-
Norway2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Svanhild Neraal, alikuwa mmoja wa mapainia hao. Dada huyo alisafiri upande wa kaskazini hadi jimbo la Finnmark mwaka wa 1946. Svanhild alikuwa amefanya upainia huko mwaka wa 1941 akiwa na Solveig Løvås na walijionea miji ya Kirkenes na Vardø ikilipuliwa na mabomu. Svanhild hakuwasahau watu wenye kupendezwa ambao yeye na Solveig walihubiria huko, kwa hiyo akaamua kurudi Kirkenes, mji uliokuwa umeharibiwa na vita. Svanhild alipohamia eneo hilo bila kujua mahali atakapoishi, wenyeji walifikiri kwamba amerukwa na akili.
Hata hivyo, Svanhild alimtegemea Yehova, na wakati wa majira ya kwanza ya baridi kali, alilala jikoni kwenye sakafu katika nyumba ndogo ambamo watu wengine watano waliishi. Hali zilikuwa mbaya sana baada ya vita na alivumilia mambo mengi magumu. Mara nyingi, akiwa ananyeshewa, alisubiri mashua ambazo zilichelewa au hata kutowasili kabisa.
Svanhild alifurahia mambo mengi alipowahubiria Wasami. Aliposhindwa kuwafikia katika maeneo yao ya mbali kwa basi, alitumia mashua au baiskeli. Wasami ni wakarimu na mara nyingi walimkaribisha ndani ya mahema yao yaliyotengenezwa na ngozi ya mbawala na kumsikiliza kwa makini alipowahubiria kwa msaada wa mkalimani. Wakati wa chakula, walimkaribisha kwa mlo wa nyama ya mbawala. Baadaye, baadhi ya watu waliohubiriwa na Svanhild waliikubali kweli.
Kjell Husby, aliyekuwa anatumika Betheli wakati huo, alisema kwamba nyakati zote ofisi ya tawi ilijua mahali ambapo Svanhild alikuwa hasa kwa sababu ya anwani za maandikisho aliyotuma. Kwa miaka mitatu aliyoishi Finnmark, alipata maandikisho 2,000 ya Mnara wa Mlinzi na kuwaachia watu vitabu 2,500!
-
-
Norway2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 130]
Svanhild Neraal, mwaka wa 1961
-