jr. mkurugenzi wa Harvard Center for International Affairs, “waendelea kuimarika badala ya kupungua katika sehemu kubwa ya ulimwengu. Badala ya ulimwengu kuwa jamaa moja makundi yanajitenga na kujitofautisha na yale mengine ingawa kunao mfumo mmoja wa kupeleka habari. Hilo nalo hutokeza uhasama.”

      Namna nyingine za chuki ni za kichinichini, huwa zimefichika ndani ya nchi au hata katika ujirani. Kalasinga mmoja mzee alipouawa na washiriki watano wa genge lenye kunyoa upara katika Kanada, tukio hilo “lilikazia kile ambacho wengine wanakiona kuwa kuibuka upya kwa uhalifu wenye kutokezwa na chuki katika nchi inayosifiwa mara nyingi kwa ajili ya uvumiliano wake wa kijamii.” Huko Ujerumani, mashambulizi dhidi ya jamii tofauti yanayofanywa na watu wenye itikadi kali yaliongezeka kwa asilimia 27 katika mwaka wa 1997 baada ya kupungua polepole katika miaka iliyopita. “Hilo ni tukio lenye kuvunja moyo,” akasema Waziri wa Mambo ya Ndani Manfred Kanther.

      Ripoti moja ilifunua kwamba watoto zaidi ya 6,000 katika sehemu ya kaskazini ya Albania wanaishi kama wafungwa nyumbani kwao kwa kuhofia kupigwa risasi na maadui wa wazazi wao. Watoto hao ni wahasiriwa wa chuki za kifamilia “ambazo zimevuruga maisha ya maelfu ya familia.” Kulingana na Shirika la Upelelezi la Federal Bureau of Investigation (FBI), katika Marekani “ubaguzi wa kijamii ulichochea zaidi ya nusu ya visa 7,755 vya uhalifu wenye kuchochewa na chuki uliofanywa katika mwaka wa 1998 na kuripotiwa kwa shirika la FBI.” Uhalifu mwingine wenye kuchochewa na chuki ulisababishwa na ubaguzi wa kidini, kikabila au wa taifa, na ubaguzi dhidi ya walemavu.

      Zaidi ya hayo, kila siku vichwa vya habari magazetini huonyesha ongezeko kubwa la kuhofu wageni kunakoelekezewa hasa wakimbizi ambao sasa wanazidi milioni 21. Kwa kusikitisha, wengi wanaoonyesha chuki kuwaelekea wageni ni vijana wanaochochewa na wanasiasa wasiojali na watu wengine wenye kutafuta visingizio. Ishara zisizo dhahiri sana za jambo hili hutia ndani kutokuwa na itibari, kukosa uvumilivu, na kuwa na maoni yasiyofaa juu ya watu walio tofauti.

      Ni nini baadhi ya sababu za kuenea huku kwa chuki? Na ni nini liwezalo kufanywa ili kukomesha chuki? Makala ifuatayo itashughulikia maswali hayo.

  • Njia Pekee ya Kukomesha Chuki
    Mnara wa Mlinzi—2000 | Agosti 15
    • Njia Pekee ya Kukomesha Chuki

      “Palipo na hofu hapakosi chuki. . . . Tunachukia kile tunachokiogopa na hivyo palipo na chuki hofu yaotea.”—CYRIL CONNOLLY, MCHAMBUZI WA FASIHI NA MHARIRI.

      WANASOSHIOLOJIA wengi wanaamini kwamba chuki imetia mizizi akilini mwa mwanadamu. “Sehemu kubwa ya chuki huenda hata ikawa imetiwa katika mfumo wote wa utendaji wa akili,” imo ndani ya asili ya kibinadamu, akasema mtaalamu mmoja wa siasa.

      Yaeleweka ni kwa nini wanafunzi wanaochunguza hali ya kibinadamu hufikia mikataa ya namna hiyo. Somo la pekee katika uchunguzi wao ni wanaume na wanawake ambao wamezaliwa “katika kosa” na “katika dhambi” kulingana na rekodi ya Biblia iliyopuliziwa. (Zaburi 51:5, NW) Hata Muumba mwenyewe, akikadiria mwanadamu asiye mkamilifu katika milenia zilizopita, ‘aliona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.’—Mwanzo 6:5.

      Ubaguzi, upendeleo, na matokeo yake ya chuki hutokana na ubinafsi na kutokamilika kwa mwanadamu kulikorithiwa. (Kumbukumbu la Torati 32:5) Kwa kusikitisha, hapana shirika lolote la kibinadamu au serikali, hata sera yake iwe gani, ambayo imeweza kufanyiza sheria iwezayo kubadilisha moyo wa mwanadamu katika mambo hayo. Mleta-habari wa nchi za kigeni Johanna McGeary alisema: “Hakuna polisi wa ulimwenguni pote, hata awe mwenye uwezo kadiri gani, awezaye kuingilia mambo na kuondoa chuki ambayo imesababisha umwagaji mwingi wa damu katika Bosnia, Somalia, Liberia, Kashmir, na Caucasus.”

      Hata hivyo, kabla ya kutafuta utatuzi, lazima tupate kuelewa kiini cha visa vya chuki.

      Chuki Yachochewa na Hofu

      Chuki hujitokeza kwa njia nyingi. Mwandishi Andrew Sullivan alifafanua hali hiyo vizuri: “Kuna chuki yenye hofu, na chuki yenye kuhisi tu kuchukizwa; kuna chuki ya kuonyesha uwezo, na chuki ya kutokuwa na uwezo; kuna ulipizaji kisasi, na kuna chuki inayotokana na husuda. . . . Kuna chuki ya mwonezi, na chuki ya mwenye kuonewa. Kuna chuki ya kichinichini, na chuki inayokwisha. Na kuna chuki ilipukayo, na chuki isiyopamba moto kamwe.”

      Bila shaka, baadhi ya sababu kuu zinazochochea mapambano ya chuki katika siku zetu ni zile za kijamii na kiuchumi. Ubaguzi mbaya sana na milipuko ya chuki mara nyingi hutokea katika maeneo ambamo mna matajiri wachache. Chuki huonekana pia katika mahali ambapo kiwango cha maisha cha sehemu fulani ya jumuiya chatishwa na mmiminiko wa wageni.

      Baadhi yao huenda wakahisi kwamba wageni hao watachukua kazi zao, wakilipwa mishahara ya chini, au kusababisha kupungua kwa thamani ya mali. Iwe hofu hiyo ina msingi au la ni jambo jingine. Hofu ya kupata hasara kiuchumi na hofu kwamba viwango vya jamii au mtindo wake wa maisha utazorota ni sababu zenye nguvu zinazotokeza ubaguzi na chuki.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki