-
Mlima Sinai—Kito Kilicho NyikaniAmkeni!—1999 | Aprili 22
-
-
Hata hivyo tunaipita nyumba hiyo, kwa kuwa lengo letu kubwa ni kukwea na kupiga kambi usiku katika kilele kilichoko upande wa kusini. Kilele hiki, kiitwacho Gebel Musa, jina limaanishalo “Mlima wa Musa,” huhusianishwa kwa kawaida na Mlima Sinai.
Baada ya kutembea kwa muda wa saa mbili tunafika katika bonde dogo linaloitwa Bonde la Eliya, linalougawanya mara mbili mgongo wa Mlima Sinai wenye urefu wa kilometa tatu. Kulingana na mapokeo, Eliya alisikia sauti ya Mungu alipokuwa katika pango lililopo hapa. (1 Wafalme 19:8-13) Tunatua kidogo ili tupumzike chini ya mteashuri wenye miaka 500. Hapa pia pana kisima cha kale. Jinsi tunavyofurahia maji yake safi, baridi, tuliyopewa na Mbedui mmoja mwenye urafiki!
Kwa kufuata njia inayotumiwa na watalii kwa ukawaida, tunajitahidi kwa dakika 20 zaidi kupanda vile vidato 750 vya mawe hadi kwenye kilele. Hapo tunapata kanisa dogo. Watawa wanadai kwamba kanisa hilo limejengwa mahali hususa ambapo Musa alipewa Sheria. Pana ufa kwenye mwamba unaopakana na kanisa hilo na wanadai kwamba hapo ndipo Musa alipojificha Mungu alipokuwa akipita. (Kutoka 33:21-23) Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu awaye yote anayejua mahali hususa ambapo matukio hayo yalitukia. Vyovyote vile, mwono kutoka juu ya mlima unastaajabisha! Tunatazama ng’ambo na kuona safu baada ya safu ya milima ya matale yenye rangi nyekundu ikiishia nyuma ya uwanda ulio chini na uliotapakaa miamba. Upande wa kusini-magharibi kuna Gebel Katherina, au Mlima Catherine—wenye kimo cha meta 2,637, na ambacho ni kilele cha eneo hili.
-
-
Mlima Sinai—Kito Kilicho NyikaniAmkeni!—1999 | Aprili 22
-
-
Kukwea Ras Safsafa Ulio Karibu
Siku nyingine hutokeza fursa ya kukwea Ras Safsafa ambacho ni kilele kilichoko kwenye mgongo uleule wa kilometa tatu ambao una Gebel Musa. Ras Safsafa ndicho kilele cha kaskazini, na ni kifupi kidogo kuliko Gebel Musa. Ras Safsafa huinuka wima kutoka kwenye Uwanda wa er-Raha, ambapo huenda Waisraeli walipiga kambi Musa alipoenda kupokea Sheria kutoka kwa Yehova.
Tunapokwea kuelekea Ras Safsafa kupitia nchi yenye vilima na mabonde madogo, tunapita vikanisa vilivyoachwa, bustani, na chemchemi—mabaki ya vitu vya wakati ambapo watawa zaidi ya mia moja walikuwa wakiishi katika sehemu hii kwenye mapango na katika vyumba vidogo vya mawe. Sasa kuna mtawa mmoja tu aliyebaki.
Tunakutana na mtawa huyo katika bustani iliyozingirwa kwa ua mrefu wa seng’enge. Anapoturuhusu kuingia, anaeleza kwamba amekuwa akifanya kazi kwenye bustani hii kwa miaka mitano, huku akienda kwenye nyumba ya watawa mara moja tu kila juma. Mtawa huyo anatuelekeza kwenda Ras Safsafa, nasi tunafuata njia yenye kupinda inayoelekea juu ya mlima, na hatimaye, tunafika katika kilele kirefu kupita vilele vinginevyo katika sehemu hii. Tunaona Uwanda wa er-Raha ulio mpana chini yetu. Na hasa nikiwa mahali hapa pafaapo, nawazia kuwa hapa ndipo mahali ambapo Musa alikwea mlima kutoka kwa kambi ya Waisraeli ili asimame mbele ya kuwapo kwa Mungu. Nawaona akilini Waisraeli milioni tatu wakiwa wamekusanyika “wakiukabili mlima” katika uwanda huo mpana. Akilini namwona Musa akishuka katika bonde lililo karibu, akiwa na yale mabamba mawili ya mawe mikononi mwake yakiwa na maandishi ya zile Amri Kumi.—Kutoka 19:2; 20:18; 32:15.
-