Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wale Wafalme Wawili Wabadilika
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • MFALME MPYA ATUMA ‘MTOZA-USHURU’

      4. Kwa nini tutarajie utawala mwingine uwe mfalme wa kaskazini?

      4 Masika ya mwaka wa 33 W.K., Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Mwonapo mara hiyo kitu chenye kuchukiza sana ambacho husababisha ukiwa, kama kilivyosemwa kupitia Danieli nabii, kikiwa kimesimama katika mahali patakatifu, . . . ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani.” (Mathayo 24:15, 16) Akinukuu Danieli 11:31, Yesu aliwaonya wafuasi wake juu ya ‘kitu chenye kuchukiza sana kinachosababisha ukiwa’ cha wakati ujao. Unabii huo unaohusu mfalme wa kaskazini ulitolewa miaka 195 hivi baada ya kifo cha Antiochus wa Nne, mfalme wa mwisho wa Siria aliyekuwa mfalme wa kaskazini. Bila shaka, utawala mwingine ungekuwa mfalme wa kaskazini. Nani huyo?

      5. Ni nani aliyesimama akiwa mfalme wa kaskazini, na kuchukua wadhifa uliokuwa wa Antiochus wa Nne wakati mmoja?

      5 Malaika wa Yehova Mungu alitabiri hivi: “Badala yake [Antiochus wa Nne] atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.” (Danieli 11:20) ‘Asimamaye’ hivyo alithibitika kuwa maliki wa kwanza wa Roma, Octavian, aliyeitwa Kaisari Augusto.—Ona “Mmoja Aheshimiwa, Yule Mwingine Adharauliwa,” kwenye ukurasa wa 248.

      6. (a) ‘Mtoza-ushuru alipitishwa’ lini katika “utukufu wa ufalme,” na hilo lilikuwa na umaana gani? (b) Kwa nini twaweza kusema kwamba Augusto alikufa “si kwa hasira, wala si katika vita”? (c) Mfalme wa kaskazini alibadilika akawa nani?

      6 ‘Ufalme wenye utukufu’ wa Augusto ulitia ndani “nchi ya uzuri”—Yudea, mkoa wa Roma. (Danieli 11:16) Mwaka wa 2 K.W.K., Augusto alimtuma ‘mtoza-ushuru’ kwa kuagiza uandikishaji, au kuhesabiwa kwa watu, huenda ili apate kujua idadi ya watu kwa minajili ya kutoza kodi na kuwaandikisha kwa lazima kwenye utumishi wa kijeshi. Kwa sababu ya agizo hilo, Yosefu na Maria walisafiri hadi Bethlehemu wakajiandikishe, kisha Yesu akazaliwa mahali palipotabiriwa. (Mika 5:2; Mathayo 2:1-12) Agosti mwaka wa 14 W.K.—“katika muda wa siku chache,” au punde baada ya kuagiza uandikishaji—Augusto akafa akiwa na umri wa miaka 76, si “kwa hasira” mikononi mwa muuaji wala “katika vita,” bali kwa sababu ya ugonjwa. Kwa kweli, mfalme wa kaskazini alikuwa amebadilika! Kufikia sasa mfalme huyo alikuwa Milki ya Roma ikiwa na watawala wake.

      ‘MWENYE KUDHARAULIWA ASIMAMA’

      7, 8. (a) Ni nani aliyechukua mahali pa Augusto akiwa mfalme wa kaskazini? (b) Kwa nini Kaisari Augusto alimpa mwandamizi wake “heshima ya ufalme” kwa shingo upande?

      7 Akiendelea na unabii huo, malaika asema hivi: “Badala yake [Augusto] atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza [“kunyakua ufalme kwa hila,” BHN]. Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika; naam, mkuu wa maagano pia.”—Danieli 11:21, 22.

      8 “Mtu astahiliye kudharauliwa” alikuwa Kaisari Tiberio, mwana wa Livia, mke wa tatu wa Augusto. (Ona “Mmoja Aheshimiwa, Yule Mwingine Adharauliwa,” kwenye ukurasa wa 248.) Augusto alimchukia mwana wake wa kambo kwa sababu ya tabia yake mbaya wala hakutaka awe Kaisari baada yake. Alimpa “heshima ya ufalme” shingo upande baada ya watu wote ambao wangeweza kuwa Kaisari kufa. Augusto alimwasilisha Tiberio mwaka wa 4 W.K. na kumfanya awe mrithi wa ufalme. Baada ya Augusto kufa, Tiberio mwenye umri wa miaka 54—mwenye kudharauliwa—‘akasimama,’ akitwaa mamlaka ya kuwa maliki wa Roma na mfalme wa kaskazini.

      9. Tiberio ‘alinyakuaje ufalme kwa hila’?

      9 “Tiberio,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “alitumia hila dhidi ya Seneti wala hakuiruhusu imteue awe maliki kwa zaidi ya mwezi mmoja [baada ya Augusto kufa].” Aliiambia Seneti kwamba hakuna mtu yeyote ila Augusto aliyekuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa kutawala Milki ya Roma na akawaomba maseneta waweke kikundi cha watu kimiliki badala ya mtu mmoja. “Bila kunuia kukubali aliyosema,” akaandika mwanahistoria Will Durant, “Seneti ilibembelezana-bembelezana naye mpaka hatimaye akaikubali mamlaka hiyo.” Durant alisema hivi pia: “Pande zote mbili zilikuwa zikijifanya. Tiberio alitaka kuwa maliki wa Roma, la sivyo angalipata njia ya kuuhepa umaliki; Seneti ilimhofu na kumchukia, lakini haikutaka tena kuwa jamhuri, kama ile ya kale, ambayo ilitegemea mabunge ya watawala ya kuwaziwa tu.” Kwa hiyo, Tiberio ‘akaunyakua ufalme kwa hila.’

      10. ‘Silaha mfano wa gharika zilivunjwaje’?

      10 “Na wale wenye silaha mfano wa gharika”—majeshi ya falme zilizozunguka—malaika alisema hivi: “Watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika.” Tiberio alipokuwa mfalme wa kaskazini, mpwa wake wa kiume Kaisari Germanicus alikuwa kamanda wa vikosi vya Roma kwenye Mto Rhine. Mwaka wa 15 W.K., Germanicus aliongoza majeshi yake dhidi ya shujaa Mjerumani Arminius, naye akafaulu kwa kiasi fulani. Hata hivyo, ushindi huo ulimgharimu sana, naye Tiberio akaacha mambo ya Ujerumani. Badala yake, kwa kuendeleza vita vya kikabila, alijaribu kuyazuia makabila ya Ujerumani yasiungane. Kwa kawaida, Tiberio alipendelea sera ya kujikinga na nchi za kigeni naye akakazia fikira kuimarisha mipaka. Sera hiyo ya kujikinga ilikuwa na mafanikio kwa kiasi fulani. Kwa njia hiyo “silaha mfano wa gharika” zikadhibitiwa na ‘kuvunjwa.’

      11. ‘Mkuu wa maagano alivunjwaje’?

      11 “Mkuu wa maagano” ambayo Yehova Mungu alikuwa amefanya na Abrahamu ili kubariki familia zote duniani ‘alivunjwa’ pia. Yesu Kristo alikuwa Mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa katika agano hilo. (Mwanzo 22:18; Wagalatia 3:16) Nisani 14, 33 W.K., Yesu alisimama mbele ya Pontio Pilato katika jumba la gavana wa Roma huko Yerusalemu. Makuhani Wayahudi walikuwa wamemshtaki Yesu kuwa mhaini dhidi ya maliki. Lakini Yesu alimwambia Pilato hivi: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu. . . . Ufalme wangu si kutoka chanzo hiki.” Kwa kuwa Wayahudi hawakutaka gavana Mroma amwachilie Yesu asiye na hatia, walipaaza sauti, wakisema: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mwenyewe mfalme asema vibaya dhidi ya Kaisari.” Baada ya kuagiza Yesu auawe, walisema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.” Kulingana na sheria ya ‘uhaini,’ ambayo Tiberio alikuwa ameipanua itie ndani kumtukana Kaisari kwa njia yoyote, Pilato akamtoa Yesu ‘avunjwe,’ au atundikwe kwenye mti wa mateso.—Yohana 18:36; 19:12-16; Marko 15:14-20.

      MKANDAMIZAJI ‘ATUNGA HILA ZAKE’

      12. (a) Ni nani waliofanya maagano na Tiberio? (b) Tiberio ‘alikuwaje hodari pamoja na watu wadogo’?

      12 Bado akitoa unabii juu ya Tiberio, malaika alisema hivi: “Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.” (Danieli 11:23) Washiriki wa Seneti ya Roma walikuwa ‘wamefanya maagano’ ya kikatiba na Tiberio, naye aliwategemea kihalali. Lakini alitenda kwa hila, hata akawa “hodari pamoja na watu wadogo.” Watu hao wadogo walikuwa Walindaji wa Praetori wa Roma waliokuwa wamepiga kambi karibu na kuta za Roma. Ukaribu huo uliogofya Seneti na kumsaidia Tiberio adhibiti maasi yoyote dhidi ya mamlaka yake miongoni mwa watu wa kawaida. Tiberio aliendelea kuwa mwenye nguvu akitumia walinzi 10,000.

      13. Tiberio alishindaje baba zake?

      13 Malaika huyo aliongeza kusema hivi kiunabii: “Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.” (Danieli 11:24) Tiberio alikuwa mwenye kushukushuku sana, naye aliagiza watu wengi wauawe alipokuwa akitawala. Hasa kwa sababu ya Sejanus, kamanda wa Walindaji wa Praetori, sehemu ya mwisho ya utawala wake iliogofya sana. Hatimaye, Sejanus mwenyewe akaanza kushukiwa kisha akauawa. Tiberio alishinda baba zake katika kuwakandamiza watu.

      14. (a) Tiberio alitawanyaje “mawindo, na mateka, na mali” kotekote katika mikoa ya Roma? (b) Watu walimwonaje Tiberio kufikia wakati alipokufa?

      14 Hata hivyo, Tiberio alitawanya “mawindo, na mateka, na mali” kotekote katika mikoa ya Roma. Alipokufa, raia zake wote walikuwa na ufanisi. Kodi hazikuwa zenye kulemea, naye alikuwa mkarimu kwa wale waliokuwa na magumu. Iwapo askari au maofisa walimwonea yeyote au kuendeleza mambo yasiyo ya kawaida katika kushughulikia mambo, wangaliweza kutarajia kisasi cha mtawala. Kuwa na mamlaka imara kulidumisha usalama, na mfumo ulioboreshwa wa kuwasiliana ulisaidia katika biashara. Tiberio alihakikisha kwamba mambo yalifanywa bila upendeleo na kwa utaratibu ndani na nje ya Roma. Kuendeleza mabadiliko yaliyoanzishwa na Kaisari Augusto kuliboresha sheria, na mifumo ya kijamii na ya kiadili. Hata hivyo, Tiberio ‘alitunga hila zake,’ hivi kwamba mwanahistoria Mroma Tasito alimfafanua kuwa mnafiki, mwenye ustadi wa kujifanya. Kufikia wakati alipokufa Machi 37 W.K., Tiberio alionwa kuwa mkandamizaji.

      15. Roma iliendeleaje mwishoni mwa karne ya kwanza na mwanzoni mwa karne ya pili W.K.?

      15 Wamaliki waliotawala baada ya Tiberio ambao walikuwa wafalme wa kaskazini walitia ndani Kaisari Gayo (Caligula), Klaudio wa Kwanza, Nero, Vaspasiani, Tito, Domitiani, Nerva, Trajani, na Hadriani. “Kwa muda mrefu,” chasema kichapo The New Encyclopædia Britannica, “wamaliki waliotawala baada ya Augusto waliendeleza sera zake za kutawala na miradi yake ya ujenzi, ingawa hawakuanzisha mambo mengi nao walikuwa wenye kujionyesha sana.” Kichapo hichohicho chataarifu hivi: “Mwishoni mwa karne ya 1 na mwanzoni mwa karne ya 2, Roma ilikuwa imefikia upeo wa utukufu nayo ilikuwa na wakazi wengi zaidi.” Ingawa Roma ilikuwa na matatizo kadhaa kwenye mipaka yake, pambano lake la kwanza lililotabiriwa dhidi ya mfalme wa kusini halikutukia hadi karne ya tatu W.K.

      ACHOCHEWA DHIDI YA MFALME WA KUSINI

      16, 17. (a) Ni nani aliyekuwa mfalme wa kaskazini anayetajwa kwenye Danieli 11:25? (b) Ni nani aliyekuja kuwa mfalme wa kusini, na hilo lilitukiaje?

      16 Malaika wa Mungu aliendelea na unabii huo, akisema hivi: “Naye [mfalme wa kaskazini] atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini [mfalme wa kaskazini] hatasimama; maana watatunga hila juu yake. Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa.”—Danieli 11:25, 26.

      17 Miaka 300 hivi baada ya Octavian kufanya Misri iwe mkoa wa Roma, Maliki Mroma Aurelian akawa mfalme wa kaskazini. Wakati huohuo, Malkia Septimia Zenobia wa koloni ya Roma ya Palmyra akawa mfalme wa kusini.a (Ona “Zenobia—Malkia Mpiganaji wa Palmyra,” kwenye ukurasa wa 252.) Jeshi la Palmyra lilikuwa likimiliki Misri mwaka wa 269 W.K. likisingizia kuwa lilikuwa likiifanya iwe salama kwa ajili ya Roma. Zenobia alitaka kufanya Palmyra liwe jiji kuu huko mashariki na alitaka kutawala mikoa ya mashariki ya Roma. Akishtuliwa na tamaa ya makuu ya Zenobia, Aurelian alichochea “nguvu zake na ushujaa wake” dhidi ya Zenobia.

      18. Matokeo ya pambano kati ya Maliki Aurelian, mfalme wa kaskazini, na Malkia Zenobia, mfalme wa kusini yalikuwa nini?

      18 Mfalme wa kusini, yaani serikali ya Zenobia, ‘alifanya’ vita dhidi ya mfalme wa kaskazini “kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi” chini ya majenerali wawili, Zabdas na Zabbai. Lakini Aurelian aliteka Misri kisha akafunga safari kwenda Asia Ndogo na Siria. Zenobia alishindwa huko Emesa (kuitwako Homs leo), akakimbia na kwenda Palmyra. Aurelian alipolizingira jiji hilo, Zenobia alilipigania kufa na kupona lakini hakufanikiwa. Yeye na mwanaye wakakimbia kuelekea Uajemi, wakakamatwa na Waroma kwenye Mto Eufrati. Watu wa Palmyra walisalimisha jiji lao mwaka wa 272 W.K. Aurelian hakumuua Zenobia, hilo likimfanya avutie watu wengi katika ule msafara wa ushindi kupitia Roma mwaka 274 W.K. Aliishi maisha yake yaliyosalia akiwa mke Mroma.

      19. Aurelian aliangukaje kwa sababu ya ‘hila zilizotungwa juu yake’?

      19 Aurelian mwenyewe ‘hakusimama kwa sababu ya hila zilizotungwa juu yake.’ Mwaka wa 275 W.K., alifunga safari kwenda kupigana na Waajemi. Alipokuwa akingoja huko Thrasi ili apate fursa ya kuvuka mlango-bahari na kuingia Asia Ndogo, wale ‘waliokula sehemu ya chakula chake’ walitunga hila juu yake na ‘kumwangamiza.’ Alinuia kumwadhibu mwandishi wake Eros kwa sababu mambo hayakuwa shwari. Hata hivyo, Eros akaandika orodha bandia ya majina ya maofisa kadhaa waliotiwa alama wauawe. Maofisa hao walipoiona orodha hiyo walipanga njama na kumwua Aurelian.

      20. “Jeshi” la mfalme wa kaskazini ‘liligharikishwaje’?

      20 Mfalme wa kaskazini hakutoweka Maliki Aurelian alipokufa. Waroma wengine walitawala baada yake. Kwa muda fulani kulikuwa na maliki wa magharibi na maliki wa mashariki. Chini yao “jeshi” la mfalme wa kaskazini ‘liligharikishwa,’ au ‘kutawanywa,’b na wengi ‘walianguka wameuawa’ kwa sababu ya uvamizi wa makabila ya Kijerumani kutoka kaskazini. Wagothi walivuka mipaka ya Roma katika karne ya nne W.K. Uvamizi uliendelea, mmoja baada ya mwingine. Mwaka wa 476 W.K., kiongozi wa Ujerumani, Odoacer alimwondoa maliki wa mwisho aliyekuwa akitawala Roma. Kufikia mwanzoni mwa karne ya sita, Milki ya Roma ya upande wa magharibi ilikuwa imevunjwa-vunjwa, na wafalme Wajerumani walikuwa wakitawala Afrika Kaskazini, Gaul, Hispania, Italia, na Uingereza. Upande wa mashariki wa milki hiyo ulidumu hadi karne ya 15.

  • Wale Wafalme Wawili Wabadilika
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • [Picha katika ukurasa wa 233]

      Augusto

      [Picha katika ukurasa wa 234]

      Tiberio

      [Picha katika ukurasa wa 235]

      Kwa sababu ya amri ya Augusto, Yosefu na Maria walisafiri kwenda Bethlehemu

      [Picha katika ukurasa wa 237]

      Kama ilivyotabiriwa, Yesu ‘alivunjwa’ kwenye kifo

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki