-
Ulimwengu Uliogawanywa na UtajiriAmkeni!—2005 | Novemba 8
-
-
Ulimwengu Uliogawanywa na Utajiri
KATIKA sehemu ya pili ya karne ya 20, ulimwengu ulikumbwa na Vita Baridi na kugawanywa kisiasa katika sehemu tatu. Mataifa ya Kikomunisti yakiongozwa hasa na Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti, na mataifa yasiyo ya Kikomunisti yakiongozwa na Marekani, yalikabiliana kutoka pande mbili za Pazia la Chuma. Mataifa ambayo hayakuunga mkono upande wowote yalifanyiza Ulimwengu wa Tatu.
Hata hivyo, baadaye ilionekana kuwa dharau kuziita nchi hizo “Ulimwengu wa Tatu,” na mataifa hayo yakaanza kuitwa “mataifa ambayo hayajasitawi.” Baada ya muda, usemi huo pia ulionwa kuwa haufai, kwa hiyo wataalamu wa uchumi wakaanza kutumia usemi “nchi zinazositawi.” Hivyo, usemi huo uliacha kukazia tofauti za kisiasa na kuanza kuonyesha tofauti za kiuchumi.
Sasa katika karne ya 21, ulimwengu haujagawanywa katika sehemu tatu za kisiasa zilizotajwa juu. Hata hivyo, bado kuna tofauti za kiuchumi na kiviwanda kati ya nchi zilizositawi na zinazositawi. Watalii kutoka nchi tajiri hukutana na maskini wanaojikakamua kulisha familia zao.
Kwa hiyo, swali hili linafaa: Je, ulimwengu utaendelea kugawanyika kiuchumi, au matajiri na maskini watapata kuwa na hali sawa ya maisha?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
© Qilai Shen/Panos Pictures
-
-
Pengo Kati ya Matajiri na MaskiniAmkeni!—2005 | Novemba 8
-
-
Pengo Kati ya Matajiri na Maskini
BILA kujali neno linalotumiwa kufafanua mataifa mbalimbali, mataifa yaliyoendelea sana na kusitawi kiviwanda na kiuchumi yana kiwango cha juu cha maisha, ilhali mataifa yaliyo na viwanda vichache, ambayo hayajasitawi sana kiuchumi, yana kiwango cha chini cha maisha. Ni kana kwamba mataifa hayo yako katika dunia mbili tofauti.
Bila shaka, hata katika taifa moja, viwango vya maisha vinaweza kutofautiana sana. Fikiria nchi tajiri ambazo zilitajwa katika makala iliyotangulia. Zina matajiri na maskini. Kwa mfano, nchini Marekani, asilimia 30 hivi ya mapato yote ya nchi hiyo hutumiwa na matajiri ambao ni asilimia 10. Wakati huohuo, familia maskini ambazo ni asilimia 20 lazima zijitosheleze kwa asilimia 5 tu ya jumla ya mapato hayo. Huenda ikawa kuna hali kama hiyo katika nchi unamoishi, hasa ikiwa watu wenye mapato ya kadiri ni wachache. Lakini hata serikali za nchi zilizo na watu wengi wenye mapato ya kadiri bado hazijafanikiwa kuziba kabisa pengo la kiuchumi kati ya matajiri na maskini.
Hakuna Jamii Isiyo na Matatizo
Hakuna jamii inayoweza kudai kwamba haina matatizo yoyote. Fikiria magumu yanayowakabili watu wanaoishi katika nchi maskini zaidi. Hawana huduma za afya za kutosha. Katika nchi 9 tajiri zaidi zilizotajwa katika sanduku kwenye ukurasa huu, kuna daktari 1 kwa watu 242 hadi 539, ilhali nchi 18 maskini zaidi zina madaktari wachache sana. Kuna daktari 1 kwa raia 3,707 hadi 49,118. Hivyo, inaeleweka ni kwa sababu gani watu katika nchi tajiri huishi kwa miaka 73 au zaidi, hali wale walio katika nchi maskini zaidi huishi kwa miaka inayopungua 50.
Pia katika nchi maskini, kuna uwezekano mdogo sana wa watu kupata elimu, na kwa sababu hiyo mara nyingi watoto watakuwa maskini vilevile. Ukosefu huo wa elimu unaonyeshwa na idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika. Asilimia 100 ya watu katika nchi 7 kati ya nchi 9 tajiri zaidi wanajua kusoma na kuandika (zile nyingine 2 zina asilimia 96 na 97). Katika nchi 18 maskini zaidi, watu wanaojua kusoma na kuandika ni kati ya asilimia 81 na asilimia 16, huku 10 kati ya nchi hizo zikiwa na chini ya asilimia 50.
Lakini wakazi wa mataifa tajiri pia hukabiliana na magumu fulani. Ingawa huenda watu wanaoishi katika nchi maskini wakakosa chakula cha kutosha, wale wanaoishi katika nchi zenye chakula tele, wanakufa kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na kula kupita kiasi. Kitabu Food Fight kinadai kwamba “kula na kunywa kupita kiasi kumekuwa tatizo kubwa zaidi ulimwenguni kuliko ukosefu wa chakula.” Nalo gazeti The Atlantic Monthly linasema: “Sasa Wamarekani milioni tisa hivi ni ‘wanene kupita kiasi,’ hilo linamaanisha kwamba uzito wao unapita kiasi kwa kilogramu 45 au zaidi, na kila mwaka, matatizo yanayotokana na unene unaopita kiasi husababisha vifo vya mapema vya watu 300,000 katika nchi hii.” Makala hiyohiyo inadokeza kwamba “huenda hivi karibuni unene unaopita kiasi ukawa tatizo kubwa zaidi la afya ulimwenguni kuliko njaa na magonjwa ya kuambukiza.”a
Ni kweli kwamba raia wa nchi tajiri wana kiwango cha juu cha maisha, lakini wakati huohuo, huenda wakaona mali kuwa muhimu zaidi kuliko kuwa na mahusiano mazuri na wengine, na hivyo kuona kwamba kuwa na mali ni muhimu kuliko kufurahia maisha. Wana mwelekeo wa kumwona mtu kuwa muhimu kwa kutegemea kazi, mshahara, au mali zake, badala ya ujuzi, hekima, uwezo, au sifa zake nzuri.
Ikikazia kwamba maisha rahisi ndiyo huleta furaha, kichwa cha makala moja katika gazeti la kila juma la Ujerumani Focus kiliuliza hivi: “Vipi Kuwa na Mali Chache Zaidi?” Makala hiyo ilisema: “Raia wengi wa nchi za Magharibi hawana furaha zaidi leo kuliko waliyokuwa nayo miaka mingi iliyopita, licha ya kwamba sasa wana mali nyingi zaidi. . . . Yaelekea mtu yeyote anayetamani kupata mali hatakuwa mwenye furaha.”
Kuwa na Usawaziko Kamili
Naam, ukweli ni kwamba, ingawa watu wanaoishi katika nchi tajiri na maskini hukabili hali fulani zinazofaa, wao pia hukabili hali zisizofaa. Ingawa huenda maskini wakaishi maisha yasiyo na anasa, matajiri wanaweza kuishi maisha yenye kutatanisha sana. Ingefaa sana iwapo maskini na matajiri wangejifunza kutoka kwa mmoja na mwenzake. Lakini je, ni jambo linalopatana na akili kufikiri kwamba siku moja kutakuwa na usawaziko kamili kati ya maskini na matajiri?
Kwa maoni ya kibinadamu, huenda ukahisi kwamba ingawa huo ni mradi mzuri, wanadamu hawawezi kuutimiza hata kidogo. Nayo mambo yaliyotukia zamani yanathibitisha ukweli wa jambo hilo. Hata hivyo, hali hiyo inaweza kurekebishwa. Huenda ikawa hujatilia maanani suluhisho bora zaidi la tatizo hilo. Suluhisho hilo ni lipi?
[Maelezo ya Chini]
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Huenda hivi karibuni unene unaopita kiasi ukawa tatizo kubwa zaidi la afya ulimwenguni kuliko njaa na magonjwa ya kuambukiza.”—The Atlantic Monthly
[Grafu katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Majina ya nchi Muda Ambao Wanaume Wanaojua
yamepangwa Wanatarajiwa Kusoma na
katika alfabeti Kuishi (Miaka) Kuandika (%)
Nchi Tisa Denmark 74.9 100
Tajiri Iceland 78.4 100
Zaidi Japani 78.4 100
Kanada 76.4 96.6
Luxembourg 74.9 100
Marekani 74.4 95.5
Norway 76.5 100
Ubelgiji 75.1 100
Uswisi 77.7 100
Nchi 18 Benin 50.4 37.5
Maskini Burkina Faso 43 23
Zaidi Burundi 42.5 48.1
Chad 47 53.6
Ethiopia 47.3 38.7
Guinea-bissau 45.1 36.8
Jam. ya Kongo 49 80.7
Madagaska 53.8 80.2
Malawi 37.6 60.3
Mali 44.7 40.3
Msumbiji 38.9 43.8
Niger 42.3 15.7
Nigeria 50.9 64.1
Rwanda 45.3 67
Sierra Leone 40.3 36.3
Tanzania 43.3 75.2
Yemen 59.2 46.4
Zambia 35.3 78
[Hisani]
Source: 2005 Britannica Book of the Year.
[Picha katika ukurasa wa 4]
© Mark Henley/Panos Pictures
-
-
Suluhisho Halisi kwa UmaskiniAmkeni!—2005 | Novemba 8
-
-
Suluhisho Halisi kwa Umaskini
MAMIA ya mamilioni ya watu ulimwenguni pote hujitahidi kujiruzuku kila siku licha ya ufukara. Ni wazi kwamba wanadamu wanahitaji serikali yenye uadilifu na isiyo na ufisadi ambayo inatamani kubadili ukosefu wa haki uliopo. Pia serikali hiyo lazima iwe na uwezo wa kutimiza makusudio yake mazuri. Je, ni jambo linalopatana na akili kutazamia wanadamu watokeze serikali kama hiyo?
Historia inathibitisha ukweli wa onyo hili la Biblia: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote.” (Zaburi 146:3) Je, umeona kwamba mara nyingi kutumaini serikali au viongozi wa kibinadamu hukatisha tamaa? Hata hivyo, tunaweza kumtumaini nani mwingine?
Kwa kweli, mamilioni ya watu wameomba wapate serikali yenye uadilifu itakayobadili hali hiyo ya ukosefu wa haki. Labda wewe pia umetoa sala hii ya kielelezo ambayo Yesu alifundisha: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako na litakaswe. Ufalme wako na uje. Mapenzi yako na yatendeke duniani kama ilivyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu kwa ajili ya siku hii; na utusamehe madeni yetu, kama vile ambavyo sisi pia tumewasamehe wadeni wetu. Na usituingize katika jaribu, bali utukomboe kutokana na yule mwovu.”—Mathayo 6:9-13.
Je, huo ndio Ufalme tunaohitaji? Je, ni wenye uadilifu na usio na ufisadi? Je, una uwezo wa kutosha kutimiza makusudio yake mazuri? Bila shaka, ndiyo! Mungu aliyeanzisha serikali hiyo, yaani, ‘Baba yetu aliye mbinguni,’ ni “Mungu mwadilifu na Mwokozi,” ambaye ni “mwadilifu katika kazi zake zote.” (Isaya 45:21; Danieli 9:14) Inasemekana hivi kumhusu: “Wewe umetakata sana usiweze kuona lililo baya,” kwa hiyo tunaweza kuwa na uhakika kwamba serikali yake haitakuwa na ufisadi kamwe. (Habakuki 1:13) Na kwa kuwa “Mungu hana ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye anamwogopa na kutenda uadilifu anakubalika kwake,” tunajua kwamba anapendezwa na hali njema ya kila mwanadamu duniani bila kumbagua yeyote.—Matendo 10:34, 35; Waroma 2:11.
Tayari Umesimamishwa na Unatenda!
Ingawa Ufalme wa Mungu ni serikali ya kimbingu, itaongoza mambo duniani ili kutimiza makusudi ya Mungu. Hilo linatia ndani kuondoa serikali za wanadamu zisizo kamilifu na mahali pake pachukuliwe na serikali kamilifu ya Mungu. Ahadi hii inatolewa katika andiko la Danieli 2:44: “Katika siku za wafalme hao [serikali], Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaharibiwa kamwe. Na ufalme huo hautapewa watu wengine wowote. Utazivunja na kuzikomesha falme hizi zote, nao utasimama mpaka wakati usio na kipimo.”
Chini ya uongozi wa Ufalme huo, hatimaye mapenzi ya Mungu yatafanywa mbinguni na duniani pia. Inatia moyo sana kujua kwamba serikali hiyo inaweza kuondoa kabisa ukosefu wa usawa uliopo ambao umechangia pengo kubwa kati ya walio matajiri zaidi na maskini zaidi. Hakutakuwa tena na matajiri wachache na maskini wengi.
Inafurahisha sana kujua kwamba tayari serikali ya Mungu ya kimbingu imesimamishwa ili isuluhishe matatizo hayo milele. Kronolojia ya Biblia na matukio ya ulimwengu yanaonyesha wazi kwamba mwaka wa 1914 ndio wakati ambapo serikali ya Mungu ilisimamishwa mbinguni.a Hivyo, kwa karne moja hivi, imekuwa ikiweka msingi wa ulimwengu mpya wenye uadilifu.
Wale ambao wametambua kwamba Ufalme huo umesimamishwa na wanaotii mwongozo wake, hawana ubaguzi. Mashahidi wa Yehova wanahubiri karibu katika nchi zote. Raia wa nchi hizo, wawe ni matajiri au maskini wanapewa nafasi ya kujifunza jinsi wanavyoweza kupata uzima wa milele. (Yohana 17:3) Mashahidi wa Yehova hawaruhusu tofauti za kiuchumi ziamue daraka ambalo mtu atapewa katika makutaniko yao. Watu hawaheshimiwi kwa sababu ya mali zao. Badala yake, wanaheshimiwa kwa sababu ya sifa zao. Viwango vya kiroho huonwa kuwa muhimu zaidi kuliko viwango vya kimwili.
Je, ungependa kujua jinsi unavyoweza kuishi chini ya serikali hiyo yenye uadilifu? Basi anza kufanya uchunguzi leo. Jifunze jinsi unavyoweza kutazamia kuishi kwa shangwe wakati ambapo ulimwengu hautagawanywa tena na utajiri.
[Maelezo ya Chini]
a Ona kitabu Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele, ukurasa wa 95 hadi 107, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Wote Ni Ndugu, Wawe Matajiri au Maskini
◼ Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Mashahidi wengi wa Yehova huko Ulaya na Asia walihitaji chakula, mavazi, na makao. Mashahidi wa nchi nyingine walituma mavazi na chakula kingi sana kwa ndugu zao wa kiroho huko Ulaya, Ufilipino, na Japani. Mashahidi nchini Marekani na Kanada walitoa misaada ambayo ingetumwa nchini Austria, Chekoslovakia (ambayo sasa ni Jamhuri ya Cheki na Slovakia), Finland, Hungaria, Italia, Poland, Rumania, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Uholanzi, Uingereza, na Ujerumani.
[Picha]
Marekani
Uswisi
Ujerumani
◼ Hivi karibuni zaidi, katika kiangazi cha 1994, kikundi cha wajitoleaji Mashahidi kutoka Ulaya walisafirisha upesi misaada ambayo ndugu na dada zao Wakristo walihitaji barani Afrika. Kambi na hospitali zilizopangwa vizuri zilijengwa kwa ajili ya wakimbizi wa Rwanda. Kiasi kikubwa sana cha nguo, blanketi, chakula, na vichapo vya Biblia kilitumwa ili kuwasaidia watu zaidi ya 7,000 walioathiriwa. Idadi hiyo ilikuwa karibu mara tatu ya idadi ya Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda wakati huo.
◼ Miaka miwili baadaye, katika mwaka wa 1996, vita vilizuka katika eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mazao yaliharibiwa, maghala ya chakula yakaporwa, na misaada ikazuiwa isifike mahali ilipohitajiwa. Watu wengi wangeweza kupata mlo mmoja tu kwa siku, na hivyo walipatwa na utapiamlo na magonjwa. Mashahidi wa Yehova huko Ulaya walichukua hatua haraka. Kikundi cha kutoa msaada cha Mashahidi kilichotia ndani madaktari, walisafirishwa kwa ndege wakiwa na dawa na pesa. Kufikia Juni 1997, Mashahidi nchini Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi walikuwa wamechanga kilogramu 500 za dawa, tani 10 za biskuti zenye protini nyingi, tani 20 za vyakula vingine, tani 90 za nguo, jozi 18,500 za viatu, na blanketi 1,000. Vitu hivyo viligharimu karibu dola 1,000,000.
◼ Mbali na kutosheleza mahitaji ya kimwili, Mashahidi wa Yehova hupendezwa hata zaidi kuwasaidia watu kiroho. Hilo linaonyeshwa na tamaa yao ya kujenga Majumba ya Ufalme yanayotumiwa kama mahali pa kujifunzia Biblia. Iliripotiwa hivi mwaka wa 1997: “Kwa msaada wa akina ndugu kutoka nchi nyingine, Sosaiti [ya Mnara wa Mlinzi] imesaidia kujenga Majumba mapya ya Ufalme 413 na kurekebisha majumba mengine 727 katika muda wa miezi minne tu katika nchi 75.” Iliripotiwa hivi kufikia mwaka wa 2003: “Kati ya nchi za Ulaya ambazo zimenufaika na mpango wa kusaidia kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi zenye uhitaji ni Rumania, ambako Majumba ya Ufalme 124 yamejengwa tangu Julai 2000. Kwa kutumia muundo uleule kwa ajili ya karibu Majumba yake yote ya Ufalme, Ukrainia ilijenga majumba 61 katika mwaka wa 2001, na mengine 76 katika mwaka wa 2002. Kwa msaada wa pesa zilizochangwa kwa ajili ya Hazina ya Majumba ya Ufalme, mamia ya Majumba ya Ufalme yamejengwa nchini Bulgaria, Kroatia, Makedonia, Moldova, Serbia na Montenegro, na Urusi.”
[Picha]
Bulgaria
Kroatia
Romania
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mjitoleaji akiwatunza wakimbizi wawili mayatima
[Hisani]
© Liba Taylor/Panos Pictures
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mashahidi wa Yehova wanaeneza ujumbe unaotoa tumaini
[Picha katika ukurasa wa 10]
Ufalme wa Mungu utamaliza umaskini
-