Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Inamaanisha Nini Kuwa Maskini wa Kupindukia?
    Mnara wa Mlinzi—2011 | Juni 1
    • Inamaanisha Nini Kuwa Maskini wa Kupindukia?

      UMASKINI wa kupindukia ni jambo linalotishia maisha. Unamaanisha kukosa chakula cha kutosha, maji, na fueli (yaani, kuni, makaa, mafuta, n.k.), kutia ndani makao yanayofaa, matibabu, na elimu. Umaskini unaathiri watu bilioni moja hivi, idadi ambayo ni karibu sawa na wakaaji wote nchini India. Hata hivyo, watu wengi katika maeneo kama vile Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini hawajawahi kuona mtu aliye maskini wa kupindukia. Hivyo, acheni tuone watu ambao ni maskini wa kupindukia.

      Mbarushimana anaishi Rwanda, barani Afrika, pamoja na mke wake na watoto wao watano. Mtoto wao wa sita alikufa kutokana na malaria. Anasema: “Baba yetu alihitaji kugawanya shamba lake kati yetu tukiwa watoto sita. Sehemu niliyogawiwa ilikuwa ndogo sana hivi kwamba ilinilazimu kuhamishia familia yangu mjini. Mimi na mke wangu tunafanya kazi ya kubeba magunia ya mawe na mchanga. Nyumba yetu haina madirisha. Tunachota maji kwenye kisima kimoja kilicho katika kituo cha polisi. Kwa kawaida tunapata mlo mmoja kila siku, lakini wakati hakuna kazi, tunakosa chakula kwa siku nzima. Hali inapokuwa hivyo mimi huondoka nyumbani, kwa kuwa siwezi kuvumilia kuwasikia watoto wangu wakilia kwa sababu ya njaa.”

      Victor na Carmen ni mafundi wa viatu. Wanaishi na watoto wao watano katika mji fulani wa mashambani nchini Bolivia. Wamekodi nyumba ndogo ya matofali ya udongo iliyochakaa. Nyumba hiyo ina paa linalovuja na haina umeme. Shule ambayo binti yao anasoma ina watoto wengi sana hivi kwamba ilimbidi Victor amtengenezee dawati ili aweze kujiunga na shule hiyo. Victor na mke wake wanatembea kilomita 10 ili kukata kuni wanazotumia kupikia chakula na kuchemshia maji ya kunywa. “Hatuna choo,” anasema Carmen. “Hivyo sisi hujisaidia kando ya mto. Pia mto huo unatumika kama mahali pa kuogea na kutupia takataka. Mara nyingi watoto wetu huwa wagonjwa.”

      Francisco na Ilídia wanaishi katika eneo la mashambani la Msumbiji. Mmoja kati ya watoto wao watano wadogo alikufa kutokana na malaria baada ya hospitali kukataa kumtibu. Francisco na mke wake hupanda mpunga na viazi vitamu katika shamba lao dogo na chakula hicho kinawatosheleza kwa miezi mitatu. Francisco anasema, “Wakati mwingine mvua inakosa kunyesha au wezi wanaiba mazao yetu, hivyo mimi ninakata na kuuza mianzi inayotumika katika ujenzi, kazi inayonisaidia kupata pesa kidogo. Pia, mimi na mke wangu tunatembea kwa muda wa saa mbili ili kukata kuni msituni. Kila mmoja wetu hubeba mzigo wa kuni—mmoja wa kupikia kwa juma zima na mwingine wa kuuza.”

      Watu wengi wanahisi kwamba kuna kasoro kubwa na pia ukosefu wa haki katika ulimwengu tunamoishi kwa sababu mtu 1 kati ya kila watu 7 anaishi maisha kama ya Mbarushimana, Victor, na Francisco, huku mabilioni ya wengine wakifurahia utajiri wa kupindukia. Wengine wamejaribu kurekebisha hali hiyo. Makala inayofuata inazungumzia jitihada zao na matumaini yao.

      [Picha katika ukurasa wa 2, 3]

      Carmen akichota maji mtoni akiwa pamoja watoto wake wawili

  • Jitihada za Kumaliza Umaskini
    Mnara wa Mlinzi—2011 | Juni 1
    • Jitihada za Kumaliza Umaskini

      KWA upande wao, tayari matajiri wamemaliza umaskini. Lakini jitihada za kuwaondolea wanadamu wote umaskini zimeshindwa nyakati zote. Kwa nini? Kwa sababu matajiri kwa ujumla hawataki yeyote au chochote kivuruge utajiri wao. Mfalme Sulemani wa Israeli la kale aliongozwa na roho ya Mungu kuandika: “Tazama! machozi ya wale wanaokandamizwa, lakini hawakuwa na mtu wa kuwafariji; nao wakandamizaji walikuwa na nguvu.”—Mhubiri 4:1.

      Je, watu wenye uwezo na mamlaka wanaweza kubadili jamii na kumaliza umaskini duniani? Sulemani aliandika: “Tazama! mambo yote yalikuwa ubatili na kufuatilia upepo. Lililopotoshwa haliwezi kunyooshwa.” (Mhubiri 1:14, 15) Tunaweza kuelewa jambo hilo vizuri kwa kuchunguza jitihada za siku hizi za kumaliza umaskini.

      Nadharia za Kumaliza Umaskini kwa Wote

      Katika karne ya 19, wakati mataifa kadhaa yalipokuwa yakijikusanyia mali kwa wingi kupitia biashara na viwanda, watu fulani mashuhuri walikuwa wakifikiria hali ya umaskini kwa uzito. Je, maliasili za dunia zingeweza kugawanywa kwa usawa zaidi?

      Watu wengine walifikiri kwamba usoshalisti au ukomunisti unaweza kutokeza jamii ya kimataifa yenye usawa, jamii ambayo ingegawanya mali zake kwa usawa. Bila shaka, matajiri hawakupendezwa na jambo hilo. Lakini watu wengi walivutiwa na mwito huu: “Kila mtu anapaswa kuchangia jamii kulingana na uwezo wake, nayo jamii imchangie kulingana na mahitaji yake.” Wengi walikuwa na matumaini kwamba ikiwa mataifa yote yangefuata usoshalisti, ulimwengu ungekuwa mahali panapofaa kabisa kuishi. Mataifa kadhaa tajiri yalianza kufuata sera fulani za usoshalisti na kuanzisha mpango wa kutoa huduma za kijamii bila malipo, yakiahidi kuwasaidia raia zake “kuanzia kuzaliwa mpaka kifo.” Mataifa hayo yanadai kwamba yamemaliza umaskini wa kupindukia miongoni mwa watu wake.

      Hata hivyo, usoshalisti haukufaulu hata kidogo kufikia kusudi lake la kuwa na jamii isiyo ya ubinafsi. Lengo la mfumo huo kwamba raia wangefanya kazi ili kuinufaisha jamii badala ya kujinufaisha wenyewe halikutimia. Watu fulani walichukia kuwasaidia maskini, wakisema kwamba ukarimu wao uliwafanya baadhi ya maskini wawe wavivu. Maneno haya ya Biblia yamethibitika kuwa ya kweli: “Hakuna mwanadamu aliye mwadilifu duniani ambaye huendelea kufanya mema na asifanye dhambi. . . . Mungu wa kweli aliwafanya wanadamu wakiwa wanyoofu, lakini wao wenyewe wametafuta mipango mingi.”—Mhubiri 7:20, 29.

      Mpango mwingine wa kumaliza umaskini ulipewa jina Ndoto ya Marekani, yaani, ndoto ya kuwa na mahali ambapo kila mtu aliye tayari kufanya kazi kwa bidii anaweza kuwa tajiri. Mataifa mengi ulimwenguni yalianza kufuata sera, kama vile demokrasia na biashara huru, zilizoonekana kuiletea nchi ya Marekani utajiri. Lakini si mataifa yote yaliyofanikiwa kama Marekani kwa sababu bara la Amerika Kaskazini halikupata utajiri wake kutokana tu na mfumo wake wa kisiasa. Bara hilo lilipata utajiri kwa sababu lilikuwa na maliasili nyingi na pia uwezo wa kutumia njia za kibiashara za kimataifa. Zaidi ya hayo, mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu wenye ushindani mkali hautokezi tu watu wanaoshinda na kufanikiwa, bali pia wanaoshindwa na kuteseka. Je, mataifa tajiri yanaweza kutiwa moyo yasaidie mataifa maskini?

      Mradi wa Marshall —Mbinu ya Kumaliza Umaskini?

      Ulaya iliathiriwa sana na Vita vya Pili vya Ulimwengu na watu wengi katika bara hilo wakakabiliwa na njaa. Serikali ya Marekani ilihangaishwa na jinsi nchi za Ulaya zilivyovutiwa na usoshalisti. Hivyo kwa miaka minne, Marekani ilitoa msaada wa pesa nyingi sana ili kufufua viwanda na kilimo katika nchi zilizokubali sera zake. Programu hiyo ya kuzisaidia nchi za Ulaya, iliyoitwa Mradi wa Marshall, ilionekana kuwa na mafanikio. Huko Ulaya Magharibi, uvutano wa Marekani uliongezeka, na umaskini wa kupindukia ukapungua sana. Je, hiyo ndiyo ingekuwa njia ya kumaliza umaskini duniani?

      Kufanikiwa kwa Mradi wa Marshall kuliichochea serikali ya Marekani kutoa msaada kwa nchi maskini duniani kote ili kuzisaidia kusitawisha kilimo, huduma za afya, elimu, na usafiri. Marekani ilikubali waziwazi kwamba ilitoa misaada hiyo ili kujifaidi yenyewe. Nchi nyingine pia zilijitahidi kueneza ushawishi wao kwa kutoa misaada. Miaka 60 baadaye, nchi hizo zilikuwa zimetumia pesa nyingi zaidi ya zile Marekani ilitumia katika Mradi wa Marshall, lakini matokeo ya jitihada zao yalikuwa yenye kuvunja moyo. Ni kweli kwamba mataifa fulani yaliyokuwa maskini yalipata utajiri mwingi, hasa huko Asia ya Mashariki. Hata hivyo, ingawa misaada hiyo ilisaidia kupunguza vifo vya watoto na kuwawezesha wengi wao kupata elimu, bado mataifa mengi yaliendelea kupambana na umaskini wa kupindukia.

      Kwa Nini Misaada ya Nchi za Nje Haijamaliza Umaskini?

      Lilithibitika kuwa jambo gumu zaidi kuyasaidia mataifa maskini kumaliza umaskini kuliko kufufua uchumi wa mataifa tajiri yaliyoathiriwa na vita. Tayari Ulaya ilikuwa na viwanda, biashara, na mfumo wa usafiri. Uchumi wake ulihitaji tu kurekebishwa. Katika nchi maskini, hata misaada ya nchi za nje ilipotumiwa kujenga barabara, shule, na hospitali, watu bado walikuwa maskini wa kupindukia kwa sababu nchi hizo maskini hazikuwa na biashara, maliasili, na uwezo wa kutumia njia za biashara.

      Ni vigumu kutatua matatizo yanayosababisha umaskini na yale ambayo umaskini unasababisha. Kwa mfano, magonjwa husababisha umaskini, nao umaskini husababisha magonjwa. Watoto wasipopata lishe bora wanaweza kudhoofika sana kimwili na kiakili hivi kwamba wanapokuwa watu wazima, wanashindwa kutunza watoto wao wenyewe. Pia, nchi tajiri zinapopeleka chakula cha ziada katika nchi maskini kama “msaada,” wakulima na wanaouza bidhaa za kilimo katika nchi hizo hupata hasara, jambo linalosababisha umaskini zaidi. Kutoa msaada wa pesa kwa serikali za nchi maskini kunaweza kutokeza tatizo lingine: Ni rahisi kuiba misaada kama hiyo, na hilo linaweza kutokeza ufisadi, nao ufisadi usababishe umaskini zaidi. Kimsingi, misaada ya nchi za nje hushindwa kumaliza umaskini kwa sababu haiondoi chanzo hasa cha umaskini.

      Chanzo cha Umaskini

      Umaskini wa kupindukia unatokea kwa sababu mataifa, serikali, na watu mmoja-mmoja wanajitahidi kuendeleza na kulinda faida zao za kibinafsi. Kwa mfano, viongozi wa nchi tajiri hawashughuliki sana na kumaliza umaskini duniani kwa sababu wanachaguliwa kidemokrasia na lazima wawafurahishe watu waliowachagua. Kwa hiyo, wanawazuia wakulima wa nchi maskini wasiuze mazao yao katika nchi tajiri ili kuwalinda wakulima wa nchi hizo tajiri wasipate hasara. Pia, viongozi wa nchi tajiri huwapa wakulima wao msaada mkubwa wa kifedha ili wauze mazao yao kwa faida kubwa zaidi ikilinganishwa na wakulima wa nchi maskini.

      Bila shaka, umaskini unasababishwa na mwelekeo wa watu na wa serikali wa kutaka kulinda faida za kibinafsi. Mwandikaji wa Biblia Sulemani alisema hivi: “Mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza.”—Mhubiri 8:9.

      Kwa hiyo, kuna tumaini lolote kwamba umaskini utaisha? Je, kuna serikali yoyote inayoweza kubadili mwelekeo wa mwanadamu?

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Sheria ya Kukabiliana na Umaskini

      Yehova Mungu aliwapa Waisraeli wa kale sheria ambazo kama wangezifuata wengi wao hawangekuwa maskini. Chini ya Sheria, kila familia, isipokuwa kabila la kikuhani la Lawi, ilipokea ardhi kama urithi. Ardhi hiyo ya familia ilikuwa salama kwa kuwa haingeweza kuuzwa milele. Baada ya kila miaka 50, ardhi yote ilipaswa kurudishwa kwa yule aliyeimiliki au kwa familia yake. (Mambo ya Walawi 25:10, 23) Ikiwa mtu angeuza ardhi yake kwa sababu ya ugonjwa, msiba, au uvivu, angerudishiwa ardhi hiyo bila malipo katika mwaka wa Yubile. Hakuna familia ambayo ingelemewa na umaskini miaka nenda miaka rudi.

      Pia, kwa huruma Sheria ya Mungu ilimruhusu mtu aliyepatwa na msiba ajiuze kuwa mtumwa. Angepewa mapema pesa ambazo angepata kwa kujiuza ili kulipia madeni yake. Kama hangekuwa amejikomboa kufikia mwaka wa saba, alipaswa kuachiliwa huru na kupewa mifugo na mbegu ili aweze kuanza kilimo tena. Zaidi ya hayo, ikiwa maskini angekopa pesa, Sheria ilikataza kutoza faida. Sheria pia iliwaagiza watu wasivune kingo za mashamba yao ili maskini waweze kuokota masalio. Hivyo, hakuna Mwisraeli angeombaomba.—Kumbukumbu la Torati 15:1-14; Mambo ya Walawi 23:22.

      Hata hivyo, historia inaonyesha kwamba Waisraeli fulani walikuwa maskini. Kwa nini? Waisraeli hawakutii Sheria ya Yehova. Kwa hiyo, kama ilivyo katika nchi nyingi, baadhi yao wakawa matajiri waliomiliki ardhi na wengine wakawa maskini wasio na ardhi. Baadhi ya Waisraeli walikuwa maskini kwa sababu watu fulani walipuuza Sheria ya Mungu na kutanguliza faida za kibinafsi tu.—Mathayo 22:37-40.

  • Habari Njema Kwa Maskini
    Mnara wa Mlinzi—2011 | Juni 1
    • Habari Njema Kwa Maskini

      NENO LA MUNGU linatuhakikishia: “Maskini hawatasahauliwa sikuzote.” (Zaburi 9:18) Biblia pia inasema hivi kumhusu Muumba wetu: “Unaufumbua mkono wako na kutosheleza tamaa ya kila kitu kilicho hai.” (Zaburi 145:16) Tumaini hilo linalopatikana katika Neno la Mungu si ndoto tu. Mungu Mweza Yote anaweza kuandaa chochote kinachohitajiwa ili kumaliza umaskini. Maskini wanahitaji nini?

      Mtaalamu fulani wa uchumi wa nchi za Afrika alisema kwamba nchi maskini zinahitaji “dikteta mwenye fadhili.” Alimaanisha kwamba ili kumaliza umaskini, kunahitajika mtawala mwenye mamlaka ya kuchukua hatua za kuumaliza, na mwenye fadhili zinazomsukuma kufanya hivyo. Tunaweza pia kuongezea kwamba mtu anayeweza kuwaondolea watu wote umaskini anapaswa kuwa mtawala wa dunia yote, kwa sababu mara nyingi umaskini wa kupindukia hutokana na kutokuwepo kwa usawa kati ya mataifa. Zaidi ya hayo, mtawala huyo anapaswa kuwa na uwezo wa kukabiliana na chanzo cha umaskini, yaani, mwelekeo wa mwanadamu wa kuwa na ubinafsi. Mtawala kama huyo anaweza kupatikana wapi?

      Mungu alimtuma Yesu akiwa na habari njema kwa maskini. Yesu aliposimama kusoma kuhusu mgawo, au kazi, aliyopewa na Mungu, alisema: “Roho ya Yehova iko juu yangu, kwa sababu alinitia mafuta kuwatangazia maskini habari njema.”—Luka 4:16-18.

      Habari Njema Ni Nini?

      Mungu amemweka Yesu kuwa Mfalme. Hizo kwa kweli ni habari njema. Yeye ndiye Mtawala anayefaa kabisa kumaliza umaskini kwa sababu (1) atatawala wanadamu wote na ana mamlaka ya kuchukua hatua zinazohitajika ili kuumaliza; (2) anawatendea maskini kwa huruma na anawafundisha wafuasi wake kuwajali; na (3) anaweza kuondoa chanzo cha umaskini ambacho ni mwelekeo tuliorithi wa kuwa na ubinafsi. Acheni tuchunguze sehemu hizo tatu za habari njema.

      1. Mamlaka ya Yesu juu ya mataifa yote Neno la Mungu linasema hivi kumhusu Yesu: “Akapewa utawala . . . ili vikundi vyote vya watu, vya mataifa na lugha vimtumikie yeye.” (Danieli 7:14) Hebu fikiria faida za kuwa na serikali moja tu duniani kote? Serikali kama hiyo inaweza kumaliza ugomvi na hali ya kung’ang’ania maliasili za dunia. Raia wote watafaidika. Yesu mwenyewe alituhakikishia kwamba atakuwa Mtawala wa ulimwengu wote, mwenye mamlaka ya kuchukua hatua. Alitangaza hivi: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”—Mathayo 28:18.

      2. Yesu anawahurumia maskini Wakati wa huduma yake yote duniani, Yesu aliwatendea maskini kwa huruma. Kwa mfano, mwanamke fulani aliyekuwa ametumia mali zake zote kulipia matibabu yake aligusa vazi la Yesu, akitazamia kuponywa. Alikuwa na mtiririko wa damu kwa miaka 12 na bila shaka alikuwa na upungufu mkubwa wa damu mwilini. Kulingana na Sheria, angemtia unajisi mtu yeyote aliyemgusa. Lakini Yesu alimwonyesha huruma. Alimwambia: “Binti yangu, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uwe na afya njema kutokana na ugonjwa wako wenye kuhuzunisha.”—Marko 5:25-34.

      Mafundisho ya Yesu yana uwezo wa kubadili mioyo ya watu ili watende kwa huruma pia. Kwa mfano, fikiria vile Yesu alivyomjibu mtu fulani aliyetaka kujua jinsi ya kumpendeza Mungu. Mtu huyo alijua kuwa Mungu anataka sisi tuwapende jirani zetu, lakini akamuuliza Yesu: “Ni nani kwa kweli aliye jirani yangu?”

      Katika jibu lake, Yesu alitoa mfano wa mtu aliyekuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko ambaye alinyang’anywa vitu na kuachwa akiwa “karibu kufa.” Kuhani aliyekuwa akishuka kwenye barabara hiyo, alipita upande ule mwingine. Mlawi naye akafanya vivyo hivyo. “Lakini Msamaria fulani aliyekuwa akisafiri katika barabara ile alikuja, akamkuta na, alipomwona, akamsikitikia.” Alisafisha majeraha ya mtu huyo, akampeleka kwenye nyumba ya wageni, na kumlipa mtu aliyekuwa akitunza nyumba hiyo ili amtunze. “Ni nani . . . alijifanya kuwa jirani kwa mtu aliyeanguka katikati ya wanyang’anyi?” Yesu akamuuliza. Naye akajibu, “Ni yule aliyemtendea kwa rehema.” Ndipo Yesu akamwambia: “Uwe ukifanya vivyo hivyo.”—Luka 10:25-37.

      Watu wanaokuwa Mashahidi wa Yehova wanajifunza mambo hayo ambayo Yesu alifundisha na kubadili mtazamo wao kuelekea kuwasaidia wenye uhitaji. Kwa mfano, mwandishi fulani kutoka Latvia aliandika kwenye kitabu chake, Women in Soviet Prisons, kuhusu ugonjwa uliompata alipokuwa akifanya kazi kwenye kambi ya gereza huko Potma katikati ya miaka ya 1960. “Wakati wote nilipokuwa mgonjwa [Mashahidi] walinitunza vizuri sana. Nilifurahia sana utunzaji wao.” Aliongeza kusema: “Mashahidi wa Yehova wanaona kuwa ni jukumu lao kumsaidia yeyote, hata awe wa dini au taifa gani.”

      Wakati matatizo ya kiuchumi yalipofanya Mashahidi wa Yehova fulani wapoteze kazi au mapato yao huko Ancón, Ekuado, Mashahidi wenzao waliamua kufanya jambo fulani ili kuwachangia pesa. Walipika chakula na kuwauzia wavuvi wanaorudi ufuoni baada ya kuvua samaki usiku (picha upande wa kulia). Wote walishirikiana, kutia ndani watoto. Walianza kupika saa saba usiku kila siku ili chakula kiwe tayari wakati wavuvi waliporudi saa kumi usiku. Pesa walizopata ziligawanywa kulingana na mahitaji ya kila mmoja.

      Visa kama hivyo vinaonyesha kwamba mfano na mafundisho ya Yesu yana uwezo wa kubadili mtazamo wa watu ili kuwasaidia walio na uhitaji.

      3. Uwezo wa Yesu wa kubadili mwelekeo wenye dhambi tuliorithi Mwelekeo wa mwanadamu wa kutenda kwa ubinafsi ni jambo ambalo sote tunajua na tunakubali lipo. Biblia inauita mwelekeo huo dhambi. Hata mtume Paulo aliandika: “Basi, mimi naona sheria hii katika hali yangu: kwamba ninapotaka kufanya yaliyo sawa, yaliyo mabaya yapo pamoja nami.” Kisha akaongeza: “Ni nani atakayeniokoa kutoka katika mwili unaopatwa na kifo hiki? Shukrani kwa Mungu kupitia Yesu Kristo.” (Waroma 7:21-25) Hapa Paulo alirejelea jinsi ambavyo Mungu kupitia Yesu, angewakomboa waabudu wa kweli kutoka katika mielekeo yenye dhambi waliyorithi, kama vile ubinafsi, ambao ndio chanzo kikuu cha umaskini. Angefanya hivyo jinsi gani?

      Muda fulani baada ya Yesu kubatizwa, Yohana Mbatizaji alimtambulisha akisema: “Ona, Mwana-Kondoo wa Mungu ambaye huondolea mbali dhambi ya ulimwengu!” (Yohana 1:29) Hivi karibuni, dunia itajaa watu waliokombolewa kutoka katika dhambi tuliyorithi, kutia ndani mwelekeo wetu wa kuwa na ubinafsi. (Isaya 11:9) Yesu atakuwa ameondoa chanzo cha umaskini.

      Tunafurahi kama nini tunapotafakari kuhusu wakati ambapo kila mtu atatimiziwa mahitaji yake! Neno la Mungu linasema: “Wataketi, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.” (Mika 4:4) Maneno hayo ni kama shairi linaloelezea wakati ambapo watu wote watakuwa na kazi yenye kuridhisha, usalama, na nafasi tele za kufurahia ulimwengu usio na umaskini. Mambo hayo yatamletea Yehova sifa.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki