Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Hesabu
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 1
    • KWENYE MLIMA SINAI

      (Hesabu 1:1–10:10)

      Waisraeli wanahesabiwa kwa mara ya kwanza wanapokuwa bado wamepiga kambi chini ya Mlima Sinai. Jumla ya wanaume wenye umri wa miaka 20 na zaidi, bila kuhesabu Walawi, ni 603,550. Yaonekana Waisraeli walihesabiwa kwa sababu za kijeshi. Huenda watu wote waliokuwa kambini, kutia ndani wanawake, watoto, na Walawi, walikuwa zaidi ya milioni tatu.

      Baada ya watu kuhesabiwa, Waisraeli wanapokea maagizo kuhusu mpangilio wa kutembea, maelezo kuhusu kazi za Walawi na utumishi wa maskani, amri kuhusu kuwatenga watu waliokuwa na magonjwa, na sheria kuhusiana na visa vya wivu na nadhiri zilizowekwa na Wanadhiri. Sura ya 7 ina habari kuhusu dhabihu zilizotolewa na wakuu wa makabila wakati wa kuzinduliwa kwa madhabahu, nayo sura ya 9 inazungumzia sherehe ya Pasaka. Pia, kusanyiko linapewa maagizo kuhusu jinsi ya kupiga kambi na kuivunja.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Hesabu
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 1
    • WATANGA-TANGA NYIKANI

      (Hesabu 10:11–21:35)

      Mwishowe, wingu juu ya maskani linapoondoka, Waisraeli wanaanza safari ambayo itawafikisha kwenye nyika za nchi tambarare za Moabu baada ya miaka 38 na mwezi moja au miwili. Huenda ukaona inafaa kutazama njia ambayo walifuata katika safari yao kwenye ramani katika ukurasa wa 9 wa broshua “Ona Nchi Nzuri,” iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      Kwenye njia ya kwenda Kadeshi, katika Nyika ya Parani, Waisraeli wanalalamika mara tatu. Malalamiko yao ya yanakomeshwa wakati Yehova anapotokeza moto na kuwateketeza baadhi yao. Kisha Waisraeli wanalalamika wapewe nyama, naye Yehova anawapa kware. Malalamiko ya Miriamu na Haruni dhidi ya Musa yanafanya Miriamu apigwe kwa ukoma kwa muda.

      Wanapopiga kambi huko Kadeshi, Musa anatuma wanaume 12 kupeleleza Nchi ya Ahadi. Wanarudi baada ya siku 40. Kwa kuiamini ripoti mbaya ya wapelelezi 10 kati ya hao, watu wanataka kuwapiga kwa mawe Musa, Haruni, na wale wapelelezi waaminifu Yoshua na Kalebu. Yehova anakusudia kupiga watu kwa tauni, lakini Musa anamsihi Mungu kwa ajili ya watu, naye Mungu anasema kwamba watatanga-tanga nyikani kwa miaka 40 mpaka wale waliohesabiwa wawe wamekufa.

      Yehova anatoa masharti ya ziada. Kora na wengine wanaasi dhidi ya Musa na Haruni, lakini waasi hao wanaharibiwa kwa moto au wanamezwa na dunia. Siku inayofuata kusanyiko lote linanung’unika dhidi ya Musa na Haruni. Kwa sababu hiyo, watu 14,700 wanakufa kwa tauni kutoka kwa Yehova. Ili kuonyesha wazi chaguo lake kuhusu kuhani mkuu, Mungu anafanya fimbo ya Haruni ichanue maua. Kisha, Yehova anatoa sheria zaidi kuhusiana na wajibu wa Walawi na utakaso wa watu. Matumizi ya majivu ya ng’ombe mwekundu yanawakilisha utakaso kupitia dhabihu ya Yesu.—Waebrania 9:13, 14.

      Wana wa Israeli wanarudi Kadeshi ambako Miriamu anakufa. Kusanyiko linanung’unika tena dhidi ya Musa na Haruni. Kwa nini? Kwa sababu ya ukosefu wa maji. Kwa kuwa Musa na Haruni wanakosa kulitakasa jina la Yehova wanapowapa watu maji kimuujiza, wanapoteza pendeleo la kuingia katika Nchi ya Ahadi. Waisraeli wanaondoka Kadeshi, naye Haruni anakufa kwenye Mlima Hori. Wanaposafiri kuzunguka Edomu, Waisraeli wanachoka nao wanasema vibaya dhidi ya Mungu na Musa. Yehova anatuma nyoka wenye sumu ili kuwaadhibu. Kwa mara nyingine tena, Musa anamsihi Mungu kwa ajili ya watu, naye Mungu anamwagiza afanye nyoka wa shaba na kumweka kwenye nguzo ili wale wanaoumwa wapate kupona kwa kumtazama. Nyoka huyo anafananisha kutundikwa mtini kwa Yesu Kristo kwa faida yetu ya milele. (Yohana 3:14, 15) Waisraeli wanawashinda Sihoni na Ogu, Wafalme wa Waamori, nao wanamiliki nchi yao.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Hesabu
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 1
    • KWENYE NCHI TAMBARARE ZA MOABU

      (Hesabu 22:1–36:13)

      Wana wa Israeli wanapopiga kambi kwenye nyika ya nchi tambarare za Moabu, Wamoabu wanahofu na kuchukizwa kwa sababu yao. Kwa hiyo, Balaki Mfalme wa Moabu, anamtumia Balaamu ili kuwalaani Waisraeli. Lakini Yehova anamlazimisha Balaamu kuwabariki. Halafu, wanawake wa Moabu na Midiani wanatumiwa ili kuwashawishi wanaume Waisraeli wafanye ngono na kuabudu sanamu. Kwa sababu hiyo, Yehova anaharibu wakosaji 24,000. Mwishowe, tauni inakomeshwa Finehasi anapoonyesha kwamba havumilii ushindani wowote kumwelekea Yehova.

      Kuhesabiwa kwa watu mara ya pili kunafunua kwamba wanaume wote waliohesabiwa mara ya kwanza walikuwa wamekufa, isipokuwa Yoshua na Kalebu. Yoshua anaagizwa kuchukua nafasi ya Musa. Waisraeli wanapokea maagizo kuhusu matoleo mbalimbali na maagizo juu ya kuweka nadhiri. Wanalipiza pia kisasi juu ya Wamidiani. Kabila la Rubeni, Gadi, na nusu ya kabila la Manase linamiliki eneo lililo mashariki ya Mto Yordani. Waisraeli wanapewa maagizo kuhusu kuvuka Yordani na kuimiliki nchi hiyo. Maelezo mengi kuhusu mipaka ya nchi yanatolewa. Urithi unapaswa kugawanywa kwa kura. Walawi wanapewa majiji 48, na 6 kati ya hayo yatatumiwa kuwa majiji ya makimbilio.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Hesabu
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 1
    • Neno la Mungu Lina Nguvu

      Tunapaswa kuonyesha heshima kwa Yehova na kwa wale waliowekwa rasmi katika vyeo vya madaraka kati ya watu wake. Kitabu cha Hesabu kinakazia ukweli huo. Hilo ni somo muhimu kama nini katika kudumisha amani na umoja kutanikoni leo!

      Matukio yanayoelezwa katika kitabu cha Hesabu yanaonyesha jinsi ilivyo rahisi kwa wale wanaopuuza hali yao ya kiroho kuanguka katika makosa, kama vile kunung’unika, uasherati, na ibada ya sanamu. Baadhi ya vielelezo na mambo tunayojifunza kutoka katika kitabu hiki cha Biblia yanaweza kutumiwa kama chanzo cha habari kwa ajili ya mahitaji ya kwenu katika sehemu ya Mkutano wa Utumishi kwenye makutaniko ya Mashahidi wa Yehova. Kwa kweli, “neno la Mungu liko hai nalo lina nguvu” maishani mwetu.—Waebrania 4:12.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki