Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Viuavisumbufu Huua Zaidi ya Wadudu
    Amkeni!—1999 | Februari 22
    • “NI BORA sana,” asema mkulima Domingos dos Santos atazamapo mazao yake ya mihogo kwenye shamba lake lililoko kusini mwa Brazili. Ana sababu ya kuridhika. Majani ya mimea yake yanaonekana kana kwamba hakuna mdudu mharibifu ambaye amewahi kuyavamia. Je, ni fanikio jingine la kemikali za kuua wadudu? Sivyo. “Mwaka uliopita na mwaka huu,” asema Domingos, “sikuhitaji kununua dawa ya kuua wadudu yoyote.”

      Domingos ni mshiriki wa kikundi kinachozidi kukua cha wakulima wasiotaka kutumia kemikali za viuavisumbufu ili kulinda mazao yao.a Badala yake, wanatumia njia ambazo huondoa au angalau hupunguza matumizi ya kemikali. “Ni njia gani hizo?” nilimwuliza Sandro Müller, mtaalamu wa kilimo ambaye amekuwa akifanya majaribio kwenye shamba la mti wa jamii ya mchungwa karibu na São Paulo. “Kwa nini ni jambo la akili kupunguza matumizi ya kifaa cha kunyunyizia dawa ya kuua wadudu mwanzoni?”

  • Viuavisumbufu Huua Zaidi ya Wadudu
    Amkeni!—1999 | Februari 22
    • IPM—Je, Ni Njia Badala?

      “IPM ni nini?” nilimwuliza profesa Evôneo Berti Filho, ambaye ni msimamizi wa Idara ya Elimu ya Wadudu kwenye Chuo Kikuu cha São Paulo katika Piracicaba na mtafiti mashuhuri katika njia za asili za kudhibiti visumbufu. Profesa Berti alieleza kwamba mradi wa IPM ni kupunguza matumizi ya dawa za kuua wadudu hadi kiwango kinachohitajiwa na kutumia tu dawa za kuua wadudu zinazoua wadudu waharibifu hususa. Kisha unyunyizaji unaodhibitiwa huongezewa nguvu na njia za asili za kudhibiti visumbufu.

      Njia moja ya kudhibiti visumbufu ni mbadilisho wa mimea. Kwa kielelezo, kutoka mwaka mmoja hadi mwingine, mkulima aweza kubadilisha mimea ya mhindi na mharagwe. Wadudu wanaopenda mhindi lakini wasiopenda mharagwe ama watakufa njaa ama watahamia kwenye maeneo yaliyo na mimea mingi ya mhindi. Kisha, wakati mwingine ambapo mhindi unapandwa, huenda wadudu wengi wakawa wameenda—angalau kwa muda fulani. Na wakati wadudu wanaopenda mhindi warudipo kwa wingi, mbadilisho wa mmea mwingine waweza kuwalazimisha waondoke tena.

      Sehemu nyingine ya IPM ni matumizi ya bakteria haribifu. Inatia ndani wakulima kutokeza wadudu, bakteria, virusi, kuvu, na maadui wengine wa kiasili wa visumbufu kuwa wasaidizi. Kwa kielelezo, watafiti Wabrazili walisema kwamba kiasili viwavi wengi walikufa baada ya kushikwa na kirusi kinachoitwa baculovirus. Walifikiri kwamba kwa kuwa kirusi hicho hakidhuru wanadamu, wangeweza kunyunyizia mimea umajimaji wenye kirusi hiki na ungefanya kazi kama kiuawadudu chenye bakteria dhidi ya viwavi wenye kula aina ya maharagwe meupe na mihogo. Walifanikiwa. Viwavi hao walikufa siku chache baada ya kutafuna mimea iliyokuwa imenyunyiziwa dawa hiyo. Zaidi ya hilo, viwavi waliokufa pia wanamwandalia mkulima silaha bila malipo kwa ajili ya mapigano ya wakati ujao. Jinsi gani?

      “Mkulima huwatia tu viwavi walioambukizwa na kufa ndani ya mashine ya kusagia vitu,” Profesa Berti alieleza, “huvisaga, huchuja mchanganyiko huo, na kuhifadhi umajimaji ndani ya friza.” Kisha mkulima huyeyusha umajimaji ulio na virusi, huuchanganya na maji, na kunyunyiza mchanganyiko huo kwenye mimea yake.

      Huenda dawa hii ya kuua wadudu yenye bakteria isiwe na matokeo ya haraka kama kemikali nyinginezo, lakini, ina mafanikio ya kiwango cha asilimia 90, asema mtafiti mmoja.

      Kuwashinda Wadudu—Njia ya Asili

      Kutokeza wadudu wenye faida kama wasaidizi ili kupigana na wadudu waharibifu ni sehemu nyingine ya maana ya udhibiti wa visumbufu kwa kutumia bakteria. Lakini, kujapokuwa jitihada za kusadikisha wakulima watumie njia hii ya kudhibiti wadudu, wakulima wengi katika Brazili na kwingineko bado wanasitasita kufanya hivyo. Kwa nini? Inaonekana kwamba wazo la kuachilia kimakusudi wadudu shambani huonekana kuwa lisilo la kiakili kwa wakulima kama vile kuachilia mende katika vyumba kungekuwa jambo lisilo la kiakili kwa wakazi wa jijini. “Kwa maoni ya wakulima wengi,” Profesa Berti aliniambia, “wadudu wote hula mimea. Kwa hakika mkulima hataki wadudu wengi zaidi.”

      Kwa wazi, basi, njia ya kudhibiti visumbufu kwa kutumia bakteria itapendwa tu wakati wakulima watakapoelewa kwamba wadudu fulani ni wasaidizi wao. Kwa kielelezo, wakulima wanaokuza matunda katika California, Marekani, walitafuta msaada wa mdudu bibi-arusi katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1800. Wakati huo, wadudu waharibifu, walioletwa bila kukusudia kutoka Australia, walikuwa wameshambulia na kuangamiza kabisa midimu na michungwa yote. Iliwachukua wadudu bibi-arusi muda unaopungua miaka miwili kudhibiti wadudu wavamizi, wakiokoa vijisitu vya miti aina ya michungwa vya California!

      Udhibiti Unaotokeza Badiliko

      Leo wakulima fulani huko Brazili wanagundua upya fungu linalotimizwa na joaninha (Joanna mdogo, jina la hapa la mdudu bibi-arusi) akiwa ‘mlinda usalama’ mwenye kutegemeka. “Wadudu Joaninha hupambana na chawa wa mimea katika ukuzi wa mti huu aina ya mchungwa,” Sandro aliniambia tulipokuwa tukitembea kandokando ya safu za michungwa katika shamba la miti aina ya michungwa lililo chini ya uangalizi wake. Alisimama kwenye mchungwa, akanyosha mkono kufikia kitawi chenye majani machanga, na kukikunja. Wadudu-wanyonyao, au chawa wa mimea—wadudu wavivu wanaotoshana na ncha ya pini—waliketi bila kujongea midomo yao ikishikilizwa katika majani, wakifyonza utomvu.

      Ingawa hivyo, chawa hawa, ni chakula cha ‘walinda usalama.’ Kwa kweli, miongoni mwa aina fulani za wadudu bibi-arusi, mdudu mmoja aweza kutafuna chawa 800 katika muda wote wa maisha yake. Je, hao wanatosha kutokeza badiliko? “Wanatosha,” akasema Sandro, “ikiwa utaacha nyasi za kutosha na magugu katikati ya miti aina ya michungwa iandae makao kwa wadudu bibi-arusi wengi sana na maadui wengine wa asili.” Zamani, wakati ambapo udhibiti wa kutumia bakteria haukutumiwa katika shamba hili la matunda, asema Sandro, kemikali za kuua wadudu zilinyunyizwa baada ya kila majuma mawili. Leo, kwa sababu ya maadui wa asili kama vile mdudu bibi-arusi na wadudu wengineo, uhitaji wa kunyunyizia dawa za kuua wadudu umepungua kufikia kila miezi miwili au mitatu.

      Mdudu bibi-arusi ni mojawapo tu wa marafiki wengi wa asili ambao wakulima hutegemea. Nyuki, nyingu, ndege, buibui, vyura, tukitaja tu wachache, wote ni washiriki wa jeshi linalofanya kazi daima kudhibiti visumbufu. Hata samaki husaidia kupunguza matumizi ya dawa za kuua wadudu waharibifu. Jinsi gani?

      Katika China, aripoti mtafiti Xiao Fan, wa Wizara ya Kilimo na Misitu katika Nanking, Mkoa wa Kiangsu, uhitaji wa dawa za kuua wadudu ulipunguzwa samaki walipoanza kulelewa katika mashamba yaliyojaa mpunga. Wakulima huvuta kamba iliyo juu ya mimea ili wadudu waanguke ndani ya maji. “Kwa sababu planthoppers hujifanya kuwa wamekufa wanapoanguka kutoka kwenye mipunga,” aeleza Fan, “wanaliwa na samaki kwa urahisi.”

      Kupunguza matumizi ya viuavisumbufu pia husaidia wadudu wenye faida waokoke. Wadudu hawa huungana na samaki wenye kula wadudu katika kupigana na visumbufu. Kwa msaada wa njia ya kudhibiti visumbufu kwa kutumia bakteria, asema Fan, sasa hakuna kutumia tena dawa za kuua wadudu kwa kiasi kikubwa. Afya na manufaa za kiikolojia, aongezea kusema, ni wazi.

      Ni kweli kwamba wakulima wanatumia IPM kwa sababu ya kuhangaikia zaidi uchumi badala ya ikolojia. Kwa vyovyote, kupunguza matumizi ya viuavisumbufu vilivyo ghali huokoa pesa, na hilo humaanisha faida zaidi—uvutio wa tufeni pote wa sikuzote. Hata hivyo, ikiwa faida zaidi za kiuchumi pia huongoza kwenye mazao machache yenye sumu na uharibifu wa mazingira wa kiwango kidogo, basi IPM hunufaisha wakulima na wanunuzi na vilevile ikolojia. Kama alivyoeleza mchunguzi mmoja, kwa kutumia IPM “kila mtu hunufaika.”

  • Viuavisumbufu Huua Zaidi ya Wadudu
    Amkeni!—1999 | Februari 22
    • Mimea Iliyobadilishwa kwa Nini Inabishaniwa?

      Taaluma ya mazingira ni silaha nyingine ya kupigana dhidi ya visumbufu. Huku ujuzi wa mwanadamu ukizidi kuongezeka kuhusu utendaji wa ndani wa molekyuli ya DNA, watafiti wameweza kuunganisha vipande vya DNA vya aina mbalimbali za mimea na kutokeza mimea yenye mfumo wa kinga wa kupigana na visumbufu.

      Mhindi ni kielelezo kimoja. Wabadilishaji-jeni walihamisha jeni kutoka chanzo kingine na kuiingiza kwenye DNA ya mhindi. Kisha jeni iliyoingizwa, ilitokeza protini ambayo ilithibitika kuwa yenye kufisha visumbufu. Tokeo ni mhindi wenye kudhibitiwa na jeni ambao haushindwi na wadudu maadui.

      Hata hivyo, mimea ambayo jeni zake zimebadilishwa inabishaniwa. Wapinzani wanabisha kwamba mimea hiyo huenda inawafanya watu wawe wagonjwa au kwamba mimea iliyobadilishwa ingeweza kuwa magugu yenye kusitawi. Wanasayansi fulani wanaonya kwamba mimea yenye jeni ziwezazo kuua wadudu waharibifu itachochea visumbufu viikinze. “Twapaswa kusawazisha shauku yetu kuhusu ubadilishaji wa jeni,” aonya mtaalamu wa elimu ya wadudu Berti. “Je, mwakumbuka jinsi watu walivyosisimuka katika miaka ya 1950 wakati dawa za kuua wadudu ziliposifiwa kuwa kitu cha ajabu sana? Leo twajua kwamba si kweli. Dawa za kuua wadudu za ajabu zimetokeza wadudu wa ajabu. Ni nani ajuaye matatizo yatakayotokezwa na mimea ya kisasa ya ajabu iliyobadilishwa jeni?”

      Hata ikiwa matatizo yote yanayohusiana na udhibiti wa bakteria yataweza kutatuliwa, watu fulani wanahangaishwa na suala la kiadili kuhusu jinsi ambavyo wanasayansi wanaingilia mifumo ya jeni. Wengine wanahisi kwamba taaluma ya mazingira yaweza kutatua matatizo ya zamani ya viuavisumbufu lakini badala yake ituache tukiwa na matatizo mapya ya kiadili.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki