-
Jinsi Dini Ilivyookoka MashambuliziAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
Jinsi Dini Ilivyookoka Mashambulizi
KABLA ya Ujerumani ya Nazi kuvamia Urusi mnamo Juni 1941, serikali ya Sovieti ilikuwa karibu kukomesha Kanisa Othodoksi la Urusi. Lakini baada ya uvamizi wa Wanazi, serikali ya Sovieti ilianza kubadili maoni yake kuelekea dini. Mbona ikabadili maoni?
Richard Overy, profesa wa historia ya kisasa katika King’s College, London, alieleza sababu katika kitabu chake Russia’s War—Blood Upon the Snow: “Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Sergei [Sergius], aliwasihi waumini siku hiyohiyo ya uvamizi wajitoe mhanga ili kushinda Ujerumani. Miaka miwili iliyofuata alichapisha angalau barua ishirini na tatu, na kuwaomba waumini wote wapambane kwa ajili ya serikali yao isiyomwamini Mungu.” Kwa hiyo, kama Overy alivyoendelea kusema, ‘Stalin aliruhusu dini isitawi tena.’
Hatimaye, Stalin aliidhinisha Kanisa Othodoksi mwaka wa 1943 alipomteua Sergius kuwa kiongozi mpya wa kanisa hilo. “Viongozi wa Kanisa hilo waliitikia kwa kuchanga pesa kutoka kwa waumini kwa ajili ya kikosi cha magari ya vita cha Sovieti,” akasema Overy. “Makasisi na maaskofu walisihi makundi yao yamtii Mungu na Stalin.”
Mrusi Sergei Ivanenko ambaye ni msomi wa dini aliandika hivi kuhusu kipindi hicho katika historia ya Urusi: ‘Kichapo rasmi cha Kanisa Othodoksi la Urusi cha The Journal of the Moscow Patriarchate, kilimsifu Stalin kuwa kiongozi na mwalimu mkuu zaidi ya wote duniani, aliyetumwa na Mungu ili kuokoa taifa hilo na uonevu, wamiliki wa mashamba, na mabepari. Kiliwasihi waumini wapigane kufa na kupona ili kulinda Muungano wa Sovieti na adui zake na kusitawisha Ukomunisti kwa hali na mali.’
“Kanisa Lilithaminiwa Sana na KGB”
Kanisa Othodoksi liliwasaidia sana Wakomunisti hata baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili kukoma mwaka wa 1945. Kichapo The Soviet Union: The Fifty Years, kilichohaririwa na Harrison Salisbury, kilieleza jinsi ilivyokuwa: “Baada ya vita kukoma, viongozi wa kanisa waliunga mkono madai ya Stalin kuhusu sera ya nchi za kigeni wakati wa Vita Baridi.”
Kitabu kilichoandikwa hivi karibuni cha The Sword and the Shield chaeleza jinsi viongozi wa kanisa walivyoendeleza masilahi ya Sovieti. Chaeleza kwamba Kiongozi wa Kanisa Alexis wa Kwanza, aliyechukua cheo cha Sergius mwaka wa 1945, “alijiunga na Baraza la Kuleta Amani Duniani, chama cha Sovieti kilichoanzishwa mwaka wa 1949.” Kitabu hicho pia chasema kwamba yeye pamoja na Askofu Mkuu Nikolai “walithaminiwa sana na wapelelezi wa KGB [Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti] kuwa watu waliosaidia serikali kutekeleza malengo yake.”
Jambo la ajabu ni kwamba mwaka wa 1955, Kiongozi wa Kanisa, Alexis wa Kwanza alitangaza hivi: “Kanisa Othodoksi la Urusi linaunga mkono kikamili sera ya amani ya serikali yetu, si kwa sababu Kanisa halina uhuru, bali kwa sababu sera ya Sovieti ni ya haki na inapatana na mafundisho ya Kikristo yanayohubiriwa na Kanisa.”
Katika toleo la Januari 22, 2000, la gazeti The Guardian la London, Uingereza, kasisi mpinzani wa Othodoksi Georgi Edelshtein alisema: “Maaskofu wote waliteuliwa kwa uangalifu ili waweze kushirikiana na serikali ya sovieti. Wote walikuwa wapelelezi wa KGB. Inajulikana kote kwamba Kiongozi wa Kanisa Alexy aliyeajiriwa na shirika la KGB, alibandikwa jina la siri la Drozdov. Leo, maaskofu hao wana siasa zilezile walizokuwa nazo miaka 20 au 30 iliyopita.”
Watumishi wa Serikali ya Sovieti
Kuhusu uhusiano kati ya Kanisa Othodoksi na Serikali ya Sovieti, gazeti Life la Septemba 14, 1959, lilisema hivi: “Kanisa lilimwona Stalin kama kiongozi kwa sababu lilipata mapendeleo fulani. Kuna wizara maalumu ya serikali inayodumisha ushirikiano na Kanisa Othodoksi. Wakomunisti wametumia kanisa tangu wakati huo kuwa chombo cha serikali ya Sovieti.”
Matthew Spinka, mtaalamu wa masuala ya kanisa nchini Urusi, alikiri katika kitabu chake The Church in Soviet Russia cha mwaka wa 1956 kuwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya Kanisa na Serikali. Aliandika kwamba “Kiongozi wa Kanisa aliyepo sasa, Alexei, amefanya Kanisa kuwa chombo cha serikali.” Kwa hivyo, Kanisa Othodoksi liliokoka kwa sababu lilitumikia Serikali. ‘Lakini kuna ubaya gani?’ huenda ukauliza. Fikiria maoni ya Mungu na ya Kristo kuhusu jambo hilo.
Yesu Kristo alisema hivi kuhusu wanafunzi wake wa kweli: “Nyinyi si sehemu ya ulimwengu, bali nimewachagua nyinyi kutoka ulimwenguni.” Na Neno la Mungu lauliza hivi waziwazi: “Wanawake wazinzi, je, hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu?” (Yohana 15:19; Yakobo 4:4) Kwa hivyo, kulingana na Biblia, kanisa lilijifanya kuwa kahaba wa kidini ambaye “wafalme wa dunia walifanya uasherati naye.” Limejithibitisha kuwa sehemu ya yule anayeitwa na Biblia “Babiloni Mkubwa, mama wa makahaba na wa mambo yenye kuchukiza sana ya dunia.”—Ufunuo 17:1-6.
-
-
Jinsi Dini Ilivyookoka MashambuliziAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Ushirikiano wa Kanisa na Sovieti
Edmund Stevens aliandika hivi katika kitabu chake Russia Is No Riddle cha mwaka wa 1945: “Kanisa lilitahadhari sana kutopinga mhisani wake. Kanisa lilitambua kabisa kwamba Serikali ilitarajia liunge mkono utawala wa Sovieti na kutii sheria zake baada ya kupewa mapendeleo.”
Stevens aliendelea kueleza hivi: “Ilikuwa rahisi sana kwa Kanisa Othodoksi kushirikiana na Serikali ya Sovieti kwa sababu kwa karne nyingi Kanisa Othodoksi lilikuwa dini rasmi ya Kitaifa.”
Taasisi ya Keston ilichunguza kindani ushirikiano kati ya Wasovieti na Alexis wa Pili, ambaye ni kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi leo. Ripoti yake ilimalizia hivi: “Ushirikiano wa Aleksi haushangazi kwani karibu viongozi wa dini zote zilizosajiliwa—kutia ndani Wakatoliki, Wabaptisti, Waadventisti, Waislamu na Wabudha—walikuwa vibaraka wa KGB. Hata, ripoti ya kila mwaka inayoeleza ushirikiano wa Aleksi na KGB inataja pia vibaraka wengine wengi, baadhi yao walikuwa viongozi wa Kanisa la Kilutheri la Estonia.”
-
-
Jinsi Dini Ilivyookoka MashambuliziAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
[Picha katika ukurasa wa 10]
Stalin aliruhusu dini kusitawi kwa muda kwa sababu kanisa lilimwunga mkono wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili
[Hisani]
U.S. Army photo
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kiongozi wa Kanisa Alexis wa Kwanza (1945-1970) alisema hivi: ‘Sera ya Sovieti yapatana na mafundisho ya Kikristo ambayo yanahubiriwa na Kanisa’
[Hisani]
Central State Archive regarding the film/photo/phono documents of Saint-Petersburg
-