Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuiba Vitu Dukani—Je, Ni Msisimuko Usiodhuru Au Ni Uhalifu Mbaya?
    Amkeni!—2005 | Juni 22
    • Kuiba Vitu Dukani—Je, Ni Msisimuko Usiodhuru Au Ni Uhalifu Mbaya?

      WAZIA tukio hili. Mlango wa duka kubwa unafunguliwa na wasichana wawili waliovalia vizuri wanaingia. Wanatembea kuelekea mahali ambapo vipodozi huwekwa. Mlinzi aliyevalia mavazi rasmi anawafuata na kusimama meta 10 hivi kutoka mahali walipo akiwa ameweka mikono nyuma. Anawatazama wasichana hao wanaposhika-shika lipstiki na wanja.

      Wanamtazama mlinzi ambaye anawakazia macho. Wanasisimuka sana. Msichana mmoja anasogea karibu na rangi za kucha na kuchukua chupa kadhaa. Anasitasita huku akijifanya kuwa anachunguza rangi mbili nyekundu zinazokaribiana. Anaweka chupa moja chini na kuchukua nyingine ambayo ni nyekundu zaidi.

      Mlinzi anatazama chini na kugeuka kutazama upande mwingine. Mara moja, wasichana hao wanaweka lipstiki na chupa za rangi za kucha katika vibeti vyao. Wanaonekana kuwa watulivu, lakini ndani wamesisimuka sana. Wanasimama mahali hapo kwa dakika chache, mmoja anaangalia tupa za kusugua kucha huku mwingine akitazama wanja.

      Wasichana hao wanatazamana kisha wanatoleana ishara, na kuanza kutembea kuelekea mlangoni. Mlinzi anawapisha, nao wanamtazama na kutabasamu wanapompita. Wanapopita karibu na vifaa vya simu za mkononi kando ya keshia, wanavitazama. Wananong’onezeana kuhusu mifuko ya ngozi ya simu za mkononi. Kisha wanatembea kuelekea mlangoni.

      Kila hatua wanayopiga inawafanya wasisimuke zaidi na kujawa na woga. Wasichana hao wanapopita mlangoni, wanataka kupiga mayowe, lakini wanajizuia. Wakiwa nje, joto linawapanda. Msisimuko waliokuwa nao unapungua, nao wanashusha pumzi. Wasichana hao wanatembea haraka huku wakicheka-cheka. Wote wanafikiria jambo moja:‘Hatukukamatwa!’

      Wasichana hao wawili si watu halisi lakini kwa kusikitisha, tukio hilo linaonyesha mambo halisi. Nchini Marekani pekee, kuna visa karibu milioni moja vya wizi wa aina hiyo, hata hivyo hilo ni tatizo la ulimwenguni pote. Kama tutakavyoona, tatizo hilo linatokeza madhara makubwa sana. Lakini watu wengi wanaoiba vitu dukani hawafikirii hasara wanayotokeza. Hata watu wengi wenye pesa huiba. Kwa nini?

  • Kwa Nini Watu Huiba Vitu Dukani?
    Amkeni!—2005 | Juni 22
    • Kwa Nini Watu Huiba Vitu Dukani?

      “Sioni kuiba vitu dukani kuwa jambo baya. Mimi huona jambo hilo kuwa sawa na kuwagawia wenye uhitaji vitu.”—KASISI WA KANISA LA ANGLIKANA.

      IKIWA hekaya husema kweli, Robin Hood hakuona ubaya wowote kuiba. Hekaya za Waingereza zinasema kwamba aliwaibia matajiri ili kuwapa maskini. Kasisi aliyenukuliwa juu pia anaamini kwamba umaskini ni sababu nzuri ya kuiba. Anasema hivi kuhusu watu wanaoiba vitu dukani: “Ninawasikitikia sana, kwa kweli ninafikiri wana sababu nzuri kabisa za kuiba.” Anadokeza kwamba mara moja kwa mwaka, maduka makubwa yanapaswa kuwaruhusu maskini wachukue chochote wanachotaka bila kulipa.

      Hata hivyo, wengi huchochewa kuiba vitu dukani na sababu nyingine mbali na umaskini. Nchini Japani, polisi waliwakamata polisi wenzao wawili kwa kuiba vitu dukani. Nchini Marekani, mkurugenzi mmoja wa shirika la chakula lisilo la kibiashara alikamatwa akiiba katika duka la shirika hilo. Mara nyingi matineja wenye pesa huiba vitu wasivyohitaji. Ni nini huwachochea watu hao kuiba?

      ‘Kunasisimua’

      Msisimuko. Woga. Uwezo. Kama wale wasichana wawili waliotajwa katika makala iliyotangulia, watu fulani ambao huiba vitu dukani hupata hisia kama hizo, na tamaa ya kuhisi hivyo huwafanya waibe tena na tena. Baada ya kuiba kwa mara ya kwanza, mwanamke mmoja alisema hivi: “Nilisisimuka. Sikukamatwa na hilo lilinisisimua!” Alisema hivi kuhusu jinsi alivyohisi baada ya kuiba kwa kipindi fulani: “Niliaibika lakini pia nilisisimuka. Nilichangamka kwelikweli. Kuiba na kukosa kukamatwa kulifanya nihisi kuwa na uwezo mkubwa sana.”

      Kijana mmoja anayeitwa Hector anasema kwamba baada ya kuacha kuiba vitu dukani kwa miezi kadhaa, alihisi tamaa ya kuiba tena.a “Niliendelea kuhisi hivyo na tamaa hiyo ikawa kama uraibu. Ningetembea madukani na kuona redio kwenye dirisha la duka na kujiambia, ‘Ni rahisi sana kuiba redio hii. Ninaweza kuiiba na nisikamatwe.’”

      Wale ambao huiba ili kupata msisimuko hawahitaji vitu wanavyoiba. Gazeti moja la India linasema: “Wanasaikolojia wanasema kwamba watu hao huchochewa na msisimuko wa kufanya mambo waliyokatazwa. . . . Baadhi yao hata hurudisha vitu walivyoiba.”

      Sababu Nyingine

      Mamilioni ya watu hupatwa na mshuko moyo. Nyakati nyingine watu walioshuka moyo huonyesha dalili hizo kupitia tabia mbaya kama vile kuiba vitu dukani.

      Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 14 alilelewa katika familia tajiri isiyo na matatizo. Licha ya hayo, msichana huyo alikata tamaa. Alisema: “Singeweza kuondoa hisia hizo.” Alianza kutumia kileo na dawa za kulevya. Kisha siku moja akakamatwa akiiba dukani. Baadaye alijaribu kujiua mara mbili.

      Kijana mwenye tabia nzuri akianza ghafula kuiba vitu dukani, wazazi wanapaswa kufikiria ikiwa ana matatizo ya kihisia. Dakt. Richard MacKenzie, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya vijana, alisema: “Ninaamini kwamba mtoto wako anapoanza kuonyesha tabia yoyote isiyo ya kawaida unapaswa kufikiria uwezekano wa kwamba ameshuka moyo mpaka uchunguzi uonyeshe sivyo ilivyo.”

      Vijana fulani huchochewa na rafiki zao kuiba vitu dukani na huenda wakalazimika kufanya hivyo ili wakubaliwe na rafiki zao. Huenda wengine wakaiba vitu dukani kwa sababu hawana jambo la kufanya. Wezi stadi hujiruzuku kwa kuiba vitu dukani. Hata sababu iwe nini, wezi huiba vitu vyenye thamani ya mamilioni ya dola kutoka madukani kila siku. Lazima mtu fulani alipie vitu hivyo.

      [Maelezo ya dnini]

      a Baadhi ya majina katika makala hizi yamebadilishwa.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      KLEPTOMANIA

      Maria anasema hivi: “Tangu nilipokuwa tineja, nimekuwa nikiiba vitu dukani. Tamaa hiyo iliendelea kuwa mbaya zaidi hadi nikaanza kuiba vitu vyenye thamani ya dola 500 hivi kwa siku.

      “Sina nia ya kuiba, lakini tamaa ya kufanya hivyo inakuwa yenye nguvu. Kwa kweli ningependa kubadilika.” Kwa kuwa ni vigumu sana kudhibiti tamaa hiyo, Maria anafikiri kwamba ana kleptomania.

      Neno “kleptomania” humaanisha “tatizo la akili ambalo humfanya mtu awe na hamu kubwa ya kuiba bila kuwa na nia ya kujifaidi kifedha.” Tatizo hilo si uraibu wa kawaida tu, linatokana na matatizo makubwa sana ya kihisia.

      Watu wengine husema kwamba mtu ambaye ana zoea la kuiba ana tatizo hilo, lakini madaktari wanaamini kwamba tatizo hilo la akili si la kawaida. Kulingana na Shirika la Marekani la Magonjwa ya Akili, watu wanaoiba vitu dukani ambao wana tatizo hilo hawafiki asilimia 5. Kwa hiyo, tunahitaji kuwa waangalifu kabla ya kusema kwamba mtu mwenye zoea la kuiba vitu dukani ana tatizo la akili. Huenda kukawa na sababu nyingine zinazomfanya aibe.

  • Kuiba Vitu Dukani—Ni Nani Hupata Hasara?
    Amkeni!—2005 | Juni 22
    • Kuiba Vitu Dukani—Ni Nani Hupata Hasara?

      HUKO Japani, mwenye duka mmoja alimkamata mvulana akiiba na kuwaita polisi. Polisi walipofika, mvulana huyo alikimbia. Polisi walimkimbiza. Mvulana huyo alipokuwa akivuka reli, aligongwa na gari-moshi, akafa.

      Kwa sababu wengi walijua jambo hilo, watu fulani walimshutumu mwenye duka kwa kuwaita polisi. Alifunga duka lake hadi hasira za watu zilipopoa. Alipofungua duka lake tena, watu wengi wanaoiba vitu dukani walilivamia. Hata hivyo, alipokumbuka kisa kilichokuwa kimetokea mapema, aliogopa kuwakabili wezi hao. Watu waliona ni rahisi kuiba katika duka lake. Muda si muda, alilazimika kulifunga kabisa.

      Ni kweli kwamba kisa hicho kilikuwa chenye kusikitisha sana kuliko visa vingine, lakini kinatufunza jambo fulani muhimu. Kuiba vitu dukani husababisha hasara kubwa kwa watu wengi na katika njia nyingi. Acheni tuchunguze habari zaidi kuhusu hasara kubwa inayosababishwa na uhalifu huo.

      Hasara kwa Wenye Maduka

      Wafanyabiashara ulimwenguni pote hupata hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka kwa sababu ya wizi wa vitu dukani. Watu wengine wanakadiria kwamba nchini Marekani pekee, wafanyabiashara hupata hasara ya zaidi ya dola bilioni 40. Biashara nyingi zitafilisika iwapo zitapoteza kiasi kikubwa kama hicho cha fedha. Maduka mengi hayawezi kukabiliana na tatizo hilo. Wezi wanapoiba vitu katika njia hiyo, wafanyabiashara wanaweza kupoteza biashara ambayo wamekuwa wakifanya muda wote wa maisha yao.

      Luke, mwenye duka huko New York City anasema hivi: “Mbali na mashindano kutoka kwa wafanyabiashara wengine, jambo lingine linalohangaisha ni wizi. Sijui tutaendelea na biashara hii kwa muda mrefu kadiri gani.” Luke hawezi kugharimia mfumo wa ulinzi. Anasema hivi kuhusu wezi hao: “Mtu yeyote anaweza kuiba vitu dukani hata wateja wa kawaida.”

      Watu fulani wanaamini kwamba tatizo la Luke si kubwa. Wao husema: “Maduka hayo hupata pesa nyingi kwa hiyo sitasababisha hasara yoyote kwa kuiba.” Lakini, je, kweli maduka hupata faida kubwa sana?

      Katika sehemu fulani, maduka huongeza bei ya vitu kwa asilimia 30, 40, au 50 lakini asilimia hiyo haiwakilishi faida wanayopata. Mfanyabiashara hutumia fedha za ziada anazopata kulipia gharama kama vile kodi ya nyumba, kodi ya mapato, mishahara na marupurupu ya wafanyakazi, gharama za udumishaji na za kurekebisha vifaa, bima, stima, maji, simu, mfumo wa ulinzi na gharama nyinginezo. Baada ya kulipia gharama hizo, huenda faida yake ikawa asilimia 2 au 3 tu. Kwa hiyo, mtu anapoiba, anamwibia mfanyabiashara sehemu ya riziki yake.

      Vipi Kuiba Vitu Visivyo na Thamani Kubwa?

      Akiwa dukani pamoja na mama yake, mvulana mdogo anaenda mahali peremende huwekwa na kufungua pakiti kisha anatumbukiza peremende moja mfukoni. Je, kuiba kitu hicho chenye thamani ndogo kunaweza kuathiri duka hilo?

      Kichapo Curtailing Crime—Inside and Out, cha Shirika la Marekani la Biashara Ndogo kinasema hivi: “Huenda kuiba vitu visivyo na thamani kubwa kusionekane kuwa jambo kubwa kwa mwizi ambaye huiba vitu vidogo kama kalamu. Lakini wizi huo huleta hasara kubwa kwa biashara ndogo-ndogo.” Kwa sababu wafanyabiashara hupata faida ndogo sana, lazima mfanyabiashara rejareja auze peremende 900 au mikebe 380 ya supu kila siku ili kulipia hasara ya dola 1,000 inayosababishwa kila mwaka na wizi. Kwa hiyo, wafanyabiashara hupata hasara kubwa wavulana wengi wanapoiba peremende. Tatizo huanzia hapo.

      Watu wengi sana, vijana kwa wazee, matajiri kwa maskini, kutoka jamii na malezi mbalimbali wanaiba vitu madukani. Kumekuwa na matokeo gani? Baraza la Kitaifa la Kuzuia Uhalifu nchini Marekani linaripoti kwamba karibu thuluthi moja ya wafanyabiashara nchini humo hulazimika kufunga biashara zao kwa sababu ya wizi huo. Bila shaka, biashara katika nchi nyingine zinakabili tisho hilohilo.

      Hasara Ambayo Mteja Hupata

      Bei za vitu huongezeka watu wanapoiba madukani. Kwa hiyo, katika sehemu fulani, wateja hulipa dola 300 zaidi kwa mwaka kwa sababu ya wizi. Hilo linamaanisha kwamba ikiwa unapata dola 60 kwa siku, mshahara wako wa juma moja hulipia vitu ambavyo watu wengine wanaiba. Je, una pesa nyingi hivyo za kupoteza? Watu waliostaafu ambao hutegemea malipo ya uzeeni au mama asiye na mwenzi ambaye anang’ang’ana kutegemeza familia yake, anaweza kuathiriwa sana akipoteza mshahara wa juma moja katika njia hiyo. Na kuna hasara nyingine zaidi.

      Jamii nzima inaweza kuathirika duka moja linapofungwa. Inaripotiwa kwamba wizi ulifanya duka moja la dawa katika jamii fulani yenye umoja huko Marekani lifungwe. Sasa inawalazimu wazee na walio wagonjwa wasafiri umbali wa kilometa mbili na nusu hivi hadi kwenye duka lingine la dawa. Afisa mmoja alisema: “Wazia ukisafiri umbali huo ukitumia kiti cha magurudumu.”

      Hasara Kubwa Ambayo Wazazi Hupata

      Bruce ni mwanamume anayeshikilia viwango vya juu vya maadili ambaye huwafundisha watoto wake kuwa wanyoofu. Siku moja, binti yake alikamatwa akiiba. Anasema hivi: “Nilifadhaika sana. Hebu wazia ukipigiwa simu na kuambiwa kwamba binti yako amekamatwa akiiba vitu dukani. Tulitumia miaka mingi kumlea binti yetu awe mtu mzuri, na sasa ona jambo alilofanya. Hatukudhani kwamba angeasi kwa njia hiyo.”

      Bruce alikuwa na wasiwasi mwingi kuhusu binti yake na wakati wake ujao. Pia alijiuzulu kuwa mwalimu wa kujitolea wa kidini. “Ningewezaje kuwafundisha wengine kutanikoni? Ningewezaje kuwafundisha kuhusu jinsi ya kuwalea watoto wao nikiwa na dhamiri safi? Nilihisi kuwa sistahili.” Inaonekana binti yake hakufikiria jinsi ambavyo uhalifu wake ungemwathiri baba yake.

      Hasara Ambayo Wezi Hupata

      Hapo zamani, wasimamizi wa maduka walipomkamata mwizi, mara nyingi walimwonya vikali na kumwachilia. Leo, mara nyingi wenye maduka huwakamata wezi na kuwaita polisi hata kama ni mara yao ya kwanza kuiba. Kwa kufanya hivyo, wezi hutambua kwamba uhalifu wao una matokeo mabaya. Mwanamke mmoja kijana anayeitwa Natalie alijionea ukweli wa jambo hilo.

      Natalie anasema: “Kadiri nilivyoiba ndivyo nilivyopata ujasiri. Nilidhani kwamba hata nikikamatwa, pesa ambazo ningemlipa wakili na ada ya mahakama zingekuwa kidogo zikilinganishwa na nguo zenye bei ghali nilizoiba.” Natalie alikuwa amekosea.

      Alikamatwa akiiba nguo na akatiwa pingu na polisi. Kwenye kituo cha polisi, alama zake za vidole zilichukuliwa na akafungiwa katika seli na wafungwa wengine. Alikaa humo kwa saa kadhaa huku wazazi wake wakitafuta pesa za kuja kumtoa.

      Natalie anamshauri hivi mtu yeyote anayefikiria kuiba: “Fuata ushauri wangu, afadhali ununue nguo au jinzi hiyo.” Anasema kwamba ukiamua kuiba, “utajutia jambo hilo kwa muda mrefu sana.”

      Mtu mwenye rekodi ya uhalifu hujuta. Huenda watu wanaoiba vitu dukani wakavunjika moyo wanapogundua kwamba kosa lao halitasahauliwa kabisa, lakini litaonekana tena na tena, kama tu doa kwenye nguo ama shati. Huenda mtu anayeiba vitu dukani akahitajika kutaja kosa lake anapotaka kujiunga na chuo kikuu. Inaweza kuwa vigumu kwake kuruhusiwa kufanya kazi kama daktari, daktari wa meno, au mchora-ramani za majengo. Huenda kampuni zikasita kumwajiri. Na matatizo hayo yanaweza kutokea hata ikiwa ameadhibiwa na korti na haibi tena.

      Kuiba vitu dukani kunaweza kutokeza hasara kubwa hata ikiwa mwizi hatafungwa. Hector aliyetajwa mapema katika mfululizo huu, aligundua jambo hilo. Anasema hivi: “Sikuwahi kukamatwa nikiiba.” Lakini alipatwa na madhara. Anasema hivi anapokumbuka jambo hilo: “Nafikiri vijana wanapaswa kuelewa jambo moja: Unavuna unachopanda. Hata kama hutakamatwa na polisi, utapatwa na madhara.”

      Kuiba vitu dukani huathiri watu wengine, na vitu ambavyo wezi huiba hutokeza hasara. Mtu yeyote aliye na zoea hilo, anapaswa kuliacha mara moja. Lakini mtu anayeiba vitu dukani anawezaje kupata nguvu za kuacha kuiba kabisa? Je, kuna wakati ambapo uhalifu huo utakomeshwa kabisa?

  • Jinsi ya Kuacha Kuiba Vitu Dukani
    Amkeni!—2005 | Juni 22
    • Jinsi ya Kuacha Kuiba Vitu Dukani

      “Kupunguza wizi si tatizo lako peke yako, ni tatizo la jamii nzima; kila mtu hunufaika wizi unapokomeshwa.”—“EVERY RETAILER’S GUIDE TO LOSS PREVENTION.”

      KAMA mazoea mengine mabaya, kuiba vitu dukani huathiri jinsi mtu anavyofikiri na kumfanya ajitetee. Kwa hiyo, kama vile mkulima hung’oa magugu pamoja na mizizi yake, yeyote anayetaka kuacha zoea la kuiba vitu dukani anapaswa kung’oa mawazo mabaya. Kwenye Waroma 12:2, Biblia inatushauri ‘tufanye upya akili yetu.’ Nalo andiko la 1 Petro 1:14 linatuhimiza hivi: “Acheni kufanyizwa kulingana na tamaa mlizokuwa nazo hapo zamani.” Mambo matano yafuatayo yanaweza kumsaidia mtu ambaye huiba vitu dukani abadili akili yake kuhusu kuiba.

      Misaada ya Kurekebisha Kufikiri Kwetu

      ◼ Kwanza, ni kinyume cha sheria kuiba vitu dukani. Kuiba kunaweza kuwa jambo la kawaida mahali ambapo mtu anaishi, na huenda asikamatwe; lakini bado mtu anayeiba vitu dukani anavunja sheria.—Waroma 13:1.

      Ni nini hutokea watu wengi wanapovunja sheria? Kulingana na Biblia, “sheria hufa ganzi.” (Habakuki 1:3, 4) Yaani, manufaa inayotokana na sheria zilizowekwa hupotea, na utengemano hukosekana katika jamii. Kila wakati mtu anapoiba vitu dukani, anadhoofisha msingi wa jamii inayotii sheria. Hilo linapotokea, kila mtu huumia.

      ◼ Pili, kuiba vitu dukani hufanya watu wakose kutumainiana. Mazoea hayo yasiyo ya unyoofu huharibu mahusiano ya kibinadamu na kufanya iwe vigumu kwa watu kuelewana na kutendeana kwa haki.—Methali 16:28.

      “Udhaifu wangu mkubwa ni kuwatumaini watu kupita kiasi.” Ndivyo alivyosema mtu mmoja mwenye duka la nguo baada ya wezi kumfilisi. Aliamini kwamba wateja na wafanyakazi wake hawawezi kumwibia. Sasa anahisi kwamba hakupaswa kuwatumaini watu hao.

      Mtu anapomdanganya mwingine, hilo hupunguza heshima ambayo mwenzake humpa. Lakini wezi hufanya wenye duka wamshuku kila mtu anayeingia katika duka lao. Hufanya watu wanyoofu washukiwe kuwa wezi. Hakuna mtu anayepaswa kufanya hivyo.

      ◼ Tatu, zoea la kuiba vitu dukani linaweza kumfanya mtu atende uhalifu mkubwa zaidi. Baada ya muda, huenda watu wanaoiba vitu dukani wakafanya mambo mabaya zaidi.—2 Timotheo 3:13.

      Mwisho wa Kuiba Vitu Dukani

      ◼ Jambo la nne lililo muhimu zaidi ni kwamba mtu anayeiba vitu dukani anapingana na Mungu Mweza Yote. Neno lake humwambia mwizi “asiibe tena,” nalo huonya kuhusu hukumu dhidi ya wale wanaokosa kumtii. (Waefeso 4:28; Zaburi 37:9, 17, 20) Lakini Yehova huwasamehe wezi wanaojirekebisha. Wanaweza kuwa na amani pamoja na Mungu.—Methali 1:33.

      ◼ Tano, kama uhalifu wote mwingine, hivi karibuni kuiba vitu dukani kutakomeshwa. Kama Biblia inavyoahidi, Ufalme wa Mungu utakapotawala dunia kwa ukamili, wanadamu watatendeana kwa utimilifu na kwa unyoofu. Hilo litakomesha madhara yanayosababishwa na kuiba vitu dukani.—Methali 2:21, 22; Mika 4:4.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      NJIA RAHISI ZA KUZUIA WIZI

      Huenda watu fulani wenye biashara ndogo wasiwe na uwezo wa kununua mifumo ghali ya ulinzi. Lakini hilo halimaanishi kwamba hawawezi kukabiliana na watu wanaoiba vitu dukani. Mara nyingi, wafanyabiashara wanaweza kulinda bidhaa zao kwa kuchukua hatua fulani rahisi.

      Katika kichapo walichoandika pamoja, wapelelezi Michael Brough na Derek Brown wanakazia uhitaji wa kuwatazama wateja kwa makini: “Mtazame kila mtu. . . . Wewe na wafanyakazi wako ndio mnaoweza kulinda vitu kwa njia bora zaidi.” Wanapendekeza umwendee mtu unayeshuku kwamba ameiba na kumwambia hivi: “Je, umepata kitu ulichokuwa unatafuta? Tafadhali kipeleke kwa keshia, naye atakuambia bei yake.” “Ungependa nikufungie kitu hicho?” “Je, fulana hiyo inakutoshea?” “Ungependa nikupe kikapu?” Wapelelezi hao wanasema: “Hilo hufanya wateja wanyoofu na vilevile wezi watambue kwamba umewaona na kwamba unapendezwa nao.”

      Wanasema hivi kuhusu kupanga vitu: “Hakikisha bidhaa zimejaa na zimepangwa vizuri kila wakati. Kuchunguza bidhaa mara nyingi kutafanya uzifahamu vizuri, na zinapopangwa vizuri inakuwa rahisi zaidi kugundua ikiwa kitu fulani kimeguswa au kuondolewa.”—Every Retailer’s Guide to Loss Prevention.

      Kachero Russell Bintliff anadokeza: “Safu zisizokuwa na vizuizi na rafu zilizojaa zitawasaidia wafanyakazi kuona kile ambacho wateja wanafanya. Mfanyakazi anapotembea kwenye safu ambapo mtu fulani anashukiwa kuwa mwizi, anaweza kutambua ni nini kinachokosekana, kisha anaweza kujifanya kwamba anaangalia bidhaa na kuona ni nini kiko ndani ya kikapu cha mteja. . . . Watu wanaoiba vitu watajua ni nini kinachoendelea; lakini mteja mnyoofu hatatambua kwamba mfanyakazi huyo anamtazama.” Anasema hivi kuhusu mpangilio wa safu: “Safu zinapaswa kupangwa katika njia ambayo [mwenye duka] pamoja na wafanyakazi wanaweza kuona wateja wanafanya nini.”—Crimeproofing Your Business—301 Low-Cost, No-Cost Ways to Protect Your Office, Store, or Business.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki