-
Simulizi la Mito MiwiliAmkeni!—2000 | Julai 8
-
-
Simulizi la Mito Miwili
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
Mito miwili iliyo muhimu kwa uhai katika bara Hindi, huandaa riziki kwa mamia ya mamilioni ya watu. Kila mto huanzia kwenye maeneo ya barafu ya safu ya milima mirefu zaidi ulimwenguni, na kutiririka taratibu kwa umbali wa zaidi ya kilometa 2,400 kupitia nchi mbili. Mito hiyo huishia katika bahari mbili tofauti. Kila mto ulikuwa chimbuko la ustaarabu wa kale. Kila mto ulihusiana na kuanza kwa dini kuu. Kila mto huthaminiwa na wanadamu kwa sababu ya faida zake, na mmoja unaabudiwa, hata leo. Inaitwaje? Mto Indus na Ganges, huo wa mwisho huitwa Ganga hapa India.
USTAARABU wa kale ulianzia karibu na mito kwa sababu maji ni muhimu kwa uhai na usitawi wa mwanadamu. Mambo hakika ya kale yaweza kufichwa na hekaya kwa sababu nyakati nyingine mito ilionwa kuwa miungu ya kiume na miungu ya kike. Ndivyo ilivyo kuhusu historia ya Mto Indus na Ganga, ambao pia huitwa Ganga Ma (Mama Ganga) hapa India.
Mlima Kailash wenye urefu wa meta 6,714 na Ziwa Manasarovar lililo karibu, huonwa na Wahindi na Wabudha kuwa makao ya miungu. Kwa muda mrefu, iliaminika kuwa mito mikubwa minne ilitiririka kutoka kwenye vinywa vya wanyama ziwani. Indus ulikuwa mto wa simba, na Ganga ulikuwa mto wa tausi.
Watibet hawakuwakaribisha wavumbuzi wageni. Hata hivyo, mnamo mwaka wa 1811, daktari Mwingereza aliye mpasuaji wa mifugo ambaye aliajiriwa na East India Company alivinjari nchini kwa kujificha. Aliripoti kwamba hakuna mito yoyote iliyotiririka kutoka kwa Manasarovar, ingawa vijito kadhaa kutoka milimani viliingia ndani yake. Vyanzo vya Mto Indus na Ganga vilivumbuliwa mwanzoni mwa karne ya 20 tu. Mto Indus huanzia Tibet, kaskazini ya Milima ya Himalaya, na Ganga huanzia kwenye pango la barafu katika miteremko ya milima ya Himalaya kaskazini mwa India.
Chimbuko la Ustaarabu wa Kale
Yaaminika kwamba wakazi wa kale zaidi wa bara Hindi walielekea upande wa mashariki na kuingia katika Bonde la Indus. Waakiolojia wamevumbua magofu ya ustaarabu wa hali ya juu sana katika eneo la Harappa na Mohenjo-Daro humo bondeni. Uvumbuzi huo uliofanywa katika miongo ya mapema ya karne ya 20, ulibadili maoni ya kwamba masetla wa awali huko India walitoka kwa makabila yasiyostaarabika ya wahamaji. Zaidi ya miaka 4,000 iliyopita, Ustaarabu wa Indus ulikuwa sawa na, au hata bora kuliko ule wa Mesopotamia. Masalio ya barabara zilizopangwa taratibu, nyumba za orofa na majengo makubwa ya makazi, mabomba na matangi bora ya maji machafu, maghala makubwa mno ya nafaka, mahekalu, na mabwawa ya kujitakasia kidesturi vyote vyathibitisha kwamba ulikuwa mji uliostaarabika kwelikweli. Pia kuna uthibitisho wa kuwapo kwa shughuli za kibiashara kati yake na Mesopotamia na Mashariki ya Kati, huku bidhaa kutoka umbali wa mamia ya kilometa barani zikisafirishwa kupitia Indus hadi Bahari ya Arabia.
Yaonekana kwamba kadiri karne zilivyopita misiba ya asili—labda matetemeko ya ardhi au mafuriko makubwa ya mito—iliharibu ustaarabu wa mjini wa Bonde la Indus. Hivyo wakawa dhaifu sana wasiweze kuzuia uvamizi mkubwa wa makabila ya wahamaji ya Asia ya Kati, ambao kwa kawaida huitwa Waarya. Waliwafukuza wakazi wengi wa mji kutoka mtoni, hivi kwamba utamaduni wa kale uliokuwa umesitawi kuzunguka Indus ukaelekea kusini mwa India, ambako leo kuna Wadravidi, mojawapo ya makabila yenye watu wengi huko India.
-
-
Simulizi la Mito MiwiliAmkeni!—2000 | Julai 8
-
-
Mito Hiyo Ikoje Leo?
Maji ya mto ni muhimu sana leo kuliko yalivyokuwa miaka 4,000 iliyopita, watu walipohamia kwenye kingo za Mto Indus na Ganga ili kujiruzuku. Ni sharti mito hiyo isimamiwe kwa uangalifu ili iweze kuruzuku wakazi wengi wa India, Pakistan, na Bangladesh. (Ona ramani kwenye ukurasa wa 16-17.) Mikataba ya kimataifa imehitaji kufanywa kwa kuwa mito hiyo hupita katika nchi kadhaa. Miongoni mwa miradi mingine, Pakistan imejenga Bwawa la Tarbela lenye urefu wa kilometa tatu na kina cha meta 143 kwa ajili ya kilimo cha kumwagilia maji. Ni mojawapo ya mabwawa makubwa zaidi ulimwenguni, limejazwa dhiraa meta 148,500,000 za ardhi.
-
-
Simulizi la Mito MiwiliAmkeni!—2000 | Julai 8
-
-
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 16, 17]
Mto Indus Wenye Nguvu
Kumekuwa na ubishi kuhusu chanzo cha Mto Indus kwa sababu vijito vingi huungana na kufanyiza mto huo. Lakini hapana shaka kwamba mto huo mkubwa huanzia kwenye milima ya Himalaya. Hutiririka kuelekea upande wa kaskazini-magharibi na kuungana na vijito vingine njiani, na kusonga kwa umbali wa kilometa 320 kupitia uwanda wa juu wa Tibet, “kilele cha ulimwengu.” Mto huo ukaribiapo mpaka wa India katika jimbo la Ladakh, hujipinda-pinda milimani, na kupenya majabali na hufanyiza mfereji kati ya safu ya milima ya Himalaya na Karakoram. Kisha huingia nchini India na kuporomoka kwa kina cha meta 3,700 hivi kwa umbali wa kilometa 560. Huporomoka na kuelekea kaskazini halafu hupiga kona kali kwenye pembe ya magharibi ya Himalaya, ambapo huungana na Gilgit, mto mkubwa utokao Hindu Kush. Halafu mto huo hutiririka kusini hadi Pakistan. Mto Indus hupenya katikati ya milima, ukijipinda-pinda na kusonga kwa nguvu nyingi hadi uwandani na kutiririka kupitia Punjab. Jina hilo lamaanisha “Mito Mitano,” mito mikubwa inayojiunga nao—Beas, Sutlej, Ravi, Jhelum, na Chenab—hutiririka kama vidole vilivyosambaa vya mkono mkubwa na kuingia kwenye Mto Indus kisha husonga taratibu hadi mwisho kwa umbali wa zaidi ya kilometa 2,900.
-