-
Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?Amkeni!—2001 | Mei 8
-
-
Watu Wazidi Kuogopa
Sababu nyingine inayofanya watu wakose kutumaini mpango wa magereza ni kwa sababu wafungwa huishi chini ya hali mbaya sana. Hali hizo zimeelezwa kwenye sanduku lililoonyeshwa. Yaelekea wafungwa ambao wametendewa kinyama vifungoni hawawezi kurekebishwa. Vikundi kadhaa vinavyotetea haki za binadamu vinashangazwa pia na idadi kubwa ya wafungwa kutoka makabila yasiyopendwa. Vikundi hivyo vinauliza kama hali hiyo imetukia tu au imesababishwa na ubaguzi wa kikabila.
Ripoti moja ya mwaka wa 1998 ya Shirika la Habari la Associated Press ilieleza hali ya wale waliokuwa wafungwa katika Gereza la Holmesburg, huko Pennsylvania, Marekani, ambao waliomba kulipwa fidia kwa sababu ya kutumiwa kwa majaribio ya kemikali walipokuwa gerezani. Vipi kuhusu kuanzishwa tena nchini Marekani kwa mtindo wa kuwafunga wafungwa wengi kwa minyororo? Shirika la Amnesty International laripoti hivi: “Wafungwa hao waliofungwa minyororo hufanya kazi kwa muda wa saa 10 hadi 12 katika jua kali. Wao hupumzika kwa muda mfupi tu ili kunywa maji, na saa moja ili kula chakula cha mchana. . . . Wafungwa hao hujisaidia kwenye ndoo tu iliyozingirwa na kiwambo. Wafungwa hawafunguliwi minyororo wakati wa kujisaidia. Wafungwa wanaposhindwa kufikia ndoo wanajisaidia popote hadharani.” Lakini, magereza yote hayana mazoea hayo. Hata hivyo, kuwatendea wafungwa kinyama huwaletea aibu wafungwa na wale wanaotenda mambo hayo.
-
-
Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?Amkeni!—2001 | Mei 8
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Hali Ilivyo Magerezani
MSONGAMANO: Haishangazi kwamba magereza nchini Uingereza yamesongamana watu sana! Uingereza ndiyo nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya wafungwa katika Ulaya Magharibi. Ina uwiano wa wafungwa 125 kwa kila watu 100,000. Huko Brazili, gereza kubwa zaidi jijini São Paulo linaweza kutoshea wafungwa 500. Badala yake lina wafungwa 6,000. Huko Urusi, vyumba vya magereza vinavyopasa kuwa na wafungwa 28 vina wafungwa wapatao 90 hadi 110. Hali ni mbaya sana kiasi cha kwamba wafungwa hulala kwa zamu. Katika nchi moja ya Asia, wafungwa 13 au 14 wamefungiwa kwenye chumba chenye ukubwa wa meta 3 za mraba. Na katika Magharibi mwa Australia, maofisa wa gereza wametatua tatizo la msongamano kwa kununua makontena ya kuwaweka wafungwa.
JEURI: Gazeti Der Spiegel la Ujerumani laripoti kwamba wafungwa wakatili huwaua na kuwatesa wafungwa wengine katika magereza ya Ujerumani. Kunakuwa na “mapambano ya makundi yanayofanya biashara haramu ya pombe na dawa za kulevya, ngono, na ulaji wa riba.” Mara nyingi chuki za kikabila husababisha jeuri gerezani. “Kuna wafungwa kutoka mataifa 72,” lasema gazeti la Der Spiegel. “Uhasama na mapambano yanayosababisha jeuri hayawezi kuepukwa.” Katika gereza moja huko Amerika Kusini, maofisa walisema kwamba kwa wastani wafungwa 12 waliuawa kila mwezi. Wafungwa walisema kwamba idadi ya wale waliouawa ilikuwa maradufu, likaripoti gazeti Financial Times la London.
KUTENDEWA VIBAYA KINGONO: Makala “Tatizo la Ubakaji Gerezani (The Rape Crisis Behind Bars),” katika gazeti la The New York Times yasema kadirio moja laonyesha kwamba huko Marekani, “zaidi ya wanaume 290,000 hutendewa vibaya kingono gerezani kila mwaka.” Ripoti hiyo yaendelea kusema hivi: “Hali ya kutisha ya kutendewa vibaya kingono ni jambo la kawaida tu.” Shirika moja lakadiria kwamba kila siku kuna visa vipatavyo 60,000 vya ngono zisizofaa katika magereza ya Marekani.
AFYA NA USAFI: Imethibitishwa kwamba magonjwa yaambukizwayo kingono yameenea sana magerezani. Watu wengi ulimwenguni wanajua kuwa wafungwa nchini Urusi na katika nchi fulani za Afrika huugua kifua kikuu. Inajulikana kote pia kuwa magereza mengi ulimwenguni hayaandai matibabu, si safi, wala hayaandai chakula kinachofaa.
[Picha]
Gereza lililosongamana watu huko São Pau
[Hisani]
AP Photo/Dario Lopez-Mills
-