Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Upendo Wetu kwa Bustani
    Amkeni!—1997 | Aprili 8
    • Upendo Wetu kwa Bustani

      JE, WEWE hufurahia utulivu wa bustani maridadi ukiwa kimbilio kutoka kwa kelele na hekaheka za maisha? Je, bustani tulivu zenye nyua, maua, miti yenye vivuli, na vidimbwi ndizo mazingira ambayo wewe hupendelea kufanyia mandari na familia yako au kutembea-tembea na rafiki yako? Ndiyo, bustani ni yenye kutuliza, kuburudisha, starehefu, na hata yenye kuponya kama nini!

      Ingawa huenda wengine wasipendelee kutunza bustani, labda kwa kukosa wakati, sisi sote hufurahia sana rangi, manukato, kelele, na matunda ya bustani. Thomas Jefferson—ambaye alikuwa msanifuujenzi, mwanasayansi, wakili, mvumbuzi na pia rais wa Marekani—alipenda bustani. Aliandika: “Hakuna kazi inayonipendeza sana kuliko kutunza dunia. . . . Bado nimejitoa kutunza bustani. Na ingawa mimi ni mzee kwa umri, mimi ni mtunza-bustani kijana.”

      Watu wengi wana maoni kama yake. Kila mwaka mamilioni ya wageni humiminikia bustani maarufu za ulimwengu—Bustani za Kew (zile Royal Botanic Gardens), Uingereza; bustani zilizo Kyoto, Japani; bustani za Makao ya Kifalme ya Versailles, Ufaransa; Bustani za Longwood, Pennsylvania, Marekani, tukitaja chache tu. Nchi nyingi pia zina maeneo ya majiji ambamo nyumba, zikiwa kandokando za barabara zenye miti, zimezingirwa na vichaka, miti, na maua yenye rangi nyingi sana—kama paradiso ndogo.

      Bustani Zaweza Kuendeleza Afya Nzuri

      Imeonekana kwamba wanadamu wanapochangamana na ulimwengu wa mambo ya asili, afya zao zaweza kuboreka, ingawa kuchangamana ni kuona tu maua, miti, vichaka, na ndege dirishani. Jambo hilo lilifanya hospitali moja ya New York City kupanda bustani kwenye paa yayo. “Ilipokewa kwa shangwe,” asema ofisa mmoja wa hospitali hiyo. “Hiyo imechochea sana wagonjwa na wafanyakazi. . . . Tunaona kwamba itasaidia sana kiafya.” Kwa kweli, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba watu wanaweza kunufaika kimwili, kiakili, na kihisia-moyo kwa kutumia hisi zao kwenye mambo ya asili.

      Isitoshe, mtu ambaye ana mtazamo wa kiroho huenda akahisi kuwa karibu zaidi na Mungu akiwa katikati ya uumbaji Wake. Jambo hilo kuhusu bustani laweza kufuatiliwa hadi nyuma kwenye bustani ya kwanza kabisa duniani, Bustani ya Edeni, ambako Mungu aliwasiliana na binadamu kwa mara ya kwanza.—Mwanzo 2:15-17; 3:8.

      Bustani inapendwa kotekote duniani. Na kama tutakavyoona jambo hilo ni la maana. Kabla ya kuzungumzia jambo hilo, twakualika “kutembea” kwenye bustani chache za kihistoria ili uone jinsi watu wanavyotamani sana Paradiso.

  • Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu
    Amkeni!—1997 | Aprili 8
    • Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu

      MAONO ya mwanadamu na Paradiso yalianza katika bustani iliyo katika eneo lililoitwa Edeni, labda karibu na Ziwa Van, la Uturuki ya kisasa. Mto uliogawanyika na kufanyiza mito minne ilitilia maji bustani hiyo kwa ajili ya Adamu na Hawa, ambao walipaswa ‘kuilima na kuitunza.’ Ingependeza kama nini kutunza bustani iliyojaa “kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa”!—Mwanzo 2:8-15.

      Edeni ilikuwa makao makamilifu. Adamu na Hawa na wazao wao walipaswa kueneza mipaka yayo, bila shaka wakitumia ubuni wa awali wa Mungu ulio maridadi sana kuwa kigezo cha kufuata. Baada ya muda, dunia yote ingekuwa paradiso iliyojaa vizuri watu. Lakini kutotii kimakusudi kwa wazazi wetu wa kwanza kulifanya waondoshwe kwenye himaya hiyo. Kwa kuhuzunisha, wengine wote wa familia ya kibinadamu walizaliwa nje ya makao hayo ya Edeni.

      Hata hivyo, mwanadamu aliumbwa na Muumba aishi katika Paradiso. Basi ni kawaida kwamba vizazi vya wakati ujao vingejizingira na miigo ya Paradiso.

      Bustani za Mapema

      Bustani za Juu za Babiloni zimesifiwa kuwa mojawapo ya maajabu ya ulimwengu wa kale. Hizo zilijengwa na Mfalme Nebukadreza zaidi ya miaka 2,500 iliyopita kwa ajili ya mke wake Mmedi aliyetamani misitu na milima ya kwao. Ujenzi huo wa kimo cha meta 22 wenye ngazi, kuba zilizopinda, zote zikiwa zimepandwa mimea sana, ulikuwa na mchanga wa kutosha kukuza miti mikubwa. Malkia huyo aliyetamani kwao alielekea kufarijika alipotembea-tembea katika eneo hilo lililofanana na Edeni.

      Utengenezaji wa mandhari ulitia fora katika Bonde la Naili lenye rutuba katika Misri. “Misri,” chasema The Oxford Companion to Gardens, “ndiyo chanzo cha picha za kale zaidi za bustani na pia mahali penye desturi ya muda mrefu sana . . . ya utunzaji wa bustani.” Plani ya mandhari ya bustani ya ofisa mmoja wa Misri katika Thebes, ambayo ni ya karibu 1400 K.W.K., yaonyesha vidimbwi, barabara zenye miti kandokando, na vibanda. Mbali na bustani za kifalme, bustani za hekalu ndizo zilizokuwa na mimea zaidi, zikiwa na miti, maua, na mimea midogo ambayo ilinyunyiziwa maji kupitia mifereji kutoka kwenye vidimbwi na maziwa yaliyojaa ndege wa majini, samaki, na lili-loto.—Linganisha Kutoka 7:19.

      Waajemi pia walikuwa watunza-bustani stadi wa awali. Bustani za Uajemi na Misri zilikuwa zenye kuvutia sana hivi kwamba wakati majeshi ya Aleksanda Mkubwa yenye ushindi yaliporudi kutoka Ugiriki katika karne ya nne K.W.K., hayo yalikuja kama yamejaza mbegu, mimea, na mawazo mapya. Katika Athene, Aristotle na mwanafunzi wake Theophrastus walikusanya mimea hiyo yenye kuongezeka na kuanzisha bustani ya mimea, ili kuchunguza na kuainisha mimea. Matajiri wengi wa Ugiriki, kama ilivyo na Wamisri na Waamedi kabla ya wao, walikuwa na bustani maridhawa.

      Wakazi wa jiji la Roma walichanganyisha makao na bustani katika nafasi ndogo ya jijini. Matajiri waliunda bustani za raha katika nyumba zao za mashambani. Hata Nero mkatili alitaka Edeni yake, kwa hiyo kwa ukatili alihamisha kwa nguvu mamia ya familia, akaharibu nyumba zao, na kutengeneza bustani yake ya zaidi ya hektari 50 kuzingira makao yake ya kifalme. Baadaye, karibu na mwaka wa 138 W.K., kwenye nyumba ya Maliki Hadrian katika Tivoli, utengenezaji wa mandhari katika Roma ukafikia upeo. Nyumba hiyo ilikuwa na hektari 243 za bustani, vidimbwi, maziwa, na mabomba ya kububujisha maji.

      Waisraeli wa kale pia walikuwa na bustani. Mwanahistoria Myahudi Josephus aandika kuhusu bustani zenye kujaa vijito katika mahali paitwapo Etam, kilometa 13 hadi 16 hivi kutoka Yerusalemu. Bustani za Etam huenda zilikuwa miongoni mwa ‘bustani, viunga, birika za maji na mwitu’ ambazo Biblia yasema Solomoni ‘alijifanyizia.’ (Mhubiri 2:5, 6) Nje tu kidogo ya Yerusalemu kwenye Mlima wa Mizeituni kulikuwa na Bustani ya Gethsemane, iliyofanywa mashuhuri na Yesu Kristo. Hapo, Yesu alipata mahali ambapo angeweza kufundisha wanafunzi wake.—Mathayo 26:36; Yohana 18:1, 2.

      Tokea Bustani za Waarabu Hadi Bustani za Waingereza

      Majeshi ya Waarabu yalipoenea mashariki na magharibi katika karne ya saba W.K., hayo, kama Aleksanda, yaliona bustani za Uajemi. (Linganisha Esta 1:5.) “Waarabu,” aandika Howard Loxton, “walipata kwamba bustani za Waajemi zilifanana sana na paradiso iliyoahidiwa katika Qurani.” Kama ilivyo na kiolezo cha Kiajemi, bustani ya kawaida ya Waarabu, tokea zile za Wamoor katika Hispania hadi Kashmir, ziligawanywa katika sehemu nne na vijito vinne vilivyokutana katikati kwenye kidimbwi au kwenye bomba la kububujisha maji, inayokumbusha juu ya mito minne ya Edeni.

      Kaskazini mwa India, kando ya Ziwa Dal katika Bonde la Kashmir lililo maridadi, watawala walioitwa Mogul wa karne ya 17 walipanda bustani zaidi ya 700 za kiparadiso. Hizo zilifanyiza rangi nyingi zenye kuvutia sana zenye mamia ya mabomba ya kububujisha maji, ngazi, na maporomoko ya maji. Banda la marumaru nyeusi lililojengwa kwenye ufuko wa Ziwa Dal na Shah Jahan (aliyeijenga Taj Mahal) bado lina mwandiko: “Ikiwa pana paradiso duniani, ipo hapa, ipo hapa, ipo hapa.”

      Karne kadhaa mapema, Ulaya ilikuwa imepitia Enzi za Kati na kuingia katika Mvuvumko wa karne ya 14. Desturi ya utunzaji wa bustani ya Roma, iliyokuwa imepuuzwa wakati Enzi za Kati zilipoanza katika karne ya tano W.K., ilianza kusitawi tena—wakati huu chini ya utawala wa kanisa. Jumuiya ya Wakristo iliona bustani kuwa ‘paradiso ya muda.’ Plani ya karne ya tisa ya makao ya watawa yaonyesha bustani mbili zilizoitwa “Paradiso.” Bustani za Jumuiya ya Wakristo upesi zikawa kubwa na zenye fahari zaidi, lakini badala ya kuonyesha mambo ya kiroho, nyingi zikawa ishara za mamlaka na mali.

      Charles 8 wa Ufaransa aliposhinda Naples, Italia, katika 1495, aliandika hivi barua ya kwenda nyumbani: “Hamwezi kuamini bustani maridadi ambazo ninazo katika jiji hili . . . Inaonekana ni Adamu na Hawa pekee ndio wanaokosekana ili iwe paradiso ya kidunia.” Lakini kama Charles angaliishi hadi karne ya 17, angaliona katika Ufaransa bustani kubwa sana za Mfalme Louis 14. Kitabu The Garden chasisitiza kwamba bustani zilizo kwenye Makao ya Kifalme ya Versailles “bado zaweza kutajwa kuwa kubwa zaidi na bora zaidi ulimwenguni.”

      Hata hivyo, ule Mvuvumko ukawa na ufafanuzi mpya wa paradiso: asili inapaswa kudhibitiwa na mwanadamu aliyeerevuka ambaye atatiisha bustani kwa kuiondolea pori. Miti na maua yote yalipangwa kwa njia fulani hususa. Hivyo, sanaa ya Waroma—ya kuunda miti na vichaka kwa kuvipogoa na kuvikunja—ilivuvumka sana.

      Kisha, katika karne za 18 na 19, uvumbuzi na biashara zilizofanywa kwa kuabiri zilitokeza mimea mipya na mawazo mapya ya kutunza bustani katika ulimwengu wa magharibi. Uingereza nayo ikajitosa katika uwanja wa kubuni bustani. “Katika Uingereza ya karne ya 18,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “mwanadamu akafahamu zaidi na zaidi ulimwengu wa asili ambamo alishiriki. Badala ya kulazimisha njia yake ya kuunda ulimwengu wa asili, alianza kufikiria kurekebisha maisha yake ili kupatana na huo.” Wanaume kama William Kent na Lancelot Brown walikuwa stadi sana katika kutengeneza mandhari. Brown alitengeneza mandhari za zaidi ya nyumba mia mbili katika Uingereza. Watu wawili waliokuja kuwa marais wa Marekani, Thomas Jefferson na John Adams, walizuru Uingereza katika 1786 ili kujifunza kutokana na bustani za Uingereza.

      Mandhari za Mashariki

      Desturi ya China ya kutunza bustani imeathiri sana ustaarabu wa Mashariki kama desturi za kutunza bustani za Misri, Ugiriki, na Roma zilivyoathiri Magharibi. Awali Wachina walikuwa waabudu-maumbile, nao waliona mito, majabali, na milima, vyote kuwa roho zilizotwaa umbo la vitu na hivyo vilipaswa kuheshimiwa. Baadaye, Dini ya Tao, Dini ya Confucius, na Dini ya Buddha zikaenea sana na kutokeza aina zazo za bustani.

      Kwenye upande ule mwingine wa Bahari ya Japani, bustani za Wajapani zilisitawisha mtindo wazo zenyewe, ambapo umbo lilikuwa la maana kuliko rangi na kila kitu kilikuwa na mahali pake pa pekee. Katika kujaribu kunasa unamna-namna na utulizo wa asili, mtunza-bustani huweka mawe kwa uangalifu na kupanda na kufanyiza bustani yake kwa uangalifu mkubwa. Jambo hilo huonekana wazi katika bonsai (linalomaanisha “mimea iliyopandwa katika chungu”), sanaa ya kuzoeza mti mdogo au labda miti kadhaa katika umbo fulani na uwiano hususa.

      Ingawa mtindo wao waweza kutofautiana na bustani ya Magharibi, bustani ya Mashariki pia huonyesha tamaa ya Paradiso. Kwa kielelezo, katika kipindi cha Heian katika Japani (794-1185), aandika mwanahistoria wa bustani za Japani Wybe Kuitert, watunza-bustani walijaribu kutokeza hisia ya “paradiso duniani.”

      Upendo wa Ulimwenguni Pote

      Kutia ndani na hata makabila ya kuwinda na kukusanya chakula, walioishi katika bustani za “kiasili”—mwitu, misitu, na nyanda—bustani inapendwa ulimwenguni pote. Kuhusu “Waaztec wa Mexico na Wainka wa Peru,” yasema Britannica, “wale washindi waliripoti kuona bustani zenye madoido sana zenye milima iliyo na ngazi, miti, mabomba ya kububujisha maji, na vidimbwi vyenye mapambo . . . vinavyofanana na bustani katika Magharibi.”

      Ndiyo, misitu ya kale yenye kuvuka Naili, mandhari za Mashariki, bustani za kisasa za majiji, na bustani za kibotania—hizo zafunua nini? Tamaa ya mwanadamu ya kutaka Paradiso. Katika kutaja “tamaa ya [kudumu] ya mwanadamu ya kutaka Paradiso,” mwandikaji Terry Comito alisema: “Bustani ni mahali ambapo watu huhisi wamestarehe.” Na ni mtu yupi asiyeweza kufurahia kusema, ‘Makao yangu ni kama Bustani ya Edeni’? Lakini, je, Edeni ya duniani pote—na si tu kwa matajiri pekee—ni ndoto tu? Au ni uhakika wa wakati ujao?

  • Njia ya Kurudia Paradiso
    Amkeni!—1997 | Aprili 8
    • Njia ya Kurudia Paradiso

      KWA sababu ya tamaa ya mwanadamu ya kupata Paradiso na majaribio makubwa na madogo ya kuifanyiza tena, mtu angedhani kwamba kufikia sasa dunia ingekuwa paradiso halisi. Lakini sivyo ilivyo.

      Badala ya hivyo, mwanadamu ametanguliza pupa, ambayo mara nyingi hutawala kwa hasara ya mazingira na unamna-namna wa viumbe vilivyo hai. Wakiamini kwamba utajiri ndio jambo kuu, watu wengi wamepoteza tumaini kabisa kwamba dunia haitapata kamwe kufanywa kuwa paradiso ya Kiedeni. Badala ya hivyo, wao hutazamia maisha baada ya kifo mbinguni kuwa tumaini lao la pekee kwa Paradiso. Maoni hayo yadokeza kwamba, kwanza, tamaa yetu ya kibinadamu kwa Edeni itafadhaishwa milele na, pili, Mungu ameiacha dunia hii kwa sababu ya upumbavu na pupa ya wanadamu. Je, ndivyo ilivyo? Wakati ujao una nini hasa? Na wakati ujao huo utakuwa wapi?

      Paradiso—Itakuwa Mbinguni au Duniani?

      Karibu miaka 2,000 iliyopita, Yesu Kristo alisema hivi alipokuwa akizungumza na mwizi aliyetubu aliyekuwa ametundikwa mtini kando yake: “Utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.” (Luka 23:43) Je, Yesu alimaanisha kwamba mwizi huyo angeenda mbinguni pamoja naye? La.

      Huyo mtenda-maovu hata hangalifikiria jambo hilo. Kwa nini? Kwa sababu labda alikuwa amefahamu mafungu katika Maandiko ya Kiebrania, ambayo yalikuwapo katika wakati wake, kama vile sehemu ya kwanza ya Zaburi 37:29: “Wenye haki watairithi nchi.” (Italiki ni zetu.) Yesu alifundisha kweli iyo hiyo, akitangaza hivi: “Wenye furaha ni wenye tabia-pole, kwa kuwa wao watairithi dunia.” (Mathayo 5:5) Andiko hili lapatana na ile ambayo kwa kawaida huitwa Sala ya Bwana, inayosema: “Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.”—Mathayo 6:9, 10.

      Biblia yafundisha kwamba Mungu aliumba dunia, bali si mbingu, kuwa makao ya familia ya wanadamu. Neno lake lataarifu kwamba yeye “hakuiumba [dunia] ukiwa” bali “aliiumba ili ikaliwe na watu.” (Isaya 45:18) Kwa muda gani? ‘Aliiweka nchi juu ya misingi yake; isitikisike milele.’ (Zaburi 104:5) Ndiyo, “dunia hudumu daima.”—Mhubiri 1:4.

      Ni kusudi la Mungu kwamba watu wengi zaidi kati ya wale wanaomtumikia waifanye dunia hii kuwa makao yao milele. Ona jinsi Neno la Mungu, Biblia, linavyoeleza jambo hili. Zaburi 37:11 latabiri: “Wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.” Kwa muda gani? Zaburi 37:29 lasema: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.” (Italiki ni zetu.) Wakati huo andiko lisemalo hivi litatimizwa: “[Wewe Mungu] waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake,” yaani, matakwa yanayopatana na mapenzi ya Mungu.—Zaburi 145:16.

      Vipi kuhusu wale ambao hawataki kufanya mapenzi ya Mungu? Mithali 2:21, 22 lasema: “Maana wanyofu watakaa katika nchi, na wakamilifu watadumu ndani yake. Bali waovu watatengwa na nchi, nao wafanyao hila watang’olewa.”

      Paradiso Inarudishwa

      Sasa upesi, hukumu za Mungu zitatekelezwa dhidi ya ulimwengu huu mwovu. (Mathayo 24:3-14; 2 Timotheo 3:1-5, 13) Lakini Mungu atahifadhi “umati mkubwa” wa watu waokoke huo uharibifu unaokuja na kuingia katika ulimwengu mpya alioufanyiza.—Ufunuo 7:9-17.

      Kisha, Mungu ataelekeza kazi hiyo yenye shangwe ambayo raia wake wa kibinadamu watafanya ya kugeuza dunia nzima kuwa makao ya paradiso ya wanadamu. Biblia yaahidi: “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi: jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. . . . Maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.”—Isaya 35:1, 6.

      Katika Paradiso hiyo yenye kupanuka, hakutakuwa tena na njaa, umaskini, mitaa ya mabanda, watu wasio na makao, au maeneo yenye kujaa uhalifu. “Na nafaka zitakuwa nyingi.” (Zaburi 72:16, Zaire Swahili Bible) “Na mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake.” (Ezekieli 34:27) “Nao watajenga nyumba na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine.” (Isaya 65:21, 22) “Wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu.”—Mika 4:4.

      Sababu Inayofanya Wengine Waende Mbinguni

      Labda watu wengi watakiri kwamba wana tamaa ya kuishi katika paradiso ya kidunia. Hilo ni jambo la kawaida, kwa kuwa Mungu hakupata kuwawekea tamaa ya kwenda mbinguni; wao hata hawawezi kuwazia jinsi maisha ya mbinguni yalivyo. Kwa mfano, katika mazungumzo na mhudumu wake wa Kanisa la Uingereza, ingawa Pat alikuwa mshiriki wa dhati wa kanisa hilo, alisema: “Sijapata kamwe kuwa na mawazo yoyote kuhusu kwenda mbinguni. Mimi sitaki kwenda, na hata hivyo nitafanya nini huko?”—Linganisha Zaburi 115:16.

      Ni kweli Biblia hufundisha kwamba idadi ndogo ya wanadamu, 144,000, wanaenda mbinguni. (Ufunuo 14:1, 4) Pia yaeleza sababu: “Ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao watatawala wakiwa wafalme juu ya dunia.” (Ufunuo 5:9, 10) Pamoja na Mfalme wao, Yesu Kristo, hao wafanyiza “ufalme,” ambao ni serikali mpya ya kimbingu juu ya dunia, ambayo Wakristo husali juu yayo. Serikali hiyo itasimamia kazi ya kugeuza kabisa dunia na wanadamu pia.—Danieli 2:44; 2 Petro 3:13.

      Hata hivyo, kwa kuwa tamaa ya kuishi mbinguni haimo kiasili katika wanadamu, utendaji wa kipekee wa roho ya Mungu “hutoa ushahidi” kwa wale 144,000 ili wahisi “mwito [huo] wa kimbingu” wa kipekee. (Waroma 8:16, 17; Wafilipi 3:14) Ingawa hivyo, bila shaka utendaji kama huo wa roho takatifu hauhitajiki kwa wanadamu kwa ujumla kwa sababu makao yao ya milele ni hapa katika dunia paradiso.

      Paradiso ya Kiroho Yatayarisha Njia

      Mtu anastahilije kupata uhai wa milele katika Paradiso duniani? “Hii yamaanisha uhai udumuo milele,” Yesu alisema, “wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.” (Yohana 17:3) Likihusianisha mahusiano ya amani kati ya wanadamu na ujuzi wa Mungu, Isaya 11:9 lasema: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Linganisha Isaya 48:18.

      Bila shaka, ujuzi huu si ujuzi wa akilini tu. Huo huathiri utu wa mtu na kukuza sifa za kimungu, kama vile “upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujidhibiti.” (Wagalatia 5:22, 23) Mashahidi wa Yehova hujaribu kukuza sifa hizi, na hivyo, hata sasa, wao wamebarikiwa na paradiso nzuri ya kiroho.—Isaya 65:13, 14.

      Hali yao ya kiroho yatofautiana kama nini na ile ya ulimwengu, ambao unazidi kudidimia katika hali ya kutomcha Mungu na ufisadi! Hata hivyo, upesi ulimwengu huu utaangamizwa na Mungu. Kwa wakati huu, Mashahidi wa Yehova wakualika kuzuru—ndiyo uchunguze—paradiso ya kiroho ambayo wanafurahia. Jionee mwenyewe kwamba sasa hivi Yesu, Mfalme wa kimbingu asiyeonekana, anaongoza kwa utulivu wakazi wa wakati ujao wa ulimwengu huo mpya katika barabara nyembamba ielekeayo kwenye Paradiso ya kidunia na uhai wa milele!—Mathayo 7:13, 14; Ufunuo 7:17; 21:3, 4.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki