-
Ndoa Isiyotazamiwa Kati ya Boazi na RuthuMnara wa Mlinzi—2003 | Aprili 15
-
-
Ndoa Isiyotazamiwa Kati ya Boazi na Ruthu
KUNA shughuli nyingi katika mahali pa kupuria karibu na Bethlehemu. Imekuwa siku yenye shughuli nyingi. Wafanyakazi wenye njaa wanatambua kwamba wakati wa kula umefika wanaposikia harufu ya nafaka iliyochomwa. Kila mtu atafurahia kazi ya mikono yake.
Boazi, tajiri mwenye shamba, anakula, anakunywa, na kustarehe karibu na nafaka. Baadaye, kila mtu anatafuta mahali pa kupumzika siku ya kuvuna inapokwisha. Boazi ameshiba, na sasa anajifunika na kulala.
Wakutana Kisiri
Usiku wa manane, Boazi anaamuka akitetemeka kwa sababu anahisi baridi. Anashangaa kuona kwamba miguu yake imefunuliwa na kuna mtu aliyelala miguuni pake! Anauliza hivi kwa sababu hawezi kumtambua mtu huyo gizani: “Ni nani wewe?” Mwanamke anajibu: “Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu.”—Ruthu 3:1-9.
Wanazungumza wakiwa peke yao gizani. Si jambo la kawaida kwa wanawake kuwa katika mahali pa kupuria. (Ruthu 3:14) Hata hivyo, Boazi anamwambia Ruthu aendelee kulala miguuni pake kisha aamke na kuondoka kabla ya mapambazuko ili kuepuka kulaumiwa bila sababu.
Je, huo ulikuwa mkutano wa kimahaba? Je, Ruthu aliyekuwa mjane maskini kutoka nchi ya wapagani alimtongoza kwa ujanja mzee huyo tajiri? Au je, Boazi alimtongoza Ruthu usiku huo kwa sababu ya hali yake na upweke wake? La. Tukio hilo linaonyesha uaminifu na upendo kwa Mungu. Na mambo mengine yanayohusu tukio hilo yanagusa moyo vilevile.
-
-
Ndoa Isiyotazamiwa Kati ya Boazi na RuthuMnara wa Mlinzi—2003 | Aprili 15
-
-
Kufikia jioni, Ruthu amekusanya karibu lita 22 za shayiri. Anampelekea Naomi shayiri hiyo pamoja na chakula kilichobakia. (Ruthu 2:15-18) Naomi anafurahi kuona chakula hicho kingi na kuuliza: “Umeokota wapi leo? . . . Na abarikiwe yeye aliyekufahamu.” Anapojua kwamba ni Boazi, Naomi anasema: “Na abarikiwe huyo na BWANA, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa. . . . Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu.”—Ruthu 2:19, 20.
Kupata “Raha”
Kwa kuwa Naomi anatamani kumtafutia binti-mkwe wake “raha,” au makao, anatumia nafasi hiyo kufanya mpango wa kuomba ukombozi, kupatana na Sheria ya Mungu. (Mambo ya Walawi 25:25; Kumbukumbu la Torati 25:5, 6) Sasa Naomi ampa Ruthu maagizo mazuri ya jinsi ambavyo angefanya ili kuvuta fikira za Boazi. Baada ya kupokea maagizo mazuri Ruthu yuko tayari na anaenda mahali pa kupuria pa Boazi usiku. Anampata akiwa amelala. Anamfunua miguu na kungoja aamke.—Ruthu 3:1-7.
Kupitia tendo la Ruthu, Boazi anapoamka anaelewa maana ya ombi la Ruthu kwamba ‘aitande nguo yake juu ya mjakazi wake.’ Tendo la Ruthu linamfahamisha mzee huyo Myahudi daraka lake la kuwa mkombozi, kwani alikuwa wa jamaa ya Maloni, mume aliyekufa wa Ruthu.—Ruthu 3:9.
Boazi hakumtarajia Ruthu usiku huo. Hata hivyo, itikio lake linaonyesha alitazamia kwamba Ruthu atamwomba awe mkombozi. Boazi alikuwa na nia ya kutimiza ombi la Ruthu.
Huenda Ruthu alisikika kuwa na wasiwasi, kwa hiyo Boazi anamhakikishia hivi: “Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.”—Ruthu 3:11.
Maneno haya ya Boazi yanaonyesha kwamba aliona matendo ya Ruthu kuwa mema: “Mwanangu, ubarikiwe na BWANA; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo.” (Ruthu 3:10) Mwanzoni Ruthu alionyesha fadhili-upendo kwa Naomi. Mwishowe, Ruthu alionyesha kwamba hakuwa na ubinafsi alipomweleza Boazi aliyekuwa mzee kwamba alikuwa tayari kukombolewa naye. Ruthu alikuwa tayari kuzaa watoto ambao wangekuwa warithi wa Maloni mumewe aliyekufa, na pia wa Naomi.
Mkombozi Akataa Daraka Lake
Asubuhi iliyofuata, Boazi amwita mtu wa jamaa wa karibu zaidi na Naomi kuliko yeye. Boazi anasema hivi mbele ya wakazi na wazee wa jiji: ‘Nilikuwa na nia ya kukujulisha wewe haki yako ya kukomboa shamba la Naomi lililokuwa la mumewe Elimeleki, kwa kuwa ni lazima aliuze.’ Boazi anaendelea: ‘Je utalikomboa? Ikiwa sivyo nitalikomboa.’ Baada ya kumsikiliza Boazi, mtu huyo akubali kulikomboa.—Ruthu 4:1-4.
Lakini mtu huyo atashangaa! Boazi anasema hivi mbele ya mashahidi wote: “Siku unaponunua shamba kwa mukono wa Naomi, sharti ulinunue vilevile kwa Ruta Mumoabu, muke wake aliyekufa, unyanyue jina lake aliyekufa katika uriti wake.” Huku akiogopa kwamba huenda akaharibu urithi wake mwenyewe, mtu wa jamaa wa karibu anapuuza haki yake ya kuwa mkombozi na kusema: “Siwezi kuikomboa.”—Ruthu 4:5, 6, Zaire Swahili Bible.
Kulingana na desturi, mtu aliyekataa kukomboa alipaswa kuvua kiatu chake na kumpa mwenziwe. Kwa hiyo, mkombozi huyo anavua kiatu chake anapomwambia Boazi, “Ujinunulie mwenyewe.” Kisha Boazi anawaambia wazee na watu wote: “Ninyi ni washuhuda leo, ya kwamba nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kiliona na Malona, kwa mukono wa Naomi. Tena Ruta Mumoabu, mke wa Malona, nimemununua awe muke wangu, ninyanyue jina lake aliyekufa lisikatike katika uriti wake . . . ninyi ni washuhuda siku hii.”—Ruthu 4:7-10, ZSB.
Watu wote waliokuwa langoni wakamwambia Boazi: “BWANA na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu.”—Ruthu 4:11, 12.
Watu wamtakia Boazi heri anapomchukua Ruthu kuwa mke wake. Alimzalia mwana, wakamwita Obedi, na hivyo Ruthu na Boazi wakawa wazazi wa kale wa Mfalme Daudi na hatimaye Yesu Kristo.—Ruthu 4:13-17; Mathayo 1:5, 6, 16.
“Thawabu Kamili”
Katika simulizi hilo lote, Boazi anathibitika kuwa mtu wa pekee, yaani, mtu asiyesita kutenda na mwenye mamlaka, kuanzia wakati alipowaamkua watumishi wake hadi alipokubali daraka la kuendeleza jina la Elimeleki. Alikuwa pia mtu mwenye kujidhibiti, mwenye imani, na mwaminifu. Vilevile alikuwa mkarimu, mwenye huruma, mwenye mwenendo safi kiadili, na alitii kabisa amri za Yehova.
-