Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kwa Nini Kuna Maskini Wengi Katika Ulimwengu Wenye Utajiri?
    Amkeni!—2007 | Mei
    • Kwa Nini Kuna Maskini Wengi Katika Ulimwengu Wenye Utajiri?

      “MNA maskini pamoja nanyi sikuzote,” akasema Yesu Kristo katika karne ya kwanza W.K. (Mathayo 26:11) Sikuzote kumekuwa na maskini wengi sana, kuanzia wakati wa Yesu hadi wakati wetu. Lakini kwa nini kuna maskini wengi katika ulimwengu wenye utajiri mwingi sana?

      Wengine waamini kuwa watu huwa maskini kwa sababu ya kufanya maamuzi mabaya. Huenda hilo linaweza kuwa kweli katika visa fulani. Wale ambao huchagua kutosheleza tamaa za kileo, dawa za kulevya, na kucheza kamari hupoteza mali zao kwa urahisi. Lakini si watu wote huwa maskini kwa sababu ya kufanya maamuzi mabaya.

      Watu wengi wamepoteza kazi kwa sababu ya mabadiliko ya kibiashara. Ni wengi pia wanaofanya kazi ambao wametumia pesa zote walizoweka akiba kulipia gharama za matibabu zinazozidi kuongezeka. Na mamia ya mamilioni ya watu maskini katika nchi zinazoendelea wanajikuta katika hali hiyo bila kupenda kwao. Kama hoja zinazofuata zinavyoonyesha, mara nyingi umaskini hutokea bila kusababishwa na watu wanaoathiriwa.

      Kujifunza Kutokana na Historia

      Katika miaka ya mapema ya 1930, ulimwengu ulikumbwa na hali ngumu za kiuchumi ambazo zilikuja kuitwa Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi. Katika nchi moja, mamilioni ya watu walipoteza kazi na familia nyingi sana zikapoteza makao. Huku watu wengi wakifa njaa, wakulima walikuwa wakimwaga maziwa mengi sana katika mitaro na maofisa wa serikali waliwaamuru wakulima waue wanyama wengi wa kufugwa.

      Kwa nini bidhaa hizo ziliharibiwa? Miongozo ya mfumo wa kiuchumi ilielekeza kwamba bidhaa za shambani na bidhaa nyingine ziuzwe kwa faida fulani. Maziwa, nyama, na nafaka zingewafaidi sana maskini. Lakini kwa kuwa vyakula hivyo havikuwaletea mapato walioviuza, vilionekana kuwa havina faida na hivyo vikaharibiwa.

      Kulikuwa na ghasia katika majiji mengi kwa sababu ya chakula. Watu fulani ambao hawakuwa na pesa za kununulia familia zao chakula, walianza kuiba kwa kutumia mabavu ili kupata chakula. Wengine walikufa njaa. Mambo hayo yalitukia nchini Marekani. Mwanzoni mwa huo Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi, mfumo wenye nguvu wa kiuchumi wa nchi hiyo haukuwasaidia watu wenye mapato ya chini. Badala ya kutanguliza mahitaji ya raia wote ya chakula, makao, na kazi, mfumo huo uliona mahitaji hayo kuwa yasiyo na maana yakilinganishwa na kupata faida.

      Hali za Leo

      Mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu uliokoka huo Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi, na sasa watu wengi wanaonekana kuwa matajiri na salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hata hivyo, licha ya utajiri mwingi uliopo, mara nyingi maskini hawapati nafasi za kuboresha hali zao maishani. Katika nchi fulani, ripoti za njaa na umaskini ni za kawaida sana hivi kwamba watu wamechoka kuzisoma. Hata hivyo, wakimbizi wanapokufa njaa kwa sababu ya vita, vyakula vilivyohifadhiwa vinapooza kwa sababu za kisiasa, na masoko yanapoongeza bei za mahitaji ya lazima hivi kwamba maskini hawawezi kuzimudu, tunajionea matokeo ya mfumo ambao umeshindwa kutosheleza mahitaji ya maskini. Mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu hupuuza mamilioni ya maskini.

  • Kwa Nini Kuna Maskini Wengi Katika Ulimwengu Wenye Utajiri?
    Amkeni!—2007 | Mei
    • [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Jitihada ya Kuendelea Kuishi

      Katika kitabu chake (The Working Poor—Invisible in America) kuhusu maskini wanaofanya kazi, mtunzi na mwandishi wa habari David K. Shipler anatusaidia kutambua jinsi watu fulani nchini Marekani huishi katika hali ya hatari kwa sababu ya umaskini. Anatoa mfano wa mama anayeishi katika nyumba duni ambaye mtoto wake anaugua ugonjwa wa pumu. Kwa sababu ya kuishi chini ya hali hizo ugonjwa huo unazidi kuwa mbaya zaidi na hilo humfanya mama amkimbize hospitali. Anaposhindwa kulipa gharama kubwa ya hospitali, riba ya mkopo wa mama huyo huongezeka na hivyo hawezi kulipia tena gari lake lililo katika hali nzuri. Kwa sababu hiyo yeye huanza kuchelewa kazini na hivyo nafasi zake za kupandishwa cheo na kupokea mapato bora zaidi hupungua basi analazimika kuendelea kuishi katika nyumba hiyo duni. Mtoto huyo na mama yake wanaishi wakitazamia chochote kibaya, hata ingawa wanaishi katika taifa tajiri zaidi duniani.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki