Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania
    Amkeni!—2007 | Agosti
    • Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania

      NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

      ZAIDI ya miaka mia nne iliyopita, vikosi viwili vya wanamaji vilipigana katika Mlango-Bahari wa Uingereza. Vita hivyo kati ya Waprotestanti na Wakatoliki vilikuwa sehemu ya mapambano yaliyotokea katika karne ya 16 kati ya majeshi ya Malkia Mprotestanti Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza na Mfalme Mkatoliki Philip wa Pili wa Hispania. Kitabu The Defeat of the Spanish Armada kinaeleza hivi: “Kwa maoni ya watu waliokuwa wakiishi wakati huo, vita hivyo kati ya majeshi ya wanamaji wa Uingereza na Hispania katika Mlango-Bahari wa Uingereza vilikuwa mapambano ya kufa na kupona kati ya majeshi ya nuru na majeshi ya giza.”

      Watu waliokuwa wakiishi Uingereza wakati huo wanafafanua Manowari za Hispania kuwa “jeshi kubwa zaidi la wanamaji kusafiri baharini.”

  • Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania
    Amkeni!—2007 | Agosti
    • Jeshi Kubwa Lililo Gumu Kuongoza

      Philip alimweka rasmi Dyuki wa Medina-Sidonia awe kamanda wa Manowari hizo. Ingawa Dyuki huyo hakuwa na ujuzi wa kuongoza majeshi ya majini, alikuwa na uwezo mzuri wa kupanga mambo na muda si muda, makapteni wake wenye ujuzi walifurahia kumuunga mkono. Pamoja, waliunda kikosi cha vita na kutafuta maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kikosi hicho kikubwa. Walikubaliana kuhusu ishara watakazotumia kuwasiliana, mpangilio wa kusafiri, na mbinu ya kudumisha umoja katika jeshi lao la kimataifa.

      Wakitumia meli 130 zilizokuwa na askari 20,000 hivi na mabaharia 8,000, waliondoka mji wa Lisbon Mei 29, 1588 (29/5/1588). Lakini upepo mkali wa dhoruba uliwafanya watue huko La Coruña, kaskazini-magharibi mwa Hispania, ili wafanye ukarabati na kuongeza bidhaa nyingine. Akiwa na wasiwasi kuhusu chakula, maji, na afya ya askari wake, Dyuki wa Medina-Sidonia alimwandikia mfalme waziwazi kuhusiana na mashaka yake juu ya safari hiyo. Lakini Philip alisisitiza kwamba kamanda wake aendelee na safari kama walivyokuwa wamepanga. Kwa hiyo Manowari hizo ziliendelea na safari, na miezi miwili baada ya kutoka Lisbon zikafika Mlango-Bahari wa Uingereza.

      Vita Kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza

      Majeshi ya Wahispania yalipofika kwenye pwani ya Plymouth, huko kusini-magharibi mwa Uingereza, majeshi ya Waingereza yalikuwa yakingoja. Pande zote mbili zilikuwa na idadi inayolingana ya meli lakini muundo wa meli hizo ulitofautiana. Meli za Hispania zilikuwa ndefu na kwenye sitaha kulikuwa na bunduki za masafa mafupi. Kulikuwa na minara kwenye omo na tezi iliyofanya zifanane na minara iliyoelea. Wanajeshi Wahispania walitaka kutumia mbinu ya kuwakaribia maadui na kuwavamia. Nazo meli za Waingereza zilikuwa fupi na zilienda kwa kasi zikiwa na mizinga ya masafa marefu. Makapteni wao walitaka kuepuka kukaribia maadui na hivyo waangamize meli za Wahispania kutoka mbali.

      Ili kukabiliana na wepesi na mizinga ya meli za Uingereza, kamanda wa Manowari za Hispania alipanga meli hizo kwa umbo la nusu mwezi. Meli zenye nguvu zilizokuwa na bunduki za masafa marefu zililinda miisho yote. Kwa hiyo, hata maadui wakitokea upande upi, Manowari hizo zingegeuka na kukabiliana nao kama vile nyati anavyoelekeza pembe zake kuelekea simba anayemkaribia.

      Majeshi hayo mawili yalizozana-zozana kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza na yakapigana vita viwili vidogo. Mpangilio huo wa meli za Wahispania uliwasaidia, na mizinga ya masafa marefu ya Waingereza haikuweza kuizamisha meli yoyote ya Wahispania. Makapteni Waingereza walikata kauli kwamba lazima wavunje mpangilio huo na kuwakaribia. Walipata nafasi hiyo Agosti (Mwezi wa 8) 7.

      Dyuki wa Medina-Sidonia alifuata maagizo aliyopewa na kuelekeza Manowari zake hadi mahali walipopaswa kukutana na Dyuki wa Parma na vikosi vyake. Dyuki wa Medina-Sidonia alipokuwa akisubiri ujumbe kutoka kwa Dyuki wa Parma, aliamrisha meli zake zitie nanga kwenye pwani ya Ufaransa huko Calais. Meli za Hispania zikiwa zimetia nanga na hivyo kukabili hatari ya kushambuliwa kwa urahisi, Waingereza walituma meli nane ambazo walizijaza vitu vinavyoweza kulipuka na kuziwasha. Makapteni wengi Wahispania walijaribu kurudi baharini ili waziepuke meli hizo. Kisha upepo mkali na mikondo ya bahari iliwasukuma upande wa kaskazini.

      Jua lilipochomoza siku iliyofuata, vita vya mwisho vilipiganwa. Majeshi ya Waingereza yalivamia meli za Wahispania kutoka karibu, na meli tatu hivi ziliteketezwa na nyingine nyingi zikaharibiwa kwa kiasi fulani. Kwa sababu Wahispania hawakuwa na silaha za kutosha, walivumilia uvamizi huo.

      Dhoruba kali iliwafanya Waingereza waache kupigana hadi siku iliyofuata. Asubuhi hiyo, Wahispania walijipanga tena katika umbo la nusu mwezi, na wakiwa na silaha chache walijitayarisha kupigana na maadui wao. Lakini kabla ya Waingereza kushambulia, meli za Wahispania zilisukumwa na upepo na mikondo na kukwama kwenye vilima vya mchanga huko Zeeland karibu na pwani ya Uholanzi.

      Ilipoonekana kwamba hawana matumaini yoyote, upepo uliwasukuma kaskazini kwenye bahari ambapo walikuwa salama. Lakini hawangeweza kurudi hadi Calais kwani meli za Waingereza zilikuwa zimefunga njia, na upepo mkali bado ulikuwa unasukuma meli za Wahispania zilizokuwa zimeishiwa nguvu kaskazini. Dyuki wa Medina-Sidonia aliamua kwamba hangeweza kuendelea na vita hivyo na badala yake aokoe meli na wanajeshi wengi iwezekanavyo. Aliamua kurudi Hispania kwa kuzunguka kupitia Scotland na Ireland.

      Dhoruba na Kuvunjika kwa Meli

      Safari ya kurudi nyumbani haikuwa rahisi kwa Manowari hizo zilizokuwa zimevamiwa. Kulikuwa na chakula kidogo sana, na kwa sababu matangi yalikuwa yanavuja, kulikuwa na maji machache. Mashambulizi ya Waingereza yalikuwa yameharibu meli nyingi na chache sana zingeweza kusafiri. Kisha, zikiwa kwenye pwani ya kaskazini magharibi ya Ireland, Manowari hizo zilikumbwa na dhoruba kali kwa majuma mawili. Meli nyingine zilipotea kabisa na nyingine zikavunjika kwenye pwani ya Ireland.

      Hatimaye, mnamo Septemba (Mwezi wa 9) 23, meli za kwanza za Manowari zilijikokota kuingia bandari ya Santander, kaskazini mwa Hispania. Ni meli 60 hivi na karibu nusu ya watu walioondoka Lisbon waliofaulu kurudi nyumbani. Maelfu walizama baharini. Wengine wengi walikufa kutokana na majeraha au magonjwa waliyopata walipokuwa wakirudi nyumbani. Kwa waokokaji waliofika kwenye pwani ya Hispania, masaibu hayakuishia hapo.

      Kitabu The Defeat of the Spanish Armada kinasema: “Meli kadhaa hazikuwa na vyakula, hivyo watu waliendelea kufa njaa,” ingawa walikuwa wametia nanga kwenye bandari moja ya Hispania. Kitabu hicho kinasema kwamba meli moja ilivunjika katika bandari ya Laredo huko Hispania, “kwa sababu hakukuwa na wanaume wa kutosha wa kuteremsha matanga na kutia nanga.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki