Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Kunenepa Kupita Kiasi ni Tatizo?
    Amkeni!—2004 | Novemba 8
    • Je, Kunenepa Kupita Kiasi ni Tatizo?

      “Idadi ya vijana ambao wamenenepa kupita kiasi inaongezeka.”—S. K. Wangnoo, mtaalamu katika Hospitali ya Indraprastha Apollo, huko Delhi, India.

      KAMA maelezo yaliyo juu yanavyoonyesha, maisha ya familia nyingi za kawaida nchini India yamebadilika na kuwafanya vijana waliobalehe wanenepe kupita kiasi. Tatizo hilo linazidi kuenea katika nchi nyingi kwa sababu watu wanaacha kufanya mazoezi na kuzoea kula vyakula ambavyo haviboreshi afya. Mtaalamu mmoja wa tiba ya vijana waliobalehe alisema hivi: “Kizazi kitakachofuata [nchini Uingereza] kitakuwa . . . na watu wanene zaidi katika historia ya wanadamu.” Gazeti Guardian Weekly liliripoti hivi: “Hapo zamani, ni watu wazima tu walionenepa kupita kiasi. Kwa sababu ya mazoea mabaya ya kula na kutofanya mazoezi, sasa vijana wa Uingereza wanapata matatizo ambayo yalianzia Marekani. Wakinenepa kupita kiasi kwa muda mrefu wanaweza kupata magonjwa kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo, na kansa.”

      Waandishi wa kitabu Food Fight wanasema hivi: “Sasa, tatizo kubwa zaidi la lishe ulimwenguni si kukosa chakula kinachofaa, bali ni kula na kunywa kupita kiasi.” Don Peck, aliandika hivi katika jarida The Atlantic Monthly: “Sasa, Wamarekani milioni tisa hivi wanakabili hatari ya kupata magonjwa kwa sababu ya kunenepa kupita kiasi, na hiyo inamaanisha kwamba wanazidi uzito wa kawaida kwa kilo 45 au zaidi.” Kila mwaka, watu wapatao 300,000 nchini humo hufa mapema kutokana na magonjwa yanayohusiana na kunenepa kupita kiasi. Hicho ndicho “kisababishi cha pili kikuu cha vifo baada ya uvutaji wa sigara.” Peck anasema hivi: “Huenda karibuni kunenepa kupita kiasi kutakuwa tatizo kubwa zaidi la afya ulimwenguni kuliko njaa na magonjwa ya kuambukiza.” Basi, hatuna budi kuzingatia tatizo la kunenepa kupita kiasi. Katika kitabu Eat, Drink, and Be Healthy, Dakt. Walter C. Willett anaandika hivi: “Zaidi ya uvutaji wa sigara, uzito wako ndilo jambo kuu zaidi linaloonyesha jinsi afya yako itakavyokuwa wakati ujao.” Tunakazia maneno haya: afya ya wakati ujao.

      Kunenepa Kupita Kiasi

      Mtu huonwa kuwa amenenepa kupita kiasi wakati gani? Kliniki ya Mayo huko Rochester, Minnesota, Marekani, inasema hivi: “Kwa ufupi, kunenepa kupita kiasi ni kuwa mzito sana kwa sababu ya mafuta mengi mwilini.” Lakini utajuaje uzito unaomfaa kila mtu? Chati zinazoonyesha uzito unaowafaa watu wa kimo fulani zinaweza kutumiwa kukadiria iwapo mtu ni mnene tu au ni mnene kupita kiasi. (Ona chati kwenye ukurasa wa 5.) Hata hivyo, chati hizo hazionyeshi uzito unaowafaa watu wenye hali mbalimbali za mwili. Kliniki ya Mayo inasema hivi: “Afya ya mtu hujulikana vizuri inapopimwa kwa kutegemea kiasi cha mafuta yaliyo mwilini mwake wala si kwa kutegemea uzito wake.” Kwa mfano, mwanariadha anaweza kuwa mzito kwa sababu ya kuwa na misuli au mifupa mikubwa. Ni mambo gani yanayowafanya watu wanenepe kupita kiasi? Makala inayofuata itazungumzia swali hilo.

  • Kunenepa Kupita Kiasi Husababishwa na Nini?
    Amkeni!—2004 | Novemba 8
    • Kunenepa Kupita Kiasi Husababishwa na Nini?

      “Tunakabili tatizo kubwa ambalo linaweza kuathiri sana afya ya watoto wetu. Hatua isipochukuliwa sasa ili kuzuia tatizo hilo, watu watazidi kunenepa kupita kiasi.”—William J. Klish, profesa wa magonjwa ya watoto.

      WATU fulani wasio na tatizo la kunenepa huwachambua watu walionenepa kupita kiasi na kuwaona kuwa wavivu na goigoi. Lakini je, kweli tatizo hilo ni dogo hivyo? Je, kunenepa kupita kiasi ni tatizo la watu wavivu wasiopenda kufanya mazoezi? Au je, mara nyingi tatizo hilo husababishwa na mambo makubwa ambayo ni vigumu kuyazuia?

      Je, Husababishwa na Urithi, Mazingira, au Yote Mawili?

      Kitabu Food Fight kinasema hivi: “Kwa muda mrefu watu wamejadili ikiwa kunenepa kupita kiasi husababishwa na urithi au mazingira.” Ni nini maana ya urithi katika habari hii? Wengine husema kwamba kwa kawaida mwili wa mwanadamu huhifadhi kalori za ziada kwa ajili ya mahitaji ya wakati ujao. Kitabu hicho kinaendelea kusema: “Kwa makumi ya miaka, uchunguzi umefanywa ili kugundua jinsi urithi unavyosababisha kunenepa kupita kiasi. . . . Utafiti mwingi umefanywa kuhusu chembe za urithi za wanadamu na kunenepa kupita kiasi. Mbinu za hali ya juu zinatumiwa kutambua chembe za urithi zinazowafanya watu wawe na uwezekano wa kunenepa na kupata magonjwa kama vile kisukari. Kulingana na wanasayansi, yaelekea kwamba asilimia 25 hadi 40 ya uzito wa mwili hutegemea chembe za urithi.” Kitabu hicho kinasema hivi pia: “Ijapokuwa watu wanene kupita kiasi hulaumiwa kwa kujisababishia hali hiyo, idadi hizo zinaonyesha wazi kwamba chembe za urithi zinahusika sana, ingawaje, inasemekana kwamba mazingira huhusika kwa asilimia 60 au zaidi katika kuamua uzito wa watu.” Hilo linaonyesha kwamba mtindo wa maisha ya mtu ni kisababishi kikuu cha kunenepa kupita kiasi. Je, kila siku yeye hula vyakula vyenye kalori nyingi na kutumia kalori chache? Je, yeye hula vyakula visivyofaa? Je, yeye hutenga wakati kila siku ili kufanya mazoezi kwa kiasi?

      Kliniki ya Mayo inaeleza kisababishi cha kunenepa kupita kiasi kwa maneno haya rahisi: “Huenda chembe za urithi zikasababisha kunenepa kupita kiasi, lakini uzito wa mwili hutegemea hasa kile unachokula na mazoezi ya mwili. Mwishowe, kula vyakula vyenye kalori nyingi kupita kiasi, kutofanya mazoezi, au yote mawili husababisha kunenepa kupita kiasi.” (Italiki ni zetu.) Kliniki hiyo inaendelea kusema hivi: “Haimaanishi kwamba ni lazima uwe mnene kwa sababu ya chembe za urithi. . . . Ingawa chembe zako za urithi zinahusika, uzito wa mwili hutegemea kile unachochagua kula na mazoezi unayofanya.”

      Mashirika ya kuwasaidia watu kupunguza uzito hupata mamilioni ya dola kwani watu wengi hutamani sana kurudia umbo lao la zamani. Hata hivyo, wataalamu husema nini kuhusu kupunguza uzito? Kitabu Food Fight kinasema: “Ni vigumu sana kushughulikia tatizo la kunenepa kupita kiasi, na wengi wanaopunguza uzito huongeza uzito tena. Inakadiriwa kwamba ni asilimia 25 [robo moja] tu ya watu ambao hufaulu kupunguza uzito na kuudumisha, baada ya jitihada nyingi.”

      Hatari za Kunenepa Kupita Kiasi

      Kunenepa kupita kiasi kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya. Dakt. Scott Loren-Selco, mtaalamu wa mfumo wa neva katika Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Southern California, anaonya kwamba hata vijana walionenepa kupita kiasi wanakabili hatari ya kupata Aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. (Ona Amkeni! la Mei 8, 2003.) Anasema hivi: “Tunaona wengi wakiugua ugonjwa huo siku hizi, na inaogopesha sana. Mimi huwaambia [watu walionenepa kupita kiasi] kwamba ninaweza kuwapeleka kwenye chumba cha wagonjwa wa kisukari ili niwaonyeshe madhara wanayoweza kupata: hiyo inatia ndani vipofu, watu waliokatwa miguu, na watu wengi sana ambao wamelemazwa kabisa na aina ya 2 [ya kisukari]—kwa sababu ya kunenepa kupita kiasi.” Ni nini husababisha hali hiyo? Loren-Selco anasema hivi: “Kwa sababu wana pesa, wao hununua mikate mikubwa iliyotiwa nyama katikati na chipsi. Hakuna anayewaonya kwamba kula vyakula vingi vya aina hiyo kutawafanya wanenepe kupita kiasi, iwe ni wenye biashara hizo za chakula, au madaktari ambao hawajafundishwa kuhusu lishe.”

      Dakt. Edward Taub, mwandishi maarufu kuhusu lishe, anasema: “Hivi karibuni, watu wameamini kwamba kunenepa sana ni jambo la kawaida na linalokubalika maishani. Wazo hilo la ajabu linaendelezwa na wenye biashara za chakula ambao hupata faida kwa kutunenepesha.”

      Wataalamu wanasema kwamba watu walio na mafuta mengi mapajani huenda wakawa na afya nzuri kuliko wale walio na mafuta mengi tumboni (hasa ikiwa kiuno chao kinazidi sentimeta 90 hadi 100). Kwa nini? Kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight kinasema kwamba “kuwa na mafuta tumboni huongeza uwezekano wa kupanda kwa shinikizo la damu, kupata ugonjwa wa moyo, kisukari, kiharusi, na aina fulani za kansa. Ikiwa una nyonga kubwa, mapaja manene, na matako makubwa, basi hukabili hatari kubwa sana ya afya.”

      Hivyo, mamilioni ya watu wazima na watoto ulimwenguni pote ambao wamenenepa kupita kiasi na wanakabili uwezekano wa kupata magonjwa hatari wanaweza kufanya nini? Je, kuna matibabu yanayofaa?

      [Sanduku/Chati katika ukurasa wa 5]

      BMI Ni Nini? Inaonyesha Nini?

      BMI (body mass index) ni kipimo cha kulinganisha kimo na uzito ili kutambua ikiwa mtu ni mnene au mnene kupita kiasi. Kulingana na Kliniki ya Mayo, BMI ya 18.5 hadi 24.9 inaonyesha kwamba mtu ana afya bora. Ikiwa BMI yako ni kati ya 25 na 29.9, basi wewe ni mnene. Ikiwa imepita 30, basi wewe ni mnene kupita kiasi. Unaweza kutumiaje chati ya BMI? Je, unahitaji mashauri ya daktari ili upate madokezo au ujue hali yako?

      Ili ujue BMI yako, gawa uzito wako katika kilo kwa kimo chako katika meta, kisha ugawe tena matokeo kwa kimo chako katika meta. Kwa mfano, ikiwa una kilo 90 na kimo cha meta 1.8, BMI yako ni 28 (90 ÷ 1.8 ÷ 1.8 = 28).

      [Chati]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      Mwenye Afya Mnene Mnene Kupita Kiasi

      BMI 18.5-24.9 25-29.9 30 au zaidi

      Kimo Uzito katika kilo

      1.47 m 53 au chini 54-64 65 au zaidi

      1.50 56 au chini 57-67 68 au zaidi

      1.52 57 au chini 58-69 70 au zaidi

      1.55 59 au chini 60-71 72 au zaidi

      1.57 61 au chini 62-73 74 au zaidi

      1.60 63 au chini 64-76 77 au zaidi

      1.63 66 au chini 67-79 80 au zaidi

      1.65 67 au chini 68-81 82 au zaidi

      1.68 70 au chini 71-84 85 au zaidi

      1.70 72 au chini 73-86 87 au zaidi

      1.73 74 au chini 75-89 90 au zaidi

      1.75 76 au chini 77-91 92 au zaidi

      1.78 79 au chini 80-94 95 au zaidi

      1.80 80 au chini 81-97 98 au zaidi

      1.83 83 au chini 84-100 101 au zaidi

      1.85 85 au chini 86-102 103 au zaidi

      1.88 89 au chini 90-106 107 au zaidi

      1.90 90 au chini 91-108 109 au zaidi

      [Hisani]

      Kwa mujibu wa Mayo Clinic on Healthy Weight

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Kalori ni nini?

      Kalori ni nini? Ni kipimo cha nishati ya joto. Hivyo, unapotokwa na jasho unatumia kalori, au nishati ya joto. “Kalori ni kiasi cha joto kinachohitajiwa kuongeza halijoto ya kilo moja ya maji kwa sentigredi moja.” (Balance Your Body, Balance Your Life) Kila mtu huhitaji viwango tofauti-tofauti vya kalori au nishati kila siku, ikitegemea kimo, uzito, umri, na shughuli anazofanya.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

      Unahitaji kufanya mazoezi ikiwa

      ◼ Unatumia wakati mwingi kila siku ukiwa umeketi, iwe ni kutazama televisheni, kufanya kazi ofisini, au kusafiri ndani ya gari

      ◼ Mara nyingi hutembei kwa zaidi ya meta 100

      ◼ Unafanya kazi ambayo haikuwezeshi kufanya mazoezi

      ◼ Hutumii dakika 20 hadi 30 kufanya mazoezi angalau mara moja kila juma

      [Hisani]

      Madokezo hayo ni ya Mayo Clinic on Healthy Weight

  • Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?
    Amkeni!—2004 | Novemba 8
    • Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?

      AMKENI! lilimhoji mtaalamu wa lishe anayeitwa Diane, na muuguzi anayeitwa Ellen. Wote wawili huwahudumia wagonjwa wanene na walionenepa kupita kiasi. Wote walisema kwamba mtu anapoacha kula vyakula vyenye wanga na kula protini nyingi (nyama) anaweza kupunguza uzito. Hata hivyo, wanasema kwamba hatimaye hilo linaweza kusababisha madhara.a Jambo hilo linathibitishwa na chati ya tiba inayoitwa Kudumisha Uzito Unaofaa. Inasema hivi: “Kuzoea kula kiasi kidogo cha wanga ni hatari, hasa bila mwongozo wa daktari.” Inaendelea kusema: “Lengo la mazoea hayo ni kupunguza uzito haraka kwa kusababisha ongezeko kubwa sana la ketoni (ambazo hutokezwa wakati mafuta yanaposagwa mwilini).” Ikiwa unafikiria kupunguza kiasi cha wanga unachokula, ingefaa kwanza umwombe daktari mashauri.

      Ikiwa unataka kupunguza uzito, usivunjike moyo. Dakt. Walter C. Willett anasema kwamba “inawezekana kupunguza uzito, na hilo halimaanishi kujinyima au kula chakula kilekile nyakati zote. Kwa kujitahidi sana na kutumia maarifa, watu wengi wanaweza kufanikiwa kupunguza na kudumisha uzito wao huku wakila vyakula wanavyovifurahia kwa usawaziko na kufanya mazoezi karibu kila siku. Jitihada hizo zinahitajiwa ili uishi muda mrefu ukiwa na afya nzuri.”b—Italiki ni zetu.

      Mazoezi Ni Muhimu Kadiri Gani?

      Dakt. Willett anasema hivi: “Zaidi ya kutovuta sigara, kufanya mazoezi ndiyo njia bora zaidi ya kuwa na afya au kudumisha afya bora, na hivyo kuepuka magonjwa hatari.” Mtu anapaswa kufanya mazoezi mara ngapi? Kuna faida gani kufanya mazoezi?

      Wataalamu fulani wanasema kwamba kufanya mazoezi kila siku, hata kama ni kwa dakika 30 tu, kunaweza kukunufaisha sana. Lakini imesemwa kwamba hata kufanya mazoezi mara tatu tu kwa juma kunaweza kumsaidia mtu aepuke matatizo makubwa wakati ujao. Tunapofanya mazoezi tunapunguza kalori. Mtu anayetaka kupunguza uzito anapaswa kujiuliza swali hili muhimu, Je, kila siku mimi hula chakula chenye kalori nyingi na kutumia kalori chache? Ukila chakula chenye kalori nyingi na kutumia kalori chache, bila shaka utaongeza uzito. Kwa hiyo, tembea au uendeshe baiskeli badala ya kusafiri kwa gari. Panda ngazi badala ya kutumia lifti. Fanya mazoezi! Tumia kalori!

      Dakt. Willett anaeleza hivi: “Watu wengi huona kwamba kutembea ni njia bora ya kufanya mazoezi kwa sababu mtu hahitaji vifaa vya pekee, anaweza kutembea wakati wowote na mahali popote, na si rahisi kuumia.” Anapendekeza watu watembee haraka-haraka badala ya kutembea kwa starehe. Pia anapendekeza watu wafanye mazoezi kwa dakika 30 kila siku ikiwezekana.

      Je, Suluhisho Ni Kufanyiwa Upasuaji?

      Ili kupunguza uzito na kuepuka kuongeza uzito, watu wengine walionenepa kupita kiasi wamefuata mashauri ya wataalamu fulani ambao hupendekeza mbinu mbalimbali za upasuaji. Ni nani wanaoweza kupasuliwa? Waandishi wa kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight wanapendekeza hivi: “Huenda daktari akataka ufanyiwe upasuaji ikiwa BMI yako inazidi 40, hilo likionyesha kwamba umenenepa kupita kiasi.” (Ona chati kwenye ukurasa wa 5.) Kichapo Mayo Clinic Health Letter kinapendekeza hivi: “Upasuaji kwa ajili ya watu walionenepa kupita kiasi unapendekezwa tu kwa watu wenye umri wa kati ya miaka 18 na 65 ambao BMI yao imezidi 40 na unene wao unahatarisha sana afya yao.”—Italiki ni zetu.

      Ni nini baadhi ya njia za upasuaji? Njia hizo zinahusisha kufupisha sehemu ya tumbo inayoitwa chango, kufunga sehemu fulani ya tumbo na kuacha nafasi ndogo ya kupitisha chakula, na kufunga sehemu ya juu ya tumbo, na kuacha kifuko kidogo kinachoweza kutoshea kiasi kidogo tu cha chakula. Katika njia hiyo iliyotajwa mwisho, chango hukatwa na kuunganishwa na kifuko hicho. Hivyo, chakula hakiingii katika sehemu kubwa ya tumbo kutia ndani duodeni (duodenum).

      Vipi watu ambao wamepunguza uzito sana? Je, wamepata faida zozote?

      [Maelezo ya Chini]

      a Madhara hayo yanatia ndani ongezeko kubwa la chuma katika damu, matatizo ya figo, na kufunga choo.

      b Inafaa Wakristo waliojiweka wakfu, ambao wanataka kutumia maisha yao kwa njia inayokubalika katika utumishi mtakatifu wa Mungu, wapunguze uzito ili wawe na afya njema. Badala ya kufa mapema, wanaweza kumtumikia Mungu kwa miaka mingi.—Waroma 12:1.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Madokezo ya Mazoea Mazuri ya Kula

      Peremende Tamutamu, peremende

      zilizotengenezwa viwandani (mara chache;

      usile zaidi ya kalori 75 kwa siku)

      Mafuta Mafuta ya zeituni, njugu, mafuta ya

      canola, parachichi (mara 3-5 kwa siku; yaani

      kila mara pakua kijiko kimoja kidogo cha mafuta

      au vijiko viwili vikubwa vya njugu)

      Protini na Vyakula vya Maziwa Maharagwe, samaki,

      nyama isiyo na mafuta mengi, mayai, vyakula

      vilivyotengenezwa kwa maziwa visivyo na mafuta mengi,

      jibini (mara 3-7 kwa siku; kila mara pakua gramu 85

      hivi tu za nyama iliyopikwa au samaki)

      Vyakula Vyenye Wanga Hasa nafaka, spageti, mkate, wali

      (mara 4-8 kwa siku; kila mara kula kipande cha mkate)

      Matunda na Mboga Kula mboga mbalimbali (kula mara nyingi; angalau 3)

      Amkeni! halipendekezi mazoea yoyote hususa ya kula na njia za kudhibiti uzito. Linawaeleza tu wasomaji wake baadhi ya njia zinazoweza kutumiwa. Watu wanapaswa kupata mashauri ya daktari kabla ya kuanza mazoezi yoyote au kufuata mazoea fulani ya kula.

      [Hisani]

      Kwa mujibu wa Mayo Clinic

      [SAnduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Wengine wametumia madokezo haya ili kupunguza uzito:

      1 Jua kiasi cha kalori zilizomo katika chakula unachokula na vinywaji unavyokunywa. Kumbuka: Vinywaji huwa na kalori nyingi, hasa vile vilivyoongezwa sukari. Vilevile, pombe huwa na kalori nyingi sana. Pia, jihadhari na soda zinazotangazwa sana na wafanyabiashara. Chunguza kiwango cha kalori kilichoonyeshwa kwenye kibandiko. Ukifanya hivyo, huenda ukashangaa kuona kiasi cha kalori kilicho katika kinywaji hicho.

      2 Epuka kushawishiwa. Bila shaka, utakula chipsi, chokoleti, au biskuti ikiwa zinapatikana kwa wingi nyumbani! Usiweke vitu hivyo nyumbani, badala yake hifadhi tu vyakula vilivyo na kalori chache, kama vile matofaa, karoti, na vyakula vya nafaka.

      3 Kula kitu kidogo kabla ya mlo. Kufanya hivyo kutapunguza hamu yako ya kula na huenda kukakufanya ule chakula kidogo.

      4 Usile kila kitu kinachoandaliwa. Chagua unachokula. Usile chochote ambacho unajua kina kalori nyingi sana.

      5 Usiharakishe. Haraka ni ya nini? Furahia mlo wako kwa kuchunguza unachokula—angalia rangi yake, onja ladha yake, na ufurahie jinsi kinavyochangamana vizuri. Tambua dalili za mwili zinazokuonyesha kwamba umeshiba.

      6 Acha kula kabla ya kuhisi kwamba umeshiba.

      7 Katika nchi fulani, mikahawa huwapakulia watu chakula kingi kupita kiasi. Unaweza kula nusu ya chakula hicho au unaweza kumgawia mtu mwingine.

      8 Si lazima ule vyakula vitamu vinavyoandaliwa baada ya mlo mkuu. Baada ya mlo, ni afadhali kula tunda au kitu kingine chenye kalori chache.

      9 Wauzaji wa vyakula hutaka ule sana. Kusudi lao ni kupata faida. Watajaribu kulenga udhaifu wako. Usipumbazwe na matangazo yao ya biashara ya ujanja na picha maridadi. Unaweza kukataa katakata kushawishiwa nao!

      [Hisani]

      Madokezo haya yametolewa katika kitabu Eat, Drink, and Be Healthy, cha Dakt. Walter C. Willett

      [Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Fanya mazoezi!

  • Je, kuna faida Kupunguza Uzito?
    Amkeni!—2004 | Novemba 8
    • Je, kuna faida Kupunguza Uzito?

      AMKENI! liliwahoji watu kadhaa ambao wamepambana na tatizo la kunenepa kupita kiasi? Je, walifanikiwa? Wanatoa madokezo gani kwa wale wanaokabili tatizo hilo?

      ◼ Fikiria mfano wa Mike, ambaye ana umri wa miaka 46, kimo cha sentimeta 183, na kilo 130. Uzito wake wa juu zaidi ulikuwa kilo 157.

      Mike: “Ama kweli, nilikuwa mnene kupita kiasi. Hata nilipokuwa kijana, nilikuwa mnene sana. Hiyo ni kawaida katika familia yetu, kwani ndugu yangu na dada zangu ni wanene sana. Hatukuwa tukibakisha chakula chochote katika sahani, hata ikiwa ingejazwa sana. Kwa nini nilibadilisha mazoea yangu ya kula? Ni kwa sababu daktari aliniambia kwamba ninakabili hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari! Niliogopa sana nilipofikiria kwamba nitalazimika kutumia dawa ya insulini katika maisha yangu yote. Pia, nilikuwa na kolesteroli nyingi sana mwilini na ilinibidi nitumie dawa.

      “Mimi hufanya kazi inayonilazimu kuketi kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nina ratiba ya kufanya mazoezi kwa ukawaida ambayo inahusisha kutumia mashine ya mazoezi ya kutembea kwa nusu saa angalau mara tatu kwa juma. Hatua nyingine muhimu ilikuwa kuandika chakula nilichokula kila siku. Kwa kuwa mtaalamu wa lishe alichunguza orodha hiyo kila juma, hilo lilinisaidia kujizuia. Nilikumbuka jambo hili, ‘Usipokula chakula fulani, hutahitaji kukiandika!’

      “Hilo limeniwezesha kupunguza kilo 28 kwa muda wa miezi 15 iliyopita. Hata hivyo, bado ninapaswa kupunguza kilo zaidi hadi nifikie kilo 102. Hivyo, nimeacha kula chipsi na vitafuno vingine. Katika miezi ya karibuni nimekula saladi na mboga nyingi kuliko wakati mwingine wowote!

      “Jambo jingine lililonichochea kupunguza uzito ni kwamba, nikiwa dereva wa lori, afya yangu huchunguzwa kila mwaka ili nipate leseni mpya. Karibu nipoteze leseni yangu kwa sababu ya uwezekano wa kupata kisukari. Sasa hali imebadilika. Sihitaji tena kutumia dawa ili kudhibiti kolesteroli. Shinikizo la damu yangu limepungua, nami situmii dawa nyingi kulitibu. Nina nguvu zaidi, na matatizo makubwa ya mgongo wangu yamepungua. Pia, nimepunguza uzito pole kwa pole!”

      Amkeni!: “Je, mke anaweza kumsaidia mume wake kupunguza uzito?”

      Mike: “Unahitaji mtu wa kukutia moyo unapojitahidi kupunguza uzito. Mke wangu alifikiri kwamba alikuwa akinionyesha upendo kwa kunipa chakula kingi. Lakini sasa ananisaidia kudhibiti kiasi cha chakula ninachokula. Ni muhimu nidumishe jitihada zangu kwa sababu ninapoacha kufanya hivyo mimi huongeza uzito haraka sana.”

      ◼ Pia, hebu ona mfano wa mtu mwingine anayeitwa Mike, kutoka Kansas, Marekani. Ana umri wa miaka 43 na kimo cha sentimeta 173. Tulimuuliza kuhusu uzito wa juu ambao amewahi kuwa nao na mambo yanayosababisha anenepe.

      Mike: “Uzito wangu wa juu zaidi ulikuwa kilo 135 hivi. Kila wakati nilikuwa mchovu na sikuwa na nguvu za kutosha kufanya mambo. Nilishindwa kulala kwa sababu ya matatizo ya kupumua. Kwa hiyo, nilienda kumwona daktari, naye akagundua kwamba kisababishi kimoja cha tatizo langu la kunenepa ni kushindwa kupumua ninapolala.a Pia aligundua kwamba nina shinikizo la juu la damu.”

      Amkeni!: “Ulisuluhishaje tatizo lako?”

      Mike: “Daktari alipendekeza nitumie kifaa fulani ambacho huniwezesha kupumua ninapolala. Hivyo, koo langu halizibi na ninaweza kupumua kama kawaida. Kwa hiyo, niliweza kutimiza mengi mchana na kuanza kupunguza uzito. Pia nilianza kutumia mashine ya mazoezi ya kutembea mara tatu kwa juma. Nilibadili mazoea yangu ya kula, na hilo lilitia ndani kudhibiti kiasi cha chakula nilichokula na kuepuka kuongeza-ongeza chakula. Sasa nimepunguza kilo 20 katika muda wa mwaka mmoja tu, na bado ninahitaji kupunguza kilo 20 zaidi. Ijapokuwa ninapunguza uzito polepole, ninajua kwamba ninaweza kufanikiwa.”

      Amkeni!: “Ni jambo gani jingine ambalo limekuchochea kupunguza uzito?”

      Mike: “Huwezi kufurahi watu wanapokudhihaki na kuchambua sura yako. Huenda wengine wakafikiri kwamba wewe ni mvivu. Hawatambui kuwa kunenepa kupita kiasi kunaweza kusababishwa na mambo mengi. Naamini kwamba huenda kwa kiasi fulani tatizo langu lilisababishwa na urithi, kwa sababu wengi katika familia yetu wana tatizo hilo.

      “Hata hivyo, ninatambua kwamba ili nipunguze uzito, ninahitaji kufanya mazoezi na kudhibiti ninachokula.”

      ◼ Pia, Amkeni! lilimhoji Wayne kutoka Oregon, aliye na umri wa miaka 38. Alipokuwa na umri wa miaka 31, alikuwa na kilo 112.

      Wayne: “Nilifanya kazi iliyonilazimu kuketi kwa muda mrefu na sikufanya mazoezi. Nilipomwendea daktari, nilishtuka kujua kwamba nilikuwa na shinikizo la juu la damu na ningepatwa na ugonjwa wa moyo. Alinishauri nimwone mtaalamu wa lishe. Mtaalamu wa lishe alinipa ratiba ya mazoezi na jinsi ya kudhibiti kiasi cha chakula nilichokula. Nilianza kutembea kilometa tano kila siku bila kupumzika, na kuamka mapema kila asubuhi kufanya mazoezi. Ilinibidi kubadili maoni yangu kuhusu mazoea yangu ya kula na kunywa. Niliacha kula vyakula visivyoboresha afya na kupunguza kiasi cha mkate nilichokula na soda nilizokunywa. Badala yake, nilianza kula matunda na mboga nyingi. Sasa uzito wangu umepungua hadi kilo 80!”

      Amkeni!: “Umepata faida gani?”

      Wayne: “Ninahisi kwamba nina afya nzuri zaidi na kwamba sasa niko hai. Kabla ya hapo, ni kana kwamba nilikuwa nimekufa. Faida nyingine ni kwamba nimeacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu. Sasa ninapokutana na watu siwi na wasiwasi, kwa sababu sitachambuliwa kwa kunenepa kupita kiasi.”

      ◼ Charles (si jina lake halisi) ana kimo cha sentimeta 196. Uzito wake wa juu zaidi ulikuwa kilo 168.

      Charles: “Nilikuwa na matatizo makubwa ya afya, na hali yangu ilikuwa ikizidi kuwa mbaya. Sikuweza kupanda ngazi. Sikuwa na nguvu za kufanya kazi. Kazi yangu hunilazimu niketi kwa muda mrefu na inahusisha utafiti na usimamizi. Nilijua kwamba ninahitaji kupunguza uzito, hasa baada ya kushauriwa na daktari. Alinionya kwamba ninaweza kupata kiharusi. Nimewahi kuona jinsi mtu anavyoathiriwa na ugonjwa huo. Hilo lilinisadikisha kwamba ninahitaji kuchukua hatua. Daktari alipendekeza nifanye mazoezi ya kutembea kwa kutumia mashine huku kukiwa na mtu wa kunichunguza, na alinipa orodha ya vyakula ninavyopaswa kula. Sasa mwaka mmoja hivi umepita na nina kilo 136, lakini ninajua kwamba ninahitaji kupunguza kilo zaidi. Faida ambazo tayari nimepata zinanisadikisha kwamba jitihada zangu si za bure. Sasa ninaweza kupanda ngazi na nina nguvu zaidi.”

      ◼ Marta, ambaye alizaliwa nchini El Salvador, alikuwa na kilo 83. Hivyo, alikuwa mnene kupita kiasi ukilinganisha na kimo chake cha sentimeta 165.

      Marta: “Nilimwona daktari, naye alisisitiza kwamba ninapaswa kupunguza uzito. Nilikubaliana na maoni yake akiwa mtaalamu. Alinishauri nimwone mtaalamu wa lishe. Mtaalamu huyo alinieleza mambo ninayopaswa kufanya. Alinionyesha jinsi ya kupunguza kiasi nilichokula na kuepuka vyakula fulani. Mwanzoni, nilihitaji kumwona kila juma; na baadaye kila mwezi, ili kumwonyesha maendeleo yangu. Daktari wangu na mtaalamu huyo walinipongeza kwa maendeleo niliyofanya. Baada ya muda, nilikuwa nimepunguza kilo 12, na sasa ninadumisha uzito wa kilo 68.”

      Amkeni!: “Vipi kufanya mazoezi na kutumia dawa?”

      Marta: “Kwa kuwa sikuwa na tatizo la kolesteroli, sikuhitaji kutumia dawa. Lakini nilianza kufanya mazoezi ya kutembea haraka kila siku.”

      Amkeni!: “Ulifanya nini ulipowatembelea marafiki ambao walisisitiza ule zaidi ya kiasi chako cha kawaida?”

      Marta: “Nilikuwa nikiwaambia hivi, ‘Daktari anataka nifuate mashauri yake kuhusu lishe ili niwe na afya njema,’ na kwa kawaida hawangeendelea kusisitiza.”

      Unaweza kufanya nini ikiwa wewe ni mnene sana au ni mnene kupita kiasi? Wahenga walisema, “Penye nia pana njia.” Je, una nia ya kupunguza uzito? Ikiwa wewe ni mtoto au mtu mzima aliyenenepa kupita kiasi, unaweza kuchagua kupunguza uzito au kupunguza maisha yako. Basi, uwe na utendaji mwingi maishani na upate uradhi unaotokana na kufanikiwa—hata katika mambo madogo, kama vile kuvaa nguo za saizi ndogo kwa sababu ya kupunguza uzito!

      [Maelezo ya Chini]

      a Kwa habari zaidi kuhusu tatizo la kushindwa kupumua unapolala, ona Amkeni! la Februari 8, 2004, ukurasa wa 10-12.

      [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      Je upasuaji wa kuondoa mafuta ndiyo suluhisho?

      Upasuaji huo unahusisha nini? Kamusi moja inasema hivi: “Kwa kawaida upasuaji huo unahusisha kufyonza mafuta ya ziada kutoka sehemu fulani ya mwili kama vile mapajani au tumboni.” (American Heritage Dictionary) Hata hivyo, je, upasuaji huo ni suluhisho la kunenepa kupita kiasi?

      Kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight kinasema kwamba upasuaji huo huboresha umbo la mtu tu. Si njia ya kupunguza uzito. Chembe za mafuta hufyonzwa kutoka mwilini wakati mrija mwembamba unapopenyezwa chini ya ngozi. Kilo kadhaa zinaweza kufyonzwa kwa wakati mmoja. Hata hivyo, “upasuaji huo si tiba ya kunenepa kupita kiasi.” Je, upasuaji huo ni salama? “Watu walio na magonjwa fulani yanayosababishwa na kunenepa kupita kiasi kama vile kisukari na ugonjwa wa moyo, wanakabili hatari kubwa zaidi wanapofanyiwa upasuaji huo.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki