Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Bado Ni Salama Kusafiri kwa Ndege?
    Amkeni!—2002 | Desemba 8
    • Je, Bado Ni Salama Kusafiri kwa Ndege?

      NDEGE nne kubwa za abiria zatekwa nyara. Ndege hizo nne zakumbwa na msiba. Majengo maarufu yaharibiwa. Ndege aina ya 767 yagonga mojawapo ya yale majengo ya Twin Towers, na tukio hilo laonyeshwa tena na tena kwenye televisheni.

      Magaidi walitumia mbinu mpya zenye kuogopesha katika mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Mashirika ya ndege yalitumiwa kutimiza lengo hatari, na ndege zikatumiwa kama mabomu.

      Kutokana na hilo, baadhi ya wasafiri wa ndege wameanza kuogopa jambo fulani: Ijapokuwa hapo awali walihisi salama kusafiri kwa ndege, sasa wanaogopa mashambulizi ya magaidi. Isitoshe, baada ya Septemba 11 kumekuwa na misiba ya ndege ambayo haikusababishwa na magaidi, nayo imewafanya wengi waogope kusafiri kwa ndege hata zaidi.

      Ni kweli kwamba usafiri wa ndege ni wa bei ghali na mamilioni ya watu ulimwenguni hawawezi kuugharimia. Hata hivyo, wengine hulazimika kusafiri kwa ndege mara nyingi. Wale walio na kazi zinazowalazimu kusafiri sana, hawana budi kupanda ndege. Mara nyingi mishonari na wahudumu Wakristo huhitaji kusafiri mbali kwa ndege ili wafike au watoke mahali walikotumwa. Nyakati nyingine, hata watu maskini hulazimika kusafiri kwa ndege wanapohitaji matibabu ya dharura. Na maelfu ya marubani na wafanyakazi wa ndege hujiruzuku kupitia usafiri wa ndege.

      Wengi kati ya watu hao wanaosafiri kwa ndege wanalazimika kuwatuliza wenzi wao wa ndoa na watoto wao wenye wasiwasi kabla ya kufunga safari zao, japo huenda ikawa wao wenyewe wana wasiwasi. Kwa kuwa safari hizo sasa zimekuwa zenye kuogopesha tofauti na ilivyokuwa hapo zamani, wasafiri wanajiuliza iwapo kusafiri kwa ndege kungali salama.

      Ili kuzungumzia mahangaiko hayo, gazeti la Amkeni! liliwahoji wataalamu wa usalama, wafanyakazi kwenye viwanja vya ndege, maafisa wa mashirika ya ndege, na mafundi wa ndege. Yaonekana wote wanakubaliana juu ya jambo hili: Ijapokuwa usafiri wa ndege ungali mojawapo ya njia salama zaidi za usafiri, hatari zilizotokea hivi karibuni zinaonyesha kwamba hatua mpya zinapasa kuchukuliwa kuimarisha usalama wa wasafiri.

      Makala zinazofuata zitazungumzia matatizo yanayohusika na mambo unayoweza kufanya ili uwe salama na ustarehe zaidi unaposafiri kwa ndege.

  • Tamaa ya Kusafiri Salama kwa Ndege
    Amkeni!—2002 | Desemba 8
    • Tamaa ya Kusafiri Salama kwa Ndege

      MAJUMA machache tu kabla ya Septemba 11, 2001, Alex aliona kuwa yuko karibu kushinda woga wake wa kusafiri kwa ndege. Ndege ya abiria ilipokuwa ikianza safari toka Athens kwenda Boston, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye ni meneja wa uhusiano mwema katika kampuni yao alianza kuwa na wasiwasi—moyo wake ulianza kupiga kwa nguvu na mikono yake na uso wake ukajaa jasho.

      Lakini alijua kile alichopaswa kufanya. Mwalimu wake aliyekuwa akimsaidia kushinda woga wa kusafiri kwa ndege alikuwa amemwambia kwamba anapaswa kuvuta pumzi, kuwazia mandhari yenye kupendeza, na kushikilia kiti kwa nguvu, na kukiachilia mara nne kila dakika. Alipobabaishwa na mitikiso na makelele ya ndege, Alex aliwazia yuko kwenye pwani tulivu. Alex alisema: “Nilidhani kwamba nimefaulu sana kushinda woga wangu.”

      Mamilioni ya abiria wameogopa kusafiri kwa ndege. Katika miaka ya hivi majuzi, wengi wameshauriwa na watu wa familia, waajiri, na mashirika ya ndege waende kwenye shule za kuwasaidia watu kushinda woga wa kusafiri kwa ndege. Abiria wengi walifanya maendeleo makubwa baada ya kuhudhuria mafunzo hayo, na katika vituo vingi asilimia 90 ya waliohudhuria mafunzo hayo walifaulu kushinda woga wa kusafiri kwa ndege.

      Lakini matukio ya Septemba 11, 2001 yaliharibu mafanikio hayo. Alex aliacha kuhudhuria mafunzo hayo mara moja. Na mwajiri wake alihuzunika sana wakati Alex alipovunja mpango wa kusafiri kwa ndege ili akutane na mtu mmoja mashuhuri ambaye angekuwa mteja wao. Alex alisema hivi: “Singeweza kustahimili woga wangu wa kusafiri kwa ndege pamoja na mashambulizi ya magaidi. Mafunzo niliyopata hayakunitayarisha kukabili mambo hayo.”

      Usalama Wachunguzwa

      Wasafiri wa ndege wenye wasiwasi wanasema kwamba wateka-nyara wa Septemba 11, 2001 waliulizwa maswali yaleyale ambayo abiria huulizwa kawaida, kama vile: “Je, mtu yeyote usiyemjua amekuomba uingize kitu fulani katika ndege hii? Je, umekuwa ukiangalia mizigo yako yote tangu ulipoifungasha?” Pasipo shaka wateka-nyara hao walijibu: “La!” Baadhi ya wataalamu wa usalama wanaonelea kwamba kwa kuwa wateka-nyara hao walifaulu kuingia katika ndege ni wazi kwamba usalama katika usafiri wa ndege umepuuzwa. Jim McKenna, aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Ndege, alisema hivi: “Kabla ya tukio hilo hakuna mtu yeyote wala jambo lolote ambalo lingesababisha mabadiliko katika usalama. Lakini sasa kwa kuwa ndege nne zilitekwa nyara na kuharibiwa, na maelfu ya watu kuuawa, huenda mabadiliko yatafanywa.”

      Baada ya maafa hayo mabaya ya ndege, usalama kwenye viwanja vya ndege na ndani ya ndege umechunguzwa sana. Kwenye kikao kimoja cha kamati iliyoteuliwa na Bunge la Marekani, Kenneth M. Mead, mkaguzi mkuu katika Wizara ya Uchukuzi ya Marekani, alisema hivi: “Licha ya hatua za usalama zilizokuwapo na zile ambazo zimechukuliwa sasa, bado kuna uzembe mwingi katika usalama na hali ya usalama inapasa kuimarishwa.” Ni hatua zipi zinazochukuliwa ili kuimarisha usalama?

      Kuwakagua Wasafiri ili Kuondosha Hatari

      Afisa mkuu wa usalama katika shirika moja kubwa la ndege huko Marekani, aliulizwa iwapo anaogopa kusafiri kwa ndege, naye akasema kuwa hababaiki hata kidogo. Alisema kwamba anaamini mfumo fulani wa kompyuta wa kuwakagua wasafiri. Mfumo huo hurekodi kila tiketi iliyouzwa na mashirika ya ndege ambayo yanautumia. Mfumo huo huonyesha kama tiketi ilinunuliwa kwenye ofisi ya kuuza tiketi ya shirika la ndege, kwenye ofisi ya usafiri, au kwenye Internet. Mfumo huo hurekodi habari nyingine kama vile, iwapo mtu anasafiri peke yake au anasafiri na watu wa familia au na marafiki wengine, na vilevile iwapo amehusika katika uhalifu au amewahi kutenda mabaya kuelekea shirika hilo la ndege, wafanyakazi wake, au kuharibu mali zake.

      Kila mara abiria anaporipoti kwenye uwanja wa ndege, habari hizo huchunguzwa tena na habari mpya huongezwa, kutia ndani jinsi mtu huyo anavyojibu maswali ya ukaguzi. Habari hususa zinazokusanywa na jinsi zinavyochanganuliwa ni siri inayotunzwa sana na mashirika ya ndege. Mifumo mbalimbali kama hiyo hutumiwa ulimwenguni pote, huku mingine ikiwa imeunganishwa moja kwa moja na mashirika ya ujasusi ya kiserikali na ya kimataifa kama vile shirika la Interpol. Mifumo ya kukagua pasipoti kwenye viwanja vingi vya ndege huko Ulaya inaweza kurekodi na kuchunguza jinsi ambavyo abiria amekuwa akisafiri kutoka nchi moja hadi nyingine.

      Uchunguzi huo hufanywa kwa sababu inadhaniwa kwamba watu wenye nia mbaya ni hatari kwa usalama kuliko mizigo inayoingizwa ndani ya ndege. Kwa hiyo, ili kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege, vifaa mbalimbali vya kuwakagua watu vimeanza kutumiwa au vinachunguzwa.

      Zaidi ya kupata habari kuhusu abiria, jambo jingine muhimu linalofikiriwa ili kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege ni kuzuia vitu hatari visiingizwe ndani ya ndege. Uchunguzi unaofanywa kwa eksirei una mipaka. Wafanyakazi wa usalama kwenye viwanja vya ndege hushindwa kutazama picha za eksirei za mizigo kwa muda mrefu kwa sababu kufanya hivyo huchosha. Wakati huohuo, vifaa vinavyotambua vitu vya chuma huwapumbaza wafanyakazi hao tena na tena, kwa sababu vinatambua funguo, sarafu, na vishikizo vya mishipi.

      Sheria Kali Zaidi

      Ili kushinda vizuizi hivyo, serikali mbalimbali zimetunga sheria za kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege. Nchini Marekani sheria hizo, ambazo zinapasa kuanza kutekelezwa kufikia mwishoni mwa mwaka 2002, zinasema kwamba mizigo haitaingizwa ndani ya ndege ikiwa mwenyewe hayupo, mizigo itakaguliwa kabisa kabla ya kuingizwa ndani ya ndege, na mizigo iliyokwisha kukaguliwa itachunguzwa tena ili kuhakikisha hakuna vilipukaji vyovyote. Milango ya chumba cha rubani inaendelea kuimarishwa na kufanywa kuwa salama zaidi. Wafanyakazi wa mashirika ya ndege wanapewa mazoezi ya ziada kuhusu hali za dharura. Maafisa wa serikali wenye silaha wa kupambana na wateka-nyara wamewekwa katika ndege za abiria.

      Kwa majuma na miezi kadhaa baada ya Septemba 11, 2001, abiria walichunguzwa na mizigo ikakaguliwa kwa mkono katika viwanja vingi vya ndege ulimwenguni. Nyakati nyingine, abiria walichunguzwa mara mbili na mizigo pia ikakaguliwa mara mbili. Wasafiri huko Ulaya hawakuona jambo hilo kuwa jipya, kwani hatua kama hizo za tahadhari zilichukuliwa katika maeneo mengi huko katika miaka ya 1970 wakati utekaji nyara ulipokuwa umechacha. Sasa abiria hawaruhusiwi kuingiza vifaa vyovyote vyenye ncha kali ndani ya ndege. Wasafiri walio na tiketi pekee ndio wanaoruhusiwa kupita kwenye vituo vya ukaguzi. Sasa watu wengi wamezoea zile foleni ndefu kwenye vituo vya ukaguzi na kuwaona wanajeshi wenye silaha kwenye viwanja vya ndege.

      Umuhimu wa Kufanya Marekebisho ya Ndege Wakaziwa

      Hebu wazia tukio hili linalotukia mara kwa mara: Baada ya kupita kwenye vituo vingi vya ukaguzi kwenye uwanja wa ndege, abiria anafika mahali pa kungoja kabla ya kuingia ndani ya ndege na kumsubiri mwakilishi wa shirika la ndege atangaze kwamba ni wakati wa kupanda ndege. Kisha abiria mwingine karibu naye aliyevalia suti yenye rangi ya kijivu anamwambia: “Umesikia? Ndege itachelewa kwa sababu ya hitilafu za kimitambo.” Akiwa amevunjika moyo, abiria wa kwanza anaongeza hivi: “Natumai ndege hiyo itakuwa shwari tunapoondoka.”

      Abiria wengi hawafahamu kwamba mashirika ya ndege hutumia muda mwingi na jitihada nyingi kukagua ndege kabisa. Marekebisho yanayohitajiwa hujulikana kwa kuchunguza kitabu kinachoonyesha safari na mambo yanayoipata ndege hususa. Ama kweli, mashirika hayo husisitiza na kuhakikisha kwamba ndege na injini zinakaguliwa kabisa na kurekebishwa kulingana na ratiba ya kufanya matengenezo hata kama ndege haijawahi kuharibika. Ndege hukaguliwa na kurekebishwa mara nyingi kuliko gari.

      Afisa mmoja wa kurekebisha ndege katika shirika moja kubwa la ndege anathibitisha hilo. Anasema hivi: “Nimefanya kazi hii kwa karibu miaka 15 na sijawahi kuona wala kuzungumza na mtu yeyote anayefanya kazi ya kurekebisha ndege ambaye hachukui usalama kwa uzito sana. Isitoshe, marafiki na familia za wafanyakazi hao hutumia ndege hiyohiyo wanayorekebisha, kwa hiyo hawafanyi mambo kiholela.”

      Mafundi wa ndege wana wajibu mkubwa sana. Mmoja wao anasema: “Sitasahau usiku ule ambao ndege yetu aina ya DC-10 ilianguka huko Sioux City, Iowa. Wakati huo nilikuwa fundi wa kurekebisha mitambo ya ndege, na nilikuwa nimepewa kazi ya kukagua na kufanya marekebisho fulani kwenye sehemu ya nyuma ya ndege nyingine ya aina hiyo. Wakati huo, hatukuwa tumepokea habari za kutosha kuhusu ndege iliyoanguka. Nakumbuka kwamba usiku huo nilifanya kazi kwa makini sana, nikijiuliza, ‘Ndege hiyo ilipatwa na nini? Je, fundi mwingine alikosa kutambua kasoro fulani ambayo huenda nikiigundua sasa nitaweza kuzuia msiba mwingine kama huo? Je, ninafanya kila kitu ipasavyo?’ Jioni hiyo, nilitumia muda mrefu kwenye sehemu ya nyuma ya ndege nikifanya ukaguzi huku nikiwaza na kuwazua.”

      Mafundi wa ndege huzoezwa mara nyingi jinsi ya kushughulikia mambo yote kuhusu kazi yao, iwe ni kufanya ukaguzi wa kawaida, ukaguzi kamili, ama kugundua na kurekebisha hitilafu. Kila mwaka, mitaala ya kuwazoeza mafundi wa ndege huwa na mafunzo mapya ili kushughulikia hali zote zinazoweza kutokea, ziwe ni hali za kawaida au zisizo za kawaida.

      Ndege inapoanguka, habari zinazokusanywa huchanganuliwa na kuingizwa katika kifaa ambacho huiga hali zinazotukia wakati wa kuendesha ndege. Marubani wanaofanya majaribio ya ndege na wahandisi wa ndege hutumia kifaa hicho kutafuta masuluhisho mengine ili mafundi waweze kushughulikia vizuri matatizo kama hayo wakati ujao. Halafu, mafunzo yanayohusu matatizo hayo hupangwa ili mafundi wa ndege wapewe mwongozo hususa. Kwa kutegemea uchunguzi huo kuhusu hitilafu zinazotokea, miundo ya ndege na pia miundo ya sehemu mbalimbali za ndege hubadilishwa. Hivyo, mafundi hujifunza mambo muhimu kutokana na kasoro hizo wakitumaini kwamba habari hizo zitapunguza misiba.

      Fundi mmoja wa ndege anamalizia hivi: “Sisi huambiwa kwamba ‘usalama haujitokezi wenyewe—lazima utokezwe kupitia mpango maalumu.’”

      Kusafiri Tena kwa Ndege

      Baada ya kukataa kusafiri kwa ndege kwa miezi minne, Alex aliamua kupambana na woga wake. Ijapokuwa polisi na wanajeshi walikuwapo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Logan huko Boston, yeye hakubabaika. Hakuona ubaya wowote kupanga foleni ndefu wala mizigo yake kukaguliwa.

      Alex aliona hatua hizo kuwa dalili zenye kutia moyo kwani anatamani sana usafiri wa ndege uwe salama. Bado yeye ana wasiwasi kidogo. Hata hivyo, anapopakia mfuko wake uliokaguliwa ndani ya ndege, anasema hivi: “Sasa ninahisi afadhali zaidi.”

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      Mambo Fulani Kuhusu Usafiri wa Ndege

      Kulingana na makadirio fulani, asilimia 20 ya abiria huogopa kusafiri kwa ndege. Hata hivyo, si wote wanaona kwamba kusafiri kwa ndege ni hatari. Mara nyingi, wasiwasi wao husababishwa na mambo mengine wanayoogopa kama vile kuwa mahali palipo juu sana au katika sehemu zenye watu wengi.

      [Chati katika ukurasa wa 8]

      UWEZEKANO WA KUPATA MSIBA

      Katika mwaka Katika maisha yako

      ni 1 kati ya: ni 1 kati ya:

      Gari 6,212 81

      Mauaji 15,104 197

      Mashine 265,000 3,500

      Kuanguka kwa ndege 390,000 5,100

      Beseni ya bafu 802,000 10,500

      Wanyama na mimea yenye sumu 4.2 million 55,900

      Radi 4.3 million 56,000

      [Hisani]

      Chanzo: National Safety Council

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Usalama umeimarishwa kwenye viwanja vya ndege

      [Hisani]

      AP Photo/Joel Page

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Abiria wanachunguzwa na kukaguliwa

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Marekebisho mengi zaidi ya ndege yanafanywa

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Marubani wamepata mazoezi ya hali ya juu

  • Kuhangaikia Usalama
    Amkeni!—2002 | Desemba 8
    • Kuhangaikia Usalama

      KUSAFIRI kwa ndege kilometa 11 juu ya dunia kwaweza kuwaogopesha watu fulani. Huenda likaonekana kuwa jambo lisilopatana na sheria za asili. Kwa kuwa sasa usalama umeimarishwa na usafiri wa ndege unategemeka zaidi, hatari zinazoweza kutokea kwa kusafiri haraka ndani ya ndege zimepungua. Hata hivyo, misiba ya ndege hutukia mara mojamoja.

      Kukabiliana na Woga

      Ingawa msiba unaweza kutokea, tangu zama za kale, mwanadamu ameonyesha tamaa yake ya kusafiri hewani. Miaka elfu moja kabla ya Kristo, Mfalme Daudi aliandika hivi: “Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa! Ningeruka mbali.” (Zaburi 55:6, Biblia Habari Njema) Kama ilivyotajwa tayari, tekinolojia ya kisasa imefanya usafiri wa ndege uwe mojawapo ya njia salama zaidi za kusafiri. Lakini usafiri huo haukosi dosari. Hakuna kitu ulimwenguni kilicho salama kabisa wala kinachoweza kujulikana kimbele kwa ukamili.

      Ni muhimu kukumbuka jambo hilo iwapo tunakuwa na wasiwasi wakati mtu mwingine anapoendesha mambo. Watu wengine wanaweza kufikiri hivi, ‘Mimi mwenyewe nikiendesha shughuli fulani, wasiwasi wangu hupungua.’ Watu kama hao wanaweza kusumbuka sana wanapojipata mahali ambapo hawawezi kufanya lolote au hawana uhuru wa kudhibiti mambo. Usafiri wa ndege ni mojawapo ya hali hizo.

      Licha ya jitihada za kuimarisha usalama katika usafiri wa ndege, mtu yeyote hapaswi kuchukua mambo kimchezo. Wote wanaohusika katika usafiri wa ndege wanaweza kushirikiana kupunguza visababishi vya hatari. Na bado wenye mamlaka hutoa maonyo kuhusu hatari zilizopo. Mithali moja yenye hekima katika Biblia inasema: “Mtu mwenye busara huona hatari iliyo mbele mapema na kutahadhari.” (Mithali 22:3, New Living Translation) Ni jambo la hekima kutambua kwamba hatari fulani yaweza kutokea katika shughuli yoyote ile. Kumbuka kwamba mtu anaposafiri kwa ndege anapaswa kuchukua tahadhari zilezile za kujilinda ambazo zinahitajika katika hali nyinginezo.

      Watu ambao husafiri kwa ndege mara nyingi wanaweza kujua vizuri zaidi jinsi ya kushughulika na hali hizo ngumu. Hiyo ni kwa sababu wamezoea ndege na viwanja vya ndege kuliko abiria wengine. Wewe pia unaweza kuzoea hali hizo na kustarehe kama wao kwa kufuata hatua sahili zinazoonyeshwa kwenye masanduku yaliyo katika makala hii.

      Kusafiri Bila Wasiwasi

      Japo vituo vya ukaguzi ni muhimu, wasafiri fulani—hasa wale wenye haraka—huudhiwa navyo. Kwa kuwa usalama umeimarishwa katika viwanja vingi vya ndege, huenda ungependa kutumia madokezo yanayofuata ili usisumbuke kwenye vituo vya ukaguzi.

      ◼ Fika mapema. Kwa kupanga kufika mapema kwenye uwanja wa ndege, unaweza kufanya mambo bila haraka, kutulia, na kuepuka mfadhaiko unaoweza kutokana na hali zisizotarajiwa au hali nyingine zenye kutatiza.

      ◼ Unapochagua shirika la ndege, chagua shirika linalotumiwa hasa na wafanyabiashara. Wao wamezoea kusafiri, hawabebi mizigo mingi, na hutaka kusafiri haraka.

      ◼ Kabla ya kupita kwenye mlango wenye kifaa cha kutambua vitu vya chuma, ondoa vitu ambavyo unafikiri vitasababisha king’ora kilie. Vitu hivyo vinatia ndani funguo, sarafu, vito, na simu za mkononi. Mkabidhi mhudumu vitu hivyo unapojitayarisha kupita kwenye mlango huo.

      ◼ Laza kabisa mifuko na mizigo mingine kwenye mkanda unaochukua mizigo; mhudumu anayetazama picha za eksirei anapoona kitu kilicho shaghalabaghala, anaweza kukuambia ufungue mfuko wako au uuweke tena kwenye mkanda huo.

      ◼ Mweleze mhudumu kuhusu vitu vyovyote vya kiajabu ambavyo unadhani vitavuta fikira zake. Yaelekea hatataka kufungua mfuko wako unapomweleza vizuri kitu ulichotia mfukoni ambacho kinaonekana kikiwa na umbo la ajabu kwenye picha ya eksirei. Iwapo una haraka sana, ondoa kitu hicho mfukoni mapema na uombe kikaguliwe kwa mkono.

      ◼ King’ora kikilia, shirikiana na mhudumu na utoe maelezo bila kukawia. Iwapo mhudumu anajua kwamba kitu kimoja tu ndicho kimesababisha king’ora kilie na kuna mhudumu mwingine mwenye kifaa cha kutambua chuma ambacho hushikwa kwa mkono, atakuelekeza kwake.

      ◼ Ama kwa hakika, ukifanya mzaha kuhusu utekaji nyara au bomu, safari yako itaishia hapo. Zaidi ya kukaguliwa kabisa na maafisa wa usalama kwenye uwanja wa ndege, huenda pia ukashtakiwa.

      Safiri Salama!

      Je, inawezekana kuchagua ndege salama? Ndiyo. Hata ukichagua kusafiri kwa ndege yoyote ile, kuna uwezekano mkubwa sana wa kuwasili salama salimini. Ukiwa na shaka, chunguza rekodi za usalama za shirika la ndege unalotaka kutumia. Kumbuka kwamba ijapokuwa misiba ya ndege hutokea, usafiri wa ndege ungali mojawapo ya njia salama zaidi za kusafiri.

      Kwa sasa, sote tunaweza kutarajia wakati ambapo kutakuwa na usalama na hali ya kuaminiana chini ya utawala wa Mungu juu ya dunia. Katika jamii ya wanadamu yenye amani na inayomhofu Mungu, watu wanaohatarisha uhai wa wanadamu hawatakuwapo. Watu “watakuwa salama salimini bila hofu ya msiba.”—Mithali 1:33, Holy Bible—Contemporary English Version.a

      [Maelezo ya Chini]

      a Ili upate habari nyingine zinazohusiana na hizi ona makala “Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi,” Amkeni!, Septemba 22, 2000; “Safiri Salama!” Amkeni!, Septemba 8, 2000; “Ni Nini Kinachohusika ili Ziendelee Kusafiri Angani?” Amkeni!, Septemba 8, 1999; “Ndege Ni Salama Kadiri Gani?” Amkeni!, Machi 8, 1999.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10, 11]

      MADOKEZO FULANI KUHUSU USALAMA

      Safiri kwa ndege inayoenda moja kwa moja bila kutua kwenye viwanja mbalimbali. Misiba mingi hutokea wakati ndege inapoanza safari, inapopaa, inaposhuka, au kutua. Kusafiri kwa ndege inayoenda moja kwa moja bila kutua kwenye viwanja mbalimbali kutapunguza hatari hizo.

      Chagua ndege kubwa. Kwa kawaida ndege inayoweza kubeba zaidi ya abiria 30 huundwa na kukaguliwa kulingana na viwango vya juu kuliko ndege ndogo. Pia, ijapokuwa uwezekano wa kupata msiba mkubwa ni mdogo sana, ni rahisi zaidi kwa abiria wa ndege kubwa kuokoka.

      Sikiliza kwa makini madokezo yanapotolewa kabla ya safari kuanza. Ijapokuwa huenda ikawa umesikia madokezo hayo mara nyingi, milango ya dharura iliyo karibu nawe inaweza kuwa mahali tofauti kabisa ikitegemea ndege unayotumia au mahali kiti chako kilipo.

      Usiweke vitu vizito kwenye sehemu ya mizigo iliyo juu yako. Huenda sehemu za kuwekea mizigo zilizo juu yako zisiweze kuhimili vitu vizito sana kunapotokea msukosuko angani, kwa hiyo iwapo unabeba kitu kizito, acha kiwekwe pamoja na ile mizigo mingine mapema.

      Funga mkanda wa usalama unapoketi. Kufunga mkanda wa usalama unapoketi kutakukinga endapo ndege itakumbwa na msukosuko wa ghafula angani.

      Wasikilize wahudumu wa ndege. Wahudumu wa ndege huwa ndani ya ndege hasa kwa sababu ya usalama, kwa hiyo mmoja wao akikuambia ufanye jambo fulani, tii mara moja, ukiwa na maswali muulize baadaye.

      Usibebe kitu chochote hatari. Kuna vitu vingi hatari ambavyo haviruhusiwi, lakini hata wewe mwenyewe unajua kwamba haifai kubeba petroli, kemikali au asidi kali, gesi zenye sumu, na vifaa vingine kama hivyo katika ndege isipokuwa uwe umepewa ruhusa na shirika la ndege na viwe vimepakiwa katika kontena inayofaa.

      Usinywe kileo kupita kiasi. Kileo huathiri mtu zaidi anapokuwa ndani ya ndege kuliko anapokuwa ardhini. Kuwa na kiasi ni muhimu kila mahali.

      Uwe chonjo. Japo si rahisi kutokee hali ya dharura, hali kama hiyo ikitokea, kama vile abiria wakihitaji kuhamishwa haraka ili kuepuka hatari, fuata maagizo ya wahudumu wa ndege na wafanyakazi wengine na uondoke katika ndege haraka iwezekanavyo.

      [Hisani]

      Chanzo: AirSafe.com

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

      KUWATULIZA WATU WA FAMILIA YAKO

      Madokezo yafuatayo yanaonyesha jinsi unavyoweza kuwasaidia watu wa familia yako wasiwe na wasiwasi unaposafiri. Yametolewa kwenye kituo cha Internet cha United Behavioral Health

      Zungumza na watu wa familia yako. Kabla ya kwenda safarini, tumia muda fulani pamoja na wapendwa wako ili mzungumzie usalama wako na vilevile usalama wao. Eleza hatua mpya ambazo zimechukuliwa kuimarisha usalama na jinsi zinavyochangia usalama wako unaposafiri.

      Acha waeleze mahangaiko yao. Acha watu wa familia yako waeleze wasiwasi wao. Wanakupenda na wanataka tu uwe salama. Sikiliza kwa makini bila kuwachambua, na uchukue mahangaiko yao kwa uzito.

      Wape uhakikisho wa kweli. Zungumzia jinsi ambavyo mashirika mbalimbali yanajaribu kuzuia mashambulizi mengine ya magaidi. Hiyo inatia ndani hatua zaidi za kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege na ndani ya ndege. Uwezekano wa msiba kutokea unaposafiri kwa ndege ni mdogo sana.

      Endelea kuwasiliana nao. Waahidi kuwa utawapigia simu utakapofika. Endelea kupiga simu nyumbani kwa ukawaida kwa muda ambao utakuwa safarini. Pia, ni muhimu familia yako ijue namna ya kuwasiliana nawe endapo hali za dharura zitatokea.

      [Hisani]

      Taken from the United Behavioral Health Web site

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Uwe tayari kushirikiana na wahudumu kwenye vituo vya ukaguzi

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki