Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Fulizeni Kunitarajia”
    Mnara wa Mlinzi—1996 | Machi 1
    • “Fulizeni Kunitarajia”

      “Basi ningojeni [“fulizeni kunitarajia,” “NW”], asema BWANA.”—SEFANIA 3:8.

      1. Ni onyo gani lililotolewa na nabii Sefania, na hilo lina upendezi gani kwa watu wanaoishi leo?

      “SIKU ya BWANA iliyo kuu i karibu.” Kilio hicho chenye onyo kilitolewa na nabii Sefania katikati ya karne ya saba K.W.K. (Sefania 1:14) Katika miaka 40 au 50 iliyofuata, huo unabii ulitimizwa wakati siku ya kutekeleza hukumu za Yehova ilipowadia Yerusalemu na pia mataifa yale yaliyokaidi enzi kuu ya Yehova kwa kuwatendea vibaya watu wake. Kwa nini jambo hili lipendeze watu wanaoishi mwishoni mwa karne ya 20? Tunaishi wakati ‘siku iliyo kuu’ ya mwisho ya Yehova inapokaribia upesi. Kama ilivyokuwa na wakati wa Sefania, “hasira kali” ya Yehova i karibu kutokea dhidi ya kifanani cha kisasa cha Yerusalemu—Jumuiya ya Wakristo—na dhidi ya mataifa yote yanayowatendea vibaya watu wa Yehova na kukaidi enzi yake kuu ya ulimwengu wote mzima.—Sefania 1:4; 2:4, 8, 12, 13; 3:8, NW; 2 Petro 3:12, 13.

      Sefania—Shahidi Mwenye Moyo Mkuu

      2, 3. (a) Twajua nini kuhusu Sefania, na ni nini kinachoonyesha kwamba alikuwa shahidi wa Yehova mwenye moyo mkuu? (b) Ni mambo gani yanayotusaidia kujua wakati na mahali ambapo Sefania alitoa unabii?

      2 Ni mambo machache tu yanayojulikana kuhusu nabii Sefania, ambaye jina lake (Kiebrania, Tsephan·yahʹ) lamaanisha “Yehova Amesitiri (Amehazini).” Hata hivyo, tofauti na manabii wengine Sefania alitaja nasaba yake hadi kizazi cha nne, kufikia “Hezekia.” (Sefania 1:1; linganisha Isaya 1:1; Yeremia 1:1; Ezekieli 1:3.) Hili ni jambo lisilo la kawaida sana hivi kwamba wafafanuzi wengi husema kwamba babu ya babu yake alikuwa Mfalme Hezekia aliyekuwa mwaminifu. Ikiwa ni kweli, basi Sefania alikuwa wa uzao wa kifalme, na hilo lingeongezea uzito shutuma yake kwa wakuu wa Yuda na kuonyesha kwamba alikuwa shahidi mwenye moyo mkuu na nabii wa Yehova. Ujuzi wake mkubwa wa mandhari ya Yerusalemu na yale yaliyokuwa yakitendeka katika baraza la kifalme wadokeza kwamba huenda ikawa alitangaza hukumu za Yehova katika jiji kuu lenyewe.—Ona Sefania 1:8-11, New World Translation of the Holy Scriptures—With References, vielezi-chini.

      3 Jambo kuu ni kwamba ingawa Sefania alitangaza hukumu za kimungu dhidi ya “wakuu” wa kijamii wa Yuda (watu wenye vyeo vikubwa, au wakuu wa makabila) na “wana wa mfalme,” yeye hakutaja kamwe mfalme mwenyewe katika uchambuzi wake.a (Sefania 1:8; 3:3) Hilo ladokeza kwamba Mfalme Yosia mchanga tayari alikuwa ameonyesha mwelekeo mzuri kwa ajili ya ibada safi, ingawa, kwa kutazama hali iliyoshutumiwa na Sefania, kwa wazi hakuwa ameanza kufanya marekebisho yake ya kidini. Hayo yote yadokeza kwamba Sefania alitoa unabii katika Yuda katika miaka ya mapema ya Yosia, aliyetawala kuanzia 659 hadi 629 K.W.K. Unabii uliotolewa kwa bidii na Sefania bila shaka ulimsaidia Yosia mchanga kutambua kwamba ibada ya sanamu, jeuri, na ufisadi ulienea katika Yuda wakati huo na kutia nguvu kampeni yake ya baadaye dhidi ya ibada ya sanamu.—2 Mambo ya Nyakati 34:1-3.

      Sababu za Hasira Kali ya Yehova

      4. Ni katika maneno gani Yehova alitaja hasira yake dhidi ya Yuda na Yerusalemu?

      4 Yehova alikuwa na sababu nzuri za kuhisi hasira dhidi ya viongozi na wakazi wa Yuda na jiji lalo kuu la Yerusalemu. Kupitia nabii wake Sefania, yeye alisema: “Nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani; na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa BWANA na kuapa pia kwa Malkamu.”—Sefania 1:4, 5.

      5, 6. (a) Kulikuwa na hali gani ya kidini katika Yuda wakati wa Sefania? (b) Viongozi wa kijamii wa Yuda na wale waliotumikia chini yao walikuwa na hali gani?

      5 Yuda lilichafuliwa na matendo yenye kupotoka ya ibada ya kiuzazi ya Baali, unajimu wa kishetani, na ibada ya mungu wa kipagani Malkamu. Ikiwa Malkamu ndiye Moleki, kama vile wengine wanavyodokeza, basi ibada bandia ya Yuda ilitia ndani tendo lenye kuchukiza mno la kuwadhabihu watoto. Mazoea hayo ya kidini yalimchukiza sana Yehova. (1 Wafalme 11:5, 7; 14:23, 24; 2 Wafalme 17:16, 17) Walimfanya akasirike hata zaidi kwa kuwa hawa waabudu sanamu bado waliapa kwa jina la Yehova. Hangevumilia tena ukosefu huo wa usafi wa kidini naye angewakatilia mbali wote makuhani wapagani na makuhani waasi-imani.

      6 Isitoshe, viongozi wa kijamii wa Yuda walikuwa wafisadi. Wakuu walo walikuwa kama “simba wangurumao,” na waamuzi wao walilinganishwa na “mbwa-mwitu” wenye pupa. (Sefania 3:3) Wale waliotumikia chini yao walishutumiwa ‘kujaza nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu.’ (Sefania 1:9) Ufuatiaji wa vitu vya kimwili ulienea. Wengi walikuwa wakitumia fursa hiyo kurundika mali.—Sefania 1:13.

      Shaka Kuhusu Siku ya Yehova

      7. Sefania alitoa unabii muda gani kabla ya “siku ya BWANA iliyo kuu,” na Wayahudi wengi walikuwa na hali gani ya kiroho?

      7 Kama tulivyokwisha kuona, hali mbaya sana ya kidini iliyoenea katika siku ya Sefania yaonyesha kwamba alifanya kazi yake akiwa shahidi na nabii kabla ya Mfalme Yosia kuanza kampeni yake dhidi ya ibada ya sanamu, karibu 648 K.W.K. (2 Mambo ya Nyakati 34:4, 5) Basi, yaelekea kwamba Sefania alitoa unabii angalau miaka 40 kabla ya “siku ya BWANA iliyo kuu” kuja juu ya ufalme wa Yuda. Katika kipindi hicho, Wayahudi wengi walikuwa na shaka ‘wakarudi nyuma’ wakiacha kumtumikia Yehova na kuwa wasiojali. Sefania asema juu ya wale “wasiomtafuta BWANA, wala kumwulizia.” (Sefania 1:6) Kwa wazi, watu mmoja-mmoja katika Yuda walikuwa na ubaridi, wasijihusishe na Mungu.

      8, 9. (a) Kwa nini Yehova angekagua “watu walioganda juu ya sira zao”? (b) Ni katika njia zipi Yehova angewapa uangalifu wakazi wa Yuda na viongozi wao wa kijamii na kidini?

      8 Yehova alijulisha kusudi lake la kukagua wale wanaodai kuwa watu wake. Miongoni mwa wale waliodai kuwa waabudu wake, angewatafuta wale waliokuwa na shaka katika mioyo yao juu ya uwezo wake au kusudi lake la kuingilia mambo ya wanadamu. Yeye alisema hivi: “Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.” (Sefania 1:12) Usemi “watu walioganda juu ya sira zao” (kwa kurejezea kutengeneza divai) warejezea wale ambao wametulia, kama sira chini ya pipa la divai, wasiotaka kusumbuliwa na tangazo lolote kwamba karibuni Mungu ataingilia mambo ya wanadamu.

      9 Yehova angeelekeza fikira kwa wakazi wa Yuda na Yerusalemu na kwa makuhani wao waliokuwa wamechanganya ibada yake na upagani. Ikiwa walihisi salama, kana kwamba walifichwa na giza la usiku ndani ya kuta za Yerusalemu, yeye angewafichua kwa taa nyangavu ambazo zingepenya giza la kiroho ambamo walikuwa wamekimbilia. Angewaondoa kwenye ubaridi wao wa kidini, kwanza kwa jumbe zenye nguvu sana za hukumu, kisha kwa kutekeleza hukumu hizo.

      “Siku ya BWANA Iliyo Kuu I Karibu”

      10. Sefania alifafanuaje “siku ya BWANA iliyo kuu”?

      10 Yehova alimpulizia Sefania kupiga mbiu: ‘Siku ya BWANA iliyo kuu i karibu; i karibu, nayo inafanya haraka sana; naam, sauti ya siku ya BWANA ni chungu.’ (Sefania 1:14) Kwa kweli siku zenye uchungu mno zilikuwa mbele ya kila mtu—makuhani, wakuu, na watu—aliyekataa kutii onyo na kurudia ibada safi. Ukifafanua siku hiyo ya kutekeleza hukumu, unabii huo waendelea kusema: “Siku ile ni siku ya ghadhabu, siku ya fadhaa na dhiki, siku ya uharibifu na ukiwa, siku ya giza na utusitusi, siku ya mawingu na giza kuu, siku ya tarumbeta na ya kamsa, juu ya miji yenye maboma, juu ya buruji zilizo ndefu sana.”—Sefania 1:15, 16.

      11, 12. (a) Ni ujumbe gani wenye hukumu uliotangazwa dhidi ya Yerusalemu? (b) Je, ufanisi wa kimwili ungeokoa Wayahudi?

      11 Katika miongo michache mifupi, majeshi ya Babiloni yangevamia Yuda. Yerusalemu halingeponyoka. Maeneo yalo ya makazi na ya biashara yangeharibiwa kabisa. “Katika siku ile, asema BWANA kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani. Haya! lieni, ninyi mkaao katika Makteshi [eneo fulani la Yerusalemu], maana wafanya biashara wote wameangamia; hao wote waliokuwa na mizigo ya fedha wamekatiliwa mbali.”—Sefania 1:10, 11.

      12 Wakikataa kuamini kwamba siku ya Yehova ilikuwa karibu, Wayahudi wengi walijihusisha sana na biashara zenye faida nyingi. Lakini kupitia Sefania, nabii wake mwaminifu, Yehova alitabiri kwamba utajiri wao “utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa.” Wao hawangekunywa divai waliyotengeneza, wala “fedha yao wala dhahabu yao havi[nge]weza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA.”—Sefania 1:13, 18.

      Mataifa Mengine Yahukumiwa

      13. Sefania alitangaza ujumbe gani wenye hukumu dhidi ya Moabu, Amoni, na Ashuru?

      13 Kupitia nabii wake Sefania, Yehova alionyesha hasira yake pia dhidi ya mataifa yaliyokuwa yamewatendea watu wake vibaya. Alitangaza hivi: “Mimi nimeyasikia matukano ya Moabu, na dhihaka za wana wa Amoni, ambazo kwa hizo wamewatukana watu wangu, na kujitukuza juu ya mpaka wao. Basi kama niishivyo, asema BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, Hakika Moabu atakuwa kama Sodoma, na wana wa Amoni kama Gomora, yaani, milki ya upupu, na mashimo ya chumvi, ukiwa wa daima. . . . Naye atanyosha mkono wake juu ya upande wa kaskazini, na kuiangamiza Ashuru; naye ataufanya Ninawi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa.”—Sefania 2:8, 9, 13.

      14. Kuna uthibitisho gani kwamba mataifa ya kigeni ‘yalijitukuza’ juu ya Waisraeli na Mungu wao, Yehova?

      14 Moabu na Amoni walikuwa maadui wa Israeli wa tangu zamani. (Linganisha Waamuzi 3:12-14.) Jiwe la Moabu, lililo katika Louvre Museum katika Paris, lina maandiko yenye taarifa ya kujisifu iliyotolewa na Mfalme Mesha wa Moabu. Yeye asimulia kwa majivuno jinsi alivyotwaa majiji kadhaa ya Israeli kwa msaada wa mungu wake Kemoshi. (2 Wafalme 1:1) Yeremia, aliyeishi wakati wa Sefania, alisema juu ya Waamoni kuwa wanakalia eneo la Israeli la Gadi katika jina la mungu wao Malkamu. (Yeremia 49:1) Kuhusu Ashuru, Mfalme Shalmanesa 5 alizingira na kuteka Samaria karibu karne moja kabla ya siku ya Sefania. (2 Wafalme 17:1-6) Baadaye kidogo, Mfalme Senakeribu alishambulia Yuda, akateka majiji mengi yenye ngome, na hata kutisha Yerusalemu. (Isaya 36:1, 2) Msemaji wa mfalme wa Ashuru alijitukuza juu ya Yehova alipokuwa akidai Yerusalemu lisalimu amri.—Isaya 36:4-20.

      15. Yehova angeaibishaje miungu ya mataifa yaliyojitukuza juu ya watu wake?

      15 Zaburi 83 hutaja mataifa kadhaa, kutia ndani Moabu, Amoni, na Ashuru, waliojitukuza juu ya Israeli, na kusema hivi kwa kujigamba: “Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, na jina la Israeli halitakumbukwa tena.” (Zaburi 83:4) Nabii Sefania alitangaza kwa moyo mkuu kwamba mataifa hayo yote yenye kiburi na miungu yayo yangeaibishwa na Yehova wa majeshi. “Mambo hayo yatawapata kwa sababu ya kiburi chao, kwa kuwa wamewatukana watu wa BWANA wa majeshi, na kujitukuza juu yao. BWANA atakuwa mwenye kuwatisha sana; kwa maana atawafisha kwa njaa miungu yote ya dunia; na watu watamsujudia yeye, kila mtu toka mahali pake; naam, nchi zote za mataifa.”—Sefania 2:10, 11.

      “Fulizeni Kunitarajia”

      16. (a) Ni kwa akina nani kuja kwa siku ya Yehova kulikuwa chanzo cha shangwe, na kwa nini? (b) Ni amri gani yenye kuamsha iliyotolewa kwa mabaki waaminifu?

      16 Huku ulegevu wa kiroho, shaka, ibada ya sanamu, ufisadi, na ufuatiaji wa vitu vya kimwili ukienea miongoni mwa viongozi na wakazi wengi wa Yuda na Yerusalemu, yaonekana kwamba baadhi ya Wayahudi waaminifu walisikiliza unabii mbalimbali wenye onyo aliotoa Sefania. Wao walisikitishwa na matendo ya kuchukiza ya wakuu, waamuzi, na makuhani wa Yuda. Matangazo ya Sefania yalikuwa chanzo cha faraja kwa hawa waaminifu-washikamanifu. Badala ya kuwa kisababishi cha huzuni, kuja kwa siku ya Yehova kulikuwa chanzo cha shangwe kwao, kwa sababu kungekomesha matendo hayo yenye kuchukiza. Hawa mabaki waaminifu walitii amri ya Yehova ya kuwaamsha: “Basi ningojeni [“fulizeni kunitarajia,” NW] asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu.”—Sefania 3:8.

      17. Ni lini na ni jinsi gani jumbe zenye hukumu za Sefania zenye hukumu zilianza kutimizwa dhidi ya mataifa?

      17 Wale waliotii onyo hilo hawakushangaa. Wengi waliishi wakaona utimizo wa unabii wa Sefania. Katika 632 K.W.K., Ninawi lilitekwa na kuharibiwa na muungano wa Wababiloni, Wamedi, na vikundi kutoka kaskazini, labda Waskaithia. Mwanahistoria Will Durant asimulia: “Jeshi la Wababiloni chini ya Nabopolasari liliungana na jeshi la Wamedi chini ya Siaksaresi na vikundi vya Waskaithia kutoka Kaukasi, na kwa urahisi na wepesi wenye kushangaza waliteka ngome za kaskazini. . . . Kwa pigo moja Ashuru ilipotea katika historia.” Hivyo ndivyo alivyotabiri Sefania.—Sefania 2:13-15.

      18. (a) Hukumu ya kimungu ilitekelezwaje juu ya Yerusalemu, na kwa nini? (b) Unabii wa Sefania kuhusu Moabu na Amoni ulitimizwaje?

      18 Wayahudi wengi waliofuliza kumtarajia Yehova pia waliishi wakaona hukumu zake zikitekelezwa juu ya Yuda na Yerusalemu. Kuhusu Yerusalemu, Sefania alikuwa ametabiri: “Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake.” (Sefania 3:1, 2) Kwa sababu ya kukosa uaminifu, Yerusalemu lilizingirwa mara mbili na Wababiloni na hatimaye kutekwa na kuharibiwa katika 607 K.W.K. (2 Mambo ya Nyakati 36:5, 6, 11-21) Kwa habari ya Moabu na Amoni, kulingana na Yosefo, mwanahistoria Myahudi, katika mwaka wa tano baada ya Yerusalemu kuanguka, Wababiloni walipiga vita nao na kuwashinda. Wao nao walipotelea mbali, kama ilivyotabiriwa.

      19, 20. (a) Yehova alithawabishaje wale waliofuliza kumtarajia? (b) Kwa nini matukio haya yanatuhusu, na ni mambo yapi yatakayozungumzwa katika makala ifuatayo?

      19 Utimizo wa jambo hili na mambo mengine madogo-madogo ya unabii wa Sefania uliimarisha imani ya Wayahudi na wasio-Wayahudi waliofuliza kumtarajia Yehova. Miongoni mwa wale waliookoka uharibifu uliopata Yuda na Yerusalemu walikuwa Yeremia, Ebed-Meleki Mwethiopia, na nyumba ya Yehonadabu, Mrekabu. (Yeremia 35:18, 19; 39:11, 12, 16-18) Wayahudi waaminifu waliokuwa katika uhamisho na wazao wao, walioendelea kumngoja Yehova, walikuja kuwa sehemu ya mabaki wenye furaha waliokombolewa kutoka Babiloni katika 537 K.W.K. na kurudi Yuda kuanzisha tena ibada safi.—Ezra 2:1; Sefania 3:14, 15, 20.

      20 Mambo haya yote yana maana gani kwetu? Katika njia nyingi hali iliyokuwa katika siku ya Sefania yalingana na mambo yenye kuchukiza yanayotendeka katika Jumuiya ya Wakristo. Isitoshe, mitazamo mbalimbali ya Wayahudi katika nyakati hizo yafanana na mitazamo iwezayo kuonwa leo, nyakati nyingine hata miongoni mwa watu wa Yehova. Haya ni mambo yatakayozungumzwa katika makala ifuatayo.

  • “Mikono Yako Isilegee”
    Mnara wa Mlinzi—1996 | Machi 1
    • “Mikono Yako Isilegee”

      “Mikono yako isilegee. BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa.”—SEFANIA 3:16, 17.

      1. Msomi mmoja wa Biblia alisema nini kuhusu unabii wa Sefania?

      UNABII wa Sefania ulielekeza mbele zaidi ya utimizo wao wa kwanza katika karne za saba na sita K.W.K. Akifafanua Sefania, Profesa C. F. Keil aliandika: “Unabii wa Sefania . . . hauanzi tu na tangazo la hukumu la ulimwengu wote mzima, ambalo linatokeza hukumu juu ya Yuda kwa sababu ya dhambi yalo, na juu ya ulimwengu wa mataifa kwa sababu ya uhasama wao dhidi ya watu wa Yehova; bali [unabii huo] wahusika kotekote katika siku ya Yehova iliyo kuu na yenye kutisha.”

      2. Kuna ulinganifu gani kati ya hali zilizokuwa katika siku ya Sefania na hali iliyoko katika Jumuiya ya Wakristo leo?

      2 Leo, uamuzi wa kihukumu wa Yehova ni kukusanya mataifa kwa ajili ya uharibifu mkubwa zaidi kuliko ule wa siku ya Sefania. (Sefania 3:8) Mataifa yale yanayodai kuwa ya Kikristo hasa yanastahili adhabu machoni pa Mungu. Kama Yerusalemu lilivyoadhibiwa vikali kwa ajili ya kukosa uaminifu kwa Yehova, ndivyo Jumuiya ya Wakristo ni lazima iadhibiwe na Mungu kwa sababu ya njia zayo zenye kupotoka. Hukumu za kimungu zilizotangazwa dhidi ya Yuda na Yerusalemu katika siku ya Sefania hutumika hata kwa nguvu zaidi dhidi ya makanisa na mafarakano ya Jumuiya ya Wakristo. Wao pia wamechafua ibada safi kwa mafundisho yao yenye kumvunjia Mungu heshima, mengi yakiwa ni ya asili ya kipagani. Wamedhabihu mamilioni ya wana wao wenye afya nzuri katika madhabahu ya kisasa ya vita. Isitoshe, wakazi wa kifanani cha Yerusalemu huchanganya ule uitwao eti Ukristo pamoja na unajimu, mazoea ya uwasiliani-roho na ukosefu wa adili katika ngono zenye kupotoka, matendo yafananayo na ibada ya Baali.—Sefania 1:4, 5.

      3. Ni nini laweza kusemwa juu ya viongozi wengi wa kilimwengu na serikali za kisiasa leo, na Sefania alitoa unabii juu ya nini?

      3 Wengi wa viongozi wa kisiasa wa Jumuiya ya Wakristo hupenda kuonwa makanisani. Lakini kama “wakuu,” wa Yuda baadhi yao hutumia watu vibaya kama “simba wangurumao” na “mbwa mwitu” wenye pupa. (Sefania 3:1-3) Watumishi wao wa kisiasa wenye kutaka upendeleo wao ‘wanaijaza nyumba ya Bwana wao udhalimu na udanganyifu.’ (Sefania 1:9) Rushwa na ufisadi umeenea. Kwa habari ya serikali za kisiasa zilizo ndani na nje ya Jumuiya ya Wakristo, idadi yenye kuongezeka ya serikali hizo ‘zinajitukuza’ juu ya watu wa Yehova wa majeshi, Mashahidi wake, zikiwaona kuwa “farakano” lenye kudharauliwa. (Sefania 2:8; Matendo 24:5, 14, NW) Kuhusu viongozi wote wa kisiasa kama hao na wafuasi wao, Sefania alitoa unabii huu: “Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha.”—Sefania 1:18.

      ‘Kufichwa Katika Siku ya Hasira ya BWANA’

      4. Ni nini kionyeshacho kwamba kutakuwa na waokokaji wa siku ya Yehova iliyo kuu, lakini ni lazima hao wafanye nini?

      4 Si wakazi wote wa Yuda walioangamizwa katika karne ya saba K.W.K. Vivyo hivyo kutakuwa na waokokaji wa siku ya Yehova iliyo kuu. Kwa hao, Yehova alisema hivi kupitia nabii wake Sefania: “Kabla haijazaa hiyo amri, kabla haijapita siku ile kama makapi, kabla haijawajilia hasira kali ya BWANA, kabla haijawajilia siku ya hasira ya BWANA. Mtafuteni BWANA, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki [“uadilifu,” NW], utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya BWANA.”—Sefania 2:2, 3.

      5. Katika wakati huu wa mwisho, ni nani waliokuwa wa kwanza kutii onyo la Sefania, na Yehova amewatumiaje?

      5 Katika wakati wa mwisho wa ulimwengu huu, waliokuwa wa kwanza kutii huo mwaliko wa kiunabii walikuwa mabaki ya Waisraeli wa kiroho, Wakristo watiwa-mafuta. (Warumi 2:28, 29; 9:6; Wagalatia 6:16) Kwa kuwa walitafuta uadilifu na unyenyekevu na kuonyesha staha kwa ajili ya maamuzi ya kihukumu ya Yehova, wao walikombolewa kutoka Babiloni Mkubwa, milki ya ulimwengu ya dini bandia, na kurudishwa kwenye upendeleo wa kimungu katika 1919. Tangu wakati huo, na hasa tangu 1922, mabaki hao waaminifu kwa ujasiri wamekuwa wakipiga-mbiu hukumu za Yehova dhidi ya makanisa na mafarakano ya Jumuiya ya Wakristo na dhidi ya mataifa ya kisiasa.

      6. (a) Sefania alitoa unabii gani kuhusu mabaki waaminifu? (b) Unabii huu umetimizwaje?

      6 Kuhusu hao mabaki waaminifu, Sefania alitabiri: “Nami kwa hakika nitaacha wabaki miongoni mwenu watu walio wanyenyekevu na wapole, nao kwa hakika watapata kimbilio katika jina la Yehova. Kuhusu wale wanaobaki wa Israeli, hawatatenda jambo lolote la kukosa uadilifu, wala kusema uwongo, wala hamtapatikana midomoni mwao ulimi wenye ujanja; kwa kuwa wao wenyewe watalisha na hata kujilaza chini, na hakuna mtu atakayewafanya watetemeke.” (Sefania 3:12, 13, NW) Sikuzote Wakristo hawa watiwa-mafuta wametanguliza jina la Yehova, lakini hasa tangu 1931, walipotwaa jina Mashahidi wa Yehova. (Isaya 43:10-12) Kwa kukazia suala la enzi kuu la Yehova, wao wameliheshimu lile jina la kimungu, na hilo limekuwa kimbilio kwao. (Mithali 18:10) Yehova amewalisha kiroho kwa wingi, nao huishi bila hofu katika paradiso ya kiroho.—Sefania 3:16, 17.

      ‘Sifa na Jina Miongoni mwa Watu Wote’

      7, 8. (a) Ni unabii gani zaidi umetimizwa juu ya mabaki ya Israeli wa kiroho? (b) Mamilioni ya watu wametambua nini, na wewe binafsi una hisia zipi kuhusu jambo hili?

      7 Ushikamano wenye kina wa mabaki kwa jina la Yehova na kwa kanuni zenye uadilifu za Neno lake haujapuuzwa. Watu wanyoofu wameona tofauti iliyoko kati ya mwenendo wa mabaki na viongozi wa kidini na wa kisiasa wenye ufisadi na unafiki wa ulimwengu huu. Yehova amewabariki “wanaobaki wa Israeli [wa kiroho].” Amewapa pendeleo la kubeba jina lake, naye amewafanya kuwa na sifa nzuri miongoni mwa watu wa dunia. Ndivyo ilivyotolewa unabii na Sefania: “Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi kuwa sifa na jina, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema BWANA.”—Sefania 3:20.

      8 Tangu 1935, mamilioni ya watu wamekuja kutambua kwamba mabaki wana baraka ya Yehova. Wao hufuata kwa furaha hawa Wayahudi wa kiroho, au Waisraeli, wakisema: “Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.” (Zekaria 8:23) Hawa “kondoo wengine” huwaona hawa mabaki watiwa-mafuta kuwa “mtumwa mwaminifu mwenye akili,” aliyewekwa rasmi na Kristo “juu ya vitu vyake vyote [vya kidunia].” Kwa shukrani wao hushiriki kula chakula cha kiroho kinachotayarishwa na jamii ya mtumwa “kwa wakati wake.”—Yohana 10:16; Mathayo 24:45-47.

      9. Ni “lugha” ipi mamilioni ya watu wamejifunza kuongea, na ni katika kazi gani kubwa kondoo wengine wanatumikia “bega kwa bega” pamoja na mabaki watiwa-mafuta?

      9 Pamoja na mabaki, mamilioni hawa wa kondoo wengine wanajifunza kuishi na kusema kwa kupatana na “lugha iliyo safi.”a Yehova alitoa unabii kupitia Sefania: “Ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja [“bega kwa bega,” NW].” (Sefania 3:9) Ndiyo, kondoo wengine wanamtumikia Yehova kwa muungano “bega kwa bega” wakiwa pamoja na washiriki waliowekwa rasmi wa “kundi dogo” katika kazi yenye uharaka ya kuhubiri “habari njema ya ufalme . . . kuwa ushuhuda kwa mataifa yote.”—Luka 12:32; Mathayo 24:14.

      “Siku ya Yehova Itakuja”

      10. Sikuzote mabaki watiwa-mafuta wamesadiki nini, na wataishi kuona nini wakiwa jamii?

      10 Sikuzote mabaki watiwa-mafuta wamedumisha akilini taarifa ya mtume Petro iliyopuliziwa: “Yehova si wa polepole kwa habari ya ahadi yake, kama watu fulani wafikiriavyo upolepole, bali yeye ni mwenye saburi kwenu kwa sababu hataki yeyote aangamizwe bali hutaka wote wafikie toba. Lakini siku ya Yehova itakuja kama mwizi.” (2 Petro 3:9, 10, NW) Washiriki wa jamii ya mtumwa mwaminifu hawajapata kamwe kuwa na shaka zozote kuhusu kuja kwa siku ya Yehova katika wakati wetu. Hiyo siku iliyo kuu itaanza kwa kutekelezwa kwa hukumu za Mungu dhidi ya Jumuiya ya Wakristo, iliyo kifanani cha Yerusalemu, na sehemu nyingine ya Babiloni Mkubwa.—Sefania 1:2-4; Ufunuo 17:1, 5; 19:1, 2.

      11, 12. (a) Ni sehemu ipi nyingine ya unabii wa Sefania ambayo imetimizwa juu ya mabaki? (b) Mabaki watiwa-mafuta wametiije mwito huu, “Mikono yako isilegee”?

      11 Mabaki waaminifu hushangilia kwa kukombolewa katika 1919 kutoka utekwa wa kiroho wa Babiloni Mkubwa, milki ya ulimwengu ya dini bandia. Wao wameona utimizo wa unabii wa Sefania: “Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. BWANA ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa.”—Sefania 3:14-17.

      12 Kwa usadikisho wenye nguvu na uthibitisho mwingi sana kwamba Yehova yuko katikati yao, mabaki watiwa-mafuta wamesonga mbele bila kuogopa ili kutimiza utume wao wa kimungu. Wao wamehubiri habari njema ya Ufalme nao wamejulisha hukumu za Yehova dhidi ya Jumuiya ya Wakristo, sehemu nyingine ya Babiloni Mkubwa, na mfumo wote mwovu wa Shetani. Japo magumu yote, kwa miongo mingi tangu 1919, wao wametii amri hii ya kimungu: “Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.” Wao wamekuwa na bidii katika kugawanya mabilioni ya trakti, magazeti, vitabu, na vijitabu vyenye kutangaza Ufalme wa Yehova. Hao wamekuwa vielelezo vyenye kuimarisha imani kwa kondoo wengine ambao wamewaunga mkono kwa wingi tangu 1935.

      “Mikono Yako Isilegee”

      13, 14. (a) Kwa nini Wayahudi fulani waliacha kumtumikia Yehova, na hilo lilionekanaje wazi? (b) Halingekuwa jambo la hekima kwetu kufanya nini, na tusilegee mikono katika kazi gani?

      13 Huku ‘tukifuliza kutarajia’ siku ya Yehova iliyo kuu, twaweza kupataje msaada wenye kutumika kutoka kwenye unabii wa Sefania? Kwanza, ni lazima tujihadhari tusiwe kama Wayahudi katika siku ya Sefania walioacha kumfuata Yehova kwa sababu walitilia shaka ukaribu wa siku ya Yehova. Si lazima kwamba Wayahudi hawa walitaja waziwazi shaka zao, lakini mwendo waliochukua ulifunua kwamba wao kwa kweli hawakuamini kwamba siku ya Yehova iliyo kuu ilikuwa karibu. Wao walikazia akili kurundika mali badala ya kufuliza kumtarajia Yehova.—Sefania 1:12, 13; 3:8.

      14 Leo si wakati wa kuacha shaka zikue mioyoni mwetu. Halingekuwa jambo la hekima kuahirisha akilini au moyoni kuja kwa siku ya Yehova. (2 Petro 3:1-4, 10) Twapaswa kuepuka kuacha kumtumikia Yehova au ‘kulegea mikono’ katika utumishi wake. Hilo latia ndani ‘kutofanya mambo kwa mkono mlegevu’ katika kuhubiri “habari njema.”—Mithali 10:4; Marko 13:10, NW.

      Kupambana na Kutojali

      15. Ni nini kiwezacho kutufanya tukose bidii katika utumishi wa Yehova, na tatizo hilo lilitabiriwaje katika unabii wa Sefania?

      15 Pili, twapaswa kulinda dhidi ya matokeo yenye kudhoofisha ya kutojali. Katika nchi nyingi za Magharibi, kutojali mambo ya kiroho kwaweza kusababisha kuvunjika moyo miongoni mwa wahubiri fulani wa habari njema. Hali kama hiyo ya kutojali ilikuwapo katika siku ya Sefania. Yehova alisema hivi kupitia nabii wake: “Nitawaadhibu watu . . . wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.” (Sefania 1:12) Akiandika kuhusu fungu hili katika Cambridge Bible for Schools and Colleges, A. B. Davidson alisema kwamba hilo fungu larejezea watu waliokuwa “wameshindwa na kutojali kabisa au hata kushindwa na hali ya kutoamini kwamba kuna uwezo wa juu zaidi utakaoingilia mambo ya wanadamu.”

      16. Ni hali gani ya akili iliyo miongoni mwa washiriki wengi wa makanisa ya Jumuiya ya Wakristo, lakini Yehova atupa kitia-moyo gani?

      16 Kutojali ndiko mtazamo wenye kuenea leo katika sehemu nyingi za dunia, hasa katika nchi zilizo tajiri zaidi. Hata washiriki wa makanisa ya Jumuiya ya Wakristo hawaamini kamwe kwamba Yehova Mungu ataingilia mambo ya kibinadamu katika siku yetu. Wao hupuuza jitihada zetu za kuwafikia kwa habari njema za Ufalme kwa tabasamu yenye kutilia shaka au kwa jibu fupi “Sipendezwi!” Chini ya hali hizo, udumifu katika kazi ya kutoa ushahidi waweza kuwa mgumu sana. Hilo hujaribu uvumilivu wetu. Lakini kupitia unabii wa Sefania, Yehova huwachochea watu wake waaminifu, akisema: “Mikono yako isilegee. BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atakutuliza katika upendo wake, atakufurahia kwa kuimba.”—Sefania 3:16, 17.

      17. Ni kielelezo kipi kizuri ambacho wapya miongoni mwa kondoo wengine wapaswa kufuata, na jinsi gani?

      17 Ni jambo la hakika katika historia ya kisasa ya watu wa Yehova kwamba mabaki, na vilevile wale walio wazee-wazee zaidi miongoni mwa kondoo wengine, wametimiza kazi kubwa sana ya ukusanyaji katika hizi siku za mwisho. Wakristo hawa wote waaminifu wameonyesha uvumilivu katika miongo ambayo imepita. Wao hawajaruhusu kutojali kwa upande wa wengi katika Jumuiya ya Wakristo kuwavunje moyo. Basi, na wale walio wapya miongoni mwa kondoo wengine na wasijiachilie wavunjwe moyo na hali ya kutojali mambo ya kiroho ambayo imeenea sana leo katika nchi nyingi. Na wasiache ‘mikono yao ilegee,’ au kukosa bidii. Na watumie kila fursa wapatayo kutoa Mnara wa Mlinzi, Amkeni!, na vichapo vingine vizuri vilivyokusudiwa kusaidia watu wenye mfano wa kondoo kujifunza kweli kuhusu siku ya Yehova na baraka zitakazofuata.

      Kusonga Mbele Tukingoja Siku Iliyo Kuu!

      18, 19. (a) Ni kitia-moyo gani cha kuvumilia tupatacho kwenye Mathayo 24:13 na Isaya 35:3, 4? (b) Tutabarikiwaje tukisonga mbele kwa muungano katika utumishi wa Yehova?

      18 Yesu alisema: “Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.” (Mathayo 24:13) Basi, tusiwe na “mikono iliyo dhaifu” au “magoti yaliyolegea” tungojapo siku ya Yehova iliyo kuu! (Isaya 35:3, 4) Unabii wa Sefania wasema hivi kwa kufariji kuhusu Yehova: “Shujaa awezaye kuokoa.” (Sefania 3:17) Ndiyo, Yehova ataokoa “umati mkubwa” kupita sehemu ya mwisho ya “dhiki ile iliyo kuu,” anapomwamuru Mwana wake kuvunja vipande-vipande mataifa ya kisiasa yanayoendelea “kujitukuza” juu ya watu wake.—Ufunuo 7:9, 14, NW; Sefania 2:10, 11; Zaburi 2:7-9.

      19 Siku ya Yehova iliyo kuu ikaribiapo, na tusonge mbele kwa bidii, tukimtumikia “bega kwa bega”! (Sefania 3:9, NW) Tukifanya hivyo, sisi wenyewe na wengine wengi wasiohesabika tutaweza ‘kufichwa katika siku ya hasira ya BWANA’ na kushuhudia utakaso wa jina lake takatifu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki