-
“Kuna Fedha Potosí!”Amkeni!—1996 | Agosti 8
-
-
Kufanywa Watumwa
Wahispania walivumilia hali ngumu sana zisizostarehesha katika utafutaji wao wa fedha. Mara nyingi, chakula kilikuwa kichache, maji yalikuwa yamechafuliwa, na machimbo yalikuwa hatari. Halihewa yenye baridi mno ilitokeza tatizo zito. Wale waliojaribu kujitia joto kwa makaa nyakati fulani walisumishwa kwa kaboni monoksidi.
Muda si muda Wahispania wakapata njia ya kupunguza hali yao mbaya. Wakiwa washindi, waliwalazimisha Wahindi wenyeji kuwa watumwa. Gazeti Bolivian Times la La Paz lilitaarifu: “Yasemekana kwamba watumwa Wahindi milioni nane waliangamia,” walikufa, katika machimbo ya Potosí wakati wa kipindi cha ukoloni. Ukatili, kufanyishwa kazi kupita kiasi, na maradhi yalisababisha kupungua kwenye kuogofya kwa idadi ya watu. Si ajabu kwamba katika 1550 msimulizi aliita Potosí “kinywa cha helo”!
-
-
“Kuna Fedha Potosí!”Amkeni!—1996 | Agosti 8
-
-
Mojapo malengo makuu ya washindi Wahispania lilikuwa kuanzisha dini ya Katoliki katika Amerika. Ingawa hivyo, watu hawa wenye kudai kuwa Wakristo waliteteaje kupata kwao faida nyingi kutokana na utumwa? Ingawa watu fulani wa kanisa walisema kwa ujasiri dhidi ya ukosefu huo wa haki, wengine walitetea utumwa kwa kudai kwamba utawala mkatili wa Wahispania haukuwa mbaya sana kama utawala mkatili wa Inca. Walidai kwamba Wahindi walikuwa wa hali ya chini na kiasili walielekea kutenda mabaya—hivyo, ilikuwa vyema wafanye kazi kwenye machimbo. Na bado wengine walidai kwamba kuleta Wahindi wafanye kazi machimboni kulikuwa hatua iliyohitajika ili kuwageuza imani wawe Wakatoliki.
Hata hivyo, historia yaonyesha kwamba, makasisi walikuwa miongoni mwa watu matajiri mno katika Potosí. Mwanahistoria Mariano Baptista asema: “Kanisa likiwa shirika, na wawakilishi walo mmoja-mmoja, walifanyiza sehemu iliyopendelewa ya wanyonyaji” wa Wahindi. Mwanahistoria huyu amnukuu gavana mmoja ambaye katika 1591 alilalamika kwamba makasisi “hunyonya Wahindi kwa pupa zaidi na kwa tamaa nyingi kuliko watu wa kawaida.”
-