Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Paradiso isiyo na taabu—Je, ni Ndoto Tu?
    Amkeni!—1997 | Oktoba 8
    • Paradiso isiyo na taabu—Je, ni Ndoto Tu?

      “KUNA utulivu sana!” Mandhari iliyoonekana kutoka kwenye msitu wa misunobari juu ya Ziwa Redfish katika jimbo la Idaho, Marekani, hakika ilikuwa shwari. “Inafanana tu na jinsi ninavyowazia paradiso kuwa,” huyo msafiri akasema.

      Jua liliangaza pwani ya kusini mwa kisiwa cha Mediterania cha Saiprasi. Mawimbi yalitua kwa uanana ufuoni. Akiwa ameketi katika mkahawa mmoja ulio juu ya genge kuelekea mandhari hiyo ya mbali, huyo mgeni akapaaza sauti akisema: “Hii ni paradiso!”

      Wengi wetu huthamini sana kumbukumbu za mandhari kama hizi. Lakini wakazi hutambua kwamba mazingira ya kiparadiso mara nyingi hufunika uhalisi mgumu wa maisha ya kila siku: mioto ya misitu kwenye miteremko ya Milima ya Rocky, uchafuzi wa bahari unaoathiri samaki na hatimaye wanadamu—kwa kuongezea mapambano yenye kutisha uhai ya kimataifa na ya kijumuiya.

      Paradiso—Hiyo Ni Nini?

      Wewe waionaje paradiso? Kamusi The New Shorter Oxford English Dictionary yasema hivi katika ufafanuzi wake wa kwanza: “Bustani ya Edeni ambayo imefafanuliwa katika Mwa[nzo] 2, 3.” Huo warejezea ufafanuzi ulio katika kitabu cha kwanza cha Biblia kuhusu eneo ambalo Mungu alimweka mwanadamu wa kwanza, Adamu. Katika Paradiso hiyo ya awali, miti ‘inayotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa’ ilisitawi sana.—Mwanzo 2:9.

      Ufafanuzi wa pili wa kamusi hiyo huhusisha “paradiso” na “Mbingu, katika theolojia ya Kikristo na ya Kiislamu” lakini kisha inaongezea: “Sasa hasa ni ya [ki]shairi.” Hata hivyo, kwa msafiri wetu na mgeni anayezuru, paradiso ilikuwa “eneo la uzuri au upendezi usio na kifani,” ambao ni ufafanuzi wa tatu wa ile kamusi.

      Mkuu wa serikali ya Uingereza wa karne ya 16, Sir Thomas More, aliandika kitabu chenye kichwa Utopia ambamo ndani yake alifafanua nchi ya kuwaziwa ambamo sheria, serikali, na hali za kijamii zilikuwa kamilifu. Ufafanuzi wake haukuwa halisi hivi kwamba leo kamusi Webster’s New Collegiate Dictionary hutoa ufafanuzi mmoja kwa neno “Utopia” kuwa “mpango usioweza kutumika wa kufanya maendeleo ya kijamii.”

      Kwa wafuasi wa kiongozi wa madhehebu ya People’s Temple aliyeitwa Jim Jones, Utopia ilikuwa mahali fulani palipo wazi katika msitu wa Guyana. Kwa kusikitisha, katika 1978 paradiso hiyo iliyotumainiwa ikawa mahali pa vifo vya zaidi ya watu 900 kati yao—ogofyo kwelikweli! Tokeo likawa kwamba nyakati nyingine watu huhusisha wazo la paradiso na madhehebu ya ajabu-ajabu yenye mazoea ya kushtusha na kusumbua.

      Katika ulimwengu ambamo uhalifu na ujeuri hutisha, ambamo maradhi hutisha watu wazima kwa watoto, na ambamo tofauti za kidini hugawanya jumuiya, mazingira maridadi mara nyingi hufunika uhalisi wa hali. Si ajabu kwamba watu hufikiri paradiso kuwa ndoto tu! Lakini jambo hili halijakomesha wengine wasijaribu kutafuta au hata kujifanyizia paradiso yao wenyewe. Wao wamefanikiwa kadiri gani?

  • Kutafuta Paradiso Isiyo na Taabu
    Amkeni!—1997 | Oktoba 8
    • Kutafuta Paradiso Isiyo na Taabu

      “KILE tu tunachotaka ni kufanyiza mtindo wa maisha ulio salama na labda wa kikale ambamo watu wanajali kila mmoja na mwenzake,” wakaeleza wenzi fulani wa ndoa Waingereza. Waliamua kutafuta paradiso moja ya kisiwa cha kitropiki na kuanzisha huko jumuiya ambayo ingeishi pamoja kwa amani. Bila shaka unaweza kuelewa hisia zao. Ni nani asingekubali mara moja toleo la kuishi katika paradiso isiyo na taabu?

      Je, Suluhisho Ni Kujitenga?

      Wazo la kuishi kisiwani huvutia watafutaji wengi wa paradiso, kwa kuwa kujitenga huwaandalia usalama wa kadiri fulani. Wengine huchagua visiwa vilivyo karibu na Pwani ya Pasifiki ya Panama au visiwa vilivyo katika Karibea, kama vile vilivyo karibu na Belize. Wengine hugeuzia uangalifu wao sehemu zenye kuvutia za Bahari ya Hindi—kwa kielelezo, Shelisheli.

      Ni vigumu sana kuwazia hatua za kufuata ili kufanyiza jumuiya iliyojitenga. Hata kama kuna pesa za kutosha, sheria zilizopo za serikali zaweza kuzuia kununuliwa kwa ardhi upesi. Lakini, tuseme kisiwa kifaacho cha kitropiki kinaweza kupatikana, je ungefurahi kuwa huko? Je, paradiso yako haingekuwa na taabu?

      Visiwa vilivyojitenga vilivyo karibu na pwani ya Uingereza sasa vinaongezeka watu. Wakazi wake wapya hasa ni watu ambao wanatafuta faragha na amani. Mtu mmoja aishiye peke yake katika kisiwa cha Eorsa chenye eka 250, karibu na pwani ya magharibi ya Scotland, adai kwamba hahisi upweke kamwe kwa sababu ana kazi nyingi sana za kuwatunza kondoo zake mia moja. Wengine ambao wamejitenga kisiwani upesi huhisi upweke. Yaripotiwa kwamba wengine wamejaribu kujiua na walihitaji kuokolewa.

      Watu wengi huamini kwamba kisiwa kidogo cha kitropiki chenye kuvutia kingekuwa paradiso. Kuishi katika hali yenye tabia ya nchi yenye uanana na isiyo yenye kuvuka mipaka sana huwavutia. Lakini hangaiko juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa joto duniani na kufuatiwa na kuinuka kwa kiwango cha bahari limesababisha hofu miongoni mwa wakazi wengi wa visiwa. Wakaaji wa visiwa vya matumbawe visivyo na kimo na ambavyo hufanyiza eneo la Tokelau katika Pasifiki ya Magharibi na vilevile wakaaji wa vile visiwa vya Maldives vilivyotawanyika katika Bahari ya Hindi na ambavyo havijainuka zaidi ya meta 2 juu ya usawa wa bahari wakati wa kujaa kwa maji wanahisi wametishwa vilevile.

      Karibu serikali 40 tofauti-tofauti zimejiunga pamoja katika shirikisho la Mataifa Yenye Kuendelea ya Visiwa Vidogo ili kutafuta msaada kwa hali yao. Ingawa kwa ujumla wakaaji wa visiwa vidogo wana tarajio la kuishi muda mrefu nao wana vifo vichache vya watoto, wao huendelea kukabili matatizo mazito ya mazingira. Tabaka za mafuta na bahari zilizotiwa uchafu hudhoofisha uchumi wa visiwa fulani. Visiwa vingine huwa mahali pa kutupia takataka zenye sumu ambazo mataifa makubwa yanataka kutupa.

      Hata kutamanika kwenyewe kwa visiwa hivyo kuwa mahali pa watafuta-paradiso hutokeza tisho. Jinsi gani? Watalii ambao humiminikia fuo zenye jua za visiwa hivyo hutokeza msongamano mkubwa sana na kupunguka kwa maliasili iliyo kidogo. Watu hao wenye kuzuru pia huongezea tatizo la uchafuzi. Kwa kielelezo, katika Karibea, ni sehemu moja kwa kumi tu za takataka zitokezwazo na wenye kuzuru milioni 20 kila mwaka ambazo hutiwa dawa kabla ya kuondolewa.

      Jambo kama hilo hutukia katika sehemu nyinginezo zenye kuvutia. Fikiria kielelezo cha Goa kwenye pwani ya magharibi ya India. “Utalii mwingi ‘unaharibu paradiso,’” likatangaza gazeti The Independent on Sunday la London. Makadirio rasmi yaonyesha kwamba watalii wameongezeka kutoka 10,000 katika mwaka wa 1972 hadi zaidi ya milioni moja katika miaka ya mapema ya 1990. Kikundi kimoja chaonya kwamba ikolojia dhaifu ya Goa na utamaduni wake wa kipekee inatishwa na pupa ya wenye hoteli wanaotamani kuchuma donge nono kutokana na mmiminiko wa watalii. Ripoti ya serikali ya India inathibitisha kwamba baadhi ya hoteli zimechipuka kwenye ufuo kinyume cha sheria. Mchanga umechimbwa, miti ikakatwa, na chungu za mchanga zimelainishwa. Takataka hutupwa kwenye ufuo au huvuja na kuingia katika mashamba yaliyo karibu ya mpunga, zikieneza uchafuzi.

      Je, Sehemu Hizo Hazina Uhalifu?

      Ongezeko la uhalifu linaharibu sifa ya hata maeneo yenye amani zaidi. Kutoka kisiwa kidogo cha Karibea kiitwacho Barbuda yaja ripoti yenye kichwa “Machinjo Katika Paradiso.” Ripoti hiyo ilitaja kindani mauaji ya kimakusudi ya watu wanne waliokuwa katika mashua ya anasa ambayo ilikuwa imetia nanga karibu na pwani ya kisiwa hicho. Visa kama hivi huongeza hangaiko juu ya kuenea kwa uhalifu kotekote katika hilo eneo.

      “Dawa za Kulevya Zazusha Vita vya Magenge Katika ‘Paradiso’” ikasema katika kichwa kikuu ripoti moja katika gazeti The Sunday Times la London kuhusu nchi moja ya Amerika ya Kati. Mhariri mmoja wa huko alilalamika kwamba amani ilikuwa imetoweka, akieleza: “Sasa ni kawaida kuamka asubuhi na kupata kijana mwenye umri wa miaka 16 akiwa amelala katika damu barabarani.”

      Wale wanaotaka kuishi katika paradiso ya jumuiya hutumaini kuvutia watu ambao watakubali kuishi kwa amani. Lakini uhalisi wa mambo ukoje? Kutofautiana kulizuka upesi katika kisa cha wale wenzi Waingereza waliotajwa mwanzoni. Baadhi ya waliopeleka maombi ya kujiunga na mradi wao kwa wazi walitaka kuchuma pesa kutokana na mpango huo. “Sisi hatutaki viongozi,” akatangaza mwendelezaji huyo. “Wazo ni kuchanga mali zetu na kuhakikisha kwamba mambo yetu yanaendelea sawa. Naiita jumuiya ya Utopia.” Huu si mradi wa kwanza kamwe.—Ona sanduku “Majaribio ya Jumuiya za Paradiso.”

      Watafuta-paradiso wengine huamini kwamba wao watatimiza mradi wao kwa kushinda mchezo wa bahati-nasibu. Lakini fedha zipatikanazo kwa njia hii mara nyingi hazileti furaha. Mnamo Februari 1995, gazeti The Sunday Times liliripoti kwamba familia ya mshindi wa bahati-nasibu iliyo kubwa zaidi nchini Uingereza kufikia sasa ilikuwa na mapigano makali; kushinda hakukuwaletea lolote ila “uchungu, ugomvi na kukata tamaa.” Hii ni kawaida katika hali hizo.

      Katika uchunguzi juu ya utafutaji wa mwanadamu wa Utopia, mwandishi wa magazeti Bernard Levin aeleza juu ya “ndoto ya kupata mali mara moja,” na kusisitiza: “Kama ilivyo na ndoto nyingi, ogofyo halipo mbali sana. Kuna habari nyingi mno zilizothibitishwa za kupata mali mara moja ambazo ziliongoza kwenye misiba mibaya sana (kutia ndani ujiuaji) hivi kwamba haziwezi kuwa sadfa tu.”

      Vipi Juu ya Mafarakano ya Hukumu?

      Mipango mingine kuhusu paradiso imeonekana kuwa hata mibaya zaidi. Likiripoti juu ya polisi kuzingira ua wa Branch Davidians kule Waco, Texas, huko nyuma katika 1993, gazeti fulani la habari lilisema juu ya “mchanganyiko hatari wa bunduki, mbinu za kudhibiti akili na nabii wa hukumu” aliyetokeza msiba huo. Kwa kusikitisha, hiki si kisa cha kipekee.

      Wafuasi wa Bhagwan Shree Rajneesh aliyekufa na ambaye alikuwa kiongozi wa kiroho Mhindi, walianzisha jumuiya katika Oregon lakini baadaye waliudhi maadili ya majirani zao. Utajiri wa kiongozi wao na majaribio ya kingono waliyoyafanya yaliharibu madai yao kwamba wamepata “himaya nzuri.”

      Madhehebu mengi yenye kuongozwa na watu wenye matumaini ya paradiso husisitiza kwamba wafuasi wao wafuate desturi fulani za ajabu, ambazo nyakati nyingine hutokeza mapambano yenye jeuri. Mwandikaji wa makala za gazeti la habari Ian Brodie aeleza hivi: “Madhehebu hutoa himaya na jamii iliyopangwa kwa uthabiti kwa wale wanaohisi wanaishi kwa upweke au ambao hawawezi kukabiliana na mikazo ya ulimwengu halisi.” Hata hivyo, maneno yake huthibitisha uhakika wa kwamba watu wengi wangependa kuishi katika paradiso.

      Paradiso Isiyo na Taabu

      Orodha ya taabu yaonekana kana kamba haina mwisho: uchafuzi, uhalifu, matumizi mabaya ya dawa, msongamano, mapambano ya kikabila, msukosuko wa kisiasa—bila kutaja taabu zilizo kawaida kwa wanadamu wote, maradhi na kifo. Ni lazima tufikie mkataa kwamba hakuna popote katika sayari hii ambapo pana paradiso ambayo haina taabu kabisa. Kama Bernard Levin anavyokiri: “Rekodi ya mwanadamu ni mbaya, na inaonekana imekuwa mbaya kwa muda ambao mwanadamu amekuwapo. Rekodi hiyo mbaya ipo kwa sababu watu hawawezi kuishi kwa furaha wakiwa karibu-karibu na wanadamu wengine wachache sana.”

      Hata hivyo, kutakuwa na paradiso ya tufeni pote ambayo kwa kweli haitakuwa na taabu. Kudumu kwa paradiso hiyo kumehakikishwa na nguvu izidiyo ile ya kibinadamu. Hakika, zaidi ya watu milioni tano hata sasa wanajitahidi kufikia lengo hilo, nao tayari wanafurahia miongoni mwao muungano wenye thamani na mazingira yasiyo na taabu kwa kulinganisha. Unaweza kuwapata wapi? Unaweza kushirikije tumaini ilo hilo na manufaa ambazo wanafurahia sasa? Na Paradiso hiyo inayokuja itadumu kwa muda gani?

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Majaribio ya Jumuiya za Paradiso

      Mapema katika karne ya 19, msoshalisti wa Ufaransa Étienne Cabet (1788-1856) na washiriki wake 280 walianzisha makazi ya jumuiya katika Nauvoo, Illinois, ili waishi kwa kutegemea mawazo yake. Lakini kwa muda wa miaka minane mgawanyiko mkubwa ulitokea katika jumuiya hiyo hivi kwamba upesi ikavunjika, kama ilivyokuwa kwa vikundi kama hivyo katika Iowa na California.

      Mfaransa mwingine, Charles Fourier (1772-1837), alisitawisha mawazo kwa ajili ya jumuiya yenye kushirikiana kwa kilimo huku washiriki wake wote wakibadilishana wajibu. Kila mtu alipaswa kupokea malipo kwa kutegemea mafanikio ya kikundi chote kizima. Lakini jumuiya kama hizo katika Ufaransa na Marekani hazikudumu.

      Karibu na wakati huo, mrekebishaji wa mambo ya kijamii wa Wales aliyeitwa Robert Owen (1771-1858) alipendekeza kuwe na vijiji vyenye kushirikiana ambamo mamia ya watu wangeishi pamoja wakiwa na jiko na maeneo ya kula ya jumuiya yote. Kila familia ingeishi katika nyumba yao yenyewe na kuwashughulikia watoto wao mpaka wafikie umri wa miaka mitatu. Baada ya hapo utunzaji wa watoto ungechukuliwa na jumuiya yote. Lakini majaribio ya Owen yalishindwa, naye alipoteza kiasi kikubwa cha mali zake binafsi.

      John Noyes (1811-1886) akaja kuwa mwanzilishi wa kile ambacho The New Encyclopædia Britannica chakiita “jumuiya yenye mafanikio zaidi kati ya jumuiya za kisoshalisti za utopia Marekani.” Wafuasi wake walipoacha ndoa za mke mmoja na kuruhusu kufanya ngono miongoni mwa wote maadamu wamekubaliana, Noyes alikamatwa kwa mashtaka ya uzinzi.

      Laissez Faire City, ambalo ni aina ya “Utopia ya kibepari” katika Amerika ya Kati, ni jaribio la hivi karibuni la kufanyiza jumuiya ya Utopia, laripoti gazeti The Sunday Times la London. Mradi huo ulitafuta waweka-rasilimali. Wakivutwa na tazamio la kuishi katika “jiji la muujiza la karne ya 21,” watafuta-paradiso walialikwa wapeleke dola 5,000 na kujiunga na mfumo fulani wa uuzaji, wakitafuta watu kama wao ambao nao wataweka rasilimali za pesa zao. Inaripotiwa kwamba jumla hiyo yote ya pesa inatoshea tu kulipia tikiti ya ndege ya kuona mradi huo “iwapo nchi hiyo inaweza kushawishika ikubali mradi huo ujengwe, na hoteli ndogo ijengwe huko,” likaeleza gazeti hilo la habari. Hakuna tumaini halisi la kuanzishwa kwa “paradiso” yoyote huko.

  • Paradiso Isiyo na Taabu—Karibuni Itakuwa Halisi
    Amkeni!—1997 | Oktoba 8
    • Paradiso Isiyo na Taabu—Karibuni Itakuwa Halisi

      “UTAKUWA pamoja na mimi katika Paradiso.” Maneno hayo yalimtumainisha kama nini huyo mtu aliyekuwa na historia ya uhalifu! La, si kwamba alihisi angeponea helo yenye kuwaka moto na kwenda mbinguni wakati afapo. Badala ya hivyo, huyo mwizi aliyekuwa kando ya Yesu alifarijika kutokana na tumaini la kwamba angefufuliwa kwenye uhai wakati ambapo Paradiso ingerudishwa katika sayari hii. Tafadhali, ona ni nani aliyeitoa taarifa hiyo yenye kutokeza juu ya Paradiso—Mwana wa Mungu mwenyewe, Yesu Kristo.—Luka 23:43.

      Ni nini lililozusha ahadi ya Kristo ya Paradiso? Yule mwizi alikuwa ameomba: “Nikumbuke mimi uingiapo katika ufalme wako.” (Luka 23:42) Ufalme huu ni nini, na kuna uhusiano gani kati yake na paradiso ya kidunia? Na huo unahakikishaje kwamba hiyo Paradiso haitakuwa na taabu?

      Nguvu Itakayoleta Paradiso

      Utakubali kwamba paradiso ya kweli inaweza tu kuja duniani wakati ambapo taabu zote za siku hizi zimetoweka. Kufikia wakati huu jitihada za wanadamu za kuondoa taabu zimeambulia patupu, kama ambavyo historia yashuhudia vizuri. Nabii Mwebrania Yeremia alikiri hivi: “Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Basi, ni nani awezaye kuondoa kabisa taabu zote za siku hizi?

      Halihewa Zenye Kupita Kiasi na Uchafuzi. Dhoruba kali ya upepo katika Bahari ya Galilaya ilipokuwa ikipeleka mawimbi makubwa yenye uwezo wa kuvunja meli, mabaharia walimwamsha mwandamani wao safarini kutoka usingizini. Naye akaiambia tu bahari: “Usu! Nyamaa!” Simulizi la Gospeli la Marko laeleza lililotukia: “Upepo ukapunguka, kukawa shwari kubwa.” (Marko 4:39) Mwandamani huyo safarini hakuwa mwingine ila Yesu. Yeye alikuwa na nguvu za kudhibiti halihewa.

      Ni Yesu uyo huyo aliyetabiri kupitia mtume Yohana kwamba wakati ungekuja ambapo ‘Mungu angewaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.’ (Ufunuo 1:1; 11:18) Hili si jambo lisilowezekana kwa Yule ambaye aliondoa ulimwengu mzima wa watu wasiomcha Mungu katika Furiko la siku ya Noa.—2 Petro 3:5, 6.

      Uhalifu na Ujeuri. Biblia yaahidi: “Watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.” (Zaburi 37:9, 11) Tena, ni Mungu, Yehova, aahidiye kuondoa uhalifu na ujeuri wote, akihifadhi Paradiso kwa wenye upole.

      Umaskini na Njaa. Ukosefu wa haki wa siku hizi huzifanya serikali katika eneo moja la ulimwengu kurundika “milima” ya vyakula vya ziada na kwa wakati uo huo nchi zilizo maskini ziking’ang’ana na umaskini. Mashirika ya kutoa kitulizo, yakiungwa mkono na watu wenye kuhangaika ulimwenguni pote, hujaribu kuandaa mahitaji ya msingi lakini mara nyingi wao hushindwa wakati mipango ya ugawanyaji inapotibuka kwa sababu ya ukosefu wa kudumisha sheria na utengamano. Tofautisha hali hiyo na yale yaliyorekodiwa na nabii Isaya: “Katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.” (Isaya 25:6) Je, hiyo haionyeshi kwamba njaa kuu na njaa haitakuwapo tena? Bila shaka.

      Vita. Majaribio ya kutawala tufe hili kupitia mamlaka ya mataifa yote hayakufua dafu. Ule Ushirika wa Mataifa ulioanzishwa mwaka wa 1920, ulishindwa kuzuia kuzuka kwa Vita ya Ulimwengu ya Pili nao ukaanguka pu! Umoja wa Mataifa, ambao mara nyingi umesifiwa kuwa tumaini bora zaidi la kupata amani, hung’ang’ana kuamua pande zenye kupigana katika maeneo ya mapambano. Japo jitihada zake za kutafuta amani ambazo zimetangazwa sana, vita zimejaa tele, ziwe ni za wenyewe kwa wenyewe, za kikabila, au za kijumuiya. Serikali ya Ufalme wa Mungu yaahidi kuondoa makundi yenye kupigana siku hizi na kuelimisha raia zake kufuatia njia za amani.—Isaya 2:2-4; Danieli 2:44.

      Mvunjiko wa Familia na wa Maadili. Kuvunjika kwa familia kumeenea. Uhalifu wa watoto umejaa. Ukosefu wa maadili umesambaa katika matabaka yote ya jamii ya kibinadamu. Lakini, viwango vya Mungu vimedumu bila kubadilishwa tangu mwanzo. Yesu alitoa ushuhuda kwamba “mtu ataacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja . . . Kwa hiyo, kile ambacho Mungu amefunga nira pamoja msiache mtu yeyote akitenganishe.” (Mathayo 19:5, 6) Yehova Mungu akaamuru zaidi: “Heshimu baba yako na mama yako . . . ili ipate kuwa vema kwako nawe upate kudumu muda mrefu juu ya dunia.” (Waefeso 6:2, 3) Viwango kama hivyo vitaenea katika dunia itakayokuwa chini ya Ufalme wa Mungu.

      Ugonjwa na Kifo. “BWANA . . . ndiye atakayetuokoa,” akaahidi nabii Isaya, “wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:22, 24) “Mshahara ambao dhambi hulipa ni kifo,” akakiri mtume Mkristo Paulo, “lakini zawadi ambayo Mungu hutoa ni uhai udumuo milele kwa njia ya Kristo Yesu.”—Waroma 6:23.

      Yehova Mungu ataondoa taabu hizi zote kupitia serikali yake ya kimbingu iliyo mikononi mwa Mwana wake, Kristo Yesu. Lakini, huenda ukasema, ‘Ufafanuzi huu ni kama ndoto tu ya Utopia. Kwa hakika ungefurahisha kama ungekuwa hivyo, lakini je, ndivyo utakavyokuwa?’

      Uhalisi wa Wakati Huu

      Kwa watu wengi, uwezekano wa kuishi katika paradiso isiyo na taabu hapahapa duniani waonekana kuwa tazamio lisilowezekana. Ikiwa ndivyo unavyohisi, chunguza ithibati inayothibitisha kwamba kwa kweli hili litatukia.

      Mashahidi wa Yehova ni jumuiya ya kimataifa ya siku hizi yenye zaidi ya watu milioni tano ambao tayari kwa kadiri fulani wana mazingira yasiyo na taabu katika makutaniko yao 82,000 ambayo yameenea kotekote katika nchi 233. Unaweza kuzuru wowote wa mikusanyiko yao, mikubwa kwa midogo, na utapata nini?

      (1) Mazingira Safi na Yenye Kupendeza. Akieleza juu ya mkusanyiko mmoja wa Mashahidi wa Yehova kule Norwich, Uingereza, meneja wa stediamu ya mchezo wa mpira wa mguu alisema: “Mazingira yenye amani katika hizo siku nne . . . yanavutia sana. Mna utulivu wa binafsi ambao hutofautiana sana na ule wa siku nyinginezo zozote nne katika ulimwengu wa biashara wenye mkazo na maisha ya kila siku yanayotuzingira. Kwa kweli Mashahidi wana jambo fulani ambalo ni tofauti na lililo gumu kueleza.”

      Mshauri mmoja wa mazoezi ya mambo ya ujenzi ambaye alizuru ofisi za London za Mashahidi wa Yehova alisema: “Nilivutiwa sana na yale niliyoona na kusikia nami nilishangaa sana kwa mazingira yenye amani kabisa na utulivu ambazo ziko si katika majengo yenu tu bali pia miongoni mwa [wanaume na wanawake]. Nahisi kwamba njia yenu ya maisha na furaha ina mengi ya kufundisha ulimwengu huu wote ulio na taabu.”

      (2) Usalama na Amani. Mwandikaji wa makala za gazeti Journal de Montréal katika Kanada aliandika: “Mimi si Shahidi. Lakini mimi nimeshuhudia jambo la kwamba Mashahidi hushuhudia ubora na mwenendo ufaao. . . . Ikiwa ni wao pekee wangekuwa ulimwenguni, hatungehitaji kuifunga milango yetu usiku na kuweka king’ora cha kuzuia wezi.”

      (3) Uaminifu-Mshikamanifu kwa serikali ya Ufalme wa Mungu hutambulisha Mashahidi. Msimamo wao wa kutokuwamo huwaudhi wengine, ingawa haipasi kuwa hivyo. Kutokuwamo kwao katika mipango ya siku hizi ya kisiasa iliyo dhaifu hakutokani na kukataa kwao kutaka kuboresha jamii. Badala ya hivyo, wao hujaribu kutenda kwa njia ambayo hupendeza yule ambaye anatawala kupitia serikali ya kimbingu, yaani, Muumba wa dunia, Yehova Mungu.

      Itikadi za Mashahidi, zikitegemea kabisa Neno la Mungu, Biblia, huwazuia wasiangukie mtego wa kuwa farakano au madhehebu. Wao hupendezwa kwa fadhili na watu wengine wote, hata wawe wa dini gani. La, wao hawajaribu kuwalazimisha watu hao wabadili maoni yao. Wao hujaribu kumwiga Kiongozi wao, Kristo Yesu, kwa kutoa uthibitisho wa Kimaandiko juu ya Paradiso isiyo na taabu ambayo itaanzishwa karibuni hapa duniani.—Mathayo 28:19, 20; 1 Petro 2:21.

      (4) Afya ya Kiroho na Furaha. Kwa uhalisi, Mashahidi wa Yehova hawadai kuwa hawana taabu kabisa wakati huu. Hili haliwezekani miongoni mwa watu ambao wamerithi dhambi kutoka kwa Adamu. Lakini kwa msaada wa roho takatifu ya Mungu, wao hujitahidi kusitawisha sifa za binafsi kama vile “upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujidhibiti.” (Wagalatia 5:22, 23) Ni ibada yao kwa Yehova kupitia Kristo Yesu ambayo huwaunganisha na kudumisha matumaini yao.

      Twatumaini kwamba kuzuru mahali pa kwenu ambapo Mashahidi hukutania kutakusadikisha kwamba Mungu atageuza dunia kuwa paradiso halisi.

      Taabu za siku hizi zitakoma. Hata kutokamilika kunakoendelea kutapotea polepole wakati manufaa za dhabihu ya fidia ya Kristo zinapotumiwa kwa wanadamu watiifu. Ndiyo, unaweza kupata afya kamili na furaha.

      Matayarisho sahili yatakusaidia kufurahia tazamio kama hilo. Omba Mashahidi wakupe nakala yako binafsi ya kitabu Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele.a Ukiwa nacho, kwa muda mfupi unaweza kujifunza jambo ambalo Mungu anataka ufanye ili wewe pia uweze kufurahia milele maisha katika paradiso isiyo na taabu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki