-
Zambia2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Nembo za Kitaifa
Katika enzi ya ukoloni, watoto wa Mashahidi wa Yehova waliadhibiwa walipokataa kusalimu bendera ya Uingereza kupatana na imani yao. Waliadhibiwa pia kwa kukataa kuimba wimbo wa taifa. Mashahidi walipowalalamikia wenye mamlaka, idara ya elimu ilibadili maoni yake na kuandika: “Maoni ya [kikundi chenu] kuhusu kusalimu bendera yanajulikana sana na kuheshimiwa, na mtoto yeyote asiadhibiwe kwa njia yoyote kwa kukataa kusalimu bendera.” Katiba mpya ya jamhuri iliwafanya watu watarajie kwamba haki za msingi, kutia ndani haki ya mtu ya kufuata dhamiri yake, maoni yake, na dini yake, zingeimarishwa. Lakini bendera mpya na wimbo mpya wa taifa ziliamsha hisia za uzalendo. Kusalimu bendera na kuimba wimbo wa taifa kulianzishwa tena na kukaziwa sana shuleni. Ingawa vijana fulani Mashahidi hawakuhusishwa, vijana wengi walipigwa na hata kufukuzwa shuleni.
Sheria mpya ya elimu iliyopitishwa katika 1966 iliwapa watu matumaini. Kifungu fulani cha sheria hiyo kiliruhusu mzazi au mlezi aombe mtoto asihusishwe katika shughuli au sherehe za kidini. Hivyo, watoto wengi waliokuwa wamefukuzwa shuleni wakarudishwa. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, vifungu fulani viliongezwa kwa siri katika sheria hiyo. Vifungu hivyo vilionyesha kwamba bendera na wimbo wa taifa ni nembo za serikali za kuwahamasisha watu. Licha ya akina ndugu kuzungumza na wakuu wa serikali, kufikia mwisho wa 1966, watoto zaidi ya 3,000 walikuwa wamefukuzwa kwa sababu ya msimamo wao.
Feliya Hakubaliwi Katika Shule Yoyote
Wakati wa kutatua tatizo hilo kisheria uliwadia. Kisa fulani kilichaguliwa. Feliya Kachasu alikuwa akisoma kwenye Shule ya Buyantanshi katika eneo la shaba. Alikuwa amefukuzwa shuleni licha ya kwamba alikuwa mwanafunzi mzuri. Frank Lewis anakumbuka jinsi kesi hiyo ilivyowasilishwa mahakamani: “Bw. Richmond Smith aliwasilisha kesi yetu, ambayo haikuwa rahisi kwani tulikuwa tukiishtaki serikali. Alimsikiliza Feliya akieleza kwa nini hakuisalimu bendera na hivyo akaamua kumtetea.”
Dailes Musonda, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi huko Lusaka, anasema: “Kesi ya Feliya ilipowasilishwa mahakamani, tulitarajia sana kupata ushindi. Ndugu kutoka Mufulira walikuja kusikiliza kesi hiyo. Mimi na dada yangu tulialikwa. Namkumbuka Feliya alipokuwa mahakamani akiwa amevalia kofia nyeupe na nguo yenye rangi iliyofifia. Kesi hiyo ilisikizwa kwa siku tatu. Bado wamishonari kadhaa walikuwamo nchini; Ndugu Phillips na Ndugu Fergusson walikuja kusikiliza kesi hiyo. Tulifikiri kuwapo kwao kungesaidia.”
Hakimu mkuu alikata kauli hii: “Hakuna jambo lolote linaloonyesha kwamba kwa matendo yao Mashahidi wa Yehova wanadharau wimbo wa taifa au bendera.” Hata hivyo, aliamua kuwa hizo ni taratibu za kitaifa na kwamba licha ya Feliya kushikilia imani yake kwa unyoofu, hawezi kutumia sheria za elimu kuomba asihusishwe katika taratibu hizo. Aliamini kwamba taratibu hizo zilihitajiwa ili kuwe na usalama nchini. Lakini hakuonyesha wazi jinsi kumlazimisha mtoto ndogo kufuata takwa hilo kunavyonufaisha watu. Feliya hangekubaliwa katika shule yoyote kwa muda wote ambao angeendelea kushikilia imani yake ya Kikristo!
Dailes anasema: “Tulivunjika moyo sana. Hata hivyo, tulimwachia Yehova mambo.” Matatizo yaliongezeka, na Dailes na dada yake wakaacha shule katika 1967. Kufikia mwisho wa 1968, karibu watoto 6,000 wa Mashahidi wa Yehova walikuwa wamefukuzwa shuleni.
-
-
Zambia2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 236, 237]
Mwenendo Wangu Uliwavutia Walimu Wengi
Jackson Kapobe
Alizaliwa: 1957
Alibatizwa: 1971
Maelezo mafupi kumhusu: Yeye ni mzee wa kutaniko.
Watoto walifukuzwa shuleni kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1964. Ofisi ya tawi iliwasaidia wazazi kuelewa umuhimu wa kuwatayarisha watoto. Nakumbuka kwamba baada ya shule Baba alizungumzia andiko la Kutoka 20:4, 5 pamoja nami.
Tulipokusanyika ili kuimba wimbo wa taifa shuleni, nilisimama nyuma ya wanafunzi wengine ili nisionekane. Wale ambao hawakuimba wimbo wa taifa waliitwa mbele. Mwalimu mkuu aliponiuliza kwa nini sikuimba, nilimjibu kwa kutumia Biblia. Huyo mwalimu mkuu akasema kwa mshangao: “Unasoma, lakini unakataa kuimba!” Alimaanisha kwamba ninapaswa kuunga mkono serikali ambayo imeandaa shule inayonifundisha kusoma.
Hatimaye, mnamo Februari 1967, nilifukuzwa shuleni. Nilivunjika moyo kwa sababu nilipenda masomo na nilikuwa mwanafunzi mwenye bidii. Ijapokuwa baba yangu alishinikizwa na wafanyakazi wenzake na watu wa ukoo wasiokuwa Mashahidi, alinihakikishia kwamba uamuzi wangu ulikuwa mzuri. Mama yangu alishinikizwa pia. Nilipoandamana naye kufanya kazi shambani, wanawake wengine walitudhihaki kwa kuuliza: “Kwa nini mtoto huyu hajaenda shuleni?”
Lakini sikukosa elimu. Madarasa ya kusoma na kuandika yalizingatiwa zaidi kutanikoni kuanzia mwaka wa 1972. Hatimaye hali ilibadilika shuleni. Nyumba yetu ilikuwa karibu na shule. Mwalimu mkuu alikuja kwetu mara kwa mara kuomba maji ya kunywa au fagio za kufagia madarasa. Hata siku moja aliomba mkopo! Bila shaka matendo ya fadhili ya familia yetu yalimgusa moyo kwa sababu siku moja alimuuliza baba yangu: “Je, mwanao anataka kuendelea na masomo?” Baba alimkumbusha kwamba bado mimi ni Shahidi wa Yehova. Mwalimu huyo mkuu akasema: “Hakuna matata.” Kisha akaniuliza: “Unataka kuanza darasa gani?” Nilichagua darasa la sita, na nikarudi kwenye shule ileile, na mwalimu mkuu alikuwa yuleyule, na wanadarasa wenzangu walikuwa walewale. Jambo moja tu ndilo lililokuwa tofauti, yaani, niliwashinda wengi wa wanadarasa wenzangu katika ustadi wa kusoma kwa sababu nilikuwa nimehudhuria madarasa ya kusoma na kuandika kwenye Jumba la Ufalme.
Bidii yangu na mwenendo wangu uliwavutia walimu wengi, kwa hiyo hali haikuwa mbaya sana shuleni. Nilifanya mitihani fulani iliyonistahilisha kupata kazi nzuri katika migodi. Baadaye kazi hiyo iliniwezesha kuruzuku familia yangu. Ninafurahi kwamba sikukana kamwe imani yangu kwa kuimba.
-