Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Urusi
    2008 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Magdalina Beloshitskaya anakumbuka: “Saa nane usiku Jumapili, Aprili 8, 1951, tuliamshwa mlango wetu ulipobishwa kwa kishindo. Mama aliruka kutoka kitandani na akakimbia na kumkuta askari amesimama mlangoni. ‘Mnapelekwa uhamishoni Siberia kwa sababu ya kumwamini Mungu,’ akatangaza. ‘Tunawapa saa mbili mpakie vitu vyenu. Chukueni chochote humu ndani, lakini hamruhusiwi kuchukua mbegu, unga, na nafaka. Pia hamruhusiwi kuchukua fanicha, vifaa vya mbao, na cherehani. Msichukue chochote kilicho nje ya nyumba. Bebeni tu shuka, blanketi, nguo, na mifuko yenu na mtoke.’

      “Tulikuwa tumesoma katika vichapo vyetu kwamba kulikuwa na kazi nyingi upande wa mashariki wa nchi yetu. Sasa tulielewa kwamba wakati ulikuwa umefika wa kufanya kazi hiyo.

      “Hakuna aliyelia. Askari alishangaa na kusema, ‘Hamjatokwa na machozi hata kidogo.’ Tulimwambia kwamba tangu 1948 tulikuwa tukisubiri kuhamishwa. Tulimwomba ruhusa tuchukue angalau kuku mmoja lakini akakataa. Askari hao waligawana mifugo yetu. Waligawana kuku wetu huku tukiwatazama. Mmoja alichukua watano, mwingine sita, na mwingine akapata watatu au wanne. Kuku wawili tu walipobaki, ofisa aliamuru wachinjwe nasi tukapewa kuku hao.

      “Binti yangu mwenye umri wa miezi minane tu alikuwa amelala. Tuliuliza ikiwa tungeruhusiwa kubeba kitanda chake, lakini ofisa akaamuru kivunjwe-vunjwe. Kisha akatupa sehemu ambayo ingeweza kumbeba mtoto.

      “Muda si muda, majirani walijua tunapelekwa uhamishoni. Mmoja wao alikuja na mfuko mdogo wenye mkate na tulipokuwa tukiondoka aliutupa ndani ya gari la kukokotwa lililokuwa limetubeba. Askari aliuona na akautupa nje. Tulikuwa watu sita, yaani, mimi, Mama, ndugu zangu wawili, mume wangu, na binti yetu mwenye umri wa miezi minane. Tulipotoka kijijini, tuliingizwa haraka ndani ya gari na kupelekwa kwenye kituo kikuu cha eneo hilo ambako hati zetu zilijazwa. Kisha tukabebwa kwa lori na kupelekwa kwenye kituo cha reli.

      “Ilikuwa Jumapili, siku yenye jua lenye kupendeza. Kituo hicho kilikuwa kimejaa watu—wanaohamishwa na waliokuja kutazama. Lori lililokuwa limetubeba lilisimama karibu na behewa la gari-moshi ambamo ndugu zetu tayari walikuwa. Gari-moshi lilipojaa, askari walihakikisha kila mtu yumo kwa kutumia jina lake la pili. Behewa letu lilikuwa na watu 52. Wale waliokuja kutuaga walianza kulia. Lilikuwa jambo la kustaajabisha kwani hata hatukuwajua wengine kati yao. Lakini wao walijua kuwa sisi ni Mashahidi wa Yehova na tulikuwa tunapelekwa uhamishoni Siberia. Gari-moshi lilipiga honi kwa nguvu. Kisha akina ndugu wakaanza kuimba wimbo katika Kiukrainia: ‘Upendo wa Kristo na uwe pamoja nanyi. Tukimpa Yesu Kristo utukufu tutakutana tena katika Ufalme wake.’ Wengi wetu tulikuwa na tumaini hakika na imani kwamba Yehova hatatuacha. Tuliimba mistari kadhaa. Kuimba kwetu kuligusa mioyo sana hivi kwamba baadhi ya askari wakaanza kulia. Kisha gari-moshi likaanza kuondoka.”

  • Urusi
    2008 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • [Picha katika ukurasa wa 102]

      Magdalina Beloshitskaya na familia yake walipelekwa uhamishoni Siberia

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki