Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Idadi ya Familia za Mzazi Mmoja Inaongezeka
    Amkeni!—2002 | Oktoba 8
    • Idadi ya Familia za Mzazi Mmoja Inaongezeka

      “Mara nyingi nilikuwa nikisali na kulia usiku nikimwambia Mungu: ‘Sijui nitafanya nini kesho.’”—GLORIA, MAMA ASIYE NA MUME, MWENYE WATOTO WATATU.

      KUNA familia nyingi za mzazi mmoja katika jamii nyingi siku hizi, nazo zitaendelea kuwapo.a Wataalamu wanaochunguza idadi ya watu katika jamii mbalimbali wanajiuliza ni kwa nini watu huacha kuishi kama familia ya kawaida yenye mume, mke, na watoto na kupendelea aina nyingine za maisha ya jamaa.

      Maprofesa wa taaluma ya jamii Simon Duncan na Rosalind Edwards wanasema kwamba “mabadiliko ya kudumu yanatokea katika familia na mitazamo ya wanaume kuwahusu wanawake na ya wanawake kuwahusu wanaume inabadilika.” Kwa nini? Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba jambo hilo ni matokeo ya maamuzi ambayo watu hufanya maishani, kwa sababu ya mabadiliko katika uchumi, tamaduni, na jamii.

      Ebu tuchunguze baadhi ya mabadiliko hayo, na maamuzi ambayo watu hufanya. Watu hulemewa sana na mambo mbalimbali maishani. Mambo yanayotukia ulimwenguni huwaathiri watu kuanzia wanapoamka hadi wanapokwenda kulala. Hapo awali watu walitumia wakati mwingi kufanya mambo pamoja na wengine katika familia, lakini sasa muda huo hutumiwa kuchunguza mambo kwenye Internet, kutazama televisheni, kupiga simu, kusafiri, na kufanya shughuli nyinginezo.

      Watu hulemewa pia na hali ngumu ya uchumi. Vitu vya kisasa ni vya bei ghali, kwa hiyo wazazi wengi hufanya kazi ya kuajiriwa. Watu hukubali pia kuhama kwa sababu ya kazi, kwa hiyo wengi huishi mbali na kwao, na hawawezi kuwaomba watu wa ukoo msaada wanapouhitaji. Na hata wengine huishi mbali na wenzi wa ndoa. Katika nchi nyingi muziki wa kisasa, sinema, na vipindi vya televisheni, vinafanya hali kuwa mbaya hata zaidi kwa sababu vinaonyesha ndoa na familia kuwa mipango isiyo na maana.b

      Mama Wasio na Waume

      Hapo awali katika nchi zilizoendelea, mama wengi wasiokuwa na waume walikuwa wasichana wadogo ambao walisaidiwa na serikali kuruzuku watoto wao. Lakini hali hiyo imebadilika. Kuwa mama asiye na mume si jambo la kuaibikia siku hizi, na hata kunaonekana kuwa jambo la kuvutia kwa sababu hata wanawake wengine maarufu wana watoto ijapokuwa hawajaolewa. Isitoshe, wanawake wengi wana elimu nzuri zaidi siku hizi na wanaweza kujiruzuku, hivyo si lazima mwanamke awe na mume ili ajiruzuku mwenyewe na mtoto wake.

      Baadhi ya akina mama wasio na waume, hasa wale wenye wazazi waliotalikiana, hubaki wakiwa waseja kwa sababu hawataki watoto wao wahuzunike kwa kumwona baba akiwaacha. Wanawake wengine wanakosa wenzi kwa sababu waume wao waliwaacha, wala si kwa kupenda kwao. Shirika la Joseph Rowntree huko Uingereza linasema hivi: “Kwa kawaida wanawake hawachagui kukaa bila mume kwa sababu ya ubinafsi, na watoto wanaolelewa na mzazi mmoja hutunzwa vizuri nao hutiwa nidhamu.”

      Hata hivyo, ongezeko la familia za mzazi mmoja ni jambo linalotia wasiwasi kwa sababu wazazi hao na watoto wao wanaweza kupatwa na mfadhaiko, hali ngumu ya uchumi, na hasara nyinginezo. Watu wengine hujiuliza ikiwa inawezekana kwa mzazi asiye na mwenzi wa ndoa kulea watoto wake kwa mafanikio. Ni magumu gani hasa ambayo wazazi wasio na wenzi wa ndoa hukabili? Mkristo asiye na mwenzi wa ndoa anaweza kulea watoto wake kwa mafanikio jinsi gani?

      [Maelezo ya Chini]

      a Wataalamu wa jamii waonyesha kwamba akina mama wasio na waume ‘ni wengi sana kuliko akina baba wasio na wake.’ Kwa hiyo, makala hizi zinazungumzia hasa akina mama wasio na waume. Hata hivyo, kanuni zinazozungumziwa zinahusu vilevile baba wasio na wake.

      b Magumu ya akina mama yanazungumziwa kwa kindani katika makala ya “Je, Mama Wana Kazi Nyingi Mno?” katika toleo la Amkeni! la Aprili 8, 2002.

      [Sanduku katika ukurasa wa 4]

      Semi Mbalimbali

      Semi mbalimbali hutumiwa ulimwenguni kote kuzungumzia mama wanaolea watoto wakiwa peke yao. Katika makala hizi tunatumia semi “mzazi asiye na mwenzi wa ndoa,” na “mama asiye na mume” kumaanisha wazazi ambao wanawalea watoto wao peke yao bila msaada wa mume au mke au mwenzi iwe ni kwa sababu ya kifo, talaka, kutengana, au hawakupata kuoa au kuolewa, au sababu nyingine kama hiyo.

      [Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 4, 5]

      IDADI YA FAMILIA ZA MZAZI MMOJA INAONGEZEKA KATIKA NCHI NYINGI

      Marekani: “Idadi ya mama wasio na waume iliongezeka kati ya mwaka wa 1970 na 2000, kutoka milioni 3 hadi milioni 10; katika kipindi hicho, idadi ya akina baba wasio na wake iliongezeka kutoka 393,000 hadi milioni 2.”—Shirika la Marekani la Sensa.

      Mexico: Kulingana na gazeti la La Jornada, karibu asilimia 27 ya mimba zote katika nchi hiyo ni za wasichana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 19.

      Ireland: Idadi ya familia za mzazi mmoja iliongezeka kutoka asilimia 5.7 mwaka wa 1981 hadi asilimia 7.9 mwaka wa 1991. “Mama wengi wasio na waume hulea watoto wao wakiwa peke yao kwa sababu ndoa zao zimevunjika.”—Single Mothers in an International Context, 1997.

      Uingereza: “Idadi ya familia za mzazi mmoja imepita asilimia 25 kwa mara ya kwanza. Jambo hilo linaonyesha kwamba idadi ya mama ambao hawajawahi kuolewa na talaka imeongezeka sana katika miaka 30 iliyopita.”—The Times, London, Machi 2, 2000.

      Ufaransa: “Tangu mwishoni mwa miaka ya 1970, idadi ya familia za mzazi mmoja imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.”—Single Mothers in an International Context, 1997.

      Ujerumani: “Idadi ya wazazi wasio na wenzi wa ndoa imeongezeka maradufu katika miaka 20 iliyopita. Karibu familia zote za mzazi mmoja . . . zinatunzwa na mama.”—Single Mothers in an International Context, 1997.

      Ugiriki: “Tangu mwaka wa 1980, idadi ya mama ambao hawajaolewa imeongezeka kwa asilimia 29.8 huku [Ugiriki]. Na kulingana na habari zilizotolewa na Muungano wa Ulaya, asilimia 3.3 ya watoto walizaliwa nje ya ndoa mwaka wa 1997, ikilinganishwa na asilimia 1.1 mwaka wa 1980.” —Gazeti la Ta Nea, Athens, Septemba 4, 1998.

      Japan: ‘Idadi ya familia zinazotunzwa na akina mama wasio na waume imeongezeka tangu miaka ya 1970.’ Asilimia 17 ya familia zote zilitunzwa na akina mama wasio na waume katika mwaka wa 1997.—Single Mothers in an International Context, 1997; The World’s Women 2000: Trends and Statistics.

      Australia: Karibu asilimia 25 ya watoto wanaishi na mzazi mmoja tu. Kwa kawaida jambo hilo lilisababishwa na kuvunjika kwa ndoa ya wazazi au wazazi walitengana. Imekadiriwa kwamba idadi ya familia za mzazi mmoja itaongezeka kwa asilimia 30 hadi 66 katika miaka 25 ijayo.—Shirika la Takwimu la Australia.

  • Mzazi Mmoja, Matatizo Mengi
    Amkeni!—2002 | Oktoba 8
    • Mzazi Mmoja, Matatizo Mengi

      “Nina uchungu mwingi moyoni. Mimi hujifungia kwenye bafu mara nyingi nikilia usiku kucha. Mambo ni magumu.” —JANET, MAMA ASIYE NA MUME, MWENYE WATOTO WATATU.

      KUNA sababu nyingi zinazofanya familia ziwe na mzazi mmoja tu. Familia kadhaa hubaki na mzazi mmoja tu kwa sababu ya vita, misiba ya asili, au magonjwa.

      Wazazi fulani huamua kutooana. Kwa mfano, huko Sweden karibu nusu ya watoto huzaliwa na akina mama ambao hawajaolewa. Talaka pia inafanya familia nyingine zibaki na mzazi mmoja tu. Makadirio yanaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya watoto Wamarekani wataishi katika familia zenye mzazi mmoja tu kwa muda fulani katika utoto wao.

      Kuelewa Magumu

      Hali ya akina mama ambao wamefiwa na waume zao hivi karibuni ni ngumu zaidi. Itawabidi kuanza kutunza familia zao huku wakiomboleza kifo cha waume zao. Inaweza kuchukua miezi kadhaa, hata miaka, kwa mama hao kuzoea wajibu huo, huku wakikabili magumu ya kiuchumi na daraka la kuwafariji watoto wao. Inaweza kuwa vigumu sana kwa mama aliye mjane kutekeleza madaraka hayo ya ziada. Huenda hali hiyo ikamfanya mtoto asitunzwe wala kuongozwa ifaavyo ijapokuwa anahitaji sana msaada na kutiwa moyo.

      Mama wengi ambao hawajaolewa na baba ya mtoto wao ni wachanga na hawana ustadi mwingi. Huenda walilazimika kuacha shule. Kwa sababu ya kukosa elimu nzuri, wengi wao ni maskini nao hufanya kazi za mshahara mdogo. Ikiwa watu wa ukoo, kama vile wazazi wao, hawawezi kuwasaidia, itawabidi wapate mtu wa kumtunza mtoto wanapokwenda kazini. Huenda mama asiyeolewa akalemewa pia na aibu na upweke. Huenda wengine wakahofia kwamba hawataweza kupata mume kwa sababu wana mtoto. Watoto wanaolelewa na mzazi mmoja wanapokua, wanaweza kusumbuka kwa kujiuliza maswali kumhusu mzazi yule mwingine na kuhisi kwamba wanahitaji kupendwa naye.

      Hali kadhalika, wazazi waliotalikiwa wana mfadhaiko mwingi sana. Baadhi ya wazazi huwa na hasira nyingi kwa sababu ya talaka. Wazazi fulani wanaona vigumu kufikiria mahitaji ya kihisia ya watoto wao kwa sababu wao wenyewe wanahisi kwamba hawafai na kwamba wametupwa. Akina mama, wanaolazimika kufanya kazi ya kuajiriwa kwa mara ya kwanza, huenda wakaona vigumu kushughulikia madaraka yote ya familia. Huenda wakahisi kwamba hawana wakati wala nguvu za kutosha kufikiria mahitaji hayo ya watoto wao. Kwa hiyo itawabidi watoto wakabili mabadiliko makubwa maishani mwao peke yao baada ya talaka ya wazazi.

      Magumu Ambayo Wazazi Waliotalikiwa Hukabili

      Wazazi wasio na wenzi wa ndoa hutambua kwamba mahitaji ya kila mtoto ni tofauti nayo hubadilika daima. Wazazi ambao wametalikiwa hukabili magumu yasiyo ya kawaida wanapojitahidi kuwapa watoto wao mwongozo wa kiroho.

      Kwa mfano, baadhi ya wazazi walio Mashahidi wa Yehova ambao wametalikiwa hawakupewa haki ya kulea watoto wao. Wao wamejitahidi kupanga watoto wao wawatembelee wakati wanapoweza kuhudhuria mikutano ya Kikristo pamoja. Hivyo, mtoto anaweza kushirikiana na ndugu na dada katika kutaniko la Kikristo kwa ukawaida, jambo ambalo huwanufaisha sana watoto wa wazazi waliotalikiana.

      Itawabidi wazazi waliotalikiana wasio na nafasi nyingi za kuwa pamoja na watoto wao watafute njia nyingine za kuwaonyesha kwamba wanawapenda. Ili kufaulu, ni lazima mzazi atambue na kuhangaikia hisia za moyoni za mtoto zinazobadilika-badilika. Jambo hilo ni muhimu hasa mtoto anapofikia umri wa kubalehe na anapoanza kupendezwa zaidi na ushirika wa watu wengine na marafiki.

      Mzazi ambaye amefaulu kulea mtoto wake huelewa uwezo, utu, na mawazo yake. (Mwanzo 33:13) Mzazi huyo huwa na uhusiano wa karibu na mtoto wake, nao huongea na kushirikiana kwa upendo. Wanaweza kuongea bila kizuizi chochote. Mtoto hushiriki katika shughuli za mzazi, na mzazi hushiriki katika shughuli za mtoto.

      Kuelewana Ni Muhimu

      Baada ya talaka, watoto wanahitaji kushirikiana na wazazi wote wawili. Vipi ikiwa wazazi wana imani tofauti, mmoja ni Shahidi wa Yehova, na yule mwingine si Shahidi? Kuzungumza mambo waziwazi na kwa ukawaida husaidia kuzuia mgongano. ‘Mwe na sifa ya kuwa wenye kukubali sababu,’ mtume Paulo aliandika. (Wafilipi 4:5, Phillips) Watoto wanapaswa kufundishwa kwamba wazazi wote wawili wana haki ya kufuata dini yao.

      Huenda mzazi asiye Shahidi akasisitiza mtoto ahudhurie ibada katika kanisa lake. Mzazi ambaye ni Shahidi wa Yehova anaweza kufanya nini katika hali hiyo? Yeye pia anaweza kumfundisha mtoto imani yake. Baadaye, mtoto ataweza kufanya uamuzi wake mwenyewe kuhusu ibada, kama kijana Timotheo, ambaye alifundishwa kanuni za Biblia na mama na nyanya yake. (2 Timotheo 3:14, 15) Mtoto akisumbuka kwa sababu ya kuhudhuria ibada ya dini nyingine, anaweza kufikiria kisa cha Naamani. Biblia inaeleza kwamba mtu huyo, hata baada ya kuwa mwabudu wa kweli, aliendelea kutimiza wajibu wake kwa kuambatana na mfalme aliyeabudu katika nyumba ya Rimoni. Huenda simulizi hilo likamhakikishia mtoto kwamba Yehova anamwelewa na kumpenda ijapokuwa yeye huhudhuria ibada nyingine ambayo hajazoea.—2 Wafalme 5:17-19.

      Mzazi mzuri anajua jinsi ya kuongoza fikira za mtoto au watoto na kuelewa hisia zao. (Kumbukumbu la Torati 6:7) Ni kweli kwamba wazazi wasiooa au kuolewa huenda wakaaibikia maisha yao ya awali. Hata hivyo, ni lazima wazazi hao wakumbuke kwamba watoto wana wazazi wawili. Watoto wanataka kuwajua wazazi wote wawili, na wanahitaji kujua kwamba wazazi wanawapenda. Na wanahitaji pia kujua kwamba kuzaliwa kwao hakukuwa tukio baya lisilotazamiwa. Kwa kusema kwa heshima juu ya yule mzazi mwingine na kujibu maswali yake kwa njia ambayo mtoto wa umri wake anaweza kuelewa, au anahitaji kujua, mzazi anaweza kumliwaza mtoto kwa upendo.

      Wazazi wanapaswa kukumbuka kwamba maoni ya mtoto kuhusu upendo, mamlaka, na nguvu hutegemea uhusiano wake pamoja na mzazi wake. Kwa kutumia mamlaka na nguvu kwa njia ya upendo mzazi Mkristo anaweza kumsaidia sana mtoto kumpenda Yehova na kuheshimu utaratibu uliopo katika kutaniko.—Mwanzo 18:19.

      Ni Lazima Watoto Wasaidie

      Watoto wanaolelewa na mzazi mmoja tu wanahitaji pia kuelewa kwamba ni lazima wawe tayari kusaidia ili familia yao ifanikiwe. (Waefeso 6:1-3) Kwa kumtii mzazi wao wanaonyesha kwamba wanampenda na kutambua kwamba mzazi huyo anajitahidi sana kufanya familia yao iwe na amani na furaha. Mawasiliano mazuri yanaweza kudumishwa tu ikiwa watoto watatambua kwamba wanahitaji kuunga mkono jitihada za mzazi za kuendeleza mawasiliano.—Mithali 1:8; 4:1-4.

      Watoto katika familia yenye mzazi mmoja hutakiwa mara nyingi kujifunza kazi mbalimbali mapema kuliko watoto wanaolelewa na wazazi wawili. Wanapofundishwa kwa upendo na subira, wavulana na wasichana watakuwa wenye kujistahi na kujiamini wanapojifunza kushughulikia madaraka ya maisha kwa mafanikio wakiwa wenye umri mdogo. Pia, watoto wanaweza kukabidhiwa kazi fulani za nyumbani ili wasaidie kudumisha utaratibu nyumbani.

      Jambo hilo halimaanishi kwamba wazazi wasio na wenzi wa ndoa wanataka watoto wao wajiamulie mambo kana kwamba wao ni watu wazima wasiohitaji mwongozo wowote kutoka kwa mzazi. Si jambo la hekima kumwacha mtoto mdogo peke yake au bila mtu wa kumtunza.

      Wazazi wengi wasio na wenzi wa ndoa hufikiri kwa makosa kwamba inawabidi kuwa marafiki tu wa watoto wao. Ijapokuwa uhusiano wa karibu ni wa lazima, wazazi hao wanapaswa kukumbuka kwamba watoto wanahitaji mzazi na mtoto hana ukomavu wa kutosha ili awe rafiki au msiri wa mzazi. Watoto wako wanataka utende kama mzazi.

      Wazazi wasio na wenzi wa ndoa na watoto wao wanaposhirikiana na kuwa na uhusiano wa karibu wanaweza kujenga familia yenye furaha. Kwa sababu idadi ya watoto wanaolelewa na mzazi mmoja inaongezeka, watu wote wanapaswa kutambua magumu ambayo wazazi hao na watoto wao hukabili na kuwa tayari kuwasaidia na kuwatia moyo kwa upendo.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      Jinsi Watoto Wanavyoathiriwa

      Wazazi wengi wasio na wenzi wa ndoa hawawezi kutumia wakati mwingi pamoja na kila mtoto kama wazazi wawili. Nyakati nyingine mzazi asiye na mwenzi wa ndoa huishi pamoja na mtu ambaye si mume wake au mke wake. Hata hivyo, watu wengi wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa hutengana kuliko wale waliofunga ndoa. Kwa hiyo, yaelekea watoto katika familia hizo watakuwa wameishi na watu wazima wengi tofauti-tofauti utotoni mwao.

      Kulingana na uchunguzi kadhaa, “kwa wastani, watoto wanaolelewa na mzazi mmoja tu wanaelekea kuwa na matatizo mengi ya maadili na kihisia kuliko watoto wanaolelewa katika familia za wazazi wawili.” Hata hivyo, uchunguzi wa kindani unaonyesha kwamba mapato ya chini ndiyo “yanayofanya watoto kutoka familia mbalimbali watofautiane kuhusiana na mwenendo na maendeleo.” Bila shaka jambo hilo halimaanishi kwamba watoto wanaolelewa na mzazi mmoja hawawezi kufaulu. Wakipata mwongozo na mazoezi yanayofaa wanaweza kushinda hali ngumu.

  • Msaada kwa Mzazi Asiye na Mwenzi wa Ndoa
    Amkeni!—2002 | Oktoba 8
    • Msaada kwa Mzazi Asiye na Mwenzi wa Ndoa

      “Watoto wangu wanaporudi nyumbani na kunikumbatia na kuniambia kwamba wananipenda ndipo ninapofurahi sana kuwa na watoto.”—DORIS, MAMA ASIYE NA MUME, MWENYE WATOTO WAWILI.

      WAZAZI wasio na wenzi wa ndoa wanaweza kutiwa moyo wanaposoma maneno haya katika Biblia: “Watoto ni baraka na zawadi kutoka kwa BWANA.” (Zaburi 127:3, Contemporary English Version) Mungu huwapenda watoto wanaolelewa na mzazi mmoja kama anavyowapenda watoto wengine. Muumba wetu anataka familia za mzazi mmoja zifaulu. Biblia inasema hivi kumhusu: “Huwategemeza yatima na mjane.” (Zaburi 146:9) Wazazi wasio na wenzi wa ndoa wanaweza kuwa na hakika kwamba Mungu yu tayari kuwasaidia.

      Mtoto ana haki ya kulelewa katika familia yenye upendo na amani ili aweze kukomaa kimwili, kihisia, na kiroho. Ni daraka na pendeleo la kila mzazi kutumiwa na Mungu kumzoeza mtoto.

      Wazazi wengi wasio na wenzi wa ndoa wameona kwamba ni muhimu kutoa sala za moyoni, kufuata kanuni za Biblia bila kigeugeu, na kumtumaini Yehova kabisa. Jambo hilo linalingana na himizo linalopatikana katika Zaburi 55:22: “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza.”

      Mara kwa mara, nyanya na babu, wazee wa kutaniko, na wazazi katika kutaniko la Kikristo, ambao wamefaulu kulea watoto, huenda wakaweza kusaidia familia yenye mzazi mmoja kushinda magumu. Ni kweli kwamba watu wa ukoo na waabudu wenzi wanaweza kuwasaidia sana wazazi wasio na wenzi wa ndoa, lakini Mungu amempa mzazi daraka la kumlea mtoto.a

      Jambo la kufurahisha ni kwamba wazazi wengi wasio na wenzi wa ndoa wamefaulu kushinda magumu na kulea watoto wenye kutegemeka, wenye mwenendo mzuri, na wenye kumcha Mungu. Mwandishi wa Amkeni! aliwahoji baadhi yao. Mambo kadhaa ambayo wazazi hao walitaja yameorodheshwa hapa chini.

      • Kupanga kazi za nyumbani vizuri. Wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu hujitahidi kupanga kazi za nyumbani na shughuli mbalimbali vizuri. Kupanga mambo vizuri na kufanya mambo kwa utaratibu ni muhimu sana. Biblia inasema hivi: “Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu.”—Mithali 21:5.

      • Kuwajibika kutunza familia. Wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu wanaona familia zao kuwa muhimu sana. Wao hutanguliza mahitaji ya watoto wao wala si mahitaji yao wenyewe.—1 Timotheo 5:8.

      • Kuwa na kiasi ni muhimu. Wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu hawapuuzi matatizo wala hawayatii chumvi; wao hutafuta suluhisho. Wao hutambua magumu na kuyashughulikia bila kujihurumia wala kuhisi uchungu.

      • Mawasiliano mazuri. Wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu hujitahidi kuwa na mawasiliano mazuri. Wao huwatia moyo watoto waeleze waziwazi mawazo na hisia zao bila kuficha. Baba mmoja asiye na mke anasema hivi kuwahusu watoto wake: “Ninaongea nao kila ninapopata nafasi. Tunafurahia kuwa pamoja tunapotayarisha chakula cha jioni. Ndipo wanaponieleza mambo yaliyomo mioyoni mwao.”

      • Kujitunza. Ijapokuwa wana shughuli nyingi mno, wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu, hutambua kwamba ni lazima wajitunze wenyewe pia kiroho, kihisia, na kiafya. Ethel, mama aliyetalikiwa mwenye watoto wawili, alieleza hivi: “Ninajaribu kuweka kando wakati kwa ajili yangu mwenyewe. Kwa mfano, wakati rafiki yangu mmoja anapowafundisha watoto kucheza ala fulani ya muziki, ninapata saa moja ya kupumzika. Wakati huo mimi huketi chini bila kuwasha televisheni.”

      • Maoni yanayofaa. Wazazi wasio na wenzi wa ndoa ambao wamefaulu wana maoni yanayofaa kuhusu daraka lao na juu ya maisha kwa ujumla. Wao huona kwamba katika hali ngumu kunaweza kuwa na faida fulani. Mama mmoja asiye na mume anasema hivi: “Mimi nimegundua kwamba kulea watoto wangu nikiwa peke yangu kunaweza kufurahisha pia.”

      Wale Waliofaulu

      Je, kanuni zilizotajwa juu, zinafanya kazi? Naam, kama tunavyoweza kuona kutokana na masimulizi mengi kuwahusu wazazi ambao wamefaulu kulea watoto wao wakiwa peke yao. Gloria, mama aliyetalikiwa, ambaye alitajwa katika makala ya kwanza, anafanya kazi ya kuajiriwa huko Uingereza na alilea wana wawili na binti mmoja akiwa peke yake. Wote watatu wakawa wahudumu Wakristo wa wakati wote, ambao hutumia maisha yao kufundisha Biblia. Alipoulizwa jinsi alivyofaulu, Gloria alieleza hivi: “Jambo gumu hasa lilikuwa kuongoza funzo la Biblia lenye kupendeza kwa ukawaida. Nilitaka watoto wawe wenye furaha, wawe na amani akilini, waridhike, na kulindwa na mitego. Nilipata kazi ya usiku. Nilitaka kuwa pamoja na watoto kila nilipoweza. Kabla ya kwenda kazini, tulitoa sala pamoja, kisha nikawalaza. Nilipokuwa kazini mama yangu mdogo alilinda nyumba.

      Gloria aliwasaidiaje watoto wake kutanguliza mambo muhimu maishani? Aongeza: “Lengo langu kuu lilikuwa kutanguliza mambo ya kiroho. Hatukuwa na fedha nyingi, na sikuficha jambo hilo kwa watoto. Kila jambo ambalo niliwaomba wafanye, nilikuwa tayari kulifanya mwenyewe pia, na wote walikuwa tayari kusaidia.” Akikumbuka jinsi alivyodumisha uhusiano mzuri pamoja na watoto wake, Gloria anasema hivi: “Nilifaulu kwa sababu tulifanya mambo pamoja. Hakuna aliyejitenga katika chumba chake. Tulipika pamoja, na tulisafisha na kupamba nyumba pamoja. Tulifanya kila kitu kwa kiasi. Sikuzote nilihakikisha kwamba tulipata nafasi ya kujiburudisha pia.”

      Carolyn, mama asiye na mume mwenye mwana mdogo anayeitwa Joseph, anafurahia kuona maendeleo yake. Nini kinachomsaidia kufaulu? “Sisi husoma Biblia kabla ya kulala,” anasema, “baadaye mimi humwuliza maswali kuhusu yale aliyojifunza. Isitoshe, sisi huchunguza mafungu fulani katika vichapo vya Biblia na kuona jinsi tunavyoweza kutumia mambo hayo katika maisha yetu. Jambo hilo humsaidia Joseph anapokabili matatizo, kama vile kuchokozwa shuleni.” Carolyn anakubali kwamba maisha yake si rahisi, lakini hajihisi mpweke. Anasema hivi: “Nahitaji kujikakamua, lakini nahisi kwamba Yehova amenisaidia sana. Mimi hutiwa moyo pia katika kutaniko la Kikristo.”

      Masimulizi ya maelfu ya mama wasio na waume kama vile Gloria na Carolyn, yanaonyesha kwamba kanuni za Biblia zinategemeka. Tangu zamani kanuni hizo zimewasaidia wazazi kulea watoto wenye sifa nzuri na wenye nguvu kiroho. (Mithali 22:6) Inawezekana kufaulu! Mzazi asiye na mwenzi wa ndoa anapatwa na magumu mengi yanayompa fursa za kufanya maendeleo na kuwasaidia wengine. Kumtegemea Mungu kikamili na kutumaini msaada wake ni njia bora ya kushinda magumu yanayowakabili wazazi wasio na wenzi wa ndoa.—Zaburi 121:1-3.

      [Maelezo ya Chini]

      a Habari zaidi kuhusu jinsi familia za mzazi mmoja zinavyoweza kufaulu zinapatikana katika kitabu Siri ya Kupata Furaha ya Familia, sura ya 9, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      [Picha katika ukurasa wa 11]

      Funzo la Biblia la familia limewasaidia watoto watatu wa Gloria kuwa wahudumu Wakristo wa wakati wote. Wanatazama barua na picha iliyotumwa na mwana wake mkubwa, ambaye ni mishonari

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Carolyn na mwana wake, Joseph

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki