-
Zawadi ya MuzikiAmkeni!—2011 | Agosti
-
-
Zawadi ya Muziki
HEBU wazia maisha bila muziki. Kuishi bila muziki unaotuliwaza, bila muziki wa kimahaba, bila nyimbo za kisasa zenye midundo yenye kuvutia, bila muziki wa kiokestra unaochochea hisia, na bila muziki mtamu usio na maneno. Huenda watu wengi wakahisi kwamba maisha bila muziki yanachosha na hayavutii.
Kwa kweli, muziki hugusa hisia zetu kwa njia mbalimbali. Unatutuliza na kutusisimua, unatuchangamsha na kutuchochea. Unatufanya tuwe na shangwe nyingi na kutufanya tutokwe na machozi. Hata hivyo, kwa sababu muziki una uwezo wa kugusa mioyo yetu, una nguvu sana. Kwa nini muziki hutuchochea sana? Jibu ni rahisi: Muziki ni zawadi nzuri sana kutoka kwa Mungu. (Yakobo 1:17) Kwa sababu hiyo, unapaswa kuthaminiwa, unapaswa kuwa wenye kujenga, na wote—wazee kwa vijana—wanapaswa kuufurahia.
Muziki umekuwapo tangu zamani. Kwa mfano, vitu vya kale vilivyochimbuliwa vinaonyesha kwamba karne nyingi kabla ya Wakati wetu wa Kawaida makabila ya Afrika yalipiga ngoma, baragumu, na kengele. Wachina wa kale walipiga kinanda cha aina fulani na zumari. Watu kutoka Misri, India, Israeli, na Mesopotamia walipiga kinubi. Huenda habari hususa na ya zamani zaidi kuhusu muziki ni ile iliyorekodiwa kwenye Biblia katika Mwanzo 4:21. Katika andiko hilo tunajifunza kwamba mwanamume mmoja aliyeitwa Yubali ndiye aliyekuwa “mwanzilishi wa wote wanaotumia kinubi na zumari.” Karne nyingi baadaye, Mfalme Sulemani wa Israeli alipendezwa sana na muziki hivi kwamba alitafuta mbao bora zaidi na kutengeneza vinubi na vinanda vya aina nyingine.—1 Wafalme 10:11, 12.
Ni wazi kwamba ili mtu afurahie muziki uliopigwa katika nyakati hizo, ilimbidi apige au amsikilize mtu mwingine akipiga ala fulani ya muziki. Hata hivyo, tofauti na hilo, mamilioni ya watu leo wanaweza kupata muziki kwa urahisi sana. Leo, unaweza kurekodi au kupakua muziki wowote na kuusikiliza kupitia vifaa mbalimbali kutia ndani vile vinavyoweza kubebwa mfukoni. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika nchi moja ya Magharibi mnamo 2009 ulionyesha kwamba vijana wenye umri wa kati ya miaka 8 na 18 hutumia zaidi ya saa 2 kila siku wakisikiliza muziki na habari nyingine zilizorekodiwa.
Mazoea hayo yanaonyesha kwa nini muziki pamoja na vifaa vya kisasa vya kurekodi na kusambaza muziki vinauzwa kwa wingi sana. Kwa kweli, uuzaji wa muziki pamoja na bidhaa za muziki umekuwa biashara kubwa sana. Lakini, je, umewahi kujiuliza ni mambo gani yanayohusika ili kutokeza muziki unaopendwa na kuuzwa kwa wingi?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 3]
Muziki Kwenye Intaneti
KUPAKUA: Kwa kawaida watu hulipia faili ya muziki ambayo wanapakua, na hivyo inakuwa mali yao. Wengine hujiandikisha—mara nyingi wanaponunua simu au vifaa vingine vya kielektroniki—na hivyo wanaweza kupakua na kucheza muziki katika kipindi walichojiandikisha.
MUZIKI UNAOCHEZA MOJA KWA MOJA: Huu ni muziki uliorekodiwa na kuhifadhiwa katika vituo fulani vya Intaneti ambavyo mtu anaweza kusikiliza moja kwa moja bila kuupakua. Muziki huo hautozwi ingawa mtu anaweza kupakua kiasi fulani iwapo atajiandikisha kwenye kituo hicho.
[Chati/Picha katika ukurasa wa 3]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Maendeleo Katika Kurekodi
Miaka ya 1880
Gramafoni
Miaka ya 1890
Kanda za sumaku
Miaka ya 1940
Kanda ya kurekodiwa moja kwa moja
Miaka ya 1960
Kanda za kaseti
Miaka ya 1980
CD
Miaka ya 1990
Faili za kielektroniki (MP3, AAC, WAV, n.k.)
-
-
Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?Amkeni!—2011 | Agosti
-
-
Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?
BIASHARA ya muziki inabadilika-badilika upesi na ina ushindani mkubwa. Mapendezi ya wasikilizaji hubadilika, miziki iliyopendwa inapitwa na wakati, na mbinu za kurekodi na kusambaza muziki zinatokea. Wadhamini “hutafuta muziki motomoto kila wakati,” anasema Kelli S. Burns mtaalamu wa mawasiliano. Lakini si rahisi kufanya “muziki fulani” uuzwe kwa wingi. “Vijana wengi hutamani sana kuwa wasanii maarufu, . . . lakini si kazi rahisi kupata mkataba na kampuni ya kurekodi,” kinasema kitabu kimoja cha mwongozo.—Ona sanduku “Mabadiliko Katika Biashara ya Muziki,” kwenye ukurasa wa 6.
Kutunga Maneno ya Muziki
Wasanii (1) hujaribu sana kutunga maneno yanayogusa hisia za watu—maneno ambayo hufanya watu watafakari kuhusu matumaini yao, matarajio, na hisia za ndani zaidi. Watu huimba hasa kuhusu nini? Ikiwa umejibu, mahaba, hilo ndilo jibu sahihi. Wasanii pia hujaribu kubuni mstari fulani wenye maneno yanayovutia sana ambayo yatanasa akili ya msikilizaji na kubaki akilini kwa muda mrefu.
Kisha, msanii hurekodi wimbo wake kwa mara ya kwanza, ili usikizwe na kampuni ya kurekodi. Ikiwa baada ya kusikiliza wimbo ule wasimamizi wa kampuni ya kurekodi wanaona kwamba wimbo huo utakuwa maarufu, huenda basi wakampa msanii huyo mkataba wa kurekodi (2). Lakini ikiwa hawana uhakika na msanii huyo (labda kwa sababu yeye si maarufu sana), wanaweza kununua wimbo huo na kumpa msanii mwingine maarufu zaidi.
Ndani ya Studio
Ili kusimamia kazi ya kurekodi (3), kwa kawaida kampuni za kurekodi humtafuta producer, au mtayarishaji, aliye na uzoefu. Yeye huamua mtindo ambao msanii atatumia na kuidhinisha rekodi ya mwisho ya wimbo huo. Yeye ndiye hutafuta na kusimamia studio ya kurekodia itakayotumiwa, anatafuta pia wapangaji wa muziki, wanakili wa muziki, wanamuziki, waimbaji wa ziada, mainjinia wa kurekodi, na vifaa vitakavyorekodi muziki wa hali ya juu ambao utawavutia wasikilizaji.
Nyimbo nyingi hurekodiwa hatua kwa hatua, mara nyingi kuanzia kwa kurekodi midundo ya ngoma, gitaa mbalimbali, na piano. Kisha, sauti za waimbaji wanaoongoza muziki hurekodiwa pamoja na zile zinazoambatana na ala za muziki, na madoido mengine ya pekee ya sauti huchanganywa ili kutokeza nakala ya awali ya wimbo uliorekodiwa kielektroniki (4).
Uuzaji
Ili muziki uwe maarufu na kuuzwa zaidi, mara nyingi makampuni ya kurekodi hutokeza video za muziki (5). Video hizo zenye urefu wa dakika tatu hadi tano huenda zikatokeza msisimuko kama ule wa tamasha ya muziki na pia kusaidia wasikilizaji kumwona na kumsikia msanii huyo. Pia video hizo zinaweza kuiletea kampuni ya kurekodi pesa nyingi sana.
Wasanii wa muziki huuza albamu nyingi zaidi katika maeneo wanakofanyia tamasha za muziki (6). Hivyo wao hutangaza kuhusu albamu zao mpya popote waendapo na wanapopanga kufanya tamasha za muziki. Pia wasanii wengi hufungua Tovuti (7) na kupachika baadhi ya nyimbo, picha, video, blogu za kibinafsi, habari kuhusu tamasha za muziki zijazo, kutia ndani viunganishi vinavyowaelekeza mashabiki kwenye vituo ambavyo wanaweza kutoa maoni yao, na pia wanawaelekeza kwenye vituo ambavyo muziki wao huuzwa.
Ni nani anayeamua ikiwa muziki utakuwa maarufu sana? Ni wewe—msikilizaji. Hivyo basi, ni nini hukuchochea uchague muziki fulani? Unapochagua muziki, je, wewe huvutiwa na mdundo tu au msanii, au wewe una viwango vinavyokuongoza? Haya ni maswali muhimu, kwa sababu muziki una nguvu na unaweza kutuathiri sana. Mambo haya yanatukumbusha shauri muhimu kutoka kwa Muumba wetu: “Linda moyo wako kuliko vitu vingine vyote vinavyopaswa kulindwa, kwa maana ndiko zinakotoka chemchemi za uzima.”—Methali 4:23.
Unaweza kutii shauri hilo lenye hekima jinsi gani unapochagua muziki? Na ikiwa wewe ni mzazi, unaweza kutimiza jinsi gani jukumu lako la kuwalinda watoto wako dhidi ya hatari za kiroho, kiakili, na kihisia?
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Mabadiliko Katika Biashara ya Muziki
Intaneti, vyombo vya kurekodi muziki vya bei ya chini, pamoja na programu za kompyuta zimechangia sana mabadiliko katika biashara ya muziki. Siku hizi, wanamuziki wanaweza kurekodi muziki wa hali ya juu kwa ustadi sana wakiwa nyumbani na kuusambaza kote ulimwenguni. Kulingana na ripoti moja katika gazeti The Economist, “wasanii maarufu sana walirekodi na kusambaza muziki bila kutumia kampuni yoyote ya kurekodi.”
-
-
Je, Utafanya Maamuzi Yenye Hekima?Amkeni!—2011 | Agosti
-
-
Je, Utafanya Maamuzi Yenye Hekima?
“Muziki ambao wazazi wangu wanasikiliza unachosha sana,” analalamika Jordan, mwenye umri wa miaka 17.a
“Muziki ambao mwanangu husikiliza umejaa maneno yenye hasira na mambo yenye kushtua,” anasema Denise, mama yake.
KWA nini wazazi huzozana na vijana wao kuhusu muziki? Jambo moja ni kwamba mapendezi ya mtu yanaweza kubadilika kadiri anavyokua. Sababu nyingine ni kwamba muziki hubadilika. Hivyo, muziki ambao ni maarufu leo, huenda kesho ukawa umepitwa na wakati.
Vyovyote vile, muziki hutuathiri kwa njia fulani. Je, umewahi kutambua jinsi ambavyo muziki huathiri hisia zako? Mfalme Sauli wa Israeli la kale aliposumbuliwa na hisia, muziki taratibu ulimtuliza. (1 Samweli 16:23) Kwa njia fulani, muziki unaweza kufananishwa na watu tunaoshirikiana nao. Muziki fulani hutufanya tuwe na hisia nzuri, kama vile furaha na upendo. Lakini mwingine hutuchochea tuwe na hasira na hata chuki.—Methali 13:20.
Kwa kuwa muziki una uvutano wenye nguvu jinsi hiyo, wazazi na watoto wanapaswa kuwa wenye hekima wanapochagua muziki watakaosikiliza. Ikiwa wewe ni mzazi, je, unapendezwa kikweli kujua vijana wako anasikiliza muziki wa aina gani na kwa muda gani? Je, unaweka viwango vya kufuatwa?
Hilo halimaanishi tu kupiga marufuku albamu fulani au muziki wa aina fulani. Bali unapaswa kuwasaidia vijana wako kuchagua muziki wa aina nyingine. Kitabu On Becoming Teenwise kinasema hivi: “Huwezi tu kumnyang’anya mtu kitu fulani anachopenda na kuthamini sana na kuacha pengo. Lazima awe na kitu kingine cha badala, kitu kipya kitakachochukua nafasi ya kile kilichoondolewa, la sivyo atarudia tabia zake za hapo awali.”
Jambo lingine la kutiliwa maanani ni hili: Watoto wako hutumia muda mwingi kiasi gani kusikiliza muziki? Je, wanatumia muda ambao wanapaswa kutumia kufanya mambo mengine ya maana zaidi, kama vile kazi ya shule, mambo ya kiroho, au majukumu mengine ya nyumbani? Kama vile tu Biblia inavyosema, “kuna wakati uliowekwa wa kila kitu.”—Mhubiri 3:1.
Huenda tatizo lingine likawa kujitenga. Ni kweli kwamba sisi sote tunahitaji kuwa na wakati wa faragha na hivyo tunapaswa kutenga wakati ili tuwe na pindi za kutafakari kwa undani mambo muhimu maishani. (Zaburi 1:2, 3) Hata hivyo, mtu anapotumia wakati mwingi akiwa amejitenga na wengine, huenda awe na mwelekeo wa kujifikiria sana na kuwa na ubinafsi. (Methali 18:1) Felipe, ambaye sasa ana umri wa miaka 20, anasema kwamba wakati aliotumia kusikiliza muziki ulikuwa ‘wakati muhimu wa kuwa peke yake.’ “Lakini,” anasema, “mama yangu alikuwa na wasiwasi kwamba ninajitenga na watu.”
Ni nini kitakachowasaidia vijana kama vile Felipe na wazazi wao waepuke kuzozana kuhusu muziki? Ni kwa njia gani sisi sote tunaweza kuchagua muziki kwa hekima? Wengi wamepata msaada kwa kutumia kanuni za Biblia. Hebu chunguza maswali matatu yafuatayo pamoja na watoto wako.
● Muziki huu unapitisha ujumbe gani? “Uasherati na ukosefu wa usafi wa kila namna au pupa visitajwe hata kidogo katikati yenu.” (Waefeso 5:3) Nyimbo nyingi huwa na maneno safi. Lakini nyingine, kwa njia iliyo wazi au iliyofichika, hukubaliana au hata kuchochea mwenendo unaovunja kanuni za maadili, kama zile zinazopatikana katika Biblia. Kwa kweli, miziki ya aina fulani inajulikana kwa upotovu wa maadili, chuki, na jeuri. Mwandikaji, Karen Sternheimer, anasema kwamba “nyakati nyingine maneno yanayotumika katika muziki wa rapu huwa yenye kushtua sana, yenye ukatili, yenye matusi, na yamejaa chuki dhidi ya wanawake.” Mara nyingi maneno ya muziki wa heavy-metal hutia ndani jeuri na uchawi. Hata miziki mingi yenye midundo ya kisasa inaweza kuwachochea wasikilizaji wawe na mwenendo usiofaa. Kwa hiyo, unapochagua muziki utakaosikiliza, unapaswa kutumia ‘nguvu zako za kufikiri’ ili ufanye uamuzi wa hekima. (Waroma 12:1) Usichague muziki kwa sababu ni maarufu tu au kwa kuwa una mdundo mtamu.
● Muziki unaathiri hisia zangu jinsi gani? “Linda moyo wako . . . kwa maana ndiko zinakotoka chemchemi za uzima.” (Methali 4:23) Muziki unaochagua unaonyesha wewe ni mtu wa aina gani. Unaweza kuathiri akili na moyo wako. Jordan aliyenukuliwa hapo awali anasema hivi: “Baada ya kusikiliza aina fulani ya muziki nilihisi nikiwa mwenye hasira na jeuri.” Jiulize hivi: ‘Muziki ninaosikiliza unaathiri jinsi gani mawazo na hisia zangu? Je, baada ya kuusikiliza, mimi huwa nimeburudishwa au ninajihisi nikiwa na wasiwasi na nimekasirika? Je, unachochea mawazo machafu?’ (Wakolosai 3:5) Ikiwa muziki fulani unakufanya uwe na hisia zisizofaa au mawazo machafu, ni jambo la hekima kuuharibu. (Mathayo 5:28, 29) Hannah, mwenye umri wa miaka 17, anasema, “Nimeona madhara yanayotokea mtu anaposikiliza muziki mbaya, nami sitaki kuusikiliza hata kidogo.”
● Je, muziki utaathiri viwango vyangu? “Chukieni yaliyo mabaya, pendeni yaliyo mema,” linasema Amosi 5:15. Siku hizi ni vigumu kufuata shauri hilo, kwa sababu kama vile tu unabii wa Biblia unavyosema, watu ni “wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda pesa, wenye kujidai, wenye majivuno, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio washikamanifu, wasio na upendo wa asili, wasiotaka makubaliano yoyote, wachongezi, wasiojizuia, wakali, wasiopenda wema, . . . wanaopenda raha badala ya kumpenda Mungu.” (2 Timotheo 3:1-4) Kwa sababu hiyo, mstari wa 5 unasema: “Nawe geukia mbali kutoka kwa hao.”
Unaweza jinsi gani kugeukia mbali kutoka kwa watu kama hao? Ni wazi kwamba unahitaji kufanya mengi zaidi ya kuwaepuka. Ni lazima pia uepuke muziki na vitu vingine vinavyohusiana na njia zao zisizo za kimungu. (Waefeso 4:25, 29, 31) Lakini je, kufanya hivyo kunamaanisha usisikilize muziki wowote? La hasha!
Panua Mapendezi Yako
Katika familia nyingi, wazazi na watoto hufurahia kusikiliza na kubadilishana rekodi za muziki. Lena anasema hivi: “Binti yangu mwenye umri wa miaka 13 aliniomba nisikilize muziki anaopenda sana, na sasa mimi ninafurahia kusikiliza muziki wake.” Heather, mwenye umri wa miaka 16, hufurahia kusikiliza muziki ambao wazazi wake husikiliza, nao hubadilishana CD kwa ukawaida.
Ulimwenguni pote, mamilioni ya Mashahidi wa Yehova wa umri wote na wa tamaduni zote hufurahia aina tofauti za muziki, kutia ndani muziki wenye kujenga kiroho unaopatikana katika kitabu cha nyimbo kinachoitwa Mwimbieni Yehova.b Hata hivyo, huenda muziki huo ukawa na mtindo tofauti na ule ambao watu wamezoea katika tamaduni nyingi.
Iwe wewe ni mzazi au kijana, unapotaka kununua albamu ya muziki au kupakua muziki kutoka kwenye Intaneti, jiulize maswali yafuatayo: ‘Ni nani aliyenipa uwezo wa kufurahia muziki? Je, si Muumba wangu, Yehova Mungu? Ninaweza kumwonyesha jinsi gani kwamba ninathamini zawadi zake? Je, si kwa kuthamini sana viwango vyake kuhusu mema na mabaya au kutofautisha kati ya jambo lenye hekima na lisilo na hekima?’ Kufikiria maswali kama hayo kutakusaidia kufanya maamuzi yenye hekima unapochagua muziki, na hivyo kukuletea shangwe moyoni, na kuufanya moyo wa Muumba wako ushangilie.—Methali 27:11.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina yamebadilishwa.
b Unaweza kupakua kutoka kwa Tovuti ya www.pr418.com.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
Miziki ya aina fulani inajulikana kwa upotovu wa maadili
[Blabu katika ukurasa wa 8]
Kuna aina nyingi ya muziki ambao unaweza kufurahia
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Sababu Iliyonichochea Kufanya Mabadiliko
“Sikumbuki mengi kuhusu miaka yangu ya ujana kwa kuwa nilikuwa nikitumia sana kileo, dawa za kulevya, na nilikuwa mjeuri,” anasema Ashley, mwenye umri wa miaka 24, “na muziki wa rapu na heavy metal ndio ulionichochea kufanya mambo hayo. Muziki uliojaa matusi, chuki, na pia midundo yake mizito ilinifanya nijihisi nikiwa shujaa. Muziki huo ulinifanya nishirikiane na marafiki waliokuwa wakitumia dawa za kulevya. Wasanii wa muziki wa rapu na heavy-metal ndio tuliowavulia kofia na kuwaona kuwa vielelezo vyetu.
“Hata hivyo, muda mfupi baadaye, maisha yangu yaliharibika zaidi. Nilipokuwa na umri wa miaka 17, nilikuwa karibu kufa kwa kutumia dawa za kulevya kupita kiasi. Niliporudiwa na fahamu, nilimwomba Mungu anisaidie. Nilikumbuka kwamba wakati fulani kijana mmoja aliniambia kuwa jina la Mungu ni Yehova, na hivyo nikatambua kuwa Mashahidi wa Yehova huwafundisha watu kumhusu. Kwa hiyo, nilitafuta namba ya simu ya Mashahidi wa Yehova kwenye kitabu cha simu, nikawapigia, na nikaanza kujifunza Biblia pamoja nao.
“Niliacha mazoea mabaya na nikatupa muziki wangu. Lakini, nilipotupa CD hizo kwenye pipa, nilisimama hapo nikizitazama kwa muda. Nilitambua kuwa haikuwa rahisi kufanya uamuzi huo. Hivyo, nilijikumbusha kwamba muziki huo, pamoja na mwenendo wangu, ulikuwa ukiniharibia maisha. Basi niligeuka na kwenda.
“Ingawa miaka kadhaa imepita, bado mimi huvutiwa na muziki wa rapu na heavy metal. Hivyo, mimi huuepuka kana kwamba ninaepuka dawa za kulevya. Leo, mimi hufurahia kusikiliza muziki wa aina nyingine, ikiwa ni pamoja na nyimbo taratibu, muziki taratibu wa roki, pamoja na baadhi ya muziki wa kale. Lakini jambo muhimu ni kwamba sasa ninaweza kuchagua muziki unaofaa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Mapendekezo ya Kuwasaidia Wazazi
Je, una wasiwasi kuhusu muziki ambao kijana wako anasikiliza? Unaweza kumsaidia jinsi gani bila kuanzisha ubishi? Hebu chunguza mapendekezo yafuatayo:
Pata habari Kabla ya kuzungumza, ni vizuri kupata habari kamili. Kwanza sikiliza muziki, elewa maneno yake, na uchunguze jalada la rekodi hiyo. Jiulize hivi, ‘Nina sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi, au ni kwamba ninafuatilia mambo madogo-madogo tu?’ Biblia inasema hivi: “Watu wenye akili wanafikiri kabla ya kusema; hivyo yale wanayosema yanakuwa yenye kushawishi zaidi.”—Methali 16:23, Today’s English Version.
Uwe na utambuzi Muziki unaweza kukusaidia kujua yale ambayo mtoto wako anafanya, anayofikiria, na jinsi anavyohisi. Mwulize kwa upole kuhusu hisia zake. Mwulize: “Kwa nini muziki huu unakuvutia? Je, unaonyesha kwa njia fulani jinsi unavyohisi?” Kisha sikiliza kwa makini anapojibu. Methali 20:5 inasema: “Fikira za mtu zimefichika kama kilindi cha maji; lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo.”—Biblia Habari Njema.
Uwe mwenye kujenga Lengo lako si kumfanya kijana atupe CD fulani tu. Bali ungependa kuzoeza ‘nguvu zake za ufahamu . . . kutofautisha yaliyo sawa na yaliyo makosa pia’ ili aweze kujifanyia maamuzi ya hekima. (Waebrania 5:14) Kwa hiyo, mfundishe mtoto wako sasa ili aweze kujitegemea hata katika maisha yake ya baadaye: Mfundishe jinsi ya kufanya utafiti na kufikiri akitumia kanuni za Biblia. Kwa njia hiyo, utamsaidia akuze nguvu zake za ufahamu na hekima ya kimungu, mambo ambayo ni yenye thamani sana kuliko dhahabu yote ulimwenguni!—Methali 2:10-14; 3:13, 14.
Uwe imara, mwenye huruma, na fadhili “Jivikeni upendo mwororo wenye huruma, fadhili, unyenyekevu wa akili, upole, na ustahimilivu.” (Wakolosai 3:12) Unapozungumza na kijana wako, usiwe mbishi wala usishikilie sana maoni yako. Kumbuka kwamba wakati mmoja hata wewe ulikuwa kijana.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Dumisha viwango vya juu unapochagua muziki
-