-
Unachunguzwa?Amkeni!—2003 | Januari 22
-
-
Unachunguzwa?
ELIZABETH huchunguzwa kwa kamera kila siku anapokuwa kazini. Kamera moja humtazama moja kwa moja usoni, na kamera nyingine nyingi huchunguza kila jambo analofanya. Uchunguzi huo wa hali ya juu ni wa kawaida katika kampuni hiyo kwa sababu inashughulikia mamilioni ya pesa taslimu kila siku.
Elizabeth anajua kwamba atachunguzwa kwa makini kazini kwa sababu alipoajiriwa alielezwa waziwazi jambo hilo. Hata hivyo, mamilioni ya watu wengine hawajui ni kwa kadiri gani wanachunguzwa kila siku.
Kuishi Katika Ulimwengu Ambamo Watu Wanachunguzwa
Je, wewe huchunguzwa kazini? Mamilioni ya wafanyakazi ulimwenguni pote huchunguzwa daima wanapotumia Internet na kuandika Barua-pepe. Uchunguzi wa kila mwaka wa Shirika la Usimamizi la Marekani wa mwaka wa 2001 uligundua kwamba “karibu robo tatu (asilimia 73.5) ya makampuni makubwa ya Marekani . . . hurekodi na kuchunguza mawasiliano ya wafanyakazi wake wakati wa kazi, kama vile mawasiliano ya simu, barua-pepe, matumizi ya Internet na faili wanazohifadhi kwenye kompyuta.”
Serikali hutumia pesa nyingi kununua vifaa vya kuchunguza utendaji wa watu. Ripoti moja iliyokabidhiwa Bunge la Ulaya mnamo Julai 11, 2001, ilisema kwamba “kuna mfumo wa kunasa mawasiliano kati ya watu ulimwenguni pote unaotumiwa kwa ushirikiano nchini Marekani, Muungano wa Uingereza, Kanada, Australia na New Zealand.” Inaripotiwa kwamba serikali hizo zinaweza kutumia mfumo unaoitwa ECHELON wenye vituo vya setilaiti ulimwenguni pote, kunasa na kukagua ujumbe wa setilaiti unaotumwa kupitia simu, faksi, Internet, na Barua-pepe. Gazeti Australian linadai kwamba kwa kutumia mfumo huo, serikali zinaweza “kunasa faksi na barua-pepe za watu fulani, na kuna programu inayoweza kutambua sauti fulani, na hivyo simu zinazopigwa na watu hao zinaweza kusikilizwa.”
Mamlaka zinazotekeleza sheria hutegemea pia mbinu za kisasa za kupeleleza. Nchini Marekani, gazeti la BusinessWeek linaripoti kwamba Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) hutumia mfumo unaoitwa Carnivore “kukagua barua-pepe, ujumbe unaotumwa haraka kwa kompyuta, na simu zinazopigwa kwa njia ya kielektroni.” Kwa sasa, sheria mpya imetungwa nchini Uingereza ili kuruhusu mamlaka zinazotekeleza sheria ‘kupeleleza kisiri maelfu ya watu wanaotumia simu, faksi na Internet,’ laripoti Shirika la Utangazaji la Uingereza.
Kamera Zilizofichwa na Hifadhi za Habari Nyingi Katika Kompyuta
Huenda mtu akawa anachunguzwa hata asipotumia simu, faksi, au Barua-pepe. Katika jimbo la New South Wales nchini Australia, watu wanaosafiri kwa gari-moshi huchunguzwa na zaidi ya kamera 5,500. Katika jimbo hilohilo, mabasi 1,900 ya serikali yana kamera za kuwachunguza abiria.
Inaripotiwa kwamba Uingereza ina kamera nyingi zaidi ulimwenguni zinazowachunguza watu ikilinganishwa na idadi ya watu—uchunguzi mmoja unaonyesha kwamba kuna kamera 1 kwa kila watu 55. Mnamo mwaka wa 1996, kulikuwa na kamera kwenye sehemu za umma za miji au majiji 74 tu katika Muungano wa Uingereza. Kufikia mwaka wa 1999, kamera hizo zilikuwa katika miji na majiji 500. Programu mpya za kompyuta zinaunganishwa na kamera ambazo zinaweza kumtambua mtu fulani hususa, hata akiwa katikati ya umati kwenye eneo la umma au katika uwanja wa ndege.
Sasa kuliko wakati mwingine wowote, maisha yako ya faraghani yanaweza kuchunguzwa bila hata wewe kujua. Simon Davies, mkurugenzi wa kikundi cha kutetea haki za binadamu cha Privacy International, anasema: “Habari kuhusu umma zimekusanywa kwa wingi sana sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Habari nyingi kuhusu mfanyakazi wa kawaida katika nchi zilizositawi zimehifadhiwa katika vituo vikuu 400 vya kompyuta—habari hizo ni nyingi sana hivi kwamba kila mtu anaweza kuwa na kitabu kikubwa chenye habari zake.”
Ni hatua gani unazoweza kuchukua ili kulinda faragha yako?
-
-
Ugumu wa Kulinda FaraghaAmkeni!—2003 | Januari 22
-
-
Ugumu wa Kulinda Faragha
“MTU ALIYE MASKINI HOHEHAHE ANAWEZA KUKINZA MAMLAKA YA MFALME WA UINGEREZA AKIWA NYUMBANI MWAKE.”—WILLIAM PITT, MWANASIASA MWINGEREZA, MWAKA WA 1759-1806.
MANENO hayo ya Pitt yanadokeza kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na faragha, kuwa na mambo ya siri maishani mwake bila kuingiliwa na mtu yeyote yule.
Watu wa tamaduni mbalimbali huwa na maoni tofauti-tofauti kuhusu faragha. Kwa mfano, kwenye kisiwa cha Samoa katika Pasifiki, kwa kawaida nyumba hazina kuta, na wapita-njia wanaweza kuona kwa urahisi mambo mengi yanayotendeka humo. Hata hivyo, kuingia katika nyumba bila kukaribishwa huonwa kuwa utovu wa adabu.
Kwa muda mrefu watu wametambua uhitaji wa kuwa na kiasi fulani cha faragha. Maelfu ya miaka kabla ya William Pitt kusema maneno hayo yanayojulikana sana, Biblia ilionyesha uhitaji wa kuheshimu faragha ya wengine. Mfalme Sulemani aliandika hivi: “Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; asije akakukinai na kukuchukia.” (Mithali 25:17) Mtume Paulo alishauri hivi: ‘Fanyeni iwe shabaha yenu kushughulika na mambo yenu wenyewe.’—1 Wathesalonike 4:11.
Likionyesha umuhimu wa kuwa na faragha, gazeti la The UNESCO Courier linasema kwamba faragha “ndiyo msingi wa haki zote za raia.” Pia, mwanasiasa maarufu wa Amerika ya Latini alisema hivi: “Kwa njia fulani, haki zote za binadamu zinahusiana na haki ya kuwa na faragha.”
Hata hivyo, uhalifu na ugaidi unapozidi kuongezeka ulimwenguni, serikali na mamlaka zinazotekeleza sheria zinahisi kwamba ni lazima ziingilie mambo ya watu ya faraghani ili kuwalinda raia. Kwa nini? Kwa sababu wahalifu katika jamii hutumia haki ya kuwa na faragha kuwa udhuru wa kutenda uovu. Kwa hiyo, tatizo lililopo ni kusawazisha jukumu la serikali la kuwalinda raia na haki ya kila mtu kuwa na faragha.
Faragha na Usalama
Mashambulizi ya kigaidi yaliyoshtua ulimwengu mnamo Septemba 11, 2001, yalibadili maoni ya watu kuhusu haki ya serikali ya kuingilia mambo fulani ya siri katika maisha ya watu. Mtu mmoja aliyekuwa mshiriki wa tume ya biashara ya Marekani aliliambia gazeti la BusinessWeek kwamba “Septemba 11 ilibadili mambo.” Alisema hivi: “Magaidi husitawi katika jamii ambayo inalinda faragha yao. Ikiwa ni lazima maisha yao ya faragha yaingiliwe kwa kiasi fulani ili kuwafichua, watu wengi watasema ‘ni sawa, fanyeni hivyo.’” Gazeti hilo linaripoti hivi: “Maoni yaliyokusanywa tangu Septemba 11 yanaonyesha kwamba asilimia 86 ya Wamarekani wanaunga mkono matumizi ya mifumo inayotambua nyuso za watu; asilimia 81 wanataka shughuli za benki na matumizi ya kadi za mikopo yachunguzwe kwa makini; na asilimia 68 wanaunga mkono matumizi ya kitambulisho cha kitaifa.”
Serikali fulani za Ulaya na Amerika zinafikiria kutumia vitambulisho ambavyo vinaweza kuhifadhi alama za vidole na picha ya retina ya jicho la mwenye kitambulisho hicho na vitatumiwa kuchunguza hali yake ya kifedha na iwapo amewahi kuhusika katika uhalifu wowote. Kwa kutumia tekinolojia fulani, inawezekana kulinganisha habari iliyo kwenye kitambulisho na habari iliyo kwenye kadi ya mkopo na kuutambua uso wa mtumiaji kwa kamera maalumu. Hivyo wahalifu wanaweza kukamatwa wanapotaka kununua vitu wanavyonuia kutumia katika uhalifu.
Wahalifu wakijaribu kuficha mabomu, bunduki, au visu ndani ya nguo, au hata kuvificha ndani ya nyumba, bado wanaweza kukamatwa. Mashine zinazotumiwa na mashirika fulani ya usalama zinaweza kutambua kitu chochote kilicho nguoni mwako. Vifaa vipya vya rada vinawawezesha polisi kutambua watu wanaotembea au hata kupumua katika chumba kilicho karibu. Lakini je, mbinu za kisasa zaidi za uchunguzi zinapunguza uhalifu?
Je, Kamera Zinawazuia Wahalifu?
Uhalifu ulipoanza kuongezeka huko Bourke, mji ulio mashambani mwa Australia, kamera nne zilizounganishwa na televisheni ziliwekwa. Kamera hizo zilisaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa. Lakini matokeo hayo hayako kila mahali. Katika jitihada za kupunguza uhalifu huko Glasgow, Scotland, kamera 32 za aina hiyo ziliwekwa mnamo mwaka wa 1994. Uchunguzi uliofanywa na Kituo Kikuu cha Utafiti cha Scotland ulionyesha kwamba mwaka uliofuata, visa fulani vya uhalifu vilipungua. Hata hivyo, ripoti hiyo inasema hivi: “Idadi ya visa vya uhalifu unaohusiana na ukosefu wa maadili, kutia ndani ukahaba, iliongezeka hadi 120; ulaghai uliongezeka hadi 2185; na makosa mengine (pamoja na makosa yanayohusu dawa za kulevya) yaliongezeka hadi 464.”
Mifumo hiyo ya uchunguzi inaweza kupunguza uhalifu katika maeneo fulani tu lakini huenda isipunguze uhalifu kwa ujumla. Gazeti la The Sydney Morning Herald lilitaja kwamba polisi na wachunguzi wa uhalifu walisema kuwa ongezeko la uhalifu husababishwa na ‘kuhama.’ Gazeti hilo lilisema: “Wahalifu wanapogundua kwamba wanaweza kunaswa kwa kamera au na polisi wa doria katika eneo fulani, wanahamia eneo jingine ili kufanya uhalifu.” Huenda jambo hilo likakukumbusha maneno yaliyoandikwa kwenye Biblia miaka mingi iliyopita: “Yeye ambaye huzoea kufanya mambo maovu huchukia nuru na haji kwenye nuru, ili kazi zake zisipate kukaripiwa.”—Yohana 3:20.
Tatizo linalokabili mamlaka zinazotekeleza sheria ni kwamba hata mfumo wa kisasa zaidi wa rada au unaotumia eksirei hauwezi kutambua mambo yaliyo akilini na moyoni mwa mtu, na humohumo ndimo mapambano ya kukomesha uhalifu, chuki na jeuri yanapaswa kuanzia.
Hata hivyo, kuna namna fulani ya uchunguzi ambao ni bora kuliko tekinolojia yoyote iliyovumbuliwa na mwanadamu. Makala inayofuata itazungumzia uchunguzi huo na jinsi unavyoweza kubadili kabisa tabia ya wanadamu.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Magaidi husitawi katika jamii ambayo inalinda faragha yao”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Je, Rekodi Zako za Tiba Ni Siri?
Watu wengi hufikiri kwamba rekodi zao za tiba na mazungumzo yao pamoja na daktari na mamlaka za hospitali ni siri kabisa. Hata hivyo, shirika la Privacy Rights Clearinghouse linalolinda faragha ya watu linaonya kwamba “huenda ukawa umedanganyika kuwa u usalama.” Simson Garfinkel anasema hivi katika kitabu chake, Database Nation—The Death of Privacy in the 21st Century: “Leo, rekodi za tiba zinatumiwa kwa makusudi mbalimbali . . . Zinatumiwa na waajiri wanapowatafuta wafanyakazi na makampuni ya bima kutafuta wanunuzi wa bima. Zinatumiwa na hospitali na mashirika ya kidini kuomba michango. Hata wafanyabiashara wananunua rekodi chungu nzima za tiba ili wajue watu wanaoweza kununua bidhaa zao.”
Garfinkel aongezea hivi: “Ni vigumu sana kuweka habari hizo zikiwa siri kwa sababu kila mara mgonjwa anapoenda hospitalini, rekodi yake ya tiba husomwa na watu 50 hadi 75.” Katika sehemu nyingine, huenda wagonjwa wenyewe wakafunua mambo yao ya siri kwa kutia sahihi bila kujua hati zinazohusu mambo mbalimbali au fomu za idhini wanapoenda hospitalini. Unapotia sahihi fomu hizo, “unamruhusu daktari atoe habari zako za tiba kwa makampuni ya bima, mashirika ya kiserikali na mashirika mengineyo,” lasema shirika la Privacy Rights Clearinghouse.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Faragha Katika Biashara
Faragha ya watu wanaotumia Internet inaweza kuingiliwa na mtu yeyote yule. Shirika la Privacy Rights Clearinghouse linasema hivi: “Hakuna huduma zozote za Internet zinazoweza kutuhakikishia haki ya faragha. . . . Watumiaji wa Internet wanaweza kupata habari kwenye vituo mbalimbali . . . , au watumiaji wanaweza tu ‘kusoma’ habari hizo bila kuzibadili. Watumiaji wengi hufikiri kwamba hawawezi kujulikana wanapofanya hivyo. Hiyo si kweli. Unaweza kujua mambo yaliyofanywa na mtu kwenye Internet, kutia ndani mashirika ya habari au faili na vituo vilivyotazamwa na mteja. . . . Rekodi zinazoonyesha ‘mazoea ya mteja ya kutumia Internet’ . . . zinaweza kutumiwa kuchuma pesa nyingi sana . . . Habari hiyo huwasaidia sana wafanyabiashara kupata orodha ya watumiaji wa Internet ambao wanapenda bidhaa au huduma fulani hususa.”
Jina lako linawezaje kuingia kwenye orodha ya wafanyabiashara wanaotafuta wateja moja kwa moja kwenye Internet? Jina lako linaweza kuingizwa kwenye orodha yao ukifanya mojawapo ya mambo yafuatayo:
◼ Ukijaza fomu ya dhamana ya bidhaa kutoka kwa watengenezaji au kadi za kukubali bidhaa fulani.
◼ Ukijiunga au kutoa michango kwa klabu, mashirika, au vyama vya kutoa misaada.
◼ Ukiandikisha magazeti, vitabu, kanda au CD za muziki.
◼ Ukiandikisha jina na anwani yako kwenye kitabu cha orodha ya namba za simu.
◼ Ukishiriki mashindano ya bahati nasibu au mashindano mengineyo.
Zaidi ya hayo, unapotumia kadi ya kutoa pesa, kadi ya mkopo, au unaponunua vitu kwa kadi ya malipo, kampuni hiyo inaweza kuandika jina na anwani yako pamoja na vitu unavyonunua wakati mashine inaposoma bei yake. Na hivyo habari nyingi kuhusu bidhaa unazopenda kununua zinaweza kukusanywa na labda kutumiwa kwa makusudi ya kibiashara.a
[Maelezo ya Chini]
a Habari hii imetolewa kwenye Kituo cha Internet cha shirika la Privacy Rights Clearinghouse.
[Picha katika kurasa za 6, 7]
Je, kamera za kuchunguza watu hupunguza uhalifu?
-