-
Mitazamo Inayobadilika Yazusha Maswali MapyaAmkeni!—1997 | Juni 8
-
-
Mitazamo Inayobadilika Yazusha Maswali Mapya
“MVUVUMKO WA KUFANYA NGONO OVYOOVYO,” “ongezeko kubwa la kufanya ngono,” “mvuvumko wa kiadili.” Semi kama hizo zilitangaza mitazamo iliyobadilika kuelekea mwenendo wa kingono, hasa katikati ya miaka ya 1960 na baadaye. Wengi walipendelea ile shime isemayo “uhuru wa kufanya mapenzi,” ambayo ilikuwa mtindo-maisha uliofanya watu wakatae ndoa na ubikira.
Usemi wa mtungaji Ernest Hemingway, “Tendo la adili ni lile linalokufanya uhisi vizuri, na tendo lisilo la adili ni lile linalokufanya uhisi vibaya,” waweza kufafanua vizuri mtazamo wa wale walionaswa na uvutio wa uhuru wa kufanya ngono na kuridhika. Kukubali falsafa hiyo kulifanya wengi waone kwamba ni sawa kuwa na mahusiano ya muda mfupi-mfupi ya kingono pamoja na wenzi kadhaa, ambamo watu, waume kwa wake, walijaribu kutosheleza tamaa zao za kingono. ‘Uradhi’ wa kingono ukakosa mpaka. Vibonge vya kudhibiti uzazi, vilivyotokea katika mwongo huohuo, vilichangia kule kufanya ngono zaidi kusiko na mipaka.
Lakini, UKIMWI na maradhi mengine yanayopitishwa kingono yakawa matokeo ya mtindo-maisha wa kufanya ngono ovyoovyo. Mitazamo ya kingono ya kizazi kilegevu ilitikiswa kwelikweli. Miaka fulani iliyopita, gazeti Time lilikuwa na kichwa hiki kikuu “Ngono Katika Miaka ya 1980—Ule Mvuvumko Umekwisha.” Tangazo hilo lilitegemea hasa wingi wa maradhi ya kupitishwa kingono ambayo yalikuwa yameathiri Wamarekani wengi. Kufikia wakati huu, jumla ya visa vya UKIMWI ulimwenguni pote imefikia kiwango chenye kushtusha sana cha karibu watu milioni 30!
Hofu ya maradhi yanayopitishwa kingono ilitokeza badiliko jingine katika mitazamo ya watu wengi kuhusu kuwa na mahusiano ya muda mfupi-mfupi ya kingono. Toleo la 1992 la gazeti la burudani liitwalo US, likiripoti juu ya uchunguzi wa serikali, lilisema hivi: “Wanawake waseja wapatao milioni 6.8 wamefanya mabadiliko katika mwenendo wao wa kingono kwa sababu ya kuhofu UKIMWI na maradhi mengine yanayopitishwa kingono.” Kulingana na makala hiyo, ujumbe u wazi: “Ngono si jambo la kuchezea-chezea. Kufanya ngono ni hatari.”
Miongo hii yenye msukosuko imeathirije mitazamo kuelekea mahusiano ya kingono? Je, kuna somo lolote ambalo watu wamejifunza kutokana na kufanya mapenzi kiholela ambako kumekuwapo katika miongo ya majuzi na pia somo kutokana na kuzuka kwa maradhi ya kupitishwa kingono katika miaka ya 1980? Je, kuanzishwa kwa masomo ya ngono katika shule za umma kumesaidia vijana wa kiume na wa kike kukabiliana vema na mwenendo wa kingono? Ni ipi njia bora zaidi ya kukabili mitazamo inayobadilika kuelekea mwenendo wa kingono?
-
-
Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?Amkeni!—1997 | Juni 8
-
-
Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?
MIAKA ipatayo 2,700 iliyopita, mwandikaji aliyepuliziwa aliandika methali hii yenye kuchochea fikira: “Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo.” (Mithali 10:23) Ukweli wa jambo hili umeonekana hasa tangu mvuvumko wa ngono ovyoovyo. Kabla ya tisho la UKIMWI, mtazamo ulioenea ulikuwa kwamba ngono ni ‘mchezo wa raha’ na kwamba tamaa ya ngono ni lazima itoshelezwe ‘bila kujali matokeo.’ Je, mtazamo huo umebadilika? Sivyo hasa.
Leo, ashiki ya kingono bado hutokeza “waraibu wa mapenzi,” ‘watu wenye kufunga mfululizo wa ndoa,’ na “waoteaji wa kingono,” ambao hubisha kwamba maadili ni mambo ya mtu binafsi na kwamba kufanya ngono na watu tofauti-tofauti ni jambo la kawaida. (Ona sanduku “Mitindo-Maisha ya Kingono,” kwenye ukurasa wa 6.) Wao wadai kwamba ‘hakuna mtu anayeumizwa’ kwa kufanya ngono na mtu yeyote yule, maadamu ni watu wazima ambao wamekubaliana. Katika 1964, mwanasoshiolojia wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa, Ira Reiss alifafanua hali hiyo kuwa “uendekevu wenye mapenzi.”
Askofu wa Anglikana wa Edinburgh, Scotland, aonekana kuhisi hivyo, kwani alisema kwamba wanadamu waliumbwa ili wawe na wapenzi wengi. Katika hotuba juu ya ngono na Ukristo, yeye alisema: “Mungu alipotuumba alijua kwamba ametupatia tamaa ya kufanya ngono ili tupande mbegu zetu. Ametupatia urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo. Nafikiri ni vibaya kwa kanisa kushutumu watu ambao wamefuata silika zao.”
Je, hayo ni maoni mazuri? Kuna hasara gani ya kufanya ngono kiholela? Je, mahusiano ya muda mfupi-mfupi pamoja na wenzi tofauti-tofauti wa kingono yaweza kuridhisha na kuleta furaha?
Mweneo wa duniani pote wa maradhi yanayopitishwa kingono na uhalisi wa mamilioni ya mimba zinazopatikana nje ya ndoa, hasa miongoni mwa matineja, huthibitisha kwamba falsafa hiyo haifai. Kulingana na gazeti Newsweek, katika Marekani pekee, maradhi yanayopitishwa kingono huambukiza matineja wapatao milioni tatu kila mwaka. Isitoshe, wengi wa hao “watu wazima wanaokubaliana” waonekana kama hawana “shauku ya asili” au kuona wajibu wao kwa yule mtoto asiyezaliwa bado ambaye mara nyingi ndiye matokeo, nao upesi wao hujaribu kutoa mimba. (2 Timotheo 3:3) Jambo hilo hufanya mtoto asiyezaliwa bado apoteze uhai wake, anapoondolewa kikatili kutoka kwa mamake. Hasara kwa mama mchanga yaweza kuwa ni kushuka moyo sana na pia hatia ambayo inaweza kumlemea maisha yake yote.
Katika miaka ya katikati ya 1990 katika Uingereza pekee, gharama za kifedha kwa athari za mvuvumko wa ngono ovyoovyo zilikuwa za kiwango cha kushtusha cha dola bilioni 20 kila mwaka, kulingana na hesabu ya Dakt. Patrick Dixon. Katika kitabu chake The Rising Price of Love, Dakt. Dixon alifikia hesabu hiyo kwa kuhesabu gharama za kutibu maradhi yanayopitishwa kingono, kutia ndani UKIMWI; gharama za talaka; gharama kwa jumuiya ya mzazi mmoja kulea watoto; na gharama za tiba ya familia na mtoto. Kama ilivyoripotiwa katika The Globe and Mail, gazeti la kila siku la Kanada, Dakt. Dixon amalizia: “Mvuvumko wa mahusiano ya ngono ovyoovyo ambao ulituahidi uhuru umetia wengi utumwani, katika ulimwengu ulioharibiwa na ngono za kiholela, misiba, upweke, maumivu ya kihisia-moyo, ujeuri na kutendwa vibaya.”
Lakini ni kwa nini watu bado wana ashiki sana ya kingono, wanapendelea mahusiano ya muda mfupi-mfupi, na kusisitiza kufanya mapenzi kiholela bila kutaka kuwajibika? Kukiwa na matunda mabaya ya wazi kama hayo katika miongo mitatu ambayo imepita, ni nini kinachochochea ashiki hiyo yenye kusababisha uharibifu?
Ponografia Yapotosha Ngono
Ponografia imetajwa kuwa jambo moja linalochochea ashiki ya kingono. Mtu mmoja aliyekiri kuwa mraibu wa ngono aandika hivi katika gazeti The Toronto Star: “Niliacha sigareti miaka mitano iliyopita, kileo miaka miwili iliyopita, lakini maishani mwangu hakuna jambo ambalo limenishinda kuacha kuliko uraibu wangu wa ngono na ponografia.”
Pia amesadiki kwamba matineja ambao wanajihatarisha kwa kutazama kwa ukawaida ponografia husitawisha maoni mabaya juu ya mwenendo wa kingono. Wao huiga fantasia zao za kingono na kupata kwamba mahusiano halisi ni yenye kutatanisha na magumu. Hilo hutokeza upweke na matatizo mengine, ambalo tatizo kubwa ni kufanyiza vifungo vyenye kudumu vya upendo.
Vitumbuizo Huonyesha Vibaya Ngono
Mitindo-maisha ya kufanya ngono ovyoovyo na wenzi tofauti-tofauti, wawe wamefunga ndoa au la, imependelewa sana na kuonyeshwa waziwazi katika vitumbuizo. Maonyesho yenye kushusha hadhi ya mwenendo wa kingono usio na upendo yanayoonyeshwa kwenye televisheni huchochea ashiki ya kingono, yakifanya kizazi hiki kiwe na maoni yaliyopotoka juu ya mwenendo wa kingono wa kibinadamu. Vyombo vya vitumbuizo mara nyingi huhusianisha isivyofaa ngono ya nje ya ndoa na ukaribu wenye upendo. Mashabiki wa watu mashuhuri katika vitumbuizo hawaonekani kama wanaweza kutambua tofauti zilizopo kati ya kuwaka tamaa kingono na upendo, kati ya mahusiano ya muda mfupi-mfupi wa kimapenzi na uwajibikaji wa muda mrefu, au kati ya fantasia na uhalisi.
Vilevile, mara nyingi zaidi matangazo ya biashara yameonyesha vibaya ngono yanapotangaza bidhaa. Ngono imekuwa “chombo cha kunasa akili kwenye bidhaa inayotangazwa,” akasema mwanatiba wa ngono. Watangazaji wa kibiashara wametumia vibaya ngono nao wameshirikisha maonyesho ya kingono na maisha mazuri, lakini huu ni “upotovu [mwingine] wa maoni ya kingono” wa karne ya 20, kama lisemavyo jarida Family Relations.
Kubadilika kwa Hali Hubadili Mitazamo
Kubadilika kwa mazingira ya kijamii na kutokezwa kwa vibonge vya kudhibiti uzazi katika masoko mwaka wa 1960 kulibadili tabia ya kingono ya mamilioni ya wanawake. Vibonge hivyo vilifanya wanawake waone kwamba walikuwa sawa kingono na wanaume, vikawapa uhuru wa kingono au ujitegemezo ambao hawakupata kamwe kuwa nao hapo awali. Kama ilivyo na wanaume, wao sasa waliweza kuwa na mahusiano ya muda mfupi-mfupi, bila woga wa kushika mimba zisizotakiwa. Wakijitosa katika shamrashamra za kufanya ngono kwa uhuru, wote wanaume na wanawake walitupilia mbali madaraka yao ya kawaida ya kifamilia na ya kingono.
Mwandikaji mmoja wa Biblia wa karne ya kwanza alisema hivi juu ya watu kama hao: “Wana macho yenye kujaa uzinzi na yasiyoweza kuachana na dhambi . . . Wana moyo uliozoezwa katika kutamani. . . . Wakiacha pito lililo nyoofu, wameongozwa vibaya.”—2 Petro 2:14, 15.
Mafunzo ya Ngono Shuleni
Uchunguzi mmoja wa Marekani uliofanyiwa wanawake waseja wapatao 10,000 wenye umri wa kwenda shule za sekondari ulifunua kwamba “ujuzi, kama uonyeshwavyo na mitaala ya mafunzo ya ngono na ujuzi juu ya vibonge vya kudhibiti uzazi ambao matineja husema wanao,” haukuathiri kiwango cha matineja kushika mimba nje ya ndoa. Hata hivyo, baadhi ya shule za umma zinakabili mweneo huo mkubwa wa matineja kushika mimba kwa kuwapa wanafunzi kondomu bila malipo, ingawa hatua hiyo inabishaniwa vikali.
Mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 17 wa shule ya sekondari aliyehojiwa na gazeti la habari Calgary Herald alisema hivi: “Ni kweli kwamba wengi wa matineja katika shule za sekondari wanafanya ngono . . . , hata baadhi ya wale wenye umri wa miaka 12.”
Upendo na Uwajibikaji Ni Nini?
Upendo, tumaini, na uandamani wenye kutamaniwa si matokeo ya moja kwa moja ya uvutio wa ghafula wa kingono wala si matokeo ya kujitosheleza kingono. Kufanya ngono kwenyewe hakuwezi kutokeza upendo wa kweli. Upendo na ukaribiano hutokezwa na mioyo miwili ya watu wawili wenye kujali ambao wanataka kujenga uhusiano wa kudumu.
Mahusiano ya muda mfupi-mfupi hatimaye hayampi mtu usalama, humfanya awe mpweke, na labda kumwambukiza maradhi ya kupitishwa kingono kama vile UKIMWI. Wateteaji wa mapenzi ya kiholela waweza kufafanuliwa na maneno yapatikanayo kwenye 2 Petro 2:19: “Huku wao wakiwaahidi uhuru, wao wenyewe wanakuwako wakiwa watumwa wa ufisadi. Kwa maana yeyote yule anayewezwa na mwingine hufanywa mtumwa na huyu.”
Kamati ya Kanisa la Uingereza yenye kushughulikia uwajibikaji wa kijamii ilitoa ripoti katika Juni 1995, yenye kichwa “Jambo la Kusherehekewa.” Tofauti kabisa na shauri la Biblia, kamati hiyo ilihimiza kanisa “lifute maneno yasemayo ‘kuishi katika dhambi’ na liache kuhukumu-hukumu wale ambao wanaishi pamoja bila kufunga ndoa,” kulingana na The Toronto Star. Ripoti hiyo ilipendekeza kwamba “makutaniko yapaswa kukaribisha wale wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa, wawasikilize, wajifunze kutokana nao, . . . ili kwamba wote waweze kugundua kuwapo kwa Mungu katika maisha zao.”
Yesu angewaitaje viongozi wa kidini kama hao? Bila shaka “viongozi vipofu.” Na vipi juu ya wale wanaofuata miongozo kama hiyo? Yeye alisababu hivi: “Basi, ikiwa kipofu aongoza kipofu, wote wawili wataanguka ndani ya shimo.” Kwa hakika, Yesu alisema waziwazi kwamba “uzinzi” na “uasherati” ni miongoni mwa mambo “yanayotia mtu unajisi.”—Mathayo 15:14, 18-20.
Kukiwa na mambo haya kadhaa yanayopotosha na kuonyesha vibaya ngono, mtu anaweza, hasa vijana, kuachaje ashiki ya kingono? Ni nini siri ya kuwa na mahusiano ya muda mrefu yenye furaha? Makala ifuatayo itakazia kile ambacho wazazi waweza kufanya ili kusaidia vijana kujitayarisha kwa ajili ya wakati ujao.
-
-
Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?Amkeni!—1997 | Juni 8
-
-
Mitindo-Maisha ya Kingono
Waraibu wa Mapenzi: Wao hupenda kushikwa na mapenzi, kwa hiyo wao huanzisha mapenzi na watu tofauti-tofauti mara tu msisimko wa mahaba yao upoapo. Maneno ya Kiingereza, attraction junkies, yamaanishayo waraibu wa mapenzi, yalibuniwa na Dakt. Michael Liebowitz, wa New York State Psychiatric Institute.
Watu Wenye Kufunga Mfululizo wa Ndoa: Watu ambao hupitia mahusiano mengi ya mapenzi yanayohusisha mambo ya kisheria ya ndoa, talaka, na ndoa nyingine huitwa hivyo na wanasoshiolojia.
Waoteaji wa Kingono: Wao hutafuta kuonyesha uwezo wao wa kufanya ngono kwa kuwa na wenzi wengi, aonelea Luther Baker, profesa wa uchunguzi wa familia aliye pia mtaalamu wa ngono. Neno hilo sasa latumiwa kumaanisha wasumbuaji wa watoto kingono.
-
-
Kuukabili Huo UgumuAmkeni!—1997 | Juni 8
-
-
Kuukabili Huo Ugumu
MASHAMBULIO dhidi ya maadili ya kingono huanza mapema maishani kwa sababu ya kupatikana kwa televisheni, vitabu, magazeti, sinema, na muziki ambao huonyesha ngono. Vijana huhimizwa kuwa na tabia za kingono za watu wazima ingawa wao si imara kihisia-moyo. Wazazi wengine hata huongezea msongo wa kingono kwa kuruhusu miadi ya kijinsia katika umri mchanga. Msongo wa marika hutia moyo kufanya miadi ya kijinsia, na vijana wengi ambao wana marafiki wa jinsia tofauti wenye kutegemeka hujiachilia na kuanza kufanya ngono. “Ni kawaida kama nini . . . kwa msichana tineja ambaye anahisi hapendwi na wazazi wake . . . kuanza kukumbatiana kimapenzi na rafiki yake mvulana kwa kudhani kimakosa kwamba kufanya hivyo kutamfanya apendwe na awe na rafiki wa karibu sana,” asema Luther Baker, profesa wa chunguzi za familia.
Vijana huelekea kuishi miaka ya ubalehe kana kwamba huo ndio mwisho wa maisha zao badala ya kuishi kana kwamba ndiyo matayarisho ya maisha. “Wakiwa wamewaka kwa uwezo wao mpya wa kingono na kusadikishwa na marika kwamba uwezo wa kingono ndio uanamume, vijana wengi wamekuwa waoteaji wa kingono” katika ubalehe wao, asema Profesa Baker. Miaka ipatayo 30 iliyopita, mwanahistoria Arnold Toynbee aliomboleza juu ya hila inayofanyiwa vijana wetu, kwa kuwa aliamini kwamba historia imeonyesha kwamba sababu moja inayofanya nchi za Magharibi ziwe na akili ni ule uwezo wa kuahirisha ‘utendaji wa kingono’ wa wabalehe ili wazingatie kupata ujuzi.
Wazazi Ambao Wana Uvutano Mzuri
Wazazi ambao hawaruhusu wabalehe kufanya miadi ya kijinsia ya kujifurahisha huonyesha hangaiko zuri kwa afya na furaha ya wakati ujao wa watoto wao. Kwa kuwa na viwango vya juu vya maadili na kudumisha uwasiliano mzuri, wao waweza kuwa na uvutano katika maisha za watoto wao. Utafiti unaochunguza tabia za kingono za vijana waonyesha kwamba “uvutano huo waweza kufanya watoto waahirishe utendaji wa kingono,” kulingana na Journal of Marriage and the Family.
Wazazi ambao huwatia watoto nidhamu na kuwafanya kuwa wenye madaraka hupata matokeo bora zaidi. “Wabalehe na wazazi wao wakiwa na maadili yenye kukazia kuwajibika, uwezekano wa wabalehe kushika mimba kabla ya ndoa hupunguka sana,” uchunguzi mmoja wathibitisha. Jambo hilo hutaka wazazi wafahamu utendaji wa watoto wao—wakichunguza mgawo wao wa masomo ya nyumbani; wakijua mahali walipo na pia washiriki wao; wakiwawekea miradi iwezayo kutimizwa; na kuwafundisha mambo ya kiroho. Watoto wanaokua wakiwa na uwasiliano wa karibu na wazazi wao watajihisi vizuri zaidi na hawatahangaikia mwenendo wao wa kingono.
Shauri bora zaidi kwa wazazi na watoto ni hekima ipatikanayo katika Biblia. Wazazi katika Israeli waliamriwa wafundishe watoto wao maadili. Yehova aliwauliza: “Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo”? Ni hizi ‘amri zenye haki’ ambazo walipaswa kufundisha watoto wao katika hali changamfu na ya upendo ya kifamilia. “Uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.” Watoto walihimizwa: “Shika maagizo ya baba yako, wala usiiache sheria ya mama yako.” Uwasiliano mchangamfu wenye ukaribu kama huo na mafundisho ya baba na mama ndiyo yanayojenga katika watoto wao mtazamo wenye usawaziko kuelekea maisha na mwenendo wa kingono, ambao ‘utamlinda’ kijana maishani mwake mwote.—Kumbukumbu la Torati 4:8; 6:7; Mithali 6:20, 22.
Vijana, kwa nini mharibu wakati wenu ujao kwa kushindwa na tamaa za kingono? Miaka ya utineja ni karibu saba. Miaka hiyo inapasa kutumiwa kukua kiakili, kihisia-moyo, na kiroho na kusitawisha mtazamo wenye usawaziko kuhusu mwenendo wa kingono, katika matayarisho ya miaka ijayo 50 au 60 ya maisha. Wazazi, chukueni madaraka yenu mliyopewa na Mungu kwa uzito, na mlinde watoto wenu wasipatwe na majonzi moyoni yanayoletwa na maradhi yanayopitishwa kingono na mimba zisizotakiwa. (Mhubiri 11:10) Acheni watoto wenu waone katika maisha zenu za kila siku jinsi upendo na ufikirio kwa wengine hujenga mahusiano yenye kudumu.
Kuukabili kwa Mafanikio Huo Ugumu
Usiruhusu ashiki ya kingono ambayo imeenea iharibu maoni yako juu ya maisha na kuharibu fursa yako ya kuwa na wakati ujao wenye kuridhisha na wenye furaha. Tafakari juu ya vielelezo vingi vya mahusiano ya kibinadamu katika Biblia. Uwe na hakika kwamba maisha na upendo hudumisha uchangamfu muda mrefu baada ya miaka ya utineja. Uhalisi huu unapofikiriwa kwa uzito kwa kupatana na mapenzi ya kimungu kwa wanaume na wanawake Wakristo, basi msingi unawekwa kwa ajili ya muungano wenye upendo na wenye kudumu kati ya watu wawili ambao wamependana.
Uchunguzapo wenzi wanaotajwa katika Biblia kama vile Yakobo na Raheli, Boazi na Ruthu, pamoja na yule kijana mchungaji na msichana Mshulami, utaona kwamba walikuwa na uvutano fulani wa kingono katika mahusiano yao. Lakini, usomapo kwa uangalifu Mwanzo sura ya 28 na ya 29, kitabu cha Ruthu, na Wimbo Ulio Bora, utaona kwamba kulikuwa na mambo mengine muhimu zaidi ambayo huboresha mahusiano hayo.a
Kubali Maandalizi ya Yehova kwa Ajili ya Uhai
Yehova, Muumba wa jamii ya wanadamu, huelewa mwenendo wa kingono wa wanadamu na tamaa zihusikazo. Kwa upendo, ametuumba katika sura yake, si tukiwa na “urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo,” lakini tukiwa na uwezo wa kudhibiti hisia zetu kwa kupatana na mapenzi ya kimungu. “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu, . . . kwamba mjiepushe na uasherati; kwamba kila mmoja wenu apaswe kujua jinsi ya kupata umiliki wa chombo chake mwenyewe katika utakaso na heshima, si katika hamu yenye tamaa ya ngono kama ile waliyo nayo pia mataifa wale wasiomjua Mungu; kwamba yeyote asifikie hatua ya kudhuru na kuziingilia haki za ndugu yake katika jambo hilo.”—1 Wathesalonike 4:3-6.
Jambo hilo ladhihirishwa na Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Wao hustahi viwango vya juu vya Mungu kwa wanaume na wanawake Wakristo. Wanaume wazee wanaonwa kama baba, “wanaume vijana zaidi kama ndugu, wanawake wazee zaidi kama mama, wanawake vijana zaidi kama dada kwa usafi wote wa kiadili.” (1 Timotheo 5:1, 2) Hayo ni mazingira yafaayo kama nini kwa wanaume na wanawake wachanga kufurahia wafikiapo uwezo wao kamili, bila misongo ya kufanya miadi ya kijinsia na kufunga ndoa kabla ya wakati ufaao au bila maradhi yanayopitishwa kingono! Familia ya Kikristo yenye utendaji, ikiwa imeimarishwa na kutaniko la Kikristo, ni mahali salama katika ulimwengu wenye kichaa cha ngono.
Kwa kutumia kanuni za Biblia maishani mwao, vijana Wakristo hawana ashiki ya kingono nao hupata shangwe katika kutii himizo hilo linalotolewa na Neno la Mungu: “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.”—Mhubiri 11:9, 10.
-