Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Tunahitaji Milima
    Amkeni!—2005 | Machi 22
    • Tunahitaji Milima

      “Ukipanda milima utafurahia mambo mazuri. Utahisi utulivu wa mazingira kama miti inayopata mwangaza wa jua. Utaburudishwa na upepo unaovuma, utahisi nguvu za upepo mkali, na mahangaiko yako yatatoweka kama majani yanayopukutika.”—JOHN MUIR, MWANDISHI NA MTAALAMU WA VITU VYA ASILI WA MAREKANI.

      KAMA vile John Muir alivyogundua zaidi ya karne moja iliyopita, milima inaweza kutuchochea. Ukuu wa milima hutuvutia, wanyama wanaoishi huko hutupendeza, na utulivu wake hututuliza. Kila mwaka, mamilioni ya watu hutembelea milima ili kufurahia mandhari na kujiburudisha. Klaus Toepfer, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Tangu kale, milima imewastaajabisha na kuwachochea watu wa jamii na utamaduni mbalimbali.”

      Lakini milima inakabili matatizo. Kwa karne nyingi milima haijaharibiwa na wanadamu kwa sababu ya kuwa mbali na makao yao. Hata hivyo, sasa inakabili hatari. Kulingana na ripoti moja ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa, “baadhi ya maeneo ambayo hayajaharibiwa yanatoweka haraka kwa sababu ya kilimo, ujenzi, na mambo mengine.”

      Sehemu kubwa ya dunia ni milima. Asilimia 50 ya watu ulimwenguni hutegemea mali za asili zinazopatikana milimani. Na mamilioni ya watu huishi milimani. Zaidi ya kuwawezesha watu kufurahia mandhari yenye kuvutia na yenye utulivu, milima ina faida nyingine nyingi. Hebu tuzungumzie baadhi ya faida ambazo wanadamu hupata kutokana na milima.

      Umuhimu wa Milima

      ◼ KUHIFADHI MAJI. Milima ndiyo chanzo cha mito mikubwa na cha maji yanayoingia katika hifadhi nyingi za maji. Huko Amerika Kaskazini, Mto Colorado na Mto Rio Grande hupata karibu maji yote kutoka kwenye Milima ya Rocky. Asilimia 50 hivi ya watu ulimwenguni huishi Asia Kusini na Asia Mashariki. Wengi wa watu hao hutegemea mvua inayonyesha kwenye milima mikubwa iliyo katika maeneo ya Himalaya, Karakoram, Pamirs, na Tibet.

      Toepfer anasema hivi: “Milima, ambayo ni hifadhi kubwa za maji ulimwenguni, ni muhimu kwa uhai wa viumbe wote duniani na kwa afya ya watu kila mahali.” Pia anaongeza hivi: “Mambo yanayotukia katika vilele virefu zaidi vya milima huathiri uhai katika maeneo ya chini, mito, na hata bahari.” Katika maeneo mengi, milima huhifadhi theluji wakati wa baridi kali, kisha katika majira ya kuchipua na ya kiangazi theluji hiyo huyeyuka polepole na kunywesha ardhi. Katika maeneo makavu ya ulimwengu, maji yanayotumiwa kunyunyizia mashamba hutokana na theluji inayoyeyuka katika milima ya mbali. Milima mingi ina miinuko yenye misitu ambayo hufyonza maji ya mvua kama sifongo na kufanya maji yatiririke polepole hadi mitoni bila kusababisha mafuriko.

      ◼ MAKAO YA WANYAMA WA PORI NA UNAMNA-NAMNA WA VIUMBE. Wanadamu hawajaiharibu milima sana kwa sababu iko mbali na makao yao na haiwezi kutumiwa sana kwa kilimo. Kwa hiyo, mimea na wanyama ambao wametoweka katika maeneo ya chini wanapatikana milimani. Kwa mfano, kuna jamii 4,500 za mimea katika Mbuga ya Kitaifa ya Kinabalu huko Malasia. Mbuga hiyo inapatikana mlimani katika eneo dogo kuliko New York City. Lakini idadi hiyo ya mimea ni zaidi ya robo ya idadi ya jamii za mimea inayopatikana huko Marekani. Wanyama fulani huko China wanaoitwa giant panda, tai fulani wa Andes, na chui fulani wanaopatikana huko Asia ya kati huishi milimani sawa na jamii nyingine nyingi za wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka.

      Kulingana na gazeti National Geographic, wataalamu fulani wa mazingira wamekadiria kwamba “zaidi ya thuluthi moja ya mimea na viumbe wenye uti wa mgongo wanaoishi kwenye nchi kavu hupatikana katika eneo lisilofikia asilimia 2 ya ukubwa wa dunia.” Jamii nyingi husongamana katika maeneo yenye rutuba ambayo hayajaharibiwa. Maeneo mengi kati ya hayo yako milimani, nayo yana jamii nyingi za viumbe ambao hutunufaisha sote. Baadhi ya mimea muhimu inayoliwa ulimwenguni hukuzwa milimani. Kwa mfano, mahindi hukuzwa katika maeneo ya milimani nchini Mexico, viazi na minyanya hukuzwa katika Milima ya Andes huko Peru, na ngano hukuzwa katika milima ya Caucasus.

      ◼ TAFRIJA NA MANDHARI YANAYOVUTIA. Pia milimani kuna vitu vya asili vyenye kuvutia. Kuna maporomoko ya maji yanayopendeza, maziwa maridadi, na sehemu nyingi zenye kuvutia zaidi ulimwenguni. Si ajabu kwamba thuluthi moja ya maeneo ya ulimwengu yanayohifadhiwa yako milimani. Na maeneo hayo hutembelewa sana na watalii.

      Mamilioni ya watalii kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu hutembelea mbuga za kitaifa zilizo mbali. Watu kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu hutembelea Mbuga ya Kitaifa ya Denali huko Alaska ili wajionee Mlima McKinley, ambao ndio mlima mrefu zaidi katika Amerika Kaskazini. Watu wengi hutembelea Bonde la Ufa ili wajionee milima mirefu ya Kilimanjaro na Meru au kuona wanyama wengi wa pori wanaoishi katika maeneo yaliyo kati ya milima hiyo. Jamii nyingi za watu wanaoishi milimani hunufaika kutokana na utalii. Hata hivyo, biashara ya utalii isipodhibitiwa inaweza kuharibu mazingira ya asili.

      Ujuzi Unaopatikana Milimani

      Kwa karne nyingi, watu wanaoishi milimani wamejifunza jinsi ya kusitawi katika hali ngumu za mazingira. Wamefanyiza matuta kwa ajili ya kilimo, na yangali yanatumiwa hata baada ya miaka 2,000. Wamefuga wanyama wanaopatikana milimani, kama vile llama na yak, ambao wanaweza kukabiliana na hali ngumu za milimani. Na mambo ambayo wamejifunza yanaweza kuwa muhimu sana katika kuhifadhi milima ambayo sisi sote hutegemea.

      Alan Thein Durning wa Taasisi ya Worldwatch anaeleza hivi: “Katika sehemu za mbali za kila bara, wenyeji wa asili ndio hutunza maeneo makubwa ambayo hayajaharibiwa sana.” Anaongeza hivi: “Ujuzi mwingi walio nao kuhusu mazingira . . . unaweza kulinganishwa na ujuzi unaopatikana katika maktaba za sayansi ya kisasa.” Ujuzi huo mwingi unahitaji kuhifadhiwa sana sawa na mali za asili zinazopatikana milimani.

      Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilidhamini Mwaka wa Milima wa Kimataifa wa 2002. Ili kukazia jinsi wanadamu wanavyotegemea milima, wasimamizi wa mradi huo walitunga msemo huu, “Sisi Sote Ni Watu wa Milimani.” Walikusudia kuwajulisha watu kuhusu matatizo yanayokabili milima ulimwenguni na kutafuta njia za kuilinda.

      Hatua hiyo ilifaa. Yule aliyetoa hotuba ya msingi katika Kongamano la Ulimwengu la Milima lililofanywa huko Bishkek nchini Kyrgyzstan mwaka wa 2002, alisema: “Mara nyingi sana, milima huonwa kuwa chanzo cha mali nyingi za asili, lakini matatizo ya watu wanaoishi huko pamoja na utunzaji wa mazingira ya milima hupuuzwa.”

      Ni nini baadhi ya matatizo yanayokabili milima na watu wanaoishi huko? Matatizo hayo huathirije kila mmoja wetu?

  • Milima Imo Hatarini
    Amkeni!—2005 | Machi 22
    • Milima Imo Hatarini

      “Kila mtu anaweza kufaidika kwa kuhakikisha kwamba maeneo ya milimani yanaendelea kutokeza mali za asili kwa ajili ya vizazi vingi vya wakati ujao.”—KOFI ANNAN, KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA.

      MILIMA humfanya mtu afikirie kuhusu ukuu, uthabiti, na nguvu. Je, kweli milima inaweza kuhatarishwa? Huenda watu fulani wakashindwa kuwazia kwamba milima inaweza kuwa hatarini. Lakini, kwa hakika milima imo hatarini. Wahifadhi wa mazingira hutaja baadhi ya matatizo hususa yanayokabili mazingira ya milimani. Matatizo yote hayo ni makubwa na hali inazidi kuwa mbaya. Hebu ona baadhi ya matatizo yanayoikumba milima.

      ◼ MIRADI YA MAENDELEO. Asilimia 25 hivi ya maeneo ya milimani yanahatarishwa na barabara, uchimbaji wa migodi, mabomba, mabwawa, na miradi mingine ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika miaka 30 ijayo. Ujenzi wa barabara unaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo kwenye miinuko mikali, na barabara hizo hutumiwa na wakataji wa miti ambao husababisha madhara zaidi. Kila mwaka, tani bilioni kumi hivi za madini huchimbuliwa hasa kwenye milima, na takataka nyingi sana hutokezwa.a

      ◼ ONGEZEKO LA JOTO LA DUNIA. Taasisi ya Worldwatch inasema hivi: “Miaka tisa yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa imekuwepo tangu 1990.” Na hasa maeneo ya milimani ndiyo yameathiriwa. Mito ya barafu imekuwa ikiyeyuka, na vilele vyenye theluji vinapungua, na kulingana na wanasayansi fulani jambo hilo litaathiri hifadhi za maji na kusababisha maporomoko hatari ya ardhi. Sasa maziwa mengi ya barafu huko Himalaya yanakaribia kufurika na kusababisha msiba. Jambo hilo limetukia mara kadhaa katika miaka iliyopita.

      ◼ KILIMO CHA KIWANGO KIDOGO. Ongezeko la idadi ya watu linawafanya wanadamu kulima katika maeneo yasiyo na rutuba. Kulingana na uchunguzi mmoja, karibu nusu ya maeneo ya milimani barani Afrika yanatumiwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji, yaani, asilimia 10 kwa ajili ya mazao na asilimia 34 kwa ajili ya malisho. Mara nyingi, kilimo hicho hakileti faida kubwa, kwani maeneo hayo hayafai kwa ukuzaji wa mimea.b Na mimea huharibiwa wakati maeneo yaleyale yanapotumiwa kupita kiasi kuwalisha ng’ombe. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba asilimia 3 tu ya maeneo ya milimani ndiyo yanayoweza kulimwa bila kuharibu mazingira.

      ◼ VITA. Ongezeko la vita vya wenyewe kwa wenyewe limesababisha uharibifu wa mazingira ya milimani. Vituo vya waasi huwa milimani. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inakadiria kwamba asilimia 67 ya maeneo ya milimani ya Afrika yameathiriwa na “mapambano ya wanadamu yenye jeuri.” Isitoshe, maeneo fulani ya milimani hutumiwa kutokeza dawa za kulevya, na mara nyingi hilo husababisha uharibifu wa mazingira na mapambano makali kwa kutumia silaha.

      Je, Jitihada Zaidi Zinahitajiwa?

      Matokeo ya uharibifu wa milima unaosababishwa na wanadamu yanaonekana. Mafuriko, maporomoko ya ardhi, na ukosefu wa maji ni baadhi ya mambo yanayoonyesha kuna matatizo. Serikali zimeanza kuchukua hatua. Miti inapandwa, na ukataji wa miti umepigwa marufuku katika sehemu fulani. Mbuga za kitaifa zimeanzishwa ili kulinda maeneo yanayovutia sana na makao ya wanyama wa pori yanayokabili hatari kubwa zaidi.

      Lakini hata maeneo yanayolindwa huathiriwa na uharibifu wa mazingira. (Ona sanduku lenye kichwa “Baadhi ya Maeneo ya Pekee ya Asili.”) Kutoweka haraka kwa jamii za viumbe kunaonyesha kwamba jitihada za kulinda maeneo ya milimani hazijafanikiwa kabisa. Wataalamu wanajua matatizo yanayokabili milima, lakini jitihada kubwa hazijafanywa ili kuhifadhi maeneo ambayo bado hayajaharibiwa. Mwanabiolojia maarufu E. O. Wilson, anasema hivi: “Ujuzi wetu wa kisayansi unanitia moyo, lakini ninavunjika moyo kwa sababu ya kuharibiwa kwa maeneo muhimu yaliyo na jamii nyingi za viumbe.”

      Je, kutoweka kwa jamii za viumbe ni tatizo kubwa? Kulingana na wanabiolojia wengi, wanadamu hufaidika sana wanyama na mimea inapohifadhiwa. Wanabiolojia hutaja mfano wa mmea unaoitwa rosy periwinkle unaopatikana huko Madagaska kwenye maeneo ya milimani yenye jamii nyingi za viumbe. Mmea huo umetumiwa kutokeza dawa muhimu ya ugonjwa wa lukemia. Isitoshe, kwa miaka mingi, mti wa cinchona unaopatikana katika Milima ya Andes umetumiwa kutengeneza kwinini na dawa nyingine za malaria. Mimea mingi inayokua katika maeneo ya milimani imetumiwa kuokoa uhai wa mamilioni ya watu. Ni kweli kwamba baadhi ya mimea hiyo inayokua milimani imepandwa na kusitawi pia katika maeneo yasiyo na milima. Hata hivyo, jambo linalohangaisha ni kwamba uharibifu mkubwa wa mimea inayopatikana milimani huenda ukasababisha kutoweka kwa mimea muhimu ambayo bado haijagunduliwa. Na huenda mimea hiyo ni muhimu kwa afya na inaweza kutumiwa kutengeneza dawa.

      Je, uharibifu huo unaweza kukomeshwa? Je, maeneo yaliyoharibiwa yanaweza kurekebishwa? Je, milima itaendelea kuvutia na kuhifadhi jamii nyingi za viumbe?

      [Maelezo ya Chini]

      a Kwa wastani, tani tatu za takataka hutokezwa wakati pete moja tu ya dhahabu inapotengenezwa.

      b Kwa upande mwingine, kwa karne nyingi watu wanaoishi milimani wamejifunza kulima katika maeneo hayo bila kuharibu mazingira.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Viumbe wa Milimani

      Puma hupatikana hasa milimani. Mnyama huyo hupatikana hasa katika Milima ya Rocky na ya Andes. Sawa na wanyama wengi wakubwa wanaowinda, puma amehamia maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa sababu ya kuhatarishwa na wanadamu.

      Dubu anayeitwa red panda anapatikana tu katika Milima ya Himalaya (hata katika maeneo ya chini ya Mlima Everest). Ijapokuwa anaishi mbali, mnyama huyo anakabili hatari ya kutoweka kwa sababu ya uharibifu wa misitu ya mianzi ambayo ndiyo chakula chake.

      [Hisani]

      Cortesía del Zoo de la Casa de Campo, Madrid

      Dubu anayeitwa brown bear alipatikana katika sehemu nyingi za Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini. Huko Ulaya, anapatikana tu katika maeneo machache ya milimani, ingawa anapatikana zaidi huko Alaska, Siberia, na kwenye Milima ya Rocky nchini Kanada. Katika karne iliyopita, idadi ya dubu hao ilipungua kwa asilimia 99 huko Marekani.

      Tai aina ya golden eagle hupatikana sana katika maeneo mengi ya milimani ya Kizio cha Kaskazini. Inasikitisha kwamba huko Ulaya idadi yao imepungua kufikia chini ya vikundi 5000 vya ndege wawili wawili wa kiume na wa kike kwa sababu hapo zamani ‘walichukiwa.’

      Mtaalamu wa vitu vya asili wa China anayeitwa Tang Xiyang anasema kwamba dubu anayeitwa giant panda “hutegemea hasa vitu vitatu.” Vitu hivyo ni “milima mirefu na mabonde yenye kina kirefu, misitu mikubwa ya mianzi, na vijito.” Kulingana na kadirio moja, idadi ya panda waliosalia porini haizidi 1,600.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Baadhi ya Maeneo ya Pekee ya Asili

      Mbuga ya Kitaifa ya Yosemite (California, Marekani) ilianzishwa katika mwaka wa 1890 kutokana na jitihada kubwa za mtaalamu wa vitu vya asili John Muir. Mandhari yake yanayopendeza huwavutia watalii milioni nne kila mwaka. Hata hivyo, wasimamizi wa mbuga hiyo hukabili matatizo wanapojitahidi kuilinda, huku wakitosheleza mahitaji ya watu wanaovutiwa na viumbe.

      Mbuga ya Kitaifa ya Podocarpus (Ekuado) ni hifadhi ya msitu unaofunikwa na mawingu katika Milima ya Andes. Msitu huo una jamii nyingi za wanyama na za mimea kwani kuna zaidi ya aina 600 za ndege na jamii 4,000 hivi za mimea. Dawa ya kwinini, ambayo imeokoa uhai wa watu wengi sana, iligunduliwa katika eneo hilo. Sawa na mbuga nyingi, mbuga hiyo inahatarishwa na ukataji wa miti na uwindaji haramu.

      Mlima Kilimanjaro (Tanzania) ni mmojawapo wa milima mikubwa zaidi ya volkeno ulimwenguni na ndio mlima mrefu zaidi barani Afrika. Tembo hulisha katika maeneo ya chini, huku mimea ya pekee kama vile giant lobelia na giant groundsel ikikua katika maeneo ya juu. Mlima huo unahatarishwa hasa na uwindaji haramu, ukataji wa miti, na ulishaji wa ng’ombe.

      Mbuga ya Kitaifa ya Teide (Visiwa vya Canary) ni hifadhi ya mimea ya pekee ambayo hupamba eneo hilo lenye milima ya volkeno. Mazingira ya visiwa vilivyo na milima ya volkeno yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na jamii mpya za viumbe.

      Mbuga za kitaifa za Pyrenees na Ordesa (Ufaransa na Hispania) ni hifadhi za milimani zilizo na mandhari yanayovutia, mimea, na wanyama wengi. Sawa na safu nyingine za milima huko Ulaya, Milima ya Pyrenees imeathiriwa na ongezeko la sehemu za kuteleza kwenye theluji na za kuwahudumia watalii. Pia, mazingira ya eneo hilo yameathiriwa sana kwa sababu ya kubadili mbinu za kilimo zilizotumiwa kwa muda mrefu.

      Mbuga ya Kitaifa ya Sǒraksan ndiyo mbuga inayotembelewa zaidi katika Jamhuri ya Korea. Vilele vyake vyenye kupendeza na miinuko yake yenye misitu huvutia sana katika majira ya kupukutika kwa majani. Hata hivyo, kwa kuwa watu wengi hutembelea mbuga hiyo, mwishoni mwa juma vijia vyake hujaa watu kama vile barabara za jiji.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      Mimea ya Milimani

      Tower of jewels. Kwa muda wa majuma machache katika majira ya kuchipua, mmea huo wenye kustaajabisha hukua kufikia urefu wa mtu. Mmea huo hupatikana tu kwenye vilele vya milima miwili ya volkeno iliyo meta 1,800 hivi juu ya usawa wa bahari katika Visiwa vya Canary. Jamii nyingi za mimea ya milimani hupatikana tu katika maeneo ya juu kama hayo.

      Carline thistle hukua katika Milima ya Alps na Pyrenees. Rangi yake nyangavu hung’aa majira ya kiangazi yanapokaribia kwisha na wadudu hula maua yake sana.

      English iris. Jamii za mmea huo zilizopatikana kwa kuchavushwa pamoja na mimea mingine hukuzwa kwenye bustani. Maua mengi yanayokuzwa kwenye bustani yalitolewa milimani.

      Mountain houseleek ni mmojawapo wa mimea mingi ya milimani ambayo hushikamana na nyufa za miamba. Mmea huo, ambao hupatikana katika milima ya Ulaya Kusini, unaitwa pia “ishi milele” kwa sababu unastahimili hali ngumu na unaishi kwa muda mrefu.

      Bromeliad. Aina nyingi za mmea huo na za mmea wa okidi husitawi kwenye maeneo ya Tropiki katika misitu ya milimani ambayo hufunikwa na mawingu. Mimea hiyo hukua hata kwenye maeneo yaliyo meta 4,500 juu ya usawa wa bahari.

      Algerian iris unapatikana katika Mlima wa Er Rif na wa Atlas, kaskazini mwa Afrika, na eneo hilo la Mediterania lina jamii nyingi za mimea inayokabili hatari ya kutoweka.

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Kuchimbua shaba na dhahabu karibu na Milima ya Maoke, huko Indonesia

      [Hisani]

      © Rob Huibers/Panos Pictures

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      “Rosy periwinkle”

  • Ni Nani Atakayeiokoa Milima?
    Amkeni!—2005 | Machi 22
    • Ni Nani Atakayeiokoa Milima?

      KATIKA mwaka wa 2002, Kongamano la Ulimwengu la Milima lilifanywa kwa siku nne huko Bishkek nchini Kyrgyzstan (Asia ya kati). Huo ulikuwa mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu milima. Wadhamini wa mkutano huo walitumaini kwamba mwaka wa 2002 ungekuwa “mwanzo wa enzi mpya, wakati ambapo watu wangetambua umuhimu wa milima.”

      Katika kongamano hilo, “Sera za Milima za Bishkek” ziliidhinishwa. Sera hizo zinatia ndani maagizo kwa ajili ya kila mtu anayehusika katika kuhifadhi milima. Kusudi la sera hizo ni “kuboresha maisha ya watu wanaoishi milimani, kuhifadhi mazingira ya milima, na kutumia mali za asili zinazopatikana milimani kwa njia bora zaidi.”

      Maendeleo fulani yamefanywa. Ulimwenguni pote, kuna mbuga za kitaifa zinazolinda maeneo yenye kuvutia sana na yenye jamii nyingi za viumbe. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, vikundi vya wanamazingira vimefaulu kwa kadiri fulani kuzuia uharibifu wa mazingira. Mradi mmoja uliopendekezwa katika Kongamano la Milima huko Bishkek ulihusu jitihada kabambe za kuondoa takataka za nyuklia katika milima ya Kyrgyzstan. Takataka hizo zenye sumu hatari zingechafua vyanzo vya maji yanayotumiwa na asilimia 20 ya watu huko Asia ya kati.

      Hata hivyo, bado miradi ya kuhifadhi milima inakabili matatizo makubwa. Kwa mfano, mwaka wa 1995, viongozi huko Kanada walianzisha “Sheria ya Misitu” ili kulinda msitu wa mvua uliobaki huko British Columbia. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa baadaye ulionyesha kwamba kampuni za kukata miti zilipuuza sheria hiyo na kuendelea kukata miti hata katika maeneo yenye miinuko mikali. Sheria hiyo ililegezwa mwaka wa 1997 kwa sababu wafanyabiashara wa mbao walisema kwamba inawalemea sana.

      Matatizo yanayoikabili milima hayasababishwi tu na shughuli za kibiashara. Azimio la mwisho katika Kongamano la Bishkek lilionyesha kwamba vita, umaskini, na njaa huchangia uharibifu wa milima unaoendelea. Milima na sehemu nyingine za dunia zitaendelea kuharibiwa mpaka visababishi vyote vya uharibifu wa mazingira vitakapokomeshwa.

      Mungu Anajali Uumbaji Wake

      Licha ya hali hizo zenye kusikitisha, tuna sababu ya kuwa na tumaini. Mungu Mweza-Yote anajua mambo yanayokabili uumbaji wake. Biblia humfafanua kuwa Yule “ambaye vilele vya milima ni vyake.” (Zaburi 95:4) Yeye pia huwajali wanyama wa milimani. Kwenye Zaburi 50:10, 11, Yehova anasema hivi: “Kila mnyama wa mwituni ni wangu, wanyama walio juu ya milima elfu moja. Najua vizuri kila kiumbe chenye mabawa cha milimani, na makundi ya wanyama wa porini yako pamoja nami.”

      Je, Mungu ana njia ya kuokoa mazingira ya ulimwengu yaliyomo hatarini? Bila shaka! Biblia inasema kwamba ‘ameusimamisha ufalme ambao hautaharibiwa kamwe.’ (Danieli 2:44) Yesu Kristo, Mtawala aliyewekwa rasmi wa serikali hiyo ya mbinguni, anaijali sana dunia na wakaaji wake. (Methali 8:31) Utawala wake utaleta amani duniani, utakomesha matumizi yote mabaya ya mali za asili, na kurekebisha maeneo ya dunia yaliyoharibiwa.—Ufunuo 11:18.

      Ikiwa unatamani sana suluhisho hilo, bila shaka utaendelea kusali kwamba ‘Ufalme wa Mungu uje.’ (Mathayo 6:9, 10) Hapana shaka sala hizo zitajibiwa. Karibuni, Ufalme wa Mungu utakomesha ukosefu wa haki na kurekebisha maeneo ya dunia yaliyoharibiwa. Wakati huo, kwa njia ya mfano, milima ‘itapiga vigelegele kwa shangwe.’—Zaburi 98:8.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki