Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Magereza Yamo Taabani
    Amkeni!—2001 | Mei 8
    • Magereza Yamo Taabani

      “Kujenga magereza zaidi ili kukabiliana na uhalifu ni kama kuchimba makaburi zaidi ili kukabiliana na ugonjwa hatari.”—ROBERT GANGI, MREKEBISHAJI STADI WA WAFUNGWA.

      WATU huona neno “gereza” kuwa neno lenye kuudhi na hivyo hutumia maneno yasiyoonyesha waziwazi hali mbaya iliyopo. Watu hupenda kutumia neno “kifungoni” au “kituo cha kuwarekebishia wafungwa,” ambamo “elimu ya kiufundi” na “huduma za kijamii” huandaliwa. Watu hupenda pia kutumia neno “mfungwa” badala ya neno “mahabusu” lenye kumshushia mtu heshima. Lakini unapochunguza hali ilivyo, utaona kwamba magereza yanapatwa na matatizo makubwa sana leo, kama vile gharama inayoongezeka ya kuwatunza wahalifu gerezani. Isitoshe, jitihada za kuwarekebisha wafungwa huambulia patupu.

      Watu fulani hutilia shaka umuhimu wa magereza. Wanasema kwamba ingawa kuna wahalifu zaidi ya milioni nane katika magereza ulimwenguni pote, uhalifu haujapungua katika nchi nyingi. Na ingawa watu wengi sana wamefungwa gerezani kwa sababu ya ulanguzi wa dawa za kulevya, biashara hiyo imepamba moto mitaani.

      Hata hivyo, watu wengi huona kuwafunga wahalifu gerezani kuwa adhabu inayofaa. Wao huhisi kwamba mfungwa anapotiwa gerezani anapokea adhabu anayostahili. Mwandishi mmoja wa habari aita juhudi za kuwatia wahalifu gerezani kuwa “msisimko wa kujaza watu gerezani.”

      Wale wanaovunja sheria hutiwa gerezani kwa sababu nne kuu: (1) kuadhibu wahalifu hao, (2) kulinda jamii, (3) kuzuia uhalifu unaoweza kutokea wakati ujao, na (4) kuwarekebisha wahalifu, na kuwasaidia wawe raia wanaotii sheria na raia wema baada ya kuachiliwa. Acheni tuone ikiwa magereza yanatimiza malengo hayo.

  • Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?
    Amkeni!—2001 | Mei 8
    • Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?

      “Kuwashushia heshima na kuwavunja moyo wafungwa ndiyo njia mbaya zaidi ya kuwarekebisha wafungwa.”—SAFU YA MHARIRI KATIKA GAZETI THE ATLANTA CONSTITUTION.

      MARA nyingi magereza huzuia uhalifu kwa muda mfupi tu. Je, kweli mfungwa anapoachiliwa huru huwa amelipia hasara iliyosababishwa na uhalifu aliotenda? Vipi wahasiriwa au wapendwa wao? “Mtoto wangu aliuawa,” akasihi Rita wakati mtu aliyemwua mwanawe mwenye umri wa miaka 16 alipoachiliwa huru baada ya kufungwa gerezani kwa miaka mitatu tu. “Hebu tua kidogo na ufikirie jambo hilo. Ni vigumu sana kuwazia jinsi ninavyohisi.” Kama kisa cha Rita kinavyoonyesha, watu waliotendewa uhalifu huendelea kuteseka baada ya wahalifu hao kuhukumiwa na hata baada ya habari hizo kusahaulika.

      Hili ni suala linalowahangaisha wale waliotendewa uhalifu na watu wengineo wote. Kwa kuwa, utulivu wako na labda usalama wako unahusika iwe wafungwa walioachiliwa huru wamerekebishwa au wamekuwa wabaya zaidi baada ya kukaa gerezani.

      Wahalifu Hujifunza Mbinu Mpya za Uhalifu Gerezani

      Baadhi ya wahalifu huendelea na uhalifu baada ya kutoka gerezani. “Pesa nyingi zinapotumiwa kujenga magereza zaidi badala ya kuwarekebisha wahalifu, kwa kawaida hilo huongoza kwa uhalifu mbaya zaidi,” aandika Jill Smolowe kwenye gazeti Time. Maelezo ya Peter,a ambaye amekuwa gerezani kwa miaka 14 yapatana na maoni hayo. “Wafungwa wenzangu wengi waliiba vitu vidogo-vidogo mwanzoni, kisha wakaiba mali zenye thamani sana, na hatimaye wakaanza kuwatendea kinyama wanadamu wenzao,” yeye asema. “Wafungwa hao wanaona magereza kuwa kama shule ya kujifunzia mbinu mpya za uhalifu. Wanapotoka gerezani wanakuwa wahalifu hatari zaidi.”

      Ingawa magereza hupunguza kwa muda idadi ya wahalifu mitaani, yaonekana kwamba magereza hayakomeshi uhalifu kwa vyovyote. Vijana wanaoishi kwenye mitaa mikubwa majijini huona kufungwa gerezani kuwa dalili ya ukomavu. Mara nyingi wengi wao wanakuwa wahalifu wabaya zaidi mwishowe. “Gereza halimrekebishi mtu hata kidogo,” asema Larry, ambaye amefungwa gerezani mara nyingi sana. “Wahalifu wanapoachiliwa huru wanaendelea kutenda mambo yaleyale.”

      Ndiyo sababu uchunguzi mmoja nchini Marekani unaonyesha kwamba asilimia 50 ya visa vyote vibaya vya uhalifu hutendwa na asilimia 5 hivi ya wahalifu. “Mara nyingi wafungwa wanapokosa la kufanya, wanatumia wakati wao kusitawisha chuki, na kujifunza njia nyingine za uhalifu, ambazo . . . watatumia wanapoachiliwa huru,” lasema gazeti Time.

      Ndivyo ilivyo katika nchi nyingine mbali na Marekani. John Vatis, daktari katika gereza la kijeshi nchini Ugiriki, asema: “Wafungwa wengi wanapotoka kwenye magereza yetu wanakuwa wakali zaidi, wajeuri, na wakatili zaidi. Wafungwa wengi huazimia kulipiza kisasi wanapoachiliwa huru.”

      Matokeo kwa Jamii

      Matatizo ya magereza huathiri hali yako ya kifedha. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba kila mfungwa nchini Marekani hutunzwa kwa dola 21,000 hivi kila mwaka. Fedha hizo zinatokana na malipo ya kodi. Wafungwa wenye umri unaozidi miaka 60 hutunzwa kwa kiasi kinachozidi hicho kwa mara tatu. Kuna sababu nyingine zinazofanya raia wa nchi nyingi watilie shaka mpango wa magereza. Wengi wanaogopa wahalifu wanaoachiliwa huru kabla ya kifungo kwisha. Wanaogopa pia wahalifu ambao kesi zao zinatupiliwa mbali kwa sababu ya kasoro fulani ya kisheria inayogunduliwa na wakili mwenye busara. Kwa kawaida, wale waliotendewa uhalifu hawahisi wamelindwa vya kutosha ili wasishambuliwe tena na mhalifu aliyeachiliwa huru. Na huenda wasiweze kujitetea mahakamani.

      Watu Wazidi Kuogopa

      Sababu nyingine inayofanya watu wakose kutumaini mpango wa magereza ni kwa sababu wafungwa huishi chini ya hali mbaya sana. Hali hizo zimeelezwa kwenye sanduku lililoonyeshwa. Yaelekea wafungwa ambao wametendewa kinyama vifungoni hawawezi kurekebishwa. Vikundi kadhaa vinavyotetea haki za binadamu vinashangazwa pia na idadi kubwa ya wafungwa kutoka makabila yasiyopendwa. Vikundi hivyo vinauliza kama hali hiyo imetukia tu au imesababishwa na ubaguzi wa kikabila.

      Ripoti moja ya mwaka wa 1998 ya Shirika la Habari la Associated Press ilieleza hali ya wale waliokuwa wafungwa katika Gereza la Holmesburg, huko Pennsylvania, Marekani, ambao waliomba kulipwa fidia kwa sababu ya kutumiwa kwa majaribio ya kemikali walipokuwa gerezani. Vipi kuhusu kuanzishwa tena nchini Marekani kwa mtindo wa kuwafunga wafungwa wengi kwa minyororo? Shirika la Amnesty International laripoti hivi: “Wafungwa hao waliofungwa minyororo hufanya kazi kwa muda wa saa 10 hadi 12 katika jua kali. Wao hupumzika kwa muda mfupi tu ili kunywa maji, na saa moja ili kula chakula cha mchana. . . . Wafungwa hao hujisaidia kwenye ndoo tu iliyozingirwa na kiwambo. Wafungwa hawafunguliwi minyororo wakati wa kujisaidia. Wafungwa wanaposhindwa kufikia ndoo wanajisaidia popote hadharani.” Lakini, magereza yote hayana mazoea hayo. Hata hivyo, kuwatendea wafungwa kinyama huwaletea aibu wafungwa na wale wanaotenda mambo hayo.

      Je, Jamii Inafaidika?

      Kwa wazi, jamii nyingi huhisi zikiwa salama wakati wahalifu hatari wanapofungwa gerezani. Jamii nyingine hupendelea magereza kwa sababu tofauti. Watu walilalamika sana wakati wenye mamlaka walipotaka kufunga gereza moja katika mji mdogo wa Cooma nchini Australia. Kwa nini? Kwa sababu wakazi wengi wenye shida ya kifedha waliandikwa kazi kwenye gereza hilo.

      Hivi karibuni serikali nyingi zimebinafsisha magereza ili kupunguza gharama. Jambo la kusikitisha ni kwamba watu fulani hupata faida kutokana na kuwapo kwa wafungwa wengi waliohukumiwa vifungo virefu. Hivyo, watu wanapata faida kifedha kutokana na magereza.

      Kwa ujumla, swali la msingi bado ni: Je, magereza yanawarekebisha wahalifu? Ijapokuwa kwa kawaida jibu ni la, utashangaa kujua kwamba wafungwa kadhaa wamesaidiwa kubadilika. Acheni tuone ilivyotukia.

      [Maelezo ya Chini]

      a Baadhi ya majina katika makala hii yamebadilishwa.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6, 7]

      Hali Ilivyo Magerezani

      MSONGAMANO: Haishangazi kwamba magereza nchini Uingereza yamesongamana watu sana! Uingereza ndiyo nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya wafungwa katika Ulaya Magharibi. Ina uwiano wa wafungwa 125 kwa kila watu 100,000. Huko Brazili, gereza kubwa zaidi jijini São Paulo linaweza kutoshea wafungwa 500. Badala yake lina wafungwa 6,000. Huko Urusi, vyumba vya magereza vinavyopasa kuwa na wafungwa 28 vina wafungwa wapatao 90 hadi 110. Hali ni mbaya sana kiasi cha kwamba wafungwa hulala kwa zamu. Katika nchi moja ya Asia, wafungwa 13 au 14 wamefungiwa kwenye chumba chenye ukubwa wa meta 3 za mraba. Na katika Magharibi mwa Australia, maofisa wa gereza wametatua tatizo la msongamano kwa kununua makontena ya kuwaweka wafungwa.

      JEURI: Gazeti Der Spiegel la Ujerumani laripoti kwamba wafungwa wakatili huwaua na kuwatesa wafungwa wengine katika magereza ya Ujerumani. Kunakuwa na “mapambano ya makundi yanayofanya biashara haramu ya pombe na dawa za kulevya, ngono, na ulaji wa riba.” Mara nyingi chuki za kikabila husababisha jeuri gerezani. “Kuna wafungwa kutoka mataifa 72,” lasema gazeti la Der Spiegel. “Uhasama na mapambano yanayosababisha jeuri hayawezi kuepukwa.” Katika gereza moja huko Amerika Kusini, maofisa walisema kwamba kwa wastani wafungwa 12 waliuawa kila mwezi. Wafungwa walisema kwamba idadi ya wale waliouawa ilikuwa maradufu, likaripoti gazeti Financial Times la London.

      KUTENDEWA VIBAYA KINGONO: Makala “Tatizo la Ubakaji Gerezani (The Rape Crisis Behind Bars),” katika gazeti la The New York Times yasema kadirio moja laonyesha kwamba huko Marekani, “zaidi ya wanaume 290,000 hutendewa vibaya kingono gerezani kila mwaka.” Ripoti hiyo yaendelea kusema hivi: “Hali ya kutisha ya kutendewa vibaya kingono ni jambo la kawaida tu.” Shirika moja lakadiria kwamba kila siku kuna visa vipatavyo 60,000 vya ngono zisizofaa katika magereza ya Marekani.

      AFYA NA USAFI: Imethibitishwa kwamba magonjwa yaambukizwayo kingono yameenea sana magerezani. Watu wengi ulimwenguni wanajua kuwa wafungwa nchini Urusi na katika nchi fulani za Afrika huugua kifua kikuu. Inajulikana kote pia kuwa magereza mengi ulimwenguni hayaandai matibabu, si safi, wala hayaandai chakula kinachofaa.

      [Picha]

      Gereza lililosongamana watu huko São Pau

      [Hisani]

      AP Photo/Dario Lopez-Mills

      [Picha katika ukurasa wa 4, 5]

      Gereza lenye ulinzi mkali la La Santé huko Paris, Ufaransa

      [Hisani]

      AP Photo/Francois Mori

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Wanawake wakiwa gerezani huko Managua, Nikaragua

      [Hisani]

      AP Photo/Javier Galeano

  • Je, Kweli Wahalifu Wanaweza Kurekebishwa?
    Amkeni!—2001 | Mei 8
    • Je, Kweli Wahalifu Wanaweza Kurekebishwa?

      “Hakuna mtu anayeweza kumrekebisha mwanadamu mwingine kwa lazima. Ni sharti mtu mwenyewe aamue na awe tayari kujirekebisha.”—VIVIEN STERN, KITABU A SIN AGAINST THE FUTURE—IMPRISONMENT IN THE WORLD.

      NJIA bora ya kuwarekebisha kabisa wafungwa ni kuwaelimisha na kuwasaidia warekebishe maadili yao na mtazamo wao. Bila shaka, kuna watu wanyoofu ambao wanajitahidi kuwaelimisha na kuwasaidia wafungwa. Wafungwa wengi wanathamini jinsi ambavyo watu hao wanajitolea kuwasaidia.

      Huenda watu fulani wakabisha kwamba mfumo wa magereza hauwezi kuboreshwa na hivyo si rahisi kwa wafungwa kurekebishwa katika mazingira hayo. Ingawa ni kweli kwamba kumfunga mtu gerezani tu hakuwezi kumfunza maadili mapya, hata hivyo, mafunzo ya Biblia yamewasaidia wafungwa fulani kurekebisha maisha yao. Hilo laonyesha kwamba mtu mmoja-mmoja anaweza kujirekebisha.

      Leo, baadhi ya wafungwa wanafanya marekebisho maishani kwa msaada wa Biblia ili wawe na fikira na mwenendo ufaao. Jinsi gani? Kwa kutii shauri hili la Biblia: “Komeni kufanyizwa kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo, bali mgeuzwe umbo kwa kufanya upya akili yenu, ili mpate kujithibitishia wenyewe mapenzi ya Mungu yaliyo mema na yenye kukubalika na makamilifu.” (Waroma 12:2) Hilo hutimizwaje?

      Umuhimu wa Biblia

      Watu wengi hufikiri kwamba dini inaweza kuwasaidia sana wafungwa watubu mwenendo mbaya waliokuwa nao hapo awali. Bila shaka, tatizo linalozuka ni kwamba mfungwa aliyerekebishwa gerezani aweza kuendelea na uhalifu mara tu aachiliwapo. Mfungwa mmoja alisema hivi: “Watu wengi hudai kwamba wamepata kumwamini Kristo gerezani—lakini wanapoachiliwa, wanamsahau Kristo kabisa!”

      Mambo yaliyoonwa yanathibitisha kwamba ni lazima marekebisho halisi yatukie ndani ya moyo na akili ya mhalifu, na kwamba ni lazima atubu kwa moyo mwenendo mwovu wa awali. Elimu ya Biblia inaweza kumsaidia mtu aelewe maoni ya Mungu kuhusu uovu na sababu inayofanya uchukize. Elimu hiyo yaweza kumsaidia aone umuhimu wa kuacha kabisa mwenendo mwovu.

      Mashahidi wa Yehova wanatoa elimu ya Biblia katika magereza mengi ulimwenguni pote, na wamepata matokeo mazuri sana. (Ona ukurasa wa 10.) “Kupitia Biblia tumefundishwa kuhusu kusudi la uhai na baraka ambazo wanadamu watapata wakati ujao,” akasema mfungwa mmoja, kisha akaongeza hivi: “Ni elimu bora sana!” Mfungwa mwingine alisema: “Tunatumia shauri la Mungu kufanya maamuzi. . . . Maisha yetu yamebadilika. Twajua mambo yanayohitaji kutangulizwa maishani.”

      Bila shaka, si wafungwa tu wanaohitaji kurekebishwa, wala magereza. Suluhisho bora kwa matatizo yanayokabili magereza ni kutatua kiini cha tatizo hilo. Mojawapo ya kweli nzuri kabisa za Biblia ambazo zimegusa mioyo ya wafungwa wengi inaonyeshwa na ahadi hii ya Mungu: “Watenda mabaya wataharibiwa . . . Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”—Zaburi 37:9, 29.

      Hilo litakapotukia, viwango bora zaidi vya Mungu vitatekelezwa na serikali isiyo na ufisadi yenye upendo na iliyo thabiti, Ufalme wa Mungu wa mbinguni utakaoongozwa na Kristo. Hiyo ndiyo serikali ambayo Wakristo wamefunzwa kusali juu yake. (Mathayo 6:10) Katika ulimwengu huo mpya, kila mkazi atakuwa amefanya marekebisho kwa kujifunza sheria bora za Mungu. Kisha kwa njia isiyo na kifani, “dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:9) Matokeo yatakuwa nini? Wakazi wenye kutii sheria wa ulimwengu huo mpya “watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      Wafungwa Wapata Fursa ya Kuwa na Tumaini

      Kwa zaidi ya miaka 20, wahudumu wajitoleaji wa Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakitoa elimu ya Biblia kwa mafanikio katika gereza kuu la Atlanta, Georgia, Marekani. Zaidi ya wafungwa 40 wamesaidiwa kuwa wahudumu waliobatizwa wa Mashahidi wa Yehova, na wafungwa wengine zaidi ya 90 wamenufaika pia kwa kujifunza Biblia kwa ukawaida.

      Hivi karibuni mwandishi wa Amkeni! aliwahoji walimu kadhaa wa Biblia ambao wamejitolea kuwaelimisha wafungwa katika gereza hilo.

      ◼ Kwa nini elimu ya Biblia ina matokeo sana katika kuwachochea wafungwa fulani warekebishe maisha yao?

      David: Wafungwa wengi ni watu ambao hawakuonyeshwa upendo, hata walipokuwa watoto. Kwa hiyo, wanapopata kujua kwamba Mungu anawapenda na wanaposali kwake kutoka moyoni na kujibiwa wanamwona kuwa halisi. Kisha mioyo yao huwachochea kumpenda.

      Ray: Nilimfunza Biblia mfungwa mmoja aliyetendewa vibaya kingono utotoni. Nilipomwuliza kilichomfanya ampende Yehova, alijibu kwamba unapojifunza kweli ya Biblia, unapata kujua kwamba Yehova anakuelewa. Hilo lilimchochea kujifunza mengi kuhusu utu wa Mungu huyo mwenye upendo.

      ◼ Watu wengine hudai kwamba wafungwa hujiunga na dini kwa makusudi mabaya—ili kupunguziwa kifungo chao au kupitisha tu wakati. Waonaje?

      Fred: Tunapojifunza na wafungwa, tunawavutia kwa kusababu nao wala si kwa kuamsha hisia zao. Sisi hujifunza tu Biblia nao. Muda si muda, wao huelewa kwamba watafunzwa Biblia, na hatujihusishi na mambo mengine. Baadhi ya wafungwa wamenijia na kuniomba niwasaidie kushughulikia kesi zao mahakamani. Mimi hukataa. Tokeo ni kwamba wale wanaojiunga na kikundi cha wanaojifunza na kuendelea ni wale wanaopendezwa kikweli kujifunza Biblia.

      Nick: Jambo moja ninaloona ni marekebisho ambayo wafungwa fulani hufanya wakiwa gerezani. Baadhi yao wamekuwa wahudumu waliobatizwa na wameteswa sana na wafungwa wenzao. Wamestahimili mno. Kama Biblia haingegusa mioyo yao, hawangeweza kubaki waaminifu chini ya hali hizo.

      Israel: Kwa kawaida hao ni watu wanaotaka kujifunza kuhusu Yehova kwa moyo wao wote. Wao hudhihirisha upendezi wao kwa njia yenye kugusa moyo sana. Waweza kuona kwamba wanapendezwa kwa moyo wote.

      Joe: Wale ambao wamekuwa Wakristo wa kweli wamepata kuelewa sababu iliyofanya maisha yao yaharibike. Wao pia wanaelewa kwamba wanaweza kufanya marekebisho na kuwa na tumaini. Sasa wanaweza kutarajia kwa moyo wote utimizo wa ahadi za Yehova za wakati ujao.

      ◼ Kwa nini mfumo wa magereza peke yake hauwezi kuwarekebisha wahalifu?

      Joe: Kusudi la magereza ni kuwatenga wahalifu na jamii wala si kuwarekebisha. Hicho ndicho kiini cha tatizo hilo—yaani, maoni ya wana-magereza kuwaelekea wahalifu.

      Henry: Magereza hayawezi kubadili mielekeo ya wakosaji. Wengi wao huendelea kutenda uhalifu uleule mara tu waachiliwapo.

      [Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Wafungwa wengi wamesaidiwa kujifunza kweli ya Biblia

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki