-
Papua New Guinea2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
VOLKANO YAHARIBU RABAUL
Jiji la Rabaul lina bandari kubwa ambayo ni shimo kubwa lililotokezwa na volkano zamani. Mnamo Septemba 1994, matundu yaliyokuwa kwenye pande za bandari hiyo yalilipuka, yakaharibu Rabaul na kubadili maisha ya watu katika jimbo hilo. Jumba la Ufalme na makao ya wamishonari yaliyokuwa kando yake yaliharibiwa, lakini hakuna ndugu yeyote aliyekufa. Hata hivyo, ndugu moja aliyekuwa na matatizo ya moyo alikufa alipokuwa akikimbia mlipuko huo. Akina ndugu wote walienda maeneo yaliyokuwa kilomita kadhaa kutoka eneo hilo kwa kutii maagizo ambayo kwa miaka kadhaa yalikuwa yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo wa Jumba la Ufalme.
Mara moja, ofisi ya tawi ilichukua hatua za kuwasaidia wale waliokuwa wameathiriwa na kuratibu mipango ya kutoa misaada. Nguo, vyandarua vya mbu, dawa, petroli, dizeli, na vitu vingine vilivyotolewa kama mchango vilitumwa, kutia ndani mchele na miyugwa kutoka kutaniko lililokuwa karibu. Kwa kweli, mpango wa kutoa misaada ulifanikiwa sana hivi kwamba wakuu wa serikali wa mahali hapo na watu wengine waliusifu.
Mwishowe, Kutaniko la Rabaul liliacha kuwepo. Siku mbili baada ya mlipuko huo, wahubiri 70 hivi na watoto wao walikusanyika katika shule moja ya ufundi ambayo haikuwa na watu. Wazee walipowasili, wahubiri waliuliza, “Funzo la kitabu litaanza saa ngapi?” Naam, licha ya hali ngumu, ndugu hawakuacha kukutanika na kuhubiri. (Ebr. 10:24, 25) Wengi wa akina ndugu walihamia kwenye vikundi vilivyokuwa karibu, na matokeo yakawa kwamba kikundi kimoja kikawa kutaniko.
Wakuu wa serikali katika jimbo hilo waliahidi dini zote ambazo majengo yao yaliharibiwa kwamba zitapewa uwanja katika mji wa Kokopo ulio kilomita 24 kutoka Rabaul. Hata hivyo, Mashahidi hawakupewa uwanja wowote ilhali dini nyingine zilipewa. Kisha, miaka saba hivi baada ya mlipuko huo, ndugu mmoja kutoka Afrika alianza kufanya kazi katika wizara ya uchoraji ramani ya mji. Alipoona jinsi Mashahidi walivyotendewa isivyo haki, mara moja akawapa uwanja unaofaa huko Kokopo na akawasaidia kujaza fomu ya maombi, ambayo ilikubaliwa. Kikundi cha wajenzi waliojitolea kilisaidia kujenga Jumba la Ufalme na makao ya wamishonari. Kwa kweli, ukosefu wa haki waliofanyiwa hapo awali uligeuka kuwa baraka. Jinsi gani? Uwanja ambao dini zile nyingine zilipewa ulikuwa juu ya mlima. Lakini uwanja ambao Mashahidi walipewa ulikuwa mahali pazuri katikati ya mji.
-
-
Papua New Guinea2011 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 152, 153]
Kushoto: Eneo la Rabaul, volkano Tavurvur ikiwa mbali; chini: Jumba la Ufalme la Rabaul lililoharibiwa mwaka wa 1994
-