Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kila Mtu Anahitaji Makao
    Amkeni!—2005 | Septemba 22
    • Kila Mtu Anahitaji Makao

      “Kila mtu ana haki ya kuishi chini ya hali zinazofaa kutia ndani . . . makao, kwa ajili ya afya na hali yake njema na ile ya familia yake.”—Azimio la Watu Wote la Haki za Binadamu, Kifungu cha 25.

      VIBARUA wengi wa shambani wanaohama-hama wameanza kuishi katika eneo fulani. Familia nyingi zinaishi katika eneo lililo karibu na mjini kwenye trela zilizoegeshwa zinazoitwa parqueaderos ambazo hukodishwa kwa bei rahisi. Katika eneo hilo, huduma za lazima kama vile mfumo wa kuondoa maji machafu na takataka, na mfumo wa maji safi ni duni sana au hata hazipo. Ripota mmoja alisema kwamba “eneo hilo ni duni sana hivi kwamba [vibarua wa shambani] wangeweza kuishi huko.”

      Miaka mitatu iliyopita, wenye mamlaka walipoanza kuwafukuza watu kutoka maeneo fulani kama hayo, familia fulani ziliuza trela zao na kuhamia nyumba ambazo tayari zilikuwa na watu wengi na katika magereji yaliyo katikati mwa mji. Wengine walifunganya tu virago vyao na kwenda kutafuta mahali pa kwenda baada ya mavuno, mahali ambapo wangehisi ni nyumbani.

      Je, unawazia kwamba eneo hilo liko Amerika ya Kati au Kusini? Huenda ikawa umekosea. Unaweza kuona eneo hilo lenye trela zilizoegeshwa karibu na mji wa Mecca kusini mwa California, Marekani, umbali wa nusu saa kutoka kwenye jiji lenye utajiri la Palm Springs. Ingawa inasemekana kwamba kwa sasa watu wengi zaidi nchini Marekani wana nyumba zao wenyewe na mapato ya familia za kawaida yalikuwa dola 42,000 hivi mwaka wa 2002, imekadiriwa kwamba zaidi ya familia milioni tano za Wamarekani bado hazina nyumba zinazofaa.

      Hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi zinazositawi. Licha ya miradi mingi ya kisiasa, kijamii, na kidini, tatizo la nyumba ulimwenguni pote linazidi kuwa baya.

      Tatizo la Ulimwenguni Pote

      Inakadiriwa kwamba idadi ya watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda ulimwenguni ni zaidi ya bilioni moja. Wataalamu wa Brazili wanaoshughulika na uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini wanahofu kwamba hivi karibuni favelas, yaani, mitaa ya mabanda inayoongezeka daima nchini humo “itakuwa mikubwa na yenye watu wengi zaidi kuliko majiji ambapo mitaa hiyo ilianzia.” Katika majiji fulani huko Nigeria, zaidi ya asilimia 80 ya watu huishi katika mitaa ya mabanda na maeneo ya maskwota. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, alisema hivi mnamo 2003: “Hatua madhubuti isipochukuliwa, idadi ya watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda ulimwenguni pote inakadiriwa kuwa itaongezeka na kufikia bilioni 2 hivi katika miaka 30 ijayo.”

      Hata hivyo, takwimu hizo pekee hazionyeshi hata kidogo athari zinazosababishwa na hali duni za maisha kwa wakazi maskini ulimwenguni. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 50 ya watu katika nchi zinazositawi hawana mfumo wa kuondoa maji machafu na takataka, asilimia 33 hawana maji safi, asilimia 25 hawana nyumba zinazofaa, na asilimia 20 hawawezi kupata matibabu ya kisasa. Watu wengi katika nchi zilizositawi hata hawawezi kamwe kuruhusu wanyama wao vipenzi waishi katika hali kama hizo.

      Haki ya Kila Mtu

      Kila mwanadamu ana haki ya kuwa na nyumba inayofaa. Azimio la Watu Wote la Haki za Binadamu, lililopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1948, lilitangaza kwamba kila mtu ana haki ya kuishi chini ya hali zinazofaa, kutia ndani kuwa na makao yanayofaa. Kwa kweli, kila mtu anahitaji kuwa na nyumba nzuri.

      Hivi karibuni, katika mwaka wa 1996, nchi kadhaa ziliidhinisha hati ya UM ambayo baadaye iliitwa Habitat Agenda. Hati hiyo inataja maazimio hususa ya kumwandalia kila mtu makao yanayofaa. Baadaye, katika Januari 1, 2002, UM liliimarisha azimio hilo kwa kufanya hati hiyo kuwa programu rasmi ya UM.

      Inashangaza kwamba wakati baadhi ya mataifa tajiri yanapoanza kutoa wito tena wa kujenga makao kwenye mwezi na kupeleleza sayari ya Mihiri, idadi inayoongezeka ya raia wao maskini zaidi hawawezi hata kugharimia mahali pazuri pa kuishi hapa duniani. Tatizo la nyumba linakuathirije? Je, kuna tumaini lolote kwamba siku moja kila mtu atakuwa na nyumba yake nzuri?

  • Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Nyumba?
    Amkeni!—2005 | Septemba 22
    • Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Nyumba?

      JOSEPHINE mwenye umri wa miaka 36 anaishi na wavulana wake watatu wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 11 kwenye kitongoji cha jiji fulani la Afrika. Ili kujiruzuku, yeye huokota plastiki na kuziuza kwenye kiwanda fulani. Yeye hupata dola mbili hivi kwa siku kwa kazi hiyo inayochosha sana. Katika jiji hilo, pesa hizo hazitoshi kuilisha familia yake au kuwalipia karo ya shule.

      Jioni, yeye hurudi mahali anapopaita nyumbani. Kuta za nyumba yake zimejengwa kwa miti myembamba na kukandikwa kwa udongo na matofali yaliyochomwa. Paa yake imetengenezwa kwa mabati yenye kutu pamoja na mikebe na plastiki. Vipande vya mawe, mbao, na vyuma vimewekwa juu ya paa ili lisipeperushwe na upepo mkali. “Mlango” na “dirisha” la nyumba yake limetengenezwa kwa magunia yaliyochakaa, ambayo hayawezi kutoa ulinzi wowote dhidi ya hali mbaya ya hewa wala wavamizi.

      Hata hivyo, nyumba hiyo duni si mali yake. Kila wakati Josephine na watoto wake huishi kwa woga kwamba watafukuzwa. Ardhi ambayo nyumba yao duni imejengwa imetengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara iliyo karibu. Kwa kusikitisha, kuna hali kama hizo katika nchi nyingi ulimwenguni.

      Nyumba Yenye Sumu

      Robin Shell, ofisa mwenye cheo cha juu katika shirika moja la kimataifa la kusaidia watu kujenga nyumba anasema kwamba kwa sababu ya kuishi katika “nyumba duni, . . . watoto huaibikia nyumba yao, . . . kila wakati washiriki wa familia huwa wagonjwa, na . . . hawajui ni lini afisa wa serikali au mwenye nyumba atakuja kubomoa [nyumba yao].”

      Kuishi katika hali hizo huwafanya wazazi wawe na wasiwasi daima kuhusu afya na usalama wa watoto wao. Badala ya kufanya kazi ili kuboresha hali yao, mara nyingi wao hutumia wakati na nguvu nyingi wakijitahidi kupata mahitaji ya lazima ya watoto wao, kama vile chakula, mapumziko, na makao.

      Mtu asiyefahamu hali hiyo anaweza kukata kauli kwamba maskini wanaweza kuboresha hali yao iwapo wangejitahidi zaidi. Lakini suluhisho si tu kuwaambia watu wajitahidi zaidi. Kuna mambo mengi mazito yanayohusika katika tatizo la nyumba ambayo yanapita uwezo wa mwanadamu yeyote. Watafiti wanataja visababishi vikuu kuwa ongezeko la idadi ya watu, watu wengi kuhamia mijini, misiba ya asili, misukosuko ya kisiasa, na umaskini usiokoma. Mambo hayo ni kama vidole vitano vinavyowanyonga watu wengi maskini.

      Mikazo Inayosababishwa na Ongezeko la Watu

      Kwa ujumla, inakadiriwa kwamba kila mwaka ulimwenguni pote watu wengine milioni 68 hadi milioni 80 huhitaji makao. Kulingana na Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, idadi ya watu ulimwenguni ilipita bilioni 6.1 mnamo 2001 na inatarajiwa kufika kati ya bilioni 7.9 na bilioni 10.9 kufikia 2050. Jambo linaloshtua hata zaidi ni kwamba inatabiriwa kuwa asilimia 98 ya ongezeko hilo katika miaka 20 ijayo litatokea katika nchi zinazositawi. Makadirio hayo yanaonyesha kwamba kutakuwa na tatizo kubwa sana la nyumba. Hata hivyo, tatizo hilo linakuwa baya hata zaidi kwa sababu katika nchi nyingi, maeneo yanayokua haraka zaidi ni majiji ambayo tayari yamesongamana.

      Watu Wengi Wanahamia Mijini

      Mara nyingi, watu huona kwamba majiji makubwa kama vile, New York, London, na Tokyo huwakilisha ukuzi wa kiuchumi wa nchi. Kwa sababu hiyo, kila mwaka maelfu ya watu wa mashambani hufurika katika majiji wakitafuta hali bora za maisha, hasa elimu na kazi.

      Kwa mfano, uchumi wa China unakua haraka. Kwa sababu hiyo, ripoti moja inakadiria kwamba katika miongo kadhaa ijayo, zaidi ya nyumba mpya milioni 200 zitahitajika katika majiji makubwa pekee. Idadi hiyo ni karibu maradufu ya nyumba zote zilizoko Marekani leo. Ni mradi gani wa ujenzi unaoweza kutosheleza mahitaji hayo?

      Kulingana na Benki ya Dunia, “kila mwaka, familia milioni 12 hadi 15 hivi, zinazohamia miji ya nchi zinazositawi, zinahitaji idadi kama hiyo ya nyumba.” Kwa kuwa hakuna nyumba za kutosha ambazo familia hizo maskini zinaweza kugharimia, zinalazimika kuishi mahali popote penye makao, mara nyingi mahali ambapo hakuna mtu yeyote angependa kuishi.

      Misiba ya Asili na ya Kisiasa

      Umaskini umewafanya watu waishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko, maporomoko ya ardhi, na matetemeko ya nchi. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba huko Caracas, Venezuela, watu zaidi ya nusu milioni “huishi katika makao ya maskwota yaliyo kwenye miteremko mikali ambayo huathiriwa daima na maporomoko ya ardhi.” Pia, kumbuka aksidenti iliyotokea katika kiwanda fulani huko Bhopal, India, mwaka wa 1984 na kuua maelfu ya watu na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa nini watu wengi hivyo walikufa au kujeruhiwa? Ni kwa sababu kitongoji kimoja duni kilikuwa kimepanuka na kufikia meta tano tu kutoka kwenye mpaka wa kiwanda hicho.

      Pia misiba ya kisiasa, kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, imechangia sana matatizo ya nyumba. Ripoti moja iliyochapishwa mwaka wa 2002 na kikundi kimoja kinachotetea haki za binadamu ilisema kwamba kati ya mwaka wa 1984 na 1999 huenda watu wapatao milioni 1.5 walilazimika kuhama vijiji vyao huko kusini-mashariki mwa Uturuki kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wanakijiji wengi walilazimika kutafuta makao mahali popote ambapo wangeweza, mara nyingi wakisongamana na watu wa jamaa na majirani wao katika makao ya muda, nyumba za kukodisha, majengo ya shambani, au nyumba ambazo hazijakamilika. Inasemekana kwamba familia kadhaa ziliishi katika mazizi, watu 13 au zaidi wakiishi katika chumba kimoja, wakitumia choo kimoja, na mfereji mmoja uliokuwa katika ua. Mmoja wa wakimbizi hao alisema: “Hatungependa kuendelea kuishi hivi. Tunaishi katika makao ya wanyama.”

      Kutokuwepo kwa Maendeleo ya Kiuchumi

      Mwishowe, kuna uhusiano mkubwa kati ya nyumba na hali ya kiuchumi ya maskini. Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia iliyotajwa awali, ilisemekana kuwa mnamo 1988 pekee, kulikuwa na maskini milioni 330 kati ya watu walioishi katika majiji ya nchi zinazositawi, hali ambayo haikutarajiwa kubadilika sana katika miaka iliyofuata. Ikiwa watu ni maskini sana hivi kwamba hawawezi kugharimia mahitaji ya lazima kama vile chakula na mavazi, watawezaje kulipa kodi au kujenga nyumba nzuri?

      Kiwango cha juu cha riba na inflesheni hufanya familia nyingi zisiweze kupata mkopo kutoka kwenye benki, na gharama za matumizi zinazoongezeka hufanya iwe vigumu kwa wengi kuboresha hali yao ya kiuchumi. Asilimia 20 hivi ya watu katika nchi fulani hawana kazi na hivyo ni vigumu kwao kupata mahitaji ya lazima.

      Sababu hizo na nyingine zimewalazimisha mamia ya mamilioni ya watu katika sehemu zote ulimwenguni waishi katika nyumba za hali ya chini. Watu huishi ndani ya mabasi makuukuu, kontena za kusafirishia vitu, na katoni. Wengine huishi chini ya ngazi, katika nyumba zilizojengwa kwa karatasi za plastiki, au vipande vya mbao. Hata wengine huishi katika viwanda vilivyoacha kutumiwa.

      Ni Jitihada Gani Zinazofanywa?

      Tayari jitihada nyingi zinafanywa na mashirika mengi, serikali, na watu wengi wanaojali ili kushughulikia tatizo hilo. Nchini Japani, mashirika kadhaa yameanzishwa ili kusaidia kujenga nyumba za bei nafuu. Mradi mmoja wa ujenzi ulioanzishwa nchini Afrika Kusini mwaka wa 1994, umesaidia kujenga nyumba zaidi ya milioni moja zenye vyumba vinne. Nchini Kenya, mradi fulani wa ujenzi unakusudia kujenga nyumba 150,000 katika maeneo ya jijini na kujenga mara mbili ya idadi hiyo katika maeneo ya mashambani kila mwaka. Nchi nyingine kama vile Madagaska zimeelekeza jitihada zao kutafuta mbinu za kujenga nyumba zisizo za gharama kubwa.

      Mashirika ya kimataifa kama vile mradi wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia makao (UN-HABITAT), yamebuniwa ili kuonyesha kwamba ulimwengu umeazimia “kuzuia na kutatua matatizo yanayosababishwa na ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini.” Mashirika yasiyojipatia faida na yasiyo ya kiserikali pia yanajaribu kusaidia. Shirika moja lisilojipatia faida limesaidia zaidi ya familia 150,000 katika nchi mbalimbali kuboresha nyumba zao za hali ya chini. Linakadiria kwamba kufikia mwaka wa 2005, litakuwa limesaidia watu milioni moja kupata nyumba sahili, nzuri, na ya bei nafuu.

      Mengi ya mashirika hayo yako tayari kutoa habari zitakazowasaidia watu wanaoishi katika nyumba za hali ya chini wakabiliane ifaavyo na hali zao au hata kuziboresha. Bila shaka, ikiwa unahitaji msaada unaweza kunufaika na mipango hiyo. Pia kuna mambo mengi ya msingi ambayo unaweza kufanya ili kujisaidia.—Ona sanduku “Nyumba na Afya Yako,” kwenye ukurasa wa 7.

      Bila kujali kama unaweza kuboresha hali yako, hakuna tumaini kwamba mtu fulani au shirika fulani la kibinadamu linaweza kuondoa na kumaliza mambo yanayosababisha tatizo la nyumba ulimwenguni pote. Jamii ya kimataifa inaendelea kushindwa kukabiliana na uhitaji wa haraka na unaoongezeka wa maendeleo ya kiuchumi na kutoa msaada wa kibinadamu. Kila mwaka mamilioni ya watoto wanazaliwa katika hali hiyo ya umaskini inayozidi kuzorota. Je, kuna tumaini lolote halisi la kutatua tatizo hilo kabisa?

  • Hatimaye Kila Mtu Atakuwa na Nyumba Nzuri!
    Amkeni!—2005 | Septemba 22
    • Hatimaye Kila Mtu Atakuwa na Nyumba Nzuri!

      NJE tu ya jiji la Nairobi, Kenya, kuna makao maridadi ya Umoja wa Mataifa ya Gigiri, yenye ukubwa wa ekari 140, yanayotia ndani makao makuu ya mradi wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia makao (UN-HABITAT). Shirika hilo lilibuniwa ili kuonyesha azimio la kimataifa la kutatua tatizo la nyumba ulimwenguni. Katika uwanja wa makao hayo huko Gigiri, kuna sehemu yenye kupendeza iliyotengwa ili kutazama mazingira, ambayo ni mfano bora wa kile kinachoweza kutimizwa kunapokuwa na jitihada madhubuti na pesa za kutosha. Eneo ambalo wakati mmoja lilijaa takataka, sasa limegeuzwa kuwa mahali maridadi pa tafrija panapoweza kutumiwa na wafanyakazi na wageni.

      Hata hivyo, kilometa chache tu kutoka hapo kuna mtaa mpya wa mabanda ambao unapanuka haraka. Mtaa huo ni kikumbusha chenye kusikitisha kuhusu jinsi ilivyo vigumu kusuluhisha tatizo la nyumba. Nyumba hizo zilizojengwa kwa udongo, vijiti, na mikebe, zina ukubwa wa meta 16 hivi za mraba. Vijia vyake vimejaa maji machafu yenye uvundo. Bei ya maji ni mara tano zaidi ya ile ambayo mkaaji wa Marekani hulipa kwa ajili ya maji. Wengi kati ya wakazi 40,000 hivi wanaoishi hapo wana umri wa kati ya miaka 20 na 30 na kitu. Si wavivu au wazembe. Walienda katika eneo hilo ili watafute kazi katika jiji la Nairobi lililo karibu.

      Tofauti na eneo hilo, viongozi wa ulimwengu hukutana katika mazingira safi, mazuri, na yenye kuvutia ili kuzungumzia wakati ujao wa wanaume, wanawake, na watoto wanaoishi katika eneo lililo katika ujirani wao. Kulingana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, jambo la kusikitisha ni kwamba “ulimwengu una mali, ujuzi, na uwezo” wa kuboresha sana maisha ya wakazi wa mitaa ya mabanda. Basi ni jambo gani linalohitaji kufanywa? Bw. Annan anasema: “Ni tumaini langu kwamba . . . wote wanaohusika [wataweza] kushinda hali ya kutojali na kutojishughulisha ambayo imezuia maendeleo.”

      Hata hivyo, tumaini hilo ni halisi kadiri gani? Ni nini kitakachohitajiwa ili wanasiasa wote, wa kimataifa na wenyeji, waache kufikiria tu masilahi yao yenyewe na kushirikiana ili kupata suluhisho la tatizo hilo? Kuna Mtu fulani aliye na mali, ujuzi, na uwezo wa kukomesha tatizo lililopo. Jambo muhimu zaidi ni kwamba yeye pia ana huruma na nia ya kuchukua hatua hivi karibuni. Kwa kweli, tayari serikali yake imefanya mipango madhubuti ya kumaliza kabisa tatizo la nyumba ulimwenguni.

      Mradi Mpya wa Kujenga Nyumba

      Katika Biblia, Muumba wetu, Yehova Mungu, anataja yale anayokusudia kufanya. Anaahidi hivi: “Mimi ninaumba mbingu mpya na dunia mpya.” (Isaya 65:17) Jambo hilo litaleta badiliko kubwa. “Mbingu” hizo mpya za kiserikali zitatimiza mambo ambayo serikali za kisasa za wanadamu zimeshindwa kutimiza. Ufalme, au serikali ya Mungu, itahakikisha kwamba kila mtu atakayekuwa sehemu ya jamii mpya ya kibinadamu duniani atakuwa na afya nzuri, usalama, na atajiheshimu. Mapema, Isaya aliambiwa kwamba watu watakaokuwa sehemu ya jamii mpya ya kidunia wangekusanywa katika “siku za mwisho.” (Isaya 2:1-4) Hilo linamaanisha kwamba mabadiliko hayo yatatukia hivi karibuni.—Mathayo 24:3-14; 2 Timotheo 3:1-5.

      Jambo muhimu ni kwamba katika maneno yaliyoandikwa katika mistari mingine ya Isaya sura ya 65, Mungu anataja kihususa kwamba wakati huo atamwandalia kila mtu makao ya kudumu. Anasema: “Hakika wao watajenga nyumba na kukaa ndani yake. . . . Hawatajenga na mtu mwingine akae ndani yake.” (Isaya 65:21, 22) Wazia ukiishi katika nyumba yako na katika mazingira safi yenye usalama katika paradiso nzuri! Ni nani asiyetamani hali kama hizo? Lakini unawezaje kuwa na hakika kuhusu kile ambacho Mungu ameahidi?

      Ahadi Unayoweza Kutumaini

      Mungu alipowaumba Adamu na Hawa, hakuwaweka katika mazingira makame. Badala yake, aliwaweka katika bustani maridadi huko Edeni iliyokuwa na hewa safi, maji na chakula tele. (Mwanzo 2:8-15) Adamu aliambiwa ‘ajaze dunia,’ lakini si kupita kiasi. (Mwanzo 1:28) Tangu mwanzo, Mungu alikusudia kila mtu afurahie utaratibu, upatano, na mambo mengi mazuri.

      Baadaye, katika siku za Noa, jamii ya kibinadamu ilikuwa na jeuri na ukosefu mwingi sana wa adili, hivi kwamba “dunia ikaharibika machoni pa Mungu wa kweli.” (Mwanzo 6:11, 12) Je, Mungu alifumbia macho tu hali hiyo? La. Alichukua hatua mara moja. Alisafisha dunia kwa kuleta Gharika ulimwenguni pote kwa ajili ya jina lake na kwa ajili ya Noa mwadilifu na wazao wake. Kwa hiyo Noa na familia yake walipotoka kwenye safina na kuingia katika makao yao mapya, waliambiwa kwa mara nyingine wasambae, ‘wawe wengi, na kuijaza dunia.’—Mwanzo 9:1.

      Hata baadaye, Mungu aliwapa Waisraeli urithi aliokuwa amemwahidi babu yao Abrahamu. Nchi hiyo ya Ahadi ilitajwa kuwa “nchi nzuri na kubwa . . . inayotiririka maziwa na asali.” (Kutoka 3:8) Kwa sababu ya kutotii, Waisraeli walirandaranda nyikani bila makao ya kudumu kwa miaka 40. Hata hivyo, ili kutimiza ahadi yake, mwishowe Mungu aliwapa nchi ambayo wangeishi. Simulizi lililopuliziwa linasema hivi: “Yehova akawapa pumziko kuwazunguka pande zote . . . Hakuna ahadi hata moja iliyokosa kutimia katika ahadi zote nzuri ambazo Yehova alikuwa ameipa nyumba ya Israeli; mambo yote yalitimia.”—Yoshua 21:43-45.

      Hatimaye Kila Mtu Atakuwa na Nyumba!

      Kwa hiyo, ni wazi kwamba maneno ya Yehova katika Isaya sura ya 65 si ahadi za bure. Kwa kuwa yeye ndiye Muumba wa vitu vyote, bila shaka ana uwezo wa kufanya lolote linalohitajika ili kuisafisha dunia na kutimiza kusudi lake la awali kuielekea. (Isaya 40:26, 28; 55:10, 11) Isitoshe, Biblia inatuhakikishia kwamba anataka kufanya hivyo. (Zaburi 72:12, 13) Alichukua hatua hapo zamani ili kuwaandalia wanadamu waadilifu nyumba zinazofaa, naye atafanya hivyo tena hivi karibuni.

      Kwa kweli, Mwana wake, Yesu Kristo, alipokuja duniani aliwafundisha wafuasi wake wasali hasa kwamba ‘mapenzi ya Mungu yatendeke duniani kama ilivyo mbinguni.’ (Mathayo 6:10) Alionyesha kwamba dunia itakuwa paradiso. (Luka 23:43) Hebu wazia hilo litamaanisha nini. Hakutakuwa tena na mitaa ya mabanda, maeneo ya maskwota, watu wanaolala barabarani, au watu kufukuzwa mahali wanapoishi. Huo utakuwa wakati wenye furaha iliyoje! Chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, mwishowe kila mtu atapata makao ya kudumu!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki