-
‘Yehova Ameufanya Uso Wake Ung’ae Kuwaelekea’Mnara wa Mlinzi—2009 | Agosti 15
-
-
USO wa mwanadamu una misuli zaidi ya 30. Ili utabasamu tu, unahitaji kutumia misuli 14! Hebu wazia jinsi ambavyo mazungumzo yangekuwa bila misuli hiyo. Je, yangevutia? Hapana. Zaidi ya kufanya mazungumzo yavutie, misuli ya uso inawasaidia viziwi kwa njia nyingine. Misuli hiyo inapotumiwa kutoa ishara za mwili, inasaidia sana kuonyesha mawazo na fikira. Watu wengi wameshangaa sana kuona jinsi lugha ya ishara inavyoweza kuonyesha hata mawazo magumu pamoja na tofauti ndogo-ndogo katika maana ya maneno.
-
-
‘Yehova Ameufanya Uso Wake Ung’ae Kuwaelekea’Mnara wa Mlinzi—2009 | Agosti 15
-
-
Kuona Ni Kusikia
Kuna maoni mengi yasiyo ya kweli kuhusu viziwi na lugha ya ishara. Acheni turekebishe baadhi ya maoni hayo yasiyo ya kweli. Viziwi wanaweza kuendesha magari. Ni vigumu sana kwao kusoma midomo. Lugha ya ishara haihusiani hata kidogo na maandishi ya vipofu, wala si kuigiza tu. Kuna lugha nyingi za ishara ulimwenguni pote. Zaidi ya hayo, viziwi kutoka sehemu mbalimbali wanatumia ishara zinazotofautiana.
Je, viziwi wanaweza kusoma? Ingawa wengine wanasoma vizuri, ukweli ni kwamba wengi wao wana matatizo ya kusoma. Kwa nini? Kwa sababu maneno yanayoandikwa yanategemea lugha inayozungumzwa. Fikiria jinsi mtoto aliye na uwezo wa kusikia anavyojifunza lugha. Kuanzia wakati anapozaliwa, anazungukwa na watu wanaozungumza lugha fulani. Baada ya muda mfupi, anaweza kuunganisha maneno na kuunda sentensi. Hilo linatukia kiasili tu kwa kusikia lugha hiyo ikizungumzwa. Hivyo, unaposikia watoto wakijifunza kusoma, utagundua kwamba wamejifunza kupatanisha maneno yaliyoandikwa, pamoja na sauti na maneno ambayo tayari wanajua.
Sasa jiwazie ukiwa katika nchi ya kigeni ndani ya chumba cha vioo ambamo huwezi kusikia sauti yoyote. Hujawahi kamwe kusikia lugha ya nchi hiyo ikizungumzwa. Kila siku, watu wa nchi hiyo wanakuja na kujaribu kuzungumza na wewe wakiwa nje ya chumba hicho cha vioo. Huwezi kusikia wanachosema. Unaona tu wakifumbua-fumbua midomo yao. Wanapotambua kwamba huwaelewi, wanaandika kwenye karatasi maneno wanayosema na kukuonyesha kwenye kioo. Wanafikiri kwamba utaelewa maandishi hayo. Je, unafikiri unaweza kuyaelewa? Utagundua kwamba si rahisi kuwasiliana nao katika hali hiyo. Kwa nini? Kwa sababu maneno wanayoandika ni ya lugha ambayo hujawahi kamwe kuisikia ikizungumzwa. Viziwi wengi wanakabili hali kama hiyo.
Lugha ya ishara ni njia bora kabisa inayowasaidia viziwi kuwasiliana. Mtu anatumia ishara za mwili ili kuonyesha mawazo fulani. Ishara anazoonyesha pamoja na ishara za uso zinafuata sheria za lugha ya ishara. Kwa kufanya hivyo, mtu anaweza kutoa ujumbe akitumia lugha ya ishara.
Kwa kweli, karibu kila ishara ambayo kiziwi anatoa kwa mikono, mwili, na uso wake anapotumia lugha ya ishara ina maana. Ishara za uso hazitolewi ili kuwavutia tu watu. Ishara za uso ni sehemu muhimu ya sheria za lugha ya ishara. Kwa mfano: Kuuliza swali ukiwa umeinua nyusi za macho kunaweza kuonyesha kwamba unauliza swali la kumsaidia kufikiri au swali ambalo linahitaji jibu la ndiyo au hapana. Ikiwa nyusi zimeshuka, huenda unauliza ni nani, ni nini, ni wapi, kwa nini, au namna gani. Ishara fulani za mdomo zinaweza kuonyesha ukubwa wa kifaa fulani au ukubwa wa tendo fulani. Jinsi kiziwi anavyotikisa kichwa chake, kuinua mabega yake, kufanya ishara kwa mashavu, na kupepesa macho yake kunakazia maana kamili ya mawazo yanayotolewa.
Ishara hizo zote zinamsaidia mtazamaji kuelewa habari kwa njia yenye kufurahisha. Kwa kutumia njia hiyo bora ya kuwasiliana, viziwi ambao wanajua vizuri lugha ya ishara wanaweza kutoa wazo lolote, iwe ni wazo la kishairi au wazo gumu, mawazo ya kimapenzi au ya kuchekesha, mambo yanayoonekana au yasiyoonekana.
-