Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Januari 1
    • Njia za Bahari za Aleksandria na Roma

      Waroma waliposhinda maeneo yaliyotawaliwa na magavana waliotawala baada ya Aleksanda, Roma ikawa soko kuu la bidhaa zenye thamani kutoka Mashariki, kama vile pembe za tembo kutoka Afrika, uvumba na manemane kutoka Arabia, vikolezo na mawe yenye thamani kutoka India, na hata hariri kutoka China. Meli zilizobeba bidhaa hizo zilikutana kwenye bandari mbili kuu, yaani, Berenice na Myos Hormos kwenye Pwani ya Bahari Nyekundu huko Misri. Kutoka kwenye bandari hizo wafanyabiashara wangefuata njia zinazoelekea Coptos, kwenye Mto Nile.

      Kutoka Coptos, bidhaa zilipitia Mto Nile, njia kuu ya Misri kuelekea Aleksandria ambako zilipakiwa kwenye meli na kusafirishwa hadi Italia na kwingineko. Njia nyingine ya kwenda Aleksandria ilikuwa kupitia mfereji uliounganisha chanzo cha Bahari Nyekundu pamoja na Mto Nile, karibu na Suez ya kisasa. Bila shaka, Misri na bandari zake zilikuwa karibu na maeneo ambayo Yesu alihubiri na zingeweza kufikiwa kwa urahisi kutoka maeneo hayo.

      Strabo mwanajiografia Mgiriki wa karne ya kwanza, anasema kwamba katika siku zake, meli 120 za Aleksandria zilisafiri kila mwaka kutoka Myos Hormos ili kufanya biashara na India. Kitabu fulani cha karne ya kwanza kuhusu usafiri katika eneo hilo kipo hadi leo. Yaelekea kiliandikwa na mfanyabiashara Mmisri aliyezungumza Kigiriki kwa faida ya wafanyabiashara wenzake. Kitabu hicho cha kale kinafunua mambo gani?

      Kitabu hicho ambacho mara nyingi kinatajwa kwa jina lake la Kilatini, Periplus Maris Erythraei (Kuabiri Bahari ya Erythra) kinaeleza kuhusu njia za baharini zenye urefu wa maelfu ya kilomita kusini ya Misri, kufika hadi Zanzibar. Kuelekea upande wa mashariki, mwandishi wa kitabu hicho anaonyesha umbali, mahali pa kutia nanga, maeneo ya biashara, bidhaa zilizouzwa, na mtazamo wa watu walioishi kando ya pwani ya kusini ya Arabia, kuelekea pwani ya magharibi ya India hadi Sri Lanka, kisha kuelekea pwani ya mashariki ya India kufikia Mto Ganges. Ufafanuzi sahihi na ulio wazi wa kitabu hicho unaonyesha kwamba mtungaji wake alitembelea maeneo aliyotaja.

      Wazungu Huko India

      Huko India wafanyabiashara kutoka Ulaya waliitwa Wayavana. Kulingana na kitabu Periplus, eneo moja ambalo walitembelea kwa ukawaida katika karne ya kwanza W.K. lilikuwa Muziris, karibu na ncha ya kusini ya India.a Mashairi ya Kitamili yaliyoandikwa katika karne za mapema W.K., yanataja mara nyingi kuhusu wafanyabiashara hao. “Meli maridadi za Wayavana zilileta dhahabu na kurudi na pilipili, na Muziris ikajaa kelele,” linasema shairi moja. Katika shairi lingine, mwana mmoja wa mfalme wa India kusini anasihiwa anywe divai bora iliyoletwa na Wayavana. Bidhaa nyingine kutoka Magharibi zilizouzwa kwa wingi huko India ni vyombo vya glasi, vyuma, marijani, na vitambaa.

      Wachimbuzi wa vitu vya kale wamechimbua bidhaa nyingi zilizoletwa India kutoka Magharibi. Kwa mfano, huko Arikamedu kwenye pwani ya kusini-mashariki ya India, baadhi ya vitu ambavyo vimechimbuliwa ni vigae vya magudulia ya divai ya Waroma na vyombo vilivyo na mihuri ya wafinyanzi waliotengeneza bidhaa hizo huko Arezzo, Italia ya kati. “Fikira za mtafiti wa kisasa zinachochewa anapopata vigae vilivyo na majina ya wafinyanzi kwenye mchanga-tope katika Ghuba ya Bengal ambao tanuru zao ziko kwenye vitongoji vya Arezzo,” anasema mwandishi mmoja. Uthibitisho zaidi wa kwamba kulikuwa na biashara kati ya eneo la Mediterania na India unaonekana pia katika sarafu za Roma za dhahabu na fedha ambazo zimepatikana kusini mwa India. Sarafu nyingi kati ya hizo ni za karne ya kwanza W.K. na zina picha za Maliki Waroma Agusto, Tiberio, na Nero.

      Uwezekano wa kwamba raia wa Roma walianzisha koloni za kudumu za kibiashara huko India kusini unaonekana katika ramani ya kale ambayo nakala yake inapatikana hadi leo. Ramani hiyo, inayoitwa Mchoro wa Peutinger, ambayo inasemekana kuwa ni ramani ya Milki ya Roma kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza W.K., inaonyesha hekalu la Agusto huko Muziris. “Jengo kama hilo,” kinasema kitabu fulani kuhusu biashara za Waroma (Rome’s Eastern Trade: International Commerce and Imperial Policy, 31 BC–AD 305), “lingeweza kujengwa tu na raia wa Milki ya Roma, na inadhaniwa kuwa wangekuwa raia walioishi Muziris au waliotumia wakati mwingi huko.”

      Rekodi za Roma zinataja angalau ziara tatu za mabalozi wa India huko Roma wakati wa utawala wa Agusto kuanzia mwaka wa 27 K.W.K. hadi 14 W.K. “Mabalozi hao walikuwa na kusudi muhimu kutoka nchi yao,” unasema uchunguzi mmoja uliofanywa kuhusu jambo hilo, yaani, walienda ili kukubaliana kuhusu mahali ambapo biashara kati ya watu wa nchi mbalimbali ingefanywa, jinsi ya kutoza kodi, mahali ambapo watu wa nchi za kigeni wangeishi, na kadhalika.

  • Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Januari 1
    • Maandishi ya Hou Han-Shou (Kumbukumbu za Kihistoria za Milki ya Baadaye ya Han), ya mwaka wa 23 W.K. hadi 220 W.K. yanaonyesha tarehe ya mojawapo ya safari hizo. Mnamo 166 W.K., balozi aliyeitwa An-tun, ambaye alitumwa na mfalme wa Daqin, aliwasili kwenye makao ya mfalme wa China akiwa na zawadi kwa ajili ya Maliki Huan-ti. Daqin lilikuwa jina la Kichina la Milki ya Roma, na yaelekea An-tun lilikuwa jina la Kichina la Antoninus, jina la familia ya Marcus Aurelius, aliyekuwa maliki Mroma wakati huo. Wanahistoria wanafikiri kwamba hiyo haikuwa ziara rasmi ya kibalozi bali ilikuwa jitihada iliyokusudiwa kuwasaidia wafanyabiashara wa ulaya wapate hariri moja kwa moja kutoka China badala ya kupitia kwa walanguzi.

  • Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Januari 1
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

      Maliki Alalamika

      Mnamo 22 W.K. Maliki Mroma Tiberio alilalamika kwamba raia zake walikuwa wakitumia mali kupita kiasi. Hamu yao isiyoweza kutoshelezwa ya anasa, na tamaa ya wanawake Waroma inayopita kiasi ya vito ilikuwa ikifuja mali ya milki yake, na kuipeleka kwa “mataifa mageni au yenye uhasama.” Pia, mwanahistoria Mroma Plini Mkubwa (23-79 W.K.) alilalamika kuhusu jambo hilo. Aliandika: “Kadirio la chini zaidi linaonyesha kwamba kila mwaka maeneo ya India, Seres, na Rasi ya Arabia, yanachukua kutoka kwa milki yetu sesterce milioni 100—kwa kweli tunatumia pesa nyingi kwa ajili ya anasa na wanawake wetu.”b

      [Maelezo ya chini]

      b Wachunguzi wanakadiria kwamba sesterce milioni 100 zilikuwa sawa na asilimia 2 ya uchumi wote wa Milki ya Roma.

      [Hisani]

      Museo della Civiltà Romana, Roma; Todd Bolen/Bible Places.com

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki