-
Amani ya Kweli—Kutoka Chanzo Gani?Mnara wa Mlinzi—1997 | Aprili 15
-
-
Amani ya Kweli—Kutoka Chanzo Gani?
“[Yehova] avikomesha vita hata mwisho wa dunia.”—ZABURI 46:9.
1. Ni ahadi gani nzuri ajabu ya amani tunayopata katika unabii wa Isaya?
“KAZI ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima. Na watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu.” (Isaya 32:17, 18) Ni ahadi nzuri kama nini! Ni ahadi ya amani ya kweli itakayoletwa na Mungu.
2, 3. Fafanua amani ya kweli.
2 Lakini, amani ya kweli ni nini? Je, ni kutokuwapo kwa vita tu? Au ni kipindi tu ambacho katika hicho mataifa hujiandaa kwa vita inayofuata? Je, amani ya kweli ni ndoto tu? Hayo ni maswali ambayo twahitaji majibu yenye kutegemeka kwayo. Kwanza, amani ya kweli ni zaidi ya ndoto. Amani ya Mungu iliyoahidiwa hupita sana chochote kile ambacho ulimwengu huu waweza kuwazia. (Isaya 64:4) Si amani ya miaka michache au miongo michache. Hiyo hudumu milele! Na si amani ya wachache tu waliopendelewa—hiyo huhusisha mbingu na dunia, malaika na wanadamu. Hiyo huenea kwa watu wa mataifa, vikundi vya kikabila, lugha, na rangi zote. Haina mipaka, vizuizi, wala hali za kutofaulu.—Zaburi 72:7, 8; Isaya 48:18.
3 Amani ya kweli yamaanisha amani kila siku. Yamaanisha kwamba waamka kila asubuhi bila wazo la vita, bila uhitaji wa kuhangaikia wakati wako ujao, wakati ujao wa watoto wako, hata wakati ujao wa wajukuu wako. Yamaanisha amani kamili ya akilini. (Wakolosai 3:15) Yamaanisha kutokuwa na uhalifu tena, kutokuwa na ujeuri tena, kutokuwa na familia zilizogawanyika tena, kutokuwa na watu wasio na makao tena, kutokuwa na watu wanaokufa njaa au kufa kwa baridi tena, na kutokuwa na hali ya kukata tamaa na kufadhaika tena. Vyema hata zaidi, amani ya Mungu yamaanisha ulimwengu usio na ugonjwa, umivu, huzuni, au kifo. (Ufunuo 21:4) Ni tumaini zuri ajabu kama nini tulilo nalo la kufurahia amani ya kweli milele! Je, hii si ndiyo aina ya amani na furaha ambayo sisi sote twatamani kwa hamu nyingi? Je, hii si ndiyo aina ya amani ambayo twapaswa kusali ije na kujitahidi kuipata?
Jitihada za Wanadamu Zilizoshindwa Kufaulu
4. Ni jitihada zipi za kupata amani ambazo mataifa yameweka, na kukiwa na matokeo yapi?
4 Kwa karne nyingi, wanadamu na mataifa wameongea juu ya amani, wamejadili juu ya amani, wametia sahihi mamia ya mikataba ya amani. Tokeo limekuwa nini? Kwa miaka 80 iliyopita, karibu kumekuwa hakuna wakati kamwe ambapo taifa fulani au kikundi fulani hakijawa vitani. Kwa wazi, amani imewahepa wanadamu. Kwa hiyo swali ni, Kwa nini jitihada zote za mwanadamu za kuimarisha amani ya kimataifa zimeshindwa kufaulu, na kwa nini mwanadamu hawezi kuleta amani ya kweli ambayo itadumu?
5. Kwa nini jitihada za wanadamu za kupata amani zimeshindwa kufaulu daima?
5 Jibu sahili ni kwamba wanadamu hawaendei chanzo kifaacho cha amani ya kweli. Chini ya uvutano wa Shetani Ibilisi, wanadamu wameanzisha mashirika ambayo hupatwa na udhaifu na maovu yao wenyewe—pupa yao na kujitakia kwao makuu, tamaa yao ya kupata mamlaka na umashuhuri. Wameenda kwenye taasisi za kielimu za masomo ya juu na kuanzisha mashirika ya kuwafaidi wakati ujao na taasisi za utafiti wa kielimu, ambazo zimetokeza tu njia zaidi za uonevu na uharibifu. Wanadamu wameelekezwa kwenye chanzo gani? Wametafuta wapi?
6, 7. (a) Ushirika wa Mataifa ulijiwekea rekodi ipi? (b) Umoja wa Mataifa una rekodi ipi?
6 Huko nyuma katika 1919 mataifa yalitumaini Ushirika wa Mataifa kuimarisha amani yenye kudumu. Tumaini hilo lilivunjwa-vunjwa katika 1935 wakati vikosi vya Mussolini vilipovamia Ethiopia na katika 1936 wakati vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoanza Hispania. Katika 1939 Ushirika huo ulikoma kutenda wakati Vita ya Ulimwengu 2 ilipofyatuka. Ile iliyoitwa amani isivyofaa haikuwa hata imemaliza miaka 20.
7 Namna gani Umoja wa Mataifa? Je, huo umeandaa tumaini lolote halisi la amani yenye kudumu duniani pote? Wapi. Tangu kuanzishwa kwao mwaka wa 1945, zaidi ya vita na mapigano 150 ya kutumia silaha yamepiganwa! Si ajabu kwamba Gwynne Dyer, msomi Mkanada juu ya vita na vyanzo vyayo, aliufafanua UM kuwa “shirika la majangili waliogeuka kuwa walinda-wanyama, si kusanyiko la watakatifu,” na “shirika lisilo na uwezo wowote ambalo katika hilo ni maongeo tu hufanywa.”—Linganisha Yeremia 6:14; 8:15.
8. Yajapoongea juu ya amani, mataifa yamekuwa yakifanya nini? (Isaya 59:8)
8 Wajapoongea juu ya amani, mataifa huendelea kuvumbua na kutengeneza silaha. Nchi zinazodhamini makongamano ya amani mara nyingi ndizo zinazoongoza katika utengenezaji wa silaha. Faida kubwa za kibiashara katika nchi hizo huendeleza utokezaji wa zana za vita zenye kufisha, kutia ndani mabomu ya kikatili sana ya kuchimbiwa ardhini ambayo kila mwaka huua au kulemaza raia walio watu wazima na watoto wapatao 26,000. Pupa na ufisadi ndizo kani zenye kuhamasisha. Rushwa na kupokea “kitu kidogo” ni sehemu muhimu katika biashara ya kimataifa ya silaha. Wanasiasa fulani hujitajirisha kwa njia hiyo.
9, 10. Wastadi walimwengu wameona nini kwa habari ya vita na juhudi za kibinadamu?
9 Katika Desemba 1995, mwanafizikia Mpolandi na mshindi wa Tuzo ya Nobeli ya Amani Joseph Rotblat aliomba mataifa yakomeshe shindano la kuunda silaha. Yeye alisema hivi: “Njia pekee ya kuzuia [shindano jipya la kuunda silaha] ni kukomesha vita kabisa.” Je, wewe wafikiri hilo laelekea kutukia? Tangu 1928 na kuendelea, mataifa 62 yaliidhinisha Mwafaka wa Kellogg-Briand ambao katika huo walikataa katakata vita kuwa njia ya kutatua matofautiano. Vita ya Ulimwengu 2 ilionyesha kwa wazi kwamba mwafaka huo ulikuwa karatasi bure.
10 Kusema wazi, vita vimekuwa kikwazo cha daima katika kijia cha historia ya wanadamu. Kama vile Gwynne Dyer alivyoandika, “vita ni shirika kuu katika ustaarabu wa kibinadamu, na ni ya kale kama walivyo wanadamu.” Ndiyo, karibu kila staarabu na milki imekuwa na mashujaa wayo wa kijeshi wenye kuheshimiwa sana, majeshi yayo yaliyopo wakati wote, mapigano yayo yajulikanayo sana, mashirika yayo matakatifu ya kijeshi, na rundo layo la silaha. Hata hivyo, karne yetu imetiwa alama na vita zaidi ya karne nyingine yoyote, katika uharibifu na vilevile katika upotezo wa uhai.
11. Ni jambo gani la msingi ambalo viongozi wa ulimwengu wamepuuza katika jitihada yao ya kupata amani?
11 Ni wazi kwamba viongozi wa ulimwengu wamepuuza hekima ya msingi ya Yeremia 10:23 (NW): “Najua vyema, Ee Yehova, kwamba njia si yake mwanadamu wa udongo. Si jukumu la mwanadamu kuelekeza hatua zake.” Mungu akipuuzwa, hakuwezi kuwa na amani ya kweli. Basi, je, yote haya yamaanisha kwamba vita ni jambo lisiloweza kuepukika katika jamii iliyostaarabika? Je, yamaanisha kwamba amani—amani ya kweli—ni ndoto isiyoweza kutimia?
Kupata Kisababishi cha Msingi
12, 13. (a) Biblia hufunua nini kuhusu kisababishi cha msingi cha vita, kisichoonekana? (b) Shetani amegeuzaje uangalifu wa wanadamu mbali na suluhisho halisi la matatizo ya ulimwengu?
12 Ili kujibu maswali hayo, twahitaji kuelewa visababishi vya vita. Biblia hutaarifu waziwazi kwamba yule malaika mwasi Shetani ndiye “muua-binadamu kikatili” na “mwongo” wa kwanza na kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu.” (Yohana 8:44; 1 Yohana 5:19) Yeye amefanya nini ili kuendeleza mbinu zake? Twasoma hivi kwenye 2 Wakorintho 4:3, 4: “Basi, ikiwa kwa kweli habari njema tutangazayo imetiwa shela, imetiwa shela miongoni mwa wale wanaoangamia, ambao miongoni mwao mungu wa huu mfumo wa mambo amepofusha akili za wasioamini, ili mmuliko wa habari njema yenye utukufu juu ya Kristo, aliye mfano wa Mungu, usipate kung’aa kwa kupenya.” Shetani hufanya kila awezalo kugeuza uangalifu wa wanadamu mbali na Ufalme wa Mungu kuwa suluhisho la matatizo ya ulimwengu. Yeye hupofusha na kukengeua watu kwa masuala ya kijamii, ya kisiasa, na ya kidini yenye kuleta migawanyiko, ili haya yaonekane kuwa ya maana zaidi kuliko utawala wa Mungu. Kielelezo kimoja ni ongezeko la hivi majuzi ulimwenguni pote la utukuzo wa taifa.
13 Shetani Ibilisi huendeleza utukuzo wa taifa na ukabila, itikadi kwamba taifa moja, jamii moja, au kabila moja ni bora kuliko jingine. Chuki zenye kina ambazo zimekandamizwa kwa karne nyingi zinaamshwa ili kuchochea vita na mapambano mengine zaidi. Federico Mayor, mkurugenzi-mkuu wa UNESCO, alionya juu ya mwelekeo huu: “Hata mahali ambapo uvumiliano ulitawala kila siku, badiliko kuelekea hali ya kuhofu wageni linakuwa dhahiri zaidi, na matamshi ya kizalendo ya kupita kiasi na ubaguzi wa kijamii yaliyoonekana kuwa jambo la kale yanasikiwa mara nyingi zaidi.” Tokeo limekuwa nini? Yale machinjo yenye kuchukiza katika iliyokuwa Yugoslavia na ule umwagaji wa damu nyingi wa kikabila katika Rwanda ni matukio mawili tu ya jinsi hiyo ambayo yamepata kujulikana ulimwenguni.
14. Ufunuo 6:4 huonyeshaje vita na matokeo yayo katika wakati wetu?
14 Biblia ilitabiri kwamba katika wakati wa mwisho wa mfumo huu, farasi mwenye rangi-moto, akifananisha vita, angeenda mbio kotekote duniani. Twasoma hivi kwenye Ufunuo 6:4: “Na mwingine akatokea, farasi mwenye rangi-moto; na kwa yeye aketiye juu yake akapewa ruhusa kuondolea mbali amani katika dunia ili wachinjane; naye akapewa upanga mkubwa.” Tangu 1914 tumeona mpanda-farasi huyu wa ufananisho ‘akiondolea mbali amani,’ na mataifa yameendelea kupigana na kupiga vita.
15, 16. (a) Fungu la dini limekuwa nini katika vita na mauaji? (b) Yehova huonaje yale ambayo dini zimefanya?
15 Jambo ambalo halipaswi kupuuzwa ni fungu la dini katika vita na mauaji hayo. Uvutano wenye kuongoza vibaya wa dini isiyo ya kweli ndio waweza kulaumiwa kwa kadiri kubwa kwa kuijaza damu historia ya wanadamu. Mwanatheolojia Mkatoliki Hans Küng aliandika hivi: “Ni jambo lisiloweza kupingwa kwamba kwa sababu ya uvutano wa dini ulio mbaya na wenye uharibifu, zimechangia sana na bado zachangia kuchochea vita. Kumekuwa na mapigano mengi sana, mapambano yenye umwagikaji wa damu, kwa kweli ‘vita vya kidini’ vyapasa kutozwa hesabu; . . . na ndivyo ilivyo pia kwa habari ya vile vita viwili vya ulimwengu.”
16 Yehova Mungu huhisije kuhusu fungu la dini isiyo ya kweli katika mauaji na vita? Mashtaka ya Mungu, yaliyorekodiwa kwenye Ufunuo 18:5 yataarifu hivi: “Dhambi zake zimetungamana pamoja hadi mbinguni, na Mungu amekumbuka matendo yake yasiyo ya haki.” Kushirikiana kwa dini isiyo ya kweli pamoja na watawala wa kisiasa wa ulimwengu kumetokeza hatia kubwa ya damu, mtungamano mkubwa wa dhambi zilizorundamana, hivi kwamba Mungu hawezi kuupuuza. Hivi karibuni ataondolea mbali kabisa kikwazo hicho kinachozuia amani ya kweli.—Ufunuo 18:21.
Njia Kuelekea Amani
17, 18. (a) Kwa nini si ndoto tu isiyoweza kutimia kuamini kwamba amani idumuyo milele inawezekana? (b) Yehova amefanya nini tayari ili kuhakikisha kwamba amani ya kweli itakuja?
17 Ikiwa wanadamu, kupitia vyombo kama vile Umoja wa Mataifa, hawawezi kuleta amani ya kweli na yenye kudumu, amani ya kweli itakuja kutoka chanzo gani, na jinsi gani? Je, ni ndoto tu isiyoweza kutimia kuamini kwamba amani idumuyo milele inawezekana? Sivyo ikiwa twakiendea chanzo kifaacho cha amani. Na ni nani aliye Chanzo hicho? Zaburi 46:9 hujibu kwa kutuambia kwamba Yehova “avikomesha vita hata mwisho wa dunia; avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.” Na Yehova tayari ameanza mwendo wa kukomesha vita na kuimarisha amani ya kweli. Jinsi gani? Kwa kumtawaza Kristo Yesu juu ya kiti chake cha enzi cha Ufalme ambacho ni haki yake katika 1914 na kwa kuendeleza kampeni ya kielimu iliyo kubwa kupita zote kwa ajili ya amani katika historia ya wanadamu. Maneno ya kiunabii ya Isaya 54:13 yatutia moyo hivi: “Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.”
18 Unabii huo hutolea kielezi kanuni ya kisababishi na tokeo—yaani, kila tokeo lina kisababishi chalo. Katika unabii huo ufundishaji wa Yehova—kisababishi—hugeuza umbo watu walio wataka-vita kuwa watu wapenda-amani ambao wana amani pamoja na Mungu. Tokeo ni badiliko la moyo ambalo hufanya watu wawe wapenda-amani. Ufundishaji huo unaobadili mioyo na akili za watu unaenea ulimwenguni pote hata sasa huku mamilioni yakifuata kielelezo cha “Mkuu wa Amani,” Yesu Kristo.—Isaya 9:6, NW.
19. Yesu alifundisha nini juu ya amani ya kweli?
19 Na Yesu alifundisha nini kuhusu amani ya kweli? Yeye hakusema tu juu ya amani kati ya mataifa bali juu ya amani kati ya watu katika mahusiano yao na juu ya amani ya ndani itokanayo na dhamiri njema. Kwenye Yohana 14:27, twasoma maneno ya Yesu kwa wafuasi wake: “Mimi nawaachia nyinyi amani, nawapa amani yangu. Mimi siwapi nyinyi hiyo kwa njia ile ambayo ulimwengu huitoa. Msiache mioyo yenu itaabishwe wala msiiache ikunyatike kwa sababu ya hofu.” Amani ya Yesu ilikuwaje tofauti na ile ya ulimwengu?
20. Yesu ataleta amani ya kweli kwa njia ipi?
20 Kwanza, amani ya Yesu ilihusiana kwa ukaribu na ujumbe wake wa Ufalme. Alijua kwamba serikali adilifu ya kimbingu, inayofanyizwa na Yesu na watawala-wenzi 144,000, ingekomesha vita na wachochea-vita. (Ufunuo 14:1, 3) Yeye alijua kwamba ingeleta hali zenye amani za kiparadiso ambazo alimtolea yule mtenda-maovu aliyekufa kando yake. Yesu hakumtolea mahali katika Ufalme wa kimbingu, bali alisema hivi: “Kwa kweli mimi nakuambia wewe leo, Utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.”—Luka 23:43.
21, 22. (a) Amani ya kweli inatia ndani tumaini jipi lenye kutegemeza vizuri ajabu? (b) Ni lazima tufanye nini ili kushuhudia baraka hiyo?
21 Pia, Yesu alijua kwamba Ufalme wake ungeleta faraja kwa wote wale wanaoomboleza wanaodhihirisha imani katika yeye. Amani yake hutia ndani lile tumaini lenye kutegemeza vizuri ajabu la ufufuo. Kumbuka maneno yake yenye kutia moyo yapatikanayo kwenye Yohana 5:28, 29: “Msistaajabie hili, kwa sababu saa inakuja ambayo katika hiyo wote wale waliomo ndani ya makaburi ya ukumbusho watasikia sauti yake na kutoka, wale waliofanya mambo mema kwenye ufufuo wa uhai, wale waliozoea kufanya mambo maovu kwenye ufufuo wa hukumu.”
22 Je, wewe watazamia wakati huo? Je, umepoteza wapendwa katika kifo? Je, watamani sana kuwaona tena? Basi ikubali amani ambayo Yesu hutoa. Uwe na imani kama ile ya Martha, dadaye Lazaro, aliyemwambia Yesu hivi: “Najua atafufuliwa katika ufufuo siku ya mwisho.” Lakini angalia jibu hili la Yesu lenye kuchangamsha kwa Martha: “Mimi ndio ufufuo na uhai. Yeye ambaye hudhihirisha imani katika mimi, hata ingawa afa, atakuja kwenye uhai; na kila mtu aliye hai na hudhihirisha imani katika mimi hatakufa hata kidogo kabisa. Je, unaamini hili?”—Yohana 11:24-26.
23. Kwa nini ujuzi sahihi wa Neno la Mungu ni muhimu katika kupata amani ya kweli?
23 Wewe pia waweza kuamini na kunufaika na ahadi hiyo. Jinsi gani? Kwa kupata ujuzi sahihi wa Neno la Mungu. Ona jinsi mtume Paulo alivyokazia umaana wa ujuzi sahihi: “Sisi . . . hatujaacha kusali kwa ajili yenu na kuomba ili nyinyi mpate kujazwa ujuzi sahihi wa mapenzi yake katika hekima yote na ufahamivu wa kiroho, kusudi mtembee kwa kumstahili Yehova kwa madhumuni ya kumpendeza yeye kikamili mnapoendelea kuzaa matunda katika kila kazi njema na kuongezeka katika ujuzi sahihi wa Mungu.” (Wakolosai 1:9, 10) Ujuzi huo sahihi utakusadikisha kwamba Yehova Mungu ndiye chanzo cha amani ya kweli. Huo utakuambia pia kile ambacho ni lazima ufanye sasa ili uweze kujiunga na mtunga-zaburi katika kusema: “Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, maana Wewe, BWANA, peke yako, ndiwe unijaliaye kukaa salama.”—Zaburi 4:8.
-
-
Tafuta Sana Amani ya Kweli na Kuifuatia!Mnara wa Mlinzi—1997 | Aprili 15
-
-
Tafuta Sana Amani ya Kweli na Kuifuatia!
“Yeye ambaye angependa uhai na kuona siku zilizo njema, . . . acheni ageuke mbali kutoka lililo baya na kufanya lililo jema; acheni atafute sana amani na kuifuatia.”—1 PETRO 3:10, 11.
1. Ni maneno gani ya Isaya yajulikanayo sana ambayo yatafanikiwa kwa hakika?
“WATAFUA panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena.” (Isaya 2:4) Hata ingawa andiko hili lijulikanalo sana linaonyeshwa karibu na makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika Jiji la New York, shirika hilo la ulimwengu halitimizi maneno hayo hata kidogo. Hata hivyo, likiwa sehemu ya neno la Yehova Mungu lisiloshindwa kufaulu, tangazo hilo halitakuwa bila matokeo.—Isaya 55:10, 11.
2. Ni jambo gani lazima litukie “katika siku za mwisho,” kulingana na Isaya 2:2, 3?
2 Maneno yanayopatikana kwenye Isaya 2:4 kwa kweli ni sehemu ya unabii mzuri ajabu, unabii juu ya amani ya kweli—nao unatimizwa katika wakati wetu wenyewe. Kabla ya kupiga mbiu ya matumaini juu ya kutokuwa na vita tena wala silaha za vita, unabii huo wasema: “Itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu.”—Isaya 2:2, 3.
Watu Waweza Kupata Kuwa Wenye Kufanya Amani
3. Mtu aweza kubadilikaje kutoka kuwa mtaka-vita hadi kuwa mwenye amani?
3 Angalia kwamba kabla ya watu kuweza kufuatia mwendo wenye amani, lazima waagizwe kwa njia za Yehova. Itikio la kutii ufundishaji wa Yehova laweza kubadili njia ambayo mtu anafikiri na kutenda, hivi kwamba mtu ambaye amekuwa mtaka-vita apata kuwa mwenye kufanya amani. Mgeuzo umbo huo unatimizwaje? Waroma 12:2 lasema hivi: “Komeni kufanyizwa kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo, bali mgeuzwe umbo kwa kufanya upya akili yenu, ili mpate kujithibitishia wenyewe mapenzi ya Mungu yaliyo mema na yenye kukubalika na makamilifu.” Tunafanya upya akili yetu, au tunaihamasisha kuelekea njia tofauti, kwa kuijaza na kanuni na amri kutoka Neno la Mungu. Funzo la ukawaida la Biblia latusaidia kufanya badiliko hilo na latuwezesha kujithibitishia wenyewe mapenzi ya Yehova kwetu, ili tuweze kuona kwa wazi njia ambayo ni lazima twende.—Zaburi 119:105.
4. Mtu anavaaje ule utu mpya wa kuwa mwenye kufanya amani?
4 Kweli ya Biblia hugeuza umbo kigezo chetu cha kufikiri na pia matendo yetu na utu wetu. Hiyo yatusaidia kufanya vile mtume Paulo alivyosihi sana: “Mweke mbali utu wa hapo zamani unaofuatana na njia yenu ya kwanza ya mwenendo na ambao unafisidiwa kulingana na tamaa zake za udanganyifu; bali . . . mfanywe upya katika kani inayotendesha akili yenu, na mvae utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na uaminifu-mshikamanifu.” (Waefeso 4:22-24) Kani inayotendesha akili ni ya ndani. Inageuzwa umbo na inapata kuwa yenye nguvu huku kumpenda kwetu Yehova na amri zake kunapoongezeka, na inatufanya tuwe watu wa kiroho na wenye kufanya amani.
5. “Amri mpya” ambayo Yesu aliwapa wanafunzi wake inachangiaje amani miongoni mwao?
5 Uhitaji wa mgeuzo umbo huo unaonwa kutokana na agizo ambalo Yesu aliwapa wanafunzi wake katika saa zake za mwisho pamoja nao: “Mimi ninawapa nyinyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile nimewapenda nyinyi, kwamba nyinyi pia mpendane. Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.” (Yohana 13:34, 35) Upendo huo ulio kama wa Kristo, usio na ubinafsi huwaunganisha wanafunzi pamoja katika muungano mkamilifu. (Wakolosai 3:14) Ni wale tu walio tayari kukubali na kuishi kulingana na “amri [hiyo] mpya” watakaofurahia amani ambayo Mungu aahidi. Je, kuna watu wowote wafanyao hivyo leo?
6. Kwa nini Mashahidi wa Yehova hufurahia amani, tofauti na watu wa ulimwengu?
6 Mashahidi wa Yehova hujitahidi kuonyesha upendo katika udugu wao wa ulimwenguni pote. Ingawa wametolewa katika mataifa yote ya ulimwengu, hawashiriki katika ubishi mbalimbali wa ulimwengu, hata wanaposongwa sana kisiasa na kidini. Wakiwa watu wenye muungano, wanafundishwa na Yehova, na wanafurahia amani. (Isaya 54:13) Wanabaki wakiwa na hali ya kutokuwamo katika mapambano ya kisiasa, hawashiriki katika vita. Watu fulani waliokuwa wajeuri hapo zamani wameacha mtindo-maisha huo. Wamepata kuwa Wakristo wapendao amani, wakiiga kielelezo cha Kristo Yesu. Nao hufuata kwa moyo wote shauri hili la Petro: “Yeye ambaye angependa uhai na kuona siku zilizo njema, acheni azuie ulimi wake kutokana na lililo baya na midomo yake isiseme udanganyo, lakini acheni ageuke mbali kutoka lililo baya na kufanya lililo jema; acheni atafute sana amani na kuifuatia.”—1 Petro 3:10, 11; Waefeso 4:3.
Wale Wanaoifuatia Amani
7, 8. Toa vielelezo vya watu walioacha vita wakawa wenye kutafuta sana amani ya kweli. (Simulia vingine ambavyo huenda ukavijua.)
7 Kwa kielelezo, kuna Rami Oved, aliyekuwa ofisa katika kikundi kilichobuniwa kimahususi kupambana na magaidi. Yeye alizoezwa kuua adui zake. Aliuamini sana utukuzo wa taifa lake la Israeli hadi siku aliyogundua kwamba marabi hawakutaka aoe mwanamke aliyempenda kwa sababu tu huyo alikuwa Mwasia, Mtu wa Mataifa. Yeye alianza kuitafuta-tafuta kweli katika Biblia. Kisha akakutana na Mashahidi wa Yehova. Kujifunza kwake Biblia pamoja na Mashahidi kulimsadikisha kwamba hangeweza tena kuwa mfuatia-utukuzo-wa-taifa shupavu. Upendo wa Kikristo ulimaanisha kuacha vita na silaha na kujifunza kupenda watu wa kila jamii. Alishangaa kama nini alipopata barua yenye fadhili yenye maneno haya ya kufungua, “Ndugu Yangu Rami”! Ni nini kilichokuwa kigeni sana kuhusu hilo? Mwandikaji alikuwa Shahidi Mpalestina. “Niliona haiaminiki,” asema Rami, “kwa kuwa Wapalestina walikuwa adui zangu, na hapa mmoja wao alikuwa akiniita mimi ‘Ndugu Yangu.’” Sasa Rami na mkeye hufuatia amani ya kweli katika njia ya Mungu.
8 Kielelezo kingine ni kile cha Georg Reuter, aliyetumikia katika jeshi la Ujerumani lililovamia Urusi wakati wa Vita ya Ulimwengu 2. Hatimaye akapata kuzindushwa na ule mpango mkuu wa Hilter wa kutawala ulimwengu. Aliporudi kutoka vitani, alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Yeye aliandika hivi: “Hatimaye, mambo yalianza kuwa wazi kwangu. Nilitambua kwamba si Mungu aliyekuwa wa kulaumiwa kwa huo umwagikaji damu wote . . . Nilijifunza kwamba kusudi lake lilikuwa kuimarisha paradiso ya duniani pote yenye baraka zidumuzo milele kwa wanadamu watiifu. . . . Hitler alikuwa amejivunia ‘Utawala wake wa Miaka Elfu’ lakini alikuwa ametawala kwa [miaka] 12 tu—na kwa matokeo yenye kuogopesha kama nini! Ni Kristo wala si Hitler . . . awezaye na atakayeimarisha utawala wa miaka elfu juu ya dunia.” Kwa miaka 50 hivi sasa, Georg amekuwa akitumikia akiwa mjumbe wa amani ya kweli katika huduma ya wakati wote.
9. Mambo yaliyoonwa na Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani ya Nazi yanathibitishaje kwamba wao ni wenye moyo mkuu na bado wenye kufanya amani?
9 Uaminifu-maadili na kutokuwamo kwa Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani wakati wa utawala wa Nazi huendelea kuwa ushuhuda wa kumpenda kwao Mungu na kupenda kwao amani hata sasa, miaka zaidi ya 50 baadaye. Kijitabu kilichochapishwa hivi majuzi na United States Holocaust Memorial Museum katika Washington, D.C., hutaarifu hivi: “Mashahidi wa Yehova walivumilia mnyanyaso mkali chini ya utawala wa Nazi. . . . Moyo mkuu ulioonyeshwa na wengi sana katika kukataa [kukana dini yao], walipokabiliwa na mateso makali, kutendewa kwa ukatili katika kambi za mateso, na nyakati fulani kuuawa, uliwapatia heshima ya watu wengi wa wakati wao.” Kisha chaongeza hivi: “Wakati wa kuwekwa huru kwa kambi hizo, Mashahidi wa Yehova waliendelea na kazi yao, wakitembea miongoni mwa waliosalimika, wakifanyiza waumini.”
Badiliko Kubwa Zaidi Sana
10. (a) Ni badiliko gani kubwa linalohitajiwa ili amani ya kweli ije? (b) Hilo lilionyeshwaje katika kitabu cha Danieli?
10 Je, hilo lamaanisha kwamba Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba wanaweza kuleta amani katika ulimwengu mzima kwa njia ya kugeuza watu wengi waamini kutokuwamo kwa Kikristo? La! Ili amani irudishwe duniani, badiliko kubwa zaidi sana linahitajiwa. Hilo ni jipi? Lazima utawala wa Ufalme wa Mungu, ambao Yesu alifundisha wanafunzi wake wasali uje, uchukue mahali pa utawala wa kibinadamu wenye migawanyiko, wenye uonevu, na ulio jeuri. (Mathayo 6:9, 10) Lakini hilo litatukiaje? Katika ndoto iliyopuliziwa kimungu, nabii Danieli alipata kujua kwamba katika siku za mwisho, Ufalme wa Mungu, kama vile jiwe kubwa ‘lisilokatwa kwa mikono ya binadamu,’ ungevunjavunja mfano mkubwa mno unaowakilisha tawala za kisiasa za wanadamu juu ya dunia. Kisha akapiga mbiu hivi: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:31-44.
11. Yehova ataleta kwa njia gani badiliko linalohitajiwa ili amani ipatikane?
11 Kwa nini kutatukia badiliko hili kubwa mno katika hali ya ulimwengu? Kwa sababu Yehova ameahidi kwamba atasafisha dunia na kuondoa wote wale wanaoichafua na kuiharibu. (Ufunuo 11:18) Mgeuzo umbo huo utatukia kwenye vita adilifu ya Yehova dhidi ya Shetani na ulimwengu wake mwovu. Twasoma hivi kwenye Ufunuo 16:14, 16: “Kwa kweli, hizo [yaani, semi zisizo safi zilizopuliziwa] ndizo semi zilizopuliziwa na roho waovu na zafanya ishara, nazo zatoka kwenda kwa wafalme [yaani, watawala wa kisiasa] wa dunia nzima inayokaliwa, kuwakusanya pamoja kwa vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote. Nazo zikawakusanya pamoja mahali paitwapo katika Kiebrania Har–Magedoni.”
12. Har–Magedoni itakuwaje?
12 Har–Magedoni itakuwaje? Haitakuwa apokalipsi ya kinyuklia wala msiba wenye kuchochewa na wanadamu. La, hii ni vita ya Mungu ya kumaliza vita vyote vya kibinadamu na kuangamiza wote wale waendelezao vita hivyo. Hii ni vita ya Mungu ya kuleta amani ya kweli kwa wale wapendao amani. Ndiyo, Har–Magedoni inakuja kama vile ambavyo Yehova amekusudia. Haitachelewa. Nabii wake Habakuki alipuliziwa kuandika, hivi: “Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.” (Habakuki 2:3) Kwa sababu ya hisia zetu za kibinadamu, huenda ikaonekana kuwa imekawia, lakini Yehova hufuata ratiba yake. Har–Magedoni itafyatuka kwa saa ambayo Yehova ameamua kimbele.
13. Mungu atashughulikaje na yule mkosaji halisi, Shetani Ibilisi?
13 Hatua hiyo ya kukata maneno itaondoa mambo yote yanayozuia amani ya kweli! Lakini ili amani iimarishwe kwa uthabiti, ni lazima jambo jingine lifanywe—kuondolewa kwa mmoja anayesababisha migawanyiko, chuki, na zogo. Na hilo hasa ndilo jambo ambalo Biblia hutoa unabii kwamba litafuata—kutiwa kwa Shetani, mchochezi wa vita na baba wa uwongo, katika abiso. Mtume Yohana aliona tukio hili katika ono la kiunabii, kama ilivyorekodiwa kwenye Ufunuo 20:1-3: “Nikaona malaika akiteremka kutoka mbinguni mwenye ufunguo wa abiso na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Naye akalikamata joka kubwa, nyoka wa awali, aliye Ibilisi na Shetani, na kumfunga kwa miaka elfu. Naye akamvurumisha ndani ya abiso na kuifunga na kuitia muhuri juu yake, ili asipate kuongoza mataifa vibaya tena kamwe mpaka miaka elfu ilipokuwa imekwisha.”
14. Tendo la Yehova lenye shangwe ya ushindi dhidi ya Shetani laweza kufafanuliwaje?
14 Hii si ndoto; ni ahadi ya Mungu—na Biblia husema hivi: “Haiwezekani Mungu kusema uwongo.” (Waebrania 6:18) Kwa njia hiyo Yehova aliweza kusema kupitia nabii wake Yeremia hivi: “‘Mimi ni Yehova, Yule ambaye hudhihirisha fadhili-upendo, haki na uadilifu katika dunia; kwa kuwa mimi hupendezwa na mambo haya,’ ni usemi wa Yehova.” (Yeremia 9:24, NW) Yehova hutenda kwa haki na uadilifu, naye hupendezwa na amani ambayo ataleta duniani.
Utawala wa Mkuu wa Amani
15, 16. (a) Ni nani anayechaguliwa na Yehova kutawala akiwa Mfalme? (b) Utawala huo unafafanuliwaje, na ni nani watakaoshiriki katika utawala huo?
15 Ili kuhakikisha kwamba amani ya kweli itakuja kwa wote wale wanaoishi chini ya mpango wake wa Ufalme, Yehova amempa utawala yule Mkuu wa Amani wa kweli, Yesu Kristo, kama ilivyotabiriwa kwenye Isaya 9:6, 7: “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme [“Mkuu,” NW] wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe. . . . Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.” Mtunga-zaburi pia aliandika kiunabii juu ya utawala wenye amani wa Mesiya: “Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.”—Zaburi 72:7.
16 Kwa kuongezea, ndugu za Kristo 144,000 waliotiwa mafuta kwa roho watakuwa wakitawala pamoja naye mbinguni. Hawa ndio warithi-washirika pamoja na Kristo ambao Paulo aliandika hivi juu yao: “Kwa upande wake, Mungu apaye amani atamponda-ponda Shetani chini ya miguu yenu upesi. Fadhili isiyostahiliwa ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi.” (Waroma 16:20) Ndiyo, hawa watashiriki kutoka mbinguni katika ushindi wa Kristo juu ya mchochea-vita, Shetani Ibilisi!
17. Ni lazima tufanye nini ili kuirithi amani ya kweli?
17 Kwa hiyo basi swali ni, Ni lazima ufanye nini ili urithi amani ya kweli? Amani ya kweli yaweza kuja tu kwa njia ya Mungu, na ili uipate lazima uchukue hatua chanya. Ni lazima umkubali Mkuu wa Amani na kumwendea. Hilo lamaanisha kwamba ni lazima umkubali Kristo katika fungu lake akiwa Mkombozi na Mfidi wa jamii ya kibinadamu yenye dhambi. Yesu mwenyewe alisema maneno haya yajulikanayo sana: “Mungu aliupenda ulimwengu sana hivi kwamba akatoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele.” (Yohana 3:16) Je, uko tayari kudhihirisha imani katika Kristo Yesu akiwa Wakili wa Mungu wa kuleta amani ya kweli na wokovu? Hakuna jina jingine lolote chini ya mbingu ambalo laweza kuimarisha amani na kuihakikisha. (Wafilipi 2:8-11) Kwa nini? Kwa sababu Yesu ni Mchaguliwa wa Mungu. Yeye ndiye mjumbe wa amani aliye mkubwa kupita wote waliopata kutembea duniani. Je, utamsikiliza Yesu na kufuata kielelezo chake?
18. Twapaswa kufanya nini katika kuitikia maneno ya Yesu yaliyorekodiwa kwenye Yohana 17:3?
18 ‘Hii yamaanisha uhai udumuo milele,’ Yesu akasema, “wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.” (Yohana 17:3) Sasa ndio wakati wa kuendelea kutwaa ujuzi sahihi kwa kuhudhuria kwa ukawaida mikutano ya Mashahidi wa Yehova kwenye Jumba la Ufalme. Mikutano hiyo yenye kuelimisha itakuhamasisha ushiriki ujuzi wako na tumaini lako na wengine. Wewe pia waweza kupata kuwa mjumbe wa amani ya Mungu. Waweza kufurahia amani sasa kwa kumtumaini Yehova Mungu, kama ilivyotaarifiwa kwenye Isaya 26:3 kulingana na tafsiri ya New International Version: “Utamweka katika amani kamilifu yule ambaye akili yake ni thabiti, kwa sababu yeye hukutumaini wewe.” Wapaswa umtumaini nani? “Mtumainini Yehova, nyinyi watu, nyakati zote, kwa kuwa katika Yah Yehova mna Mwamba wa nyakati zisizo dhahiri.”—Isaya 26:4, NW.
19, 20. Ni jambo gani linalowangojea wale leo wanaotafuta sana amani na kuifuatia?
19 Chukua msimamo wako sasa kwa ajili ya uhai udumuo milele katika ulimwengu mpya wa Mungu wenye amani. Kwenye Ufunuo 21:3, 4, Neno la Mungu hutuhakikishia: “Tazama! Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao, nao watakuwa vikundi vya watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.” Je, huo sio wakati ujao wenye amani unaotamani sana?
20 Basi kumbuka kile ambacho Mungu ameahidi. “Wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani. Umwangalie sana mtu mkamilifu, umtazame mtu mnyofu, maana mwisho wake mtu huyo ni amani.” (Zaburi 37:11, 37) Siku hiyo yenye furaha itakapofika, na tuseme kwa shukrani, “Hatimaye amani ya kweli! Shukrani kwa Yehova Mungu, chanzo cha amani ya kweli!”
-