Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ni Nani Wanaofurahia Nyakati Nzuri Kiuchumi?
    Amkeni!—2007 | Mei
    • Ni Nani Wanaofurahia Nyakati Nzuri Kiuchumi?

      TUNAISHI katika ulimwengu wenye utajiri. Je, ni rahisi kuamini hilo? Kwa kweli, mataifa fulani yana pesa nyingi kuliko yanavyoweza kutumia. Imekadiriwa kwamba jumla ya mapato ya nchi zote ulimwenguni kutokana na bidhaa na huduma zilizotolewa katika mwaka wa 2005, ilizidi dola trilioni 60. Ikiwa pesa hizo zingegawanywa, kila mtu ulimwenguni angepata dola 9,000. Na mapato hayo yanaongezeka.

      Lakini takwimu hizo zinatofautiana sana na hali halisi. Kulingana na kichapo cha karibuni cha Umoja wa Mataifa, watu watatu matajiri zaidi ulimwenguni wana mali nyingi zaidi kuliko jumla ya mapato ya mataifa 48 maskini zaidi. Na ripoti ya shirika la Mpango wa Ustawi wa Umoja wa Mataifa inasema kwamba watu bilioni 2.5 wanapata chini ya dola mbili kila siku. Mamia ya mamilioni hawapati chakula cha kutosha na hawawezi kupata maji safi ya kunywa.

      Nchini Marekani, wanasoshiolojia wanachunguza kikundi cha watu ambao wanaelekea kuwa maskini. Watu hao wanakabili hatari ya kuwa maskini. Zaidi ya watu milioni 50 nchini humo wako katika hali hiyo licha ya utajiri mkubwa wa nchi hiyo.

      Kwa nini pesa nyingi sana zinamwagika katika hazina na akaunti za benki huku mamia ya mamilioni ya maskini wakizidi kuzama katika umaskini? Kwa nini watu wengi hawafaidiki kutokana na utajiri wa ulimwengu unaozidi kuongezeka?

      [Blabu katika ukurasa wa 3]

      Watu watatu matajiri zaidi ulimwenguni wana mali nyingi zaidi kuliko jumla ya mapato ya mataifa 48 maskini zaidi

      [Picha katika ukurasa wa 2, 3]

      Watoto walioajiriwa katika kiwanda hiki cha matofali hulipwa senti 50 za Marekani kwa siku

      [Hisani]

      © Fernando Moleres/ Panos Pictures

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

      © Giacomo Pirozzi/Panos Pictures

  • Kwa Nini Kuna Maskini Wengi Katika Ulimwengu Wenye Utajiri?
    Amkeni!—2007 | Mei
    • Kwa Nini Kuna Maskini Wengi Katika Ulimwengu Wenye Utajiri?

      “MNA maskini pamoja nanyi sikuzote,” akasema Yesu Kristo katika karne ya kwanza W.K. (Mathayo 26:11) Sikuzote kumekuwa na maskini wengi sana, kuanzia wakati wa Yesu hadi wakati wetu. Lakini kwa nini kuna maskini wengi katika ulimwengu wenye utajiri mwingi sana?

      Wengine waamini kuwa watu huwa maskini kwa sababu ya kufanya maamuzi mabaya. Huenda hilo linaweza kuwa kweli katika visa fulani. Wale ambao huchagua kutosheleza tamaa za kileo, dawa za kulevya, na kucheza kamari hupoteza mali zao kwa urahisi. Lakini si watu wote huwa maskini kwa sababu ya kufanya maamuzi mabaya.

      Watu wengi wamepoteza kazi kwa sababu ya mabadiliko ya kibiashara. Ni wengi pia wanaofanya kazi ambao wametumia pesa zote walizoweka akiba kulipia gharama za matibabu zinazozidi kuongezeka. Na mamia ya mamilioni ya watu maskini katika nchi zinazoendelea wanajikuta katika hali hiyo bila kupenda kwao. Kama hoja zinazofuata zinavyoonyesha, mara nyingi umaskini hutokea bila kusababishwa na watu wanaoathiriwa.

      Kujifunza Kutokana na Historia

      Katika miaka ya mapema ya 1930, ulimwengu ulikumbwa na hali ngumu za kiuchumi ambazo zilikuja kuitwa Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi. Katika nchi moja, mamilioni ya watu walipoteza kazi na familia nyingi sana zikapoteza makao. Huku watu wengi wakifa njaa, wakulima walikuwa wakimwaga maziwa mengi sana katika mitaro na maofisa wa serikali waliwaamuru wakulima waue wanyama wengi wa kufugwa.

      Kwa nini bidhaa hizo ziliharibiwa? Miongozo ya mfumo wa kiuchumi ilielekeza kwamba bidhaa za shambani na bidhaa nyingine ziuzwe kwa faida fulani. Maziwa, nyama, na nafaka zingewafaidi sana maskini. Lakini kwa kuwa vyakula hivyo havikuwaletea mapato walioviuza, vilionekana kuwa havina faida na hivyo vikaharibiwa.

      Kulikuwa na ghasia katika majiji mengi kwa sababu ya chakula. Watu fulani ambao hawakuwa na pesa za kununulia familia zao chakula, walianza kuiba kwa kutumia mabavu ili kupata chakula. Wengine walikufa njaa. Mambo hayo yalitukia nchini Marekani. Mwanzoni mwa huo Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi, mfumo wenye nguvu wa kiuchumi wa nchi hiyo haukuwasaidia watu wenye mapato ya chini. Badala ya kutanguliza mahitaji ya raia wote ya chakula, makao, na kazi, mfumo huo uliona mahitaji hayo kuwa yasiyo na maana yakilinganishwa na kupata faida.

      Hali za Leo

      Mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu uliokoka huo Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi, na sasa watu wengi wanaonekana kuwa matajiri na salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hata hivyo, licha ya utajiri mwingi uliopo, mara nyingi maskini hawapati nafasi za kuboresha hali zao maishani. Katika nchi fulani, ripoti za njaa na umaskini ni za kawaida sana hivi kwamba watu wamechoka kuzisoma. Hata hivyo, wakimbizi wanapokufa njaa kwa sababu ya vita, vyakula vilivyohifadhiwa vinapooza kwa sababu za kisiasa, na masoko yanapoongeza bei za mahitaji ya lazima hivi kwamba maskini hawawezi kuzimudu, tunajionea matokeo ya mfumo ambao umeshindwa kutosheleza mahitaji ya maskini. Mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu hupuuza mamilioni ya maskini.

      Kwa kweli, hakuna mfumo wa kiuchumi wa wanadamu ambao umetosheleza mahitaji ya msingi ya wanadamu wote. Karne 30 zilizopita, mtu mmoja aliyekuwa akitazama hali za ulimwengu alisema hivi: “Nami nikarudi nipate kuona matendo yote ya uonevu yanayofanywa chini ya jua, na, tazama! machozi ya wale wanaokandamizwa, lakini hawakuwa na mtu wa kuwafariji; nao wakandamizaji walikuwa na nguvu, hivi kwamba hawakuwa na mtu wa kuwafariji.” (Mhubiri 4:1) Ingawa leo kuna utajiri mwingi, bado kuna matendo mengi ya uonevu wa kiuchumi.

      Sasa mamilioni hawana nafasi ya kujiinua kimaisha kutoka katika shimo la umaskini. Lakini watu wengi wamejifunza kukabiliana na matatizo yao ya kiuchumi kwa mafanikio. Pia wamejifunza kutazamia maisha mazuri wakati ujao.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Jitihada ya Kuendelea Kuishi

      Katika kitabu chake (The Working Poor—Invisible in America) kuhusu maskini wanaofanya kazi, mtunzi na mwandishi wa habari David K. Shipler anatusaidia kutambua jinsi watu fulani nchini Marekani huishi katika hali ya hatari kwa sababu ya umaskini. Anatoa mfano wa mama anayeishi katika nyumba duni ambaye mtoto wake anaugua ugonjwa wa pumu. Kwa sababu ya kuishi chini ya hali hizo ugonjwa huo unazidi kuwa mbaya zaidi na hilo humfanya mama amkimbize hospitali. Anaposhindwa kulipa gharama kubwa ya hospitali, riba ya mkopo wa mama huyo huongezeka na hivyo hawezi kulipia tena gari lake lililo katika hali nzuri. Kwa sababu hiyo yeye huanza kuchelewa kazini na hivyo nafasi zake za kupandishwa cheo na kupokea mapato bora zaidi hupungua basi analazimika kuendelea kuishi katika nyumba hiyo duni. Mtoto huyo na mama yake wanaishi wakitazamia chochote kibaya, hata ingawa wanaishi katika taifa tajiri zaidi duniani.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Je, Inatosha Kuwa na Nia Njema?

      Mnamo Novemba 1993, ndani ya jengo la serikali huko Washington, D.C., kikundi cha maofisa wa serikali kilikuwa kikijaribu kutatua tatizo kubwa. Wakiwa na mamia ya mamilioni ya dola, maofisa hao walitaka kuwasaidia watu wasio na makao nchini Marekani. Walipokuwa wakizungumza, polisi, wazima-moto, na wafanyakazi wa kitiba wanaoshughulikia hali za dharura walikusanyika katika kituo cha basi upande ule mwingine wa barabara. Wafanyakazi wa gari la wagonjwa walikuwa wakichukua mwili wa mwanamke ambaye hakuwa na makao. Alikuwa amekufa mbele ya jengo la Wizara ya Marekani ya Makao na Ustawi wa Majiji (HUD), ambayo ni wizara ya serikali yenye jukumu la kuwasaidia watu wasio na makao.

      Baadaye mwandishi wa habari wa gazeti The New York Times alimhoji mfanyakazi wa wizara hiyo, ambaye alizungumza kuhusu idadi ya watu na magari yaliyokuja kumshughulikia mwanamke huyo alipokufa: “Inashangaza kuona ni msaada mwingi kadiri gani mtu hupata anapokufa, lakini hapewi msaada wowote akiwa hai.”

      [Picha katika ukurasa wa 4, 5]

      Mhamiaji akiwa na watoto wake watatu wakati wa ule Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi katika miaka ya 1930

      [Hisani]

      Dorothea Lange, FSA Collection, Library of Congress

      [Picha katika ukurasa wa 6, 7]

      Katika kiwanda kama hiki, mshahara wa wastani ni dola 14 kwa mwezi, nao wafanyakazi wanaweza kufanyishwa kazi saa 70 kwa juma

      [Hisani]

      © Fernando Moleres/Panos Pictures

  • Kuna Tumaini Gani kwa Maskini?
    Amkeni!—2007 | Mei
    • Kuna Tumaini Gani kwa Maskini?

      HAKUNA ubaya wowote wa kufanya kazi ngumu ili kupata riziki, ikiwa mtu anayefanya kazi hiyo anapata malipo yanayofaa. Ona maelezo haya ya mwandishi fulani wa Biblia: “Nimekuja kujua kwamba hakuna jambo lingine bora . . . kuliko mtu kufurahi . . . na pia kwamba kila mtu ale, naam, anywe na kuona mema kwa ajili ya kazi yake yote iliyo ngumu. Hiyo ndiyo zawadi ya Mungu.”—Mhubiri 3:12, 13.

      Lakini kama tulivyoona, mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu hutazamia watu wafanye kazi ngumu lakini wanapata malipo yasiyotosha. Wengi hubaki wakiwa maskini, waking’ang’ana na maisha kila siku. Ni nadra sana wao “kufurahi” na “kufanya mema” kwa sababu ya maisha yao. Kuna utajiri mwingi sana ulimwenguni, lakini huenda nusu ya wanadamu hawafaidiki na utajiri huo.

      Mungu Anapendezwa na Maskini

      Muumba wa wanadamu, Yehova Mungu, hapendezwi na hali hiyo. Yehova anawahurumia maskini. Tunasoma hivi katika Biblia: “[Mungu] hatakisahau kilio cha wenye kuteseka.” (Zaburi 9:12) Yehova ni Mungu anayewajali maskini.

      Kumhusu Yehova, Biblia inasema: “Mtu mwenye taabu, mvulana asiye na baba, anajikabidhi kwako. Wewe mwenyewe umekuwa msaidizi wake.” (Zaburi 10:14) Ona jinsi mstari huo wa Biblia unavyowataja wanaoteseka kama mtu mmoja-mmoja.a Naam, Mungu humtazama kila mtu na kufikiria mahitaji yake. Kwake kila mtu ana thamani na anastahili uangalifu. Yehova anawaalika watu wote wajifunze kumhusu na wafurahie urafiki wake haidhuru hali yao ya kiuchumi.

      Jambo moja ambalo watu hujifunza kutoka kwa Mungu ni kuonyesha wengine huruma na hisia-mwenzi. Mashahidi wa Yehova hujiona kuwa familia kubwa ya kiroho. Wao huthaminiana, na kati yao kuna upendo wa kweli wa Kikristo. Wakati mmoja Bwana Yesu Kristo aliwaambia hivi wafuasi wake: “Ninyi nyote ni ndugu.” (Mathayo 23:8) Kwa hiyo, wote wanaokubali ibada ya kweli wanakuwa sehemu ya undugu usiobaguana kwa misingi ya utajiri. Kila mmoja humjali mwenzake, nao hutiana moyo nyakati za taabu.

      Biblia ina kanuni zinazoweza kumsaidia mtu kupunguza madhara ya umaskini. Maandiko yanaonyesha kwamba Mungu hushutumu kuchafua mwili, kama vile kwa kutumia tumbaku na kutumia kileo vibaya. (Methali 20:1; 2 Wakorintho 7:1) Mtu anayeishi kupatana na kanuni hizo huweka akiba ya pesa ambazo zingepotezwa kupitia mazoea mabaya. Yeye huepuka magonjwa yanayosababishwa na uvutaji wa sigara na ulevi, na gharama ya matibabu ambayo ingesababishwa na magonjwa hayo. Pia Biblia inawafundisha watu kukataa kufikiri kwa njia ya kimwili na pupa. (Marko 4:19; Waefeso 5:3) Mtu anapoheshimu Neno la Mungu kuhusiana na mambo hayo, yeye huepuka pia kupoteza pesa zake kwa kucheza kamari.

      Biblia hutoa kanuni zinazotusaidia kuishi vizuri hata tukiwa maskini. Ona mfano ufuatao:

      Katika nchi ambayo watu wengi sana hawana kazi, mwanamke anayefanya kazi katika kiwanda fulani alihatarisha kazi yake kwa kuomba ruhusa ya kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Msimamizi wake angemwachisha kazi mara moja. Badala yake, alimshangaza mwanamke huyo na wafanyakazi wenzake kwa kumpa ruhusa. Isitoshe, msimamizi huyo alimwambia angependa aendelee kufanya kazi katika kiwanda chake na akamsifu kwa kuwa “mfanyakazi mzuri.” Kwa nini?

      Mfanyakazi huyo ambaye ni Shahidi wa Yehova, anaishi kulingana na kanuni za Biblia. Akitamani “kujiendesha kwa unyoofu katika mambo yote,” hakusema uwongo au kuiba na hivyo akawa na sifa nzuri ya unyoofu. (Waebrania 13:18) Kupatana na kanuni iliyoongozwa kwa roho inayopatikana katika Wakolosai 3:22, 23, alifanya kazi yake “kwa nafsi yote.” Hilo linamaanisha alimtii mwajiri wake, na alihakikisha kwamba kila siku alifanya kazi kwa bidii ili astahili kulipwa.

      Bila shaka, tunaishi katika mfumo wa kiuchumi ambao unaongozwa na ubinafsi na jambo kuu ni kupata faida. Huenda wengine ambao wanaheshimu sana kanuni za Biblia wakahitaji kung’ang’ana ili kupata chakula, mavazi, na makao wanayohitaji. Lakini wana dhamiri safi mbele za Muumba nao wanatazamia kwa uhakika kwamba kutakuwa na wakati ujao mzuri, kwa sababu Yehova ni “Mungu anayetoa tumaini.”—Waroma 15:13.

      Suluhisho Kamili la Umaskini

      Biblia inafunua hisia zenye nguvu za Yehova dhidi ya wale wanaochochea kuteswa kwa maskini. Neno la Mungu lililoongozwa kwa roho linasema: “Ole wao wanaotunga masharti yenye kudhuru na wale ambao, wakiandika sikuzote, wameandika taabu tupu, ili kuwasukuma mbali watu wa hali ya chini kutoka kwenye kesi na kuwanyang’anya haki wale wanaoteseka . . . , ili wajane wawe nyara yao, na ili hata wapore wavulana wasio na baba!” (Isaya 10:1, 2) Iwe wanawapuuza maskini kwa kupenda au bila kujua, wale wanaoongoza mfumo wa kiuchumi wa jamii ya kibinadamu ni sehemu ya mfumo utakaoharibiwa na Mungu Mweza-Yote.

      Nabii Isaya anawauliza wanyanyasaji hao swali lenye uzito: “Nanyi mtafanya nini katika ile siku ya kukaziwa uangalifu na wakati wa uharibifu, utakapokuja kutoka mbali?” (Isaya 10:3) Yehova atawaangamiza watu hao kwa kuharibu mfumo usiofuatia haki wanaoendeleza.

      Lakini kusudi la Mungu linahusisha mengi zaidi ya kuchukua hatua dhidi ya wanyanyasaji. Atawapa wanadamu wenye mwelekeo unaofaa maisha yasiyokuwa na ukosefu wa haki. Atatumia mfumo bora zaidi wa kiserikali, naye atawaruhusu wanadamu kufurahia maisha yenye kuridhisha bila umaskini. Ili ufanikiwe wakati huo, hutahitaji kupata urithi mkubwa wa pesa, kujua watu wenye vyeo, au kuwa na ustadi wa kibiashara. Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba mabadiliko hayo yatatukia?

      Yesu Kristo ambaye Yehova amemweka rasmi atawale wanadamu, alitaja wakati huo kuwa “uumbaji-mpya.” (Mathayo 19:28) Maneno hayo yanamaanisha kufanywa upya, kuanzishwa upya kwa uhai wa binadamu. Kwa kutumia maneno “uumbaji-mpya,” Yesu alikazia kwamba Yehova atawapa wanadamu waadilifu nafasi ya kuishi kama Muumba wetu mwenye upendo anavyotaka. Kati ya faida nyingi ambazo atawapa wanadamu wakati huo ni kuondolewa kwa matatizo ya kiuchumi yanayowakumba watu wengi sana leo.

      Biblia ilitoa unabii huu kuhusu utawala wa Yesu Kristo: “Atamkomboa maskini anayelilia msaada, pia mwenye kuteseka na yeyote ambaye hana msaidizi. Atamsikitikia mtu wa hali ya chini na maskini, naye ataziokoa nafsi za maskini. Ataikomboa nafsi yao kutoka katika ukandamizaji na katika jeuri, nayo damu yao itakuwa na thamani machoni pake.”—Zaburi 72:12-14.

      Unaweza kuwa na wakati ujao mzuri kama huo. Lakini ili kutimiza matakwa ya Mungu ya kuishi katika ulimwengu huo mpya, ni muhimu kwanza ujifunze kisha ufanye mapenzi ya Mungu wa kweli. Fanya maamuzi yanayofaa kwa kutegemea ujuzi wa Neno la Mungu. Ishi ukitazamia wakati ujao mzuri ambao Mungu anawatolea wanadamu wote. Hutatamaushwa kamwe. Neno la Mungu linaahidi: “Maskini hawatasahauliwa sikuzote, wala tumaini la wapole halitaangamia kamwe.”—Zaburi 9:18.

      [Maelezo ya Chini]

      a Mistari mingine miwili ya Biblia inayozungumzia jinsi Mungu anavyowahangaikia watu wanaoteseka ni Zaburi 35:10 na Zaburi 113:7.

      [Blabu katika ukurasa wa 9]

      Unaweza kuwa na wakati ujao mzuri

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      Je, Nihamie Nchi Bora Zaidi Kiuchumi?

      Neno la Mungu haliwaambii watu wanapaswa kuishi na kufanya kazi wapi. Hata hivyo, kanuni za Biblia zinaweza kumsaidia mtu kuamua ikiwa inafaa kuhamia nchi nyingine kwa sababu za kiuchumi. Chunguza maswali na kanuni za Maandiko zifuatazo.

      1. Je, ninadanganywa na uvumi? Methali 14:15 inasema: “Mtu asiye na uzoefu hu- amini kila neno, lakini mtu mwerevu huzifikiria hatua zake.” Baada ya kuhamia nchi tajiri, mtu mmoja kutoka Ulaya Mashariki alisema: “Nilisikia kwamba huku pesa huchipuka juu ya miti kama majani. Bado ninatafuta miti hiyo.”

      2. Je, nina maoni yenye usawaziko kuhusu mahitaji ya familia yangu? Je, ninafuatia mahitaji ya lazima au ni tamaa zangu mwenyewe? Kichwa cha kila familia anapaswa kuandaa mahitaji ya kimwili ya mke na watoto. (1 Timotheo 5:8) Lakini akina baba wana daraka mbele za Mungu la kuwafundisha watoto wao kiadili na kiroho. (Kumbukumbu la Torati 6:6, 7; Waefeso 6:4) Huenda baba akafaulu kuandaa mahitaji mengi zaidi ya kimwili akihamia nchi nyingine. Lakini hawezi kuandaa mazoezi ya maadili na kiroho ya watoto wake ikiwa hatawaona kwa majuma kadhaa, miezi, au miaka.

      3. Je, ninatambua kwamba kumwacha mke wangu kwa muda mrefu kunatokeza hatari ya sisi wawili kufanya uzinzi? Neno la Mungu linawaonya watu waliooana wafikirie mahitaji ya kingono ya wenzi wao.—1 Wakorintho 7:5.

      4. Je, ninatambua kwamba kuingia nchi fulani bila kibali kunaweza kutokeza matatizo makubwa ya kisheria? Wakristo wa kweli wanapaswa kutii sheria za nchi.—Waroma 13:1-7.

      [Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Kanuni za Biblia zinafaa iwe sisi ni matajiri au maskini

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]

      Top: © Trygve Bolstad/Panos Pictures

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki