-
Tunda la Manjano Lenye Historia ya KupendezaAmkeni!—2003 | Februari 22
-
-
Tunda la Manjano Lenye Historia ya Kupendeza
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI
NI MWAKA wa 1789. Mashua isiyo na tanga yenye urefu wa meta saba iliyojaa wanaume, inaonekana ikiwa ndogo sana inapokuwa katika bahari kubwa. Wanaume hao ni dhaifu sana kwa sababu ya kukosa chakula na uchovu wa safari ambayo imechukua siku nyingi. Pia wamekabili mawimbi yenye nguvu na upepo mkali. Bado wanahitaji kusafiri kilometa 5,000 katika bahari wasiyoifahamu, na kuna hatari ya miamba ya tumbawe. Chakula ni haba na kila mwanamume anaruhusiwa kula gramu 30 za mkate (biskuti ya melini) kwa siku na kunywa maji kidogo. Hakuna tumaini la kuokoka.
Juma moja hivi mapema, abiria wa meli hiyo walikuwa wameasi na kutoroka wakitumia mashua za kuokolea na mmoja wao aliuawa wakati wenyeji wa huko walipowavamia. Pia walikabili dhoruba kali ya radi na mvua na kuokoka shambulizi la wenyeji waliowafukuza kwa mashua karibu na visiwa vilivyoitwa Visiwa vya Cannibal.
Kwa nini watu hao walisafiri hadi eneo hatari la Pasifiki Kusini, mbali sana na Uingereza, nchi ya kwao yenye mashamba mazuri ya matunda na mabustani? Walikuwa wakitafuta miti maridadi ya mishelisheli. Hebu tuone jinsi miti hiyo yenye kuvutia na matunda yake yenye matumizi mengi ilivyokuwa muhimu katika hadithi hiyo na katika safari maarufu za kale zaidi za uvumbuzi.
Huenda umetambua kwamba wanaume waliotajwa awali walikuwa waokokaji wa uasi unaojulikana sana wa meli ya Bounty. Meli hiyo ya jeshi la wanamaji la Uingereza yenye uzito wa tani 215, iliyoongozwa na Nahodha William Bligh, ilikuwa ikisafiri kutoka Uingereza hadi Tahiti. Ilipowasili Tahiti, meli hiyo ilibeba “abiria” wasio wa kawaida—karibu miche 1,000 ya mshelisheli. Miche hiyo iliyokuwa imepandwa ingeweza kuleta faida baadaye kwa kuzaa matunda ya rangi ya manjano ilipopandwa shambani na kunawiri katika makoloni ya Uingereza huko Karibea.
Mradi huo ulitokana na ushauri aliotoa Bwana Joseph Banks kwa serikali ya Uingereza. Wakati huo, Uingereza ilikuwa ikitafuta njia nyingine ya kuandaa chakula kwa ajili ya watumwa wake waliofanya kazi katika mashamba ya miwa. Hapo awali Banks, ambaye wakati huo alikuwa mshauri wa Bustani ya Kew karibu na London, Uingereza, alikuwa amesafiri pamoja na Nahodha James Cook katika safari yake ya uvumbuzi huko Pasifiki.a Yeye na Cook walikuwa wametambua umuhimu wa mshelisheli.
Ingawa yeye mwenyewe hangeandamana na Bligh, Banks alipanga jinsi ambavyo miche hiyo ingetunzwa wakati wa safari hiyo ndefu, akifikiria hasa uhitaji wa kuitilia maji yasiyo na chumvi. Waandishi fulani wanaamini kwamba uangalifu mkubwa uliopewa miche hiyo na maji mengi ambayo yalimwagwa—huku mahitaji ya wasafiri yakipuuzwa—ndio uliowachochea wasafiri hao waliokuwa wanalalamika waasi. Mnamo Aprili 28, 1789, Bligh na wanaume 18 walilazimishwa kung’oa nanga asubuhi na mapema karibu na pwani ya Tonga walipotishwa kuuawa. Huenda miche ya mshelisheli ilitupwa baharini na waasi wenye furaha wakati wa uasi.
Hata hivyo, Bligh hakukata tamaa. Alifunga safari nyingine iliyotajwa kuwa “safari maarufu zaidi kati ya safari zote za baharini zilizofungwa kwa kutumia mashua isiyo na tanga.” Kwa majuma saba yenye matatizo mengi, aliendesha meli hiyo ndogo umbali wa zaidi ya kilometa 5,800 kaskazini-magharibi kupitia visiwa vya sasa vya Fiji, kuelekea pwani ya mashariki ya New Holland (Australia), hadi eneo salama katika kisiwa cha Timor.
Aliporudi Uingereza, Bligh alipewa meli mbili zaidi ili aende Tahiti kuchukua miche ya mshelisheli. Mnamo mwaka wa 1792, alisafirisha miche 700 hadi kisiwa cha St. Vincent na Jamaika huko West Indies. Mishelisheli inapatikana huko hata leo na inazaa matunda yenye manufaa nyingi katikati ya matawi yake mapana.
-
-
Tunda la Manjano Lenye Historia ya KupendezaAmkeni!—2003 | Februari 22
-
-
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mchoro wa Robert Dodd unaoonyesha uasi uliotokea katika meli ya “Bounty”
[Hisani]
National Library of Australia, Canberra, Australia/Bridgeman Art Library
-