Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Matukio Yenye Kuongezeka ya Habari Mbaya
    Mnara wa Mlinzi—1996 | Aprili 15
    • Matukio Yenye Kuongezeka ya Habari Mbaya

      JE, UMEPATA kugundua kwamba vichwa vikuu vinavyotangaza habari mbaya huamsha upendezi mwingi zaidi wa wasomaji kuliko vile vinavyotoa habari njema? Iwe ni kichwa kikuu cha gazeti la habari cha msiba wa asili au porojo yenye kupendeza sana iliyoonyeshwa kwa maandishi makubwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti lenye kuvutia, yaonekana kwamba habari mbaya huuza vichapo vingi zaidi kuliko habari njema.

      Leo hakuna uhaba wa habari mbaya. Lakini nyakati fulani mtu hujiuliza ikiwa maripota na waandishi wanazoezwa kutafuta na kutokeza habari mbaya—wakiacha kando habari zozote njema.

      Nyingi Katika Historia Yote

      Kwa kweli, habari mbaya zimekuwa nyingi katika karne zote, zikishinda habari zozote njema. Katika rekodi za kihistoria, mizani zimelala sana upande wa kuteseka kwa wanadamu, mafadhaiko, na kukata tamaa, ambako kumekuwa sehemu ya maisha ya wanadamu.

      Ebu tufikirie vielelezo vichache tu. Kitabu Chronicle of the World, kilichotungwa na Jacques Legrand, hutoa masimulizi kadhaa, kila simulizi likiwa limeandikwa kwa tarehe hususa ambayo tukio lilitendeka lakini kana kwamba lilikuwa likielezwa na mwandishi wa habari wa kisasa akiripoti tukio hilo. Kutokana na ripoti hizi zilizofanyiwa utafiti mzuri, twaona kwa njia yenye manufaa kuenea kwa habari mbaya ambazo mwanadamu amesikia katika kuwapo kwake kote kulikojaa taabu hapa kwenye sayari Dunia.

      Kwanza, fikiria ripoti hii ya mapema kutoka Ugiriki katika 429 K.W.K. Inaripoti juu ya vita iliyokuwa ikipiganwa wakati huo kati ya Athene na Sparta: “Jiji lenye kujitawala la Potidaea limelazimika kusalimu amri kwa Waathene wenye kulizingira baada ya kukumbwa na njaa hivi kwamba watu walo wamekuwa wakila miili ya wafu wao.” Habari mbaya kwelikweli!

      Tukisonga mbele kwenye karne ya kwanza kabla ya Wakati wa Kawaida wetu, twapata ripoti iliyofafanuliwa wazi ya kifo cha Kaisari Yuliasi, yenye tarehe Roma, Machi 15, 44 W.K. “Kaisari Yuliasi ameuawa kihila. Yeye aliuawa kwa kudungwa kisu na kikundi cha wahaini, wengine wao wakiwa marafiki wake wa karibu zaidi, alipokuwa akiketi Bungeni leo, tarehe 15, Machi.”

      Katika karne zilizofuata, habari mbaya ziliendelea kuongezeka. Kielelezo kimoja chenye kushtua ni habari hizi kutoka Mexico katika 1487: “Katika wonyesho wenye kutazamisha zaidi uliopata kuonwa katika jiji kuu la Aztec, Tenochtitlan, mioyo ya watu 20,000 ilitolewa dhabihu kwa Huitzilopochtli, mungu wa vita.”

      Ukatili wa mwanadamu haujatoa tu habari mbaya bali uzembe wake umeongezwa katika orodha ndefu ya matukio yaletayo habari mbaya. Moto mkubwa wa London yaonekana ulikuwa msiba mmoja kama huo. Ripoti kutoka London, Uingereza, yenye tarehe Septemba 5, 1666, yasomeka hivi: “Hatimaye, baada ya siku nne mchana na usiku, moto wa London umesimamishwa na Dyuki wa York, ambaye alileta vikundi vya meli za kivita vyenye baruti ili kulipua majengo yaliyokuwa njiani mwa miale ya moto. Hektare zipatazo 160 zimeharibiwa kabisa pamoja na makanisa 87 na zaidi ya nyumba 13,000. Kimuujiza, ni watu tisa tu waliokufa.”

      Katika vielelezo hivi vya habari mbaya lazima tuongeze maradhi yenye kuenea sana ambayo yameenea bila kudhibitiwa kotekote katika kontinenti nyingi—kwa kielelezo, maradhi yenye kuenea ya kipindupindu ya mapema katika miaka ya 1830. Kichwa kilichochapishwa kilichoripoti hilo chasomeka: “Madhila ya kipindupindu yahangaisha Ulaya.” Ripoti yenye uhalisi ifuatayo yaonyesha habari mbaya katika hali mbaya zaidi yenye kutisha: “Kipindupindu, ambacho hakikujulikana katika Ulaya hadi 1817, kinaenea kuelekea magharibi kutoka Asia. Tayari idadi za watu katika majiji ya Urusi kama vile Moscow na St. Petersburg zimepunguzwa kwa kifo—wengi wa majeruhi wakiwa maskini wa majijini.”

      Ongezeko Katika Miaka ya Majuzi

      Kwa hiyo ingawa ni kweli kwamba habari mbaya zimekuwa uhalisi wa maisha katika rekodi yote ya historia, miongo ya majuzi ya karne ya 20 hutoa uthibitisho kwamba habari mbaya zinaongezeka, kwa hakika zinaongezeka kwa haraka.

      Hakuna shaka kwamba habari za vita zimekuwa aina mbaya kupita zote ya habari mbaya ambazo zimesikiwa katika karne yetu ya sasa. Vita viwili vikuu zaidi katika historia—vikiitwa kwa kufaa Vita ya Ulimwengu 1 na Vita ya Ulimwengu 2—vilikuwa na ripoti za habari mbaya kwa kiwango chenye kuogofya. Lakini hilo limekuwa kiasi kidogo tu cha habari mbaya ambazo zimetolewa na karne hii isiyo na furaha.

      Fikiria vichwa vikuu vichache tu vilivyochaguliwa hapa na pale:

      Septemba 1, 1923: Tetemeko laharibu Tokyo Vibaya—300,000 wafa; Septemba 20, 1931: Tatizo—Uingereza yapunguza thamani ya pauni; Juni 25, 1950: Korea Kaskazini yaingilia kivita Korea Kusini; Oktoba 26, 1956: Wahungaria waasi dhidi ya utawala wa Sovieti; Novemba 22, 1963: John Kennedy auawa kwa kupigwa risasi Dallas; Agosti 21, 1968: Vifaru vya Urusi vyawasili kuvunja-vunja waasi wa Prague; Septemba 12, 1970: Ndege zilizotekwa nyara zalipuliwa jangwani; Desemba 25, 1974: Kimbunga Tracy chatandaza jiji la Darwin—66 wafa; Aprili 17, 1975: Kambodia yashindwa na majeshi ya Kikomunisti; Novemba 18, 1978: Ujiuaji wa kimakusudi wa watu wengi katika Guyana; Oktoba 31, 1984: Bi. Gandhi auawa kwa kupigwa risasi; Januari 28, 1986: Chombo cha angani chalipuka kinapoanza kuondoka; Aprili 26, 1986: Kitendanishio cha Sovieti chashika moto; Oktoba 19, 1987: Soko la hisa laporomoka; Machi 25, 1989: Alaska yaathiriwa vibaya na mmwagiko wa mafuta ghafi; Juni 4, 1989: Majeshi yachinja waandamanaji katika Uwanja wa Tiananmen.

      Ndiyo, historia yaonyesha kwamba sikuzote habari mbaya zimekuwa nyingi, huku habari njema zikiwa chache kwa kulinganishwa. Kadiri ambavyo habari mbaya zimezidi katika miongo ya majuzi, ndivyo habari njema zimedidimia kila mwaka ukipita.

      Kwa nini iwe hivyo? Je, sikuzote itakuwa hivyo?

      Makala ifuatayo itashughulikia maswali haya mawili.

  • Kuna Habari Njema Mbele!
    Mnara wa Mlinzi—1996 | Aprili 15
    • Kuna Habari Njema Mbele!

      SOTE huhuzunishwa wakati wowote tupatapo habari mbaya zenye kutuathiri kibinafsi. Kwa upande ule mwingine, sisi hufurahi habari njema zijapo—habari njema za shangwe kwa ajili yetu na wapendwa wetu. Lakini habari mbaya ziathiripo wengine wala si sisi, mara nyingi watu huwa wadadisi; wengine hata hufurahia kujua kuhusu matokeo mabaya ya wengine. Hili huenda likaeleza kwa sehemu kwa nini habari mbaya zauzwa sana!

      Katika sehemu ya mapema ya Vita ya Ulimwengu 2, kulikuwa na kielelezo cha wazi cha upendezi wenye kuogofya katika msiba wa watu wengine. Meli ya kivita ya tani 10,000, Graf Spee, ilikuwa ndiyo fahari ya meli za Ujerumani katika 1939. Kwa majuma kadhaa meli hii ya kivita ilikuwa imesababisha uharibifu mwingi miongoni mwa meli za kibiashara za Mataifa ya Muungano katika bahari kuu za Atlantiki Kusini na Hindi. Hatimaye, manowari tatu za kuvinjari zikafuatia na kushambulia Graf Spee, zikisababisha kupotea kwa uhai na kulazimisha meli hiyo kujikokoteza kuingia bandari ya Uruguai ya Montevideo kwa ajili ya marekebisho. Serikali ya Uruguai iliamuru meli hiyo ya kivita irudi baharini mara moja, sivyo ingefungiwa. Kwa hiyo pigano kali ambalo Uingereza ingeelekea kushinda lilikuwa karibu kutokea.

      Kiliposikia hilo, kikundi cha wafanyabiashara katika Marekani kilikodi ndege, kwa gharama ya dola 2,500 hivi kila mmoja, ili kwenda kwa ndege hadi Uruguai kushuhudia pigano hilo lenye kujaa damu. Kwa fadhaiko lao, pigano hilo halikutukia. Adolf Hitler alitoa amri Graf Spee itobolewe ili izame. Maelfu ya watazamaji waliokuja kwa wingi bandarini ili kushuhudia tamasha hiyo ya pigano kali la baharini, badala ya hilo waliona na kusikia, mlipuko mkubwa sana uliozamisha Graf Spee, iliyotobolewa na wafanyakazi wayo yenyewe. Nahodha alijiua kimakusudi kwa kujipiga risasi kichwani.

      Licha ya dalili zenye kuogofya katika watu fulani, wengi watakubali kwamba wanapendelea habari njema zaidi ya habari mbaya. Je, wewe huhisi hivyo? Kwa nini basi, historia hurekodi habari nyingi zilizo mbaya na chache sana zilizo nzuri? Je, hali hiyo itapata kubadilishwa?

      Visababishi vya Habari Mbaya

      Biblia hutueleza juu ya wakati ambapo ni habari njema tu zilizokuwapo. Habari mbaya hazikujulikana wala kusikiwa. Wakati Yehova Mungu alipomaliza kazi zake za uumbaji, sayari Dunia ilikuwa tayari kwa mwanadamu na mnyama kuifurahia. Simulizi la Mwanzo latueleza hivi: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.”—Mwanzo 1:31.

      Baada ya kuumbwa kwa mwanadamu, kutokuwako kwa habari mbaya hakukudumu kwa muda mrefu. Kabla ya Adamu na Hawa kuzaa mtoto yeyote, habari mbaya ya uasi dhidi ya Mungu na mpango wake wa mema wenye utaratibu wa ulimwenguni pote iliripotiwa. Mwana wa kiroho mwenye cheo cha juu akasaliti cheo chake alichokabidhiwa na kufaulu kufanya mume na mke wa kwanza wa kibinadamu kujiunga naye katika mwendo wake wenye uasi na usaliti.—Mwanzo 3:1-6.

      Wingi wa habari mbaya zinazoshuhudiwa na wanadamu ulianza wakati huo. Si ajabu kwamba hila, madanganyo, uwongo, ukosefu wa kweli, na kweli-nusu zimeonekana waziwazi sana katika habari mbaya ambazo zimejaa ulimwenguni tangu wakati huo. Yesu Kristo alimwekea lawama waziwazi Shetani Ibilisi kuwa mwanzilishi wa habari mbaya, akiwaambia viongozi wa kidini wa siku Yake hivi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”—Yohana 8:44.

      Kadiri idadi ya wanadamu ilipoongezeka, habari mbaya ziliongezeka pamoja nayo. Bila shaka, hili halimaanishi kwamba hakukuwa na nyakati za shangwe na furaha, kwa kuwa kulikuwa na vitu vingi maishani vilivyosababisha shangwe. Hata hivyo, hali zenye kusikitisha za taabu na huzuni zimedhihirika kote katika kila kizazi cha wanadamu hadi sasa.

      Kuna sababu nyingine muhimu inayotokeza hali hii yenye kuhuzunisha. Hiyo ni kuegemea kwetu kulikorithiwa kuelekea kutenda makosa na msiba. Yehova mwenyewe atambulisha kisababishi hiki kisichoepukika cha habari mbaya kwa kusema: “Mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake.”—Mwanzo 8:21.

      Kwa Nini Kuna Ongezeko la Habari Mbaya?

      Hata hivyo, kuna sababu ambayo imefanya habari mbaya ziongezeke katika karne hii ya 20. Sababu hii yataarifiwa waziwazi katika Biblia, ambayo ilitabiri kwamba wanadamu katika karne ya 20 wangeingia katika kipindi cha kipekee cha wakati kinachoitwa “siku za mwisho” au “wakati wa mwisho.” (2 Timotheo 3:1; Danieli 12:4) Unabii wa Biblia na kronolojia ya Kibiblia hutambulisha hiki “kipindi cha mwisho,” ambacho kilianza katika 1914. Kwa uthibitisho wa Kimaandiko wa jambo hilo, tafadhali ona sura ya 11 ya kitabu Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

      Siku za mwisho zilipaswa kuanza kwa tukio ambalo moja kwa moja lingesababisha habari mbaya duniani ziongezeke. Hilo lilikuwa nini? Lilikuwa kutupwa chini kwa Shetani Ibilisi na mashetani wake kutoka mbinguni. Unaweza kusoma ufafanuzi huu halisi wa ongezeko lisiloepukika la habari mbaya kwenye Ufunuo 12:9, 12: “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. . . . Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”

      Kwa hiyo katika wakati wowote ule ambao bado umebaki hadi siku za mwisho zifikie umalizio wazo, twaweza kutarajia habari mbaya ziendelee na hata kuongezeka zaidi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki