-
Watu Wanaotafuta UsalamaAmkeni!—2002 | Januari 22
-
-
Watu Wanaotafuta Usalama
“Umwagaji-damu na mnyanyaso unaowalazimisha watu kutoroka ili kuokoa uhai wao haukumalizika katika karne ya 20. Milenia mpya ilipoanza makumi ya mamilioni ya watu walikuwa katika kambi za wakimbizi na kwenye makao mengine ya muda, wakihofu kwamba watauawa wakijaribu kurudi makwao.”—Bill Frelick, Kamati ya Wakimbizi ya Marekani.
JACOB alitamani sana jambo fulani. Alitamani sana kuishi mahala penye amani, ambapo mbuzi wa familia yake hawangeuawa kwa mabomu, na mahala ambapo angeweza kwenda shuleni.
Watu wa mji wa kwao walimweleza kwamba mahala pa aina hiyo palikuwapo, ingawa palikuwa mbali sana. Babake alimwambia kwamba safari ya kwenda mahala hapo ilikuwa hatari sana, kwani watu fulani walikuwa wamekufa njaa na kwa kukosa maji njiani. Lakini wakati jirani yake, ambaye mume wake alikuwa ameuawa, alipoanza safari pamoja na watoto wake wawili, Jacob aliamua kusafiri peke yake.
Jacob hakubeba chakula wala nguo. Siku ya kwanza, alikimbia bila kusimama. Barabara ilikuwa imejaa maiti. Siku iliyofuata, alikutana na mwanamke mmoja wa mji wa kwao aliyemwambia kuwa angeweza kusafiri pamoja naye na rafikize. Walitembea kwa siku nyingi huku wakipita vijiji vilivyokuwa mahame. Siku moja walipita katikati ya eneo lililotegwa mabomu ya ardhini, na mtu mmoja katika kikundi chao akauawa. Walikula majani.
Siku kumi baadaye, watu wakaanza kufa kwa sababu ya uchovu na njaa. Punde baadaye, wakashambuliwa na ndege za vita. Hatimaye, Jacob alivuka mpaka na akafika kwenye kambi ya wakimbizi. Sasa yeye huenda shuleni, naye hatishwi tena na sauti ya ndege. Ndege zote anazoona siku hizi ni zile zinazobeba vyakula badala ya mabomu. Lakini anakosa sana familia yake, na angependa kurudi nyumbani.
Kuna watu wengi ulimwenguni wanaokumbwa na hali kama ya Jacob. Wengi wao wamefadhaishwa na vita na wanateseka kwa sababu ya njaa na kiu. Wengi wao hawajaishi kamwe na familia zao, na wengi hawatarudi kamwe nyumbani kwao. Wao ni maskini hohehahe.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi huwaainisha hao maskini wanaohamahama katika vikundi viwili. Mkimbizi ni mtu anayetoroka nchi yake kwa sababu ya kuhofu mnyanyaso au ujeuri. Kikundi cha pili ni cha watu waliolazimishwa kuhama makwao hadi eneo jingine la nchi yao kwa sababu ya vita au hatari nyingine kubwa.a
Hakuna ajuaye idadi kamili ya wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao ambao wanaishi kwa shida katika kambi za muda au wanahamahama wakitafuta usalama. Kwa mujibu wa vyanzo fulani vya habari, huenda kuna wakimbizi milioni 40 hivi ulimwenguni pote na nusu ya idadi hiyo ni watoto. Wakimbizi wote hao hutoka wapi?
Tatizo la Siku Zetu
Tatizo la wakimbizi liliongezeka mwishoni mwa vita ya kwanza ya ulimwengu. Vita ilipokwisha, milki zilivunjika na makabila madogo-madogo yalikandamizwa. Kwa sababu hiyo, mamilioni ya Wazungu walikimbilia nchi nyingine. Vita ya pili ya ulimwengu—ambayo ilikuwa mbaya zaidi ya ile ya kwanza—iliwalazimu tena mamilioni ya watu kuondoka makwao. Tangu mwaka wa 1945, vita vimepiganwa katika nchi chache lakini bado vimewafadhaisha watu wanaoishi katika nchi hizo.
“Ingawa sikuzote vita vimetokeza wakimbizi, ni katika karne ya ishirini tu ambapo vita kati ya mataifa mbalimbali vimeathiri watu wote katika mataifa hayo,” ndivyo anavyoeleza Gil Loescher katika kitabu chake cha mwaka wa 1993 cha Beyond Charity—International Cooperation and the Global Refugee Crisis. ‘Kwa kuwa wapiganaji na vilevile watu wasiopigana waliuawa wakati wa vita, watu wengi wakawa wakimbizi ili kuepuka jeuri hiyo iliyoelekezwa kwa watu wote.’
Isitoshe, vita vingi vya leo ni vya wenyewe kwa wenyewe na vinawaathiri sana wanaume waliofikisha umri wa kwenda vitani na vilevile wanawake na watoto. Baadhi ya vita hivyo huendelea kwa muda mrefu kwa sababu vinachochewa na migawanyiko mikubwa ya kikabila na ya kidini. Katika nchi moja ya Afrika, ambako vita ya wenyewe kwa wenyewe imeendelea kwa miaka 18, kuna watu milioni nne waliolazimishwa kuhama makwao, huku mamia ya maelfu ya watu wengine wamekimbilia nchi nyingine.
Sikuzote, inawabidi watu wanaoishi katika maeneo yenye vita wahame makwao ili kuepuka jeuri. Kitabu The State of the World’s Refugees 1997-98 chasema hivi: “Wakimbizi huhama makwao na kuingia katika nchi nyingine kwa sababu inawalazimu kufanya hivyo, wala si kwa sababu ya starehe au kwa kupenda.” Hata hivyo, siku hizi si rahisi kupata kibali cha kuingia katika nchi nyingine.
Katika miaka ya 1990, idadi ya wakimbizi ulimwenguni ilipungua kutoka milioni 17 hivi hadi milioni 14. Hayo yanaonekana kuwa maendeleo, lakini sivyo ilivyo. Katika mwongo huohuo, inakadiriwa kwamba idadi ya watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao ilifikia milioni 25 hadi milioni 30. Mbona kukawa na ongezeko hilo?
Imekuwa vigumu zaidi kupata hati rasmi za kuwa mkimbizi kwa sababu mbalimbali. Huenda nchi zikakataa kukubali wakimbizi, ama kwa sababu haziwezi kushughulikia wakimbizi wengi au kwa sababu zinahofu kwamba idadi kubwa ya wakimbizi inaweza kusababisha hali mbaya ya kiuchumi na ya kisiasa. Hata hivyo, nyakati nyingine wakimbizi wenye hofu hukosa nguvu, chakula, au fedha za kuwategemeza wanapotembea hadi mpakani. Wao hukosa la kufanya ila tu kuhamia eneo lenye usalama katika nchi yao.
Ongezeko la Wakimbizi wa Kiuchumi
Kuongezea mamilioni ya wakimbizi wa kawaida, kuna mamilioni ya watu wengine maskini ambao hutaka kuboresha hali yao ya maisha wakitumia njia moja tu wanayojua—kuhamia nchi nyingine ambako hali za maisha ni afadhali.
Mnamo Februari 17, 2001, meli moja kuukuu ilikwama kwenye pwani ya Ufaransa. Wanaume, wanawake na watoto elfu moja hivi walikuwa wamesafiri kwa meli hiyo kwa muda wa juma moja hivi bila kula chochote. Kila abiria alikuwa amelipa dola 2,000 za Marekani kwa ajili ya safari hiyo hatari, bila hata kujua nchi aliyokuwa akielekea. Nahodha na mabaharia wa meli hiyo walitoweka mara tu walipopandisha meli hiyo ufukoni. Lakini abiria hao wenye hofu waliokolewa, na serikali ya Ufaransa ikaahidi kushughulikia maombi yao ya kuishi nchini humo. Watu wengi kama hao hujaribu kufunga safari kama hizo kila mwaka.
Wengi kati ya wahamiaji hao wa kiuchumi huwa tayari kukabili magumu na hatari kubwa. Wao hujaribu juu chini kupata nauli ya safari hiyo kwa sababu umaskini, ujeuri, ubaguzi, au serikali katili—na nyakati nyingine mambo yote hayo manne—hufanya wakose tumaini maishani.
Wengi wao hufa wanapojaribu kutafuta maisha bora. Katika mwongo uliopita, wahamiaji 3,500 hivi walizama au kutoweka wakati walipojaribu kuvuka Mlango-Bahari wa Gibraltar walipokuwa wakisafiri kutoka Afrika hadi Hispania. Katika mwaka wa 2000, wahamiaji 58 Wachina walikufa kwa kukosa hewa walipokuwa wamefichwa ndani ya lori lililokuwa likiwasafirisha kutoka Ubelgiji hadi Uingereza. Wahamiaji wengi sana hufa kwa kukosa maji kwenye jangwa la Sahara wakati malori yao makuukuu, yanayobeba watu wengi mno, yanapoharibika jangwani.
Licha ya hatari hizo, kuna ongezeko kubwa la wakimbizi wa kiuchumi ulimwenguni. Kila mwaka, watu wapatao nusu milioni huingizwa Ulaya kiharamu; na watu 300,000 huingizwa Marekani vivyo hivyo. Mnamo mwaka wa 1993, Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa ilikadiria kwamba kulikuwa na wahamiaji milioni 100 ulimwenguni, na theluthi moja kati yao walihamia Ulaya na Marekani. Tangu wakati huo, idadi ya wahamiaji imeongezeka sana.
Wahamiaji wengi hawapati kamwe usalama wanaotafuta. Na ni wakimbizi wachache tu wanaopata makao salama na ya kudumu. Mara nyingi, wahamiaji hao hukimbia matatizo fulani na kuingia katika matatizo mengine. Makala inayofuata itazungumzia baadhi ya matatizo hayo na mambo yanayoyasababisha.
[Maelezo ya Chini]
a Katika mfululizo huu, tunapozungumzia watu waliolazimishwa kuhama makwao, hatuzungumzii wale watu milioni 90 hadi milioni 100 ambao wamelazimishwa kuhama makwao kwa sababu ya miradi ya maendeleo kama ujenzi wa mabwawa, kuchimba migodi, kupanda miti, au miradi ya kilimo.
-
-
Kupata Makao ya KudumuAmkeni!—2002 | Januari 22
-
-
Kupata Makao ya Kudumu
“Hata ikiwa ni kwa hali ya chini sana, kwetu ndiko kuzuri.”—John Howard Payne.
KWANZA vita ilizuka, vita iliyodumu muda mrefu. Kisha ukame ukatokea, ukame uliodumu muda mrefu. Baada ya ukame, kukaja njaa. Na watu wakalazimika kuhama makwao ili kutafuta maji, chakula, na kazi.
Maelfu ya watu walifika mpakani. Lakini kwa kuwa katika miaka ya karibuni wakimbizi milioni moja walikuwa tayari wameingia katika nchi hiyo jirani, haikukubali wakimbizi wengine. Mapolisi wa mpakani wenye marungu, waliwazuia watu wasivuke mpaka.
Afisa mmoja wa uhamiaji katika eneo hilo alitaja wazi sababu za kuwazuia wakimbizi hao wasiingie nchini humo. Alisema hivi: “Hawalipi kodi. Wao huharibu barabara. Wao hukata miti. Wao humaliza maji. La, hatutaki wakimbizi wengine.”a
Matukio hayo ya kuhuzunisha yameongezeka sana. Watu waliolazimishwa kuhama hukabili ugumu wa kupata makao ya kudumu. Ripoti moja ya hivi majuzi ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ilisema hivi: ‘Idadi ya wakimbizi inapoongezeka, nchi mbalimbali zinakataa hata zaidi kuwasaidia.’
Huenda wale wanaofanikiwa kufika kwenye kambi ya wakimbizi wakapata usalama wa kadiri, lakini hawajihisi kwamba wako nyumbani. Na hali katika kambi zaweza kuwa ngumu sana.
Hali Katika Kambi za Wakimbizi
Mkimbizi mmoja huko Afrika alilalamika hivi: “Unaweza kufa kwa kupigwa risasi [huko nyumbani], lakini hapa [katika kambi ya wakimbizi] watoto wako watakufa njaa.” Kama vile baba huyo alivyong’amua, kambi nyingi huwa chafu nazo hukumbwa na uhaba wa chakula, maji na makao. Sababu za hali hiyo ni wazi. Huenda serikali za nchi zinazoendelea, ambazo hukumbwa na maelfu ya wakimbizi kwa ghafula, tayari zinashindwa kulisha raia zake. Serikali hizo haziwezi kuwasaidia sana wakimbizi wote wanaotaka kuingia katika nchi zao. Na kwa kuwa mataifa tajiri yana matatizo yao yenyewe, yanaweza kusita kuwasaidia wakimbizi walio katika nchi nyingine.
Wakati watu zaidi ya milioni mbili walipokimbia nchi moja ya Afrika mwaka wa 1994, kambi za wakimbizi zilizojengwa haraka zilikuwa chafu na hazikuwa na maji. Jambo hilo lilitokeza ugonjwa wa kipindupindu ambao uliua maelfu ya watu kabla haujadhibitiwa. Isitoshe, wapiganaji wenye silaha walichangamana na wakimbizi wengine na punde baadaye wakaanza kusimamia ugawanyaji wa misaada. Tatizo hilo halikutokea tu wakati huo. Ripoti moja ya shirika la Umoja wa Mataifa yasema hivi: ‘Kuwepo kwa vikundi vyenye silaha katika kambi kumewahatarisha sana wakimbizi wengine. Wametishwa, wamenyanyaswa, na kulazimishwa wajiunge na jeshi.’
Huenda wenyeji pia wakaumia kwa sababu ya ongezeko kubwa la wakimbizi wenye njaa. Katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika, maafisa fulani walilalamika hivi: “[Wakimbizi] wameharibu maghala yetu, mashamba yetu, mifugo yetu, mbuga zetu, wamesababisha njaa na kueneza magonjwa . . . [Wao] hupata misaada ya chakula lakini sisi hatupati chochote.”
Hata hivyo, huenda tatizo kubwa zaidi likawa kwamba kambi nyingi za wakimbizi za muda hugeuzwa kuwa makao ya kudumu. Kwa mfano, katika nchi moja ya Mashariki ya Kati, wakimbizi 200,000 hivi wamesongamana katika kambi iliyojengwa kwa ajili ya wakimbizi 50,000 hivi. Mmoja wao alisema hivi kwa huzuni: “Hatuna mahala pengine pa kwenda.” Wakimbizi hao ambao wameteseka kwa muda mrefu, wamewekewa vikwazo vikali vya kuajiriwa kazi katika nchi hiyo, na asilimia 95 kati yao hawana kazi au wameajiriwa kazi yenye mshahara mdogo. Afisa mmoja wa wakimbizi alisema hivi: ‘Sijui jinsi wanavyojiruzuku.’
Lakini ikiwa hali ni mbaya katika kambi za wakimbizi, huenda zikawa mbaya hata zaidi kwa watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao.
Majonzi ya Kulazimishwa Kuhama
Kwa mujibu wa mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi, ‘kiwango cha tatizo hilo la kulazimishwa kuhamia eneo jingine, kuteseka kwa wanadamu ambako husababisha tatizo hilo, na pia athari yake juu ya amani na usalama ulimwenguni, imesababisha hangaiko kubwa ulimwenguni pote.’ Watu hao wasio na makao hukabili hatari kubwa kuliko wakimbizi kwa sababu kadhaa.
Hakuna shirika la kimataifa ambalo hushughulikia mahitaji ya watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao, na matatizo yao hayatajwi mara nyingi kwenye vyombo vya habari. Serikali zao, zinazohusika katika vita ya aina fulani, hushindwa au hukataa kuwasaidia. Mara nyingi familia hugawanyika wakati zinapokimbia maeneo hatari. Kwa kuwa mara nyingi wao hutembea, watu fulani wanaolazimishwa kuhama hufa safarini wanapokimbilia mahala salama.
Wengi kati ya watu hao waliolazimishwa kuhama hukimbilia majiji, nao huishi katika hali ngumu kwenye vibanda au majengo yaliyoachwa ukiwa. Wengine huenda kwenye kambi za muda, ambazo hushambuliwa nyakati nyingine. Kwa kawaida, wao hukabili hatari kubwa ya kufa kuliko watu wengine katika nchi hiyo.
Hata jitihada zinazofanywa kwa nia nzuri ili kuwasaidia watu hao waliolazimishwa kuhama zaweza kuwadhuru. Kitabu The State of the World’s Refugees 2000 chasema hivi: ‘Katika mwongo wa mwisho wa karne ya 20, mashirika ya ufadhili yanayohudumia watu katika nchi zilizokumbwa na vita yaliokoa maelfu ya watu na kupunguza sana kuteseka. Hata hivyo, somo moja muhimu ambalo watu walijifunza katika mwongo huo ni kwamba wakati wa vita, vikundi vinavyopigana vinaweza kwa urahisi kutumia misaada vibaya, na kuimarisha watu wenye mamlaka wanaokandamiza haki za binadamu. Pia, misaada inayotolewa na mashirika ya ufadhili inaweza kutumiwa kuinua uchumi wa makundi yanayopigana, na hivyo kuendeleza vita.’
Kutafuta Maisha Bora
Mbali na wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao, kuna ongezeko la wakimbizi wa kiuchumi. Kuna visababishi kadhaa vya tatizo hilo. Tofauti iliyopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini za ulimwengu inazidi, na kila siku watu fulani walio maskini hohehahe hutazama vipindi vya televisheni vinavyoonyesha maisha ya hali ya juu ya watu wanaoishi katika nchi fulani. Imekuwa rahisi kusafiri duniani na kuvuka mipaka. Pia, vita vya wenyewe kwa wenyewe na ubaguzi wa kikabila na wa kidini umewachochea sana watu kuhamia nchi zenye ufanisi.
Na ijapo wahamiaji fulani—hasa wale walio na watu wa jamaa katika nchi zilizoendelea kiviwanda—hufanikiwa kuhama, wengine huharibu maisha yao. Wale wanaodanganywa na wahalifu huwa hatarini. (Ona masanduku.) Familia yapaswa kufikiria kwa makini hatari hizo kabla ya kuhama kwa sababu za kiuchumi.
Mnamo mwaka wa 1996, meli moja kuukuu ilizama katika Bahari ya Mediterania, na watu 280 wakafa. Watu hao waliokufa walikuwa wakihama kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka nao walikuwa wamelipa kati ya dola 6,000 na dola 8,000 za Marekani ili wapelekwe Ulaya. Kabla ya tukio hilo, walikuwa tayari wameteseka kwa majuma kadhaa kutokana na njaa, kiu, na kuteswa kimwili. Safari yao ya kuboresha maisha iligeuka kuwa msiba.
Kila mkimbizi, mtu aliyelazimishwa kuhama, au mhamiaji haramu amewahi kupatwa na matatizo hayo. Iwe watu hao wamehamia mahala pengine kwa sababu ya vita, mnyanyaso, au umaskini, kuteseka kwao hutokeza maswali haya: Je, tatizo hilo litasuluhishwa? Au, je, wakimbizi watazidi kuongezeka daima?
[Maelezo ya Chini]
a Hali iliyotajwa hapo juu ilitokea mnamo Machi 2001 katika nchi moja ya Asia. Lakini matatizo kama hayo yametokea pia katika nchi kadhaa za Afrika.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Matatizo ya Wahamiaji Haramu
Mbali na wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao, idadi ya “wahamiaji haramu” ulimwenguni ni kati ya milioni 15 na milioni 30. Wengi kati ya watu hao ni wale wanaotaka kuhepa umaskini—na labda dhuluma na mnyanyaso pia—kwa kuhamia nchi tajiri.
Kwa kuwa imekuwa vigumu kupata hati halali za uhamiaji katika miaka ya karibuni, biashara haramu ya kuhamisha wahamiaji imeanzishwa. Kwa hakika, mashirika mengi ya wahalifu ya kimataifa yanachuma pesa nyingi kupitia biashara hiyo ya kuhamisha wahamiaji. Wapelelezi fulani wanakadiria kwamba biashara hiyo huleta faida ya dola bilioni 12 za Marekani kila mwaka bila kuwahatarisha sana wahalifu hao. Pino Arlacchi, msaidizi mmoja wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba “hiyo ndiyo biashara haramu inayositawi haraka sana ulimwenguni.”
Wahamiaji haramu hawalindwi na sheria, na wahalifu hao huwanyang’anya pasipoti zao. Wahamiaji hao huajiriwa kazi kwenye karakana ambako wanafanya kazi katika hali mbaya na kulipwa mshahara mdogo, huajiriwa kazi za nyumbani, kazi ya kilimo, au katika biashara ya uvuvi. Wengine huwa makahaba. Wanapokamatwa na wenye mamlaka, wanaweza kufukuzwa nchi hiyo, bila hata ndururu. Wanapolalamika kuhusu hali ngumu za kikazi, huenda wakapigwa, wakabakwa au hata familia zao walizoacha nchini kwao zikatishwa.
Mara nyingi magenge ya wahalifu wanaowahamisha watu kiharamu huwavutia watu kwa kuwaahidi kazi zenye mishahara minono. Hivyo, huenda familia maskini ikawakabidhi wahalifu hao mali zake zote ili kumpeleka mshiriki mmoja wa familia yao Ulaya au Marekani. Iwapo mhamiaji hawezi kugharimia nauli yake, itampasa kufanya kazi ili kulipa deni hilo. Deni hilo laweza kuwa dola 40,000 za Marekani. Badala ya kupata maisha mazuri kama alivyoahidiwa, mhamiaji anakuwa mtumwa.
[Picha]
Wakimbizi haramu huko Hispania
[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 9]
Watoto Wazuri Huharibiwa
Familia ya Siri iliishi katika vilima vilivyoko Kusini-Mashariki mwa Asia, ambako wazazi wake walikuza mpunga. Siku moja mwanamke mmoja aliwaambia wazazi wa Siri kwamba angemtafutia kazi yenye mshahara mzuri jijini. Aliahidi kuwapa dola 2,000 za Marekani nao wakakubali kwani hizo zilikuwa pesa nyingi sana kwa wakulima hao. Hata hivyo, punde si punde Siri akaajiriwa kazi kwenye nyumba ya makahaba. Waajiri wake walimwambia kwamba alihitaji kulipa dola 8,000 za Marekani ili awekwe huru. Wakati huo Siri alikuwa na umri wa miaka 15.
Siri hangeweza kulipa deni hilo. Alipigwa na kubakwa ili akubali kufanya kazi hiyo. Maadamu angewaletea faida, hangeachiliwa huru. Jambo la kusikitisha ni kwamba hatimaye makahaba wengi huachiliwa wanapopata UKIMWI ili warudi wakafe kwenye vijiji vyao.
Biashara kama hiyo inasitawi katika nchi nyingine. Ripoti moja ya 1999 yenye kichwa International Trafficking in Women to the United States ilikadiria kwamba wanawake na watoto kati ya 700,000 na 2,000,000 huhamishwa kiharamu kila mwaka, hasa ili wawe makahaba. Baadhi yao huenda wakadanganywa, wengine hutekwa nyara; lakini karibu wote hulazimishwa kufanya kazi hiyo. Kijana mmoja wa Ulaya Mashariki aliyeokolewa kutoka kwenye genge la makahaba alisema hivi kuhusu watu hao waliomteka: “Sikufikiria jambo hilo linaweza kutukia. Watu hao ni wanyama.”
Baadhi ya watu hao wanaodhulumiwa wamechukuliwa kwenye kambi za wakimbizi na kuahidiwa kuwa wataajiriwa kazi zenye mishahara minono huko Ulaya au Marekani. Wanawake wengi waliotaka kuboresha maisha yao wamelazimishwa kuwa makahaba.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
Chunguza Mambo kwa Makini Kabla ya Kuhama kwa Sababu za Kiuchumi
Kwa sababu kuna magenge mengi ya wahalifu wanaohamisha wahamiaji kiharamu na kwa sababu ya ugumu wa kupata hati halali za kuhamia nchi zilizoendelea, waume na akina baba wapaswa kufikiria kwa makini maswali yafuatayo kabla ya kufanya uamuzi.
1. Je, hali yetu ya kiuchumi ni mbaya sana hivi kwamba ni lazima mshiriki mmoja wa familia au familia yote kuhamia nchi ambako mishahara ni minono?
2. Tutahitaji kukopa pesa ngapi ili kulipia safari hiyo, na deni hilo litalipwaje?
3. Je, kuna faida kutenganisha familia ili kutafuta faida za kiuchumi ambazo huenda tukakosa kupata? Wahamiaji wengi haramu hushindwa kupata kazi ya kudumu katika nchi zilizoendelea.
4. Je, niamini habari ninazosikia kuhusu mishahara minono na misaada inayotolewa na serikali katika nchi hiyo? Biblia husema kwamba “mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.”—Mithali 14:15.
5. Nina uhakika gani kwamba hatutajihusisha na shirika la wahalifu?
6. Ikiwa shirika la wahalifu litapanga safari hiyo, je, ninafahamu kwamba huenda mke wangu—au binti yangu—akalazimishwa kuwa kahaba?
7. Je, ninang’amua kwamba nikihamia nchi nyingine kiharamu, ninaweza kukosa kuajiriwa kazi ya kudumu na huenda nikafukuzwa, na kupoteza pesa zote nilizotumia kulipia safari hiyo?
8. Je, ninataka kuwa mhamiaji haramu au kutumia njia zisizo halali ili kuingia katika nchi yenye ufanisi?—Mathayo 22:21; Waebrania 13:18.
[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 8, 9]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Jinsi Wakimbizi na Wafanyakazi Wahamiaji Wanavyohama
Maeneo yenye idadi kubwa ya wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao
Jinsi wafanyakazi wahamiaji wanavyohama hasa
[Hisani]
Vyanzo: The State of the World’s Refugees; The Global Migration Crisis; na World Refugee Survey 1999.
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mkimbizi asubiri kupelekwa kwenye makao mapya
[Hisani]
UN PHOTO 186226/M. Grafman
-
-
Ulimwengu Ambao Kila Mtu AtafurahiaAmkeni!—2002 | Januari 22
-
-
Ulimwengu Ambao Kila Mtu Atafurahia
“Kwa kuwa tatizo la wakimbizi linakumba ulimwengu wote, ni lazima masuluhisho yatafutwe ulimwenguni pote.”—Gil Loescher, profesa wa mahusiano ya kimataifa.
WENZI wawili wachanga walianza safari usiku. Kwa kuwa alihangaikia usalama wao, mume huyo hakupoteza wakati, hata ingawa walikuwa na mtoto mchanga. Alikuwa amesikia kwamba mtawala mkatili wa nchi hiyo alipanga njama kutekeleza mauaji katika mji huo. Baada ya safari ngumu ya zaidi ya kilometa 160 hivi, hatimaye familia hiyo ilivuka mpaka na kupata usalama.
Baadaye, familia hiyo maskini ikawa maarufu ulimwenguni pote. Mtoto huyo aliitwa Yesu, na wazazi wake waliitwa Maria na Yosefu. Wakimbizi hao hawakuhama ili kutafuta mali. Badala yake, maisha yao yalikuwa hatarini. Kwani, mtoto wao ndiye aliyekuwa shabaha ya shambulizi hilo!
Sawa na wakimbizi wengine, Yosefu na familia yake hatimaye walirudi nyumbani kwao hali ya kisiasa ilipotulia. Lakini, pasipo shaka uhai wa mtoto wao mchanga uliokolewa kwa sababu walikimbia bila kukawia. (Mathayo 2:13-16) Misri, nchi waliyokimbilia, ilijulikana kwa kukubali wakimbizi wa kisiasa na wa kiuchumi. Karne nyingi kabla ya hapo, babu za Yesu walikuwa wamekimbilia Misri wakati nchi ya Kanaani ilipokumbwa na njaa.—Mwanzo 45:9-11.
Wako Salama Lakini Hawajatosheka
Mifano ya Biblia na ya siku hizi huonyesha wazi kwamba kukimbilia nchi nyingine kwaweza kuokoa uhai. Hata hivyo, familia hufadhaika sana wakati inapolazimika kuacha makao yake. Ijapo makao yao yaweza kuwa madogo, huenda walitumia pesa na miaka mingi ili kuyatengeneza. Na huenda ikawa walirithi makao hayo ambayo yanawahusianisha na utamaduni wao na nchi yao. Isitoshe, wakimbizi wanaweza kukimbia na mali chache tu au hata bila chochote. Hivyo, mara nyingi wakimbizi hutumbukia katika umaskini, haidhuru jinsi hali yao ya kiuchumi ilivyokuwa hapo awali.
Wakimbizi wanaweza kusahau haraka kwamba wamepata usalama iwapo hawana tumaini jingine ila tu kuishi katika kambi ya wakimbizi daima. Na hali yao huwa yenye kufadhaisha zaidi inapoendelea kwa muda mrefu na hasa wasipochangamana na wenyeji wa eneo walilokimbilia. Sawa na watu wengine, wakimbizi hutaka kuwa na makao ya kudumu. Kambi ya wakimbizi si mahala pazuri pa kuwalea watoto. Je, kuna wakati ambapo kila mtu atakuwa na makao ya kudumu?
Je, Warudishwe Makwao?
Katika miaka ya 1990, watu milioni tisa hivi waliokuwa wamelazimishwa kuhama makwao walirudi nyumbani hatimaye. Baadhi ya watu hao walifurahia jambo hilo, na walianza mara moja maisha mapya. Lakini wengine walikuwa wamekata tamaa. Walirudi tu kwa sababu hali ilikuwa mbaya katika nchi waliyokuwa wamekimbilia. Matatizo waliyokabili katika nchi hiyo yalikuwa makubwa sana hivi kwamba waliona ilikuwa afadhali kurudi nyumbani, japo hawangekuwa salama.
Hata katika hali nzuri kabisa, watu wanaorudishwa makwao hukabili magumu kwa sababu inawabidi kuhama kwa mara ya pili. Kitabu The State of the World’s Refugees 1997-98 chasema hivi: ‘Kila mara wakimbizi wanapohamishwa, wanapoteza mashamba, kazi, nyumba, na mifugo. Na wanakabili ugumu wa kuanza maisha mapya.’ Uchunguzi mmoja uliofanywa kuhusu wakimbizi waliorudishwa makwao huko Afrika ya kati uliripoti kwamba ‘huenda wakimbizi waliosaidiwa walipokuwa uhamishoni wakakabili magumu mengi zaidi makwao kuliko yale waliyokuwa nayo uhamishoni.’
Hata hivyo, hali ya mamilioni ya wakimbizi wanaolazimishwa kurudi nchini kwao inasikitisha hata zaidi. Wao hupata nini wanaporudi? Ripoti moja ya shirika la Umoja wa Mataifa ilisema hivi: “Huenda ikawabidi wakimbizi hao wanaorudishwa makwao kuishi mahala ambapo hakuna sheria, mahala penye wavamizi na uhalifu wa kijeuri, mahala ambapo maaskari walioondolewa jeshini wanawashambulia raia na mahala ambapo watu wengi wanaweza kupata silaha ndogondogo.” Kwa wazi, watu waliorudishwa makwao hawawezi kuwa salama hata kidogo katika mazingira hayo magumu.
Ulimwengu Ambamo Watu Wote Watakuwa Salama
Pasipo kushughulikia visababishi vyenyewe, matatizo ya wakimbizi hayawezi kamwe kusuluhishwa kwa kuwalazimisha kurudi nyumbani. Bi. Sadako Ogata, aliyekuwa mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi, alisema hivi mnamo mwaka wa 1999: “Matukio ya mwongo huu—na hasa yale ya mwaka uliopita—yanaonyesha wazi kwamba haiwezekani kuzungumzia masuala ya wakimbizi bila kuongea juu ya usalama.”
Na mamilioni ya watu ulimwenguni pote hawaishi kwa usalama. Kofi Annan, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Katika sehemu fulani za ulimwengu, mataifa yameanguka kwa sababu ya vita vya kikabila na vya wenyewe kwa wenyewe na hivyo yameshindwa kuwalinda raia wake. Kwingineko, serikali zimehatarisha usalama wa watu kwa kukataa kutimiza masilahi ya watu wote, kwa kuwanyanyasa wapinzani wake na kuwaadhibu watu wasio na hatia wa makabila madogo.”
Kwa kawaida, vita, mnyanyaso, na ujeuri wa kikabila—visababishi vya ukosefu wa usalama ambavyo Kofi Annan alitaja—husababishwa na chuki, ubaguzi, na dhuluma. Maovu hayo hayatamalizwa kwa urahisi. Je, hilo lamaanisha kwamba tatizo la wakimbizi litazidi?
Tatizo hilo lingezidi ikiwa wanadamu wangeruhusiwa waendelee kushughulikia mambo. Lakini katika Biblia, Mungu anaahidi ‘kuvikomesha vita hata mwisho wa dunia.’ (Zaburi 46:9) Pia, kupitia nabii wake Isaya, yeye asema kuhusu wakati ambao watu “watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. . . . Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao.” (Isaya 65:21-23) Bila shaka, hali hizo zitakomesha kabisa tatizo la wakimbizi. Je, inawezekana hali hizo ziwepo?
Utangulizi wa hati ya Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa wasema hivi: ‘Kwa kuwa vita huanza katika akili za watu, vivyo hivyo amani yapaswa kuanza katika akili za watu.’ Muumba wetu anajua kwamba watu wanapaswa kubadili mawazo yao. Nabii huyohuyo anaeleza ni kwa nini siku moja watu wote duniani wataishi wakiwa salama: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.
Tayari Mashahidi wa Yehova wanajua kwamba ujuzi juu ya Yehova unaweza kushinda ubaguzi na chuki. Kupitia kazi yao ya ulimwenguni pote ya kuhubiri, wao hufundisha kanuni za Maandiko ambazo zinawatia watu moyo kupendana badala ya kuchukiana, hata katika nchi zenye vita. Pia, wao huwasaidia wakimbizi kadiri wawezavyo.
Kwa upande mwingine, wanafahamu kwamba suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi litaletwa na Mfalme aliyewekwa na Mungu, Yesu Kristo. Yeye anajua jinsi chuki na ujeuri zinavyoweza kuharibu maisha ya watu kwa urahisi. Biblia hutuhakikishia kwamba atahukumu maskini kwa uadilifu. (Isaya 11:1-5) Chini ya utawala wake wa mbinguni, mapenzi ya Mungu yatafanywa duniani, kama huko mbinguni. (Mathayo 6:9, 10) Wakati huo utakapofika, hakuna mtu atakayelazimika kuwa mkimbizi tena. Na kila mtu atakuwa na makao yake mwenyewe ya kudumu.
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Ni Nini Kinachohitajiwa Ili Kusuluhisha Tatizo la Wakimbizi?
“Kutosheleza mahitaji ya wakimbizi wote na ya watu wote waliolazimishwa kuhamia maeneo mengine ya nchi yao, kunahusisha mengi zaidi ya kuandaa usalama na msaada wa muda. Kunahusisha kuondoa mnyanyaso, ujeuri, na mapambano yanayowalazimisha watu kuhama. Kunahusisha kufahamu kwamba wanaume, wanawake, na watoto wote wana haki ya kuwa na amani, usalama, na adhama bila kulazimika kukimbia makwao.”—The State of the World’s Refugees 2000.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]
Ufalme wa Mungu Utaleta Suluhisho Gani?
“Haki itadumu katika nchi iliyokuwa nyika, uadilifu utatawala katika mashamba yenye rutuba. Kutokana na uadilifu watu watapata amani, utulivu na usalama utadumu milele. Watu wangu watakaa katika makao ya amani, katika maskani salama na mazingira matulivu.”—Isaya 32:16-18, Biblia Habari Njema.
-