Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Siri Iliyofichwa Sana
    Amkeni!—2000 | Machi 8
    • Siri Iliyofichwa Sana

      “Hakuna mtu atakayewekwa utumwani au kutumikishwa: utumwa na biashara ya utumwa itazuiwa katika namna zake zote.”-Azimio La Haki Za Kibinadamu Kwa Wote.

      WAKATI mwingine utakapoweka sukari ndani ya kahawa, mfikirie Prevot, kutoka Haiti aliyeahidiwa kazi nzuri katika nchi nyingine ya Karibea. Badala yake, aliuzwa kwa dola nane.

      Prevot alipatwa na mambo kama yale yanayowapata maelfu ya wananchi wenzake wanaotumikishwa ambao hulazimishwa kukata miwa kwa miezi sita au saba kwa mshahara mdogo sana au bila malipo. Mateka hao huwekwa kwenye mazingira yaliyojaa watu na yenye uchafu mwingi. Baada ya mali zao kutwaliwa, wanapewa panga. Lazima wafanye kazi ili kupata chakula. Wakijaribu kutoroka, huenda wakapigwa.

      Fikiria kisa cha Lin-Lin, msichana kutoka Kusini-Mashariki ya Asia. Alikuwa na umri wa miaka 13 mama yake alipokufa. Shirika la kutafutia watu kazi lilimnunua kutoka kwa baba yake kwa dola 480 za Marekani, huku likimwahidi kazi nzuri. Bei iliyolipwa kwa ajili yake iliitwa “mapato yake ya kimbele”—njia ya kuhakikisha kwamba hatatoka kamwe kwa wamiliki wake wapya. Badala ya kupewa kazi inayofaa, Lin-Lin alipelekwa kwenye danguro, ambapo wateja humlipa mmiliki dola 4 za Marekani kwa saa. Lin-Lin anakaribia kuwa mtumwa, kwa sababu hawezi kuondoka hadi deni lake litakapolipwa. Hilo latia ndani gharama ya mmiliki wa danguro kwa kuongezea riba na gharama nyinginezo. Lin-Lin akikataa kukubaliana na mwajiri wake, huenda akapigwa au kuteswa. Jambo baya hata zaidi ni kwamba akijaribu kutoroka, huenda akauawa.

      Je, Watu Wote Wako Huru?

      Watu wengi wanafikiri kwamba utumwa haupo tena. Kwa kweli, baada ya mikusanyiko mingi, maazimio, na sheria, utumwa umezuiwa rasmi katika nchi nyingi. Utumwa unachukiwa kwa dhati kila mahali. Sheria za kitaifa hupiga marufuku utumwa, na umezuiwa na sheria za kimataifa—hasa Kifungu cha 4 cha Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote la 1948, kilichotajwa hapo juu.

      Hata hivyo, utumwa ungalipo na unanawiri—ijapokuwa kwa watu fulani ni siri iliyofichwa sana. Kutoka Phnom Penh hadi Paris, kutoka Mumbai hadi Brasília, mamilioni ya wanadamu wenzetu—wanaume, wanawake, na watoto—wanalazimishwa kuishi na kufanya kazi wakiwa watumwa au chini ya hali za utumwa. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa la London, shirika la kale zaidi ulimwenguni linalochunguza kazi ya kulazimishwa, lataja idadi ya watu walio watumwa kuwa mamia ya mamilioni. Kwa kweli, huenda kukawa na watumwa wengi zaidi ulimwenguni leo kuliko wakati mwingine wowote!

      Ni kweli kwamba pingu, mijeledi, na minada tunayojua si ishara ya utumwa wa siku ya kisasa. Kazi ya kulazimishwa, ndoa ya kiutumwa, kufungwa kwa ajili ya deni, kuajiriwa kwa watoto, na mara nyingi ukahaba ni baadhi tu ya njia zilizo wazi zaidi za utumwa wa wakati wetu. Huenda watumwa wakawa masuria, wapanda-ngamia, wakataji-miwa, wafumaji-mikeka, au wajenzi wa barabara. Ni kweli kwamba wengi wao hawauzwi kwenye minada ya umma, lakini kwa kweli wako sawa tu na watumwa wenzao wa kale. Katika visa fulani wao hupatwa na mambo yenye kuhuzunisha hata zaidi maishani.

      Ni nani wanaokuwa watumwa? Wanakuwa watumwa jinsi gani? Ni nini kinachofanywa ili kuwasaidia? Je, utumwa utakomeshwa hivi karibuni?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

      UTUMWA WA KISASA NI NINI?

      Hili ni swali ambalo limekuwa gumu sana kujibiwa hata na Umoja wa Mataifa baada ya kujitahidi kwa miaka mingi. Fasiri moja ya utumwa ni ile iliyobuniwa na Mkusanyiko wa Utumwa wa mwaka wa 1962, iliyosema hivi: “Utumwa ni hali ya kutumia nguvu za kiasi au nguvu zote zinazohusu haki ya kumiliki mtu fulani.” Hata hivyo, neno hilo laweza kufasiriwa vinginevyo. Kulingana na mwandishi wa habari Barbara Crossette, “utumwa ni jina wanaloitwa wafanyakazi wa mshahara mdogo kwenye viwanda vya kutengenezea nguo na mavazi ya michezo huko ng’ambo na kwenye viwanda vya kutumikisha watu katika miji ya Marekani. Hutumiwa kushutumu biashara ya ngono na kazi ya jela.”

      Mike Dottridge, mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, aamini kwamba “kwa kuwa utumwa huwa wa namna tofauti-tofauti—au kadiri neno hilo litumiwavyo kurejezea hali nyingi—kuna hatari kwamba maana yake itapotea.” Aonelea kwamba “utumwa hutambulishwa na kumiliki au kudhibiti maisha ya mtu fulani.” Unatia ndani kushurutisha na kunyima uhuru wa kutembea—uhakika wa kwamba “mtu fulani hayuko huru kuondoka, wala kubadili mwajiri.”

      A. M. Rosenthal, akiandika katika The New York Times, asema: “Watumwa huishi maisha ya utumwa—kazi ya kuumiza, kubakwa, njaa, kuteswa, kudhalilishwa kabisa.” Aliongezea hivi: “Waweza kununua mtumwa kwa dola hamsini, kwa hiyo [wamiliki] hawajali wataishi kwa muda gani kabla miili yao haijatupwa ndani ya mto fulani.”

      [Hisani]

      Ricardo Funari

  • Ni Nani Walio Watumwa Leo?
    Amkeni!—2000 | Machi 8
    • Ni Nani Walio Watumwa Leo?

      HEBU wazia idadi yao. Inakadiriwa kwamba kati ya watoto milioni 200 na 250 wenye umri unaopungua miaka 15 hutumia muda mwingi wakati wa asubuhi kazini. Watoto robo milioni, wengine wakiwa na umri mchanga wa miaka saba, waliingizwa vitani mnamo mwaka wa 1995 na 1996 pekee, hivyo wengine wao wakawa watumwa wa vita. Idadi ya watoto na wanawake wanaouzwa wakiwa watumwa kila mwaka inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja.

      Lakini tarakimu haziwezi kufunua hali ya kukatisha tamaa ya watu hao. Kwa mfano katika nchi moja iliyoko kaskazini mwa Afrika, mwandishi Elinor Burkett alikutana na Fatma, mwanamke kijana aliyefaulu kumtoroka bwana wake mkatili. Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye, Burkett aling’amua kwamba Fatma “atakuwa mtumwa milele kulingana na maoni yake.” Je, Fatma aweza kuwazia wakati ujao ulio bora? “Hawezi kufanya mipango yoyote kunapopambazuka sembuse ya wakati ujao,” asema Burkett. “Wakati ujao ni mojawapo ya mambo mengi ya kuwaziwa tu asiyokuwa nayo.”

      Ndiyo, katika pindi hii, mamilioni ya wanadamu wenzetu ni watumwa wasio na tumaini. Ni kwa nini na jinsi gani watu hawa wote huwa watumwa? Wako katika utumwa wa aina gani?

      Wauzaji wa Binadamu

      Broshua ya watalii inayoenezwa Marekani ilisema hivi kinagaubaga: “Safari za ngono hadi Thailand. Wasichana halisi. Ngono halisi. Bei rahisi kweli. . . . Je, ulijua kwamba unaweza kununua msichana bikira kwa dola za Marekani 200 peke yake?” Jambo ambalo halikutajwa na broshua hiyo ni kwamba “bikira” hao yaelekea wametekwa nyara au kuuzwa kwa lazima kwenye madanguro, ambapo wanahudumia kwa wastani wateja 10 hadi 20 kwa siku. Wakikataa kutoa huduma za ngono, wanapigwa. Moto ulipozuka kwenye danguro moja katika Kisiwa cha Phuket, mahali pa kutalii huko kusini mwa Thailand, makahaba watano walichomeka hadi wakafa. Kwa nini? Kwa sababu wamiliki wao walikuwa wamewafungia vitandani kwa minyororo ili wasitoroke kutoka utumwani.

      Wanawake hawa wachanga hutoka wapi? Inaripotiwa kwamba, sekta hii ya biashara ya ngono imejaa mamilioni ya wasichana na wanawake kutoka ulimwenguni pote ambao wametekwa nyara, wametishwa, na kuuzwa kwenye ukahaba. Biashara ya kimataifa ya ngono inanawiri kwa sababu ya umaskini katika nchi zinazositawi, utajiri katika nchi zenye ufanisi, na sheria zinazopuuza ulanguzi wa kimataifa na mikataba ya kuwa utumwani.

      Mashirika ya wanawake katika Kusini-Mashariki ya Asia yamekadiria kwamba kuanzia miaka ya katikati ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, wanawake milioni 30 waliuzwa ulimwenguni pote. Walanguzi wa kibinadamu hutembea-tembea kwenye stesheni za gari-moshi, vijiji maskini, na barabara za mjini wakitafuta wasichana na wanawake wachanga wanaoweza kushambuliwa kwa urahisi. Kwa kawaida wahasiriwa huwa hawajaelimika, mayatima, walioachwa, au mafukara. Hupewa ahadi bandia za kazi, husafirishwa na kuvushwa mipakani, kisha huuzwa kwenye madanguro.

      Tangu kuporomoka kwa muungano wa nchi za Kikomunisti mwaka wa 1991, kumekuwa na wanawake na wasichana wengi sana mafukara. Kuondoa vizuizi, ubinafsishaji, na kuongezeka kwa pengo kati ya matabaka kumeongeza uhalifu, umaskini, na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Wanawake na wasichana wengi Warusi na wa Ulaya-Mashariki wamekuwa wakitumiwa vibaya ili kufaidi mashirika ya kimataifa ya kikahaba yaliyopangwa. “Kulangua wanadamu si hatari sana kuliko kulangua dawa za kulevya,” akasema aliyekuwa Mjumbe wa Haki wa Ulaya Anita Gradin.

      Hali ya Utotoni Iliyoharibiwa

      Katika kiwanda kimoja kidogo cha mikeka huko Asia, watoto wenye umri mdogo wa miaka mitano wanafanya kazi kuanzia saa kumi usiku hadi saa tano usiku bila malipo. Katika visa vingi watoto hao walioajiriwa hukabili hatari kubwa za kiafya: mashine zisizo salama, saa nyingi katika mazingira yasiyo na nuru na hewa ya kutosha, na kemikali hatari zinazotumiwa kutengeneza vitu.a

      Kwa nini watoto hutafutwa kwa bidii ili wawe wafanyakazi? Kwa sababu ni rahisi kulipa watoto na kwa sababu kwa asili watoto hufundishika, ni rahisi kuwatia nidhamu, na huogopa kulalamika. Umbo lao dogo na vidole vyepesi huonwa na waajiri wasiozingatia kanuni zozote kuwa rasilimali ya kufanya aina fulani za kazi kama vile, kufuma mikeka. Mara nyingi watoto hao huajiriwa, huku wazazi wao wakikaa nyumbani, bila kazi ya kuajiriwa.

      Jambo linalofanya hali ya watoto walioajiriwa kufanya kazi ya nyumbani iwe mbaya zaidi, hasa ni uwezekano wa kutendwa vibaya kingono na kimwili. Watoto wengi hutekwa nyara, huzuiwa kwenye kambi za mbali, na kufungiwa usiku ili kuwazuia wasitoroke. Huenda wakafanya kazi ya kujenga barabara na kuchimba mawe wakati wa mchana.

      Njia nyingine ambayo hali ya utotoni huharibiwa ni kupitia ndoa ya kiutumwa. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa laeleza kisa kimoja cha mfano: “Msichana mwenye umri wa miaka 12 aambiwa kwamba familia yake imepanga afunge ndoa na mwanamume mwenye umri wa miaka 60. Ni wazi kwamba ana haki ya kukataa, lakini kihalisi hana fursa ya kudhihirisha haki hiyo na hana habari kwamba anaweza kufanya hivyo.”

      Watumwa wa Deni

      Mamia ya maelfu ya wafanyakazi hufungwa kwa waajiri wao na mahali walipoajiriwa kwa sababu ya mikopo ambayo wao au wazazi wao wamepewa. Kidesturi, ufungwa wa kikazi hutokea hasa katika maeneo ya kilimo, ambapo wafanyakazi hufanya kazi wakiwa watumishi wa kawaida au wakulima. Katika visa fulani, deni hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, na kuhakikisha kwamba washiriki wa familia wanabaki katika ufungwa huo daima. Katika visa vingine, wanaowiwa pesa, huuza deni hilo kwa mwajiri mpya. Katika visa visivyo vya kawaida, wafanyakazi waliofungwa hawalipwi chochote kwa kazi yote wanayofanya. Au huenda wakafungwa na pesa chache wanazolipwa kimbele za mshahara wao, jambo linalorudiwa bila kikomo, ili wafungwe kwa mwajiri wao.

      Utumwa wa Kidesturi

      Binti, kutoka Afrika Magharibi, ana umri wa miaka 12 na ni mmojawapo kati ya maelfu ya wasichana wanaotumikia wakiwa trocosi, linalomaanisha katika lugha ya Ewe “watumwa wa miungu.” Amelazimishwa kuishi maisha ya utumwa ili kulipia uhalifu ambao hakuwa ameufanya—kubakwa ambako kulifanya azaliwe! Kwa sasa wajibu wake unatia ndani tu kufanya kazi nyumbani mwa kasisi wa hapo mwenye sanamu inayoabudiwa. Baadaye kazi za Binti zitaongezeka na kutia ndani kumhudumia kingono kasisi anayemmiliki. Kisha afikapo umri wa makamo, mahali pa Binti patachukuliwa na mwingine—kasisi huyo atatafuta wasichana wengine wanaovutia ili kumhudumia wakiwa trocosi.

      Kama vile Binti, maelfu ya wasichana ambao ni watumwa wa kidesturi hutolewa na familia zao wafanye kazi wakiwa watumwa katika jitihada za kulipia tendo ambalo huonwa kuwa dhambi au kosa dhidi ya agizo takatifu. Katika sehemu kadhaa za ulimwengu, inawabidi wasichana au wanawake watekeleze wajibu wa kidini na kuwahudumia kingono makasisi au wengineo—kwa kisingizio cha kwamba wanawake hao wameolewa na mungu. Katika visa vingi wanawake hao huandaa huduma nyingine bila kulipwa. Hawaruhusiwi kuhama wanapoishi au kufanya kazi tofauti na mara nyingi hubaki utumwani kwa miaka mingi.

      Utumwa wa Kawaida

      Ijapokuwa nchi nyingi zinadai kwamba zimepiga marufuku utumwa kisheria, hivi karibuni katika maeneo fulani kumetokea utumwa wa kawaida. Mara nyingi huo hutokea mahali palipo na mapambano ya kiraia au ya kivita. “Sheria imepuuzwa katika maeneo yenye mapambano,” laripoti Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, “na askari au wanamgambo wenye silaha wanaweza kuwalazimisha watu wawafanyie kazi bila malipo . . . bila kuogopa adhabu; mazoea hayo yameripotiwa hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na vikundi vyenye silaha ambavyo havijatambuliwa ulimwenguni pote.” Hata hivyo, kulingana na shirika hilohilo, “hivi karibuni kumekuwako pia na ripoti za askari wa serikali wanaowalazimisha raia kufanya kazi kama watumwa, bila kufuata sheria yoyote. Imeripotiwa kwamba askari pamoja na wanamgambo huhusika katika biashara ya watumwa, wakiuza wale waliowateka ili wawafanyie kazi wengine.”

      Kwa kusikitisha, laana ya utumwa ingali inasumbua wanadamu katika njia nyingi na mbinu zisizo wazi. Tua na kufikiri tena juu ya idadi ya watu wanaohusika—mamilioni ya watu wanaoteseka wakiwa watumwa tufeni pote. Kisha fikiri juu ya watumwa wa kisasa mmoja au wawili ambao umesoma masimulizi yao katika kurasa hizi—labda Lin-Lin au Binti. Je, ungependa kuona zoea la utumwa wa kisasa likikomeshwa? Je, kukomeshwa kwa utumwa kutapata kuwa jambo halisi? Kabla hakujawa hivyo, lazima mabadiliko makubwa sana yatukie. Tafadhali soma juu yake katika makala yanayofuata.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona “Kuajiriwa kwa Watoto—Mwisho Wake Wakaribia!” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1999.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

      KUTAFUTA UTATUZI

      Mashirika rasmi mbalimbali, kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto na Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni, yanafanya kazi kwa bidii kubuni na kutekeleza mbinu za kuondoa utumwa wa kisasa. Kwa kuongezea, mashirika mengine mengi yasiyo ya kiserikali, kama vile Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa na shirika la Human Rights Watch, yamejitahidi kuelimisha umma kuhusu utumwa wa kisasa na kuweka huru wale wanaohusika. Baadhi ya mashirika hayo yanataka vibandiko vya pekee vianzishwe vitakavyoonyesha kwamba bidhaa hazikutengenezwa na watumwa au na watoto walioajiriwa. Ili kwamba watu wanaofanya ngono na watoto washtakiwe wanaporudi katika nchi ya kwao, mashirika fulani yanatoa mwito sheria itungwe katika nchi ambamo “safari za ngono” huanzia. Watetezi fulani wa haki za kibinadamu hata wamefikia hatua ya kulipa wafanya-biashara wa utumwa na wakubwa wao kiasi kikubwa cha fedha kusudi wakomboe watumwa wengi kadiri wawezavyo. Jambo hilo limetokeza ubishi fulani, kwa kuwa mazoea hayo yaweza kutokeza fursa ya kuuza watumwa kwa faida na kuongeza bei yao kwa kiasi kikubwa.

  • Utumwa wa Kisasa—Mwisho Wake Wakaribia!
    Amkeni!—2000 | Machi 8
    • Utumwa wa Kisasa—Mwisho Wake Wakaribia!

      “Uhuru wa mtu mmoja ni sehemu muhimu ya uhuru wa ulimwenguni pote. Huwezi kuhalifu uhuru wa mtu na wakati huohuo ukose kuhatarisha uhuru wa ulimwenguni pote.”-Victor Schoelcher, Mwandishi Wa Habari Na Mwanasiasa Mfaransa, 1848.

      “NI UOVU gani unaomchochea mwanadamu daima kudharau, kushinda, na kushushia heshima wanadamu wenzake?” wauliza wahariri wa The UNESCO Courier. “Na imekuwaje kwamba uhalifu huo dhidi ya binadamu haujaadhibiwa hata tangu Haki za Kibinadamu zianzishwe?”

      Jibu ni tata. Pupa ndiyo huchochea kuajiriwa kwa watoto ili walipwe mshahara mdogo na pia hali ya kufungwa na deni. Umaskini na kukosa elimu vimelaumiwa kwa kufanya wasichana wauzwe kwenye ukahaba na kwenye ndoa za kiutumwa. Desturi za kidini na mawazo ya kitamaduni ndiyo huchangia utumwa wa kidesturi. Na kuhusu wanaume wanaozuru Bangkok au Manila ili kutafuta wavulana au wasichana wachanga wasio na UKIMWI, nia yao ni upotovu wa kingono na ukosefu wa adili ulio wazi. Yote hayo ni sehemu ya ulimwengu wa watu ambao ni “wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, . . . wasio na shauku ya kiasili, . . . wasio na hali ya kujidhibiti, wakali,” kupatana na maneno ya mtume Paulo, mwanafunzi wa sheria wa karne ya kwanza. (2 Timotheo 3:1-5) Ni sehemu ya ulimwengu ambamo “yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, wala yasiyokuwapo hayahesabiki,” kupatana na maneno ya mtawala wa kale anayeitwa Solomoni.—Mhubiri 1:15.

      Badiliko la Akili

      Je, hilo lamaanisha kwamba hakuna jambo lolote linaloweza kufanywa au litakalofanywa ili kukomesha utumwa daima—ama kwa namna yake ya kale ama kwa namna ya kisasa zaidi? Sivyo kamwe!

      Ofisi ya UM ya Mjumbe Mkuu wa Haki za Kibinadamu (OHCHR) yasema kwamba utumwa ni “hali ya akili,” ikiongezea hivi: “Hata unapokomeshwa, utumwa huacha alama fulani. Unaweza kudumu akilini—miongoni mwa wale walioathiriwa pamoja na wazao wao na pia miongoni mwa warithi wa watu waliotumikisha wengine—muda mrefu baada ya kutoweka rasmi.”

      Hivyo njia moja ya kukomesha utumwa ingekuwa kuanzisha badiliko la kufikiri—badiliko la moyo—ulimwenguni pote. Na hilo lahusisha badiliko la elimu—kufundisha watu wapendane na kustahi adhama ya wengine. Inamaanisha kusaidia watu wang’oe pupa mioyoni mwao na kufuata viwango vya juu vya adili. Ni nani anayeweza kuandaa elimu hiyo? Shirika la OHCHR lasema kwamba “kila mtu apaswa kuchangia utengamano wa ulimwengu unaopinga kuwatumia vibaya wanadamu.”

      Fikiria programu ya elimu ambayo imetekelezwa ulimwenguni pote na kikundi cha Kikristo cha Mashahidi wa Yehova. Programu hiyo imefanikiwa kufundisha watu wenye moyo wa haki wasivumilie au kuruhusu kutumiwa vibaya kwa wanadamu. Kupitia programu hiyo, mamilioni ya watu katika nchi zaidi ya 230 wamefundishwa kutendea wanadamu wenzao kwa adhama. Kwa nini programu hiyo imefaulu?

      Kwa sababu inategemea Biblia, kitabu kilichopuliziwa na Muumba wa mwanadamu. Ni kitabu kinachotegemeza adhama ya kibinadamu. Watu waliofundishwa na Biblia kupitia programu ya elimu ya Mashahidi wa Yehova hujifunza kwamba Muumba wetu, Yehova, ni Mungu wa adhama. (1 Mambo ya Nyakati 16:27) Huwapa adhama viumbe wake wote. Hao hutia ndani wanaume na wanawake, kutoka rangi zote, malezi ya kijamii, na hali za kiuchumi.—Ona sanduku “Uhuru na Adhama ya Kibinadamu—Kutoka Chanzo Gani?”

      Usawa na Kuheshimu Adhama

      Biblia hufundisha kwamba Mungu “alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” (Matendo 17:26) Hivyo, hakuna mtu anayeweza kudai kuwa juu ya wanadamu wenzake au haki ya kuonea au kutumia wengine vibaya. Watu walio tayari kujifunza hupata kuthamini uhakika wa kwamba “Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” (Matendo 10:34, 35) Wanatambua kwamba upendo wa Mungu huhusisha wote, kwa kuwa pendeleo la uhusiano wa karibu naye hupatikana kwa watu wote. Kwa hakika, “Mungu aliupenda ulimwengu sana hivi kwamba akatoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele.”—Yohana 3:16.

      Elimu hii inayotegemea Biblia huathiri sana nyutu za watu. Kupitia elimu hiyo mioyo na akili za watu zaweza “kufanywa upya kabisa.” (Waefeso 4:22-24, Today’s English Version) Huwachochea wawatendee wanadamu wenzao kwa adhama na staha. Wameazimia ‘kufanya lililo jema kuelekea wote.’ (Wagalatia 6:10) Hakuna mtu awezaye kuwa Mkristo wa kweli na ashiriki kutumia vibaya na kuonea wanadamu wenzake. Mashahidi wa Yehova wanafurahi kuwa kikundi cha Kikristo kama vile kutaniko la Kikristo la karne ya kwanza, ambapo ‘hakukuwa Myahudi wala Mgiriki, na hakukuwa mtumwa wala mtu huru. Wote walikuwa mtu mmoja katika muungano na Kristo Yesu.’—Wagalatia 3:28.

      Badiliko la Serikali

      Hata hivyo, ili utumwa wa namna zote ukomeshwe kabisa, badiliko kubwa katika jamii ya kibinadamu lahitajiwa. Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni lasema kwamba ili kukomesha kutumiwa vibaya kwa wanadamu, kuna uhitaji wa “kubadili hali ambazo huruhusu kuwepo” kwa mazoea hayo. Hatua za kimataifa, ushirikiano wa kimataifa, na uwajibikaji wa jumuiya ya ulimwengu ni miongoni mwa madokezo zaidi yaliyotolewa na shirika hilo.

      Hilo lingehitaji serikali itakayodhibiti kabisa sayari yetu, serikali itakayohakikisha uhuru ulimwenguni pote. Boutros Boutros-Ghali aliyekuwa katibu-mkuu wa UM, alisema kwamba matatizo halisi yanayokumba sayari yetu lazima yatatuliwe “ulimwenguni pote.” Lakini si kila mtu aliye na hakika kwamba jambo hilo linaweza kutukia. Mambo ya kale yaonyesha kwamba watu wengi walio mamlakani ni wachoyo sana na ni wenye kufikiria mapendezi na miradi yao sana hivi kwamba ni vigumu kufikia ushirikiano wa kimataifa.

      Hata hivyo, Biblia—kitabu kilekile ambacho kimefundisha mamilioni ya watu kuheshimu adhama ya wanadamu wenzao—yaonyesha kwamba Mungu anakusudia kusimamisha serikali ya ulimwengu ya namna hiyo. Katika Biblia utapata ahadi nyingi za ulimwengu mpya wa uadilifu. (Isaya 65:17; 2 Petro 3:13) Mungu anakusudia kuondoa kabisa duniani mtu yeyote asiyempenda Mungu na jirani. Mungu amefunua kusudi lake la kusimamisha serikali ya ulimwenguni pote juu ya wanadamu ili itawale dunia kwa uadilifu. Yesu alituambia tusali kwa ajili ya serikali hiyo katika ile inayoitwa kwa kawaida Sala ya Bwana au Baba Yetu.—Mathayo 6:9, 10.

      Kutumiwa vibaya kwa wanadamu na kila namna ya utumwa itakomeshwa chini ya utawala wa serikali hiyo kwa sababu Kristo Mfalme atatawala “kwa hukumu na kwa haki.” (Isaya 9:7) Wale walioonewa watafunguliwa chini ya utawala wake wa haki, kwa kuwa Biblia husema: “Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu.”—Zaburi 72:12-14.

      Ikiwa unatamani kuona mwisho wa utumwa—namna zote za utumwa—twakualika ujifunze mengi zaidi kuhusu kusudi la Mungu la kusimamisha serikali hiyo ya ulimwengu itakayoleta uhuru. Mashahidi wa Yehova katika eneo lenu watafurahi kukusaidia kufanya hivyo.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

      UHURU NA ADHAMA YA KIBINADAMU—KUTOKA CHANZO GANI?

      Sote tumezaliwa tukiwa na uhitaji na tamaa ya asili ya adhama na uhuru. Kofi Annan, katibu-mkuu wa UM, alirudia maoni yanayojulikana ulimwenguni pote alipouliza hivi: “Ni nani awezaye kukanusha kwamba sote twataka maisha yasiyo na hofu, mateso na ubaguzi? . . . Ni lini uliposikia mtu aliye huru akitaka uhuru ukomeshwe? Ni wapi uliposikia mtumwa akitetea utumwa?”

      Mawazo hayo si mapya kamwe. Akikanusha wazo la kwamba watu fulani walizaliwa wawe watumwa, mwanafalsafa Mroma wa karne ya kwanza Seneca, katika kichapo chake Letters to Lucilius, aliandika hivi: “Tafadhali kumbuka kwamba mtu unayemwita mtumwa wako alitokana na mbegu ileile, anga zuri lilelile liko juu yake, hupumua kama wewe, huishi kama wewe, hufa kama wewe!”

      Imam ʽAlī, anayeonwa kuwa mwandamizi wa nne wa Muḥammad, alisema kwamba watu wote ni “sawa katika uumbaji.” Saʽdī, mshairi Mwajemi wa karne ya 13, alitangaza hivi: “Watoto wa Adamu ni viungo vya mmoja na mwenzake na wameumbwa kwa kitu kimoja. Ulimwengu unapoumiza mshiriki mmoja, washiriki wengine huumia pia.”

      Historia iliyopuliziwa na Mungu iliyo katika Biblia hukazia adhama ya wanadamu wote. Kwa mfano, Mwanzo 1:27 hueleza kuumbwa kwa mwanadamu, isemapo: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Muumba wetu ni Mungu wa uhuru. “Iliko roho ya Yehova, kuna uhuru,” akasema mtume Paulo. (2 Wakorintho 3:17) Kwa kumwumba mtu kwa mfano wake, Yehova aliwapa wanadamu kiasi fulani cha kujiona wanafaa, kujistahi, na adhama. Kwa kuweka huru uumbaji wake kutoka kwa “utumwa wa uharibifu,” pia atahakikisha kwamba watu watafurahia uhuru huo na adhama hiyo milele.—Waroma 8:21.

      [Picha katika kurasa za 9, 10]

      Kila mtu ana haki ya kuwa na adhama na uhuru

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      ELIMU YA BIBLIA HUKAZIA STAHA KWA ADHAMA YA KIBINADAMU NA HUTOKEZA TUMAINI LA WAKATI UJAO LA ULIMWENGU MPYA UJAO

      Funzo la Biblia la familia katika Papua New Guinea

      Umaridadi wa maporomoko haya ya Blue Nile katika Ethiopia ni mmweko wa kimbele wa paradiso iliyorudishwa

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki