-
Chakula Kinapokuwa Adui YakoAmkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Chakula Kinapokuwa Adui Yako
Akitafakari juu ya miaka alipokuwa tineja, Jean akumbuka waziwazi akitaniwa na kudhihakiwa. Sababu ilikuwa gani? Alikuwa msichana mrefu na mnene zaidi katika darasa lake shuleni. Lakini si hivyo tu. “Jambo lililokuwa baya zaidi ya kuwa mkubwa, ni kwamba nilikuwa mwenye haya na mwenye kujifikiria sana,” asema Jean. “Mara nyingi nilikuwa mpweke, nikitaka nikubaliwe, lakini mara nyingi nilihisi kama mgeni.”
Jean alisadiki kwamba ukubwa wa mwili wake ndio uliokuwa chanzo cha matatizo yake yote na kwamba kama angekuwa na umbo zuri jembamba matatizo yake yote yangekwisha. Si kwamba Jean alikuwa mnene kupita kiasi. Kinyume cha hilo, akiwa na urefu wa futi sita na uzito wa kilogramu 66, hakuwa amezidisha uzito. Hata hivyo, Jean alijihisi kuwa mnene, na alipokuwa na umri wa miaka 23 aliamua kupunguza uzito. Alifikiri hivi, ‘Nikiwa mwembamba, watu wengine watataka kuwa karibu nami. Mwishowe nitajiona kuwa ninakubalika na kuwa wa pekee.’
“Kusababu huko kwa kipumbavu kuliongoza kwenye mtego wa miaka kumi na miwili wa kuwa na tatizo la kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida,” aeleza Jean. “Ni kweli nilikuwa mwembamba, mwembamba sana hivi kwamba nilikaribia kufa, lakini badala ya kuishi maisha yenye furaha, niliharibu afya yangu na kusababisha mshuko-moyo na taabu iliyodumu kwa zaidi ya mwongo mmoja.”
JEAN hayuko peke yake. Kulingana na kadirio moja, 1 kati ya wanawake 100 Wamarekani hupatwa na tatizo la kujinyima chakula akiwa tineja au kijana, na labda idadi inayozidi hiyo mara tatu wanakuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. “Nimefanya kazi shuleni na kwenye vyuo kwa miaka kadhaa,” asema Dakt. Mary Pipher, “na ninajionea moja kwa moja kwamba matatizo ya kula yameenea tu kama wakati wowote.”
Pia ni ya namna nyingi. Wakati mmoja yalifikiriwa kuwa tatizo la matajiri lakini sasa yanaonwa kuwa ya kawaida katika watu wa viwango vyote vya jamii na kiuchumi. Hata idadi ya wanaume wanaopatwa na tatizo hili inaongezeka, ikilifanya gazeti la Newsweek liyaite matatizo ya kula kuwa “yanayoshambulia wanaume na wanawake bila kubagua.”
Ingawa hivyo, jambo linalohangaisha zaidi hasa, ni kwamba wastani wa umri wa watu wanaotibiwa kwa matatizo ya kula unazidi kupungua. “Kuna wasichana chini ya umri wa miaka 10, hata wengine ni wachanga sana wakiwa na umri wa miaka 6, wanaolazwa hospitalini,” asema Margaret Beck, kaimu mkurugenzi wa kitivo cha matatizo ya kula katika Toronto. “Bado ni idadi ndogo,” aongezea, “lakini inakua.”
Kwa ujumla, matatizo ya kula huathiri mamilioni—hasa wasichana na wanawake vijana. “Hawafikiri juu ya chakula au kula chakula kama wafanyavyo watu wengi,” asema mfanyakazi wa huduma za jamii Nancy Kolodny. “Badala ya kula wanapohisi njaa, kula kwa sababu ya lishe na afya njema, kula kwa ajili ya kujifurahisha, au kula ili kufurahia ushirika unaofaa na wengine, wanakula chakula kupita kiasi na kufanya mambo ambayo hayaonwi kuwa ya ‘kawaida’—kama vile kusitawisha desturi zisizo za kawaida kabla hawajaanza kula, au kujilazimisha kutapika mara moja chakula walichokula.”
Acheni tuchunguze kwa makini matatizo mawili ya kula: kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
-
-
Kujinyima Chakula na Kuwa na Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida—Mambo Hakika, HatariAmkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Kujinyima Chakula na Kuwa na Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida—Mambo Hakika, Hatari
“Chakula hubeba mzigo wa kihisia-moyo ulio mzito zaidi ya kitu chochote kiwezacho kupimwa kwa kalori au kwa gramu.”—Janet Greeson, mwandishi.
MATATIZO mawili ya kula yaliyo ya kawaida zaidi ni kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Kila moja lina mambo yake ya kipekee. Lakini kama tutakavyoona, yote mawili yaweza kuwa hatari—hata yenye kufisha.
Kujinyima Chakula—Njaa ya Kujiletea
Watu wanaoteseka kwa kujinyima chakula, ama hukataa kula au hula kiasi kidogo sana hivi kwamba wanakosa lishe ya kutosha. Mfikirie Antoinette mwenye umri wa miaka 17, anayesema kwamba wakati fulani huenda uzito wake ulipungua kufikia kilogramu 37—uzito kidogo sana kwa kijana mwenye urefu wa futi tano na inchi saba. “Sikula zaidi ya kalori 250 kwa siku na niliandika kwenye kitabu chakula nilichokula,” yeye asema.
Watu wanaojinyima chakula wana hofu ya chakula, na watafanya yote wawezayo ili kujizuia kuongeza uzito. “Nilianza kutema chakula changu kwenye karatasi ya kupangusia mdomo nikijifanya kwamba nilikuwa nikipangusa mdomo wangu,” asema Heather. Susan alifanya mazoezi kwa bidii ili kupunguza uzito wake. “Karibu kila siku,” asema, “nilikimbia kilometa 12, au kuogelea kwa muda wa saa moja, au sivyo nilihisi wasiwasi na hatia iwapo sikufanya mazoezi. Na kila asubuhi nilifurahia sana, kwa kawaida furaha yangu pekee, kupanda juu ya mizani ili kuthibitisha kwamba uzito wangu ulipungua kilogramu 45.”
Jambo la kinyume, watu fulani wanaojinyima chakula huwa wapishi bora na wataandaa chakula kitamu sana ambacho wao wenyewe hukataa kukionja. “Hali yangu ilipokuwa mbaya sana,” asema Antoinette, “nilitayarisha chakula chote cha mchana nyumbani na kuwatayarishia ndugu na dada yangu mdogo chakula cha kubeba. Singewaruhusu wakaribie friji. Nilihisi kana kwamba jiko lilikuwa langu peke yangu.”
Kulingana na kitabu A Parent’s Guide to Anorexia and Bulimia, watu fulani wanaojinyima chakula “huwa safi kupita kiasi na waweza kuwadai wengine katika familia nzima wafikie viwango vyao visivyo halisi na visivyofikika. Hakuna gazeti au viatu au kikombe cha kahawa kiwezacho kuachwa mahali pasipopafaa hata kwa dakika chache. Huenda wakahangaikia sana afya ya kibinafsi na sura, wakitumia muda mwingi kuvalia, mlango ukiwa umefungwa na kuwakataza wengine wasiingie ili kujitayarisha kwenda shuleni au kazini.”
Tatizo hili la kujinyima chakula husitawi namna gani? Hasa, tineja au mtu mzima mchanga—mara nyingi mwanamke—huanza harakati za kupunguza ratili kadhaa. Hata hivyo, anapofikia mradi wake, hukosa kuridhika. Anapojitazama kwenye kioo, bado hujiona kuwa mnene, na kwa hiyo anaamua kwamba litakuwa jambo bora kupunguza ratili nyingine chache. Jambo hili huendelea mpaka mwenye kupunguza uzito anapofikia asilimia 15 au zaidi chini ya kiwango cha kawaida kwa urefu wake.
Kufikia kiwango hiki marafiki na washiriki wa familia huanza kuonyesha wasiwasi kwamba mwenye kupunguza uzito anaonekana mwembamba sana, hata kuwa amedhoofika. Lakini mtu anayejinyima chakula huona mambo kwa njia tofauti. “Sikudhani nilionekana nimekonda,” asema Alan, mwanamume mwenye urefu wa futi tano na inchi tisa anayejinyima chakula ambaye wakati mmoja uzito wake ulipungua na kufikia kilogramu 33. “Kadiri upunguzavyo uzito,” asema, “ndivyo akili yako hupotoka na kukosa kujiona waziwazi.”a
Baada ya muda, kujinyima chakula kwaweza kuongoza kwenye matatizo makubwa ya afya, kutia ndani kupoteza ugumu wa mifupa na kuharibika kwa figo. Hata kwaweza kuua. “Daktari wangu aliniambia kwamba nilikuwa nimeunyima mwili wangu virutubishi vingi sana hivi kwamba ningaliendelea na mazoea yangu ya kula kwa miezi miwili, ningalikufa kutokana na utapiamlo,” asema Heather. Jarida The Harvard Mental Health Letter laripoti kwamba kwa pindi inayozidi miaka kumi, karibu asilimia 5 ya wanawake wanaobainishwa kuwa wanajinyima chakula hufa.
Hamu ya Chakula Isiyo ya Kawaida —Kula kwa Wingi na Kusafisha Tumbo
Tatizo la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida hutambuliwa na kula kwa wingi (kula upesi kiasi kikubwa cha chakula, labda kalori 5,000 au zaidi) na kisha kusafisha tumbo (kuacha tumbo likiwa tupu, mara nyingi kwa kutapika au kwa kutumia dawa za kuharisha).b
Kwa kutofautishwa na kujinyima chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida hakutambuliwi kwa urahisi. Huenda mwenye tatizo hili asiwe mwembamba isivyo kawaida, na mazoea yake ya kula yaweza kuonekana kuwa ya kawaida—angalau kwa watu wengine. Lakini kwa mtu aliye na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, kwa hakika maisha si ya kawaida. Kwa kweli, yeye huhangaikia chakula kupita kiasi hivi kwamba kila kitu kingine huwa hakina maana. “Kadiri nilivyokula kwa wingi na kutapika, ndivyo nilivyokosa kujali juu ya mambo mengine au watu wengine,” asema Melinda mwenye umri wa miaka 16. “Kwa kweli nilisahau kufurahia ushirika wa marafiki zangu.”
Geneen Roth, mwandishi na mwalimu katika uwanja wa kitaaluma wa matatizo ya kula, afafanua kula kwa wingi kuwa “kichaa cha dakika thelathini, kuingia kwenye eneo lisilokuwa na vizuizi.” Asema kwamba wakati wa kula kwa wingi, “hakuna kitu kinachokuwa cha maana—si marafiki, si familia . . . Hakuna kitu kinachokuwa cha maana ila chakula.” Lydia mwenye umri wa miaka 17 aliye na tatizo hili afafanua hali yake kwa kutumia mfano ulio wazi. “Ninahisi kuwa kama kifaa cha kuponda takataka,” asema. “Kula chakula kingi, kitafune, kitapike. Kwa kurudia jambo hilo hilo.”
Mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hujaribu sana kuzuia kuongeza uzito ambao kwa kawaida ungeletwa na kula kusikodhibitiwa. Kwa hiyo, mara tu baada ya kula kwa wingi, ama hujaribu kutapika ama kunywa dawa za kuharisha ili kuondoa chakula kabla hakijageuzwa kuwa mafuta ya mwili.c Ingawa wazo hilo laweza kuonekana kuwa lenye kuchukiza, mtu mwenye kula kwa wingi halioni hivyo. “Kadiri unavyokula kwa wingi na kusafisha tumbo, ndivyo iwavyo rahisi kwako,” aeleza mfanyakazi wa huduma za jamii Nancy Kolodny. “Hisi zako za mapema za kuchukizwa au hata hofu hubadilishwa mara moja na kichocheo cha kurudia mambo haya ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.”
Kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni jambo lililo hatari sana. Kwa kielelezo, kurudia-rudia kusafisha tumbo kwa kutapika hufanya mdomo upatwe na asidi kali za tumbo, ambazo zinaweza kumomonyoa tabaka ya nje ya meno ya mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Zoea hilo pia laweza kuharibu umio, ini, mapafu, na moyo wa mwenye tatizo hili. Katika visa vinavyopita kiasi, kutapika kwaweza kusababisha tumbo lipasuke na hata kifo. Dawa za kuharisha zinapotumiwa kupita kiasi zaweza kuwa hatari pia. Zaweza kuharibu matumbo na pia kusababisha kuharisha mfululizo na kuvuja damu kwa utumbo mpana. Kama vile kutapika mara kwa mara, matumizi mabaya ya dawa za kuharisha, katika visa vinavyopita kiasi, husababisha kifo.
Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili, athari za matatizo ya kula zinaongezeka daima. Ni nini kinachomchochea mwanamke mmoja kijana achezee kifo kwa kujinyima chakula? Kwa nini mwingine anatamani sana chakula hivi kwamba anakula kwa wingi na kisha ahangaishwa sana na uzito wake hivi kwamba ashurutika kutapika alichokula? Maswali haya yatachunguzwa katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Wataalamu fulani wanadai kwamba upungufu wa asilimia 20 hadi 25 wa uzito wa mtu kwa ujumla waweza kuchochea mabadiliko ya kemikali katika akili yanayoweza kubadili mtazamo wake, yakimfanya aone mafuta mahali hayapo.
b Kula kupita kiasi kusikodhibitiwa bila kusafisha tumbo pia huonwa na wengine kuwa tatizo la kula.
c Ili wasiongeze uzito, watu wengi wenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hufanya mazoezi kwa bidii kila siku. Baadhi yao hufaulu sana katika kupunguza uzito hivi kwamba baada ya muda hujinyima chakula, na baada ya hapo hali yao yaweza kuwa ikibadilika kati ya kujinyima chakula na kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
-
-
Ni Nini Husababisha Matatizo ya Kula?Amkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Ni Nini Husababisha Matatizo ya Kula?
“Tatizo la kula haliibuki ghafula tu bila sababu. Ni dalili, ishara ya kwamba kuna tatizo fulani katika maisha ya mtu.”—Nancy Kolodny, mfanyakazi wa huduma za jamii.
MATATIZO ya kula si mapya. Kujinyima chakula ni tatizo lililogunduliwa rasmi katika mwaka wa 1873, na dalili zake zimejulikana kwa miaka 300 iliyopita. Hata hivyo, tangu Vita ya Ulimwengu ya Pili, idadi ya watu wenye tatizo la kujinyima chakula imeongezeka kwa njia yenye kutazamisha. Hali hiyo inafanana na ile ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Tatizo hili limejulikana kwa karne kadhaa, lakini katika miongo ya karibuni, kama kitabu kimoja kuhusu habari hii kisemavyo, “limeongezeka kwa njia yenye kutazamisha.”
Ni nini kisababishi cha matatizo ya kula? Je, yanarithiwa, au ni itikio lisilo la kawaida kwa utamaduni unaotukuza wembamba? Familia inatimiza fungu gani? Si rahisi kuyajibu maswali haya. Kama asemavyo mfanyakazi wa huduma za jamii Nancy Kolodny, kufasiri tatizo la kula “si jambo lililo la moja kwa moja kama vile kutambulisha hali fulani ya kitiba kama surua, au tetewanga, ambapo daktari hujua kisababishi hasa, namna unavyoweza kupatwa na ugonjwa huo, muda ambao ugonjwa huo utadumu, na matibabu yaliyo bora ni yapi.”
Hata hivyo, watafiti wanataja mambo kadhaa yanayoweza kuchangia ukuzi wa matatizo ya kula. Acheni tuchunguze machache kati yake.
Utamaduni Unaotukuza Wembamba
Katika nchi zenye utajiri, viwanda vya mitindo ya nguo huonyesha vigezo vya wanawake wembamba kwa watazamaji wachanga wenye kuvutiwa, wakichochea wazo la kwamba msichana huwa mrembo tu kwa kadiri alivyo mwembamba. Ujumbe huu uliopotoka huwashurutisha wanawake wengi wajitahidi kufikia uzito wa mwili usio na afya na usio halisi. Dakt. Christine Davies asema: “Mwanamke wa kawaida ana urefu wa futi tano na inchi tano na uzito wa kilogramu 66. Kigezo cha kawaida ni mwanamke mwenye urefu wa futi tano na inchi 11 na uzito wa kilogramu 50. Asilimia 99 kati yetu hatujafikia kiwango hicho na hatutakifikia kamwe.”
Licha ya uhakika huu, wanawake fulani wanapita kiasi ili kuwa na mwili wanaouona kuwa bora. Kwa kielelezo, katika uchunguzi wa mwaka wa 1997 uliofanyiwa wanawake 3,452, asilimia 24 ya wanawake walisema kwamba wangekuwa tayari kudhabihu miaka mitatu ya maisha yao ili kufikia mradi wao wa uzito. Kwa wale wanaotambuliwa kuwa tofauti, uchunguzi huo ulisema, “maisha yana thamani tu ikiwa wewe ni mwembamba.” Kwa kuwa asilimia 22 ya wale waliofanyiwa uchunguzi walisema kwamba vigezo wa kike walio katika magazeti ya mitindo waliathiri umbo la miili yao walipokuwa wachanga, ripoti hiyo ilimalizia kwa kusema kwamba: “Haiwezekani tena kukanusha uhakika wa kwamba sura za vigezo katika vyombo vya habari zinaathiri sana jinsi wanawake wanavyojiona.”
Bila shaka, wale wanaoelekea kunaswa zaidi na mawazo bandia ya vyombo vya habari ni wale ambao kwanza hawajistahi wenyewe. Kama asemavyo mfanyakazi wa huduma za jamii kuhusu utibabu, Ilene Fishman, “jambo la msingi ni kujistahi.” Imeonwa kwamba watu wanaokubali namna wanavyoonekana huwa nadra sana wahangaikie chakula kupita kiasi.
Kula na Hisia-Moyo
Wataalamu wengi wanasema kwamba kuna mengi yanayohusika katika tatizo la kula kuliko chakula. “Tatizo la kula ni onyo,” asema mfanyakazi wa huduma za jamii, Nancy Kolodny, “likuambialo kwamba unahitaji kukazia uangalifu hali fulani maishani mwako ambayo unapuuza au kuepuka. Tatizo la kula ni kikumbusha kwamba unakosa kuzungumza kuhusu mikazo na kukatishwa tamaa ambako huenda unakabili.”
Ni aina zipi za mikazo na kukatishwa tamaa? Kwa wengine yaweza kuhusisha taabu nyumbani. Kwa kielelezo, Geneen Roth akumbuka kwamba wakati wa utoto wake, chakula,—hasa peremende—zilikuwa “ulinzi dhidi ya ugomvi wa wazazi.” Asema hivi: “Nilipohisi kwamba wazazi wangu walikaribia kupigana, ningegeuza fikira zangu kwa urahisi kama vile ugeuzavyo idhaa ya televisheni, ziondoke kwenye udhibiti wa mama na baba hadi kwenye hali isiyokuwa na lolote ila mimi na utamu uliopo mdomoni mwangu.”
Nyakati nyingine tatizo la kula linasababishwa na kitu kikuu zaidi. Kwa kielelezo, The New Teenage Body Book chasema: “Uchunguzi unaonyesha kwamba wale walio na vurugu ya ngono (kutendwa vibaya au kusumbuliwa kingono) bila kufahamu wanaweza kujilinda wenyewe kwa kufanya miili yao isivutie kingono na kwa kuelekeza uangalifu wao kwa kitu kilicho salama kama vile chakula.” Bila shaka, watu hawapaswi kufikia mkataa wa kwamba mtu anayeteseka kutokana na tatizo la kula ametendwa vibaya kingono.
Tatizo la kula laweza kukua katika hali inayoonekana kuwa tulivu. Kwa kweli, mtu anayeweza hasa kujinyima chakula aweza kuwa msichana anayeishi katika mazingira ambayo hana uhuru wa kujifanyia maamuzi yoyote au kuonyesha hisia zake zisizofaa. Kwa nje, akubali; lakini kindani, ana msukosuko na ahisi kwamba hadhibiti maisha yake. Kwa kutothubutu kulalamika waziwazi, anaelekeza fikira kwenye sehemu moja ya maisha yake anayoweza kudhibiti—mwili wake.
Hata hivyo, inapasa kutambuliwa kuwa sikuzote matatizo ya kula hayawi tokeo la msukosuko wa familia au vurugu ya ngono. Kwa wengine, matatizo ya kula husitawi kwa sababu familia hukazia zaidi suala la uzito. Labda mzazi ni mnene kupita kiasi au anafuata miiko ya milo na kusababisha athari inayopita kiasi—au hata mtazamo—wenye hofu kuelekea chakula. Kwa wengine, mwanzo wa kubalehe wenyewe ni jambo linalochangia. Mabadiliko ya mwili ambayo ni sehemu ya maana katika kuwa mtu mzima yanaweza kumfanya msichana ahisi kuwa mnene—hasa ikiwa anakomaa upesi kuliko marika zake. Anaweza kuchukua hatua kali za kuondoa makunyanzi ya wanawake ikiwa aona badiliko hili kuwa lenye kuogofya.
Kwa kuongezea kutaja mambo ya kihisia-moyo, watafiti fulani wanasema kwamba huenda kukawa na jambo fulani la kimwili linalohusika. Kwa kielelezo, wanataja kwamba kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni tatizo linaloweza kuwa na chanzo kwenye utendaji wa akili ya mwenye tatizo hilo. Wanadai kwamba sehemu ya akili inayodhibiti hali ya moyo na hamu ya chakula inahusika na kwamba hili laweza kuonyesha sababu gani nyakati nyingine dawa za kupunguza hamu ya chakula huwa na matokeo katika kupunguza dalili za mtu mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
Kwa vyovyote vile, ni vigumu kwa watafiti kutaja kitu fulani hususa kinachosababisha kujinyima chakula au kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Lakini ni nini kinachoweza kufanywa kusaidia wale wanaong’ang’ana na matatizo haya ya kula?
-
-
Matatizo ya Kula—Ni Nini Kinachoweza Kusaidia?Amkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Matatizo ya Kula—Ni Nini Kinachoweza Kusaidia?
IKIWA binti yako ana tatizo la kula, anahitaji msaada. Usiahirishe mambo ukidhani kwamba tatizo hilo litaisha lenyewe. Tatizo la kula ni ugonjwa ulio tata, unaohusisha mwili na hisia-moyo.
Bila shaka, wataalamu wametoa matibabu mengi yenye kutatanisha kwa matatizo ya kula. Wengine hupendekeza utibabu. Wengine huunga mkono matibabu ya kisaikolojia. Wengine husema kwamba kuunganisha aina zote mbili za matibabu huwa na matokeo zaidi. Kisha kuna mashauri ya familia, ambayo wengine husema ni ya maana hasa ikiwa mwenye tatizo hilo angali anaishi nyumbani.a
Ingawa huenda wataalamu wakatofautiana katika mfikio wao, wengi huafikiana kwa angalau jambo moja: Matatizo ya kula hayahusishi chakula tu. Acheni tuchunguze baadhi ya masuala yenye kina kirefu ambayo hasa yanahitaji kushughulikiwa mtu fulani anaposaidiwa apone kutokana na kujinyima chakula au kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
Maoni Yaliyosawazika juu ya Umbo la Mwili
“Niliacha kununua kabisa magazeti ya mitindo ya mavazi nilipokuwa na umri wa miaka 24 hivi,” asema mwanamke mmoja. “Kujilinganisha na vigezo kulileta madhara makubwa na makali sana.” Kama ilivyozungumziwa tayari, vyombo vya habari vyaweza kupotosha maoni ya msichana kuhusu urembo. Kwa kweli, mama mmoja mwenye binti aliye na tatizo la kula asema juu ya “usambazaji usioisha katika magazeti yetu ya habari na matangazo ya biashara ya televisheni ya kuwa mwembamba, mwembamba, mwembamba.” Yeye asema: “Mimi na binti yangu tunapenda kuwa wembamba, lakini tunahisi mbano wa mambo mengi wa wakati uleule hufanya hangaiko la kuwa mwembamba liwe jambo la maana zaidi maishani, la kutangulizwa.” Kwa wazi, kupona kutokana na matatizo ya kula kwaweza kuhitaji maoni mapya kuhusu kinachohusika katika urembo wa kweli.
Biblia yaweza kusaidia katika habari hii. Mtume Mkristo Petro aliandika: “Msiache urembo wenu uwe ule wa kusuka nywele kwa nje na wa kuvalia madoido ya dhahabu au kuvalia mavazi ya nje, bali acheni uwe yule mtu wa siri wa moyoni katika vao lisilofisidika la roho ya utulivu na ya upole, ambayo ni ya thamani kubwa machoni pa Mungu.”—1 Petro 3:3, 4.
Petro anasema kwamba tunahitaji kuhangaikia zaidi sifa za ndani kuliko sura ya nje. Kwa kweli, Biblia inatuhakikishia: “BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.” (1 Samweli 16:7) Jambo hili hufariji, kwa kuwa ingawa hatuwezi kubadili mambo fulani kuhusu maumbile yetu, sikuzote twaweza kuboresha utu wetu.—Waefeso 4:22-24.
Kwa kuwa matatizo ya kula yanaweza kusitawi katika mazingira ya watu wasiojistahi, huenda ukahitaji kujichunguza tena mwenyewe. Kweli, Biblia hutuambia tusijifikirie wenyewe zaidi kuliko ilivyo lazima kufikiri. (Waroma 12:3) Lakini pia hutuambia kwamba hata shore mmoja ana thamani machoni pa Mungu, ikiongezea: “Nyinyi ni bora zaidi kuliko shore wengi.” (Luka 12:6, 7) Hivyo, Biblia yaweza kukusaidia usitawishe kujistahi kunakofaa. Uthamini mwili wako, na utautunza.—Linganisha Waefeso 5:29.
Lakini vipi ikiwa kwa kweli unahitaji kupunguza uzito? Labda kufuatia miiko fulani ya milo inayofaa na mazoezi yatasaidia. Biblia husema kwamba “mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa,” hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo. (1 Timotheo 4:8) Lakini kamwe usihangaikie kupita kiasi uzito wako. “Labda mwendo wa hekima zaidi,” uchunguzi kuhusu umbo la mwili wafikia mkataa, “ni kufanya mazoezi mengi—na kukubali jinsi ulivyo badala ya kujaribu kujifinyanga ufikie kiwango cha urembo chenye vizuizi visivyo na msingi.” Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 33 nchini Marekani aliona mfikio huu kuwa wenye kusaidia. “Nimekuwa na sheria moja sahili,” yeye asema. “Fanyia kazi jambo unaloweza kubadili kihalisi, na usitumie muda kwa jambo usiloweza kubadili.”
Ukiwa na mtazamo wa maisha unaofaa na kuongezea mwiko unaofaa wa mlo na mazoezi ya kutosha, yaelekea kilogramu zozote unazohitaji kupunguza zitapungua.
Kutafuta “Mwandamani wa Kweli”
Baada ya kufanyia uchunguzi idadi ya watu kadhaa wenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida, Profesa James Pennebaker alifikia mkataa kwamba kwa kiwango kikubwa, utaratibu wao wa kula na kutapika ulikuwa ukiwalazimisha wanawake hao waishi maisha maradufu. Asema: “Karibu kila mtu aliyehojiwa kwa hiari alisema kuhusu wakati na jitihada nyingi mno iliyohitajiwa kuficha marafiki wake wa karibu na familia mazoea yake ya kula. Wote waliishi kwa kudanganya na walichukia jambo hilo.”
Kwa hiyo, hatua itakayotokeza nafuu, ni kuacha kunyamaza. Watu wanaojinyima chakula na wenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida wanahitaji kuzungumza kuhusu tatizo hilo. Lakini kwa nani? Mithali moja ya Biblia husema: “Rafiki [“mwandamani wa kweli,” NW] hupenda sikuzote; na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.” (Mithali 17:17) Huyo ‘mwandamani wa kweli’ aweza kuwa mzazi au mtu mzima mwingine aliyekomaa. Wengine wameona uhitaji wa kumfunulia siri mtu fulani aliye na uzoefu wa kutibu matatizo ya kula.
Mashahidi wa Yehova wana msaada wa ziada—wazee wa kutaniko. Wanaume hawa wanaweza kuwa “kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu.” (Isaya 32:2) Bila shaka, wazee si madaktari, kwa hiyo kwa kuongezea shauri lao huenda bado ukahitaji matibabu. Hata hivyo, wanaume hawa wenye sifa za kiroho wanaweza kuwa msaada mkubwa sana katika kupona kwako.b—Yakobo 5:14, 15.
Hata hivyo, mtu unayeweza kumtumaini zaidi aweza kuwa Muumba wako. Mtunga-zaburi aliandika: “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.” (Zaburi 55:22) Naam, Yehova Mungu anapendezwa na watoto wake wa kidunia. Kwa hiyo usipuuze kamwe kusali kwake kuhusu mahangaiko yako ya ndani. Petro atuonya kwa upole: “Huku mkitupa hangaiko lenu lote juu yake, kwa sababu yeye huwajali nyinyi.”—1 Petro 5:7.
Inapokuwa Lazima Kulazwa Hospitalini
Kulazwa hospitalini kwenyewe si ponyo. Hata hivyo, ikiwa msichana amekosa lishe ya kutosha kwa kukosa sana hamu ya chakula, huenda ikawa lazima apewe utunzaji wa pekee. Kwa kukiri wazi, si rahisi mzazi kuchukua hatua hii. Mfikirie Emily, ambaye binti yake alihitaji kulazwa hospitalini baada ya maisha kuwa, kama asemavyo Emily, “yasiyovumilika kwake na kwetu.” Aongezea hivi: “Kumpeleka hospitalini, akilia, ni jambo lililokuwa gumu zaidi kunipata, ni siku mbaya zaidi ambayo nimepata kuwa nayo.” Hali ya Elaine ilifanana na yake, ambaye pia alilazimika kumlaza hospitalini binti yake. “Nafikiri pindi iliyokuwa mbaya zaidi ninayoweza kukumbuka,” asema, “ni wakati alipokuwa hospitalini na akakataa kula na ikawa lazima wamlishe kwa mipira. Nilihisi kana kwamba wamevunja mapenzi yake.”
Huenda kulazwa hospitalini kusipendeze, lakini katika visa fulani huenda kukahitajika. Kwa idadi kubwa ya watu walio na matatizo ya kula, inasaidia kupona. Emily asema hivi kuhusu binti yake: “Alihitaji kulazwa hospitalini. Alianza kupata nafuu alipolazwa hospitalini.”
Kuishi Bila Matatizo ya Kula
Hatua za kupona zatia ndani kujifunza kuishi bila tatizo la kula kwa mtu asiyekuwa na hamu ya chakula au mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Hili laweza kuwa jambo gumu. Kwa kielelezo, Kim, akadiria kwamba katika awamu yake ya kujinyima chakula, alipoteza kilogramu 18 katika miezi kumi. Lakini, ili apate tena kilogramu 16, ilimchukua muda wa miaka tisa! “Kwa magumu makubwa,” asema Kim, “pole kwa pole nilijifunza kula kwa njia ya kawaida tena, bila kuhesabu kila kalori, kupima chakula, kula vyakula vyenye kalori chache tu, kuwa na wasiwasi ikiwa sikujua kilichomo ndani ya chakula au kitindamlo, au kula chakula cha mchana kwenye mikahawa yenye kuuza saladi mbalimbali.”
Lakini ili Kim apate kupona, mengi zaidi yalihusika. “Nilijifunza kutambua na kuonyesha hisia zangu kwa maneno badala ya matendo au tabia za chakula,” yeye asema. “Kufahamu njia mpya za kukabili na kutatua mahitilafiano pamoja na wengine kulitokeza fursa za uhusiano wa karibu pamoja na marafiki na familia.”
Kwa wazi, ni vigumu kupata nafuu kutokana na tatizo la kula, lakini jitihada zilizofanywa mwishowe zinafaidi. Ndivyo Jean, aliyenukuliwa katika makala ya kwanza ya mfululizo huu, aaminivyo. “Kurudia kula kusiko na utaratibu,” asema, “kungekuwa sawa na kurudi kwenye chumba cha wagonjwa wa akili baada ya kuishi ukiwa huru kwa muda fulani.”
[Maelezo ya Chini]
a Amkeni! haliungi mkono matibabu yoyote hususa. Wakristo wanapaswa kufanya uamuzi wao wenyewe wakihakikisha kwamba matibabu yoyote wanayopata hayahitilafiani na kanuni za Biblia. Wengine hawapaswi kuchambua au kuhukumu maamuzi hayo.
b Kwa habari zaidi kuhusu jinsi ya kusaidia watu wasiokuwa na hamu ya chakula na wenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida, ona makala “Kusaidia Wenye Matatizo ya Kula,” katika toleo la Amkeni! la Februari 22, 1992, la Kiingereza, na mfululizo “Matatizo ya Kula—Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?,” katika toleo la Desemba 22, 1990, la Kiingereza.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Kuweka Msingi wa Kupona
UNAPASWA kufanya nini unaposhuku kwamba binti yako ana tatizo la kula? Bila shaka, huwezi kupuuza hali hiyo. Lakini utaanzishaje mazungumzo hayo? “Nyakati nyingine kumwuliza moja kwa moja hufanya kazi, lakini mara nyingi hutokeza hisia za mfadhaiko kwa sababu ya yeye kukosa kujibu,” asema mwandishi Michael Riera.
Kwa sababu hii, mfikio wenye upole waweza kuwa wenye matokeo zaidi. “Unapozungumza na binti yako,” apendekeza Riera, “anahitaji kuelewa na kuhisi kwamba haumshtaki kwa kosa lolote. Ikiwa unaweza kutokeza hali ya namna hii, vijana wengi watakuwa wanyofu kuzungumza nawe, hata watahisi wametulizwa kwa njia fulani. Wazazi fulani wamefanikiwa kuwaandikia barua vijana wao wakiwaeleza hangaiko na utegemezo wao. Kisha, wanapokuwa na maongezi, tayari msingi unakuwa umewekwa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Ugumu kwa Wazazi
KUWA na mtoto mwenye tatizo la kula hutokeza magumu mengi kwa wazazi. “Lazima mzazi awe thabiti na mwenye kudhamiria ikiwa mtoto atasaidiwa,” asema baba mmoja. “Unamwona mtoto wako akiharibiwa machoni pako.”
Ikiwa una mtoto mwenye tatizo la kula, inatazamiwa tu kwamba nyakati nyingine utafadhaishwa na tabia yake ya ukaidi. Lakini uwe mwenye saburi. Usiache kuonyesha upendo. Emily, ambaye binti yake alikuwa na tatizo la kujinyima chakula, akiri kwamba sikuzote jambo hili halikuwa rahisi. Hata hivyo, asema: “Sikuzote nilijaribu kuendelea kumgusa; nilijaribu kumkumbatia; nilijaribu kumbusu. . . . Nilifikiri ikiwa nitaacha kumwonyesha shauku na kuacha kumwonyesha upendo, hatutakuwa na uhusiano mzuri wa familia tena.”
Mojawapo njia bora ya kusaidia mtoto wako apone kutokana na tatizo la kula ni kuwasiliana naye. Katika kufanya hivyo, huenda ukahitaji kumsikiliza zaidi kuliko kuongea. Na ujizuie usimkatishe kwa kumwambia “Hiyo si kweli” au, “Hupaswi kuhisi namna hiyo.” Kwa kweli, ‘usizibe masikio yako usisikie kilio cha maskini.’ (Mithali 21:13) Kunapokuwa na mazungumzo yaliyo wazi, kijana atakuwa na mahali pa kupata msaada nyakati za taabu na huenda asielekee kuishia kwa mazoea ya kula yasiyofaa.
-