Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Watu Wengi Wana Deni la Usingizi?
    Amkeni!—2004 | Februari 8
    • Je, Watu Wengi Wana Deni la Usingizi?

      MAMILIONI ya watu leo wana “deni” kubwa. Deni hilo linaweza kuwa ndicho kisababishi kikubwa cha kuharibu magari yao, kazi, na hata ndoa zao. Linaweza kudhuru afya na kupunguza sana maisha yao. Linachangia kudhoofika kwa mfumo wa kinga, na hivyo mtu anaweza kupata maambukizo kwa urahisi. Magonjwa kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo, kunenepa kupita kiasi, na matatizo mengine ya afya yamesababishwa na deni hilo. Hata hivyo, watu wengi hawafahamu kwamba wana deni hilo.

      Tunazungumzia deni la usingizi, ambalo hutokea wakati mtu anapokosa usingizi anaohitaji ili awe na afya bora. Deni hilo linaweza kusababishwa na kukosa kulala kimakusudi kwa sababu ya mtindo wa mtu wa maisha au kwa sababu ya ugonjwa.

      Watafiti wa tiba wanakadiria kwamba watu duniani leo wamepunguza muda wao wa kulala kwa saa moja hivi kila siku kuliko inavyohitajika. Ingawa huenda jambo hilo likaonekana kuwa dogo, deni hilo la usingizi la saa bilioni sita kila siku ulimwenguni pote limechochea watu wafanye utafiti wa magonjwa mbalimbali ya usingizi na jinsi yanavyoathiri maisha.

      Hapo zamani wanatiba walifikiri kwamba kuna ugonjwa mmoja tu wa usingizi, yaani, kukosa usingizi. Hata hivyo, tume moja iliyoteuliwa na Bunge la Marekani ilitambulisha magonjwa 17 ya usingizi. Kwa vyovyote vile, tatizo la kukosa usingizi husababishwa na mambo mengi hivi kwamba mara nyingi linaonwa kuwa dalili ya magonjwa mengine, kama vile homa ilivyo dalili ya ugonjwa fulani.

      Hata kukosa usingizi mara mojamoja kunaweza kuwa hatari. Kwa mfano, ingawa Tom ni dereva wa lori mwenye uzoefu, aligongesha lori kubwa kwenye ukuta ulio kando ya barabara kuu na kumwaga lita 400 za asidi ya sulfuriki. Tom anakubali hivi: “Nilikuwa nimelala.” Uchunguzi kuhusu barabara mbili kuu za Marekani ulikadiria kwamba madereva wanaosinzia walisababisha nusu ya misiba katika barabara hizo.

      Pia, fikiria hatari za kufanya kazi pamoja na mtu mwenye usingizi. Mtafiti wa Australia, Ann Williamson, anasema hivi: “Watu waliokuwa na deni la usingizi la saa 17 mpaka 19 walipochunguzwa, walitenda kama watu wenye asilimia 0.05 [ya kileo katika damu] au hata vibaya zaidi.” Hiyo inamaanisha kwamba watu hao walikuwa kama watu waliokunywa kileo kingi au kama watu waliopitisha kiwango cha ulevi kinachoruhusika kisheria katika nchi fulani! Kwa kuwa kila mwaka mamia ya maelfu ya misiba inayotukia barabarani na kazini inasababishwa na usingizi, hilo husababisha hasara kubwa kazini na nyumbani.a

      Ni mambo gani yanayoweza kusababisha deni la usingizi? Sababu moja ni kufanya kazi kila siku kwa saa 24. Gazeti USA Today linaeleza kwamba hilo ni “tatizo baya sana la kijamii ambalo linaharibu maisha yetu,” na kwamba “wauzaji wa rejareja na watoaji wa huduma wanapata faida kubwa kwa kufanya kazi mchana na usiku.” Katika nchi nyingi, watu hutazama televisheni usiku kucha na kutumia Internet wakati ambapo wanapaswa kulala. Pia, deni hilo linaongezwa na matatizo ya kihisia, ambayo mara nyingi husababishwa na mahangaiko na kuongezwa na mfadhaiko na hekaheka za maisha. Mwishowe, magonjwa fulani husababisha deni la usingizi.

      Madaktari wengi hushindwa kuwasadikisha wagonjwa kuchukua tatizo la usingizi kwa uzito. Daktari mmoja alisema kwamba watu fulani huona kwamba kuchoka kila wakati ni “jambo la kuheshimika.” Na kwa kuwa tatizo lao huongezeka polepole, huenda watu wanaokosa usingizi wasitambue kwamba wana ugonjwa hatari wa usingizi. Wengine husema, ‘Nimeanza kuzeeka’ au, ‘Maisha ni magumu, kwa hiyo siwezi kufanya mengi’ au, ‘Sikuzote mimi huwa mchovu kwa sababu sipati wakati wa kutosha wa kupumzika.’

      Ni vigumu kulipa deni la usingizi. Hata hivyo, kuelewa hatua za usingizi na kujua dalili za deni la usingizi kunaweza kukuchochea ubadilike. Kutambua dalili za magonjwa hatari ya usingizi kunaweza kuokoa uhai.

      [Maelezo ya Chini]

      a Inaaminika kwamba uchovu ulichangia misiba mingi mikubwa ya karne ya 20. Ona gazeti la Amkeni! la Februari 8, 2001, ukurasa wa 6.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Hata kukosa usingizi mara mojamoja kunaweza kusababisha misiba mikubwa

  • Kupata Usingizi Unaohitaji
    Amkeni!—2004 | Februari 8
    • Kupata Usingizi Unaohitaji

      MAMBO mengi yanayohusu usingizi yamejulikana katika miaka 50 iliyopita. Mambo ambayo yamegunduliwa yamepinga dhana zenye kasoro ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu. Dhana moja inasema kwamba wakati ambapo mtu amelala huwa hatendi kwani viungo vingi vya mwili hupumzika.

      Watafiti wa tiba wamechunguza mawimbi ya umeme yanayopita kwenye ubongo na kugundua kwamba kuna hatua mbalimbali za usingizi. Utendaji mwingi huendelea haraka-haraka katika ubongo wa mwanadamu katika vipindi fulani vya usingizi. Ili mtu apate usingizi wa kutosha, hatua hizo hujirudia mara nne au zaidi kila usiku, na kila hatua huchukua muda fulani.

      Utata wa Usingizi

      Usingizi wa kawaida umegawanywa katika vikundi viwili: kipindi cha kusogeza macho haraka (wakati wa ndoto) na kipindi cha kutosogeza macho haraka (wakati ambapo mtu haoti ndoto). Unaweza kutambua mtu akiwa katika kipindi cha kusogeza macho haraka kwa kuona mboni za macho zikisonga haraka macho yakiwa yamefungwa.

      Kipindi cha kutosogeza macho haraka kinaweza kugawanywa katika hatua nne. Baada tu ya kujiwekelea kitandani, unaingia katika hatua ya kwanza pole kwa pole, yaani, unasinzia. Katika hatua hiyo misuli hulegea na mawimbi ya umeme huongezeka ubongoni na hutukia bila mfuatano maalumu. Hatua hiyo inapotukia mara ya kwanza huchukua kati ya sekunde 30 na dakika 7. Katika hatua ya pili, mawimbi ya ubongo huwa makubwa, na hatua hiyo huchukua asilimia 20 ya muda wa kulala. Huenda ukawa na mawazo au picha zisizo kamili akilini, lakini hutambui kinachoendelea wala kuona hata ukifungua macho.

      Hatua ya tatu ni ya usingizi mzito na ya nne ni ya usingizi mzito zaidi. Katika hatua hizo ubongo hutokeza mawimbi makubwa yanayosonga polepole. Wakati huo si rahisi kuamka, kwa sababu sehemu kubwa ya damu huelekezwa kwenye misuli. Wakati huo (ambao ni asilimia 50 hivi ya usingizi) ndipo mwili hujirekebisha na watoto wadogo hukua. Ni muhimu kujua kwamba mtu yeyote, iwe ni kijana au mtu mzima asiyepata sehemu hizo za usingizi anaweza kujihisi mchovu, atakosa uchangamfu, na hata kushuka moyo siku inayofuata.

      Baada ya kila hatua kuna kipindi cha kusogeza macho haraka. Katika kipindi hicho cha kuota ndoto (kinachoanza baada ya kila dakika 90 hivi), damu zaidi huelekezwa kwenye ubongo na mawimbi ya ubongo hutenda kazi kwa njia ileile kama wakati ambapo mtu hajalala. Hata hivyo, huwezi kusogeza viungo vyako. Huenda hilo humzuia mtu anayeota ndoto asitende kupatana na ndoto zake, hivyo anaepuka kujiumiza au kuwaumiza wengine.

      Vipindi vya kusogeza macho haraka, au vipindi vya ndoto, huchukua muda mrefu zaidi kila vinapotukia na yaelekea vinafaidi sana ubongo. Kama kompyuta, ubongo huchanganua habari zilizohifadhiwa, hufuta zile zisizo muhimu na kuhifadhi zile muhimu kwenye kumbukumbu la kudumu. Mtu asipopata vipindi vingi vya ndoto anaweza kupata matatizo ya kihisia. Kwa mfano, watu ambao hukosa usingizi hawapati vipindi vya kutosha vya ndoto na hilo huchangia mfadhaiko.

      Hivyo, ni nini hutukia tunapokosa kulala usingizi wa kutosha kwa ukawaida (kimakusudi au tunaposhindwa kulala), yaani, kuwa na deni la usingizi? Tukikosa kulala vya kutosha mfululizo, hatutapata kipindi cha mwisho cha kusogeza macho haraka ambacho ndicho kirefu zaidi na muhimu kwa ubongo. Ikiwa hatulali vya kutosha kwa sababu ya kukatisha-katisha usingizi, hatuwezi kufikia kipindi cha usingizi mzito ambacho husaidia kurekebisha miili yetu. Wale wenye deni kubwa la usingizi hushindwa kukaza fikira kwa muda mrefu, husahau-sahau na kukosa maneno ya kutumia, hupunguza uwezo wao wa kufikiri vizuri na wa kubuni mambo.

      Kwa nini mtu huhisi usingizi? Inaonekana mambo kadhaa yanahusika katika taratibu za kawaida za kulala na kuamka. Inaonekana kemikali za ubongo zinahusika. Pia, kuna kiini cha chembe za neva za ubongo ambacho hudhibiti vipindi vya usingizi. Kiini hicho kiko karibu na mahali ambapo neva za kuona hukutana. Mwangaza huathiri usingizi. Mwangaza mwingi hukuamsha, na giza hukusaidia kulala.

      Joto la mwili linahusika pia. Ukiwa na joto jingi zaidi, hasa karibu na wakati wa adhuhuri na alasiri, wewe huwa macho zaidi. Kadiri joto la mwili linavyopungua, ndivyo unavyosinzia. Watafiti wanakubali kwamba kila mtu ana utaratibu wake wa kulala na kuamka.

      Unahitaji Kulala kwa Muda Gani?

      Wanasayansi wanasema kwamba kwa wastani wanadamu wanahitaji kulala kwa saa nane hivi kila usiku. Lakini uchunguzi unaonyesha kwamba watu wana viwango mbalimbali vya usingizi.

      Unaweza kutambua ikiwa unalala vya kutosha au una deni la usingizi ukijichunguza kinaganaga. Wataalamu wanasema mambo yafuatayo yanaonyesha kwamba mtu analala vya kutosha:

      ◼ Mtu anapata usingizi bila kutumia dawa za kulala au analala bila wasiwasi au mahangaiko.

      ◼ Mtu hatambui anapoamka usiku, lakini anapoamka anapata usingizi haraka.

      ◼ Mtu huamka saa zilezile kila asubuhi bila ugumu na bila kuamshwa na kengele ya saa.

      ◼ Mtu anapoamka, hasikii usingizi na anakuwa macho siku nzima.

      Madokezo Muhimu

      Vipi wale wanaokosa usingizi mara kwa mara? Wataalamu fulani wanatoa madokezo yafuatayo:

      1. Usinywe kileo, kahawa au chai kabla tu ya kulala. Watu wengi wanaamini kimakosa kwamba kunywa vileo fulani kunaweza kuwasaidia kulala. Hata hivyo, uchunguzi wa kitiba unaonyesha kwamba vileo vinaweza kukufanya upoteze usingizi.

      2. Acha kuvuta sigara. Kitabu kimoja kinasema: “Wavutaji wa sigara hawalali kwa urahisi kwa sababu sigara huongeza shinikizo la damu, mpigo wa moyo, na kusisimua ubongo. Wavutaji wa sigara huamka usiku mara nyingi, labda kwa sababu wakati huo hawavuti sigara.”

      3. Epuka kufanya mambo yanayochosha akili na mwili kabla tu ya kulala. Mazoezi ya mwili humsaidia mtu kupata usingizi wa kutosha lakini si yanapofanywa kabla tu ya kulala. Kusuluhisha matatizo makubwa au kufanya kazi inayochosha akili kabla tu ya kulala kunaweza kukufanya ushindwe kutulia ambako hukusaidia upate usingizi.

      4. Hakikisha kwamba hakuna kelele na mwangaza katika chumba chako cha kulala, na ikiwezekana kiwe baridi kidogo. Fikiria uchunguzi mmoja maarufu uliohusisha watu wanaoishi karibu na uwanja wa ndege ambao walidai kwamba hawasikii tena kelele za ndege. Walipochunguzwa, ilibainika kwamba bongo zao zilirekodi kelele za kila ndege iliyotua na kuondoka! Wachunguzi walikata kauli kwamba watu hao walipoteza saa moja ya usingizi kwa wastani kila usiku kuliko watu wanaoishi katika maeneo yenye utulivu. Vitu vya kuziba masikio na njia nyingine za kupunguza kelele vingewasaidia sana kupata usingizi mwanana. Wengine wameona kwamba mvumo mwanana kama vile wa feni unawasaidia kupunguza kelele zinazotoka nje.

      5. Uwe mwangalifu kuhusu kutumia dawa za usingizi. Uthibitisho mwingi unaonyesha kwamba dawa nyingi za usingizi humfanya mtu awe mzoefu, huacha kufanya kazi baada ya muda, na zina madhara. Ikiwa ni lazima zitumiwe, basi inafaa kuzitumia kwa muda mfupi.

      Kwa kuwa mfadhaiko unaweza kumfanya mtu akose usingizi, imeonekana kwamba jambo moja muhimu ni kustarehe na kutulia muda mfupi tu kabla ya kulala. Inafaa kusahau mahangaiko na kufanya jambo lenye kufurahisha, kama vile kusoma. Inafaidi sana kufuata shauri hili la Biblia: “Msihangaike juu ya kitu chochote, bali katika kila jambo kwa sala na dua pamoja na kutoa shukrani maombi yenu na yajulishwe Mungu; na amani ya Mungu . . . itailinda mioyo yenu na nguvu zenu za akili.”—Wafilipi 4:6, 7.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Maoni ya Kawaida Yenye Makosa

      1. Kunywa vinywaji vyenye kafeini ndiyo njia bora ya kuwa macho unapoendesha gari kwa muda mrefu.

      Uchunguzi unaonyesha kwamba mara nyingi madereva hujidanganya kwamba wako macho. Ikiwa huwezi kuepuka kuendesha gari kwa muda mrefu usiku, afadhali uegeshe gari mahali salama na kulala kidogo (kwa dakika 15 mpaka 30), kisha utembee au kukimbia-kimbia ukinyoosha mikono na miguu.

      2. Ikiwa ninashindwa kulala, suluhisho ni kulala kidogo mchana.

      Huenda hilo ni kweli, lakini wataalamu wengi wanaamini kwamba inafaa zaidi kulala kwa muda mrefu kila siku. Kulala kidogo mchana (kwa dakika 15 mpaka 30) kunaweza kukusaidia uwe macho alasiri bila kuharibu usingizi wako. Lakini kulala kidogo saa nne kabla ya wakati wa kulala kunaweza kuharibu usingizi wako.

      3. Ndoto tunazokumbuka zinatuharibia usingizi.

      Ndoto (ambazo sisi huota katika kipindi cha kusogeza macho haraka) huonyesha tulilala vizuri na kwa kawaida zinatokea mara nne au zaidi tunapolala usiku. Uchunguzi unaonyesha kwamba ndoto ambazo tunakumbuka ni zile ambazo tulikuwa tunaota wakati tulipoamshwa au ziliisha dakika chache kabla ya kuamka. Kwa upande mwingine, ndoto mbaya zinaweza kutufadhaisha na kutufanya tushindwe kulala tena.

      [Picha katika ukurasa wa 6, 7]

      Kulala vya kutosha hukusaidia uwe macho na makini mchana kutwa

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Sasa wanasayansi wamegundua kwamba kuna hatua mbalimbali za usingizi

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Wavutaji wa sigara hupata matatizo ya kulala

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Uwe mwangalifu kuhusu dawa za usingizi

  • Kutambua Matatizo ya Kukosa Usingizi
    Amkeni!—2004 | Februari 8
    • Kutambua Matatizo ya Kukosa Usingizi

      NYAKATI nyingine dalili za mtu zinaweza kuonyesha kwamba ana tatizo kubwa la usingizi. Kuna tatizo la kukosa usingizi ambalo hudumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na mara nyingi huhusianishwa na magonjwa mengine makubwa, kama vile kushuka moyo. Tatizo hilo linaweza pia kuwa dalili ya ugonjwa mbaya.

      Kushindwa Kupumua Unapolala

      Mario alikuwa na tatizo la kusinzia kupita kiasi mchana. Alipokuwa akiendesha gari lao, ilimbidi mke wake amtazame kwa uangalifu kwa kuwa alikuwa na zoea la kusinzia kwa ghafula na hakukumbuka jambo hilo. Alikoroma kwa sauti kubwa mara kwa mara kila usiku na wakati mwingine alishtuka na kuamka, huku akipumua kwa shida.a

      Mario alikuwa na dalili za tatizo la kushindwa kupumua anapolala. Mtu anaweza kushindwa kupumua kwa sekunde kumi mpaka dakika mbili au tatu. Mara nyingi mtu mwenye tatizo hilo hupinduka-pinduka akipumua kwa shida kisha hurudi kulala, na tatizo hilo hujirudia mara nyingi sana kila usiku. Kuna aina tatu za tatizo hilo.

      Tatizo la kwanza hutukia wakati ubongo hautoi ishara inayomwezesha mtu kupumua kikawaida. Katika tatizo la pili, sehemu ya kupitisha hewa iliyo nyuma ya koo huziba kabisa hivyo mtu hushindwa kupumua. Tatizo la tatu linahusisha tatizo la kwanza na la pili na huathiri watu wengi zaidi. Mtu aliye na mojawapo ya matatizo hayo ni kama mtu ambaye halali usiku kucha kila siku!

      Huenda watu wenye matatizo ya kushindwa kupumua wanapolala wakawa hatarini kwa kuwa wanaweza kulala ghafula kazini au wanapoendesha gari. Huenda wakapata shinikizo la damu, moyo wao ukafura, na wakakabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kiharusi au moyo wao ukaacha kufanya kazi. Dakt. William Dement wa Chuo Kikuu cha Stanford, anakadiria kwamba Wamarekani 38,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya madhara ya moyo yanayosababishwa na tatizo la kushindwa kupumua wanapolala.

      Ingawa tatizo hilo huwapata sana wanaume wanene kupita kiasi waliozidi umri wa miaka 40, linaweza pia kuwapata watu wenye umri wowote, hata watoto. Kuna matibabu mbalimbali na yote yanapaswa kutolewa na daktari wa matatizo ya usingizi. Njia bora zaidi ya kutibu tatizo la kuziba koo mtu anapolala ambayo haihusishi upasuaji ni kutumia mashine ya kuingiza hewa mapafuni. Mgonjwa huvaa kifaa kinachodhibiti hewa (kilichorekebishwa na daktari ili kifae hali zake) kwenye pua usiku ili apate hewa inayohitajiwa kuzuia tatizo hilo. Ikiwa kifaa hicho hakisuluhishi tatizo hilo, kuna upasuaji mbalimbali unaoweza kufanywa, ambao unatia ndani kutumia miale ya leza au ya redio kuzibua koo.

      Kusinzia Mchana

      Tatizo lingine linalohitaji kutibiwa ni kusinzia sana mchana na linasababishwa na mfumo wa neva. Kwa mfano, Buck alikuwa akisinzia daima. Alikuwa analala ghafula hata wakati wa mikutano muhimu. Alianza kushikilia funguo mkononi ili zikianguka zimwamshe. Kisha magoti yake yalianza kulegea na alianguka aliposisimuka. Halafu alipokuwa akilala au kuamka mwili wake ulikufa ganzi na alianza kuona maono kabla tu ya kulala.

      Tatizo la kusinzia mchana huanza mtu anapokuwa na umri wa miaka 10 mpaka 30. Nyakati nyingine watu wenye tatizo hilo huonekana kuwa timamu lakini hawatambui wakati ukipita. Ubaya wa tatizo hilo ni kwamba mara nyingi halitambuliwi kwa miaka mingi, huku mtu anayeugua akidhaniwa kuwa mvivu, kwamba anafikiri polepole, au anaonekana kuwa mtu asiyeeleweka. Kwa sasa tatizo hilo halina tiba, lakini dalili zake zinaweza kutibiwa kwa kiasi fulani kwa dawa na kufanya mabadiliko maishani.b

      Magonjwa Mengine ya Usingizi

      Magonjwa mengine mawili ambayo nyakati nyingine humpata mtu wakati mmoja, huathiri miguu na mikono na kumfanya mtu akose usingizi kabisa. Ugonjwa mmoja huifanya miguu ya mtu ishtuke-shtuke anapolala na nyakati nyingine mikono hufanya hivyo pia. Fikiria mfano wa Michael. Uchunguzi ulionyesha kwamba miguu yake iliposhtuka aliamka karibu mara 350 kila usiku!

      Ugonjwa mwingine hufanya miguu isitulie,c na mgonjwa huhisi akitaka sana kusogeza miguu na magoti na hivyo hawezi kulala. Ingawa nyakati nyingine hali hiyo husababishwa na kukosa kufanya mazoezi au damu inaposhindwa kuzunguka kikamili, inaonekana wakati mwingine inasababishwa na kula na kunywa vitu vyenye kafeini. Pia kunywa kileo huongeza hali hiyo nyakati nyingine.

      Ugonjwa mwingine ni ule wa kusaga au kukaza meno sana wakati mtu anapolala. Ukitokea kwa ukawaida, ugonjwa huo unaweza kuharibu meno na kusababisha maumivu makali ya taya, hivyo mtu hushindwa kulala kabisa. Kuna tiba mbalimbali kama vile upasuaji wa mdomo na kutumia kifaa cha kukinga meno usiku, ikitegemea kiwango cha ugonjwa.

      Mazungumzo haya mafupi kuhusu magonjwa kadhaa ya usingizi yanaonyesha kwamba ni hatari kuyapuuza. Huenda matibabu yakawa sahili au tata, lakini mara nyingi ni ya lazima. Ikiwa wewe au mpendwa wako ana ugonjwa mbaya wa kukosa usingizi au dalili zake, inafaa kupata msaada wa kitiba haraka. Hata kama tiba haitaondoa matatizo kabisa, huenda ikapunguza sana hatari zinazohusika na kufanya hali hiyo iwe rahisi kuvumilia. Kisha, wakati ujao, wakati ahadi za Biblia zitakapotimia, “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’” Magonjwa yote yataondolewa kabisa Mungu atakapofanya “vitu vyote kuwa vipya.”—Isaya 33:24; Ufunuo 21:3-5.

      [Maelezo ya Chini]

      a Kukoroma kwa sauti kubwa wakati wowote ule ambapo koo limeziba ni tofauti na jinsi watu wengi hukoroma kidogo mara kwa mara na kuwasumbua au kuwaamsha wengine wanaolala.

      b Kwa habari zaidi kuhusu kusinzia mchana, ona gazeti la Amkeni! la Aprili 8, 1991, ukurasa wa 19-21, la Kiingereza.

      c Ona gazeti la Amkeni! la Novemba 22, 2000 kwa habari zaidi kuhusu ugonjwa huo.

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Matibabu ya magonjwa ya usingizi yanapaswa kutolewa na daktari

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Huenda kukoroma kukawa dalili ya tatizo la kushindwa kupumua mtu anapolala

      [Picha katika ukurasa wa 11]

      Mara nyingi watu walio na ugonjwa wa kusinzia mchana hueleweka kimakosa kuwa wavivu

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Vifaa vinavyoingiza hewa mapafuni vinaweza kumsaidia mtu anayeshindwa kupumua anapolala

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki