Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Singapore—Kito cha Asia Kilichopoteza Mng’ao
    Amkeni!—1997 | Juni 8
    • Mashahidi wa Yehova Wapigwa Marufuku

      Yote hayo yalibadilika mnamo Januari 12, 1972. Amri ya ufukuzaji ilitolewa chini ya Sheria ya Serikali ya Kufukuza Nchini, sura ya 109, ikimwamuru mishonari Mkristo Norman David Bellotti pamoja na mkewe, Gladys, waliokuwa wakazi wa Singapore kwa miaka 23, waondoke nchi hiyo. Hiyo ilifuatwa haraka na agizo la kuondoa usajili wa Kutaniko la Mashahidi wa Yehova la Singapore. Kwa muda wa saa chache tu Jumba la Ufalme lilitwaliwa na polisi ambao walivunja mlango wa mbele na kuingia. Iliyofuatia karibu wakati huohuo ni marufuku rasmi dhidi ya fasihi yote ya Watch Tower Society. Hivyo kikaanza kipindi cha ukandamizaji wa Mashahidi wa Yehova.

      Baadaye Jumba la Ufalme liliuzwa na serikali ikiwa sehemu ya hatua ya uamuzi wayo yenyewe, yote hayo yakifanywa bila taarifa—bila uchunguzi wa mwanzoni, bila kesi, bila fursa ya kujitetea.

      Serikali ya Singapore imetaja kwa kurudia-rudia kule kutoshiriki kwa Mashahidi wa Yehova katika utumishi wa kijeshi kuwa sababu ya kisheria ya kuwapiga marufuku kikamili. Hivi karibuni kama Desemba 29, 1995, Bw. K. Kesavapany, mwakilishi wa kudumu wa Singapore wa Umoja wa Mataifa katika Geneva, katika barua aliyoandikia Mheshimiwa Ibrahim Fall, Naibu wa Katibu-Mkuu wa Haki za Kibinadamu, wa Umoja wa Mataifa katika Geneva, alitaarifu yafuatayo:

      “Marufuku ya serikali yangu dhidi ya harakati ya Mashahidi wa Yehova hutokana na mafikirio ya usalama wa kitaifa. Kuwapo kwenye kuendelea kwa harakati hiyo kwaweza kuwa hatari kwa hali-njema ya umma na utengamano mzuri katika Singapore. Jambo lililofaa kuambatana na kuondolewa usajili wa Mashahidi wa Yehova ni kwamba vichapo vyao vyote visiruhusiwe ili kuimarisha marufuku hiyo dhidi ya harakati hiyo na kuzuia kutawanywa na kusambazwa kwa itikadi zao.”

      Kwa habari ya mateto ya serikali juu ya hatari ya usalama wa kitaifa wa Singapore, yapasa kuonwa kwamba idadi ya wanaume vijana wanaokataa utumishi wa kijeshi ni watu wapatao watano kwa mwaka. Singapore ina jeshi la kivita la watu 300,000. Serikali ya Singapore imekataa hata kuzungumza kuhusu utumishi wa kiraia wa kitaifa kwa ajili ya watu wachache sana wanaohusika.

      Ukandamizaji wa Wazi

      Baada ya miaka kadhaa ya ustahimilivu usio thabiti, hali mpya ya ukandamizaji wa wazi wa haki za kibinadamu ilianza katika 1992 wakati watu kadhaa walipokamatwa—wakishtakiwa kwa kupatikana na fasihi iliyokatazwa chini ya Sheria ya Vichapo Visivyofaa. Katika 1994 Watch Tower Society ilimtuma Singapore W. Glen How, Q.C. mwenye umri wa miaka 75, ambaye ni wakili na mmoja wa Mashahidi wa Yehova muda wote wa maisha yake. Hadhi yake akiwa Mshauri wa Malkia ilimpa hali ya kutambuliwa na serikali ambayo ilimruhusu kwenda mbele ya mahakama za Singapore. Kwa kuzingatia uhakikisho wa kidini unaoandaliwa na Katiba, rufani ilipelekwa kwenye Mahakama Kuu ya Singapore, kutia ndani pingamizi dhidi ya uhalali wa kisheria wa kukamatwa kulikofanywa na marufuku ya 1972. Katika Agosti 8, 1994, rufani hiyo ilitupiliwa mbali na Hakimu Mkuu, Yong Pung How, wa Mahakama Kuu ya Singapore. Jitihada za ziada za kukata rufani uamuzi huo hazikufua dafu.

      Kufikia mapema 1995 ilionekana kwamba lile pingamizi la kisheria lililotegemea Katiba ya Singapore lilikuwa limechochea hatua zenye kukandamiza hata zaidi. Chini ya mpango kama wa kijeshi ulioitwa Operation Hope, maofisa wa kisiri kutoka Secret Societies Branch of Criminal Investigation Department walishambulia ghafula vikundi vidogo vya Wakristo waliokutanika katika nyumba za faragha. Maofisa wapatao 70 hivi na wasaidizi walifanya mashambulizi kama ya kikosi maalumu cha kijeshi, ikitokeza kukamatwa kwa watu 69. Wote walisafirishwa hadi kwenye vituo vya kuhojiwa, wengine walihojiwa usiku kucha, na wote wakashtakiwa kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova na kumiliki vichapo vya Biblia. Wengine walizuiliwa kwa njia ya kukatiwa uwasiliano kwa hadi muda wa saa 18, wasiweze hata kupigia simu familia zao.

      Mashtaka dhidi ya wageni yaliondolewa. Lakini 64 ambao ni wananchi wa Singapore walifanyiwa kesi mahakamani mwishoni mwa 1995 na mapema 1996. Wote 64 walipatwa na hatia. Watu 47 wenye umri kati ya miaka 16 na 72, hawakulipa faini za maelfu ya dola nao wakatiwa gerezani kuanzia juma moja hadi majuma manne.

      Kabla ya kupelekwa jela, wanaume na wanawake walivuliwa nguo na kufanyiwa msako mbele ya watu kadhaa. Wanawake fulani waliambiwa wanyooshe mikono yao, wachuchumae mara tano, na kufungua vinywa vyao na kuinua ndimi zao. Angalau mwanamke mmoja aliambiwa atumie vidole vyake kufungua mkundu wake. Katika magereza, baadhi ya wanaume walilazimika kunywa maji kutoka kwenye mabakuli ya choo. Wanawake fulani vijana walitendewa kama wahalifu hatari, wakizuiliwa katika vifungo vya upweke kwa muda wote wa vifungo vyao, na kupewa nusu ya chakula wanachopewa wafungwa. Askari-gereza fulani hata waliwanyima Mashahidi Biblia zao.

      Lakini acheni tuone maelezo machache ya wanawake waliofungwa. Kilichofunuliwa na ripoti zao wenyewe ni kinyume sana cha sura ya nje ya usafi ya jiji hili la kisasa.

      “Jela lilikuwa chafu. Beseni la kuogea na choo zilikuwa katika hali ya kusikitisha. Zilikuwa zenye utelezi na chafu. Chini ya benchi nililokalia kulikuwa na tando za buibui na uchafu.”

      “Niliambiwa nivue nguo zote, kisha nikapewa mavazi ya gerezani, kisahani cha kuwekea sabuni (bila sabuni), na mswaki. Niliambiwa na wale wafungwa wengine katika jela nilimokuwa kwamba wafungwa wa muda mfupi hawakuwa wakipewa dawa ya meno au karatasi ya chooni.”

      “Tulikuwa 20 katika jela moja. Choo kilikuwa cha aina ya kuchuchumaa ukuta ukifika kiunoni pangu. Bafu ilikuwa na mfereji mmoja tu wa manyunyu na beseni moja la kuogea lenye mfereji. Ilitulazimu kuoga kwa vikundi vya watu sita—sote kwenye jela tulilazimika kuoga kwa kipindi cha nusu saa asubuhi.”

      Japo kiwewe cha kufungwa, wote waliona hali hiyo kuwa pendeleo la kumtumikia Mungu—wakati wowote ule, mahali popote pale, na hata hali ziwe zipi. Ona maelezo yafuatayo kutoka kwa msichana tineja:

      “Tangu dakika niliyoingia gerezani, sikuzote nilijikumbusha kusudi la kuwa huko. Kila siku nilisali kwa Yehova kwamba asikilize sala yangu na asiniache. Nilihisi kwamba alijibu sala yangu kwa sababu ni roho yake takatifu iliyonisaidia kuvumilia. Ndipo nilipotambua ukaribu niliokuwa nao pamoja naye, nao umenisaidia sana, nikijua kwamba anatulinda. Nahisi nimependelewa kuweza kupitia jaribu hili kwa ajili ya jina lake.”

      Muda si muda magazeti ya habari ulimwenguni pote yakapata habari hiyo. Waandishi wa habari katika Australia, Hong Kong, Kanada, Malaysia, Marekani, Ulaya, na kwingineko wakarudia-rudia kuripoti matukio hayo. Gazeti The Toronto Star, la Kanada, lilijumlisha hasira ya wakati huo kwa kichwa chalo “Nyanya Ahukumiwa Hatia kwa Kumiliki Biblia.” Yakubalika kwamba ulimwengu una matatizo mengi mazito yanayohusisha watu wengi zaidi, lakini katika kisa hiki swali lililoulizwa na watu walioshangaa kila mahali ni lilelile. “Haya yanatukia katika Singapore?”

      Ni vigumu kuelewa kwa nini dini ambayo hutenda kazi waziwazi ikipata ulinzi kamili wa sheria katika nchi zaidi ya 200 tufeni pote yafanywa kuwa shabaha ya mnyanyaso katika Singapore. Ni vigumu hata zaidi kuelewa tufikiriapo kwamba hakuna dini nyingineyo yote katika Singapore ambayo imetendewa kwa ukosefu wa busara na kidhalimu jinsi hiyo.

      Hata naibu msimamizi wa polisi ambaye aliongoza kikundi cha ushambulizi dhidi ya Mashahidi wa Yehova alikiri mahakamani kwamba hiyo ndiyo iliyokuwa mara pekee kwamba yeye na maofisa wake walikuwa wameamriwa kuvunja mkutano wa kidini. Manukuu yafuatayo yanatoka kwenye nakala za uthibitisho:

      Swali: (Kwa naibu msimamizi) Kadiri unavyofahamu je, Secret Societies Branch imepata wakati wowote kuchunguza na kushtaki vikundi vyovyote vya kidini ambavyo havijasajiliwa, isipokuwa Mashahidi wa Yehova?

      Jibu: Hakuna kikundi kingine ninachojua.

      Kisha maswali yakaendelea.

      Swali: (Kwa naibu msimamizi) Je, umepata wakati wowote binafsi kufanya shambulizi kama hilo kwa kikundi kidogo cha kidini, kilichokutana katika nyumba na ambacho hakijasajiliwa chini ya Sheria ya Sosaiti?

      Jibu: Sijapata.

      Mwito wa Kuomba Kuchukuliwa kwa Hatua

      Shirika la Kimataifa la Haki za Kibinadamu na Shirika la Kimataifa la Mawakili kila moja lilipeleka mtazamaji walo lenyewe wa kipekee ili achunguze uaminifu wa kesi hizo. Mtazamaji asiyependelea, wa Shirika la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, Andrew Raffell, mwenyewe akiwa wakili wa Hong Kong, alisema yafuatayo: “Nasema katika ripoti yangu kwamba kesi hiyo ilikuwa na mwonekano wa mahakama bandia isiyo halali.” Yeye alieleza zaidi kwamba maofisa wa serikali walioitwa kuwa mashahidi hawakuweza kueleza mahakama kwa nini fasihi ya Mashahidi wa Yehova ilionekana kuwa isiyofaa. Raffell aliorodhesha baadhi ya vichapo vya Biblia vilivyopigwa marufuku kutia ndani Furaha—Namna ya Kuipata na Kupata Faida Zote za Ujana Wako. Yeye aliongeza kwamba havingeweza kikweli kuonwa kuwa visivyofaa katika maana yoyote ile ya neno hilo.

      Mtazamaji kutoka Shirika la Kimataifa la Mawakili, Cecil Rajendra, alitaarifu yafuatayo:

      “Tangu mwanzoni, ilikuwa wazi kwangu kwamba kesi yote ilikuwa hasa . . . wonyesho wa kipuuzi ulioonyeshwa waziwazi ili kudhibitishia ulimwengu kwamba bado demokrasia inazoewa katika Singapore.

      “Matokeo yalikuwa hakika na hakukuwa na tashwishi yoyote wakati wowote ule kabla ya, wakati wa au mwishoni mwa kesi hiyo kwamba washtakiwa wote wangepatikana na hatia kama walivyoshtakiwa.

      “Ingawa kesi hiyo ilifanywa katika mahakama ya chini na mashtaka yalikuwa uvunjaji mdogo wa Sheria ya Sosaiti hali iliyozunguka mahakama ilikuwa ya hofu na tisho.

      “Hali hiyo ilikuwa hasa kwa sababu ya uhakika wa kwamba kulikuwa na polisi wenye yunifomu zaidi ya 10 (6 ndani ya mahakama na 4 nje) kukiwa na wanaume kadhaa wa Kikosi cha Upelelezi wakiwa wamevalia kiraia na kuketi kwenye roshani.”

      Akitoa maelezo juu ya uendeshaji wa kesi yenyewe, Rajendra aliendelea kusema hivi:

      “Mwenendo wa Hakimu aliyetajwa wakati wa kipindi cha utazamaji (na vilevile jinsi ambavyo kesi yenyewe ilifanywa, kama inavyothibitishwa na nakala) ulithibitisha kwamba mengi zaidi yanatakiwa. . . . Kinyume cha kanuni zote za kesi isiyopendelea, Hakimu huyo pindi kwa pindi aliingilia kwa upande wa mashtaka na kuzuia upande wa utetezi kuhoji mashahidi wa upande wa mashtaka kuhusu vizibiti k.m. Biblia ya tafsiri ya King James, iliyotolewa na upande wa mashtaka kuonyesha kwamba washtakiwa walimiliki vichapo vilivyopigwa marufuku!”

      Hangaiko la kimataifa linalotokana na ukandamizaji wa Singapore wa haki za kibinadamu ni kubwa sana hivi kwamba gazeti la Ubelgiji lenye kichwa Human Rights Without Frontiers lilichapisha ripoti yenye kurasa 18 iliyohusika hasa na shambulizi la serikali ya Singapore dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Akiandika kihariri, Willy Fautré, mhariri mkuu wa jarida hilo, alifafanua kwa maneno machache na dhahiri sana hatua halisi ya uhuru wa kibinadamu katika hali yoyote ile ya kisiasa:

      “Ingawa uhuru wa kidini ni moja ya ishara bora zaidi za hali ya kawaida ya uhuru wa kibinadamu katika jamii yoyote ile, ni mashirika machache sana ya kilimwengu ya haki za kibinadamu ambayo yamehusika ama katika utarabibu wa kuondosha aina hizo za ubaguzi na ukosefu wa ustahimilivu unaotegemea dini au itikadi, ama katika maendeleo ya sera ambazo zingelinda na kuendeleza uhuru wa kidini.”

      Hilo jarida Human Rights Without Frontiers lilichapisha orodha ya mapendekezo kwa herufi nzito katika jalada la nyuma la ripoti yalo.

  • Singapore—Kito cha Asia Kilichopoteza Mng’ao
    Amkeni!—1997 | Juni 8
    • Ulimwengu Watazama

      1. “Wakati polisi wa Singapore walipovamia nyumba tano usiku mmoja Februari uliopita katika shambulizi la ghafula la aina ya kijeshi, wanaume, wanawake na matineja 69 walikamatwa na kupelekwa kwa ajili ya kuhojiwa kwenye makao makuu ya polisi. Hivyo si ndivyo mikutano ya kujifunza biblia ilipaswa kuisha.”—The Ottawa Citizen, Kanada, Desemba 28, 1995, ukurasa wa A10.

      2. “Kingekuwa chanzo cha utoshelezo kamili kwa wote wenye kuhusika na uhuru wa kidini na haki za dhamiri ikiwa Serikali ya Singapore ingerekebisha msimamo wayo kuhusiana na washiriki wa kikundi cha watu wasio na hatia na wasioweza kudhuru na kuwaruhusu kuzoea na kutangaza imani yao bila hofu au uzuizi.”—Profesa Bryan R. Wilson, Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.

      3. “Katika mfululizo wa kesi ambazo zilichochea malalamiko kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya haki za kiraia, mahakama za Singapore zimehukumia hatia Mashahidi wa Yehova 63 tangu mwezi wa Novemba uliopita.”—Asahi Evening News, Japani, Januari 19, 1996, ukurasa wa 3.

      4. “Mashahidi wa Yehova wapasa kuruhusiwa kukutana na kuzoea dini yao kwa amani bila tisho la kukamatwa au kutiwa gerezani. Uhuru wa kidini ni haki ya msingi ambayo inahakikishwa na Katiba ya Singapore.”—Shirika la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, Novemba 22, 1995.

      5. Chan Siu-ching, mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Dayosisi ya Katoliki ya Hong Kong, katika barua aliyomwandikia Lee Kuan Yew, Waziri Mkubwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, ya Juni 1, 1995, alitaarifu hivi: “Suala kuu ni kwamba hata ikiwa serikali ya Singapore inafikiri kwamba kukataa utumishi wa kijeshi ni kuvunja sheria na wanaovunja wanapasa kushtakiwa, wengine wanaoshiriki tu katika kikusanyiko cha kidini kwa kusudi la kuabudu hawapaswi kuathirika. . . .

      “Kwa hiyo twaandika kuomba Serikali yako:

      1. isipige marufuku Mashahidi wa Yehova ili wafurahie uhuru wa ibada na dhamiri;

      2. iwaondolee mashtaka Mashahidi wa Yehova ambao walihudhuria tu vikusanyiko kwa makusudi ya kidini.

      3. iwaachilie huru Mashahidi wa Yehova ambao wamekamatwa hivi majuzi kwa kuhudhuria tu utendaji mbalimbali wa kidini.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki