Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Milima Imo Hatarini
    Amkeni!—2005 | Machi 22
    • Milima Imo Hatarini

      “Kila mtu anaweza kufaidika kwa kuhakikisha kwamba maeneo ya milimani yanaendelea kutokeza mali za asili kwa ajili ya vizazi vingi vya wakati ujao.”—KOFI ANNAN, KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA.

      MILIMA humfanya mtu afikirie kuhusu ukuu, uthabiti, na nguvu. Je, kweli milima inaweza kuhatarishwa? Huenda watu fulani wakashindwa kuwazia kwamba milima inaweza kuwa hatarini. Lakini, kwa hakika milima imo hatarini. Wahifadhi wa mazingira hutaja baadhi ya matatizo hususa yanayokabili mazingira ya milimani. Matatizo yote hayo ni makubwa na hali inazidi kuwa mbaya. Hebu ona baadhi ya matatizo yanayoikumba milima.

      ◼ MIRADI YA MAENDELEO. Asilimia 25 hivi ya maeneo ya milimani yanahatarishwa na barabara, uchimbaji wa migodi, mabomba, mabwawa, na miradi mingine ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika miaka 30 ijayo. Ujenzi wa barabara unaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo kwenye miinuko mikali, na barabara hizo hutumiwa na wakataji wa miti ambao husababisha madhara zaidi. Kila mwaka, tani bilioni kumi hivi za madini huchimbuliwa hasa kwenye milima, na takataka nyingi sana hutokezwa.a

      ◼ ONGEZEKO LA JOTO LA DUNIA. Taasisi ya Worldwatch inasema hivi: “Miaka tisa yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa imekuwepo tangu 1990.” Na hasa maeneo ya milimani ndiyo yameathiriwa. Mito ya barafu imekuwa ikiyeyuka, na vilele vyenye theluji vinapungua, na kulingana na wanasayansi fulani jambo hilo litaathiri hifadhi za maji na kusababisha maporomoko hatari ya ardhi. Sasa maziwa mengi ya barafu huko Himalaya yanakaribia kufurika na kusababisha msiba. Jambo hilo limetukia mara kadhaa katika miaka iliyopita.

      ◼ KILIMO CHA KIWANGO KIDOGO. Ongezeko la idadi ya watu linawafanya wanadamu kulima katika maeneo yasiyo na rutuba. Kulingana na uchunguzi mmoja, karibu nusu ya maeneo ya milimani barani Afrika yanatumiwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji, yaani, asilimia 10 kwa ajili ya mazao na asilimia 34 kwa ajili ya malisho. Mara nyingi, kilimo hicho hakileti faida kubwa, kwani maeneo hayo hayafai kwa ukuzaji wa mimea.b Na mimea huharibiwa wakati maeneo yaleyale yanapotumiwa kupita kiasi kuwalisha ng’ombe. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba asilimia 3 tu ya maeneo ya milimani ndiyo yanayoweza kulimwa bila kuharibu mazingira.

      ◼ VITA. Ongezeko la vita vya wenyewe kwa wenyewe limesababisha uharibifu wa mazingira ya milimani. Vituo vya waasi huwa milimani. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inakadiria kwamba asilimia 67 ya maeneo ya milimani ya Afrika yameathiriwa na “mapambano ya wanadamu yenye jeuri.” Isitoshe, maeneo fulani ya milimani hutumiwa kutokeza dawa za kulevya, na mara nyingi hilo husababisha uharibifu wa mazingira na mapambano makali kwa kutumia silaha.

      Je, Jitihada Zaidi Zinahitajiwa?

      Matokeo ya uharibifu wa milima unaosababishwa na wanadamu yanaonekana. Mafuriko, maporomoko ya ardhi, na ukosefu wa maji ni baadhi ya mambo yanayoonyesha kuna matatizo. Serikali zimeanza kuchukua hatua. Miti inapandwa, na ukataji wa miti umepigwa marufuku katika sehemu fulani. Mbuga za kitaifa zimeanzishwa ili kulinda maeneo yanayovutia sana na makao ya wanyama wa pori yanayokabili hatari kubwa zaidi.

      Lakini hata maeneo yanayolindwa huathiriwa na uharibifu wa mazingira. (Ona sanduku lenye kichwa “Baadhi ya Maeneo ya Pekee ya Asili.”) Kutoweka haraka kwa jamii za viumbe kunaonyesha kwamba jitihada za kulinda maeneo ya milimani hazijafanikiwa kabisa. Wataalamu wanajua matatizo yanayokabili milima, lakini jitihada kubwa hazijafanywa ili kuhifadhi maeneo ambayo bado hayajaharibiwa. Mwanabiolojia maarufu E. O. Wilson, anasema hivi: “Ujuzi wetu wa kisayansi unanitia moyo, lakini ninavunjika moyo kwa sababu ya kuharibiwa kwa maeneo muhimu yaliyo na jamii nyingi za viumbe.”

      Je, kutoweka kwa jamii za viumbe ni tatizo kubwa? Kulingana na wanabiolojia wengi, wanadamu hufaidika sana wanyama na mimea inapohifadhiwa. Wanabiolojia hutaja mfano wa mmea unaoitwa rosy periwinkle unaopatikana huko Madagaska kwenye maeneo ya milimani yenye jamii nyingi za viumbe. Mmea huo umetumiwa kutokeza dawa muhimu ya ugonjwa wa lukemia. Isitoshe, kwa miaka mingi, mti wa cinchona unaopatikana katika Milima ya Andes umetumiwa kutengeneza kwinini na dawa nyingine za malaria. Mimea mingi inayokua katika maeneo ya milimani imetumiwa kuokoa uhai wa mamilioni ya watu. Ni kweli kwamba baadhi ya mimea hiyo inayokua milimani imepandwa na kusitawi pia katika maeneo yasiyo na milima. Hata hivyo, jambo linalohangaisha ni kwamba uharibifu mkubwa wa mimea inayopatikana milimani huenda ukasababisha kutoweka kwa mimea muhimu ambayo bado haijagunduliwa. Na huenda mimea hiyo ni muhimu kwa afya na inaweza kutumiwa kutengeneza dawa.

  • Milima Imo Hatarini
    Amkeni!—2005 | Machi 22
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Viumbe wa Milimani

      Puma hupatikana hasa milimani. Mnyama huyo hupatikana hasa katika Milima ya Rocky na ya Andes. Sawa na wanyama wengi wakubwa wanaowinda, puma amehamia maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa sababu ya kuhatarishwa na wanadamu.

      Dubu anayeitwa red panda anapatikana tu katika Milima ya Himalaya (hata katika maeneo ya chini ya Mlima Everest). Ijapokuwa anaishi mbali, mnyama huyo anakabili hatari ya kutoweka kwa sababu ya uharibifu wa misitu ya mianzi ambayo ndiyo chakula chake.

      [Hisani]

      Cortesía del Zoo de la Casa de Campo, Madrid

      Dubu anayeitwa brown bear alipatikana katika sehemu nyingi za Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini. Huko Ulaya, anapatikana tu katika maeneo machache ya milimani, ingawa anapatikana zaidi huko Alaska, Siberia, na kwenye Milima ya Rocky nchini Kanada. Katika karne iliyopita, idadi ya dubu hao ilipungua kwa asilimia 99 huko Marekani.

      Tai aina ya golden eagle hupatikana sana katika maeneo mengi ya milimani ya Kizio cha Kaskazini. Inasikitisha kwamba huko Ulaya idadi yao imepungua kufikia chini ya vikundi 5000 vya ndege wawili wawili wa kiume na wa kike kwa sababu hapo zamani ‘walichukiwa.’

      Mtaalamu wa vitu vya asili wa China anayeitwa Tang Xiyang anasema kwamba dubu anayeitwa giant panda “hutegemea hasa vitu vitatu.” Vitu hivyo ni “milima mirefu na mabonde yenye kina kirefu, misitu mikubwa ya mianzi, na vijito.” Kulingana na kadirio moja, idadi ya panda waliosalia porini haizidi 1,600.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki