-
Jinsi Unavyoweza Kuishi MilimaniAmkeni!—2004 | Machi 8
-
-
Mambo Unayopaswa Kutazamia
Watu wengi huhisi kama Doug alivyohisi alipofika kwenye milima ya Andes. Anasema: “Nilihisi kizunguzungu ghafula na karibu nizimie nilipokuwa nikibeba masanduku yetu kwenye uwanja wa ndege. Ingawa tatizo hilo lilikwisha, katika majuma mawili ya kwanza niliumwa na kichwa na sikulala vizuri. Ghafula ningeamka nikihisi kwamba ninakosa hewa. Kisha, kwa miezi kadhaa sikuwa na hamu ya chakula, nilichoka upesi, na nililala sana.” Katty anaongeza hivi: “Sikuamini mambo ambayo watu walikuwa wakisema kuhusu matatizo yanayosababishwa na kuwa milimani. Sasa ninaelewa.”
Kulingana na madaktari, Doug alikosa usingizi kwa sababu ya matatizo ya kupumua. Tatizo hilo huwapata watu wanapofika milimani. Lakini huenda ukawa na wasiwasi tatizo hilo likikupata. Mara kwa mara, unapokuwa usingizini, unaweza kushindwa kupumua kwa sekunde kadhaa. Wakati mwingine, jambo hilo linaweza kufanya uamke ghafula ukijaribu kupumua.
Watu wengine hawana tatizo hata kidogo wanapofika milimani. Watu wengine huathiriwa wanapokuwa kwenye milima yenye urefu wa meta 2,000. Karibu nusu ya watu wanaopanda milima kwa mara ya kwanza huathiriwa na mwinuko wa meta 3,000. Hata wakazi wa milimani wanaporudi baada ya juma moja au mawili tu kutoka katika maeneo ya chini, wao hupatwa na matatizo hayohayo mara nyingi. Kwa nini?
Kwa Nini Milima Huathiri Mwili Wako?
Matatizo mengi husababishwa na ukosefu wa oksijeni. Kwa sababu shinikizo la hewa angani hupungua kadiri unavyopanda, kwenye meta 2,000 juu ya usawa wa bahari oksijeni hewani hupungua kwa asilimia 20 hivi, na kwenye meta 4,000 oksijeni unayopumua hupungua kwa asilimia 40. Ukosefu wa oksijeni huathiri utendaji mwingi wa mwili. Utendaji wa misuli hupungua, mfumo wa neva hushindwa kustahimili mifadhaiko, na mfumo wa kusaga chakula hushindwa kufyonza mafuta. Kwa kawaida mwili wako unapohitaji oksijeni nyingi, unapumua zaidi. Kwa hiyo, kwa nini isiwe hivyo unapofika milimani?
Haieleweki vizuri jinsi mwili wako unavyodhibiti kiasi cha hewa unachopumua. Lakini unapopumua sana kwa sababu ya kutumia nguvu nyingi, haimaanishi kwamba jambo hilo limesababishwa na ukosefu wa oksijeni. Badala yake, inaonekana kaboni-dioksidi iliyojikusanya kwenye damu kwa sababu ya utendaji wa misuli ndiyo inayokufanya upumue zaidi. Unapokuwa milimani unapumua zaidi, lakini hilo halilipii upungufu wa oksijeni.
Ni nini kinachosababisha maumivu ya kichwa? Msemaji mmoja katika Kongamano la Kwanza la Ulimwengu Kuhusu Tiba na Magonjwa ya Milimani huko La Paz, Bolivia, alieleza kwamba dalili nyingi za ugonjwa unaosababishwa na kuwa milimani huletwa na kukusanyika kwa umajimaji ubongoni. Kwa watu wengine, hilo husababisha shinikizo kichwani. Yaelekea kwa sababu ya ukubwa wa fuvu la kichwa, watu wengine hawapatwi na matatizo hayo. Hata hivyo, mara chache hali hiyo inaweza kuhatarisha uhai. Misuli inapolegea, unaposhindwa kuona vizuri, unapopata maono, na kuchanganyikiwa, unapaswa kumwona daktari mara moja na kuondoka kwenye eneo hilo.
Tahadhari
Athari za kuwa milimani huzidi siku ya pili au ya tatu, kwa hiyo siku chache kabla na baada ya kufika ni vizuri kula vyakula vyepesi, hasa usiku. Badala ya kula vyakula vyenye mafuta mengi, unapaswa kula vyakula vyenye wanga, kama vile wali, shayiri, na viazi. Huenda ikafaa kufuata shauri hili, “Kula kiamsha-kinywa kama mfalme, lakini chakula cha jioni kama maskini.” Pia, epuka kutumia nguvu nyingi, kwa kuwa hiyo inaweza kusababisha ugonjwa mbaya wa milimani. Kwa kuwa vijana wengi hupuuza shauri hilo, wao ndio huumia zaidi.
Pia inafaa “uvae kofia, na ujipake mafuta yanayozuia miale ya jua,” kwa kuwa hakuna angahewa la kutosha kuzuia miale hatari ya jua. Miale hiyo inaweza kuwasha au hata kuharibu macho yako, kwa hiyo tumia miwani mizuri ya jua. Hewa ya mlimani hukausha machozi na kuwasha macho. Kwa hiyo, unywe maji mengi.
Madaktari wamewashauri watu wenye shinikizo la juu la damu, anemia selimundu, ugonjwa wa moyo au mapafu au wanene kupita kiasi wachunguzwe vizuri na madaktari kabla ya kuamua kutembelea sehemu za milimani.a Ikiwa una mafua makali, ugonjwa wa kupumua, au nimonia, huenda ikafaa kuahirisha safari yako kwa sababu unapokuwa milimani ukiwa na magonjwa hayo au ukifanya mazoezi mengi, yanaweza kusababisha hatari ya maji kujikusanya mapafuni. Matatizo ya kupumua yanaweza kufanya hata watu ambao wameishi mlimani kwa miaka mingi kukosa oksijeni na hivyo kupata magonjwa hatari. Kwa upande mwingine, mara nyingi watu wanaougua pumu hufurahia kuishi milimani. Kikundi kimoja cha madaktari Warusi kililiambia Kongamano la Kwanza la Ulimwengu Kuhusu Tiba na Magonjwa ya Milimani kwamba wao huwapeleka milimani wagonjwa wenye matatizo fulani kama sehemu ya matibabu.
-
-
Jinsi Unavyoweza Kuishi MilimaniAmkeni!—2004 | Machi 8
-
-
a Madaktari fulani hupendekeza dawa ya acetazolamide ili kuwasaidia kupumua wanapokuwa milimani. Dawa nyingine za ugonjwa wa milimani hutangazwa, lakini madaktari fulani hawazipendekezi.
-